Sunday, June 30, 2013

VILLAS-BOAS KUSTAAFU MIAKA 10 IJAYO.

MENEJA wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Andre Villas-Boas amebainisha mipango ya kustaafu kufundisha wakati atapofikisha miaka 45. Kocha huyo mwenye miaka 35 raia wa Ureno amekuwa kocha mdogo zaidi kushinda taji la Europa League wakati akiwa na klabu ya Porto miaka miwili iliyopita, kabla ya kwenda Chelsea ambako alitimuliwa kwa kushindwa kufanya vyema na kwenda Spurs alipo sasa. Pamoja na kwamba Villas-Boas amesisitiza kuwa anafurahia kazi hiyo ya ukocha lakini haoni kama atafanya shughuli hiyo kwa kipindi kirefu kama makocha wengine. Villas-Boas amesema amapenzi yake katika soka yanamfanya aishi maisha ya wasiwasi kwa kipindi cha miezi 11 katika mwaka na anadhani maisha yamruhusu mtu kufurahia vitu vingine zaidi ndio maana ameamua baada ya miaka 10 ijayo atastaafu rasmi shughuli hiyo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa amekuwa na ndoto za kipindi kirefu kushiriki mashindano ya Dakar Rally hivyo akiachana na mambo ya ukocha ataelekeza shughuli zake katika mashindano hayo yenye historia ya kipekee duniani. 


WILLIAMS, DJOKOVIC WAENDELEA KUPASUA ANGA WIMBLEDON.

MWANADADA nyota wa mchezo wa tenisi kutoka Marekani, Serena Williams amefanikiwa kuingia katika mzunguko wan ne wa michuano ya Wimbledon baada ya kumuengua Kimiko Date-Krumm wa Japan katika mzunguko wa tatu wa michuano hiyo. Williams ambaye anashika namba moja katika orodha za ubora duniani na bingwa mtetezi wa michuano katika mchezo huo alimshinda Krumm kwa 6-2 6-0 akitumia muda wa dakika 61 pekee. Krumm mwenye umri wa miaka 42 amekuwa mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi kuingia mzunguko wa tatu wa michuano hiyo inayoendelea jijini London, Uingereza. Kwa upande wanaume Novak Djokovic wa Serbia naye amefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora baada ya kumtandika Jeremy Chardy wa Ufaransa kwa 6-3 6-2 6-2.

CHELSEA YATHIBITISHA KUWATEMA WANNE.

KLABU ya Chelsea imethibitisha kuwatema wachezaji wake Paulo Ferreira, Yossi Benayoun, Florent Malouda na Ross Turnbull baada ya mikataba yao kumalizika. Ferreira ameichezea klabu hiyo mechi 217 katika kipindi cha miaka tisa aliyokuwepo Stamford Bridge na kuisaidia kunyakuwa mataji matatu ya Ligi Kuu nchini Uingereza na moja la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya walilochukua mwaka jana. Benayoun alitua Chelsea mwaka 2010 ili kuziba nafasi ya Joe Cole lakini alishinda kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara na kupelekwa kwa mkopo katika vilabu Arsenal na West Ham United katika vipindi tofauti. Malouda alichukuliwa kutoka mwaka mabingwa wa Ligi Kuu nchini Ufaransa mwaka 2007 klabu ya Olympique Lyon na kushinda vikombe kadhaa vya ligi na ligi ya mabingwa lakini alienguliwa ghafla katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo msimu uliopita na kufanya mazoezi na wachezaji wa akiba wa timu hiyo. Turnbull alisajiliwa akitokea Middlesbrough mwaka 2009 kama golikipa wa akiba akimsaidia Petr Cech na kucheza mechi 19 pekee katika miaka minne ambayo amekuwepo katika klabu hiyo yenye maskani yake magharibi mwa jiji la London.

NEYMAR, INIESTA, PIRLO, SUAREZ, RAMOS NA PAULINHO KUCHUANA TUZO YA MCHEZAJI BORA MICHUANO YA KOMBE LA SHIRIKISHO.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetangaza orodha ya wachezaji sita watakaogombea tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho ambao ni Neymar, Andres Iniesta, Andrea Pirlo, Luis Suarez, Sergio Ramos na Paulinho. Majina hayo yamechaguliwa na kamati maalumu ya ufundi ya FIFA na mshindi atatambulishwa mbele ya waandishi wa habari baada ya mchezo wa fainali utakaochezwa baadae leo. Wachezaji wanne kati hao wanatarajiwa kuwemo katika vikosi vya nchi zao katika mchezo wa fainali kati ya wenyeji Brazil na Hispania katika Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro. Neymar amefunga mabao matatu kwa timu yake ya Brazil na ni mchezaji pekee kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara mbili katika michuano hiyo huku mbrazil mwenzake Paulinho akifunga mabao mawili katika mechi tatu.

HADHI YA FIFA IMEIMARIKA - BLATTER

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amedai kuwa hadhi ya shirikisho hilo imeimarika kutokana na fainali za michuano ya Kombe la Shirikisho inayoendelea nchini Brazil licha ya maandamano yanayoendelea nchini humo. Akiongea kwa mara ya kwanza, tangu maandamano hayo kuanza, Blatter amesema anawahurumia raia wa nchi hiyo wanaoandamana katika miji mia moja nchini Brazil. Maandamano zaidi yanategemewa kuwepo kabla ya fainali yamichuano hiyo kati ya Brazil na Hispania katika Uwanja wa Maracana uliopo jijini Rio de Janeiro na kuna wasiwasi mkubwa kuwa huenda rais wa nchi hiyo Dilma Rousseff huenda asihudhurie fainali hiyo. Blatter amesema FIFA imekuwa na nguvu zaidi na hadhi yake imeimarishwa huku mchezo wa soka umekuwa na nafasi kubwa miongoni mwa watu wa Brazil na imewapa fursa ya kuelelezea hisia zao. Blatter amesema anawahurumia sana raia wa nchi hiyo kwa kuwa anafahamu masuala wanayoyapinga kupitia maandamano hayo ya amani na ameongea kuwa anatarajiwa serikali ya nchi hiyo itatatua masuala hayo kabla ya kuanza kwa fainali ya Kombe la Dunia itakayoandaliwa nchini humo mwaka ujao.

Friday, June 28, 2013

TUNA UWEZZO WA KUPAMBANA NA WALIO BORA - PRANDELLI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Italia Cesare Prandelli amesema kikosi chake kina uwezo wa kupambana na timu bora kufuatia kuenguliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati 7-6 katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mabara. Italia jana usiku walifanikiwa kuing’ang’ania Hispania inayonolewa na Vicente del Bosque kwenda sare ya bila kwa bila katika dakika tisini za kawaida na baadae kuongezewa dakika zingine ambazo nazo hazikuzalisha mabao na kupelekea mchezo huo kuamuliwa kwa matuta. Prandelli amesema wametolewa katika michuano hiyo kwa heshima na kuonyesha uma kuwa wanaweza kushundani na timu bora kabisa duniani. Italia walifanikiwa kuwabana wapinzani wao na kushindwa kupiga mpira wowote uliolenga goli katika kipindi cha kwanza na Prandelli amewasifu wachezaji wake ka kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kutoruhusu makosa ambayo yangewagharimu. Pamoja na kucheza vyema na timu bora kabisa duniani Prandelli hakuwa tayari kuzungumzia mikakati yake katika michuano ya Kombe la Dunia mwakani akidai kuwa muda bado haujafika kwakuwa bado hawajafuzu kucheza michuano hiyo.

