Monday, February 29, 2016

TETESI ZA USAJILI ZILIZOJIRI HUKO MAJUU.

KLABU ya Real Madrid inadaiwa kuwahi kufikiria kumuwania kocha Mauricio Pochettino majira ya kiangazi lakini ilirudhishwa nyuma kwa sababu mbili kubwa ambazo ni uwezo wake kwa nyota atakaokuwa nao pamoja na rais wa Madrid kutotaka kufanya biashara tena na Daniel Levy.
Chanzo: El Pais

KLABU ya Real Madrid ilijaribu kumrejesha Jose Mourinho Santiago bernabeu baada ya Rafa Benitez kutimuliwa lakini wanadhani hatua yao hiyo ilitumiwa na kocha huyo pamoja na wakala wake Jorge Mendes kusaini mkataba wa awali wa makubaliano na Manchester United.
Chanzo: El Pais

KLABU ya Arsenal iko tayari kuingia katika vita vya kumuwania winga wa Leicester City Riyad Mahrez huku Manchester United, Chelsea, Barcelona na Real Madrid nazo zikihusishwa na tetesi za kumtaka nyota huyo wa kimataifa wa Algeria.
Chanzo: ESPN

KLABU ya Inter inajipanga kumpa ofa ya mkataba wa miaka mitano meneja wa Atletico Madrid Diego Simeone wenye thamani ya euro milioni 100, ili aweze kuwarejesha katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Chanzo: Fichajes.net

MENEJA wa AS Roma, Luciano Spalletti yuko tayari kumruhusu kiungo Daniele De Rossi kuondoka katika klabu hiyo msimu huu huku Los Angeles Galaxy wakiwa tayari kumpatia mkataba.
Chanzo: transfermarketweb.com

KLABU ya Deportivo La Coruna wamepanga kumrejesha La Liga kiungo wa Aston Villa Carlos Sanchez, majira ya kiangazi.
Chanzo: Gol Digital

EL-CLASICO KUCHEZWA APRILI 2.

TAREHE rasmi ya mchezo wa marudiano ya Clasico ambayo huwakutanisha mahasimu wa Ligi Kuu ya Hispania Barcelona na Real Madrid imetangazwa. Timu hizo mbili zinatarajiwa kukwaana na Aprili 2 mwaka huu katika Uwanja wa Camp Nou ambapo Madrid watakwenda huko kujaribu kulipiza kisasi cha kutandikwa mabao 4-0 Novemba mwaka jana. Katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, Barcelona ilipata mabao yake kupitia kwa nyota wake Luis Suarez aliyefunga mawili na moja kwa Neymar na Andres Iniesta huku Isco akionyeshwa kadi nyekundu dakika za majeruhi. Toka wakati huo Madrid waliamua kumtimua Rafa Benitez na nafasi yake kuchukuliwa na Zinedine Zidane lakini bado wamekuwa wakisuasua na kujikuta wakiachwa mbali na Barcelona katika msimamo wa La Liga.

WENGER AWATAKA WACHEZAJI WAKE KUSAHAU KIPIGO CHA UNITED NA KUZINGATIA MCHEZO WAO UJAO DHIDI YA SWANSEA.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amekitaka kikosi chake kusahau kipigo walichopata kutoka Manchester United na kujaribu kurejesha nguvu zao katika mbio za ubingwa katika mchezo dhidi ya Swansea City Jumatano hii. Pamoja na kipigo cha jana cha mabao 3-2 walichoapata Old Trafford, Arsenal wameendelea kushikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa alama tano nyuma ya vinara Leicester City. Akihojiwa kuelekea katika mchezo huo wa kesho kutwa Wenger amesema hawapaswi kujionea huruma kwani pamoja na kupoteza alama tatu muhimu lakini waliwaonyesha kuwa wanaweza kupambana. Kocha huyo ameendelea kudai kuwa wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo yao ijayo.

RASHFORD APANIA KUENDELEZA MOTO ALIOANZA NAO.

MSHAMBULIAJI chipukizi wa Manchester United, Marcus Rashford anataka kuendelea moto wake alioanza nao katka kikosi cha kwanza cha United baada ya kuifungia timu yake mabao mawili muhimu katika mchezo dhidi ya Arsenal jana. Rashford mwenye umri wa miaka 18, alifunga mabao mawili wakati alipocheza kwa mara kwanza katika kikosi cha wakubwa kwenye ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Midtjylland ya Denmark katika mchezo wa Europa League Alhamisi iliyopita. Chipukizi huyo amerudia tena kufunga idadi hiyo ya mabao wakati alitambulishwa kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu na kuiwezesha United kuibuka ushindi muhimu wa mabao 3-1 dhidi ya Arsenal. Rashford amesema kujumuishwa kwake katika kikosi dakika za mwisho Alhamisi iliyopita baada ya Anthony Martial kuumia pengine ndio kulikomsaidia kufanya vyema. Nyota huyo amesema ni jambo zuri kuanza Ligi Kuu kwa kufunga na ana matumaini ya kuendelea kufanya hivyo ili kuisaidia timu yake.

CABALLERO ADAI PENATI ZA CITY ALIZOOKOA NI ZAWADI KWA PELLEGRINI KWA KUMUAMINI.

