Thursday, July 31, 2014

EVERTON YAMCHUKUA LUKAKU MOJA KWA MOJA.

HATIMAYE klabu ya Everton imefanikiwa kumchukua moja kwa moja mshambuliaji Romelu Lukaku kwa kitita cha paundi milioni 28. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mwenye miaka 21 aliyefunga mabao 16 akiwa Everton kwa mkopo msimu uliopita sasa ataitumikia timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitano. Meneja wa Everton Roberto Martinez amesema usajili huo sio muhimu tu kwa msimu huu lakini pia ni siku muhimu katika historia ya klabu hiyo. Lukaku alijiunga Chelsea akitokea Anderlecht kwa paundi milioni 18 mwezi August 2011 lakini aliichezea mechi 15 tu. Kocha wa Chelsea Jose Mourinho amedai kuwa ameamua kumuuza Lukaku kwasababu mchezaji huyo alikuwa haonyeshi moyo kwa kupambania nafasi yake katika kikosi cha chake.

MAKOCHA WA KIGENI WATAWALA ORODHA YA MAKOCHA WANAWANIA NAFASI KOREA KUSINI.

KAMATI ya Ufundi ya Chama cha Soka cha Korea Kusini, imedai kuwa imepunguza orodha ya ya makocha wanaowania nafasi ya kuonoa timu ya taifa ya nchi hiyo na kubakiwa na makocha watatu wa kigeni. Kiongozi wa kamati hiyo Lee Yong-Soo aliwaambia waandishi wa habari kuwa kama ilikuwa na kazi ya kuchambua majina 17 ya makocha wazawa na 30 ya makocha wa kigeni mpaka kutoka orodha hiyo ya wlaiobakia. Aliyekuwa kocha wa nchi hiyo Hong Myung-Bo alijiuzulu wadhifa wake huo baada ya kampeni mbovu za michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil ambazo zilipelekea nchi kumaliza mkiani katika kundi lao wakiambulia alama moja. Yong-Soo majina matatu ya mwisho yaliyotoka ni ya makocha wa kigeni huku kocha mmoja pekee wa mzalendo akifikia viwango lakini baada ya majadiliano waliamua kumuondoa kwa kipindi hiki. Makocha waliopenya katika orodha hiyo ni pamoja na Neil Lennon aliyewahi kuinoa Celtic, nyota wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi Frank Rijkaard na kocha wa zamani wa Tottenham Hotspurs na Fulham Martin Jol.

HOSSAM HASSAN KUCHUKUA NAFASI YA MIDO ZAMALEK.

KLABU kongwe ya Zamalek imetangaza kuwa imefikia makubaliano na kocha wa timu ya taifa ya Jordan Hossam Hassan kuingoza timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao. Zamalek ilimtimua Ahmed Hossam maarufu kama Mido juzi baada ya kupata sare ya bila kufungana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Congo, DRC. Maofisa wa klabu hiyo walitangaza kuwa na mazungumzo na Hossam Hassa ambaye alikubaliana na mambo yao na anatarajiwa kuingoza timu hiyo katika mchezo ujao dhidi ya AS Vita ya Congo, DRC itakayochezwa Agosti 10. Mkataba wa Hassan na timu ya taifa ya Jordan umemalizika toka Juni mwaka huu na pande zote hazijafikia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya. Hassan ambaye aliwahi kuichezea Zamalek kati ya mwaka 2000 na 2004, pia aliwahi kuwa kocha wa timu hiyo kuanzia mwaka 2009 mpaka 2011.

MECHI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA YASIMAMISHWA KWA SABABU YA VURUGU.

VURUGU baina ya mashabiki mahasimu zimesababisha kukosekana amani kwa dakika 15 katika mhcezo wa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kati ya Dnipro Dnipropetrovsk na FC Copenhagen uliochezwa katika Uwanja wa Olimpiysky jijini Kiev jana. Mashabiki wa FC Copenhagen wa Denmark walishambuliwa na kundi la watu wasiojulikana wanaoaminika kuwa mashabiki wa Dnipro na kulazimika kutafuta mahali pa kujificha katika majukwaa huku mwamuzi Andre Marriner akichelesha mchezo kuanza katika kipindi cha pili kwa dakika 15 zaidi. Tayari viongozi wa Fc Copenhagen wameshatuma barua ya malalamiko kwa Shirikisho la Soka barani Ulaya mara baada ya mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana. Hata hivyo mmoja wa wawakilishi wa mashabiki wa Dnipro ametuhumu mashabiki wa Denmark kwa kuamsha vurugu hizo kwa kupeperusha bendera ya urusi. Serikali ya Ukraine inapambana na waasi wanaotaka kujiunga na Urusi mashariki mwa nchi hiyo baada ya Crimea kufanya hivyo machi mwaka huu.

RAIS WA SHIRIKISHO LA ARGENTINA AAGA DUNIA.

RAIS mkongwe wa Chama cha Soka nchini Argentina-AFA na makamu wa rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Julio Grondona amefariki dunia jan akiwa na umri wa miaka 82 katika kliniki moja huko Buenos Aires. Kiongozi huyo mkongwe ambaye amekuwa rais wa AFA kuanzia mwaka 1979 alipelekwa hospitali akisumbuliwa na matatizo ya moyo na alifariki wakati akifanyiwa upasuaji wa dharura. Mapema wiki hii rais huyo alifanya mazungumzo na Alejandro Sabella ambaye aliamua kutoendelea kuwa kocha wa Argentina baada ya kuingoza timu hiyo kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Dunia iliyomalizika nchini hivi karibuni. Grondona amekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya FIFA toka mwaka 1988 akiongoza kamati ya fedha na alichaguliwa kuongoza AFA miaka tisa kabla na serikali ya kijeshi iliyokuwa madarakani. Amekuwa akichaguliwa kwa mafanikio kuendelea kuwa kiongozi wa AFA kila baada ya miaka minne toka mwaka 1979 huku akiungwa mkono vilabu zaidi ya 22,000 vya nchi hiyo. Akiwa madarakani kwa kipindi chote hicho Grondona amefanikiwa kuiwezesha nchi hiyo kushinda taji la Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico, Copa Amerika mwaka 1991 na 1993 na kupata medali ya dhahabu katika michuano ya olimpiki mwaka 2004 na 2005.

WAAMUZI WA LIGI KUU RUKSA KUTUMIA SPRAY.

LIGI Kuu nchini Uingereza imetangaza jana kuwa waamuzi watakaochezesha mechi za ligi hiyo watatumia dawa maalumu ya kupuliza kwa ajili ya kutambua eneo la mipira ya adhabu katika msimu wa mwaka 2014-2015. Katika taarifa yake iliyotumwa katika mtandao wa kijamii wa twitter ilithibitisha kufanyika kwa suala hilo kama ilivyokuwa ikifanyika katika michuano ya Kombe la Dunia iliyomalizika nchini Brazil. Dawa hiyo maalumu iliyo katika mfumo wa povu ambayo huyayuka ndani ya dakika moja, hupuliziwa katika uwanja na mwamuzi kutambua eneo ambalo mpira wa adhabu utapigwa na umbali ambapo wachezaji wanatakiwa kuweka ukuta kwa ajili ya kuzuia adhabu hiyo. Dawa hiyo ya kupuliza imeonekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika Kombe la Dunia mpaka kupelekea kukubalika na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA ambapo nao wataitumia katika mechi za Ligi ya Mabingwa na Europa League. Utaratibu huo pia aunatarajiwa kutumika katika msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Ufaransa.

