Sunday, April 29, 2012

FENERBAHCE YAJITOA KUMWANIA DIARRA.

KLABU ya Fenerbahce ya Uturuki imejitoa katika mbio za kumwania kiungo wa klabu ya Real Madrid ya Hispania Lassana Diarra. Klabu hiyo inayotoka jijini Istanbul ilikuwa ikimhitaji kiungo huyo wa zamani wa Arsenal ili kuongeza nguvu katika safu ya kiungo ya klabu hiyo lakini kutokana matatizo ya kifedha yanayoikabili klabu hiyo imeshindwa kuendelea na mbio zake na kumchukua. Diarra hivi sasa amekuwa ziada ya mahitaji ya klabu ya Madrid ambapo hivi sasa klabu hiyo ipo tayari kupokea pesa kutoka timu yoyote kama watamuhitaji mchezaji huyo. Kiungo huyo ambaye pia ameshawahi kuichezea klabu ya Chelsea pia anahusishwa na kuhitajika katika klabu ya Galatasaray ambapo taarifa zinasema kwamba wako katika mazungumzo.

BALOTELLI CAN BE TRUSTED - MANCINI.

MENEJA wa Manchester City, Roberto Mancini amesema kuwa atamwamini mshambuliaji wake Mario Balotelli kama atamchezesha katika mchezo dhidi ya mahasimu wao Manchester United. Katika mkutano na waandishi wa habari wiki nne zilizopita Mancini alinukuliwa akisema kuwa hawezi kumwani mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Italia kwakuwa haeleweki. Balotelli mwenye umri wa miaka 21 hajacheza mechi toka alipotolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Arsenal mapema mwezi huu ambapo katika kipindi hicho Mancini alisema kuwa hawezi kuchezesha tena mshambuliaji huyo msimu huu. Mancini amesema kuwa baada ya mchezaji huyo kuomba msamaha kutokana na tukio alilofanya anaweza kumpa nafasi ya kucheza katika mchezo huo kwakuwa amekuwa akifanya vyema kwenye mazoezi na wenzake wa kikosi cha kwanza. Balotelli alitolewa katika Uwanja wa Emirates baada ya kuchezea vibaya Bacary Sagna na kupewa kadi ya pili ya njano ambapo City walifungwa bao 1-0 na Arsenal.

WENGER AKERWA NA VITENDO VYA UNYANYASAJI KUTOKA KWA MASHABIKI.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesema kuwa kuna kubwa ya kufanya ili kudhibiti vitendo vya unyanyasaji kutoka kwa mashabiki. Kauli ya kocha huyo imekuja baada ya baadhi ya mashabiki wa timu ya Stoke City kutoa kauli za matusi wakati wa mchezo baina ya timu hizo ambao walitoka sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Britannia. Wenger amesema kuwa anafikiri siku moja mchezo wa mpira wa miguu unaweza kuachana na mambo hayo kwani soka ni mchezo wa burudani na sio uadui kama baadhi ya mashabiki wanavyofikiri. Upinzani kati ya timu ya Arsenal na Stoke ulikuwa zaidi katika kipindi karibuni ambapo pia walikuwa wakimzomea kiungo wa Arsenal Aaron Ramsey atika mchezo huo. Mashabiki wa Stoke kumzomea Ramsey kunakuwa kama ni kulipiza kisasi baada ya kiungo huyo kuvunjika mguu baada ya kuchezewa vibaya na Ryan Showcross Februari mwaka 2010 katika mchezo baina ya timu hizo ambapo toka kipindi hicho beki huyo wa Stoke amekuwa akizomewa na baadhi ya mashabiki wa Arsenal.

ROBINHO AACHWA MILAN.

MSHAMBULIAJI wa AC Milan, Robinho ameachwa katika kikosi cha timu hiyo na kocha Massimiliano Allegri kutokana na kushuka kiwango chake katika siku za karibuni. Akihojiwa Allegri alikiri kuwa mchezaji huyo hayuko katika kiwango chake hivyo ameona ni bra kumpumzisha kwanza. Robinho ambaye ana umri wa miaka 28 amefunga mabao matano tu mpaka sasa katika michezo 26 alizocheza rekodi ambayo imemkera Allegri akidai kuwa hapendi kuwa na mchezaji ambaye msimu mzima anacheza chini ya kiwango. Kocha huyo pia akasirishwa na kiwango cha kiungo mkongwe kutoka Uholanzi Clarence Seedorf ingawa kumuacha kwake kwenye kikosi hicho ambacho kitachuana na Siena ni kutokana na majeruhi yanayomsumbua. Kinara wa mabao Zlatan Ibrahimovic ambaye ana mabao 24 msimu huu anatarajiwa kuanza kucheza katika kikosi hicho pamoja na Antonio Cassano au Stephan El-Shaarawy wakisaidiwa na Kevin-Prince Boateng. Milan inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Italia wakiwa nyuma kwa alama tatu kwa vinara wa ligi hiyo Juventus huku wakiwa wamebakiwa na michezo minne kabla msimu kumalizika.

Saturday, April 28, 2012

FAINALI YA CHAMPIONS LEAGUE KUONYEHSWA LIVE OLYMPIC STADIUM, MUNICH.

Olympic Stadium, Munich, Germany.
SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA limesema kuwa Uwanja wa Olimpiki uliopo jijini Munich, Ujerumani utaonyesha mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati Bayern Munich itakapochuana na Chelsea katika Uwanja wa Allianz Arena Mei 19 mwaka huu. Beyern imepata maombi ya tiketi zaidi ya milioni ya mashabiki wakihitaji tiketi katika uwanja wao wa Allianz Arena ambapo klabu hiyo imepewa tiketi 17,000 katika uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza mashabiki wapatao 66,000. Mashabiki ambao watakosa tiketi za kushudia mchezo huo sasa wataweza kuona mchezo huo moja kwa moja kupitia luninga katika uwanja wa Olimpiki ambapo tiketi zitakuwa zikiuzwa kwa euro tano moja katika viti 65,000 vilivyopo uwanja huo ambao ulikuwa ukitumiwa na Bayern kabla ya kuhamia Allianz Arena mwaka 2005. Hii ni mara ya kwanza kwa fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya kuonyeshwa rasmi katika luninga uwanjani na tiketi zake kuuzwa katika mtandao.

BARCELONA YAPATA UDHAMINI KUTOKA THAILAND.

KLABU ya Barcelona imetangaza ratiba yake ya kufanya ziara nchini Thailand mwaka ujao baada ya kusaini mkataba wa udhamini wa miaka mitatu wenye thamani ya euro milioni 12 na Kampuni ya Thai Beverage. Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Javier Faus amethibitisha ziara hiyo na kusema kwamba wana nia ya kuongeza mashabiki katika bara ya Asia hususani upande wa Kusini Mashariki mwa bara hilo. Faus amesema kuwa ziara hiyo ina manufaa makubwa kwao kwani hivi sasa wamejikusanyia mashabiki wengi zaidi barani Asia kuliko Ulaya hivyo wanatarajia kuweka mpango wa miaka 10-20 katika ukanda huo. Aliendelea kusema kuwa wamefurahishwa na Thailand kuwa nchi ya kwanza Asia kuwaunga mkono na mkataba walioingia utasaidia mashabiki nchini humo kuielewa klabu hiyo. Naye Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Sorrakit Latitham pia alieleza kuwa kampuni yake inajivunia kuandaa ziara ya klabu hiyo ambayo ndio inayohesabika kuwa ni klabu bora zaidi duniani kwa sasa.

WATUHUMIWA WA MABOMU SCOTTLAND WAHUKUMIWA MIAKA MITANO.

Neil Lennon
WATU wawili ambao walituma bomu kwenye barua kumwendea meneja wa klabu ya Celtic ya Scottland Neil Lennon wamehukumiwa vifungo vya miaka mitano jela. Watu hao ambao ni Trevor Muirhead na Neil McKenzie mara ya kwanza walikuwa wameshitakiwa na makosa ya kula njama za mauaji, lakini badala yake walihukumiwa na makosa ya kula njama za mashambulizi baada ya kutuma kifaa ambacho waliamini kwamba kingelipuka. Watu hao walituma mabomu hayo mwaka uliopita kwenda kwa Lennon, Mshauri wa Kisheria wa klabu ya Celtic Trish Godman na wakili wa Lennon ambaye ni marehemu anayeitwa Paul McBride. Vifurushi hivyo vya mabomu vilikamatwa kabla ya kuwafikia walengwa waliokusudiwa na havikulipuka.

FIFA TO TEST GOAL-LINE TEKNOLOGY IN LIVE MATCHES.

SHIRIKISHO la Soka la Dunia-FIFA limepanga kufanya majaribio ya teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli katika baadhi ya mechi. FIFA imesema kuwa mfumo unaoitwa GoalRef unatarajiwa kufanyiwa majaribio katika mechi mbili kwenye Ligi Kuu nchini Denmark au watafanya mchezo mmoja kwenye ligi na mwingine kwenye mchezo wa kimataifa wa kifariki. Mfumo mwingine ambao umependekezwa na Bodi ya Kimataifa ya Vyama vya Soka-IFBA ambacho ndicho chombo kinachotunga sheria za mpira, unaitwa Hawk-Eye wenyewe unatarajiwa kufanyiwa majaribio nchini Uingereza Mei 16 mwaka huu katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA. IFBA inajipanga kutoa maamuzi yake kama wataruhusu mfumo huo utumike katika mkutano wao unaotarajiwa kufanyika Julai 2 mwaka huu.