KIPA Manchester City, Willy Caballero amesema amemlipa meneja wake Manuel Pellegrini kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kucheza katika fainali ya Kombe la Ligi iliyofanyika Wembley jana. Kipa huyo wa kimataifa wa Argentina aliokoa penati tatu za Liverpool na kuwafanya City kushinda kwa changamoto ya penati 3-1, baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida. Caballero mwenye umri wa miaka 34, alikuwa akipondwa vikali baada ya kichapo cha mabao 5-1 walichopata katika mzunguko wa tano wa Kombe la FA kutoka kwa Chelsea wiki moja iliyopita. Akihojiwa Caballero ambaye alichukua nafasi ya kipa namba moja wa City, Joe Hart amesema alistahili kucheza katika fainali hiyo. Caballero ameanza katika mechi nne pekee za Ligi Kuu toka ajiunge na City akitokea Malaga Julai mwaka 2014.

POCHETTINO APUUZA HABARI ZA UBINGWA.

MENEJA wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino amesema wachezaji wake hawazungumzii suala la kushinda taji la Ligi Kuu msimu huu. Spurs wanashika nafasi ya pili katika msimamo wakiwa alama mbili nyuma ya vinara Leicester City baada ya kutoka nyuma na kuitandika Swansea kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa White Hart Lane jana. Akihojiwa Pochettino amesema hakuna yeyote anayezungumzia ubingwa kwasasa katika vyumba vyao vya kubadilishia nguo. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa wanachoamini wao ni kushinda katika kila mchezo na kuona kitu gani kitatokea mwishoni mwa msimu. Wakiwa wamebaki ya mechi 11, Spurs wako alama tatu juu ya mahasimu wao Arsenal ambapo walifungwa na Manchester United jana. Hata hivyo Pochettino amesema kwa upande wake Arsenal kupoteza mchezo sio muhimu, na jambo muhimu kwake ni kuhakikisha wanacheza kwa kiwango chao bora kwani bado wana mechi nyingi zilizobaki.

VAN GAAL RADHI KWA KUJIANGUSHA MBELE YA KAMISAA.

MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal ameomba radhi kwa kujiangusha mbele ya kamisaa wa mchezo wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ambao waliitandika Arsenal kwa mabao 3-2 jana. Meneja huyo raia wa Uholanzi alijiangusha mbele ya kamisaa huyo ili kujaribu kumwelewesha na kutoridhishwa kwake na maamuzi ya mwamuzi Mike Dean aliyechezesha pambano hilo. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Van Gaal amesema tukio alilofanya kalikuwa sahihi hivyo anaomba radhi kitendo hicho. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa alikuwa na hisia kubwa kwasababu ya aina ya mchezo wenyewe lakini anashukuru walipata matokeo waliyohitaji.

MESSI AFIKISHA MABAO 30 KWA MSIMU WA NANE MFULULIZO.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona Lionel Messi jana amefanikiwa kufikisha mabao 30 kwa msimu wa nane mfululizo wakati akiwasaidia mabingwa hao wa La Liga kutoka nyuma ya kuitandika Sevilla kwa mabao 2-1. Sevilla wanaoshika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi ndio timu ya mwisho kuifunga Barcelona Octoba mwaka jana. Messi aliisawazishia Barcelona kwa bao la mipira wa adhabu baada ya Vitolo kuifungia Sevilla bao la kuongoza huku Gerard Pique akipigilia msumari wa mwisho. Barcelona ambao hawajafungwa katika mechi 34 zilizopita sasa wanaongoza ligi kwa tofauti ya alama nane huku wakiwazidi mahasimu wao Real Madrid kwa alama 12.

Sunday, February 28, 2016

TETESI ZA USAJILI ZILIZOJIRI HUKO MAJUU.

KLABU ya West Ham United imemjumuisha Andre Ayew wa Swansea City katika orodha ya wachezaji wanaowahitaji majira ya kiangazi wakati wakijaribu kuimarisha safu ya ushambuliaji msimu ujao.
Chanzo: Daily Star

KLABU ya Real Madrid inadaiwa kumuwania mshambuliaji wa Sevilla Kevin Gameiro ambapo mahasimu wao wa La Liga wanatajwa kuwa hawatopokea chini ya euro milioni 40 kwa ajili ya nyota huyo.
Chnazo: Fichajes.net

SHIRIKISHO la Soka la Italia linamtaka meneja wa Leicester City Claudio Ranieri kuchukua nafasi ya Antonio Conte ambaye anatarajiwa kwenda Chelsea msimu ujao, baada ya kumalizika kwa michuano ya Euro 2016.
Chanzo: Fichajes.net

KLABU ya Manchester United inadaiwa kumfuatilia kwa karibu Andrew Robertson wa Hull City wakati huu wakiwa katika mawindo ya kutafuta beki wa kushoto. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 21 pia kiwnago chake kimewavutia Manchester City, Arsenal na Tottenham Hotspurs.
Chanzo: Daily Star

KLABU ya Chelsea inadaiwa kufikiria kumuwania beki wa Crystal Palace Scott Dann lakini wanaweza kulazimika kutoa kitita cha paundi milioni 20. Chelsea wamefikia hatua hiyo baada ya kuhofu John Stones anaweza kunyakuliwa na Manchestyer City.
Chanzo: Mail on Sunday

KLABU ya Arsenal inaendelea kumfuatilia kwa karibu kiungo wa Ajax Amsterdam Riechedly Bozoer. Maskauti wa Arsenal wanadaiwa kuwepo kwa karibu kila mchezo ambao chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19 amekuwa akicheza.
Chanzo: The People


CECH ADAIWA MIPANGO MIKAKATI YA WENGER NDIO ILIYOMVUTIA KWENDA ARSENAL.