NITAJIUZULU KAMA WAKINICHOKA - CAPELLO.

KOCHA wa timu ya taifa ya Urusi Fabio Capello amesema anaweza kujiuzulu kama waajiri wake na wachezaji wa kikosi chake watapoteza imani naye. Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza toka Urusi ishindwe kuvuka hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Dunia, kocha huyo wa zamani wa Uingereza amesema anategemea sana kuungwa mkono na kuaminiwa kwa kile anachokifanya. Kocha liendelea kudai kuwa huwa anafanya kazi kwa kuangalia na shauku kama akiona anaungwa na wote wanaomzunguka na kama akiona imani hiyo imetoweka atajiuzulu mwenyewe. Capello aliongeza mkataba wake wenye thamani ya euro milioni tisa kwa mwaka Januari mwaka huu ambapo utamalizika baada ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 itakayofanyika nchini humo. Naye rais wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo, Nikolav Tolstykh aliondoa shaka kwamba hakuna yeyote mwenye mpango wa kumtimua kocha huyo kwasasa ambapo hakuna mjumbe yeyote wa kamati ya utendaji anayetaka Capello aondoke.

GASGOW 2014: SIKU YA NANE MICHUANO YA MADOLA TANZANIA BADO BILABILA.

WAKATI michuano ya Jumuiya ya Madola inayoendelea jijini Glasgow, Scotland ikiingia siku yake ya nane leo, Tanzania imeendelea kuboronga kwa kushindwa kuambulia walau medali moja. Baada ya kuchemka katika michezo ya ngumi, meza, judo na kuogelea sasa itakuwa zamu ya wanariadha ambapo Dotto Ikangaa na Brazili John watakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha wanafuzu katika fainali yam bio za mita 1,500. Mpaka sasa Uingereza ndio wanaoongoza katika orodha ya medali kwa kujizolea 105, dhahabu 38, fedha 35 na shaba 32 wakifuatiwa na Australia waliojizolea medali 106, dhahabu 35, fedha 32 na shaba 39 huku Canada wao wakishika nafasi ya tatu kwa kuzoa medali 51 dhahabu 22 fedha saba na shaba 22. Kwa upande wa Afrika, Afrika Kusini ndio wanaoondoza kwa kuchukua medali nyingi ambapo mpaka wameshachukua medali 31, dhahabu tisa fedha 10 na shaba 12 wakifuatiwa na Nigeria waliozoa medali 19, dhahabu sita, fedha tano na shaba nane. Kenya ndio walioitoa kimasomaso Afrika Mashariki kwa kuzoa medali 12 mpaka sasa ambapo tano kati ya hizo ni dhahabu, tano zingine za fedha na mbili shaba huku Uganda wakifuatia kwa kuambulia medali moja ya shaba.

Wednesday, July 30, 2014

KEITA AENDELEZA BIFU LAKE NA PEPE.

BIFU la wachezaji Seudou Keita na Pepe limeibuka upya baada ya Keita anayecheza AS Roma kushindwa kushikana na mikono na Pepe kabla ya kuanza kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Real Madrid jijini Dallas. Keita alimpotezea Pepe kwa kumnyima mkono wake na badaae kutupa chupa iliyoonekana kumgonga beki huyo wa kimataifa begani. Wawili hao wamekuwa na bifu toka Keita akiwa anaitumikia Barcelona ambapo mshambuliaji huyo wakimataifa wa Mali alimtuhumu Pepe kwa kunfanyia vitendo vya ubaguzi wa rangi katika mchezo wa Super Cup nchini Hispania mwaka 2011. Pepe ambaye amehusika katika matukio kadhaa yenye utata, alionekana kutulia jana na hata kucheka wakati chupa hiyo ilipompiga begani. Katika mchezo huo Roma iliitandika Madrid bao 1-0.


MICHUANO YA YA KOMBE LA COSAFA YAFUTWA.

BARAZA la Michezo kwa nchi za Kusini mwaka Afrika-COSAFA limetangaza kuwa michuano ya Kombe la Cosafa ambayo ilikuwa ifanyike nchini Botswana kuanzia Septemba 13 hadi 28 mwaka huu imefutwa. Rais wa Cosafa Seketu Patel amesema kwasasa wako katika mchakato wa kutafuta mwenyeji mwingine kwa ajili ya kuandaa michuano hiyo. Patel amesema wamelazimika kufuta michuano hiyo kutokana na matatizo ya kifedha na miundo mingine ya kuwezesha michuano hiyo kuchezwa. Rais huyo amesema kwasasa wanasubiria maombi yao waliyotuma na kuahidiwa kupewa mwishoni mwa wiki hii kabla ya kutoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari.

TOURE ATHIBITISHA KUBAKIA MAN CITY.

KIUNGO wa klabu ya Manchester City, Yaya Toure amesema anataka kubakia klabuni hapo kwa kipindi kirefu kijacho. Kumekuwa na taarifa katika kipindi hiki cha kiangazi kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 31 alikuwa hana furaha Etihad huku wakala wake Dimitry Seluk akidai Toure anafikiri haheshimiwi na mabosi wa mabingwa hao wa Ligi Kuu. Lakini Toure ameuambia mtandao wa klabu hiyo kuwa hakuwa na nia ya kuondoka kwani amemua kubakia hapo kwa kipindi kirefu kadri atakavyoweza. Seluk alilalama kuwa siku ya kuzaliwa ya mteja wake ilidharauliwa na mabosi wake wakati kikosi cha timu hiyo kilipokwenda Abu Dhabi kwa ajili ya kushangilia taji lao la ligi Mei mwaka huu. Baadae Seluk aliiambia BBC kuwa mteja anataka kuhakikishiwa kibarua chake pamoja na kuudhiwa na jinsi alivyofanyiwa.

EL HILAL YAMTIMUA KOCHA BAADA YA KIPIGO.

KLABU ya El Hilal ya Sudan imetangaza kumtimua kocha wake Mbrazil Paulo Campos kufuatia tabia mbovu wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika mzunguko wa nne hatua ya makundi waliofungwa na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita. Katika mchezo huo wa ugenini waliocheza jijini Kinsasha, Al Hilal ilikuwa imepata sare ya bao 1-1 dhidi ya Vita lakini penati ilitolewa dakika za mwisho kwa wenyeji na kusababisha Campos kushindwa kuzuia jazba na kumvamia mwamuzi. Campos alikimbia kuingia uwanjani na kufuatiwa na wachezaji kumlalamikia mwamuzi kwa penati hiyo, tabia ambayo uongozi wa Hilal baadae waliikemea vikali katika taarifa yao. Baada kufanya kikao cha dharura bodi ya klabu hiyo iliamua kusitisha mkataba wa kocha huyo kwasababu ya tabia mbovu na kuonyesha mfano mbaya kwa wachezaji anaowaongoza. Katika mchezo huo Hilal ilitandikwa mabao 2-1 na sasa wanashika nafasi ya tatu katika kundi A linaloongozwa na TP Mazembe wakifuatiwa na AS Vita wote wakiwa wamefungana alama huku Zamalek wakiburuza mkia.