WAKANYAGANA KUMUONA MESSI SENEGAL.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Argentina Lionel Messi ametua nchini Senegal jana kwa ndege binafsi na kulakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Dakar na mashabiki wa soka na vijana wadogo waliotoka pembe mbalimbali za nchi hiyo. Nyota huyo anayecheza katika klabu ya Barcelona alialikwa na shule ya soka ya Qatar Aspire ambao wana tawi lao nchini humo kwa ajili ya kwenda kwenye kampeni ya kupiga vita ugonjwa wa malaria. Kwa mujibu wa waratibu ya ziara hiyo maelfu ya neti ambazo zitakuwa na picha ya Messi zitasambazwa kwa watoto na familia katika vijiji mbalimbali nchini humo. Messi atasafiri kwa helikopta kwenda Saly eneo la karibu na mji wa Dakar ambapo atatembelea nyumba za yatima na kuongea na wenyeji wa hapo jinsi watakavyoweza kujikinga na malaria.

FENERBAHCE KUKATA RUFANI KUPINGA ADHABU YAO.

MWENYEKITI wa klabu ya Fenerbahce ya Uturuki kwa mara nyingine amekana tuhuma za kupanga matokeo zinazoikabili klabu hiyo na kudai kuwa ana uhakika rufani yao walioiwasilisha Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA itabadilisha uamuzi wa kuwafungia kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa barani humo. Mwenyekiti huyo aitwaye Aziz Yildirim amesema Fenerbahce itatoa ndege kwa ajili ya watu watakaopeleka ushahidi wa kuitetea klabu hiyo katika usikilizwaji wa rufani yao. Fenerbahce walifungiwa mapema wiki hii kutoshiriki michuano yoyote inayoandaliwa na UEFA ambayo watafuzu kucheza kuwanzia msimu ujao kutokana na kukutwa na hatia ya kupanga matokeo katika mechi za Ligi Kuu nchini Uturuki mwaka 2011. Yildirim ambaye alihukumiwa mwaka jana kwa makosa ya jinai ambapo amekata rufani katika mahakama ya juu nchini humo, amedai kuwa klabu hiyo ni safi na hawajajihusisha na suala hilo wanalotuhumiwa nalo. Klabu hiyo imemaliza katika nafasi ya pili kwenye ligi kuu ya nchi hiyo na wamefuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo wataanzia hatua ya mtoano kabla ya kuingia kwenye hatua ya makundi ya timu 32.

UNITED YATAKA KUIBOMOA EVERTON TENA.

KLABU ya Manchester United imeamua kumtengea kitita cha paundi milioni 15 kwa ajili ya kumnasa beki wa Everton, Leighton Baines. Baada ya kukataa ofa ya awali ya United ya Pauni Milioni 12, Everton imesisitiza kuwa beki huyo wa kushoto wa kimataifa wa England hauzwi. Lakini United imepania kupanda dau hadi paundi milioni 20 katika kuwania saini ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28. Mrithi wa Moyes, Everton, Roberto Martinez anataka kumbakzia beki huyo na klabu hiyo inataka kumpa mkataba mpya ikimuongezea mshahara hadi paundi 70,000 kwa wiki. Mpango huu unamuweka shakani beki Mfaransa, Patrice Evra juu ya mustakabali wake Old Trafford na wazi sasa anaweza kuhamia Monaco au Paris Saint-Germain. 




Thursday, June 27, 2013

WEBBER AAMUA KUACHANA NA LANGALANGA MWISHONI MWA MSIMU.

DEREVA nyota wa langalanga wa timu ya Red Bull, Mark Webber ameamua kuachana na mashindano hayo ikifikapo mwishoni mwa msimu huu. Katika miaka 12 ambayo amekuwa akishiriki michuano ya langalanga Webber ambaye pia amewahi kuendesha katika timu za Minard, Jaguar na Williams ameshinda mashindano mbalimbali ya Grand Prix mara tisa na kumaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano ya dunia mara tatu. Akihojiwa kuhusiana na uamuzi huo Webber amedai kuwa anadhani huo ni wakati muafaka kwake kuachana na mbio za langalanga na kuangalia mambo mengine. Msimu wake mzuri ulikuwa ni mwaka 2010 ambapo aliongoza karibu msimu wote kabla ya kuteleleza katika mashindano matatu ya mwisho na kushuhudia dereva mwenzake wa Red Bull Sebastian Vettel na Fernando Alonso wa Ferrari wakimpita. Dereva wa Lotus Kim Raikkonen ambaye ni bingwa wa michuano ya dunia mwaka 2007 ndio anapewa nafasi kubwa kuchukua nafasi ya Webber ambaye aliingia katika langalanga mwaka 2002.


TEVES ATUA JUVENTUS.

KLABU ya Juventus ya Italia jana ilimtangaza rasmi kumsajili mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Argentina, Carlos Tevez kutoka timu ya Manchester City kwa mkataba wa miaka mitatu. Taarifa zinadai kuwa klabu yenye maskani yake katika jiji la Turin wamelipa kiasi cha paundi milioni 10 kwa nyota huyo mwenye umri wamiaka 29. Lakini Tevez atatakiwa kumaliza adhabu yake ya kutumikia jamii kwa saa 250 ili kuondoka jijini London salama na kuepuka kuburuzwa tena mahakamani. Tevez alikatisha likizo yake huko Amerika Kusini na kupanda ndege kuelekea Italia jana lakini pia atatakiwa kumaliza adhabu yake aliyopewa na mahakama ya Macclefield April mwaka huu kwa kuendesha huku akiwa amefungiwa kufanya hivyo.

KIRUI, KIPSANG WAJITOA MARATHON MOSCOW.

BINGWA mara mbili wa dunia mashindano ya mbio ndefu Abel Kirui na mshindi wa medali ya shaba katika michuano ya olimpiki Wilson Kipsang wamejitoa katika timu ya wanariadha ya Kenya itakayoshiriki michuano ya riadha ya dunia itakayofanyika jijini Moscow. Makamu wa rais wa Chama cha Riadha cha nchi hiyo Paul Mutwii amedai kuwa Kurui aliwafahamisha kwamba amejitoa kwasababu ya kusumbuliwa na majeraha wakati Kipsang yeye amewaambia kuwa ana majukumu mengine. Kirui ambaye alishinda taji la dunia la mbio ndefu mwaka 2009 na 2011 amekuwa akisumbuliwa jeraha la kifundo cha mguu wake wa kulia na anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita. Kuziba nafasi hizo Mutwii amesema wamewaita Mike Kipyego ambaye alishinda mbio za marathon jijini Tokyo mwaka jana, Bernard Kipyego mshindi wa medali ya fedha mbio za nusu marathon 2009 na bingwa wa mbio za marathoni za Paris Peter Some. Kikosi cha mwisho kitakachokwenda Moscow kitatajwa mwezi ujao baada ya kufanyika mbioza mchujo.

BADO SIJAFULIA - FEDERER.