KIPA wa Arsenal, Petr Cech amebainisha kuywa mazungumzo yake na Arsene Wenger yalisaidia kwa kiasi kikubwa uamuzi wake wa kutoka Chelsea na kwenda Arsenal kiangazi mwaka jana. Baada ya kupoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza kwa Thibaut Courtois pele Stamford Bridge, Cech mwenye umri wa miaka 33 aliamua kujiunga na Arsenal. Cech anaamini msimamo utakuwa kitu muhimu kama Arsenal watataka kunyakuwa taji la Ligi Kuu msimu huu. Akihojiwa Cech amesema wakati alipokutana na Wenger alimfafanulia jinsi gani mambo yanavyofanyika na kupangwa katika klabu na alipenda alichoambiwa. Cech aliendelea kudai kuwa anafahamu kuwa timu hiyo inapenda ushindani lakini wanapaswa kuwa na msimamo na kuhakikisha hawapoteza alama ili kuweza kushindani taji.

LAMPARD AHOFIA MUSTAKABALI WA CHELSEA PINDI TERRY ATAKAPOONDOKA.

KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Uingereza, Frank Lampard amesema ana mashaka kuhusu mustakabali wa Chelsea baada ya John Terry kuondoka katika klabu hioyo. Nahodha huyo anatarajiwa kuondoka Stamford Bridge majira ya kiangazi kufuatia kubainisha Januari kuwa mkataba wake wa sasa hautaongezwa. Lampard, ambaye aliondoka katika klabu hiyo mwaka 2014 baada ya kuitumikia kwa zaidi ya muongo mmoja, anadhani Chelsea wako hatarini kupoteza utambulisho wake. Kiungo huyo mkongwe amesema kinachomuogopesha ni kuhusu suala la haiba ya kweli katika timu pindi Terry atakapoondoka.

KLOPP APANIA KUIHARIBIA CITY.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema ana hamu ya kutwaa Kombe la Ligi wakati kikosi chake kikijitupa uwanjani kukwaana na Manchester City katika mchezo wa fainali utakaofanyika katika Uwanja wa Wembley. Meneja huyo raia wa Ujerumani anategemea mchezo mgumu kutoka kwa City haswa kutokana na timu hiyo kurejea katika kiwango chao kwa ushindi mzuri waliopata katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Dynamo Kiev uliochezwa katikati ya wiki. Klopp ana matumaini ya kutwaa taji lake la kwanza akiwa Na Liverpool baada ya klupita miezi mitano pekee toka akabidhiwe mikoba ya kuinoa. Akihojiwa Klopp amesema anafahamu kuwa City wako vizuri kwasasa na utakuwa mchezo mgumu lakini ana hamu kubwa ya kushinda taji hilo.

Saturday, February 27, 2016

CHIELLINI FITI KUIVAA INTER.

KLABU ya Juventus imethibitisha beki wake Giorgio Chiellini yuko fiti na anaweza kurejea katika mchezo wa Serie A dhidi ya Inter Milan utakaochezwa baadae leo. Chiellini alikosa mechi tatu zilizopita za Juventus kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya msuli aliyopata katika mchezo dhidi ya Frosinone ambao walishinda mabao 2-0. Hata hivyo, beki huyo mwenye umri wa miaka 31, ametajwa katika kikosi cha wachezaji 23 ambacho kitakuwa ugenini leo kuivaa Inter Milan. Meneja wa Juventus, Massimiliano Allegri pia amewajumuisha Kwadwo Asamoha na Alex Sandro katika kikosi hicho.

Friday, February 26, 2016

UCHAGUZI FIFA: SASA UKOMO NI VIPINDI VITATU PEKEE, SEXWALE AJITOA DAKIKA ZA MAJERUHI.

RAIS atakayechaguliwa kuliongoza Shirikisho la Soka Duniani-FIFA anatarajiwa kuwa ukomo wa uongozi wa vipindi vitatu baada ya shirikisho hilo kuamua kupitisha mageuzi hayo ili kujinasua kutoka katika janga la ufisadi linaloikabili kwasasa. Baraza jipya linatarajia kuchukua nafasi ya kamati ya utendaji ya sasa huku kukiwapo na kila mwakilishi mwanamke kutoka katika kila shirikisho. Mageuzi hayo yalitangazwa leo katika mkutano mkuu maalumu uliofanyika jijini Zurich, ambayo pia yameamua kuweka wazi suala la mishahara. 
Wakati wowote kuanza sasa FIFA itapata rais mpya atakayechukua mikoba ya Sepp Blatter ambaye ameliongoza shirikisho hilo kwa miaka 18 yenye vipindi vitano. Wagombea wamebaki wanne wanaogombea nafasi hiyo ambao ni Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa wa Bahrain, Gianni Infantino ambaye ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, Prince Ali bin al-Hussein wa Jordan na Jerome Champagne wa Ufaransa baad ya Tokyo Sexwale wa Afrika Kusini kujitoa dakika za mwisho.

DFB KWAWAKA MOTO: BAADA YA RAIS SASA KATIBU MKUU.

KATIBU mkuu wa Shirikisho la Soka la Ujerumai-DFB, Helmut Sandrock amejiuzulu wadhifa wake huo akidai kashfa ya ufisadi iliyolikumba shirikisho hilo kuwa inahitaji watu wapya. Sandrock anakuwa ofisa wa pili wa ngazi ya juu ya DFB kujizulu kufuatia rais wa zamani Wolfsgang Niersbach kufanya hivyo kufuatia kashfa ya kulilipa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA ili waweze kuhakikisha wanapata uenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006. DFB inatarajia kuwasilisha taarifa yake kutoka tume huru kuhusiana na masuala hayo wiki ijayo huku pia ikitarajia kumpigia kura Reinhard Grindel kuwa rais wake mpya Aprili mwaka huu. Katika taarifa yake Sandrock amesema kwa mustakabali wa soka lao na DFB ni lazima kuanza upya ndio maana ameamua kujiuzulu ili kuwapisha viongozi wengine watakaochaguliwa.

