Friday, May 29, 2015

SOUTHAMPTON YAKATAA OFA KIDUCHU YA LIVERPOOL KWA AJILI YA BEKI WAO CLYNE.

KLABU ya Southampton imekataa ofa ya paundi milioni 10 za Liverpool kea ajili ya kumsajili beki wao wa kulia Nathaniel Clyne. Clyne mwenye umri wa miaka 24, amekuwa akiwindwa na Liverpool kutokana na Glen Johnson mwenye umri wa miaka 30 kukaribia kumaliza mkataba wake Anfield. Liverpool wanatarajiwa kuboresha ofa yao kwa ajili ya kumsajili nyota huyo ambaye amebakisha mkataba wa mwaka mmoja na Southampton. Liverpool inawawinda mshambuliaji wa Burnley Danny Ings na kiungo wa Manchester City James Milner.

WILSHERE APANIA TAJI LA FA.

KIUNGO wa Arsenal, Jack Wilshere anaamini msimu wao utaamuliwa vyema kama wakifanikiwa kutetea taji lao la Kombe la FA. Arsenal imemaliza katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu na kiungo huyo amesema utakuwa msimu mzuri kama wakifanikiwa kuichapa Aston Villa kesho katika mchezo wa fainali utakaofanyika katika Uwanja wa Wembley. Wilshere mwenye umri wa miaka 23, amesema lengo lilikuwa kumaliza katika nafasi ya pili lakini hilo halikufanikiwa hivyo itakuwa vyema zaidi kama wakimaliza kwa kubeba walau Kombe la FA. Kiungo huyo alikosa sehemu kubwa ya msimu, kufuatia kuumia kifundo cha mguu katika mchezo dhidi ya Manchester United Novemba mwaka jana na kukiri kuwa alikuwa mpweke katika kipindi chote alipokuwa peke yake gym wakati wenzake wanafanya mazoezi.

PEPE ADAI BENITEZ BONGE LA KOCHA.

BEKI mahiri wa Real Madrid, Pepe amemtaja Rafa Benitez kama kocha mkubwa baada ya kukaribia kutua Santiago Bernabeu. Benitez alitangaza jana kuwa ataachia nafasi yake ya ukocha katika klabu ya Napoli, huku Madrid wakitarajiwa kumthibitisha kama mbadala wa Carlo Ancelotti wiki ijayo. Pepe anaamini kocha huyo wa Hispania ndio atakuwa chaguo la juu kwa Madrid ingawa mpaka sasa hakuna chochote kilichpafikiwa kati ya pande hizo mbili. Akihojiwa Pepe amesema benitez ni kocha mkubwa ambaye amefanya kazi nzuri popote alipokwenda haswa kaika klabu ya Liverpool. Hata hivyo Pepe alienmdelea kudai kuwa kwasasa bado ni mazungumzo katika vyombo vya habari, wacha waone kitakachotokea siku zijazo.

CITY YAHIRISHA MCHEZO WAKE DHIDI YA HOUSTON DYNAMO.

KLABU ya Manchester City imeahirisha mchezo wake wa kirafiki dhidi ya timu ya Houston Dynamo ya Marekani uliokuwa uchezwe jana baada ya mafuriko yalioacha uwanjani kushindwa kuchezeka. City walisafiri kwenda Houston baada ya kushinda bao 1-0 katika mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Toronto FC Jumatano, wakati mvua kubwa iliponyesha katika miji ya Texas na Oklahama. Pamoja na jitihada za wahudumu wa uwanja wa Dynamo, mkaguzi wa uwanja alidai kuwa uwanjani huyo hautakuwa salama kuchezewa. City sasa watasafiri kwenda jijini New York kutizama mchezo wa klabu yao nyingine ya New York City FC itakayovaana na Houston katika mchezo wa Ligi Kuu ya Marekani utakaofanyika katika Uwanja wa Yankee, Jumamosi hii.

PALESTINA WAZIDI KUIKOMALIA ISRAEL.

WAANDAMANAJI wa Kipalestina walimkatisha Sepp Blatter na kutaka kadi nyekundu kwa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA wakati wa mkutano mkuu wa leo. Blatter ambaye anatarajiwa kuchaguliwa tena kuongoza FIFA kwa kipindi cha tano, alikuwa akizungumza wakati waandamanaji hao walipovamia ukumbi mkubwa wa mikutano wa Hallenstadion jijini Zurich. Wakati watu wakiwa hawajaleta vurugu zozote, Blatter aliwataka watu wa usalama kushughulikia tatizo hilo kabla hajaendelea na mkutano kea kuwakumbuka watu waliokufa katika soka kwa mwaka mzima. Baada ya hapo Blatter aliomba ukimya wa dakika moja katika kumbukumbu ya miaka 30 ya tukio lililotokea Uwanja wa Heysel ambapo watu 39 walifariki dunia. Maofisa wa Palestina hivi karibuni wameitaka FIFA kuisimamisha Israel kwa kile walichodai mamlaka za nchi hiyo kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji katika eneo la ukanda ukanda wa Gaza wa mechi za soka.

HERNANDEZ ALIMWA ADHABU KUFUATIA KUMPIGA PHIL JONES.

CHAMA cha Soka cha Uingereza-FA kimemlima adhabu ya kutocheza mechi tatu mshambuliaji wa Hull City Abel Hernandez kea kosa la kumpiga beki wa Manchester United Phil Jones katika mchezo baina ya timu hizo uliochezwa Jumapili iliyopita. Hernandez alifanya tukio hilo katika dakika ya 70 lakini halikuonwa na mwamuzi katika mchezo ambao Hull walipata sare ya bila kufungana ambayo iliwashusha daraja. Katika taarifa yake, FA ilithibitisha taarifa hizo na kudai kuwa Hernandez anatarajiwa kuanza kutumikia adhabu yake kuanzia msimu ujao. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya nyota huyo kukubalia kutenda kosa hilo ambalo pamoja na kuwa halikuonwa na mwamuzi lakini picha za video zilinasa. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay alijiunga na Hull akitokea Palermo ya Italia mwaka jana kea kitita cha paundi milioni tisa lakini ameshindwa kung’aa baada ya kufunga mabao manne katika mechi 25 alizocheza za mashindano yote.

URUGUAY WATAKA SUAREZ AFUTIWE ADHABU.