MCHEZAJI tenisi nyota wa Switzerland, Roger Federer amesisitiza kuwa bado ataendelea kucheza mchezo huo kwa miaka mingi ijayo pamoja na kutolewa mapema katika michuano ya Wimbledon jana. Nyota huyo ambaye anashika namba tatu katika orodha za ubora duniani amesema hana hofu yoyote pamoja na kutolewa na Sergiy Stakhovisky wa Ukraine katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo. Katika mchezo huo Federer aliburuzwa kwa kufungwa 6-7 7-6 7-5 7-6 na Stakhovsky anayeshika namba 116 katika orodha za ubora duniani. Baadhi ya wadau wa mchezo huo wamekuwa wakihoji kiwango cha Federer mwenye umri wa miaka 31 na kudai kuwa amekwisha lakini mwenye amesisitiza kuwa bado yuko fiti na ataendelea kucheza kwa miaka kadhaa ijayo. Kwa upande wa wanawake mwanadada nyota anayeshika namba mbili kwa ubora kwa upande wanawake Maria Sharapova wa Urusi naye aliyaaga mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha 6-3 6-4 kutoka kwa Michelle Larcher de Brito wa Ureno anayeshika namba 131 katika orodha hizo.

BADO HATUKO FITI KWA KOMBE LA DUNIA - SCOLARI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luis Felipe Scolari amekiri kuwa kikosi chake bado hakiwezi kuanza kuota kunyakuwa taji lao la sita la Kombe la Dunia mwaka ujao lakini wamebakisha mechi moja kunyakuwa taji lao la tatu la Kombe la Shirikisho baada ya kuiengua Uruguay katika hatua ya nusu fainali. Scolari amesema anafikiri kikosi hicho kimefikia mahali pazuri lakini bado kuna vitu vingi vya kufanyia marekebisho mpaka kikamilike kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kwasasa wanahamishia nguvu zao katika mchezo wa fainali na baada ya hapo wataangalia mapungufu yalijitokeza ili kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara kitakachoweza kulibakisha Kombe la Dunia nyumbani. Brazil kwasasa wanasubiri mshindi wa nusu fainali nyingine ya michuano hiyo itakayopigwa baadae leo kati ya mabingwa wa Ulaya na Dunia Hispania watakaochuana na Italia.

Wednesday, June 26, 2013

RONALDO AZIDI KUWATIA TUMBO JOTO MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo anaweza kuwa njiani kurejea Manchester United kutokana na tetesi kuwa atafanya mazungumzo na viongozi wa Old Traford katika siku tatu zijazo. Nyota huyo wa klabu ya Real Madrid amekuwa akihusishwa na tetesi za kurejea Uingereza baada ya kuonekana kukosa furaha huko Santiago Bernabeu lakini inaaminika kwamba ujio wa Carlo Ancelotti unaweza kushawishi kubakia nchini Hispania. Gazeti moja nchini Hispania liliripoti kuwa Ronaldo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Ureno atakutana na viongozi hao wa United kabla ya kurejea Madrid kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi. Meneja mstaafu wa United Sir Alex Ferguson katika kipindi cha karibuni amekuwa akimfukuzia Ronaldo ambaye inaaminika kutaka nafasi ya kuiwakilisha klabu hiyo ambayo ndiyo iliyomtengeneza mpaka kuwa mmoja wa wachezaji bora duniani. Rais wa Madrid Florentino Perez amenyesha kuwa na uhakika wa nyota huyo mwenye thamani ya paundi milioni 80 kusaini mkataba mwingine ambao utambakisha nchini humo lakini Ronaldo alikanusha habari hizo katika mitandao ya kijamii.

NEYMAR HAWEZI KUMFUNIKA MESSI BARCELONA - SYLVINHO.

BEKI wa zamani wa klabu ya Barcelona, Sylvinho anaamini kuwa Neymar atapata wakati mgumu wa kumfunika Lionel Messi kufuatia uhamisho wake kutoka klabu ya Santos kwenda kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu nchini Hispania. Mambo makubwa yanategemewa ka mshambuliaji huyo nyota wa kimataifa wa Brazil kufuatia kiwango bora anachokionyesha katika michuano ya Kombe la Shirikisho lakini Sylvinho anafikiri Neymar mwenye miaka 21 anaweza kuishia kucheza nyuma ya Messi kwenye klabu hiyo. Sylvinho anakiri kuwa Neymar ni mchezaji wa wachezaji bora kabisa kwasasa lakini suala la kumfunika Messi ambaye ameshinda tuzo nne za Ballon d’Or litakuwa suala gumu sana. Beki huyo aliendelea kusema kuwa kumekuwa na wachezaji wengi nyota wa Brazil kama Ronaldo, Romario na Ronaldinho lakini wote hao hawajapata kufikia kiwango alichonacho Messi kwasasa. Sylvinho amewahi kushinda mataji matatu ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona katika kipindi cha kuanzia mwaka 2004 mpaka 2009.

WIMBLEDON: FEDERER AKATAZWA KUVAA RABA ZAKE, AZARENKA AJITOA.

MCHEZAJI nyota wa tenisi Roger Federer kutoka Switzerland amekatazwa kutovaa viatu vyake ambavyo vina soli ya rangi ya chungwa baada ya kuonekana kama amevunja sheria za michuano ya Wimbledon ambayo wachezaji wanatakiwa kuvaa mavazi meupe kuanzia juu mpaka viatu. Federer mwenye umri wa miaka 31 bingwa mara saba wa michuano hiyo alikuwa amevaa viatu hivyo wakati wa mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo aliocheza Jumatatu. Katika sheria za michuano ya Wimbledon wachezaji wote ambao wanashiriki michuano hiyo wanatakiwa kuvaa mavazi meupe hata kama wakiwa katika mazoezi. Wakati huohuo mwanadada nyota katika mchezo huo anayeshika namba mbili katika orodha za ubora duniani Victoria Azarenka amelazimika kujitoa katika michuano hiyo dakika chache kabla ya kuanza kwa mchezo wake wa mzunguko wa pili. Azarenka raia wa Belarus ambaye ni bingwa wa michuano ya wazi ya Australia aliumia goti lake la kulia katikati ya mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Maria Jaoo Koehler wa Portugal lakini alifanikiwa kuendelea na kushinda mchezo huo.

USHINDI DHIDI YA URUGUAY UTAWAUNGANISHA WABRAZIL - SCOLARI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luis Felipe Scolari ameuelezea mchezo wa nusu fainali wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Uruguay kama mchezo muhimu huku akidai kuwa ushindi watakaopata huko Belo Horizonte utasaidia kuwaunganisha wananchi wa taifa hilo. Waandamanaji zaidi ya 100,000 wanatarajiwa kuandamana karibu na maeneo ya Uwanja wa Estadio Mineirao kabla ya mechi ya Jumatano lakini Shirikisho la Soka Duniani-FIFA limedai kuwa wana uhakika kwamba kutakuwa na ulinzi wa kutosha kupelekea mchezo huo kuchezwa kama ulivyopangwa. Scolari amesema mchezo huo ni muhimu timu yao lakini wanahitaji kupiga hatua moja zaidi kwa kuifunga Uruguay ili waweze kufika fainali kwasababu mashabiki wa soka wa nchi hiyo wamekuwa pamoja nao kwa kipindi chote. Kocha aliongeza kuwa wananchi wa taifa wanatakiwa kutafuta jinsi ya kufanya kazi pamoja na sio kupigana wenyewe kwa wenyewe, labda katika miaka mitano au kumi wanaweza kuwa wamepiga hatua kubwa ya kimaendelea.

FENERBAHCE WAFUNGIWA MIAKA MIWILI KWA KUPANGA MATOKEO.

SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA limeifungia klabu ya Fenerbahce ya Uturuki kushiriki michuano ya bara hilo kwa misimu miwili huku pia klabu ya Besiktas nayo ikifungiwa msimu mmoja. Klabu hizo mbili zenye maskani yake jijini Istanbul zimekumbwa na dhahma hiyo baada ya kukutwa na hatia ya upangaji wa matokeo mwishoni mwa msimu wa 2010-2011. Katika taarifa ya UEFA iliyotolewa baada ya uchunguzi ilidai kuwa Fenerbahce wamefungiwa kwa misimu miwili kushiriki michuano hiyo kuanzia msimu unaokuja huku wakitakiwa kutofanya kosa kama hilo kwa kipindi cha miaka mitano watakaoyokuwa chini uchunguzi. Fenerbahce ambao walikuwa washiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu unaokuja baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini humo sasa wataikosa michuano hiyo pamoja na msimu ujao kama wakifuzu tena kutokana na adhabu waliyopewa.

FIFA YAWASHUSHIA NYUNDO WAAMUZI WALIOKUTWA NA HATIA YA KUPEWA RUSHWA YA NGONO ILI WAPANDE MATOKEO.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limewapiga marufuku waamuzi wasaidizi wa Lebanon kuchezesha mechi za soka popote duniani ambao wamefungwa jela nchini Singapore kwa kukubali rushwa ya ngono ili wapange matokeo. Ali Eid na Abdallah Taleb tayari walikuwa wamefungiwa na Shirikisho la Soka la Asia-AFF huku kesi yao ikisikilizwa na sasa FIFA nao wameongeza adhabu hiyo na kuwa dunia nzima. Wawili hao walihukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela Juni 10 kwenye kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa April 4 mwaka huu huku mwamuzi Ali Sabbagh yeye akifungwa miezi sita siku iliyofuata. Waamuzi hao watatu walikuwa wamepangwa kuchezesha mechi ya AFF kati ya Tampines Rovers ya Singapore na East Bengal ya India mwezi April lakini walibadilishwa muda mchache kabla ya kuanza kwa mechi hiyo.

Tuesday, June 25, 2013

ANCELOTTI ACHUKUA MIKOBA YA MOURINHO MADRID.

KLABU ya Real Madrid imemtangaza rasmi Carlo Ancelotti raia wa Italia kuwa kocha mpya wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu. Kocha huyo wa zamani wa klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa atatangazwa rasmi mbele ya waandishi wa habari Jumatano kuchukua nafasi ya Jose Mourinho aliyekwenda kufundisha klabu yake ya zamani ya Chelsea. Katika mtandao wa wake klabu hiyo imedai kufikia hatua hiyo kutokana na uzoefu wa Ancelotti wa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika vilabu vikubwa kama Juventus, AC Milan, Chelsea na PSG. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 amekuwa akihusishwa kwenda Madrid toka Mourinho alipoondoka lakini alishindwa kuondoka mpaka PSG walipopata mbadala wake ambaye ni kocha wa zamani wa Ufaransa Laurent Blanc. Vyombo vya habari nchini Hispania vimedai Madrid wamelazimika kuilipa PSG euro milioni 4 kama kifuta jasho kwasababu Ancelotti alikuwa amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake kwenye klabu hiyo.

KUTOLEWA KWANGU SIO JAMBO LA KUTISHA - NADAL.

BINGWA wa michuano ya wazi ya Ufaransa, Rafael Nadal amedai kuwa kutolewa kwake katika mzunguko wa kwanza wa michuano ya Wimbledon kwa kufungwa na Steve Darcis sio jambo kubwa na kukataa kulaumu kutoka kwake kumetokana na majeruhi ya kifundo cha mguu ambayo yamemuweka nje kwa kipindi kirefu. Akihojiwa Nadal ambaye amewahi kunyakuwa michuano ya Wimbledon mara mbili amekiri kutolewa mapema katika michuano ni jambo gumu lakini kama limetokea haina jinsi kwani maisha yanaendelea. Nadal alimsifu mpinzani wake kwa kucheza vizuri na kushindwa kupata nafasi ya kucheza anavyotaka na kwasasa anaenda nyumbani kujipanga kuangalia alikosea wapi ili ajipange kwa ajili ya michuano ijayo. Kutolewa kwa Nadal kunampa ahueni Andy Murray wa Uingereza kusafishiwa njia ya kwenda mpaka fainali ya michuano hiyo kwasababu walikuwa wamepangwa kundi moja.

KOMBE LA DUNIA LITACHEZWA BRAZIL - VALCKE.

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amesema kuwa hawana mpango wa kubadili mahali patakapochezwa michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Valcke alibainisha kwamba michuano hiyo itafanyika nchini Brazil katika miji 12 kama ilivyopangwa na hakuna mpango mwingine wowote wa kuhamisha mashindano hayo kwenda sehemu nyingine. Kauli ya Valcke imekuja kufuatia maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea nchini humo wakati huu wa michuano ya Kombe la Shirikisho wakipinga gharama kubwa za matayarisho ya Kombe la Dunia wakati wananchi wake wana hali duni katika maisha yao ya kawaida. Valcke pia alipinga kauli ya Waziri wa Michezo wa Brazil, Aldo Rebelo aliyekuwa amekaa pembeni yake katika mkutano na waandishi wa habari aliyedai kwamba kuna nchi zimeonyesha nia ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kama Brazil ikijitoa. Katibu mkuu huyo amesema hajapokea ofa yoyote kutoka katika nchi yoyote duniani kutaka kuandaa michuano hiyo ya 2014 na kumuondoa hofu Rebelo ambaye alidai amesoma katika vyombo vya habari kwamba nchi za Marekani, Uingereza, Ujerumani na Japan zinamendea nafasi hiyo.

SHIRIKISHO LA SOKA LA ETHIOPIA LAMTOA KAFARA KATIBU MKUU WAKE.

SHIRIKISHO la Soka la Ethiopia-EFF limemtimua kibarua katibu mkuu wake wake baada ya kukiri kumtumia mchezaji kimakosa katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 hatua ambayo inaweza kuigharimu timu nchi hiyo kukatwa alama tatu. Kamati ya Utendaji ya EFF ilipiga kura za kumtimua katibu huyo aitwaye Ashenafi Ejigu lakini walipinga barua ya kujiuzulu kwa makamu wa rais wa shirikisho hilo Berhanu Kebede ambaye ndiye alikuwa akilaumiwa kutokana na mkanganyiko huo. Baadhi ya wajumbe na waandishi wa habari za michezo waliokuwepo katika mkutano huo walikuwa wakitaka uongozi mzima wa shirikisho hilo ujiuzulu kwa kile walichokiita uzembe. Rais wa EFF, Sahilu Gebremariam alikiri kuwa suala hilo ni la kizembe na wanapaswa wote kujiuzulu na kudai kuwa atafanya hivyo katika mkutano mkuu utakaofanyika Septemba mwaka huu. Akihojiwa kuhusiana na suala la kumchezasha mchezaji aliyepewa kadi mbili za njano kocha wa Ethiopia Sewnet Bishaw alijitetea kuwa anapokuwa uwanjani huwa hatumii karatasi na kalamu anachofanya yeye ni kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.

BALOTELLI NJE KOMBE LA MABARA.