RATIBA EUROPA LEAGUE: LIVERPOOL VS MAN UNITED.

KLABU ya Liverpool imepangwa kucheza na mahasimu wao Manchester United katika hatua ya timu 16 bora ya michuano ya Europa League. Kwa upande wa Tottenham Hotspurs wao wamepangwa kucheza na wakongwe wa soka wa Ujerumani Borussia Dortmund. Valencia wanaonolewa na Gary Neville wanatarajiwa kupambana na wapinzani wao katika La Liga Athletic Bilbao, wakati wa mabingwa watetezi wa michuano hiyo Sevilla wao watakuwa wageni wa FC Basel ya Uswisi ambao uwanja wao ndio uliotumika katika fainali iliyopita. Mechi hizo zinatarajiwa kuchezwa Alhamisi ya Machi 10 na 17 ambapo mshindi wa michuano wa michuano hiyo atafuzu moja kwa moja michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Ratiba kamili ya michuano hiyo ni kama ifuatavyo.Shakhtar Donetsk v Anderlecht
Basel v Sevilla
Villarreal v Bayer Leverkusen
Athletic Bilbao v Valencia
Liverpool v Manchester United
Sparta Prague v Lazio
Borussia Dortmund v Tottenham
Fenerbahce v Braga

VAN GAAL AMPONGEZA MARCUS RASHFORD.

MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal amempongeza Marcus Rashford kwa ushujaa alioonyesha katika ushindi wa mabao 5-1 waliopata dhidi ya Midjylland katika mchezo wa Europa League uliofanyika jana. Katika mchezo huo Rashford alifunga mabao mawili ndani ya dakika ya 12 ukiwa ni mchezo wa kwanza kupangwa katika kikosi cha kwanza kufuatia kuumia kwa Anthony Martial dakika za mwishoni. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 18 sasa anakuwa ameipita rekodi iliyowekwa na George Best ya mchezaji mdogo zaidi katika klabu hiyo kufunga katika michuano ya Ulaya. Akihojiwa Van Gaal amesema kipindi cha kwanza Rashford alikuwa akikimbia sana maeneo ya pembezoni hivyo ilivyofika mapumziko alimrekebisha na kumwambia aingie ndani zaidi kwani anaweza kufunga na ndivyo ilivyotokea. United sasa wanakuwa wamesonga mbele kwa jumla ya mabao 6-3 baada ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika Denmark kwa mabao 2-1.

BARCELONA YAFANIKIWA KUMTULIZA NEYMAR.

KLABU ya Barcelona imefanikiwa kuzipiku Real Madrid, Manchester United, Manchester City pamoja na Paris Saint-Germain kwa kumshawishi nyota wake Neymar kusaini mkataba mwingine mpya wa miaka mitano. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu kwenye tuzo za Ballon d’Or anadaiwa kusaini mkataba huo mpya ambao utamuweka Camp Nou mpaka mwaka 2021 na kumfanya kuwa mchezaji wa pili anayelipwa zaidi katika timu hiyo baada ya Lionel Messi. Mustakabali wa Neymar ulikuwa ukitiliwa shaka haswa kutokana na kesi ya masuala ya kodi inayomuandama hali ambayo ilizua tetesi kuwa anaweza kuondoka majira ya kiangazi. Hata hivyo, kumshawishi nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kusaini mkataba mwingine ni hatua nzuri kwa klabu hiyo ambayo aliisaidia kushinda mataji matano mwaka uliopita pekee.

OLISEH AACHIA NGAZI SUPER EAGLES.

NAHODHA wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria maarufu kama Super Eagles, Sunday Oliseh amejiuzulu wadhifa wake wa ukocha w atimu hiyo. Katika baru yake aliyotuma kwa Shirikisho la Soka la Nigeria-NFF jana, Oliseh alitangaza kujiuzulu na kulishukuru shirikisho hilo kwa nafasi waliyompa ya kulitumikia taifa lake. Oliseh ambaye alichukua mikoba ya kuinoa Super Eagles Julai mwaka 2015, amekuwa na haelewani na baadhi ya viongozi wa NFF na pia wachezaji wachache. Katibu Mkuu wa NFF Dkt. Mohammed Sanusi alithibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kwa kiungo huyo wa zamani wa Ajax Amsterdam. Hata hivyo, Sanusi amesema hawezi kwenda kwa undani kabisa kuhusiana na suala hilo kwasababu wapo katika mkutano wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA huko Zurich na pindi watakavyorudi watalishughulikia.

BARCELONA KUONGEZA MKATABA NA UNICEF.

KLABU ya Barcelona imeongeza mkataba wa ushirikiano na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa-UNICEF ambao utadumu mpaka mwaka 2020. Katika mkataba huo mpya utashuhudia Barcelona wakichangia kiasi cha euro milioni kwa mwaka ili kuinua suala la elimu kwa watoto. Katika taarifa ya klabu hiyo iliytumwa katika mtandao imedai kiasi hicho ni ongezeko la euro nusu milioni kulinganisha na euro milioni 1.5 ambazo walikuwa wakilipa kwa mwaka katika makubaliano ya awali. Makubaliano kati ya klabu hiyo na UNICEF yalianza mwaka 2006 wakati Barcelona walipovunja utamaduni wao wa kuweka nembo mbele ya fulana zao na kuamua kuweka nembo ya UNICEF. Toka wakati huo nembo ya UNICEF imehamishwa na kuhamia nyuma ya fulana za Barcelona ili kupisha wadhamini waliotoa mamilioni ya euro ambao ni kampuni ya ndege ya Qatar. Hata hivyo, mchango wa Barcelona bado umeendelea kusaidia mamilioni ya watoto katika nchi za Ghana, China, Brazil na Afrika Kusini.

