KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Hispania, Xavi anatarajia kutangaza uamuzi wake wa kuondoka Barcelona Alhamisi hii wakati akijiandaa kuhamia katika klabu ya Al Sadd ya Qatar. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akiitumikia Barcelona kipindi chote na kuisaidia kushinda mataji 23 lakini anataka kuamua kuondoka baada ya muda mwingi msimu huu akiutumia akiwa benchi. Xavi ambaye alikaribia kwenda Al Sadd kiangazi mwaka jana kabla ya kushawishiwa kubakia Barcelona na meneja Luis Enrique, anatarajiwa kukutana na wanahabari wiki hii kufafanua uamuzi wake huku akitarajiwa kuaga Camp Nou katika mchezo wa La Liga dhidi ya Deportivo La Coruna. Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amemuelezea Xavi kama kiungo bora kabisa kuwahi kutokea katika historia ya klabu hiyo. Xavi anaweza kuongeza medali zingine mbili kati ya nyingi alizonazo kabla ya kuondoka, wakati Barcelona itakapokwaana na Athletic Bilbao katika mchezo wa Kombe la Mfalme baadae mwezi huu kabla ya kukabiliana na Juventus katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Juni 6.
No comments:
Post a Comment