UMOJA wa wachezaji nchini Uruguay umedai kuwa adhabu ya kufungiwa mechi tisa Luis Suarez kwa kosa la kumng’ata nyota wa kimataifa wa Italia Giorgio Chiellini katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana nchini Brazil inapaswa kuondolewa. Umoja unataka suala hilo kujadiliwa tena katika mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA utakaofanyika leo jijini Zurich, Uswisi ambapo pamoja na mambo mengine pia utafanyika uchaguzi mkuu wa kutafuta rais mpya. Hatua hiyo ya kuhoji adhabu ya Suarez inakuja kufuatia tuhuma nzito za rushwa zinalikabilishi shirikisho hilo baada ya maofisa kadhaa kukamatwa. Mshauri wa masuala ya kisheria wa umoja huo, Ernesto Liotti amesema tuhuma za rushwa zinazolikabili shirikisho hilo zinathibitisha ukweli kuwa baadhi ya maamuzi yaliyofanyika katika kipindi cha karibuni hayakuwa ya haki. Liotti amesema hawana ushahidi kuwa adhabu aliyopewa Suarez ilitolewa chini ya shinikizo la viongozi hao waliokamatwa na rushwa lakini hakuna chochote kinachowahakikishia tofauti. Liotti aliendelea kudai kuwa mmoja wa maofisa waliokamatwa, ambaye in rais wa Shirikisho la Soka la Venezuela Rafael Esquivel alikuwepo katika kamati ya nidhamu iliyotoa adhabu kea Suarez.

Thursday, May 28, 2015

SINA MPANGO WA KUAJILI – MOURINHO.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho amesema kipaumbele kikubwa katika usajili wa majira ya kiangazi kitakuwa ni kuhakikisha anabaki na kikosi chake kilichoshinda taji la Ligi Kuu na kutosajili wachezaji wapya. Mourinho amekiri kuwa itakuwa vigumu kukiimarisha kikosi chake hicho zaidi ya kilivyo hivi sasa. Chelsea walitawadhwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu msimu wa 2014-2015 huku wakiwa wamebakisha michezo mitatu mkononi. Akihojiwa Mourinho anataka kutetea taji lake hilo msimu ujao lakini hadhani kama wachezaji wapya watamsaidia kufanikisha adhma yake hiyo kulinganisha na alionao sasa katika kikosi chake. Mabingwa hao hivi sasa wako Bangkok, Thailand kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya wachezaji nyota wa Ligi Kuu ya nchi hiyo utakaofanyika katika Uwanja wa Rajamangala, Jumamosi hii.

AYEW KUTIMKIA ROMA.

KIUNGO wa kimataifa wa Ghana, Andre Ayew anatarajiwa kukamilisha mkataba wa miaka minne na klabu ya AS Roma akiwa kama mchezaji huru. Ayew alimaliza mkataba wake na klabu ya Olympique Marseille msimu huu, na ameamua kuchagua kwenda kwa wakongwe hao wa Italia badala ya Ligi Kuu na Bundesliga. Inaaminika kuwa Ayew aliwapa masharti Roma kuwa aataka kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya sharti ambalo limefanikishwa. Taarifa zinadai kuwa Ayew atakuwa akikunja kitita cha euro milioni tatu kila mwaka katika mkataba huo wa miaka minne atakaosaini. Ayew ameichezea Marseille kwa zaidi ya 10, klabu ambayo ndio imemkuza toka akiwa mdogo.

MICHUANO YA AFRIKA YA U-23 KUANZA KUTIMUA VUMBI NOVEMBA 28.

SHIRIKISHO la Soka la Afrika-CAF, limethibitisha kuwa Novemba 28 mwaka huu kuwa tarehe rasmi ya michuano ya Ubingwa wa Afrika kwa vijana chini ya miaka 23, itakayofanyika huko Senegal. Michuano hiyo ya pili ya vijana mara ya kwanza ilikuwa imepangwa kufanyika huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lakini ilibadilishwa baada ya wenyeji hao kujitoa kutokana na kukabiliwa na uchaguzi mkuu kipindi hicho. Senegal ambao hivi karibuni waliandaa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 20, ndio wamepewa uenyeji wa kuandaa michuano hiyo ambayo wachezaji wake watakuwa wale waliozaliwa baada ya Januari mosi mwaka 1993. Kamati ya utendaji ya CAF ambayo iko jijini Zurich kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA ilkutana juzi kupitisha tarehe hiyo. Michuano hiyo sasa inatarajiwa kufanyika katika miji miwili ya Dakar na M’bour kuanzia Novemba 28 mpaka Desemba 12.

MARSEILLE YAITAKA CLUB AFRICAIN KUTOA EURO MILIONI MOJA.

KLABU ya Olympique Marseille ya Ufaransa, imeitaka Club Africain kulipa kitita cha euro milioni moja kama wanataka kumnunua Saber Khalifa kwa mkataba wa moja kwa moja. Khalifa alijiunga na Club Africain kwa mkopo akitokea Marseille na kuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu wa timu hiyo. Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Tunisia, Africain ilituma ombi lake Marseille kutaka kumnunua Khalifa moja kwa moja hatua ambao wamejibiwa kwa kutakiwa kutoa euro milioni moja. Mkopo wa Khalifa na Club Africain unatarajiwa kumalizika mwishoni msimu huu, huku yeye mwenyewe akidai hajui hatma yake kwasasa.

GERRARD KUCHEZA MECHI YAKE YA KWANZA GALAXY JULAI 11.

NAHODHA Liverpool anayeondoka, Steven Gerrard anatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza akiwa na klabu yake mpya ya Los Angeles Galaxy Julai 11 mwaka huu. Kiungo huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 34, anatarajia kuwepo katika mchezo wa nyumbani dhidi ya klabu ya America ya Mexico michuano ya Kombe la Kimataifa. Ofisa mkuu wa Galaxy, Bruce Arena wanategemea Gerrard kuwepo kabla ya Julai 11 kwa ajili ya kufanya mazoezi na wenzake kwa ajili ya mchezo huo. Kwasasa Gerrard yuko katika mapumziko ya msimu na wachezaji wenzake wa Liverpool, Dubai lakini anatarajiwa kuelekea nchini Marekani kuanza changamoto mpya na anatarajiwa kuwa mchezaji rasmi wa Galaxy kuanzia Julai 8 mwaka huu. Gerrard ameasaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo baada ya kutangaza Januari kuwa ataondoka Liverpool klabu ambayo ameitumikiakwa miaka 17.

SEVILLA YATETEA TAJO LAO LA EUROPA LEAGUE.