Thursday, February 25, 2016

Manchester United Vs Midtjylland 5-1 [6-3] - All Goals & Match Highlight...

Liverpool vs Augsburg 1-0 25.02.2016 Europa League 1/16 Highlights & goa...

FC Porto vs Borussia Dortmund (BVB) 0-1 (0-3) 25.02.2016 Europa League 1...

Tottenham vs Fiorentina 3 0 All Goals & Highlights Europa League 24/2/ 2016

RONALDO ASISITIZA HANA MPANGO WA KUONDOKA MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amesisitiza kuwa na furaha katika klabu hiyo na hana mpango wowote wa kuondoka. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno amekuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka Santiago Bernabeu katika siku za karibuni huku Paris Saint-Germain ikitajwa kama timu atakayokwenda. Lakini pamoja na kukosolewa kiwango chake msimu huu na tetesi zilizozagaa kuhusu mustakabali wake, Ronaldo amesisitiza bado anadhani anakubalika na mashabiki wa Madrid na anataka kuendelea kuwepo hapo kwa kipindi kirefu. Ronaldo amesema Madrid ni klabu yenye shinikizo kubwa ndani na nje ya uwanja lakini amekuwa hapo kwa miaka mingi hivyo ameshazoea.

PIRES ATUNDIKA DARUGA AKIWA NA UMRI WA MIAKA 42.

WINGA wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Arsenal, Robert Pires ametangaza rasmi kutundika daruga zake akiwa na umri wa miaka 42. Pires pia amecheza katika klabu za Metz, Marseille, Villarreal na Aston Villa kabla ya kwenda kumalizia soka lake katika klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya India, Goa ambako aliondoka Machi mwaka jana. Mkongwe huyo aliliambia jarida la L’Equipe kuwa kwa umri aliofikia anadhani wakati wa yeye kuacha kucheza soka umefika ili aweze kupisha nafasi kwa vijana wanaochipukia. Akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, Pires alifanikiwa kushinda taji la Kombe la Dunia mwaka 1998, Euro mwaka 2000 na mataji mawili ya Kombe la Shirikisho kabla ya kuacha mechi za kimataifa mwaka 2004. Kwa upande wa vilabu, Pires alifanikiwa kucheza kwa mafanikio akiwa na Arsenal kuanzia mwaka 2000 mpaka 2006 na kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu ikiwemo msimu wa 2003-2004 ambao walishinda taji hilo bila kufungwa mechi yeyote.

RAIS WA ZAMANI WA BAYERN ATAKA KUBAKIA MSHABIKI WA KAWAIDA BAADA YA KUTOKA GEREZANI.

RAIS wa zamani wa Bayern Munich, Uli Hoeness amesema anataka kubakia kuwa mshabiki pekee kufuatia kuachiwa kutoka jela juzi ambako ametumikia nusu ya kifungo chake kutokana na makosa ya ukwepaji kodi. Hoeness ametumikia miezi 21 jela katika miaka mitatu ya kifungo chake baada ya kuhukumiwa Machi mwaka 2014 kufuatia kukutwa na hatia ya kukwepa kodi inayofikia euro milioni 28.5. Hoeness alitumikia kifungo chake katika gereza la Landsberg na alikuwa akitumikia kifungo cha nje toka Januari mwaka 2015 ambapo alikuwa akifanya kazi katika akademi ya vijana ya Bayern nyakati za mchana na kurejea jela jioni. Akihojiwa Hoeness amesema kwasasa anataka kufurahia soka na jambo kubwa atakalokuwa akifanya ni kwenda uwanjani na kushuhudia mechi kama mshabiki wa kawaida. Hoeness amewahi kuitumikia Bayern akiwa mchezaji, meneja na rais katika kipindi cha miongo minne iliyopita.

DE GEA KUWAKOSA WADENMARK.

GOLIKIPA wa Manchester United, David de Gea anatarajiwa kukosa mchezo wa tatu mfululizo wakati watakapokuwa wenyeji wa FC Midtjylland katika mchezo wa marudiano wa Europa League. De Gea amekosa michezo miwili toka alipoumia goti wakati wa mazoezi kabla ya mchezo wao wa mkondo wa kwanza dhidi ya timu hiyo ya Denmark ambapo United ilitandikwa mabao 2-1. Meneja wa United, Louis van Gaal amethibitisha kutokuwepo kwa De Gea katika mchezo huo wa leo. Naye winga wa United Antonio Valencia ambaye yuko nje ya uwanja toka Octoba, anakaribia kupona lakini hatakuwepo katika mchezo wa leo.

AL AHLY YAMUAJIRI KOCHA WA ZAMANI WA SPURS.

