Saturday, June 30, 2012

TAARIFA KUTOKA TFF.

YANGA KUANZIA KWA ATLETICO KOMBE LA KAGAME
Mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) wataanza kutetea ubingwa wao Julai 14 mwaka huu dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye ametangaza ratiba ya michuano hiyo leo (Juni 29 mwaka huu) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Timu 11 zitashiriki katika michuano hiyo itakayoanza Julai 14 hadi 28 mwaka huu ambapo kwa siku zitachezwa mechi mbili (saa 8 mchana na saa 10 jioni) huku Tanzania Bara ikiwakilishwa na Yanga, Simba na Azam. Mechi ya kwanza siku ya ufunguzi (saa 8 mchana) itakuwa kati ya APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan Kusini. Kundi A lina timu za Simba, URA ya Uganda, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Ports ya Djibouti. Azam, Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya ziko kundi B. Yanga inaunda kundi C lenye timu za APR ya Rwanda, Wau Salaam ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi. Timu nane zitaingia robo fainali itakayochezwa Julai 23 na 24 mwaka huu. Kundi A na C kila moja litatoa timu tatu kwenda robo fainali wakati B litatoa timu mbili. El Merreikh ya Sudan, Red Sea ya Eritrea, Coffee ya Ethiopia na Elman ya Somalia hazitashiriki katika mashindano ya mwaka huu ambayo yanafanyika Tanzania Bara kwa mwaka wa tatu mfululizo kutokana na sababu mbalimbali. Coffee haitashiriki kwa vile ligi ya Ethiopia inaanza Julai 14 mwaka huu wakati El Merreikh wikiend ya Julai 13-15 mwaka huu itakuwa na mechi ya michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Bingwa wa michuano hiyo atapata dola 30,000, makamu bingwa dola 20,000 na mshindi wa tatu dola 10,000. Michuano hiyo itaoneshwa moja kwa moja (live) na Televisheni ya SuperSport.

DOS SANTOS KUTIMKIA ATLETICO MADRID.

KIUNGO wa kimataifa wa Mexico na klabu ya Tottenham Hotspurs Giovani dos Santos anatarajiwa kuikacha klabu yake hiyo baada ya kuruhusiwa kuondoka katika kambi ya kikosi cha nchi hiyo kinachojiandaa na michuano ya olimpiki ili aweze kushughulikia uhamisho wake wake. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23 ana thamani ya paundi milioni nane ana anatarajiwa kujiunga na klabu ya Atletico Madrid ya nchini Hispania mwishoni mwa wiki hii baada ya kutua London. Nayo klabu ya Paris Saint-Germain imeendelea na mbio zake za kumuwania mshambuliaji wa Manchester City Carlos Tevez mwenye umri wa miaka 28. Mbali na Tevez pia klabu hiyo ambayo imeonyesha nia ya kumwaga fedha nyingi katika kipindi hiki cha usajili pia inamuwania beki wa kimataifa wa Brazil na klabu ya AC Milan, Thiago Silva ambaye ana umri wa miaka 27. Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo tajiri ametamba kuwa pesa usajili sio tatizo kwa klabu hiyo ila jambo linawapa tatizo ni kuwashawishi wachezaji hao ili waweze kujiunga na klabu hiyo.

PRANDELLI AANZA KUSHEHEREKEA UBINGWA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Italia Cesare Prandelli ameonekana akijipongeza na maofisa wa soka wa nchi hiyo baada ya kuitoa Ujerumani katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Ulaya na kufanikiwa kutinga fainali ambapo watakutana na Hispania kesho jijini Kiev, Ukraine. Katika tafrija hiyo ndogo Prandelli amesema kuwa anafurahia changamoto ya kumfundisha mshambuliaji mtukutu wa timu hiyo na klabu ya Manchester City Mario Balotelli na wamekuwa wakielewana vizuri katika michuano hiyo mpaka sasa. Mwanzoni kabla ya kuanza kwa michuano hiyo kulikuwa na tetesi kuwa Prandelli angemuacha Balotelli kutoka na tabia za utovu wa nidhamu ndani na nje ya uwanja ambapo baada ya kumwita katika kikosi chake wadau walikuwa wakiuliza kama kocha huyo ataweza kummudu mchezaji huyo mtukutu. Prandelli alitamba kuwa mbali na kumfundisha Balotelli pia amewahi kuwafundisha wachezaji kama Adriano, Antonio Cassano na Adrian Mutu ambao ni watukutu lakini mwisho wa siku ndio wamekuwa wachezaji ambao huibuka kuwa nyota ya mchezo tofauti na watu wanavyowategemea.