ZAMALEK YAMTIMUA MIDO.

KLABU kongwe ya Misri, Zamalek imemtimua kocha wake Ahmed Hossam maarufu kama Mido na wanatarajiwa kutangaza kocha mpya katika kipindi kifupi kijacho. Mido alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo Januari mwaka huu akichukua nafasi ya Helmy Tolan aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabovu. Mido aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa mjumbe wa bodi wa klabu hiyo Ahmed Soliman alimpigia simu na kumpatia taarifa hizo za kusitisha mkataba wake. Bodi ya klabu hiyo ilikutana jana na kufikia maamuzi ya kumtimua kocha na kuajiri mwingine atakayeingoza timu hiyo kwa ajili ya mechi zao zote za Ligi ya Mabingwa Afrika zilizobakia pamoja na msimu mpya wa Ligi Kuu.

VAN GAAL BADO AANATAKA BEKI MMOJA ZAIDI MAN UNITED.

MENEJA mpya wa klabu ya Manchester United, Louis van Gaal, amekiri kuwa bado anatafuta beki mmoja kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu. United tayari imeshawasajili Luke Shaw na Ander Herrera katika kipindi hiki cha kiangazi wakati Van Gaal naye akiwapa nafasi chipukizi Reece James, Michale Keane na Tyler Blackett katika ziara za maandalizi ya timu hiyo. Lakini suala la kuimarisha nafasi ya ulinzi limekuwa jambo muhimu kwa United baada ya kuondoka kwa mabeki wake wazoefu kama Nemanja Vidic, Rio Ferdinand na Patrice Evra katika kipindi hiki cha kiangazi. United wana uhakika wa kukamilisha usajili wa nahodha wa Arsenal Thomas Vermaelen lakini dili hilo limesimama kutokana na nia ya kocha Arsene Wenger kutaka kusajili mbadala wake kabla ya kuamua kumuuza. Akihojiwa Van Gaal amesema pamoja na kwamba mabeki alionao wameonyesha kucheza vyema lakini ni muhimu kuimarisha eneo hilo kwasababu ligi ni ndefu na kuna wakati wachezaji wanaweza kucheza chini ya kiwango kutokana na uchovu au majeruhi hivyo ni lazima kuwe na mbadala.

SABELLA AITEMA ARGENTINA.

VYOMBO vya habari nchini Argentina, vimeripoti kuwa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Alejandro Sabella ameamua kujiuzulu. Sabella mwenye umri wa miaka 59 ameisaidia nchi hiyo kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Dunia iliyomalizika nchini Brazil mapema mwezi huu. Taarifa zimesema kuwa Sabella alimuambia rais wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo Julio Grondona kuwa anaachia nafasi yake hiyo. Argentina inatarajiwa kuanza maandalizi yake ya michuano ya Copa America itakayofanyika nchini Chile kwa kucheza mechi za kirafiki dhidi ya mabingwa wa Kombe la Dunia Ujerumani huko Duesseldorf Septemba 3 mwaka huu.

SOUTHAMPTON INA CHIPUKIZI WENGI WALIO TAYARI KUCHEZA KIKOSI CHA KWANZA - CHAMBERS.

NYOTA wa zamani wa klabu ya Southampton, Calum Chambers amesema timu hiyo ina wachezaji wengi zaidi chipukizi waliopo tayari kucheza katika kikosi cha kwanza baada ya wachezaji kadhaa wenye majina kuondoka. Chambers mwenye umri wa miaka anayecheza nafasi ya beki wa kulia amekuwa mchezaji wa tano kuondoka Southampton katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi kwa ada ya paundi milioni 16 kwennda Arsenal. Lakini mchezaji huyo aliyepandishwa katika kikosi cha kwanza msimu uliopita anaamini kuwa wachezaji wengi chipukizi watapata nafasi ya kupandishwa msimu huu. Chambers amesema Southampton wana mfumo mzuri wa timu za vijana hivyo watazalisha wachezaji wengi zaidi. Wachezaji wengine wa Southampton walioondoka kiangazi hiki ni pamoja na Rickie Lambert, Adam Lallana na Dejan Lovren ambao wote wamekwenda Liverpool wakati Luke Shaw yeye amekwenda Manchester United.

Monday, July 28, 2014

BEKI3 INAWATAKIA WAISLAMU WOTE SIKUKUU NJEMA YA EID-UL-FITR.


PAMOJA NA KUKARIBIA KUMNASA CHAMBERS, WENGER AKIRI DILI HILO NI BAHATI NASIBU.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuwa klabu hiyo inakaribia kumsajili kinda la Southampton Calum Chambers ingawa amekiri dili hilo ni kama kubahatisha. Arsenal inatarajiwa kutangaza usajili huo wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 baada ya kufikia makubaliano ya kutoa kitita cha euro milioni 20 cha uhamisho kwenda Emirates. Wenger amesema Chambers anaweza kucheza katika nafasi kama beki wa kati, beki wa kulia na kiungo wa kati hivyo ni mategemeo yake ataleta changamoto katika nafasi hizo kwa wachezaji wenzake. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa pamoja na kuwa Chambers hajacheza mechi nyingi lakini wachezaji wengi wa Uingereza ni ghali hivyo ameamua kubahatisha kwasababu anaweza kuwa mchezaji muhimu siku zijazo. Kinda huyo ambaye ni zao la chipukizi wa wanaopikwa na Southampton anatarajiwa kufuata nyayo za kina Theo Walcott na Alex Oxlade-Chamberlain ambao wote wametokea huko kabla ya kwenda Arsenal.

SIJUTII UAMUZI WA KUJIUNGA NA MADRID - KAKA.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa zamani wa Brazil, Kaka amesisitiza kuwa hajutii uamuzi wake wa kujiunga na Real Madrid katika kipindi cha usajili wa kiangazi mwaka 2009 na anafikiri hakushindwa katika kipindi chote alichokuwepo Santiago Bernabeu. Nyota huyo alijiunga na Madrid akitokea AC Milan kwa ada ya paundi milioni 65 lakini hakuwahi kung’ara kama alivyotegemewa katika timu hiyo kongwe La Liga. Muda mrefu Kaka alikuwa akikaa benchi kama mchezaji wa akiba lakini bado anadai aliridhika katika muda aliokuwepo Madrid huku akiitetea rekodi yake. Kaka amesema hakushindwa wakati alipokuwa Madrid na kufafanua kuwa alicheza mechi 120 na kufunga mabao 28, hivyo kumfanya kucheza kucheza kwa wastani wa mechi 30 katika kila msimu. Nyota huyo ambaye kwasasa anacheza kwa mkopo katika timu ya Sao Paulo aliendelea kudai kuwa Jose Mourinho alimsaidia kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango chake na kumfanya kuwa na subira. Kaka aliondoka Milan katika kipindi hiki cha kiangazi baada ya kumaliza msimu mmoja toka arejee San Siro akitokea Madrid na sasa amesaini mkataba wa mwaka mmoja na timu ya Orlando City ya Marekani ambayo nayo imempeleka kwa mkopo Sao Paulo mpaka mwakani.