MENEJA wa zamani wa Tottenham Hotspurs na Fulham, Martin Jol ameteuliwa kuwa kocha mpya wa klabu kongwe nchini Misri ya Al Ahly. Kocha huyo raia wa Uholanzi anatachukua mikoba ya Jose Peseiro wa Ureno ambaye aliondoka Januari mwaka huu kwenda kuifundisha FC Porto. Hatua hiyo inamaanisha kuwa mahasimu wa jiji la Cairo Al Ahly na Zamalek wote wameajiri makocha wapya kufuatia Zamalek wao kumchukua Alex McLeish. Al Ahly kwasasa ndio vinara wa Ligi Kuu nchini humo wakiwa juu ya Zamalek ambao ni mabingwa watetezi. Mbali na kuzinoa klabu hizo za Uingereza, Jol pia amewahi kusifundisha Humburg ya Ujerumani na Ajax Amsterdam ya Uholanzi. Jol mwenye umri wa miaka 60 amekuwa bila kibarua toka lipotimuliwa Fulham mwaka 2013.

PELLEGRINI ASIFIA UAMUZI WAKE.

MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amesema uamuzi wake wa kuipa kipaumbele michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya badala ya Kombe la FA umewasaidia kwa kiasi kikubwa kupata ushindi dhidi ya Dynamo Kiev jana. Pellegrini alikosolwa vikali kwa kuchezesha kikosi dhaifu katika mchezo wa Jumapili iliyopita ambao walitandikwa mabao 5-1 na Chelsea, lakini jana walifanikiwa kushinda mabao 3-1 katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza kwa mabao 3-1. Akihojiwa Pellegrini amesema kikubwa kilichochangia kuwapumzisha nyota wake wengi katika mchezo dhidi ya Chelsea ni upungufu wa wachezaji alionao katika kikosi chake hivi sasa. Mabao ya Sergio Aguero, David Silva na Yaya Toure yalitosha kuihakikishia City ushindi huo, wakati Joe hart ambaye pia alipumzishwa katika mchezo wa FA naye alifanya kazi kubwa kuzuia mashambulizi ya Kiev.

UCHAGUZI FIFA: SEXWALE AKANUSHA TETESI ZA KUTAKA KUJITOA.

MFANYABIASHARA na mwanasiasa wa Afrika Kusini, Tokyo Sexwale amesisitiza leo kuwa ataendelea na mbio za kuwania urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA pamoja na wasiwasi uliopo katika kampeni zake. Akizungumza na wanahabari katika kikao chake maalumu na maofisa wa mashirikisho ya nchi za Amerika Kaskazini na Kusini jijini Zurich, Sexwale amesema pamoja na magumu yote anayopitia lakini bado ataendelea kupambana. Sexwale mwenye umri wa miaka 62 aliendelea kudai kuwa wamekwenda pale kwa ajili ya FIFA kwani shirikisho hilo ni kama nyumba iliyobomoka hivyo inahitaji mtu sahihi wa kuirekebisha. Sexwale anachuana na Sheikh Salman bin Ibrahim Al-Khalifa wa Bahrain, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Gianni Infantino, makamu wa zamani wa rais wa FIFA Prince Ali bin al-Husein na Ofisa wa amani wa FIFA Jerome Champagne. Uchaguzi wa shirikisho hilo ambao utashirikisha wajumbe 207 unatarajiwa kufanyika kesho huko Zurich, Uswisi.

UCHAGUZI WA FIFA KAMA KAWA PAMOJA NA PINGAMIZI.


UCHAGUZI wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA unatarajiwa kuendelea kama ulivyopangwa kesho baada ya mgombea Prince Ali bin al-Hussein kushindwa kesi yake ya kutaka uchaguzi usimamishwe. Prince Ali mwenye umri wa miaka 40, alifungua kesi kutokana na kutofurahishwa na taratibu za upigaji kura zilivyo lakini Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS imetupilia mbali kesi hiyo. Mgombea huyo raia wa Jordan alikuwa akitaka uwazi zaidi katika vyumba vya kupigia kura ili kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa huru na haki. Akihojiwa Prince Ali amesema amefanya kila analoweza na anajutia kwasababu mfumo ndio umewaangusha.

Wednesday, February 24, 2016

MOURINHO AKANUSHA TETESI ZA KWENDA UNITED.

MENEJA wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho amesema hafahamu kuhusu yeye kuja kuwa meneja ajaye wa Manchester United lakini ana matumaini ya kurejea katika soka majira ya kiangazi. Mapema mwezi huu, taarifa zilizagaa kuwa United walikuwa wamefanya mazungumzo na wawakilishi wa meneja huyo raia wa Ureno. Mourinho mwenye umri wa miaka 53, alitimuliwa na Chelsea Desemba mwaka jana ikiwa imepita miezi saba toka atwae taji la Ligi Kuu. Akijibu swali la mwana habari wakati akiwa katika shughuli za kijamii huko Singapore, Mourinho amesema hafamu lolote kuhusu yeye kuja kuwa meneja wa United lakini anachofahamu yeye ni kuwa atarejea katika masuala ya soka ifikapo majira ya kiangazi.

RONALDO NDIO MFALME WA MITANDAO YA KIJAMII, AFIKISHA MASHABIKI MILIONI 200.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ameweka historia katika mitandao ya kijamii kufuatia kuwa mwanamichezo wa kwanza kufikia idadi ya watu milioni 200 wanaomfuatilia katika mitandao ya Facebook, Instagram na Twitter. Ronaldo ana mashabiki milioni 109.7 wanaomfuatilia katika Facebook, milioni 49.6 wanaomfuatilia katika Instagram na milioni 40.7 wanaomfuatilia katika Twitter. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno sasa wanakuwa na mashabiki wengi wanaomfuatilia katika mitandao hiyo kuliko wanamichezo wengine wa zamani na wa sasa wakiemo nyota wa zamani wa NBA Michael Jordan, Kobe Bryant, LeBron James, Kevin Durant na Stephen Curry ambao wote kwa pamoja wana mashabiki milioni 187 wanaowafuatilia katika mitandao hiyo. Ronaldo anaweza kuwa ameshindwa tuzo ya Ballon d’Or na Lionel Messi lakini mshambuliaji huyo amempita kwa mbali Muargentia huyo ambaye ana mashabiki milioni 120.8 pekee katika mitandao ya kijamii.