VILLAS-BOAS KUPOTEZA KIASI CHA PAUNDI MILIONI 11 KAMA AKITUA WHITEHART LANE.

ALIYEKUWA kocha wa Chelsea Andre Villas-Boas anatarajiwa kupoteza kiasi cha paundi milioni 11 kama atatangazwa kama meneja mpya wa kikosi cha Tottenham Hotspurs wiki ijayo. Kocha huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 34 hajapatiwa malipo yake wakati alipofukuzwa na Chelsea Machi mwaka huu akiwa ametumikia miezi nane katika miaka mitatu ya mkataba huo. Badala ya kulipwa moja kwa moja fedha hizo Chelsea walikubali kumlipa kocha huyo kiasi cha paundi 100,000 kwa wiki mpaka hapo atakapopata kibarua kingine ambapo alikuwa amepokea mshahara wa miezi mitatu tu. Lakini kama kocha huyo akiamua kukubali kuinoa klabu ya Tottenham, tajiri wa Chelsea Roman Abramovic atasitisha malipo ya kocha huyo ambayo amekuwa akipata hivyo kupoteza kiasi cha paundi milioni 11 katika miezi 25 iliyobakia.

ARMSTRONG AFUNGULIWA MASHITAKA YA KUTUMIA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU.

Lance Armstrong.
BINGWA mara saba wa michuano ya baiskeli ya Tour de France, Lance Armstrong amefungiliwa mashtaka ya kutumia dawa za kuongeza nguvu na wakala wa kupinga dawa hizo nchini marekani. Kesi hiyo sasa itasikilizwa na jopo la kamati ya upatanishi ambalo litaamua matokeo ya kusikilizwa kwa kesi hiyo. Armstrong ambaye alishinda michuano hiyo mara saba mfululizo kuanzia mwaka 1999 mpaka 2005 anaweza kunyang’anywa mataji yake hayo na kufungiwa kushiriki mbio za baiskeli kama akikutwa na hatia ya kutumia dawa hizo. Hatahivyo Armstrong ambaye ana umri wa miaka 40 alikana tuhuma hizo na kudai kuwa hakuwahi kushindwa katika vipimo vya dawa za kuongeza nguvu katika kipindi chote ambacho amekuwa akishiriki mbio hizo.
Armstrong ambaye alifanikiwa kupona kansa ya korodani na kufanikiwa kuweka rekodi ya michuano hiyo ya Ufaransa alistaafu mbio hizo mwaka 2005 lakini alirejea tena mwaka 2009 kabla ya kustaafu kwa mara ya pili Februari mwaka 2011.

BOLT ACHEMSHA MBELE YA BLAKE.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi wa Jamaica Usain Bolt ameshindwa kutamba katika fainali ya mbio za taifa za nchi hiyo baada ya kushika nafasi ya pili akitumia muda wa sekunde 9.86. Nafasi ya kwanza katika mbio hizo ilishikiliwa na Yohane Blake ambaye alitumia muda wa sekunde 9.75 na kuipiku rekodi ya Bolt aliyoweka mwaka huu ya sekunde 9.76 katika mashindano yaliyofanyika jijini Rome, Italia mwezi uliopita. Katika mbio hizo Bolt alianza taratibu mwisho lakini alijitutumua karibu mwishoni wa mbio hizo na kujikuta akimaliza mbele ya Asafa Powell ambaye alishika nafasi ya tatu akitumia muda wa sekunde 9.88. Akihojiwa mara baada yam bio hizo Bolt alikiri kuwa alipata tatizo katika kuanza lakini alipuuzia na kujipa moyo kwamba hatakiwi kukata tamaa ndio maana akafanikiwa kukamata nafasi ya pili imemuwezesha kufuzu michuano ya Olimpiki itakayofanyika jijini London mwaka huu. Hii ni mara ya kwanza Bolt kushindwa mbio za nchini kwake toka mwaka 2004 alipojiunga rasmi na mbio za kulipwa ambapo pia ni bingwa mtetezi wa mbio za mita 200 katika michuano olimpiki.

Friday, June 29, 2012

VALCKE ARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA WORLD CUP NCHINI BRAZIL.

Jerome Valcke.

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amesema kuwa Brazil inaendelea vizuri na maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 baada ya kufaya ziara ya siku tatu nchini humo kukagua maendeleo ya maandalizi hayo. Valcke alitembelea miji ya Racife, Natal na Brasilia mbayo itakuwa wenyeji wa michuano pamoja na kuzungumza na wajumbe wa kamati ya maandalizi ambao walimpa taarifa ya hatua walizofikia katika maandalizi ya Kombe la Dunia na Kombe la shirikisho ambalo litachezwa mwaka kesho. Valcke amesema kuwa miradi mingi inaenda vizuri kila mtu anafanya kazi kwa bidii kuhakikisha wanaandaa michuano iliyo bora. FIFA pia ilitangaza kuwa ratiba ya Kombe la Dunia itapangwa katika mji wa Costa do Sauipe ambao uko Kaskazini-Mashariki mwa nchi hiyo Desemba mwaka 2013 wakati ratiba ya michuano ya Confederation itapangwa Desemba mwaka huu jijini Sao Paulo.

ITALIA YAKATA TIKETI CONFEDERATION CUP BAADA YA KUIADHIRI UJERUMANI.


 

TIMU ya taifa ya Italia imekata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho litakalofanyika mwakani nchini Brazil baada ya kufanikiwa kuingia fainali ya michuano ya Ulaya kwa kuifunga Ujerumani mabao 2-1 jijini Warsaw, Poland. Hispania pia wamefuzu hatua ya fainali ambayo itachezwa Jumapili jijini Kiev, Ukraine lakini wenyewe walikuwa wamefuzu moja kwa moja michuano ya shirikisho kwakuwa wenyewe ndio mabingwa wa dunia kwa sasa hivyo Italia ndio watakaowakilisha Ulaya kwenye michuano hiyo. Katika michuano hiyo Spanish na Italia zitawakilishwa bara la Ulaya wakati Japan ikiwakilisha bara la Asia kwakuwa ndio mabingwa wa bara hilo huku Mexico na Uruguay zikiwakilisha bara la Amerika Kusini na CONCACAF na Brazil wenyewe watakuwepo kama wenyeji wa michuano hiyo. Nchi ya Tahiti nayo imefuzu baada ya kuwa mabingwa wa Oceania wakati mwakilishi wa Afrika atapatikana katika michuano ya Mataifa ya Afrika yatakayofanyika mapema mwakani. Michuano ya Kombe la Shirikisho inatarajiwa kuanza kutimua vumbi June 15 mpaka 30 mwakani ambapo michezo ya ufunguzi itafanyika jijini Brasilia nusu fainali itachezwa katika miji ya Belo Horizonte na Fortaleza wakati fainali itapigwa katika jiji la Rio de Janeiro.

NADAL NJE WEMBLEDON.

Lukas Rosol

BINGWA mara mbili wa michuano ya Wimbledon Rafael Nadal ameondolewa katika michuano hiyo inayoendelea jijini London baada ya kukubali kipigo cha seti tano kutoka kwa Lukas Rosol ambaye yuko katika nafasi ya 100 katika orodha za ubora wa mchezo huo duniani. Katika mchezo huo Nadal ambaye anashika namba mbili katika orodha hizo alishindwa kutamba kwa Rosol mwenye umri wa miaka 26 raia wa Jamhuri ya Czech kwa 6-7 6-4 6-4 2-6 6-4 katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo. Hii ni mara ya kwanza kwa Nadal kutolewa katika mzunguko wa pili wa michuano mikubwa toka alipofungwa na Gilles Mueller katika mzunguko wa pili wa michuano ya Wimbledon mwaka 2005. Matokeo hayo yamemsafishia njia Andy Murray wa Uingereza ambaye ilikuwa akutane na Nadal ambaye ni raia wa Hispania katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.