MOTO WAWAKA YANGA, WAZEE WACHUKUA TIMU.

BARAZA la Wazee la klabu ya Yanga ya Dar es Salaam imeamua kuichukua timu ili kuiandaa na mechi dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC Mei 5, mwaka huu kufuatia mgogoro unaoendelea klabuni. Asubuhi ya leo, wazee wa Yanga wakiongozwa na Katibu wao Mkuu, Ibrahim Ally Akilimali walifika makuu ya klabu, makutano ya mita ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kufanya Mkutano na Waandishi wa Habari. Katika Mkutano huo, Mzee Akilimali alisema maamuzi hayo yana Baraka za Mwenyekiti wa klabu, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga. Kwa sasa Yanga ipo katika mgogoro, kufuatia Wajumbe wake wawili wa Kamati ya Mashindano na Usajili, Abdallah Ahmed Bin Kleb kujiuzulu kwa kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi. Machi mwaka jana, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha naye alijiuzulu kwa sababu za kutoelewana na Mwenyekiti wake, Nchunga. Yanga iliyopoteza matumaini hata ya kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, inaingia kwenye mechi dhidi ya watani wa wa jadi, Simba walio katika hali nzuri. Kwanza wana uhakika wa kuchukua ubingwa na pili wanaendelea vizuri kwenye michuano ya Afrika, kesho wakicheza mechi ya kwanza ya hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan.

ROONEY-WILBECK NEW YORKE-COLE - FERGIE.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson anaamini kuwa washambuliaji wake Wayne Rooney na Danny Welbeck wanaweza kufikia rekodi ya klabu hiyo iliyowekwa na kipindi cha na washambuliaji Dwight Yorke na Andy Cole. Welbeck alifunga bao lake la 12 msimu huu wakati United ilipotoa sare ya mabao 4-4 na Everton wakati Rooney alifunga mawili na mabao 33 msimu huu. Uelewano wa Rooney na Welbeck katika safu ya ushambuliaji wa klabu hiyo kwasasa unarudisha nyuma kumbukumbu ya miaka ya nyuma wakati Yorke na Cole kufunga mabao 53 katika msimu wa 1998-1999 na kuiwezesha timu hiyo kushinda mataji matatu muhimu. Ferguson amesema kuwa kiwango walichokionyesha wachezaji hao kinakaribiana na kipindi cha kina Cole na katika miaka michache ijayo wataweza kufikia huko kwani umri wao bao unaruhusu.

Friday, April 27, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF.

WATANZANIA WAWILI WAOMBEWA ITC UGHAIBUNI
Wachezaji wawili Watanzania wameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu katika nchini za Denmark na Jamhuri ya Czech. Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU) kimemuombea hati hiyo William Benard Okum kama mchezaji wa ridhaa ili ajiunge na timu ya Brabrand IF. Klabu ya zamani ya Okum ni Viko Pham FC ya Zanzibar. Naye Samwel Jonathan Mbezi ameombewa hati hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu cha Jamhuri ya Czech (FACR) ili aweze kuchezea timu ya Sokol Dolany akiwa mchezaji wa ridhaa. Katika maombi hayo, FACR imeonesha kuwa Mbezi kwa sasa hana timu anayochezea hapa nchini. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanya mawasiliano na pande husika kabla ya kutoa hati hizo kwa wachezaji hao kama walivyoomba DBU na FACR.

MECHI KUCHANGIA TWIGA STARS MEI 4
Mechi maalumu ya hisani kwa ajili ya kuchangia timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars), kati ya timu hiyo na wasanii wa filamu maarufu kama Bongo Movie itachezwa Mei 4 mwaka huu. Kwa mujibu wa kampuni ya Edge Entertainment iliyoandaa mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni kwa kiingilio cha sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000. Twiga Stars kwa sasa hivi haina mdhamini na iko kambini katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani inashiriki michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) ambapo Mei 26 mwaka huu itacheza na Ethiopia jijini Addis Ababa. Fainali za AWC zitafanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.

MECHI ZA LIGI KUU WIKIENDI HII
Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea katika raundi ya 25 kesho (Aprili 28 mwaka huu) ambapo Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mtibwa Sugar ikiwa mgeni wa African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi. Aprili 30 mwaka huu Azam na Toto African zitacheza Chamazi wakati Mei 1 mwaka huu Villa Squad itaumana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi. Ligi hiyo itafunga msimu wa 2011/2012, Mei 5 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa uwanjani. Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Polisi Dodoma (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Ruvu Shooting vs Villa Squad (Mabatini, Mlandizi). Mechi nyingine zitakuwa kati ya Coastal Union vs Toto African (Mkwakwani, Tanga), African Lyon vs JKT Ruvu (Manungu, Morogoro), Azam vs Kagera Sugar (Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro).

GUARDIOLA KUIKACHA BARCELONA MWISHONI MWA MSIMU HUU.

MENEJA wa timu ya Barcelona, Pep Guardiola anatarajiwa kuacha kuinoa klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu baada ya kukataa kuongeza mkataba wake. Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Hispania alikutana na Rais wa klabu hiyo Sandro Rosell na Mkurugenzi wa Michezo Andoni Zubizarreta jana na kuwaeleza uamuzi wake huo aliouchukua wakupumzika za mambo ya soka kwa muda. Viongozi hao wa Barcelona walimuomba Guardiola kuangalia upya uamuzi wake kwani bado walikuwa wakimuhitaji kuendelea kuinoa klabu hiyo lakini kocha huyo ambaye ana umri wa miaka 41 ameshaamua kuiacha klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu. Guardiola ambaye alikiongoza kikosi cha Barcelona kushinda mataji 13 toka alipochukua mikoba mwaka 2008 tayari ameshawapa taarifa wachezaji kuhusu kuondoka kwake katika mkutano uliofanyika asubuhi leo ambao baadae anatarajiwa kuongea na vyombo vya habari.

WAKAGUZI FIFA KUITEMBELEA MIJI MIWILI BRAZIL.

WAKAGUZI wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA wameanza ziara nchini Brazil kukagua miji miwili ambayo inaweza kuwa wenyeji wa michuano ya Kombe la Confederations inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwaka kesho. Wakaguzi hao wanatarajiwa kutembelea miji ya Salvador na baadae Recife ili kuangalia maendeleo ya ujenzi miundo mbinu pamoja na viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michuano hiyo. Baada ya ziara hiyo wakaguzi hao wanatarajia kuandaa taarifa ambayo wataiwasilisha kwa viongozi wa FIFA pamoja na Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Dunia ya nchi hiyo na maamuzi yatatolewa kama miji hiyo itapewa nafasi ya kuandaa michuano hiyo inayotarajiwa kufanyika Juni mwakani. Miji ya Salvador na Recife kama ikipitisha itaungana na miji mingine minne ambayo ni Rio de Janeiro, Brasilia, Belo Horizonte na Fortaleza ambayo yenyewe tayari imeshapitishwa kuandaa michuano hiyo.

HISPANIA YATUPIA TIMU MBILI FAINALI EUROPA LEAGUE.

TIMU za Athletic Bilbao na Atletico Madrid zote za Hispania zimefanikiwa kutinga katika hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Ligi la Ulaya maarufu kama Europa League baada ya kushinda michezo yao ya pili ya nusu fainali iliyochezwa jana usiku. Bilbao ilifanikiwa kutinga katika hatua hiyo baada ya kifunga mabao 3-1 timu ya Sporting Lisbon ya Ureno hivyo kufanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3 katika michezo yote miwili waliyocheza. Kwa upande wa Atletico wao walitinga katika hatua hiyo baada ya kufanikiwa kuifunga Valencia bao 1-0 na hiyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 5-2 katika michezo yao miwili waliocheza. Bilbao ambao pia walizitoa timu za Manchester United na Schalke, itakuwa inacheza fainali yake ya kwanza kwenye michuano hiyo ya Ulaya toka mwaka 1977 wakati walipofungwa na Juventus. Timu hizo zinatarajiwa kukutana katika mchezo wa fainali utakaochezwa Mei 9 mwaka huu katika Uwanja wa Bucharest, Romania.

UINGEREZA KUJIFUA NA BRAZIL OLIMPIKI.

TIMU ya soka ya Olimpiki ya Uingereza inatarajiwa kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Brazil kwa ajili kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ambayo wanashiriki kwa mara ya kwanza baada ya miaka 52. Kikosi hicho ambacho kiko chini ya kocha Stuart Pearce, kitaingia uwanjani kupambana Brazil Julai 20 katika Uwanja wa Riverside iliopo jijini Middlesbrough kabla ya kuanza kampeni ya kutafuta medali ya dhahabu wakati watapocheza na Senegal Julai 26 katika Uwanja wa Old Trafford jijini Manchester. Brazil ambao ni mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia lakini hawajawahi kushinda medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki wenyewe wataanza kampeni yao kwa kucheza na Misri tarehe kama hiyo katika Uwanja wa Millennium uliopo jijini Cardiff, Wales. Katika michuano ya soka kwenye Olimpiki timu za wanaume zinaruhusiwa kuwa na vijana chini ya miaka 23 huku kila timu ikiruhusiwa wachezaji watatu ambao watakuwa wamezidi umri huo wakati kwa upande wa wanawake wenyewe wanaruhusiwa kuwa na wachezaji wao wa timu za taifa.

Thursday, April 26, 2012

Real Madrid vs Bayern Munich - 2-1 [Agg. 3-3] - HIGHLIGHTS + Penalties

WAAMUZI TISA KUTOKA AFRIKA KUCHEZESHA OLIMPIKI.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetoa orodha ya waamuzi na wasaidizi watakaochezesha michuano ya Olimpiki jijini London ya soka kwa wanaume na wanawake. Waamuzi tisa kutoka Afrika ni miongoni jumla ya waamuzi 84 waliopo katika orodha hiyo kutoka nchi 36 ambao watachezesha michuano hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kati ya Julai 27 hadi Agosti 12 mwaka huu. Waamuzi sita kati ya hao wanatarajiwa kuchezesha soka kwa upande wa wanaume ambapo waamuzi wa kati watakuwa ni, Bakary Papa Gassama-Gambia na Slim Jedidi-Tunisia, washika vibendera ni Jason Joseph Damdoo-Shelisheli, Angesom Ogbamariam-Eritrea, Bechir Hassani-Misri na Sherif Hassan-Misri. Watatu waliobakia wenyewe watachezesha mpira kwa upande wa wanawake ambapo mwamuzi wa kati watakuwa ni Therese Raissa Neguel-Cameroon huku washika vibendera wakiwa ni Tempa Ndha-Benin na Lidwine Pelagie Rokotozafinoro-Madagascar. Katika michuano hiyo timu kutoka nchi za Gabon, Morocco, Misri na Senegal ndio watakuwa wawakilishi wa Afrika kwa upande wa wanaume wakati kwa upande wanawake Cameroon na Afrika Kusini ndio timu pekee zitakazowakilisha Afrika.

UEFA KUMJADILI TERRY.

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA inatarajia kukutana kumjadili nahodha wa klabu ya Chelsea, John Terry baada ya kutolewa nje katika mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa ya Ulaya dhidi ya Barcelona, Jumanne. Kwa kadi hiyo aliyopewa Terry atakosa mchezo mmoja ambao utakuwa ni wa fainali itakayochezwa Mei 9 jijini Munich lakini kwa sheria za UEFA inaruhusu kamati ya nidhamu kuongeza adhabu ambayo anaweza kuitumikia katika michuano ijayo ya Ulaya msimu ujao. Chelsea itapata pigo kubwa baada ya Branislav Ivanovic, Raul Meireles na Ramires nao kukosa mchezo w fainali baada ya kufungiwa mchezo mmoja kwa kupewa kadi za njano kwenye michezo mitatu mfululizo kwenye michuano hiyo. Kamati hiyo inatarajiwa kukutana Mei 31 ili kujadili hatma Terry kuhusiana na sula lake hilo.

NILIMGWAYA CASILLAS KUPIGA PENATI YA PILI.

MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich, Arjen Robben amekiri kuwa hakutaka kupiga penati katika mchezo wa pili wa nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa ya Ulaya dhidi ya Real Madrid akidai kuwa golikipa Iker Casillas anamfahamu vyema. Robben alipiga penati ya kwanza dakika 27 na kufanikiwa kuirejesha timu yake katika mchezo baada ya kufungwa mabao mawili ya mapema na wapinzani na kupelekea mchezo huo kuamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya kufungana mabao 3-3 katika michezo miwili walioyokutana. Hatahivyo Robben alijitoa kupiga penati nyingine ilipofikia hatua hiyo akidai kuwa ingekuwa ni ngumu zaidi kwake kutokana na Casilas kumfahamu vizuri udhaifu wake kwa kuwa walicheza wote katika kipindi cha miaka miwili alipokuwa Madrid. Katika mchezo huo Bayern walifanikiwa kushinda mchezo huo kwa changamoto ya mikwaju ya penati ambapo sasa watacheza na Chelsea katika fainali itakayofanyika Mei 9 mwaka huu katika uwanja wao wa nyumbani wa Alianz Arena, jijini Munich.

MOURINHO WANTS CHELSEA FINAL VICTORY.

KOCHA wa klabu ya Real Madrid, Jose Mourinho anataka Chelsea iwafunge Bayern Munich katika mchezo wa fainali ya Kombe la Klabu Bingwa ya Ulaya baada ya timu yake kutolewa katika hatua ya nusu fainali kwa changamoto ya mikwaju ya penati. Chelsea ilifanikiwa kuingia katika hatua hiyo baada ya kufanikiwa kuifunga Barcelona, pamoja na kucheza wachezaji kumi karibu kipindi chote cha pili baada ya Terry kutolewa kwa kadi nyekundu. Mourinho amewahi kuinoa Chelsea kipindi cha nyuma amesema kuwa angependa timu hiyo washinde kombe hilo kwani walionyesha ushujaa mkubwa walipoweza kuwafunga Barcelona wakiwa pungufu. Pia aliongeza kuwa anajivunia kikosi chake pamoja na kutolewa katika michuano hiyo na sasa wanaelekeza nguvu zao katika kuhakikisha wananyakuwa Kombe la Ligi Kuu nchini Hispania. Bayern ambao watakuwa wakifukuzia taji lao la tano, watakuwa ni klabu ya kwanza katika historia ya michuano hiyo kucheza fainali ya michuano hiyo wakiwa uwanja wa nyumbani toka AS Roma walipofanya hivyo mwaka 1984 ingawa walifungwa na Liverpool kwa changamoto ya mikwaju ya penati.

Wednesday, April 25, 2012

CITY KUFANYA ZIARA MALAYSIA.

KLABU ya Manchester City inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na nyota wa Malaysia mchezo ambao utafanyika jijini Kuala Lumpur Julai mwaka huu. City itakuwa katika ziara nchini humo wakati watakapocheza mchezo huo katika Uwanja wa Bukit Jalil ambao una uwezo wa kuchukua mashabiki 90,000 Julai 30 mwaka huu. Makamu wa rais wa Chama cha Soka cha Malaysia, Tengku Abdullah Sultan Ahmad Shah alithibisha kuwepo kwa mchezo huo na kusema kuwa ni heshima kubwa kwao kuwa nchi pekee barani Asia kucheza na City katika ziara yao ya kwanza barani humo. Mabingwa hao wa Kombe la Chama cha Soka cha Uingereza-FA pia watacheza na Arsenal katika Uwanja wa Bird Nest jijini Beijing, China Julai 27 siku ambayo ambayo kutafanyika sherehe za ufunguzi za Olimpiki.

MARADONA ATISHIA KUIHAMA AL WASL.

KOCHA wa klabu ya Al Wasl, Diego Maradona ametishia kuihama klabu hiyo ya Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE baada ya msimu huu wa Ligi Kuu ya nchi hiyo. Maradona amesema kuwa ana mpango wa kukutana na Ofisa Mkuu wa klabu hiyo wiki ijayo ili aweze kumuongeza kumuongeza fungu la kununua wachezaji ambao watamuwezesha kuiweka timu kiushindani zaidi kuliko hivi sasa. Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Argentina ambaye alichukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo Mei mwaka jana amesema kuwa kuondoka katika klabu hiyo hakumaanishi kwamba amepata timu nyingine bali anahisi klabu hiyo imevunja waliompa ya kununua wachezaji ambao atawahitaji. Hii sio mara ya kwanza kwa Maradona kutishia kusitisha mkataba na klabu hiyo kutokana na kutokuwa na wachezaji wazoefu kwani alitishia kuondoka Februari mwaka huu kutokana na pesa kidogo anayopewa kwa ajili kununua wachezaji.

PEARCE KUMFUATA BECKHAM MAREKANI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Stuart Pearce anatarajiwa kusafiri kwenda Marekani kumuona mchezaji wa Los Angeles Galaxy David Beckham akicheza kabla ya kuamua kumuita mchezaji huyo katika michuano ya Olimpiki itakayofanyika jijini London. Beckham ni miongoni mwa wachezaji 80 ambao wako katika orodha ya kuteuliwa katika kikosi cha nchi hiyo ambacho kitashiriki michuano hiyo huku wachezaji ambao watahitajika katika orodha hiyo ni 18 tu. Mchezaji atakuwa na nafasi ya kumshawishi Pearce kumteua katika kikosi chake wakati kocha huyo atapotizama mchezo kati ya Galaxy na Seattle Sounders utakaofanyika Mei 2 mwaka huu. Beckham ambaye ni nahodha wa zamani wa Uingereza angependa kucheza michuano hiyo ya Olimpiki kabla ya kustaafu kucheza soka.

MOURINHO KUENDELEA KUINOA MADRID.

KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho amesema kuwa angependa kubakia kuinoa klabu hiyo ambayo leo itakuwa ikitafuta nafasi kucheza fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich. Kwasasa kocha huyo mkataba wake unaishia mwaka 2014 na mara nyingi amekuwa akikataa kuthibisha kama ataendelea na klabu hiyo huku kukiwa na taarifa za kurejea katika klabu yake ya zamani ya Chelsea au Manchester City. Akihojiwa na waandishi wa habari kabla ya mchezo wao na Bayern Munich, Mourinho ambaye ni raia wa Ureno amesema kuwa anadhani ataendelea kuinoa klabu hiyo kwa kuwa hana sababu ya kuondoka. Ameendelea kusema kuwa atazungumza na wachezaji pamoja na viongozi wa klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu kama watamuhitaji kubakia katika klab u hiyo.

NILISTAHILI KADI NYEKUNDU-TERRY.

NAHODHA wa Chelsea, John Terry amesema kuwa alistahili kadi nyekundu wakati kikosi chake kilipotoa sare na mabao 2-2 na kufanikiwa kuingia fainali ya michuano ya Kombe la Klabu Bingwa ya Ulaya. Terry alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 37 na mwamuzi Cuneyt Cakir kutoka Uturuki ambaye alichezesha mchezo huo baada ua kumkwatua Alexis Sanchez kwa nyuma. Mchezaji huyo ambaye sasa atakosa mchezo wa fainali ya michuano hiyo itakayofanyika Mei 9 mwaka huu amesema kuwa anajutia kufanya kutendo hicho lakini akakiri kuwa hakudhamiria kama inavyoonekana katika picha za video. Chelsea pia itamkosa beki wake mwingine Branislav Ivanovic katika mchezo huo wa fainali utaofanyika jijini Munich, Ujerumani baada ya beki huyo kupewa kadi nyingine ya njano katika mchezo huo.

Champions League Semi-Final - Barcelona Vs Chelsea 2-2 Fernando Torres Goal

Tuesday, April 24, 2012

LONDON 2012: MAKUNDI YA TIMU ZITAKAZOSHIRIKI OLIMPIKI.

Ronaldo de Lima akisaidia upangaji wa ratiba za michuano ya Olimpiki.

 MEN'S DRAW:
Group A: Great Britain, Senegal, United Arab Emirates, Uruguay
Group B: Mexico, South Korea, Gabon, Switzerland
Group C: Brazil, Egypt, Belarus, New Zealand
Group D: Spain, Japan, Honduras, MoroccoWOMEN'S DRAW:
Group E: Great Britain, New Zealand, Cameroon, Brazil
Group F: Japan, Canada, Sweden, South Africa
Group G: USA, France, Colombia, Korea DPR

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

WATANZANIA KUCHEZESHA AFRIKA KUSINI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua waamuzi wane wa Tanzania kuchezesha mechi ya marudiano ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho kati ya Black Leopards ya Afrika Kusini na Warri Wolves ya Nigeria itakayochezwa nchini Afrika Kusini kati ya Mei 4, 5 na 6 mwaka huu. Waamuzi hao ni Waziri Sheha atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake watakuwa John Kanyenye na Erasmo Jesse. Mwamuzi wa akiba (fourth official) atakuwa Israel Mujuni. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Aurelio Mathias wa Msumbiji. Mechi ya kwanza kati ya timu hizo itachezwa Jumapili (Aprili 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Warri City ulioko Jimbo la Delta nchini Nigeria na itachezeshwa na waamuzi kutoka Senegal wakati Kamishna atakuwa Inyangi Bokinda wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

1,635 WASHUHUDIA MECHI YA YANGA, POLISI DODOMA
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Polisi Dodoma iliyochezwa (Aprili 22 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ilishuhudiwa na watazamaji 1,635 na kuingiza sh. 5,666,000. Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 864,305.08 kila klabu ilipata sh. 193,858.47, uwanja sh. 26,469.49. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 26,469.49, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 108,687.80. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 13,234.75, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 2,646.95 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 26,469.49. Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. Mwamuzi wa akiba sh. 30,000, posho ya kujikimu kwa kamishna na waamuzi sh. 160,000, gharama ya tiketi sh. 1,500,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 1,500,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 1,000,000. Kutokana na mechi hiyo kuingiza kiasi kidogo baadhi ya gharama zililipwa nusu au kutolipwa kabisa na kuacha madeni. Madeni hayo ni tiketi sh. 1,500,000, maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 850,000 na Wachina sh. 1,000,000.

POLISI MORO, MGAMBO, PRISONS ZAPANDA VPL
Fainali ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iliyoshirikisha timu tisa imemalizika jana (Aprili 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku tatu zikifuzu kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2012/2013 utakaonza Agosti mwaka huu. Timu hizo ni Polisi Morogoro iliyofikisha pointi 20 ikifuatiwa na Mgambo Shooting ya Tanga (15) na Tanzania Prisons ya Mbeya iliyomaliza katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 14. Nyingine zilizofuatia na pointi zao kwenye mabano ni Polisi Dar es Salaam (13), Mbeya City Council (11), Rhino Rangers ya Tabora (8), Mlale JKT ya Ruvuma (8), Polisi Tabora (6) na Transit Camp ya Dar es Salaam (2).

SIMBA, MORO UNITED ZAINGIZA MIL 28/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Moro United lililochezwa jana (Aprili 23 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 28,688,000. Jumla ya watazamaji 7,945 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000. Watazamaji 6,946 kati ya hao walishuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000. Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 4,376,135.59 kila klabu ilipata sh. 4,919,009.32, uwanja sh. 1,454,286.44. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 1,454,286.44, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,058,414.58, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 727,143.22, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 145,428.64 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 1,454,286.44. Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000, mwamuzi wa akiba sh. 30,000, posho ya kujikimu kwa kamishna na waamuzi sh. 80,000, gharama ya tiketi sh. 3,000,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000. Nayo mechi kati ya Villa Squad na African Lyon iliyochezwa Aprili 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam iliingiza sh. 496,000 ambapo kila klabu ilipata sh. 68,061.70 wakati watazamaji walioshuhudia mechi hiyo ni 469. Vilevile mechi kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Sudan iliyochezwa Aprili 21 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliingiza sh. 9,717,000 kutokana na washabiki 2,562.

MECHI ZA LIGI KUU WIKIENDI HII
Ligi Kuu ya Vodacom imeingia raundi ya 25 ambapo kesho (Aprili 25 mwaka huu) Oljoro JKT itaikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. Raundi hiyo itakamilika kwa mechi nne; Aprili 28 mwaka huu Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mtibwa Sugar ikiwa mgeni wa African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi. Azam na Toto African zitacheza Chamazi, Aprili 30 mwaka huu wakati Mei 1 mwaka huu Villa Squad itaumana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi. Ligi hiyo itafunga msimu wa 2011/2012, Mei 5 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa uwanjani. Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Polisi Dodoma (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Ruvu Shooting vs Villa Squad (Mabatini, Mlandizi). Mechi nyingine zitakuwa kati ya Coastal Union vs Toto African (Mkwakwani, Tanga), African Lyon vs JKT Ruvu (Manungu, Morogoro), Azam vs Kagera Sugar (Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro).

FRANKFURT YAREJEA BUNDESLIGA BAADA YA KUPOROMOKA MSIMU ULIOPITA.

KLABU ya Eintracht Frankfurt imefanikiwa kurejea katika Ligi Kuu nchini Ujerumani wakiungana na timu ya Greuther Fuerth kama timu mbili ambazo zimepanda daraja kutoka daraja la pili zilipokuwa. Hakuna timu yoyote kati ya Frankfurt au Fuerth ambazo zinaweza kuondolewa katika nafasi hizo mbili za kupanda daraja baada ya timu hizo kuongoza kwa lama nane ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine katika msimamo wa ligi hiyo. Kocha Mkuu wa Frankfurt, Armin Veh ambaye alichukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo wakat iliposhuka daraja msimu uliopita amesema kuwa anahitaji muda ili kujua hatma yake huko mbele baada ya kuiwezesha klabu hiyo kurejea Bundesliga. Hatahivyo Mkurugenzi wa klabu hiyo amesema kuwa anaamini kuwa Veh mwenye umri wa miaka 51 ambaye amewahi kuvinoa vilabu vya VFB Stuttgart, Wolfsburg na SV Hamburg kwamba atasaini mkataba mpya na klabu hiyo.

DENMARK BANS PLAYERS FROM TWEETING.

SHIRIKISHO la Soka nchini Denmark limesema kuwa wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo hawataruhusiwa kutumia mitandao ya kijamii wakati wa michuano ya Ulaya itakayofanyika June mwaka huu. Golikipa wa kikosi cha nchi hiyo Thomas Sorensen amesema kuwa ni aibu kwa wachezaji kutowasiliana na mashabiki wao kuwajuza wanachofanya bila kuweka wazi mikakati yao. Msemaji wa shirikisho hilo Lars Behrendt amesema kuwa kocha wa timu hiyo amefanya hivyo ili wachezaji wa timu hiyo waweze kuweka mawazo yao katika mchezo huo na sio kitu kingine. Behrendt aliendelea kusema wachezaji wataruhusiwa kuwasiliana na mashabiki kupitia mtandao wa kijamii wa timu hiyo ambao utafunguliwa na sio wa mchezaji binafsi ingawa suala hilo limepingwa na Waziri wa michezo wa nchi hiyo Uffe Elbaek akisema kuwa unawanyima wachezaji hao uhuru wa kuongea.

BOSI WA RANGERS AWEKWA 'LUPANGO' MAISHA.

KLABU ya Glascow Rangers imefungiwa kusajili wachezaji kwa muda wa mwaka mmoja na mmiliki wa klabu hiyo Craig Whyte yeye amefungiwa maisha kutojishughulisha na mchezo wa soka nchini Scotland kufuatia matatizo ya kifedha yanayoikabili klabu hiyo. Rangers ambao taji la ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo mara 54 waliingia katika mfumo wa utawala ambao ungewalinda wasifilisike Februari mwaka huu wakiwa na deni linalofikia dola milioni 14 toka Whyte alipoichukua klabu hiyo Mei mwaka jana. Mahakama ya Nidhamu ilimkuta Whyte na makosa mawili ya uvunjaji wa nidhamu kati ya Mei 6 mwaka 2011 na machi 6 2012 na kumtoza faini ya kiasi cha dola 320,000 wiki sita zilizopita ambapo Chama cha Soka cha nchi hiyo kilimuelezea kama mtu asiyefaa kujishughulisha na michezo. Kikwazo katika usajili iliyowekewa klabu hiyo kwa mwaka mmoja imekuja baada ya klabu hiyo kuvunja sheria tano za kinidhamu kwa wakati mmoja hivyo kifungo hicho kinapelekea Rangers kusajili wachezaji wa umri chini ya miaka 18 katika kipindi chote hicho cha adhabu. Rangers ambayo pia imetozwa faini ya dola 260,000 inaweza kufilisiwa kama haitapata mnunuzi mwingine ifikapo mwishoni mwa msimu huu.

SENEGAL FOOTBALL FEDERETION ACCOUNTS FROZEN.

SHIRIKISHO la Soka la Senegal-FSF limefungiwa akaunti zake kwa maagizo ya mahakama ya jijini Dakar kufuatia kesi waliyofunguliwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo Amara Traore. Rais wa FSF Augustin Senghor aliwapa taarifa hizo waandishi wa habari nchini humo kwa njia ya simu kutoka jijini Coventry, Uingereza ambapo timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ya nchi hiyo ilifanikiwa kuifunga Oman na kufanikiwa kufuzu michuano ya Olimpiki itakayofanyika jijini London mwaka huu. Mahakama ya Saint Louis iliyopo Kaskazini mwa Senegal mapema mwezi huu iliamuru FSF kumlipa Traore Francs milioni 36 zikiwa ni pesa za malimbikizo ya mshahara wa miezi miwili pamoja na posho za likizo. Traore alitimuliwa kukinoa kikosi cha nchi hiyo baada ya kutolewa katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Januari mwaka huu ambapo walitolewa katika hatua ya makundi.

SENEGAL YAFUZU OLIMPIKI.

TIMU ya taifa wa Senegal ya vijana chini ya miaka 23, imekuwa timu ya mwisho kukata tiketi ya kucheza michuano ya Olimpiki baada ya kufanikiwa kuifunga Oman kwa mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa jijini Coventry, Uingereza. Bao kuongoza la Senegal lilifungwa katika dakika za mwanzo za mchezo kupitia mpira wa adhabu wa adhabu uliopigwa na Pape Ndiaye Souare anayecheza katika klabu ya Lille ya nchini Ufaransa kabla ya Ibrahima Balde kumalizia anayecheza klabu ya Osasuna ya Hispania kumalizia mpira huo kwa kichwa. Mara baada ya bao hilo Oman walionekana kuongeza mashambulizi ili kurejesha bao hilo juhudi ambazo hazikuzaa matunda baada ya kiungo Abdoulaye Sane anayecheza katika klabu ya Rennes nayo ya Ufaransa kuipatia timu yake bao la pili katika dakika 86 na kuzima ndoto za za Oman kushiriki michuano hiyo. Senegal inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza wakati watakapojumuika na timu zingine 14 ambazo tayari zimefuzu michuano hiyo ambazo ni Korea Kusini, Japan, Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE, Gabon, Morocco, Misri, Uingereza, Hispania, Switzerland, Belarus, Honduras, Mexico, New Zealand, Brazil na Uruguay.

BRITAIN, SPAIN, BRAZIL, MEXICO SEEDED.

TIMU za Uingereza ambao ndio wenyeji wa michuano ya Olimpiki, Hispania ambao ni mabingwa wa dunia, Brazil na Mexico zimetajwa na Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA kuongoza makundi yao kati ya timu 16 za soka za wanaume zitakazoshiriki michuano hiyo katika ratiba itakayopangwa baadae leo. Kwa upande wa wanawake ambapo kutakuwa na timu 16, Uingereza, Japan ambao ni mabingwa wa dunia kwenye soka la wanawake, na bingwa mtetezi wa michuano hiyo Marekani wao ndio watakaoongoza makundi yao katika soka la wanawake katika michuano hiyo. Katika michuano hiyo kwa upande wa wanaume timu 16 zitagawanywa katika makundi manne ambapo Uingereza itaongoza kundi A kwa mara ya kwanza toka walipoandaa michuano hiyo mwaka 1960. Mexico wenyewe wataongoza kundi B wakati Brazil ambao nndio timu pekee ambayo ina rekodi nzuri na michuano hiyo pamoja na kwamba hawajawahi kupata medali ya dhahabu wataongoza kundi C na Hispania wataongoza kundi D.

Monday, April 23, 2012

TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA (TFF) LEO

Mkutano mkuu wa mwaka 2011 wa TFF Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) wa 2011 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umefanyika kwa siku mbili (Aprili 21-22 mwaka huu) kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront na kuhudhuriwa na wajumbe 104. Mkutano ulipokea taarifa, kufanya uamuzi katika masuala mbalimbali na mengine yaliyojitokeza kama ifuatavyo;
Sais El  Maamry , Muhidini  Ndolanga  Watunikiwa  Urais wa Heshima  AGM ilipitisha pendekezo la kuwatunuku urais wa heshima wa TFF, Alhaji Said Hamad El Maamry na Muhidin Ahamadi Ndolanga lililowasilishwa na Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Rais wa TFF, Leodegar Tenga.Alhaji El Maamry ambaye ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) alikuwa Mwenyekiti wa TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) kuanzia mwaka 1973 hadi 1986. Alhaji Ndolanga aliongoza FAT kuanzia mwaka 1993 hadi 2004.Bajeti ya mwaka  2012Bajeti ya Mwaka 2012 ya sh. 7,246,628,650 kwa ajili ya matumizi ya TFF ilipitishwa. Kwa mwaka 2012 TFF inatarajia kukusanya sh. 7,572,991,433 kupitia vyanzo mbalimbali. Vyanzo hivyo ni viingilio vya uwanjani vinavyotarajiwa kuingiza asilimia 22 ya mapato yote, udhamini (asilimia 74) na vyanzo vingine kama haki za matangazo ya televisheni, ada za ushiriki wa timu katika mashindano mbalimbali, misaada kutoka FIFA na CAF ambayo kwa pamoja vinatarajiwa kuingiza asilimia nne ya mapato yote. Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itaendelea na mchakato wa kupendekeza mifumo mitatu tofauti ya chombo kitakachosimamia/kuendesha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ikieleza faida na athari za kila mfumo uliopendekezwa na baadaye kuwafanya mawasilisho (presentation) kwenye Kamati ya Utendaji.Baada ya kuwasilisha mifumo hiyo kwa Kamati ya Utendaji, Kamati ya Ligi itapendekeza mfumo upi kati yao hiyo inaoona unafaa kabla ya kufanyika uamuzi wa mwisho. Lengo la kuunda chombo maalumu cha kuendesha ligi ni kuongeza ufanishi katika uendeshaji wa VPL na FDL, na pia kuifanya Sekretarieti ya TFF kushughulikia zaidi shughuli za maendeleo.Uuzwaji wa Timu, linabaki kuwa suala la kisheria. Lakini TFF imeweka utaratibu ufuatao; lazima Mkutano Mkuu wa klabu husika uidhinishe uuzaji, na timu ikishauzwa inabaki katika mkoa husika. Mfumo wa mashindano kwa vile kuna tatizo la ligi mbalimbali kuwa fupi, hali inayosababisha baadhi ya wachezaji katika madaraja ya chini kucheza ligi zaidi ya moja katika msimu mmoja, mfumo wa ligi/mashindano utaangaliwa upya.Mfumo uliopo sasa uliwekwa kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika mpira wa miguu ambapo mwekezaji anaweza kuanzisha timu, na ndani ya miaka mitatu ikacheza Ligi Kuu. Pili, ilikuwa ni kuondoa mlolongo mrefu wa ligi, na kuwafanya wanachama wa TFF (mikoa) nao kuendesha ligi zao mikoani. Ijulikane kuwa ligi za mikoa (regional leagues) zinachezwa. Kwa sababu TFF inaendeshwa kwa mfumo wa shirikisho (federation), nia ni wanachama wa federation nao kuwa na majukumu ya kusimamia na kuendesha ligi, kwa vile TFF haiwezi kusimamia ligi zote. Marekebisho ya katiba ya Mkutano Mkuu wa TFF umepitisha marekebisho ya Katiba katika maeneo mawili; moja ni kuanzisha Baraza la Wadhamini ambalo linatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua watatu na wasiozidi watano.Marekebisho mengine ni kuongeza idadi ya kanda kutoka kumi na moja za sasa hadi 13. Marekebisho hayo yamefanyika kutokana na Serikali kuongeza mikoa mipya ya kijiografia. Kanda mpya sasa zitakuwa Kagera/Geita, Arusha/Manyara, Kilimanjaro/Tanga, Katavi/Rukwa, Njombe/Ruvuma, Dodoma/Singida, Dar es Salaam, Shinyanga/Simiyu, Mwanza/Mara, Lindi/Mtwara, Kigoma/Tabora, Mbeya/Iringa na Pwani/Morogoro.Ukiondoa mamlaka ya uteuzi aliyonayo Rais kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji huchaguliwa kwa kanda. Hesabu zilizokaguliwa na Mkutano Mkuu ulipitisha hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2010 (Audited Accounts) , na pia kuiteua kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya TAC Associates kuwa mkaguzi wa hesabu za TFF kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Yanga yaomba radhi mkutano mkuu ,Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Bhinda aliwaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kitendo cha wachezaji wake kumpiga mwamuzi Israel Nkongo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu.Pia alimuomba Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutoa msamaha wa adhabu ya kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji wawili wa Yanga ambao mpaka sasa hawajalipa faini hiyo. Rais Tenga alimshukuru Bhinda kwa ujasiri alioonesha wa kuomba radhi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kitendo kile. Aliongeza kuwa kwa vile yeye ni muumini wa kanuni, na adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni hawezi kutoa msamaha, hivyo wachezaji hao walipe faini hizo.Pia Rais Tenga alisema binafsi haziingilia kamati za TFF katika uamuzi ambao zinafanya kwa vile zina watu waadilifu, na angekuwa yeye binafsi ndiye anayetoa adhabu, angetoa adhabu kali zaidi kwa vile vitendo vya kupiga waamuzi havikubaliki katika mchezo wa mpira wa miguu. Kanuni za nidhamu ,mahakama ya usuluhishi - Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Rais Tenga aliwaambia wajumbe kuwa Kanuni za Nidhamu (Disciplinary Code) za TFF na uundaji wa Mahakama ya Usuluhishi (Arbitration Tribunal) ya TFF ambacho ndicho kitakuwa chombo cha juu cha kutoa haki kwa masuala ya mpira wa miguu nchini vitakamilika mwaka huu.Pia TFF itaendelea kutafuta wadhamini kwa ajili ya timu za Taifa za vijana na wanawake, itaendelea kuendesha semina na makongamano katika nyanja mbalimbali za mpira wa miguu, kutengeneza mtaala wa academy na kutengeneza mpango wa maendeleo (Comprehensive Plan) baada ya ule wa awali kumalizika mwaka huu.

ADRIANO KUISHITAKI CORINTHIANS.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Corinthians, Adriano ameelezea nia yake ya kuchukua hatua za kisheria kwa klabu yake hiyo akidai kuwa walimfanya mfungwa wakati klabu hiyo ilipomfungia hotelini na kumpa mazoezi ya kupunguza uzito kwa muda wa wiki moja. Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amesema hayo wakati akihojiwa na luninga moja nchini Brazil akimtupia lawama kocha wa klabu hiyo akisema kuwa wamemwacha huku wakiwa wamemdhalilisha. Aliendelea kusema kuwa atachukua hatua za kisheria kwa klabu hiyo kwa kumuweka kama mfungwa kwa wiki moja kitendo ambacho hakuwa ameridhika nacho hivyo aliona kama adhabu. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Inter Milan katika mahojiano hayo amekiri kuwa na matatizo kutokana na kuongezeka uzito wakati akiichezea klabu hiyo.

UKRAINE HATARINI KUMKOSA NA GOLIKIPA WAKE WA TATU.

TIMU ya taifa wa Ukraine ambao ni wenyeji wenza wa michuano ya Ulaya 2012 iko katika hatari ya kumpoteza golikipa wake wa tatu baada ya Oleksandr Shovkovskiy anayecheza katika klabu ya Dynamo Kiev kuumia bega wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo jana. Kocha Mkuu wa Kiev, Yuri Syomin amesema kuwa mchezaji huyo atafanyiwa vipimo zaidi ilikujua ukubwa wa tatizo lake lakini kwa jinsi inavyoonekana tatizo linaweza kuwa kubwa. Kuumia kwa kipa huyo itakuwa ni pigo kwa kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo kutokana na kuwapoteza makipa wengine wazoefu wawili. Oleksandr Rybka ambaye ndiye kipa chaguo la kwanza katika kikosi hicho amefungiwa kutokana na kutumia madawa ambayo yamekatazwa michezoni wakati Andriy Dykan ambaye ndiye chaguo la pili yeye amevunjika mkono wakati mechi mwezi uliopita. Katika michuano ya Ulaya ambayo Ukraine imeandaa kwa pamoja na Poland imepangwa kundi na timu za Uingereza, Ufaransa na Sweden katika kundi D.

VAN PERSIE WIN PFA PLAYER AWARD.

MSHAMBULIAJI wa Arsenal, Robin van Persie ametajwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa kulipwa katika Ligi Kuu nchini Uingereza. Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 amefunga mabao 38 msimu huu yakiwemo mabao 34 katika mashindano yote akiwa na klabu ya Arsenal. Akihojiwa mara baada ya kupokea tuzo hiyo mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi ambaye kwasasa ndiye anayeongoza kwa ufungaji katika ligi hiyo amesema tuzo hiyo ni kitu muhimu sana kwake na aliwashukuru wachezaji wenzake kwani bila ushirikiano wao asingefika hapo alipo. Van Persie amenyakuwa tuzo hiyo mbele ya mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney, Scott Parker wa Tottenham Hotspurs na Sergio Aguero, Joe Hart na David Silva wote wa Manchester City.

Sunday, April 22, 2012

KUPONA KWANGU NI ZAIDI YA MAAJABU-MUAMBA.

KIUNGO wa klabu ya Bolton Wanderers, Fabrice Muamba amesema kuwa kupona kwake kufuatia ugonjwa wa moyo wake kusimama ghafla ni zaidi ya maajabu ambayo hayakutegemewa. Muamba mwenye umri wa miaka 24 aliongea na gazeti la Sun la Uingereza kwa mara ya kwanza toka mapigo yake ya moyo yaliposimama kwa dakika 178 baada ya kuanguka wakati wa mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs mwezi uliopita. Mchezaji huyo amesema kuwa kilichomtokea ni maajabu kwani asubuhi kabla ya mchezo huo alienda kwenye maombi na baba yake na kumuomba mungu amlinde na alifanya hivyo baada kumponya na umauti baada ya kuanguka jioni yake. Muamba aliruhusiwa kutoka hospitalini Jumatatu iliyopita baada ya kuonyesha kupona vizuri ikiwa ni zaidi ya mwezi toka alipoanguka ingawa haijajulikana kama mchezaji huyo atarejea tena kucheza soka katika siku za mbeleni.


GUARDIOLA AWAPONGEZA MADRID.

KOCHA wa Barcelona Pep Guardiola amewapongeza Real Madrid kama mabingwa wapya wa Ligi Kuu nchini Hispania baada ya kikosi chake kufungwa mabao 2-1 na mahasimu wao hao katika Uwanja wa Camp Nou jana. Kipigo kinaifanya Madrid kuongoza ligi hiyo kwa alama saba huku wakiwa wamebakiza michezo minne na kukaribia kunyakuwa taji hilo ambalo wamelikosa toka mwaka 2008 huku katika historia wakiwa wamelinyakuwa mara 32. Guardiola alikisifu kikosi cha Madrid kwa ushindi huo ambao amesema kuwa hana shaka kuwa watanyakuwa taji la ligi ingawa pia alikisifu kikosi chake kwa kucheza soka safi lakini bahati haikuwa yao safari hii. Kwasasa Barcelona inabidi wajipange upya kwa ajili ya mchezo wao wa nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Chelsea ambapo itabidi watafute ushindi wowote baada ya kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza.

BLATTER AMTEMBELEA MWENZAKE.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amemtembelea rais aliyemtangulia Joao Havelange ambaye amelazwa kwa zaidi ya mwezi katika hospitali moja jijini Rio de Janeiro, Brazil. Blatter aliandika taarifa ya kwenda kumtembelea Havelange katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter kuwa alikuwa katika safari binafsi yeye pamoja na binti yake aitwaye Carinne wakielekea hospitalini Rio De Janeiro kumtembelea Havelange. Madaktari katika hospitali ya Samaritano anapotibiwa Havelange wamesema kuwa kifundo cha mguu wa kulia ambacho ndicho kilichosababisha kulazwa kwa rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 95 tayari umepona kwasasa bado anatumia dawa kujaribu kutibu matatizo ya moyo ambayo yalimkumba karibuni. Mara baada ya kumuona Havelange ambaye aliwahi kuingoza FIFA kuanzia mwaka 1978 mpaka 1998, Blatter aliandika katika mtandao huo kuwa amefurahi kuona anaendelea vizuri na ana matumaini atapona kabisa na kuendelea na shughuli zake.

MADRID WAVUNJA REKODI YAO WENYEWE.

KLABU ya Real Madrid imefanikiwa kuvunja rekodi ya mabao katika Ligi Kuu ya Hispania kwa msimu mmoja baada ya kufanikiwa kuwafunga mahasimu wao Barcelona kwa mabao 2-1. Bao la Sami Khedira alilofunga katika dakika ya 17 liliifanya timu hiyo kufikisha mabao 108 katika msimu huu wakivunja rekodi yao wenyewe ya mabao 107 waliyoiweka katika msimu wa mwaka 1989-1990 wakati kikosi hicho kikinolewa na Hugo Sanchez kutoka Mexico. Mshambuliaji wa Madrid Cristiano Ronaldo alifanikiwa kuongeza bao lingine la ushindi dakika ya 73 na kufanikiwa kufikisha mabao 42 katika msimu huu ikiwa ni bao moja zaidi ya mpinzani wake Lionel Messi ambaye ana mabao 41. Katika msimu wa 1989-1990 Madrid walifanikiwa kushinda taji la ligi kuu ikiwa ni taji lao la tano mfululizo kushinda katika kipindi hicho.

WELBECK ASAINI MKATABA MREFU NA UNITED.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Manchester United Danny Welbeck anatarajiwa kutia saini ya mkataba wa miaka mitano mwishoni mwa msimu huu baada ya kufikia makubaliano na klabu hiyo. Welbeck mwenye umri wa miaka 21 amekubali kusaini mkataba huo utakaomuwezesha kuwa akilipwa kiasi cha paundi 45,000 kwa wiki. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza ambaye mkataba wake wa awali unaisha mwishoni mwa msimu huu aliwaambia wachezaji wenzake kuwa amefurahishwa na kusaini mkataba mrefu na klabu hiyo kabla hajakwenda kuitumikia nchi yake katika michuano ya Ulaya baadae mwaka huu. Welbeck ambaye msimu uliopita alipelekwa kwa mkopo katika klabu ya Sunderland, amefunga mabao 11 katika mashindano yote msimu huu huku akichukua nafasi ya Dimitar Berbatov na Juvier Hernandez kama chaguo la kwanza kwa washambuliaji wa klabu hiyo ambaye anaweza kucheza sambamba na Wayne Rooney.

Fc Barcelona vs Real Madrid 1-2 all goals & full match highlights 21.04....

Saturday, April 21, 2012

EL MAAMRY, NDOLANGA WAULA TFF.

WENYEVITI wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Said Hamad El Maamry na Muhiddin Ahmad Ndolanga wameteuliwa kuwa Marais wa heshima wa shirikisho hilo, katika Mkutano Mkuu wa TFF unaoendelea kwenye ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam. Habari kutoka ndani ya Mkutano huo, ambao utaendelea hadi kesho, zimesema kwamba viongozi hao wa zamani nchini wamepewa heshima hiyo na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kutokana na mchango wao katika soka ya Tanzania, enzi zao wakiwa madarakani wakati TFF ikiitwa FAT (Chama cha Soka Tanzania). Aidha, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wameambiwa kuwa Hati ya Uwanja wa Karume haishikiliwi na benki kutokana na deni la ziara ya timu ya taifa ya Brazil Juni 2012, zaidi ya Sh. Bilioni 3, kwani deni hilo lilidhaminiwa na Serikali. Mkutano huo unatarajiwa kufungwa muda si mrefu katika siku yake ya kwanza leo, ili Wajumbe wakawahi kuangalia mechi ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro dhidi ya Sudan, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mkutano huo, utaendelea tena kesho katika siku ya mwisho na tarehe ya uchaguzi Mkuu, utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu, inatarajiwa kupangwa rasmi hiyo kesho.

MESSI KARIBUNI KUITWA BABA.

Messi na mpenzi wake Antonella wakivinjari.
Lionel Messi anahesabika kuwa mchezaji bora kuwahi kutokea katika mchezo wa soka hivi karibuni anaweza kukabiliwa na changamoto nyingine nje ya uwanja kutokana na ripoti zilizozagaa kuwa anaweza kuitwa baba. Habari hizo zilianza kusambaa kwa mara ya kwanza katika radio moja nchini Argentina na toka hapo vyombo mbalimbali vya habari vimekuwa vikitangaza habari hizo kwamba mshambuliaji huyo wa Barcelona anategemea kupata mtoto na rafiki yake wa kike wa siku nyingi aitwae Antonella Roccuzzo. Gazeti moja nchini Argentina liitwalo Diario Uno ambapo linatengenezwa katika mji ambao Messi ametokea liliripoti kuwa walijaribu kuwasiliana na wazazi wa Messi kuthibitisha habari hizo lakini hakuna aliyekuwa habari hiyo lakini pia hawakukataa kuhusiana na tetesi hizo. Messi amekuwa mfungaji anayeongoza kwa mabao mengi katika historia ya klabu ya Barcelona akiwa amefunga mabao 234 mpaka sasa akiwa bado na umri mdogo wa 24 tu. Kocha wake Pep Guardiola amethubutu kumfananisha mchezaji huyo na nyota wa zamani wa mpira wa kikapu kutoka Marekani, Michael Jordan.

RIJKAARD KUELEKEA MEXICO.

KOCHA wa zamani wa Barcelona Frank Rijkaard ameripotiwa kuhusishwa na tetesi za kuhamia katika klabu ya Chivas ya nchini Mexico. Rijkaard ambaye ana umri wa miaka 49 kwasasa anakinoa kikosi cha timu ya taifa ya Saudia Arabia lakini kwa mujibu chanzo kimoja kilichopo karibu na klabu hiyo kocha huyo yuko karibu kuhamia Mexico kama wakifikia muafaka katika suala la mshahara. Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi wakati akiinoa Barcelona alifanikiwa kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu nchini Hispania na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kuondoka klabuni hapo mwaka 2008. Baada ya kuiacha Barcelona alienda kuinoa Galatasaray kabla ya kwenda Saudi Arabia mwaka jana ingawa hivi sasa anaonekana kutamani kurejea kunoa vilabu baada ya nchi hiyo kutolewa katika mzunguko wa tatu wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 kwa nchi za bara la Asia.

Friday, April 20, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

KOCHA NGORONGORO HEROES AAHIDI USHINDI
Kocha Kim Poulsen anayeinoa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 cha Tanzania (Ngorongoro Heroes) ameahidi kikosi chake kufanya vizuri kwenye mechi dhidi ya Sudan. Akizungumza jana (Aprili 20 mwaka huu) kwenye mkutano na Waandishi wa Habari, Poulsen amesema timu yake imejiandaa vizuri kwa mechi hiyo na kiu yao ni kushinda. Kwa upande wake Kocha wa Sudan, Azhari Osman El Tahir amesema ingawa haifahamu vizuri timu ya Tanzania, lakini wamejiandaa kushinda kwani kwa muda mrefu walikuwa hawajashiriki mashindano ya vijana ya kimataifa. Mechi hiyo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri huo itachezwa kesho (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000. Sudan iliwasili nchini jana (Aprili 19 mwaka huu) ikiwa na kikosi cha wachezaji 20, viongozi kumi na mwandishi wa habari mmoja kwa ajili ya mechi hiyo ya kwanza kabla ya timu hizo kurudiana jijini Khartoum kati ya Mei 4, 5 na 6 mwaka huu. Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Brian Miiro atakayesaidiwa na Mark Ssonko, Lee Patabali na Denis Batte wote kutoka Uganda. Ejigu Ashenafi wa Ethiopia ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 15. Fainali za Afrika kwa michuano hiyo zitafanyika Machi mwakani nchini Algeria wakati za Dunia zitafanyika nchini Uturuki kuanzia Juni hadi Julai mwakani. Katika fainali za Dunia, Afrika itawakilishwa na timu nne za kwanza kwenye fainali za Algeria.


MALINZI MGENI RASMI MKUTANO MKUU TFF
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika kwa siku mbili (Aprili 21 na 22 mwaka huu) kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano huo watawasili jijini kesho (Aprili 20 mwaka huu) na watafikia kwenye hoteli ya Royal Valentino. Wajumbe wanatoka katika vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom. Mkutano huo utakaoanza saa 3 asubuhi utakuwa na ajenda kumi na moja. Baadhi ya ajenda hizo ni hotuba ya Rais wa TFF, taarifa ya utendaji ya mwaka 2011, bajeti ya mwaka 2012 na taarifa ya ukaguzi wa hesabu (audited accounts).

MECHI ZA VPL WIKIENDI HII, MAREKEBISHO
Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 24 wikiendi hii kwa mechi mbili zitakazochezwa Aprili 22 jijini Dar es Salaam. Villa Squad itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi wakati Yanga itakuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma katika Uwanja wa Taifa. Azam na Mtibwa Sugar zilizokuwa zicheze Aprili 21 mwaka huu sasa zitacheza Aprili 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati siku hiyo hiyo jioni kutakuwa na mechi kati ya Simba na Moro United. Mechi zote zitaanza saa 10.30 jioni. Aprili 25 mwaka huu Oljoro JKT itaikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. Raundi ya 25 itakamilika kwa mechi nne; Aprili 28 mwaka huu Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mtibwa Sugar ikiwa mgeni wa African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi. Azam na Toto African zitacheza Chamazi, Aprili 30 mwaka huu wakati Mei 1 mwaka huu Villa Squad itaumana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi. Ligi hiyo itafunga msimu wa 2011/2012, Mei 5 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa uwanjani. Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Polisi Dodoma (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Ruvu Shooting vs Villa Squad (Mabatini, Mlandizi), Coastal Union vs Toto African (Mkwakwani, Tanga), African Lyon vs JKT Ruvu (Manungu, Morogoro), Azam vs Kagera Sugar (Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro).

WASWAZI KUCHEZESHA SIMBA, AL AHLY SHANDY
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Swaziland kuchezesha mechi ya kwanza ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Al Ahly Shandy ya Sudan itakayochezwa Aprili 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Waamuzi hao wa mechi hiyo namba 71 ni Nhleko Simanga Pritchard atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake ni Mbingo Petros Mzikayifani na Sibandze Thulani. Mwamuzi wa mezani atakuwa Fakudze Mbongiseni Elliot. CAF pia imemteua Kayijuga Gaspard wa Rwanda kuwa Kamishna wa mechi hiyo.

KAMPUNI NNE ZAPITA TENDA YA TIKETI
Kampuni nne kati ya sita zimepita hatua ya kwanza ya mchakato wa kupata moja itakayofanya kazi ya kutengeneza tiketi za elektroniki kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na nyingine zinazosimamiwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Shughuli ya ufunguzi wa maombi ya hatua ya awali ya kuonesha nia (Expression of Interest) kwa ajili ya tenda hiyo ilifanywa jana (Aprili 19 mwaka huu) na Kamati ya Mipango na Fedha ya TFF ambayo ndiyo Bodi ya Tenda ya shirikisho. Kampuni ambazo zimepita hatua hiyo ya kwanza sasa zinatakiwa kuwasilisha rasmi tenda zao kwa ajili ya shughuli hiyo ndani ya kipindi cha wiki tatu tangu ulipofanyika ufunguzi wa hatua ya kwanza. Baadaye Bodi ya Tenda itakutana tena kupitia tenda zitakazokuwa zimewasilishwa na kufanya uteuzi wa kampuni moja itakayofanya kazi hiyo. Kampuni ambazo zimefanikiwa kuingia katika hatua hiyo ya pili ni CRDB Bank PLC, SKIDATA People Access Inc., Prime Time Promotions na Punchlines (T) Limited.

CHELSEA KATIKA KIBARUA KINGINE EMIRATES STADIUM.

BAADA ya ushindi walioupata dhidi ya Barcelona Jumatano, Chelsea wanatarajiwa kuwa na kibarua kingine kesho wakati wataposafiri kuifuata Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza utakaofanyika katika Uwanja wa Emirates. Arsenal ambao wanakamata nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo wameizidi Chelsea ambao wanashika nafasi ya sita kwa alama saba lakini wakiwa na mchezo mmoja zaidi, lakini kufungwa kwa timu hiyo na Wigan Athletic Jumatatu kumetoa nafasi kwa timu nne kuwa katika nafasi ya kugombania nafasi ya tatu na nne kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa. Arsenal itaingia uwanjani bila ya kiungo wake Mikel Arteta ambaye ana majeraha katika kifundo chake cha mguu aliyopata wakati wa mchezo dhidi ya wigan. Tottenham Hotspurs ambao wanashika nafasi ya nne baada ya kusuasua katika michezo yao ya hivi karibuni wao watasafiri kuifuata Queens Park Rangers. Mbio za ubingwa zitakuwa Jumapili ambapo Manchester United itakapopata nafasi ya kusogeza pengo la pointi wakati wakakapocheza na Everton majira ya mchana wakati mahasimu wao Manchester City wao watacheza na Woverhampton Wanderers jioni.

IYA MUST GO-ROGER MILLA

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Cameroon, Roger Milla amesema kuwa rais wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo Iya Mohammed anatakiwa kujiuzulu wadhfa huo. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Yaounde, Milla ambaye amewahi kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mwaka 1987 amesema kuwa Mohammed pamoja na viongozi wote wa shirikisho hilo ndio chanzo cha kiwango kibovu kilichoonyeshwa na timu ya taifa ya nchi hiyo katika siku za karibuni.
Cameroon ambao wameshawahi kunyakuwa taji la michuano ya Afrika mara nne walishindwa kufuzu michuano hiyo iliyochezwa mapema mwaka huu ambayo iliandaliwa na nchi majirani zao Gabon na Equatorial Guinea. Kutokana na matatizo hayo Milla na baadhi ya wachezaji wa zamani wan chi hiyo wamekaa kikao cha siri ilin kuangalia uwezekano wa kuuondoa uongozi wa Mohammed madarakani wakiamini ndio njia pekee ya kuihakikishia kikosi cha nchi hiyo kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani pamoja na michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014. Kundi hilo pia linadai kutenguliwa mara moja kwa adhabu aliyopewa nahodha wa kikosi cha timu ya nchi hiyo Samuel Eto’o na kusema kuwa wanahitaji wachezaji wake bora wote kwa ajili ya changamoto iliyopo mbele yao. Shirikisho la soka la nchi hiyo lilimfungia Eto’o miezi nane kutokana na kuongoza mgomo ambao ulipelekea kikosi cha nchi hiyo kukosa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Algeria Octoba mwaka 2011.

BECKHAM HASTAHILI KUITWA UINGEREZA-LINEKER

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Uingereza Gary Lineker amesema kuwa David Beckham hastahili nafasi katika kikosi cha Uingereza kitakachoshiriki michuano ya Olimpiki baadae mwaka huu. Kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Stuart Pearce anaweza kuchagua wachezaji watatu wenye umri mkubwa ili kuongeza nguvu katika kikosi chake cha vijana chini ya miaka 23. Akinukuliwa Lineker amesema kuwa kama unatakiwa kuchagua majina matatu ya wachezaji ambao wamevuka umri sidhani kama Beckham atakuwa mmojawapo. Mshambuliaji huyo wa zamani wan chi hiyo pia alitoa wito kwa Chama cha Soka cha nchi hiyo-FA kuteua kocha mapema atakayekinoa kikosi hicho kabla ya michauno ya Olimpiki. Beckham ambaye ni nahodha wa zamani wa Uingereza ni mmoja kati ya wachezaji 80 ambao wako katika kinyang’anyiro cha kugombania nafasi katika kikosi hicho na ameonyesha nia ya kukiongoza kikosi hicho katika michuano hiyo itakayofanyika jijini London.MAN UNITED YAONGOZA KWA UTAJIRI KATIKA VILABU BARANI ULAYA.

Top 20 clubs in the Forbes Football Valuation League1. Manchester United (£1.4bn)
2. Real Madrid (£1.17bn)
3. FC Barcelona (£814m)
4. Arsenal (£805m)
5. Bayern Munich (£769m)
6. AC Milan (£616m)
7. Chelsea (£474m)
8. Liverpool (£386m)
9. Juventus (£368m)
10. Schalke 04 (£365m)
11. Tottenham Hotspur (£352m)
12. Internazionale (£305m)
13. Manchester City (£276m)
14. Borussia Dortmund (£245m)
15. Olympique Lyonnais (240m)
16. Hamburger SV (£221m)
17. AS Roma (£220m)
18. Olympique de Marseille (£217m)
19. Valencia (£179m)
20. Napoli (£176m)

Real Madrid vs Valencia 2-0 Full Highlights and All Goals 18/04/2010

Thursday, April 19, 2012

TIMU YA TAIFA YA SUDANI KUWASILI LEO MCHANA

Timu ya Taifa ya Sudan (U20) inawasili leo saa 7.25 mchana (Aprili 19 mwaka huu) kwa ndege ya Ethiopian Airlines namba ET 805 ikiwa na msafara wa watu 30. Sudan inatarajia kufikia kwenye hoteli ya Rungwe iliyoko eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.
Timu hiyo inatarajia kufanya mazoezi leo saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Karume, na kesho itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa. Vilevile kesho saa 4 asubuhi kutakuwa na mkutano wa makocha wa Tanzania U20 na Sudan U20 na Waandishi wa Habari ofisi za TFF.