DAKTARI wa timu ya taifa ya Italia, Enrico Castellacci ametangaza kuwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo Mario Balotelli hatacheza tena mechi zilizobakia za Kombe la Shirikisho na anatakiwa kurudi nyumbani kwa ajili ya kupata matibabu ya msuli aliyopata. Taarifa hiyo ya daktari inashabihiana na ile iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Italia-FIGC iliyobainisha kuwa nyota huyo asingecheza mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo dhidi ya Hispania baada ya vipimo vya x-ray kuonyesha kuwa amechanika msuli wa paja lake la kushoto. FIGC walikuwa na mategemeo kuwa Balotelli angerejea katika mchezo wa fainali au wa kutafuta mshindi wa tatu lakini Castellacci alifuta matumaini ya nyota huyo kurejea tena kumalizia michuano hiyo kwa jinsi alivyoumia. Daktari huyo aliendelea kusema kuwa tayari ameshazungumza na kocha wa timu hiyo Cesar Prandelli na kukubaliana kumruhusu mchezaji wake kwenda katika klabu yake ya AC Milan ili kupata matibabu zaidi.

Monday, June 24, 2013

RAMBIRAMBI MSIBA WA MATHIAS KISSA.

Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Cosmopolitan na Taifa Stars, Mathias Kissa (84) kilichotokea leo alfajiri (Juni 24 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam. Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani enzi zake, Kissa akiwa na timu ya Tabora alitamba katika michuano ya Kombe la Taifa wakati huo ikiitwa Sunlight Cup. Alikuwa akicheza katika nafasi ya ulinzi. Baadaye alijiunga na Cosmoplitan ya Dar es Salaam, na pia kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ambapo enzi zake akiwa na wachezaji kama Yunge Mwanansali wakiiwakilisha Tanganyika na baadaye Tanzania Bara walitamba katika michuano ya Kombe la Chalenji wakati huo ikiitwa Gossage, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima. Kissa ambaye alipata tuzo ya mchezaji bora wa karne kwa upande wa Tanzania, tuzo inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) alikuwa ndiye mchezaji msomi kupita wote wakati akichezea timu ya Taifa akiwa amehitimu elimu ya Darasa la Kumi. Kwa mujibu wa binti yake, Erica, marehemu ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi (stroke) alioupata miaka mitano iliyopita, na kisukari. Baadaye alipata kidonda ambacho ndicho kilichosababisha kifo chake.



Msiba uko nyumbani kwa marahemu, Masaki, Mtaa wa Ruvu karibu na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST). Maziko yatafanyika keshokutwa, Jumatano (Juni 26 mwaka huu) kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.



TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kisa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Cosmopolitan na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Kisa mahali pema peponi. Amina

ARSHAVIN MBIONI KUTUA ZENIT.

NAHODHA wa zamani wa timu ya taifa ya Urussi, Andrei Arshavin anategemewa kukamilisha taratibu za kurejea klabu yake ya zamani ya Zenit Saint Petersburg baada ya kuitumikia Arsenal kwa muda wa miaka mitano. Klabu hiyo ndio ilimuibua nyota huyo mwenye miaka 32 sasa wakati akiwa kinda kabla ya Arsenal kumuona na kumyakuwa. Arshavin ambaye alitua Zenit kwa mkopo kwa muda wakati wa msimu wa pili wa 2011-2012 kwasasa yuko huru baada ua kuachwa na Arsenal mwishoni mwa msimu huu. Nyota likuwemo katika kikosi cha Zenit kilichonyakuwa taji la Europa League mwaka 2008 na pia katika kikosi cha Urusi kkilichoshiriki michuano ya Ulaya 2008 kabla ya kwenda Arsenal.

CAMACHO CHALI CHINA.

CHAMA cha Soka nchini China-CFA kimetimua koha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Jose Antonio Camacho baada ya kuinoa timu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. Kocha huyo wa zamani wa Real Madrid na Hispania ametimuliwa baada ya nchi hiyo kushindwa kufanya vyema katika mechi tatu za kirafiki walizocheza Juni mwaka huu kikiwemo kipigo cha aibu cha mabao 5-1 kutoka kwa Thailand na kutolewa mapema katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwaka jana. Katika taarifa iliyotolewa na CFA imedai kuwa wamefikia uamuzi huyo baada ya pande zote kukubaliana kuvunja mkataba na tayari taratibu za kumpata mbadala wa Camacho zimeshaanza. Camacho aliteuliwa Agosti mwaka 2011 na katika kipindi chote hicho nchi hiyo imechapwa mechi 11 kati ya 20 kikiwemo kipigo cha mabao 8-0 kutoka kwa Brazil Septemba mwaka jana.

HONG MYUNG-BO KOCHA MPYA KOREA KUSINI.

CHAMA cha Soka cha Korea Kusini kimteua nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Hong Myung-bo kuwa kocha mpya wa timu hiyo. Hong ambaye alikuwa nahodha katika kikosi kilichoshika nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2002 iliyofanyika nchini kwao amechukua nafasi ya Choi Kang-hee ambaye amebwaga manyanga baada ya kuisadia nchi hiyo kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 kwa mara ya nane mfululizo. Hong alikua kocha wa kikosi cha nchi hiyo ambacho kilinyakuwa medali ya fedha kwenye michuano ya olimpiki iliyofanyika London mwaka jana ambapo kwa kipindi kirefu alitegemewa kuteuliwa wadhfa huyo. Choi alichukua mikoba ya kuinoa nchi hiyo mwaka 2011 na kipindi alidai kuwa kazi yake kubwa ni kuhakikisha wanapata nafasi ya kwenda Brazil kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2014 na baada ya hapo angejiuzulu.

MWAMUZI AKIRI KUWAPA ITALIA BAO LA MDONDO.

SHIRIKISHO la Soka Dunia-FIFA limedai kuwa mwamuzi Ravshan Irmatov amekiri kuwapa Italia bao pili kwa makosa wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho baina ya timu hiyo na Brazil ambao wenyeji walishinda kwa mwabao 4-2. Bao lililofungwa na Giorgio Chiellini lilikubaliwa ingawa mwamuzi alishapuliza filimbi kuashiria penati kwenda kwa Italia kitendo ambacho kiliwaudhi wachezaji wa Brazil na kuzonga mwamuzi juu ya uwamuzi wake huo. FIFA imesema kuwa mwamuzi huyo wa Uzbekstan baadae alikiri kufanya kosa hilo na kukiri kupuliza filimbi kuashiria penati. Lakini pamoja na kukiri kutenda kosa kwa mwamuzi huyo FIFA hawajathibitisha kama watamrudisha nyumbani au ataendelea kuchezesha mechi za nusu fainali ya michuano hiyo.

SUAREZ AWEKA REKODI URUGUAY.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Uruguay, Luis Suarez ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo wa Kombe la Shirikisho ambao waliibigiza Tahiti kwa mabao 8-1. Nyota anayekipiga katika klabu ya Liverpool ya Uingereza alifunga bao lake la 35 na 36 na kumpita mchezaji mwenzake wa nchi hiyo Diego Forlan wakati timu hiyo ilipokata tiketi ya kucheza nusu fainali dhidi ya wenyeji Brazil Jumatano huko Belo Horizonte. Mabao mengine ya Uruguay katika mchezo huo yalifungwa na Abel Hernandez aliyefunga manne huku Diego Perez na Nicolas Lodeiro wakifunga bao moja kila mmoja na kupelekea Tahiti chovu kuaga mashindano hayo na mzigo wa magoli 24 ya kufungwa. Uruguay ilitinga uwanjani bila kuwaanzisha nyota wake kama Forlan, Edinson Cavani na Suarez ambaye aliingia kipindi cha pili kwa ajili ya kuwapumzisha kwa ajili ya mchezo wa Jumatano.

TYSON GAY AFUZU MBIO ZA DUNIA ZA MITA 200 KWA KISHINDO.