SINA HARAKA YA KUZIBA NAFASI YA SUAREZ - RODGERS.

MENEJA wa Liverpool, Brendan Rodgers amesisitiza hawatakuwa na haraka ya kununua mshambulliaji mpya kuziba nafasi ya Luis Suarez baada ya uhamisho wa Loic Remy kutoka Queens Park Rangers kwenda Anfiled kushindikana. Uhamisho huo wa euro milioni 10 ulikuwa kama umekamilika na Remy alisafiri kwenda nchini Marekani kufanyiwa vipimo vya afya lakini matatizo yaliyogundulika wakati wa vipimo yakasababisha Liverpool kuacha kumsajili. Rodgers sasa amebakiwa na Daniel Sturridge na Rickie Lambert kama washambuliaji pekee anaowategemea lakini kocha huyo amesema hata kuwa na haraka ya kutafuta mshambuliaji mwingine. Akihojiwa mara baada ya Liverpool kuichabanga Olympiakos kwa bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa huko Chicago, Rodgers amesema kuna baadhi ya maeneo anahitaji kuyaboresha katika kikosi chake lakini hajapata wachezaji anahitaji pamoja na kuwa na fedha ya kutosha. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kama itamaanisha kusubiri mpaka Januari ili aweze kupata mchezaji anayehitaji atasubiri lakini hawezi kufanya haraka ya kusajili kwasababu fedha zipo.

NYONGA YAMRUDISHA RAFAEL UINGEREZA.

BEKI wa klabu ya Manchester United, Rafael amerejea nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu kutokana na majeruhi ya nyonga. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil aliumia wakati wa mazoezi jijini Denver kuelekea katika mchezo wao walioshinda mabao 3-2 dhidi ya AS Roma. Rafael ambaye kuna uwezekano asicheze tena katika mechi za kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi, kurejea kwake nyumbani kunaweza kumpa nafasi ya kupona kwa wakati na kuelendelea na maandalizi mengine timu hiyo itakaporejea. United itafungua pazia la Ligi Kuu kwa kucheza na Swansea City katika Uwanja wa Old Trafford Agosti 16 mwaka huu.

RENARD BADO APEWA NAFASI YA KUINOA IVORY COAST.

KOCHA Mfaransa Herve Renard ametajwa katika orodha ya majina matatu ya mwisho katika kugombea nafasi ya kuinoa timu ya taifa ya Ivory Coast. Orodha hiyo ilitolewa na Shirikisho la Soka la nchi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo mshindi wa nafasi hiyo anatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwezi huu. Renard ambaye aliiongoza timu ya taifa ya Zambia maarufu kama Chipolopolo kushinda kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012 anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Mfaransa mwenzake Frederic Antonetti ambaye alikuwa akiifundisha Rennes na kocha wa zamani wa Sporting Lisbon na Benfica Jose Manuel De Jesus wa Ureno. Watatu hao wanatarajiwa kuhojiwa na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo kabla ya uamuzi wa mwisho. Shirikisho hilo limedai kuwa linataka kuteua kocha mpya kabla ya kuanza kwa michuano ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mapema Septemba.

LIGI YA MABINGWA AFRIKA: ZAMALEK YANG'ANG'ANIWA NA TP MAZEMBE.

KLABU ya Zamalek ya Misri imeshindwa kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani jijini Alexandria baada ya kung’ang’aniwa sare ya bila kufungana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC katika mchezo wa kundi A wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika. Sare hiyo imeiacha Zamalek ikiburuza mkia katika kundi hilo wakiwa na alama nne wakati Mazembe wao waliporomoka kwa nafasi mpaka nafasi ya pili kwa alama saba walizonazo wakifungana na Wacongo wenzao AS Vita ambao waliichapa Al Hilal ya Sudan kwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa mapema jana jijini Kinsasha. Katika mchezo huo timu zote mbili zilipata nafasi sawa za kuibuka na ushindi lakini walishindwa kuzitumia nafasi zao za kufunga walizopata hizo kuepelekea mchezo huo kumazika kwa sare. Zamalek watabakia nyumbani kwa mchezo wao pili mfululizo pale watakapowakaribisha vinara Vita Agosti 9 mwaka huu wakati Mazembe watawasubiri Al Hilal siku hiyohiyo.

SANCHEZ ATARAJIWA KUONEKANA KATIKA MSHINDANO MADOGO YA KOMBE LA EMIRATES.

MSHAMBULIAJI mpya aliyesajiliwa na Arsenal, Alexis Sanchez anatarajiwa kuripoti kambini tayari kwa mazoezi lakini kuna uwezekano akaikosa ziara ya siku nne ya mazoezi ya timu hiyo huko Austria. Sancehz aliyesajili kwa paundi milioni 30 ameanza maisha rasmi kama mchezaji wa Arsenal leo kufuatia uhamisho wake kutokea Barcelona lakini anatakiwa kuhakiki kibali chake cha kusafiria jijini Paris kabla ya kutua London. Arsenal walirejea kutoka katika ziara yao ya siku nne nchini Marekani jana ambapo walichapwa bao 1-0 na New York Red Bulls na wanatarajiwa kufanya mazoezi leo asubuhi kabla ya kusafiri kwenda Austria. Sanchez ambaye atabakia nchini Uingereza akifanya kazi na makocha wa viungo anaweza kucheza mechi yake ya kwanza katika michuano ya Kombe la Emirates dhidi ya Benfica Jumamosi hii. Wachezaji wenzake waliosajiliwa msimu huu beki wa kimataifa wa Ufaransa, Mathieu Debuchy, golikipa wa Colombia David Ospina na bekiwa Southampton Calum Chambers nao wanatajiwa kuripoti kambini wiki hii.

ETO'O APEWA OFA YA KUJIUNGA NA WEST HAM.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea, Samuel Eto’o amepewa ofa ya kujiunga na klabu ya West Ham United lakini nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 anahitaji kulipwa kitita cha paundi 100,000 kwa wiki. Meneja wa West Ham Sam Allardyce ambaye anataka mshambuliaji mbadala baada ya Andy Carroll kuumia pia ameonyesha nia ya kumtaka Joel Campbell ambaye anawindwa na AC Milan. Kwasasa Wst Ham imeanza mazungumzo na Hugo Almeida mwenye umri wa miaka 30 ambaye ni mchezaji huru lakini naye anataka mshahara wa paundi milioni 2.5 kwa mwaka. Kwa upande mwingine West Ham wamejiweka katika nafasi nzuri ya kumsajili kwa mkopo beki wa kati wa Arsenal Carl Jenkinson.

RASMI: LIVERPOOL YAKAMILISHA USAJILI WA LOVREN.