WENGER ATUPA TAULO, ADAI BARCELONA WAMEFUZU KWA ASILIMIA 95.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amedai kuwa Barcelona wamefuzu kufika robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa asilimia 95 baada ya kikosi chake kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa mabingwa hao wa Hispania. Wenger raia wa Ufaransa ameilaumu safu yake ya ushambuliaji kwa kushindwa kutumia vyema nafasi walizopata katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Emirates. Nyota wa Arsenal Alex Oxlade-Chamberlain na Olivier Giroud walikosa nafasi za wazi kabla ya Barcelona hawajafunga bao la kuongoza kupitia kwa nyota wake Lionel Messi. Akihojiwa Wenger amesema kwa jinsi walivyokuwa wakitumia nafasi za mwisho ni tatizo hivyo wanapaswa kujirekebisha haraka kabla ya mchezo wa maruadiano. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kimahesabu Barcelona wameshafuzu kwa asilimia 95 lakini wanataka kwenda Camp Nou kucheza hivyo anaamini wanaweza kupata nafasi hata hiyo kiduchu iliyobakia.

SHABIKI WA LEICESTER ATAKA KUMPA BINTI YAKE JINA LA VARDY KAMA KUMBUKUMBU.

SHABIKI mmoja wa Leicester City ana matumaini ya kumpa jina la Jamie Vardy binti yake lakini kama ataungwa mkono vya kutosha ili kumshawishi mpenzi wake. Vardy ameng’ara ghafla katika soka la Uingereza msimu huu akivunja rekodi ya kushinda mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu huku akiongoza kwa kutia nyavuni mabao 19 mpaka sasa. Sasa shabiki huyo Ashley Marriot anataka kuweka kumbukumbu ya msimu huu wa 2015-2016 ambao unaweza kumalizika kwa Leicester kuibuka mabingwa wa ligi, kwa kuongeza Vardy katika majina ya binti yake. Hata hivyo, suala hilo litakubaliwa na mpenzi wake Rebekah endapo tu ataungwa mkono za watu 5,000 katika mitandao.

ZIDANE ATAKA VIUNGO WAWILI KIANGAZI.

MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amepanga kuwawania Paul Pogba na Youri Tielemans majira ya kiangazi. Taarifa zinadai kuwa Zidane anahofia kumtegemea sana Luka Modric katika nafasi ya kiungo na anataka kuimarisha safu hiyo kwa ajili ya msimu ujao. Pogba ni aina ya mchezaji ambaye anaweza kucheza moja kwa moja katika kikosi cha kanza cha Madrid na Zidane ana matumaini ya kumnasa Mfaransa mwenzake huyo. Tielemans kwa upande wake amekuwa katika kiwango bora toka alipoibuka katika kikosi cha kwanza cha Anderlecht na Madrid wanaona chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 18 ataweza kuisadia timu hiyo siku zijazo.

INFANTINHO ANA UHAKIKA WA KUPATA KURA NYINGI AFRIKA.

MGOMBEA urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Gianni Infantino ana uhakika kuwa atakusanya kura nyingi kutoka mataifa ya Afrika katika uchaguzi Ijumaa hii. Infantino alifnya ziara fupi Afrika Kusini kwa mwaliko wa hasimu wake katika kinyang’anyiro hicho Tokyo Sexwale ambapo wawili hao walikutana katika kisiwa cha Robben, gerea ambalo Sexwale aliwahi kufungwa katika kipindi cha ubaguzi wa rangi. Kisiwa cha Robben pia ndio ambako rais wa zamani wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela alifungwa. Lakini pamoja na Shirikisho la Soka la Afrika-CAF kutoa msimamo wake kuwa watamuunga mkono Sheikh Salman bin Ibrahim al-Khalifa wa Bahrain, katibu mkuu huyo wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA ameema ana uhakika wa kuungwa mkono na mataifa ya Afrika.

MENSAH AENDA ANZHI.

BEKI wa kimataifa wa Ghana, Jonathan Mensah amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu na klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi. Beki huyo mwenye umri wa miaka 25, alikuwa akiichezea klabu ya ligi daraja la pili ya Ufaransa, Evian Thonon Gaillard ambapo mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Sasa Mensah anatarajiwa kujiunga na kikosi cha Anzhi wakati watakapokuwa katika kambi ya mazoezi ya majira ya baridi nchini Hispania. Mensah alishinda taji la Kombe la Dunia mwaka 2009 akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Ghana cha vijana chini ya umri wa miaka 20 na amewahi kukichezea kikosi cha wakubwa katika Kombe la Dunia mwaka 2010 na 2014.

BARCELONA NDIO TIMU BORA DUNIANI - SUAREZ.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Luis Suarez amesisitiza kuwa malengo yao makubwa ni kutetea taji lao la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuifunga Arsenal kwa mabao 2-0 jana. Mabao mawili yaliyofungwa na Lionel Messi katika kipindi cha pili yalitosha kuwapa uongozi Barcelona katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza hatua ya 16 bora uliofanyika katika Uwanja wa Emirates. Barcelona wanaonolewa na Luis Enrique wamepania kutetea taji lao hilo ili ije kuwa timu ya kwanza kuwahi kufanya hivyo toka AC Milan walivyofanikiwa miaka 25 iliyopita. Akihojiwa Suarez amesema wana matamanio makubwa ya kutaka kuendelea kushinda mataji kwasababu wana kikosi bora kabisa duniani.