KLABU ya Sevilla ya Hispania imefanikiwa kushnda taji lake la nne la michuano ya Europa League baada ya kuitandika Dnipro ya Ukraine katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Warsaw, Poland jana. Sevilla ambao pia walikuwa wakitetea taji hilo walilazimika kutoka nyuma katika mchezo huo baada ya Dnipro kutangulia kufunga bao la mapema kupitia kwa nyota wao Nikola Kalinic kabla ya kusawazisha na kuongeza lingine haraka haraka. Hata hivyo Dnipro walikuja juu na kusawazisha bao hilo na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimetoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2.Alikuwa ni Carlos Bacca aliyewainua mashabiki wa Sevilla kwa kufunga bao la tatu na la ushindi katika dakika ya 73 na kuifanya timu yake kutetea taji lao hilo.Sevilla mbali na kufuzu moja kwa moja michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao pia inakuwa timu ya kwanza kunyakuwa taji hilo kwa mara nne.

Monday, May 25, 2015

FAINALI KOMBE LA FA: ARTETA FITI KUIVAA ASTON VILLA.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema nahodha wake, Mikel Arteta ambaye hajacheza toka Novemba mwaka jana kwasababu ya majeruhi anaweza kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Aston Villa utakaofanyika Jumamosi hii. Akihojiwa Wenger amesema uwezekano wa kumtumia Arteta katika mchezo huo ni mkubwa kwasababu yuko fiti na amekuwa akifanya mazoezi na wenzake. Kocha huyo aliongeza kuwa beki wa kimataifa wa Ufaransa Mathieu Debuchy pia ana nafasi ya kuwepo katika kikosi chake lakini mshambuliaji wa kimataifa wa Uingereza Danny Welbeck hatakuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo. Wenger pia amepata ahueni baada ya nyota wake Jack Wilshere na Theo Walcott kuonyesha kurejesha makali yao kwa kucheza kwa kiwango cha juu katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya West Bromwich Albion ambao walishinda mabao 4-1.

VAN DE VAART AICHOMOLEA AJAX.

WAKALA wa Rafael van de Vaart amebainisha kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi hatarejea katika klabu ya Ajax Amsterdam kiangazi hiki. Mkataba wa sasa wa Van de Vaart katika klabu ya Hamburg unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Juni mwaka huu na amekuwa akihusishwa na tetesi za kurejea Ajax ambako ndipo alipokulia na kuja kuwa kiungo bora kabisa Ulaya. Hata hivyo, wakala wa kiungo huyo, Roberto Geerlings amebainisha kuwa mteja wake hajaamua mahali anapotaka kwenda mpaka sasa. Wakala huyo amesema ni vyema kuihabalisha Ajax ili waweze kutafuta mbadala mwingine kwani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakisubiri uamuzi wake.

LIVERPOOL KUMTOA SADAKA LAMBERT ILI WAMNASE BENTEKE.

KLABU ya Liverpool iko tayari kumtoa Rickie Lambert ili waweze kumsajili Christian Benteke kutoka Aston Villa. Mshambuliaji huyo ni mmoja kati ya nyota waliopo katika mipango ya usajili ya Liverpool majira haya ya kiangazi na wanaweza kuchuana na Chelsea kuwania saini yake. Hata hivyo Liverpool wanafahamu kuwa Villa walikuwa wakimtaka Lamberty Januari na wanawea kuwa tayari kumuofa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uingereza ili waweze kumpata Benteke. Lambert mwenye umri wa miaka 33 aliamua kubakia Januari na kupigania nafasi yake Anfield lakini Villa, Crystal Palace na Bournemouth wote wameonyesha nia ya wazi kutaka kumsajili kiangazi hiki. Liverpool wamepania kufanya usajili mkubwa kiangazi hiki huku nyota kama James Milner na danny Ings wote wakitegemewa kutua Anfield.

ARSENAL YARIPOTIWA KUMSAJILI VIDAL.

KLABU ya Arsenal, imeripotiwa kupanga muda wao kwa ajili ya kutangaza usajili wa nyota wa Juventus, Arturo Vidal. Vidal alikuwa katika mipango ya usajili ya Manchester United kiangazi mwaka jana lakini walikatishwa tamaa kufuatia Juventus kutaka kitita cha paundi milioni 40. Hata hivyo, kutokana na taarifa zilizotolewa hivi karibuni nchini Italia, Liverpool wameambiwa kuwa wanaweza kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Chile kwa paundi milioni 25. Taarifa hizo zinachanganya zaidi baada ya mwandishi wa habari kutoka Argentina Hernan Feler sasa kudai usajili wa Vidal kwenda Arsenal umeshakamilika. Mwandishi huyo ambaye anaripotiwa kuwa ndiye aliyevujisha taarifa za Arsenal kutaka kumsajili Alexis Sanchez kutoka Barcelona msimu uliopita, aliandika katika ukurasa wake wa twitter kuwa baada ya michuano ya Copa America klabu itatangaza rasmi kumsajili nyota huo.

UNITED YATHIBITISHA KUMUACHA FALCAO.

KLABU ya Manchester United imefikia uamuzi wa kumuacha Radamel Falcao kufuatia kumaliza mkopo wake akitokea Monaco. Nyota huyo wa kimataifa wa Colombia ambaye alikosa mchezo wa Jumapili hii wa sare ya bila ya kufungana na Hull City kwasababu ya majeruhi, ameifungia United mabao manne katika mechi 29 alizocheza. Kutoka na hilo United imeamua kutomnunua moja kwa moja falcao mwenye umri wa miaka 29 kama ilivyokuwa katika makubaliano yao mwanzoni. Meneja wa United Louis van Gaal alithibitisha taarifa hizo kupitia mtandao wa klabu na kumtakia kila la heri nyota huyo popote aendapo. Mara ya mwisho Falcao kuifungia United ilikuwa katika mchezo dhidi ya Leicester City Januari 31 mwaka huu.

UCHAGUZI FIFA: PLATINI AMPIGA "MAWE" BLATTER.

RAIS wa Shirikisho la Soka la Ulaya, Michel Platini amesema mchezo wa soka utaingia dosari kama Sepp Blatter akichaguliwa tena kushikilia wadhifa wa urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA.  Blatter mwenye umri wa miaka 79, anapigiwa chapuo ya kushinda uchaguzi huo kwa kipindi cha tano baada ya kudai mwaka 2011 ataachia ngazi. Akihojiwa Platini amesema kama Blatter akiendelea kuliongoza shirikisho hilo ni wazi kuwa litapoteza heshima, muonekano na mvuto wake. Platini aliendelea kudai kuwa atamuunga mkono Prince Ali Bin Al Hussein wa Jordan katika uchaguzi huo unaotarajiwa mwishoni mwa mwezi huu huko Zurich, Uswisi. Platini amesema Blatter alimdanganya wakati alipodai kuwa kipindi hiki ikingekuwa cha mwisho kwake hivyo haoni sababu ya kumuunga mkono kwani kufanya hivyo ni kulirudisha soka nyuma.