KLABU ya Liverpool, imefanikiwa kukamilisha usajili wa Dejan Lovren uliowagharimu kitita cha euro milioni 24 na kuwa mchezaji wa tatu wa timu hiyo kusajiliwa kutoka Southampton. Beki huyo wa kati alilalamika mapema Julai baada ya kubainisha Southampton walikataa ofa kama hiyo bila kumhusisha lakini sasa amethibitishwa kuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na Liverpool kiangazi hiki. Akihojiwa na mtandao wa Liverpool, Lovren amesema ndoto zake zimetimia kuitumikia klabu hiyo ambayo ina mamilioni ya mashabiki duniani kote. Lovren alibainisha kuwa baada ya kucheza katika Uwanja wa Anfield msimu uliopita alijipa matumaini kuwa siku moja lazima aichezee Liverpool na anashukuru ndoto zake zimetimia haraka. Lovren anaongeza orodha ya wachezaji walioihama Southampton msimu huu akiwemo Rickie Lambert na Adam Lallan ambao nao walijiunga na Liverpool, Luke Shaw aliyejiunga na Manchester United, Calum Chambers aliyejiunga na Arsenal huku Morgna Schneiderlin naye akiwa njiani kuondoka baada ya vilabu vya Tottenham Hotspurs na Arsenal kuonyesha nia ya kumtaka.

Sunday, July 27, 2014

YANGA YATEUA WAJUMBE WAPYA WA KAMATI YA UTENDAJI.

WAJUMBE WAPYA WA KAMATI YA UTENDAJI YA YANGA NI HAWA WAFUATAO:


1. Bw.Abubakar Rajabu - Mradi wa Jangwani City
2. Bw.Sam Mapande - Sheria na Utawala Bora
3. Bw.George Fumbuka - Uundwaji wa Shirika
4. Bw.Waziri Barnabas - Vibali vya Hatimiliki na Mahusiano
na Wafadhili
5. Bw.Abbas Tarimba - Mipango na Uratibu
6. Bw.Isaac Chanji na Bw.Seif Ahmed - Uendelezaji wa Mchezo
7. Bw.Musa Katabalo - Mauzo ya Bidhaa
8. Bw.Mohammed Bhinda - Ustawishaji wa Matawi
9. Bw.David Ndeketela Sekione - Uongezaji wa Wanachama
10. Bw.Mohammed Nyenge - Utangazaji wa Habari, Taarifa,
Matangazo n.k.


WAJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI ILIYOUNDWA UPYA WATASIMAMIA KIMSINGI KAMATI NDOGO ZIFUATAZO:


· Kamati ya Maadili - Bw.Sam Mapande
· Kamati ya Nidhamu - Bw.Sam Mapande
· Kamati ya Uchaguzi - Bw. Sam Mapande
· Kamati ya Uchumi na Fedha - Bw.George Fumbuka na Bw.Waziri
Barnabas
· Kamati ya Mashindano - Bw.Seif Ahmed &Bw.Isaac Chanji


· Kamati ya Soka la Vijana na
Wanawake - Bw.Seif Ahmed &Bw.Isaac Chanji
· Kamati ya Ufundi - Bw.Seif Ahmed&Bw.Isaac Chanji


5. Mwenyekiti na Makamo Mwenyekiti wa YANGA wanamategemeo makubwa kuwa waliotajwa hapo juu watahakikisha wana timiza malengo yaliyokusudiwa naYANGA ili“DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO” mpaka hapo itakapoamuliwa kubadilishwa au kutenguliwa vinginevyo.


6. Mwisho,tunawaomba ushirikiano wa dhati ili kuhakikishakuwa YANGA inapiga hatua mbele na inafanikiwa katika kufikia malengo na mipango yake ya maendeleo ya muda mfupi na ya muda mrefu kwa manufaa ya Klabu, Timu na wana YANGA popote walipo duniani.

“MUNGU AIBARIKI YANGA.”

SERENGETI BOYS KWENDA AFRIKA KUSINI KESHO.

KIKOSI cha wachezaji 19 cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys kinatarajiwa kuondoka kesho kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mechi dhidi ya Afrika Kusini. Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili itachezwa Jumamosi, Agosti 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa Dobsonville uliopo Soweto, Johannesburg kuanzia saa 9 kamili mchana kwa saa za Afrika Kusini. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam timu hizo zilitoka suluhu. Mshindi katika mchezo huo atacheza raundi ya mwisho ya michuano hiyo ya Afrika na mshindi wa mechi kati ya Misri na Congo Brazzaville. Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitafanyika mwakani nchini Niger.


FALCAO KUSHIRIKI MICHUANO YA KOMBE LA EMIRATES WIKI IJAYO.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Colombia na klabu ya Monaco, Radamel Falcao anatarajiwa kurejea uwanjani mwishoni mwa wiki ijayo katika michuano ya Kombe la Emirates inayoandaliwa na klabu ya Arsenal. Falcao mwenye umri wa miaka 28 alipata majeruhi ya goti katika mchezo wa Kombe la Ligi nchini Ufaransa, Januari 26 hivyo kulazimika kuikosa michuano ya Kombe la dunia iliyofanyika nchini Brazil. Meneja wa klabu ya Monaco Leonardo Jardim amesema nyota huyo kwasasa yuko katika hatua za mwisho ili aweze kupona kabisa hivyo anadhani atakuwepo katika michuano hiyo itakayofanyika jijini London. Pamoja na tetesi za nyota huyo kwenda klabu ya Real Madrid, Jardim amesema kwasasa anajua Falcao bado ni mchezaji wa Monaco na amemuweka katika mipango yake. Monaco, Valencia na Arsenal watachuana katika michuano ya Kombe la Emirates itakayofanyika jijini London Agosti 2 na 3.

BAYERN WAMUHAKIKISHIA KIBARUA GUARDIOLA.

OFISA mkuu wa klabu ya Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge amewahakikishia mashabiki kuwa Pep Guardiola hatatimuliwa na klabu hiyo. Januari mwaka 2007 Bayern walimtimua kocha wao Felix Magath wakati Louis van Gaal naye alitimuliwa April mwaka 2011 kutoka na kusuasua kwa timu hiyo vipindi hivyo. Lakini Rummenigge amewahakikishia mashabiki kuwa jambo kama halitaweza kutokea safari na Guardiola anatakiwa kuwa na uhakika wa kibarua chake. Rummenigge aliongeza kuwa Guardiola bado ataendelea kuwa kocha wa Bayern mpaka Juni 30 mwaka 2016 kama mkataba unavyoeleza.

CSKA MOSCOW WATWAA SUPER CUP URUSI.

MABINGWA wa soka nchini Urusi, CSKA Moscow wamefanikiwa kutoka nyuma na kufanikiwa kushinda taji lao la sita la Super Cup jana baada ya kuitandika Rostov kwa mabao 3-1 huko Krasnodar. Mchezo huo wa ngao ya hisani kwa ajili ya ufunguzi wa pazia la ligi za nchi hiyo ambao hukutanisha bingwa wa Ligi Kuu na bingwa wa Kombe la Taifa ulichezwa kwa mara ya pili katika mji wa Krasnodar baada ya mara ya mwisho mechi kama hiyo kuchezwa mwaka 2011. Rostov ndio waliokuwa wa kwanza kuona lango la wapinzani wao katika dakika ya 37 kupitia kwa beki wa kimataifa wa Croatia Hrvoje Milic kabla ya CSKA nao kuzinduka kurejesha bao hilo na kuongeza mengine mawili yaliyowapa ushindi. Ligi Kuu nchini Urusi inatarajiwa kuanza rasmi katikati ya mwezi ujao kama ilivyo ratiba nyingi za ligi za Ulaya.

