Friday, December 23, 2016

AUBAMEYANGA, MAHREZ, MANE WAINGIZWA ORODHA YA MWISHO YA CAF.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Gabon na klabu ya Borussia Dortmund bado yuko katika nafasi ya kutetea taji lake la Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika baada ya kuingia katika orodha ya mwisho ya wachezaji wa tatu iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Afrika-CAF. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 atachuana na winga wa kimataifa wa Algeria na Leicester City Riyad Mahrez ambaye ni mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika ya BBC kwa mwaka huu pamoja na winga wa kimataifa wa Senegal na Liverpool Sadio Mane. CAF imethibitisha kuwa mshindi anatarajiwa kutangazwa katika sherehe zitakazofanyika Alhamisi ya Januari 5 huko jijini Abuja, Nigeria. Aubameyang ndio aliyemaliza utawala wa kiungo wa Ivory Coasy na Manchester City Yaya Toure aliyetwaa tuzo hiyo kwa miaka minne mfululizo. Kiungo wa Zambia na klabu ya TP Mazembe, Rainford Kalaba, mshambuliaji wa Zimbabwe na Mamelodi Sundowns, Khama Billiat na kipa wa Uganda na Mamelodi Sundowns Denis Onyango wenyewe watagombea tuzo hiyo kwa wachezaji wanaocheza ndani ya bara hili.

No comments:

Post a Comment