ANCELOTTI KUFANYIWA UPASUAJI WA SHINGO.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti anatarajiwa kusafiri kwenda Vancouver, Canada kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa shingo. Ancelotti anasubiria mustakabali wake kama atatimuliwa Madrid baada ya kumaliza msimu bila kushinda taji lolote, huku tamko rasmi la klabu likitarajiwa wakati wowote. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 55 ana mkataba ambao unamalizika baada ya msimu ujao lakini rais wa Madrid Florentino Perez anategemewa kumtimua kutokana na kushindwa kufanya vyema. Akihojiiwa Ancelotti amesema kama akiendelea kupoteza muda na kutolitibu tatizo hilo ameambiwa kuwa lineweza kukua na kumletea madhara zaidi huko mbele ndio maana ameamua kufanya upasuaji.

RODGERS AKUBALI YAISHE LIVERPOOL

MENEJA wa Liverpool, Brendan Rodgers amekubali kuwa kibarua chake kiko mashakani baada ya mchezo wa mwisho wa nahodha Steven Gerrard kumalizika kwa kipigo kizito. Liverpool ilimuaga nahodha wake huyo kwa kukubali kipigo cha mabao 6-1 dhidi ya Stoke City na kuwafanya kumaliza nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu. Akihojiwa Rodgers ambaye ameshinda michezo miwili katika ya tisa aliyoisimamia Liverpool hivi karibuni, amesema yuko tayari kuondoka kama wamiliki wakimtaka kufanya hivyo. Kocha huyo aliendelea kwa kuomba radhi kwa kipigo hicho kizito walichopata ingawa amedai bado kuna mengi mazuri anayoweza kuifanyia klabu hiyo.

Friday, May 22, 2015

ANCELOTTI ABADO ATAKA KUENDELEA KUBAKIA MADRID.

MENEJA wa Real Madrid, Carlo Ancelotti bado anataka kuendelea kuinoa timu hiyo lakini amesema mustakabali wake utaamuliwa katika mchezo wa mwisho dhidi ya Getafe Jumamosi hii. Ancelotti aliingoza Madrid kunyakuwa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, lakini kufuatia kushindwa kunyakuwa taji la La Liga na kuondolewa katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya Ulaya wiki iliyopita, klabu inafikiria kumtimua na nafasi yake kuchukuliwa Rafa Benitez. Pamoja na tetesi hizo za kutimuliwa, Ancelotti ameonyesha utulivu huku akidai kuwa mustakabali wake ataujua baada ya mchezo mwisho, ingawa mwenyewe angependa kubakia. Kocha huyo amesema bado hajazungumza na klabu kuhusu mustakabali wake hivyo ataenndelea kuwa kocha mpaka itakapoamuliwa vinginevyo. Ancelotti aliendelea kudai kuwa baada ya mchezo wa Jumapili hii au Jumatatu ndio atakaa na kuzungumzia mustakabali wake na klabu na baadae ndio uamuzi utatoka kama aondoke au abakie.

NINA NDOTO ZA KUITUMIKIA BARCELONA - FEKIR.

KIUNGO wa klabu ya Lyon ya Ufaransa, Nabil Fekir amebainisha ana ndoto za kuichezea Barcelona katika siku zijazo. Fekir mwenye umri wa miaka 21 amekuwa katika kiwango bora msimu huu, akiifungia Lyon mabao 13 wakati wakipambana kugombea taji la Ligue 1 mpaka katika mwezi wa mwisho wa msimu na Paris Saint-Germain. Kiwango chake hicho kinamfanya kuhusishwa na tetesi za kutimikia Inter Milan katika majira ya kiangazi lakini mwenyewe amekiri uhamisho wa kwenda Barcelona ndio chaguo analohitaji. Akihojiwa Fekir amesema toka akiwa mdogo amekuwa na ndoto za kuichezea Barcelona na kama akipata bahati ya kucheza huko siku moja itakuwa in mafanikio makubwa kwake.

VAN GAAL SASA AMUWINDA SCHEINSTEIGER.

MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal yuko tayari kutumia mwanya wa Bastian Schweinsteiger kusimamisha mazungumzo ya mkataba mpya na Bayern Munich kwa kumpa ofa ya kuhamia Old Trafford. Van Gaal ambaye bado anamuwania beki wa Borussia Dortmund Mats Hummels, pamoja na madai ya klabu hiyo kuwa atabakia Signal Iduna Park, anataka kuongeza kingo mmoja mzoefu katika kikosi chake msimu ujao kutokana na Michael Carrick kusumbuliwa na majeruhi ya mara kea mara. Mazungumzo tayari yameashaanza kati ya pande hizo mbili na Van Gaal anaamini anaweza kumshawishi Schweinsteiger kujiunga nao baada ya kukataa kusaini mkataba mpya na Bayern. Akihojiwa kuhusu mustakabali wake Schweinsteiger amesema hana haraka ya kusaini mkataba mpya kwani amebakisha mwaka mmoja zaidi kabla ya huu wa sasa haujaisha. Kiungo huyo aliendelea kudai kuwa jambo la msingi kwake hivi sasa ni kuhakikisha anapona majeruhi yake ambayo yamekuwa yakimsumbua kea kipindi kirefu.

RODGERS AMTAKA STERLING KUMALIZA MKATABA WAKE.

MENEJA wa Liverpool, Brendan Rodgers amesema anategemea Raheem Sterling kumaliza miaka miwili ya mkataba wake uliobakia pamoja na msuguano uliopo kati ya mchezaji huyo na klabu kuhusu mkataba mpya. Wakala wa Sterling, Aidy Ward amesisitiza jana kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 hatabakia Anfield hata kama akipewa ofa ya kulipwa kitita cha euro milioni 1.3 kwa wiki. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Rodgers amesema in vigumu kuzungumzia kilichosemwa na wengine kwani mkutano wowote unaofanyika katika klabu hiyo mambo yake hubakia kuwa siri. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kama kutakuwa na mazungumzo au la, Sterling bado ana mkataba wa miaka miwili na anategemea nyota huyo ataheshimu hilo. Rodgers amesema haoni kama Sterling hana furaha, hivyo anategemea kuendelea kumtumia katika mchezo wao wa mwisho wa ligi msimu huu utakaofanyika Jumapili hii.