OSPINA ATUA RASMI ARSENAL.

KOCHA wa klabu ya Nice, Claude Puel amedai kuwa Arsenal tayari imekamilisha usajili wa golikipa wa kimataifa wa Colombia David Ospina. Ospina mwenye umri wa miaka 25 amekuwa akiichezea klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ufaransa toka mwaka 2008 huku akiisaidia nchi yake kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia iliyomalizika nchini Brazil hivi karibuni. Kocha wa Arsenal Arsene Wenger naye alithibitisha kumsajili kipa huyo na kusifia kwamba ni usajili mzuri hususani kwa kiwango alichoonyesha golikipa huyo kwa kufanya vizuri katika Kombe la Dunia. Wenger amekuwa katika mawindo ya kutafuta golikipa mwingine atakayempa changamoto Wociech Szczesny katika kugombea nafasi katika kikosi cha kwanza baada ya kuondoka kwa Lukas Fabianski.

WILSHERE AJUTIA NA KUOMBA RADHI KWA KITENDO CHAKE CHA KUVUTA SIGARA.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Arsenal Jack Wilshere amekiri na kujutia kitendo chake cha kuvuta sigara katika picha aliyopigwa akiwa katika likizo ya Kombe la Dunia na kusisitiza kuwa atafanya jitihada kuhakikisha anarejea katika kiwango chake bora msimu huu unaokuja. Wilshere alizua utata wakati picha ikimuonyesha akivuta sigara katika bwawa la kuogolea jijini Las Vegas ilipovuja mapema mwezi huu, muda mfupi baada ya Uingereza kutolewa katika michuano ya Kombe la Dunia. Meneja Arsene Wenger amekuwa akiipinga vikali tabia hiyo kwa wachezaji wake na toka wakati huo amefanya nae mazungumzo na nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 amekiri hadharani kuwa alifanya tukio hilo na kwamba ni bahati mbaya. Akihojiwa Wilshere amesema anajutia kitendo chake hicho hususani kwa kukirudia kwa mara ya pili na kudai kuwa bado ana umri mdogo hivyo anajifunza kutokana na makosa anayofanya.

JAMES RODRIGUEZ NI HAZINA YA MADRID KWA SIKU ZIJAZO - ANCELOTTI.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema James Rodriguez ni hazina kwa ajili ya timu hiyo siku zijazo. Kauli ya Ancelotti imekuja kufuatia mchezo wa kirafiki dhidi ya Inter Milan uliofanyika jana ambapo timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na kupelekea timu hizo kwenda kwenye hatua ya changamoto ya mikwaju ya penati. Akihojiwa Ancelotti amesema Rodriguez anatarajiwa kuwasili rasmi Agosti mosi na kuongeza kuwa ni mchezaji muhimu na ana uwezo uwezo wa kucheza katika kikosi chake cha kwanza. Ancelotti pia akiri kuwa klabu hiyo kwasasa haina mpango wa kusajili tena mshambuliaji kwasasa tayari wanao wengi wakiwemo Rodriguez na Tony Kroos waliosajiliwa kiangazi hiki. Kocha huyo pia alithibitisha kuwa winga wake Angel Di Maria anakaribia kusajiliwa na klabu ya Paris Saint-Germain.

BOLT ATUA GLASGOW TAYARI KWA AJILI YA MASHINDANO YA JUMUIYA YA MADOLA.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi wa Jamaica, Usain Bolt amesema anatarajia kukimbia mbio za kufuzu za mita 400 kupokezana vijiti katika michuano ya Jumuiya ya Madola inayoendelea jijini Glasgow, Scotland. Bolt mshindi wa medali sita za dhahabu katika michuano ya olimpiki, hajashindana katika michuano yoyote kwa mwaka huu na hajawahi kushindana katika michuano ya Jumuiya ya Madola hapo kabla. Lakini mwaka huu Bolt aliowaondoa hofu mashabiki wake baada ya kutua Glasgow jana na kuthibitisha kukimbia mbio za kufuzu kabla ya kuanza safari ya kugombea medali katika mbio hizo za kupokezana vijiti. Mbio hizo za kufuzu zinatarajiwa kufanyika Ijumaa ijayo huko Hampden Park kabla ya fainali zenyewe ambazo ndio itakuwa tukio la mwisho katika michuano hiyo Agosti 2 mwaka huu.

MAN UNITED BADO WAMKOMALIA VERMAELEN.

KLABU ya Manchester United bado imeendelea kuwa na uhakika wa kukamilisha usajili wa Thomas Vermaelen katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi pamoja na Barcelona nao kuonyesha nia ya kumtaka beki huyo. United bado hawajafikia makubaliano ya ofa ya kumsajili beki huyo wa kati na Arsenal lakini inaaminika kuwa klabu bado ina nia ya kumsajili pamoja na dau lao la euro milioni kukataliwa. Vermaelen mwenyewe anataka kuondoka Arsenal kiangazi hiki lakini meneja Arsene Wenger anahitaji kusajili mbadala wake kabla ya kuamua kumuuza. United wanaoenekana hawako peke yao katika vita hiyo ya kumsajili Vermaelen kwasababu Barcelona nao bado wanahitaji kusajili beki mwingine baada ya kumnyakua Jeremy Mathieu kutoka Valencia.

Saturday, July 26, 2014

JUVENTUS BADO INAHITAJI KUSAJILI - ALLEGRI.

MENEJA mpya wa klabu ya Juventus, Massimiliano Allegri amethibitisha kuwa anataka kusajili mshambuliaji na beki kabla ya dirisha la usajili majira ya kiangazi halijafungwa. Mabingwa hao wa Italia walikamilisha uhamisho wa winga wa Udinese Roberto Pereyra jana kwa mkopo ikiwa ni siku chache baada ya kuwasajili beki wa kushoto wa Manchester United Patrice Evra na mshambuliaji wa Real Madrid Alvaro Morata. Usajili huo wa wachezaji hao watatu umekuja kufuatia kocha Antonio Conte kujiuzulu ghafla mwiki iliyopita na Allegri ambaye alichukua nafasi yake amebainisha mipango yake ya kuimarisha kikosi hicho kabla ya kuanza kwa msimu mpya. Akihojiwa Allegri amesema kama wakisajili beki mmoja na mshambuliaji kikosi chao kitakuwa katika hali nzuri tayari kwa ajili ya kutetea taji lao la ligi.