MWANARIADHA nyota wa Marekani, Tyson Gay amefanikiwa kufuzu kushiriki mbio za mita 200 za duniani zitakazofanyika jijini Moscow kwa kutumia muda wa sekunde 19.74 ambao ni muda wa haraka zaidi kwa mwaka huu. Gay ambaye ni bingwa wa dunia wa mwaka 2007, sasa atachuana na mwanariadha mwenye kasi zaidi duniani kutoka Jamaica, Usain Bolt katika mbio za mita 100 na 200 kwenye mashindano ya dunia yatakayofanyika jijini Moscow, Urusi Agosti mwaka huu. Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka aliwashinda Isiah Young aliyeshika nafasi ya pili na Curtis Mitchell alishika nafasi ya tatu. Kwa upnde wa wanawake mwanadada nyota katika mbio fupi kutoka Marekani Allyson Felix alishindwa kutamba kwenye mbio za mita 200 baada kushindwa na Kimberlyn Duncan.

MABINGWA WA AFRIKA WAPIGWA CHINI KOMBE LA SHIRIKISHO.

MABINGWA wa Afrika, timu ya taifa ya Nigeria maarufu kama Super Eagles imeondolewa kwenye michuano ya kombe la mabara baada ya kutandikwa mabao 3-0 na mabingwa wa dunia Hispania. Mabao mawili ya beki wa klabu ya Barcelona, Jordi Alba na moja la mshambuliaji wa Chelsea, Fernando Torres yalitosha kuzamisha jahazi la Nigeria ambao wameshinda mechi moja pekee dhidi ya Tahiti wikiendi iliyopita. Nigeria wameyaaga mashindano hayo baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi B wakiwa na pointi tatu nyuma ya Uruguay walioko kwenye nafasi ya pili wakiwa na point sita. Hispania ni vinara wa kundi B wakiwa wamemaliza hatua ya makundi na ushindi wa asilimia mia moja wakiwa na pointi tisa ambapo sasa watakwenda kuwavaa Italia katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo hapo siku ya siku ya alhamisi mjini Fortaleza. Uruguay wao wametoa kipigo cha magoli 8-0 kwa timu chovu kwenye michuano hiyo Tahiti ambao wameondoka na jumla ya magoli 24 ya kufungwa na kupata bao moja pekee walipocheza na Nigeria. Kwa matokeo hayo, Uruguay watacheza nusu fainali dhidi ya wenyeji Brazil, hapo siku ya jumatano.


Sunday, June 23, 2013

JAPAN INAHITAJI KUWA NA WACHEZAJI WENGI ZAIDI KATIKA LIGI KUBWA - HONDA.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Japan, Keisuke Honda anaamini kuwa wachezaji wengi zaidi wa timu ya taifa ya nchi hiyo wanahitaji kucheza katika ligi kubwa duniani baada ya timu hiyo kupata kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mexico na kuenguliwa katika michuano ya Kombe la Shirikisho inayoendelea nchini Brazil. Mabao mwili ya Mexico yaliyofungwa na Javier Hernandez yalitosha kuwapa ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa kundi A na kufanikiwa kusonga mbele pamoja na bao la dakika za majeruhi la kufutia machozi la Japan lililofungwa na Shinji Okazaki. Na baada ya kipigo hicho Honda ambaye anakipiga katika klabu ya CSKA Moscow ya Urusi anaamini kuwa wachezaji wenzake wanahitaji kutafuta timu katika vilabu vikubwa dunia ili waweze kupata uzoefu utakaowawezesha kuongeza ushindani zaidi katika timu hiyo. Honda amesema walifungwa na Italia ambao walipata siku mbili pekee za mapumziko hivyo wanahitaji akili na nguvu kama hizo kushinda katika hali yoyote na hayo yanaweza kutokea kama wachezaji wa nchi hiyo watacheza katika vilabu vikubwa.

BOLT AJITOA MASHINDANO YA OSTRAVA.

MWANARIADHA nyota wa Jamaica, Usain Bolt ametangaza kujitoa katika mashindano ya Golden Spike yaliyokuwa yafanyike Juni 27 jijini Ostrava, Jamhuri ya Czech, na badal yake ameamua kubakia nyumbani na kufanya mazoezi zaidi. Katika taarifa yake aliyotoa mapema leo, Bolt aliwaomba radhi mashabiki wake wa Ostrava kwa kutokwenda huko kushiriki mbio hizo na badala yake anataka kuongeza juhudi zaidi katika mazoezi akiwa na kocha wake nchini Jamaica kabla ya kusafiri kwenda Ulaya. Katika mbio za Ostrava Bolt alikuwa amepangwa kukimbia katika mbio za mita 400 kupokezana vijiti pamoja na nyota mwingine wa Jamaica, Yohan Blake ambaye naye alijitoa mapema kutokana na majeraha. Bolt, Blake, Michael Frater na Nesta Carter walifanikiwa kuweka rekodi mpya ya dunia katika mbio hizo kwa kutumia muda wa sekunde 36.84 katika mashindano ya olimpiki yaliyofanyika jijini London, Uingereza mwaka jana.

SHARAPOVA AMPONDA WILLIAMS KWA KAULI YAKE.

MWANADADA nyota katika tenisi anayeshika namba mbili katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanawake, Maria Sharapova amemponda hasimu wake Serena Williams na kuchunga kauli zake kwa kutoropoka hovyo. Williams kutoka Marekani ambaye ni bingwa mtetezi wa michuano ya Wimbledon ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho hivi karibuni alilazimika kuomba radhi kwa kauli aliyoitoa kuhusiana na kesi ya ubakaji inayomhusu msichana wa miaka 16 huko jijini Ohio. Sharapova ambaye ni raia wa Urusi amesema amesikitishwa na kauli aliyotoa Williams ambaye anashika namba moja katika orodha kuhusiana na kesi hiyo. Williams alimfunga Sharapova na kutwaa ubingwa wa michuano ya wazi ya Ufaransa mapema mwezi huu na wawili hao hawawezi kukutana mapema katika michuano ya Wimbledon mpaka fainali.

FORLAN NA WENZAKE WACHELEWA MAZOEZINI KWA KUKWAMA KWENYE LIFTI BRAZIL.

MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya taifa ya Uruguay, Diego Forlan na wachezaji wenzake wawili wa tmu hiyo wamekumbwa na kadhaa ya kukwama katika lifti ya hoteli waliyofikia kwa zaidi ya dakika 30 kitendo ambacho kilipelekea kuchelewa kuanza kwa mazoezi ya timu hiyo ili kujiwinda na mchezo wao wa mwisho wa Kombe la Shirikisho unaotarajiwa kupigwa leo. Forlan, Diego Perez, Sebastian Eguren pamoja na mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi walikuwa wakishuka chini kutoka ghorofa ya saba kwenye hoteli hiyo iliyopo jijini Recife lakini ilikwama ghafla na kushindwa kufanya kazi. Perez alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai walikwama kwa zaidi ya nusu sasa lakini walikuwa wanaweza kupumua vizuri na mwanga wa kutosha ulikuwepo ndani ya lifti hiyo. Uruguay inatarajia kumaliza mchezo wake wa mwisho wa kundi B na timu vibonde ya Tahiti baadae leo katika mji huo uliopo kaskazini mwa nchi hiyo.

Saturday, June 22, 2013

MCHEZAJI WA CROATIA AFIA UWANJANI.