WALCOTT, RAMSEY HAWAENDI POPOTE - WENGER.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger anategemea Theo Walcott na Aaron Ramsey kubakia katika klabu hiyo katika majira ya kiangazi. Walcott amepoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza toka aliporejea kutoka katika majeruhi ya goti, wakati Ramsey amekuwa akihusishwa na tetesi za kuwindwa na klabu ya Barcelona. Hata hivyo Wenger amekanusha tetesi zozote zinzohusiana na wachezaji hao kuondoka akidai kuwa hana shaka kuwa watabakia tayari kea ajili ya msimu ujao. Walcott alitokea benchi na kutengeneza nafasi ya bao la kusawazisha katika sare ya bao 1-1 waliyopata kutoka Manchester United, lakini nyota huyo amekuwa akilalamika kupewa muda mchache wa kucheza. Pamoja na kutokuwa na furaha Wenger anaamini Walcott mwenye umri wa miaka 26 atarejea katika kikosi cha kwanza akiwa katika kiwango chake bora msimu ujao. Arsenal inatarajiwa kupambana na West Bromwich Albion katika mchezo wa mwisho wa ligi kabla ya kuvaana na Aston Villa katika fainali ya Kombe la FA Mei 30 mwaka huu.

MOURINHO MENEJA BORA WA MWAKA EPL.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho ameshinda tuzo ya meneja bora wa mwaka kea kuingoza timu hiyo kunyakuwa taji lake la tano la Ligi Kuu, wakati Eden Hazard akinyakuwa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka. Chelsea imefanikiwa kunyakuwa taji hilo huku wakiwa bado wana michezo mitatu mkononi na wanaweza kumaliza kwa tofauti ya alama 11 na mahasimu wao kama wakishinda mchezo wa mwisho wa ligi Jumapili hii. Huu in msimu wa pili kwa Mourinho toka arejee Stamford Bridge na amepiga hatua moja mbele bada ya kuiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili msimu uliopita. Pia in mara ya tatu Mourinho kunyakuwa tuzo hiyo baada ya kuwahi kunyakuwa tena msimu wa mwaka 2004-2005 na 2005-2006.

DAVID LUIS AKANUSHA KUWA BIKRA.

BEKI wa klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa, David Luis amevituhumu vyombo vya habari kukosa heshima baada ya kusambaza habari kuwa yeye bado hajawahi kukutana kimwili na mwanamke. Taarifa zilianza kuzagaa baada ya nyota huyo wa zamani wa Chelsea mwenye umri wa miaka 28, kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kuwa anataka kusubiri mpaka wakati wa ndoa kabla ya kukutana kimwili na mpenzi wake. Akihojiwa Luiz amesema watu wanasema mambo ambayo hawayafamu kwani sio kweli kwamba hajawahi kukutana kimwili na mwanamke. Beki huyo aliendelea kudai kuwa tayari ameshakuwa na wapenzi zaidi ya mmoja katika maisha yake hivyo watu wanapaswa kuheshimu maisha binafsi ya mtu.

Thursday, May 21, 2015

WAKALA WA STERLING ADAI HATA LIVERPOOL WANGEMPA OFA YA PAUNDI 900,000 KWA WIKI ASINGESAINI MKATABA MPYA.

WAKALA wa mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Uingereza, Raheem Sterling amesema mteja hatasaini mkataba mpya na Liverpool hata kama akipewa ofa ya kulipwa paundi 900,000 kwa wiki. Wakala huyo Aidy Ward pia alimponda beki wa zamani wa klabu hiyo Jamie Carragher kwa kukosoa mpango wa Sterling kuondoka. Ward amesema hajali watu wanasemaje kwasasa kwani kitu muhimu in kuhakikisha mteja wake anapata timu ambayo atafurahia kuitumikia. Sterling bado ana mkataba na Liverpool unaomalizika mwaka 2017 na amekataa mkataba mpya ambao ungemuwezesha kulipwa kitita cha paundi 100,000 kea wiki.

XAVI ATANGAZA RASMI KUONDOKA BARCELONA MWISHONI MWA MSIMU NA KWENDA QATAR.

KIUNGO mkongwe wa Barcelona, Xavi ametangaza nia yake ya kuondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu na kujiunga na klabu ya Al Sadd ya Qatar. Xavi ameitumikia Barcelona kwa kipindi cha miaka 24 toka alipojiunga nao akiwa na umri wa miaka 11 na kuwa mchezaji wa kwanza katika klabu hiyo kucheza mechi zaidi ya 750 katika kikosi cha kwanza. Ingawa amecheza zaidi ya mara 41 katika msimu huu, Xavi amekuwa akitumiwa zaidi akitokea benchi toka meneja Luis Enrique alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo kiangazi mwaka jana. Akizungumza mbele ya wanahabari leo, Xavi amesema uamuzi wake huo aliochukua in mgumu sana lakini anadhani wakati wake wa kuondoka umefika. Kiungo huyo aliendelea kudai kuwa klabu hiyo ilimpa ofa nzuri ya kuongeza mkataba lakini tayari alishachukua uamuzi wa kuondoka. Xavi aliendelea kudai kuwa atakwenda kucheza katika timu ya Al Sadd ambako amesaini mkataba wa miaka miwili lakini anaweza kuongeza kama akiona muda unamruhusu kuendelea.

HABARI MBAYA KWA UNITED BAADA YA HUMMELS KUSISITIZA KUMALIZA MKATABA WAKE DORTMUND.

BEKI mahiri wa kimataifa wa Ujerumani Mats Hummels amezima tetesi za kuhamia Manchester United kea kuthibitisha kuwa anatarajia kuendelea kuitumikia Borussia Dortmund msimu ujao. Hummels mwenye umri wa miaka 26 amekaririwa na gazeti Kicker la Ujerumani akidai kuwa anataka kumaliza mkataba wake na Dortmund utakaokwisha mwaka 2017. Mkurugenzi wa michezo wa Dortmund, Michael Zorc amesema mara nyingi amekuwa akieleza kuwa Hummels yuko katika mipango yao na anashukuru mwenyewe kulifafanua hilo. Kwa kipindi kirefu United walikuwa wakihusishwa na tetesi za kumtaka beki huyo huku meneja Louis van Gaal akiripotiwa kuwa tayari kutenga kitita cha euro milioni 40 ili kupata saini yake. Lakini sasa nyota huyo ataingia katika mipango ya kocha mpya wa Dortmund Thomas Tuchel ambaye atachukua nafasi ya ya kocha wa sasa Jurgen Klopp.

MALDINI NAYE AZINDUA TIMU YAKE MIAMI.

NGULI wa soka Italia, Paolo Maldini anatarajiwa kuhasimiana na David Beckahm baada ya kuzindua klabu yake ya soka jijini Miami, Marekani. Klabu ya Soka ya Miami inatarajiwa kucheza katika Ligi Daraja la Pili ikiwa chini ya Ligi Kuu nchini humo maarufu kama MLS. Maldini mwenye umri wa miaka 46 atakuwa mmliki mwenza katika klabu hiyo ambayo inatarajiwa kuleta upinzani kea Beckham ambaye naye anataka kuingiza timu kutoka Miami kwenye Ligi Kuu siku zijazo. Mpango huo wa Beckham ulikwama kidogo wakati mkakati wa kijenga uwanja mpya wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 25,000 ulipokataliwa mwaka jana. Beckham na Maldini wamewahi kucheza pamoja kwa kipindi kifupi mwaka 2009 katika klabu ya AC Milan.