NILISHINDWA KUMSAJILI SHAW KWA SABABU YA MSHAHARA - MOURINHO.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho amedai alijitoa katika kinyang’anyiro cha kumsajili beki wa kushoto Luke Shaw katika kipindi hiki cha usajili wa kiangazi kwasababu mshahara aliohitaji ungeweza kuivuruga klabu hiyo. Shaw amekuwa beki wa nne ghali zaidi katika historia wakati Manchester United walipomsajili mapema mwezi huu kwa paundi milioni 27 akitokea Southampton. Mourinho amesema Shaw alikuwa akitaka mshahara wa paundi 100,000 kwa wiki ambao amedai ni mkubwa sana kwamchezaji mwenye umri wake wa miaka 19. Kocha huyo alidai kuwa kama wangefanya hivyo wangepunguza morari ya timu kwa kiasi kikubwa kwani kuna wachezaji wengi klabuni hapo ambao wamecheza mechi zaidi ya 200 na kushinda karibu kila kitu lakini hawajafikia kiwango hicho. Mourinho amesema kutokana na sababu hiyo pamoja na kuogopa kukiuka sheria ya matumizi ya fedha ndio mambo yalimfanya kujitoa katika kinyang’anyiro hicho.

VAN GAAL AWAKOMALIZA WACHEZAJI WAKE KUWASILIANA KWA KIINGEREZA WAWAPO UWANJANI.

KIUNGO aliyevunja rekodi ya usajili katika klabu ya Manchester United, Juan Mata amebainisha meneja mpya Louis van Gaal amewaambia wachezaji wake kuwa wanatakiwa kuwasiliana kwa lugha ya kiingereza. Mata tayari alikuwa ameungana na Ander Herrera wanaotoka nchi moja ambaye alijiunga nao akitokea Atletico Madrid mapema katika kipindi hiki usajili wa kiangazi, hata hivyo wakiwa uwanjani hawataruhusiwa kuzungumza lugha ya kwao Hispania. Hayo sio mabadiliko pekee aliyofanya Van Gaal toka ametua United mapema mwezi huu kwani kocha huyo aliyeingoza vyema Uholanzi kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Dunia pia amemua kutumia mabeki wake wa pembeni kama mawinga katika kampeni zake. Aina hiyo ya uchezaji ilimsadia kwa kiasi kikubwa katika michuano hiyo lakini bado haijajulikana kama itaweza kufanya kazi vyema katika Ligi Kuu. Mata aliongeza kuwa kwasasa wanajaribu kucheza katika mfumo huo mpya, hajui muda gani wanaweza kuuuzoea lakini wanafanya kila wanaloweza kuhakikisha wanauzoea na kuamini wanachokifanya.

AJALI YA NDEGE YA ALGERIA YAPELEKEA LIGI KUAHIRISHWA HUKO BURKINA FASO.

WIZARA ya michezo ya Burkina Faso imeahirisha ratiba ya Ligi Kuu nchini humo kufuatia ajali mbaya ya ndege ya Air Algeria iliyotokea Alhamisi iliyopita. Mechi ya 30 na ya mwisho ya ligi ilikuwa imepangwa kuchezwa Jumamosi hii lakini wachezaji na mashabiki walitaarifiwa kupumzika majumbani kwao. Kwa mujibu wa ratiba mpya iliyotolewa na Shirikisho la Spoka la nchi hiyo, timu zitalazimika kusimama kwa dakika moja ili kuwakumbuka watu waliokufa katika ajali hapo kesho. Taarifa zinadai kuwa abiria wote 116 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walifariki dunia katika ajali hiyo huku mamlaka za ndani zikidai 24 kati ya abiria hao walikuwa raia wa Burkina Faso.

LIVERPOOL YAZIDI KUIBOMOA SOUTHAMPTON.

BEKI mahiri wa klabu ya Southampton, Dejan Lovren anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya Liverpool mwishoni mwa wiki hii baada ya klabu hiyo kufikia makubaliano ya kumnunua kwa paundi milioni 20. Beki huyo wa kimataifa wa Croatia mwenye umri wa miaka 25 ambaye alicheza mechi zote za Kombe la dunia akiw ana nchi yake, amewahi kuzungumza waziwazi nia yake ya kujiunga na Liverpool. Lovren anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya katika Uwanja wa Anfield kabla ya Liverpool hawajarejea kutoka katika ziara yao nchini Marekani. Kocha wa Southampton Ronaldo Koeman alithibitisha kuwa Liverpool wanakaribia kumsajili Lovren na kazi yao kwasasa ni kuhakikisha wanapata mbadala wake haraka. Lovren aliyejiunga na Southampton akitokea Lyon kwa ada ya paundi milioni 8.5 katika kipindi cha kiangazi mwaka jana ataondoka Saint Mary akiwa ametumikia miezi 12 ya mkataba wake wa miaka minne aliokuwa nao.

LALLANA KUUKOSA MWANZO WA MSIMU.

KIUNGO mpya wa klabu ya Liverpool, Adam Lallana anatarajiwa kuukosa mwanzo wa msimu wa Ligi Kuu baada ya kuumia mguu wakati akiwa mazoezini. Lallana ambaye aliondoka Southampton mapema mwezi huu kwa ada ya paundi milioni 25 alipata majeruhi hayo wakati wa maandalizi ya msimu mpya huko nchini Marrekani. Kiungo huyo wa kimataifa wa Uingereza bado hajapangwa katika mechi yoyote ya kirafiki ya Liverpool na ingawa haitaji kufanyiwa upasuaji lakini hatarajiwi kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Southampton utakaochezwa Agosti 17 mwaka huu. Mbali na kukosa mchezo huo Lallana ambaye alikuwemo katika kikosi cha Uingereza kilichoshiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu, pia kuna uwezekano wa kuzikosa mechi dhidi ya Manchester City na Tottenham Hotspurs.

ARSENAL YANASA KINDA LA SOUTHAMPTON.

KLABU ya Arsenal imekubali dili la kumsajili nyota wa klabu ya Southampton Calum Chambers. Mchezaji huyo kinda mwenye umri wa miaka 19 ambaye anaweza kucheza kama beki wa kulia, beki wa kati na nafasi ya kiungo amekuwa akitajwa kama mmoja wa wachezaji bora wanaochipukia katika soka la Uingereza na Arsenal wanakaribia kumsajili kwa ada inayoweza kufikia euro milioni 20. Inaaminika kuwa Chambers tayari amehafanyiwa vipimo vya afya kuelekea kusaini dili hilo ambalo Southampton watalipwa kitita cha paundi milioni 13 kwasasa. Meneja wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers alikuwa akimtaka kumpeleka kinda huyo Anfield lakini Chambers mwenyewe ameamua kuchagua Arsenal ili aweze kuwa karibu na kocha Arsene Wenger. Chambers anakuwa mchezaji nne kuondoka Southampton katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi baada ya kuondoka kwa Adam Lallana na Rickie Lambert kwenda Liverpool na Luke Shaw kwenda Manchester United.

CESAR AITWA QPR.

KLABU ya Queens Park Rangers-QPR imemuita golikipa wake Julio Cesar aliyekuwa akicheza kwa mkopo katika timu ya Toronto FC ya Marekani. Golikipa huyo mwenye umri wa miaka 34 alihamia katika Ligi Kuu ya Marekani Februari mwaka huu baada ya kushindwa kupata muda wa kucheza chini ya kocha Harry Redknapp ambaye alikuwa akimpa nafasi Rob Green. Katika taarifa yake meneja mkuu wa Toronto waliwashukuru QPR kwa niaba ya klabu hiyo kwa kuwapa nafasi ya kumtumia Cesar huku pia wakimshukuru kipa huyo kwa mambo aliyowasaidia wakati akiwa hapo. Cesar alifanikiwa kucheza mechi zote za Kombe la Dunia nchini Brazil ambapo nchi yake waliokuwa wenyeji walipomaliza katika nafasi ya nne kufuatia kufungwa na Ujerumani katika nusu fainali na Uholanzi katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.