MCHEZA soka wa Croatia Alen Pamic mwenye umri wa miaka 23 ameanguka ghafla na kufariki uwanjani wakati mchezo ukiendelea. Mchezaji huyo ambaye alikuwa kicheza katika klabu ya NK Istra 1961 inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo amekuwa na hitoria ya matatizo ya moyo na ameshawahi kuanguka zaidi ya mara tatu katika kipindi cha nyumba kabla ya kufariki. Februari mwaka huu alianguka na kupoteza fahamu katika mechi baina ya timu yake dhidi ya timu ya Lokomotiva lakini pamoja na tatizo hilo alisisitiza kuendelea kucheza soka na daktari alimruhusu. Pamic ni mtoto wa mchezaji wa kimataifa wa zamani wan chi hiyo aitwaye Igor ambaye kwasasa ndiye kocha wa Istra.

PSG YAMCHUKUA BLANC KUZIBA PENGO LA ANCELOTTI ANAYETAKA KUONDOKA.


KLABU ya Paris Saint-Germain-PSG imefikia makubaliano na Laurent Blanc ili aje kuwa meneja mpya wa klabu hiyo ambao ndio mabingwa wa Ligi Kuu nchini Ufaransa maarufu kama Ligue 1 msimu uliopita. Blanc mwenye umri wa miaka 45 amekaa bila kibarua toka alipoacha kuinoa timu ya taifa ya Ufaransa kufuatia kuenguliwa katika hatua ya robo fainai katika michuano ya Ulaya mwaka jana. Blanc ambaye alikuwa beki enzi zake akicheza soka amewahi kufundisha katika klabu ya Bordeaux kuanzia mwaka 2007 mpaka 2010 na kuisaidia timu hiyo kunyakuwa taji la Ligue 1 mwaka 2009. Hatua hiyo ya PSG imekuja kufuatia kocha wa sasa wa klabu hiyo Carlo Ancelotti kuomba kuondoka baada ya kuinoa kwa miezi 18 huku kukiwa na tetesi kuwa anataka kwenda Real Madrid ya Hispania.

BOLT AFUZU MICHUANO YA DUNIA.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt amefanikiwa kufuzu kushiriki mbio za mita 100 za dunia kwa kushinda michuano ya mchujo iliyofanyika nchini kwake kwa kutmia muda wa sekunde 9.94. Katika mbio hizo Bolt alianza taratibu lakini aliongeza kasi zaidi alipofikia mita 50 na kumkumpita Nickel Ashmeade na kujihakikishia nafasi ya kwenda jijini Moscow katika michuano ya dunia ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Agosti 10 mpaka 18. Mjamaica mwingine mkali katika mbio Yohan Blake yeye alishindwa kushiriki mbio za kuvuzu za mita 200 kwasababu ya majeraha lakini atashiriki mbio za mita 100 kama bingwa mtetezi baada ya Bolt kuenguliwa katika mbio hizo kwenye michuano ya dunia iliyofanyika jijini Daegu mwaka 2011. Kwa upnde wa Marekani nyota wa mbio hizo Tyson Gay naye amefanikiwa kukata tiketi ya kwenda Moscow baada ya kumshinda Justin Gatlin katika mbio za mita 100 kwa kutuimia muda wa sekunde 9.75 ukiwa ni muda wake wa haaka zaidi kwa mwaka huu.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

LUHENDE AONGEZWA KIKOSINI TAIFA STARS
Beki wa Yanga, David Luhende ameongezwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini. Kocha Kim Poulsen amesema kutokana na uamuzi huo wa kumuongeza beki huyo wa kushoto amemuondoa mchezaji mmoja kwenye kikosi chake. Mchezaji huyo ni mshambuliaji Zahoro Pazi wa JKT Ruvu. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager sasa itaingia kambini kwenye hoteli ya Tansoma jijini Dar es Salaam, Julai 3 mwaka huu badala ya Julai 4 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali. Mechi ya Uganda itachezwa Julai 13 mwaka huu, saa 9 kamili alasiri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati ile ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye jijini Kampala, Uganda. Wachezaji wanaotakiwa kambini ni Aggrey Morris (Azam), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruni Chanongo (Simba), John Bocco (Azam), Juma Kaseja (Simba), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar) na Kelvin Yondani (Yanga). Wengine ni Khamis Mcha (Azam), Mrisho Ngasa (Simba), Mudathiri Yahya (Azam), Mwadini Ali (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Shomari Kapombe (Simba), Simon Msuva (Yanga) na Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).



TIMU NNE KUCHEZA NUSU FAINALI RCL
Timu nne zimefuzu kucheza hatua ya nne (nusu fainali) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) baada ya kushinda mechi zao za hatua ya tatu ya michuano hiyo itakayotoa washindi watatu watakaocheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao. Katika hatua hiyo Polisi Jamii ya Mara itaikaribisha Kimondo SC ya Mbeya kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma wakati Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Friends Rangers ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Azam Chamazi. Mechi za kwanza zitachezwa Juni 23 mwaka huu wakati zile za marudiano zitafanyika kwenye viwanja vya Sokoine jijini Mbeya na Kambarage mjini Shinyanga, Juni 30 mwaka huu. Kwenye hatua ya tatu ya RCL, Friends Rangers iliing’oa Kariakoo ya Lindi kwa jumla ya mabao 2-0, Stand United FC ikaitoa Machava FC ya Kilimanjaro kwa mabao 2-1, Kimondo SC ikaishinda Njombe Mji mabao 6-5 wakati Polisi Jamii iliitambia Katavi Warriors kwa mabao 7-6. Hatua ya mwisho ya ligi hiyo itachezwa Julai 3 mwaka huu kwa mechi za kwanza wakati zile za marudiano zitakuwa Julai 7 mwaka huu.

PRANDELLI AOMBA RADHI KWA KAULI YAKE DHIDI YA BALOTELLI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Italia, Cesar Prandelli ameomba radhi kwa kauli yake aliyosema juu ya mshambuliaji nyota wa klabu Mario Balotelli akidai kuwa nyota huyo alikuwa mchezaji pekee aliyeruhusiwa kutoka hotelini kwasababu ni mweusi. Washauri wa mambo ya kiusalama waliwaambia wachezaji wan chi hiyo kutotoka hotelini wakati maandaano yakiendelea kurindima katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho. Prandelli amesema nyota huyo nayekipiga katika klabu ya AC Milan aliruhusiwa kutoka kwasababu rangi yake ni tofauti na wachezaji wenzake lakini baadae aliomba radhi na kudai kuwa alikuwa akitania. Balotelli aliruhusiwa kutoka hotelini kwa ajili ya kwenda kufanya shughuli za kijamii kuwasaidia watoto wanaotoka katika sehemu masikini katika mji wa Salvador nchini Brazil. Italia inatarajiwa kukwaana baadae leo na wenyeji wa michuano hiyo Brazil ili kutafuta bingwa wa kundi lao kabla ya kwenda katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Friday, June 21, 2013

MMOJA AFA KATIKA MAANDAMANO BRAZIL.

RAIS wa Brazil, Dilma Rousseff ameitisha mkutano wa dharura leo ikiwa ni siku moja baada ya muandamanaji kuuwawa na wengine zaidi ya milioni 1.25 wakiendelea kuandamana nchi nzima wakidai huduma nzuri kwa jamii. Pilikapilika hizo za uandamanaji ambazo mara nyingine zinaleta vurugu kubwa, zinafanyika wakati nchi hiyo iikiwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Shirikisho inayoendelea ambayo huchezwa mwaka mmoja kabla ya Kombe la Dunia. Raia wengi wa Brazil wamekuwa wakigadhabika juu ya gharama kubwa za maandalizi zilizotumika kwa ajili ya kuandaa na Kombe la Dunia 2014 na michuano ya olimpiki kipindi cha kiangazi itakayofanyika jijini Rio de Janeiro 2016.  Jijini Rio polisi wamekuwa wakipambana na waandamanaji hao ambao hujikusanya karibu na Uwanja wa Maracana ambapo wamekuwa wakilazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto ili kuwatawanya.