KOCHA WA LAZIO ADAI BAHATI NDIO ILIYOWASAIDIA JUVENTUS KUNYAKUWA KOMBE LA ITALIA.

MENEJA wa klabu ya Lazio, Stefano Pioli amedai kuwa kikosi chake hakikupaswa kupoteza mchezo wao wa fainali wa Kombe la Italia na kuongeza kuwa wapinzani wao Juventus walikuwa na bahati. Juventus ilifanikiwa kunyakuwa taji hilo baada ya kushinda mabao 2-1 katika muda wa nyongeza baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Olimpiki. Juventus sasa wamejiweka katika nafasi nzuri ya kunyakuwa mataji matatu kea mkupuo baada ya kuwa tayari wameshachukua lile la Serie A huku wakitarajiwa kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Barcelona Juni 6 mwaka huu. Akihojiwa Pioli amesema ulikuwa ni mchezo uliokuwa na uwiano sawa kutokana na kila timu kuwa na nafasi ya kupata ushindi lakini ilihitajika bahati kidogo jambo ambalo hawakuwa nalo katika mchezo huo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa walistahili matokeo tofauti na hayo lakini kutoka na timu waliyocheza nayo hana jinsi zaidi ya kuwapongeza wachezaji wake kea mchezo mzuri.

VAN PRAAG AJITOA KINYANG'ANYIRO CHA URAIS FIFA.

MGOMBEA urais wa Shirikisho la Soka duniani-FIFA, Michael van Praag amejitoa katika kinyang’anyiro hicho na kuwaacha wagombea wawili kuchuana na rais wa sasa Sepp Blatter. Van Praag mwenye umri wa miaka 67 ambaye in rais wa Shirikisho la Soka la Uholanzi amesema atamuunga mkono Prince Ali Bin Al-Hussein wa Jordan katika uchaguzi huo utakaofanyika Mei 29 mwaka huu. Mchezaji nyota wa zamani wa Ureno Luis Figo mwenye umri wa miaka 42 in mgomea watatu katika kinyang’anyiro hicho. Blatter mwenye umri wa miaka 79, anategemewa na wengi kushinda katika uchaguzi huyo na kuendelea kuongoza kea kipindi cha tano.

PALESTINA YAIKOMALIA ISRAEL IONDOLEWE FIFA.

PALESTINA imesema itaendelea na juhudi zake za kutaka kusitishwa ushiriki wa Israel katika mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Palestina imeazimia hivyo licha ya rais wa shirikisho hilo Sepp Blatter kukutana na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na maafisa wa Ukingo wa magharibi jana. Blatter amesema Israel imependekeza kulegeza vizuizi vya kusafiri kwa wachezaji wa Palestina, wageni na maafisa wa michezo, zilizowekwa kutokana na matatizo ya kiusalama. Chama cha Soka cha Palestina kimeishutumu Israel kwa kuzuia shughuli za kimichezo na kuzuia wachezaji kusafiri kati ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa magharibi. Wajumbe watapiga kura kusitisha ushiriki wa Israel katika michezo Mei 29.

MORENO AKIRI KUWA SHABIKI WA EUROPA LEAGUE.

BEKI wa Liverpool, Alberto Moreno amesisitiza kuwa shabiki mkubwa wa michuano ya Europa League wakati timu hiyo ikijiandaa kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano hiyo ya pili kwa vilabu Ulaya. Baada ya kushindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, Liverpool wanaweza kupata nafasi ya Europa League pamoja na kukabiliwa na upinzani kutoka kea Tottenham Hotspurs na Southampton kuelekea katika mechi zao za mwisho wa msimu. Kama Liverpool wakifanikiwa kuitandika Stoke City Jumapili hii watakuwa wamejihakikishia nafasi ya kushiriki michuano hiyo na Moreno angependa wafanikishe hilo. Moreno ambaye amewahi kunyakuwa taji la michuano hiyo akiwa na Sevilla msimu uliopita, amesema anaihusudu michuano hiyo ana matumaini wanaweza kupata nafasi hiyo Jumapili.

ADEBAYOR AENDELEA KULIA NA NDUGU ZAKE, ADAI ALITAKA KUJIUA KWA AJILI YAO.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Togo na klabu ya Tottenham Hotspurs, Emmanuel Adebayor amebainisha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook kuwa alifikiria kujiua kutokana na matatizo ya familia yake. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31, ambaye ameichezea Spurs mechi chache msimu huu, pia amedai kuwa alishikiwa kisu na kaka zake Kola na Peter aliyefariki Julai mwaka 2012. Adebayor amesema mara kadhaa amekuwa akitaka kukata tamaa na kumpigia dada yake kumuelezea nia yake hiyo. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa alipofikiria kwa makini akaona hata akifa hakuna atayejua taarifa hizo ndio maana ameamua kuziweka wazi ili watu wengine haswa wanaotoka katika familia za kiafrika waweze kujifunza kutoka kwake. Hii ni mara ya tatu Adebayor kutuma ujumbe katika facebook kuelezea jinsi walivyokorofishana na mama pamoja na ndugu zake, matatizo ambayo yanatishia kumaliza kipaji chake cha soka. Adebayor pia amedai siku akiwa amelala alishangaa kaka zake wawili kumuwekea kisu shingoni baada ya kukataa kumpa Kola mtaji wa kufanyia biashara ya magari wakati akiichezea Monaco. Adebayor ambaye pia amewahi kucheza katika klabu za Arsenal, Manchester City na Real Madrid, amekuwa akiichezea Spurs mwaka 2011, lakini amecheza mechi 10 pekee msimu huu na kufunga mabao mawili.

FABREGAS APUNGUZIWA ADHABU.

KIUNGO wa Chelsea, Cesc Fabregas amepunguziwa adhabu ya kufungiwa kutoka mechi tatu mpaka mechi moja baada ya kutolewa nje katika mchezo wa Ligi kuu dhidi ya West Bromwich Albion. Katika mchezo huo uliofanyika Jumatatu iliyopita, Fabregas alionyeshwa kadi nyekundu kwa kuonyesha kitendo kisicho cha uanamichezo wakati walipotandikwa mabao 3-0. Mwamuzi alimnyuka kadi hiyo baada ya Fabregas kupiga mpira uliompiga mchezaji wa West Brom kichwani wakati mchezo ukiwa umesimama. Katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imedai kuwa adhabu hiyo imepunguzwa baada ya kuikatia rufani hivyo Fabregas atakosa mchezo wao mwisho wa msimu dhidi ya Sunderland.

AMNESTY INTERNATIONAL YAITUHUMU QATAR KUENDELEA KUWANYANYAPAA WAFANYAKAZI.

SERIKALI ya Qatar imepinga madai ya shirika linalopigania haki za kibinadamu lenye makao yake nchini Marekani, Amnesty International, iliyodai kuwa maelfu ya wafanyakazi nchini humo wanaojenga viwanja vitakavyotumika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 kuwa bado wanaonewa. Amnesty International ilikuwa imedai kuwa licha ya serikali hiyo kuahidi kuwalipa wafanyakazi mishahara yao kwa wakati unaofaa wengi bado hawapokei malipo yao kwa wakati unaostahili. Aidha Amnesty imelalamikia vikali mtindo wa Hawala ambao unamzuia mfanyakazi kuondoka nchini humo bila ruhusa ya mwajiri wake. Serikali ya Qatar imesema kuwa mabadiliko yanaendelea na kudai kuwa tayari mfumo wa kielektroniki ndio unaotumika kuwalipa wafanyakazi hatua inayohakikisha kuwa wanalipwa kwa wakati unaofaa. Hata hivyo Amnesty wanasema Qatar imepiga hatua kidogo sana kutekeleza ahadi nyingi walizozitoa mwaka jana, kwani wafanyakazi bado wanahitaji ruhusa kutoka kwa waajiri wao, kubadili ajira au kuondoka nchini humo huku malipo yao yakifanyika taratibu mno kea mfumo huo mpya.

Tuesday, May 19, 2015

CECH ANATAKA KWENDA ARSENAL, MAN UNITED AU PSG - WAKALA.

WAKALA wa golikipa wa Chelsea Petr Cech, amedai kuwa mteja wake angependelea kujiunga na klabu za Arsenal, Manchester United au Paris Saint-Germain katika usajili wa majira ya kiangazi. Cech ameshushwa mpaka kuwa golikipa namba mbili kutokana na ujio wa Thibaut Courtois katika klabu hiyo na wakala wake Viktor Kolar amebainisha awali kuwa mteja wake amepewa ruhusa ya kuondoka Stamford Bridge mwishoni mwa msimu. Arsenal wamekuwa wakihusishwa kwa muda mrefu na tetesi za kumtaka golikipa huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Czech, wakati United wao wanadhani Cech anafaa kuwa mbadala wa David De Gea kama akiondoka kwenda Real Madrid. Kolar amesema wanakarisha ofa kutoka timu hizo na kuongeza kuwa meneja wake Jose Mourinho hatakuwa na ushawishi wowote kuhusiana na mustakabali wake.

MOURINHO ATUPIA LAWAMA UPINZANI HAFIFU, KUFUATIA KIPIGO WALICHOPATA DHIDI YA WEST BROM.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho amewalaumu mahasimu wao katika Ligi Kuu kuwa ndio chanzo cha wao kutandikwa mabao 3-0 na West Bromwich Albion jana. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo ambao kiungo wake Cesc Fabregas alitolewa nje kea kadi nyekundu dakika ya 29, Mourinho amesisitiza wachezaji wake wamepoteza ari baada ya kufanikiwa kunyakuwa taji. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa wapinzani wao wakubwa Manchester City, Manchester United, Arsenal na Liverpool waliwaacha kushinda taji hilo mapema, hivyo kuwafanya kupoteza ile ari waliyokuwa nayo kabla. Mourinho amesema jambo hutokea kea timu nyingi akiifananisha Bayern Munich ambao nao wamepoteza michezo yao mitatu ya Bundesliga baada ya kunyakuwa taji hilo.

WENGER AMUWEKA STERLING KIPORO.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amekataa kuweka wazi kama atatuma ofa kwa ajili ya kumuwania mshambuliaji wa Liverpool, Raheem Sterling. Mapema mwezi Aprili Sterling alibainisha nia ya Arsenal kumuhitaji, akifafanua kuwa ni heshima kubwa kwake, wakati Wenger akijibu kea kusisitiza hana nafasi ya kuleta mchezaji mpya katika kikosi chake. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Wenger amesema ni kweli watafanya usajili lakini kwasasa hataki kuzungumzia chochote kuhusiana na hilo kwani anaweza kudanganya. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kama akikubali kuwa atamuwania Sterling halafu asifanye hivyo kipindi cha usajili wanaweza kumuita muongo, hivyo ni vyema wakasubiri wakati muafaka wa kufanya hivyo.

XAVI KUTANGAZA UAMUZI WA KUNG'ATUKA BARCELONA WIKI HII.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Hispania, Xavi anatarajia kutangaza uamuzi wake wa kuondoka Barcelona Alhamisi hii wakati akijiandaa kuhamia katika klabu ya Al Sadd ya Qatar. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akiitumikia Barcelona kipindi chote na kuisaidia kushinda mataji 23 lakini anataka kuamua kuondoka baada ya muda mwingi msimu huu akiutumia akiwa benchi. Xavi ambaye alikaribia kwenda Al Sadd kiangazi mwaka jana kabla ya kushawishiwa kubakia Barcelona na meneja Luis Enrique, anatarajiwa kukutana na wanahabari wiki hii kufafanua uamuzi wake huku akitarajiwa kuaga Camp Nou katika mchezo wa La Liga dhidi ya Deportivo La Coruna. Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amemuelezea Xavi kama kiungo bora kabisa kuwahi kutokea katika historia ya klabu hiyo. Xavi anaweza kuongeza medali zingine mbili kati ya nyingi alizonazo kabla ya kuondoka, wakati Barcelona itakapokwaana na Athletic Bilbao katika mchezo wa Kombe la Mfalme baadae mwezi huu kabla ya kukabiliana na Juventus katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Juni 6.

SOUTHAMPTON YATAKA PAUNDI MILIONI 25 KWA SCHNEIDERLIN.

KLABU ya Southampton inatarajia kutaka kitita cha paundi milioni 25 kwa ajili ya kiungo Morgan Schneiderlin(pichani) ambaye anawindwa na klabu za Arsenal na Tottenham Hotspurs. Klabu hizo zinazotoka kaskazini mwa jiji la London, zote zimeonyesha nia ya kumtaka kiungo huyo lakini Southampton wamedai hawatamuachia chini ya kiwango hicho. Southampton waligoma kupokea ofa yeyote kea ajili ya Schneiderlin kiangazi mwaka jana, wakati mchezaji huyo alipojaribu kulazimisha kuhamia Spurs. Klabu hiyo imepania kufanya kama usajili wa kiangazi mwaka jana ambapo walikunja kitita cha paundi milioni 25 kwa ajili ya Adam Lallana na paundi milioni 20 kwa Dejan Lovren ambao wote walikwenda Liverpool. Arsenal wamepanga kutuma ofa ya paundi milioni 20 kea ajili ya Schneiderlin wakati Spurs wao wako tayari kutoa kitita cha paundi milioni 15.