Friday, July 25, 2014

FIFA YAENDELEA KUIBEBA URUSI KUANDAA KOMBE LA DUNIA 2018.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA bado limeendelea na dhamira yake ya Urusi kuandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na kusema kuwa mgomo sio nia sahihi za kupunguza mvutano katika ukanda huo. Mgogoro uliopo kati ya waasi wanaotaka kujiunga na Urusi na serikali ya Ukraine uliangazwa duniani kote wiki iliyopita baada ya kuitungua ndege ya abiria ya Malaysia na kuuwa watu wote 298 waliokuwemo. Moscow wamekuwa wakikanusha kuwasaidia waasi hao lakini kufuatia maafa hayo wabunge waandamizi nchini Ujerumani wamependekeza Urusi kunyang’anywa haki ya kuandaa michuano hiyo. Katika taarifa ya FIFA iliyotumwa katika mtandao wake imedai kuwa bado inachukulia jukumu la kusimamia masuala ya soka kwa makini na wanaunga mkono midahalo yoyote ya amani na kidemokrasia. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa pamoja na kwamba FIFA haipendezwi na masuala yoyote ya vurugu au uvunjifu wa amani lakini wanajua hawawezi kila migogoro kuitafutia ufumbuzi hususani ile inayohusiana na masuala ya kisiasa. Hivyo FIFA bado itaendelea kuitambua Urusi kama mwenyeji wa michuano hiyo itakayofanyika katikam kipindi cha miaka minne ijayo.


RANIERI ATEULIWA KUWA KOCHA WA UGIRIKI.

CHAMA cha Soka cha Ugiriki-HFF kimethibitisha kumuajiri Claudio Ranieri kama kocha wao mpya wa timu ya taifa. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62 amesaini mkataba wa miaka miwili akichukua nafasi ya Fernando Santos aliyekiongoza kikosi cha timu hiyo katika michuano ya Kombe la Dunia mpaka hatua ya mtoano alipongolewa na Costa Rica kwa changamoto ya mikwaju ya penati. Ranieri ambaye aliiwezesha klabu ya Monaco ambayo ilikuwa imepanda daraja katika Ligi Kuu nchini Ufaransa kumaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita lakini amekuwa akishukutumiwa vikali hatua mabayo imepelekea kuangalia nafasi nyingine. Kibarua cha kwanza cha Ranieri akiifundisha Ugiriki itakuwa ni kuhakikisha wanaanza vyema mechi zao za kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016, ambapo Septemba 7 mwaka huu watakwaana na Romania. Ugiriki ambao walinyakuwa taji la michuano hiyo miaka 10 iliyopita pia watachuana na Hungary, Finland, Ireland Kaskazini na Visiwa vya Faroe katika kundi F walilopangwa.

MOURINHO AKIRI KUFIKIRIA KUMSAJILI DROGBA.

MENEJA wa klabu ya Chelsea Jose Mourinho amethibitisha kuwa anafikiria kumsajili tena Didier Drogba. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast aliichezea timu hiyo kwa kipindi cha miaka nane kabla ya kuondoka mwaka 2012 baada ya kuiwezesha Chelsea kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini sasa yuko huru baada ya kuamua kuondoka Galatasaray. Mourinho amesema, Drogba mwenye umri wa miaka 36 bado anaweza mikikimikiki ya Ligi Kuu pamoja na umri alionao ndio maana anafikiria kumrejesha tena Stamford Bridge. Mourinho aliendelea kudai kuwa hafikirii kumsajili kwasababu ya jina lake au kufunga mabao muhimu katika historia ya klabu hiyo au kwasababu anahitaji msaidizi bali ni uwezo wake ambao unaweza kuifanya timu kuwa imara.

OZIL, PODOLSKI, MARTESACKER KUKOSA MECHI YA UFUNGUZI WA LIGI YA ARSENAL.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amebainisha kuwa nyota wake walioshinda Kombe la Dunia wanaweza kukosa mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu nchini Uingereza dhidi ya Crystal Palace. Nyota hao ambao ni Mesut Ozil, Per Martesacker na Lukas Podolski wote wamepewa likizo baada ya kuisaidia Ujerumani kushinda taji la michuano hiyo iliyomalizika hivi karibuni nchini Brazil. Wachezaji hao wanatarajiwa kurejea mazoezini ya maandalizi ya msimu Agosti 11 ikiwa ni siku tano kabla ya mchezo huo dhidi ya Palace. Wenger amesema amewapa wachezaji hao likizo ndefu kidogo kwasababu ana uzoefu na wachezaji waliocheza fainali za Kombe la Dunia kwamba wanahitaji muda wa kupumzika. Kocha huyo aliongeza kuwa anajua wanaweza kujiandaa vizuri lakini kwa ajili ya mchezo wa kwanza utakaochezwa Agosti 16 hadhani kama watakuwa tayari.

VAN GAAL ANAFANANA NA FERGUSON - GIGGS.

KOCHA msaidizi wa klabu ya Manchester United, Ryan Giggs amesema kocha mpya wa timu hiyo Louis van Gaal kuna baadhi ya mambo yake anafanana na Sir Alex Ferguson. Mholanzi huyo alisimama kama kocha wa United kwa mara ya kwanza jana na kuchuhudia kikosi hicho kikiicharanga Los Angeles Galaxy kwa mabao 7-0 katika mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu mpya uliochezwa Marekani. Van Gaal anajulikana kwa kushinda mataji akiwa na vilabu vya Ajax Amsterdam, Bayern Munich na Barcelona katika kipindi chake cha ukocha na Giggs hashangazwi na mafanikio hayo. Akihojiwa Giggs amesema kuna baadhi ya vitu makocha hao wawili wanashabihiana akimaanisha Van Gaal na Ferguson huku akiongeza kuwa wote wanapenda wachezaji kujitoa na kuwa na heshima. Giggs aliendelea kudai kuwa Van Gaal anataka kila kitu kwenda sawa mwanzoni mwa mazoezi hadi mwisho kitu ambacho hata Ferguson alikuwa nacho.

GYAN AJITIA KITANZI AL AIN.

NAHODHA wa timu ya taifa ya Ghana, Asamoah Gyan ameongeza mkataba wake na klabu ya Al Ain ya Falme za Kiarabu ambao unamalizika mwaka 2018. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Sunderland alikuwa amebakisha mkataba wa miaka mwili na nusu lakini aliongezwa mkataba mwingine ulioboreshwa zaidi jana. Gyan mwenye umri wa miaka 28 amekuwa mfungaji anayeongoza katika Ligi Kuu ya huko kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo. Nyota huyo ambaye alijunga na Al Ain akitokea Sunderland kwa mkopo mwaka 2011, amefunga mabao 82 katika mechi 66 za ligi alizocheza.