Tuesday, June 25, 2013

KOMBE LA DUNIA LITACHEZWA BRAZIL - VALCKE.

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amesema kuwa hawana mpango wa kubadili mahali patakapochezwa michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Valcke alibainisha kwamba michuano hiyo itafanyika nchini Brazil katika miji 12 kama ilivyopangwa na hakuna mpango mwingine wowote wa kuhamisha mashindano hayo kwenda sehemu nyingine. Kauli ya Valcke imekuja kufuatia maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea nchini humo wakati huu wa michuano ya Kombe la Shirikisho wakipinga gharama kubwa za matayarisho ya Kombe la Dunia wakati wananchi wake wana hali duni katika maisha yao ya kawaida. Valcke pia alipinga kauli ya Waziri wa Michezo wa Brazil, Aldo Rebelo aliyekuwa amekaa pembeni yake katika mkutano na waandishi wa habari aliyedai kwamba kuna nchi zimeonyesha nia ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kama Brazil ikijitoa. Katibu mkuu huyo amesema hajapokea ofa yoyote kutoka katika nchi yoyote duniani kutaka kuandaa michuano hiyo ya 2014 na kumuondoa hofu Rebelo ambaye alidai amesoma katika vyombo vya habari kwamba nchi za Marekani, Uingereza, Ujerumani na Japan zinamendea nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment