BARAZA la Wazee la klabu ya Yanga ya Dar es Salaam imeamua kuichukua timu ili kuiandaa na mechi dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC Mei 5, mwaka huu kufuatia mgogoro unaoendelea klabuni. Asubuhi ya leo, wazee wa Yanga wakiongozwa na Katibu wao Mkuu, Ibrahim Ally Akilimali walifika makuu ya klabu, makutano ya mita ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kufanya Mkutano na Waandishi wa Habari. Katika Mkutano huo, Mzee Akilimali alisema maamuzi hayo yana Baraka za Mwenyekiti wa klabu, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga. Kwa sasa Yanga ipo katika mgogoro, kufuatia Wajumbe wake wawili wa Kamati ya Mashindano na Usajili, Abdallah Ahmed Bin Kleb kujiuzulu kwa kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi. Machi mwaka jana, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha naye alijiuzulu kwa sababu za kutoelewana na Mwenyekiti wake, Nchunga. Yanga iliyopoteza matumaini hata ya kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, inaingia kwenye mechi dhidi ya watani wa wa jadi, Simba walio katika hali nzuri. Kwanza wana uhakika wa kuchukua ubingwa na pili wanaendelea vizuri kwenye michuano ya Afrika, kesho wakicheza mechi ya kwanza ya hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan.
No comments:
Post a Comment