QPR YAMPA MIAKA MITATU RAMSEY.

KLABU ya Queens Park Rangers-QPR, imeteua kocha wa muda Chris Ramsey(pichani) kuchukua kibarua cha moja kwa moja kuinoa timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu. Ramsey mwenye umri wa miaka 53 alichukua mikoba hiyo kutoka kea Harry Redknapp Februari mwaka huu lakini alishindwa kuiwezesha timu hiyo kubakia katika Ligi Kuu.M Kocha huyo ambaye alikuwa mkuu wa zamani wa kitengo cha kukuza vipaji cha Tottenham hotspurs alijiunga na QPR Novemba mwaka 2014 kufuatia kuondoka kea Redknapp. QPR walishuka daraja kufuatia kutandikwa mabao 6-0 na Manchester City Mei 10 mwaka huu huku Ramsey akiwa amefanikiwa kupata ushindi kwenye mechi tatu kati ya 14 alizokuwa akiisimamia timu hiyo.

BERLUSCONI KUMUONYESHA INZAGHI MLANGO WA KUTOKEA.

VYOMBO vya habari nchini Italia, vimeripoti kuwa Silvio Berlusconi amethibitisha kuwa atamtimua meneja wa AC Milan Filippo Inzaghi mwishoni mwa msimu baada ya matokeo yasiyoridhisha. Berlusconi ambaye ndiye mmiliki wa timu hiyo amesema Inzaghi amekuwa na mahusiano mazuri na kikosi chake lakini mara kadhaa wamekuwa wakipishana kutokana na maono tofauti. Bilionea huyo aliendela kudai kuwa jambo in kitu ambacho wanataka kuzungumza na kocha huyo muda ukifika kabla ya kuamua cha kufanya. Berlusconi amesema kwasasa wanajipanga na tayari wameshapata majina kadhaa ya makocha kama wakishindwa kufikia muafaka na Inzaghi.

UEFA KUIFANYIA MAREKEBISHO SHERIA KALI YA MATUMIZI YA FEDHA ZA ZIADA WA VILABU.

SHIRIKISHO la soka la Ulaya-UEFA linajiandaa kulegeza sheria ya mwaka 2011 inayozuia vilabu vya bara hilo kufanya matumizi ya ziada. Katika mahojiano na redio ya Ufaransa RTL, rais wa UEFA Michel Platini amesema kuwa sheria hiyo ilikuwa ikifanya kazi vizuri lakini itaboreshwa zaidi mwishoni mwa msimu huu. Hatua hiyo inafuatia ripoti katika gazeti la Le Parisien siku ya jumapili iliyosema kuwa kuna mabadiliko muhimu yatakayofanywa katika sheria hiyo. Manchester City, Barcelona na Paris Saint-Germain wamekuwa wahanga wa kwanza wa sheria hiyo baada ya kupigwa faini na adhabu mwaka jana.

WATU 50 WAKAMATWA ITALIA KWA KOSA LA UPANGAJI MATOKEO.

ZAIDI wa watu 50 wamekamatwa na wengine kuwekwa chini ya upelelezi ikiwa in matokeo ya uchunguzi wa tuhuma za upangaji matokeo katika mechi za soka nchini Italia. Waendesha mashitaka wanaopambana na kundi haramu la Mafia katika mji wa Catanzaro uliopo kusini mwa Italia ndio walioongoza uchunguzi huo ambao umepeleka kukamatwa kwa watu hao. Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya Italia, waliokamatwa in wachezaji 15, marais sita wa vilabu, maofisa nane wa michezo, makocha na viongozi 10 wa taasisi za kamari nchini humo. Uchunguzi huo uliohusisha polisi ilifanyika kwa kuzifuatilia mechi za ligi daraja la tatu, nne na tano ambazo ndio zimekuwa zikiongoza kwa tuhuma za upangaji matokeo. Mpango huo wa kupiga vita upangaji matokeo in mkakati wa kuliokoa soka la nchi hiyo ambalo lilikuwa limegubikwa na vitendo hivyo kuanzia timu za daraja la juu mpaka chini. Mwaka 2006 mabingwa wa sasa wa Serie A Juventus walishushwa daraja huku timu zingine zikikatwa alama baada ya kukutwa na hatia ya kuhonga waamuzi ili wawape upendeleo.

Monday, May 18, 2015

VAN GAAL AKATA TAMAA KUMBAKISHA DE GEA.

MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal ameonyesha dalili za wazi za kumkosa golikipa wao David De Gea anayeweza kwenda Real Madrid. De Gea alitolewa nje baada ya kupata majeruhi msuli wakati wa mchezo dhidi ya Arsenal uliofanyika katika Uwanja wa Old Trafford jana hivyo kumfanya kuwa katika hatihati ya kuukosa mchezo wa mwisho dhidi ya Hull City. Madrid wamekuwa wakimuwinda kipa huyo wa kimataifa wa Hispania ili aweze kuchukua nafasi ya mkongwe Iker Casillas na Van Gaal ana uhakika De Gea anapata wakati mgumu kuchagua. Van Gaal amesema anajua sio rahisi kwa De Gea kuchagua kati ya klabu mbili kubwa, ingawa amedai watafurahi kama akibakia.

LUIS ENRIQUE HAENDI POPOTE - BARTOMEU.

RAIS wa Barcelona, Josep Bartomeu amesisitiza kuwa meneja wa Luis Enrique hataondoka katika timu hiyo mwishoni mwa msimu huu. Enrique alichukua mikoba ya Gerardo Martino aliyeondoka baada ya kushindwa kuipa mafanikio Barcelona msimu wa 2013-2014. Toka achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo, Enrique amefanikiwa kubadilisha mambo na kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la La Liga msimu huu kufuatia kuifunga Atletico Madrid bao 1-0 jana. Tetesi zimezagaa kuwa kocha huyo anaweza kutimka kiangazi hiki lakini Bartomeu amekanusha vikali tetesi hizo na kudai ataendelea kubakia Camp Nou. Bartomeu amesema wako katika mazungumzo ya kumuongeza mkataba mpya hivyo hakuna shaka kuwa ataendelea kuwa nao.