MARCEDES WAFUNGIWA KUFANYA MAJARIBO MSIMU HUU.

TIMU ya Marcedes imefungiwa kufanya majaribio kwa madereva wake chipukizi kwa mwaka huu pamoja na kupewa onyo kali kwa kosa la kufanyia majaribio magurudumu ya Pirelli kinyume cha utaratibu. Kampuni hiyo ya magurudumu ya Pirelli nayo pia imepewa onyo kwa kutumia gari jipya linalotumiwa katika mashindano ya langalanga na dereva Lewis Hamilton katika majaribio ya siku tatu waliyofanya nchini Hispania mwezi uliopita. Kamati maalumu ya uchunguzi wa suala hilo iliyoundwa na Chama cha Kimataifa cha Langalanga-FIA kilichukua hatua hiyo baada ya kuwakuta Mercedes na hatia ya kutenda kosa hilo ambalo ni kinyume cha utaratibu wa mashindano hayo. Katika sheria za langalanga timu yoyote hairuhusiwi kufanya majaribio magurudumu kwa zaidi ya kilometa 1000 pindi msimu wa mshindano hayo unapoanza na hata wakifanya majaribio hayo hawapaswi kutumia gari zao mpya zinazotumika katika msimu husika.

PIRLO KUIKOSA BRAZIL.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Italia, Andrea Pirlo anatarajiwa kukosa mchezo wa mwisho wa kundi A dhidi ya wenyeji Brazil kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kupata majeraha ya msuli katika mguu wake wa kulia. Kocha wa viungo wa nchi hiyo, Enrico Castellacci amesema anamatumaini Pirlo anaweza kurejea katika mechi ya nusu fainali lakini ukijumuisha na kukosekana kwa Daniele De Rossi ambaye naye pia atakosa mchezo wa mwishoni itabidi kocha wa timu hiyo Cesar Prandelli abadili kikosi chake. Italia ilitinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibugiza Japan ka mabao 4-3 na kufikisha alama sawa na Brazil katika kundi lao ambapo mechi ya mwisho ndio itakayoamua nani atasonga mbele kama mshindi wa kundi. Timu zote mbili itabidi zipange vikosi vyao kamili ili kutafuta ushindi na kuepuka kukutana na bingwa wa dunia Hispania katika hatua ya nusu fainali.

HISPANIA WAPORWA HOTELINI KWAO WAKATI WAKIWA KATIKA MECHI.

VYOMBO vya habari nchini Hispania vimeripoti kuwa wachezaji sita wa timu ya taifa ya Hispania wameibiwa fedha zao katika vyumba walivyofikia katika hoteli moja jijini Recife wakati wanacheza mchezo wao ufunguzi wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Uruguay. Mojawapo ya wachezaji waliokumbwa na mkasa huo ni beki wa Barcelona, Gerard Pique ambaye aligundua kaibiwa wakati aliporejea chumbani kwake baada ya mchezo dhidi ya Uruguay ambao walishinda kwa mabao 2-1. Msemaji wa Shirikisho la Soka Dunia-FIFA, Pekka Odriozola alikiri kupata taarifa hizo lakini wameziachia mamlaka husika kushughulikia na kisha kuwaletea taarifa kamili. Hispania ambao wako kundi B jana wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa kishindi baada ya kuishindilia Tahiti kwa mabao 10-0 wakati wawakilishi pekee wa Afrika kwenye mashindano hayo walishindwa kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Uruguay.

MIAMI HEAT YANYAKUWA TAJI LA NBA KWA MARA YA PILI MFULULIZO.

TIMU ya mpira wa kikapu Miami Heat imefanikiwa kutwaa taji la pili mfululizo la Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani-NBA baada ya kuifunga timu ya San Antonio Spurs kwa vikapu 95-88 katika fainali ya saba iliyofanyika katika Uwanja wa American Airlines uliopo jijini Miami, Florida. San Antonio walibakiza kidogo kulinyakuwa taji hilo Jumanne kabla ya Miami kupambana na kushinda hivyo kuzifanya timu hizo kutoka sare ya kufunga 3-3 katika fainali ya sita kati ya saba ambazo wanatakiwa kucheza. 
Katika mchezo wa Alfajiri kuamkia leo nyota wa timu ya Heat, LeBron James mwenye umri wa miaka 28 alifanikiwa kuisadia vyema timu yake kwa kufunga vikapu 37 na kutajwa kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi katika ligi hiyo kwa mara ya pili mfululizo. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo James ambaye aliingia matatani baada ya kudaiwa kucheza chini ya kiwango katika mechi muhimu amesema anajisikia fahari kunyakuwa taji hilo katika uwanja wao wa nyumbani na yote yaliyopita yanabaki kuwa historia.

Thursday, June 20, 2013

NEYMAR AUNGA MKONO MAANDAMANO YA BRAZIL.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Brazil, amejiunga na wachezaji wenzie wa timu ya taifa ya nchi kuunga mkono maandamano yanayoendelea nchi nzima na kuikosoa serikali ya rais wa nchi hiyo Dilma Rousseff kwa kushindwa kutoa huduma za kijamii za kutosha. Neymar aliandika katika mtandao wake wa kijamii saa chache kabla ya Brazil haijachuana na Mexico katika mechi yao ya pili ya Kombe la Shirikisho akidai kuwa nasikitishwa na kinachoendelea nchini humo. Neymar aliendelea kuandika kuwa mara nyingi amekuwa na imani kwamba haina haja ya kuingia mtaani kuandamana ili kudai mazingira mazuri kwenye masuala ya usafiri, afya, elimu na usalama kwakuwa suala hilo ni jukumu la serikali. Nchi hiyo imekuwa ikikumbwa na maandamano makubwa wiki hii juu ya dola bilioni tano zilizotumika kwa ajili ya kuandaa michuano ya Kombe la Shirikisho na Kombe la Dunia litakalofanyika mwaka ujao wakati hakuna fedha fedha zozote zilizotengwa kwa ajili ya kuendeleza elimu na afya. Waandamanaji hao pia wamekuwa wakipinga nauli kubwa kwenye vyombo vya usafirishaji kwa kudai kuwa hatua ya kufanya hivyo ni ufisadi.

BLAKE KUTOSHIRIKI MBIO ZA DUNIA ZA MITA 200.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Yohan Blake anatarajiwa kutoshiriki mashindano ya dunia yam bio za mita 200 baada ya kujitoa katika mbio za kufuzu zitakazofanyika mwishoni mwa wiki hii kwasababu ya kusumbulia na msuli. Blake mwenye umri wa miaka 23 alikumbwa na majeraha hayo April mwaka huu na mpaka sasa bado hajapona sawasawa. Akiwa kama bingwa mtetezi wa mbio za mita 100 zitakazofanyika jijini Moscow, Blake hatahitajika kukimbia mbio za mchujo. Mwanariadha mwenzake Usain Bolt yeye tayari ameshavuzu moja kwa moja mbio za mita 200 kwakuwa ndio bingwa mtetezi lakini atalazimika kukimbia mbio za mchujo za mita 100 baada ya kuenguliwa katika michuano ya dunia ya mbio hizo kwa kudanganya jijini Daegu mwaka 2011.