JINSI ARSENAL WALIVYOZIDIWA MAARIFA NA BARCELONA.KLABU ya Barcelona jana imefanikiwa kupiga hatua moja muhimu kuelekea hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuichapa Arsenal kwa mabao 2-0 katika uwanja wao wa Emirates. Nyota wa Barcelona Lionel Messi ndio aliibuka shujaa wa mchezo kwa kufunga mabao yote mawili katika dakika 71 na lingine la penati katika dakika ya 86. Hiyo inakuwa mara ya kwanza kwa Messi kumfunga kipa wa Arsenal Petr Cech katika mara saba walizokutana huku akifikisha mabao nane aliyoifunga Arsenal katika michuano hiyo. Katika mchezo mwingine uliochezwa jana Juventus walilazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo uliofanyika jijini Turin. Mechi za maruadiano kwa timu hizo zinatarajiwa kuchezwa Machi 16 mwaka huu.

Monday, February 22, 2016

HENRY ADAI ARSENAL WANAPASWA KUSAHAU VYENGA VYAO KAMA WANATAKA KUIFUNGA BARCELONA.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry amedai kuwa timu hiyo inapaswa kutumia mipira ya kushtukiza na kuepuka kukaa na mipira kama wanataka kuwa na nafasi ya kuifunga Barcelona. Arsenal wanatarajiwa kuwa wenyeji wa Barcelona katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora kesho kabla ya kurudiana nao tena Camp Nou Machi 16 mwaka huu. Barcelona wanapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo lakini Henry anaamini Arsenal wanaweza kuwa na nafasi kama meneja wake Arsene Wenger akibadilisha mbinu zake. Katika makala yake aliyoandika katika gazeti la The Sun kuhusiana na mchezo huo, Henry amedai Arsenal wanapaswa kukubali kuwa hawatakuwa na nafasi ya kumiliki mpira kwa kipindi kirefu kama walivyozoea na pindi wanapopata nafasi wanapaswa kuitumia ipasavyo. Henry amesema ni mara chache timu inaweza kupata nafasi ya kucheza na Barcelona hivyo Wenger anapaswa ajiandae kubadili mbinu zake za kushambulia pindi awapo nyumbani na ugenini. Barcelona imekuwa katika kiwnago bora msimu huu, wakiongoza La Liga kwa tofauti ya alama nane baada ya kuichapa Las Palmas kwa mabao 2-1 juzi.

NILIKATAA OFA YA MAN UNITED - VIDAL.

KIUNGO wa Bayern Munich, Arturo Vidal amebainisha alikataa uhamisho wa kwenda Manchester United ili aweze kujiunga na mabingwa wa Bundesliga. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 aliondoka Juventus kuelekea Allianz Arena kiangazi mwaka jana lakini pia alikuwa amepata ofa kadhaa kutoka klabu zingine wakiwemo United. Vidal amesema kulikuwa na nafasi ya kwenda kujiunga na United lakini alibadili mawazo yake na kuamua kujiunga na Bayern. Mchezaji huyo aliendelea kudai kuwa alipenda nafasi ambayo United walimpatia lakini haikuwezekana na kuamua kwenda Ujerumani.

AUBAMEYANGA ADAI ALIKATAA KWENDA NEWCASTLE.

MSHAMBULIAJI nyota wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang amebainisha kuwa alikaribia kujiunga na Newcastle United miaka mitatu iliyopita lakini alibadili uamuzi na kuamua kwenda Ujerumani. Nyota huyo wa kimataifa wa Gabon sasa ni mmoja kati ya washambuliaji hatari barani Ulaya akiwa amefunga mabao 21 katika Bundesliga msimu huu huku akiripotiwa kuwindwa na klabu za Manchester United na Chelsea kwa kitita cha paundi milioni 70. Mwaka 2013 klabu ya zamani ya mshambuliaji huyo Saint-Etienne ya Ufaransa ilimlazimisha kujiunga na Newcastle lakini aliwakatalia na kuamua kwenda Dortmund pamoja na dau kubwa alilowekewa na klabu hiyo. Akihojiwa Aubameyang amesema alipata ofa kutoka Qatar ambayo ingemuwezesha kukunja kitita cha euro milioni 10 kwa mwaka lakini aliamua kubakia Saint-Etienne ambako alikuwa akipata euro 70,000 kwa mwezi akifahamu kuwa kutokana na ubora wake atakuja kupata fedha nyingi zaidi baadae. Nyota huyo anaendelea kudai kuwa msimu uliofuata Saint-Etienne ilitaka kumuuza Newcastle lakini aliamua kuichagua Dortmund kwakuwa baba yake aliona mbinu za Jurgen Klopp zingemfaa kwenye klabu hiyo pamoja na mshahara mdogo atakaopokea.

MCHEZAJI ATOLEWA NJE BADA YA KUMUONYESHA MWAMUZI KADI NYEKUNDU.

MCHEZAJI wa klabu ya Trabzonspor, Salih Dursun ametolewa nje kwa kumuonyesha mwamuzi kadi nyekundu wakati wa mchezo waliofungwa mabao 2-1 na Galatasaray katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uturuki uliofanyika jana. Tukio hilo lilitokea dakika ya 86 ya mchezo baada ya mwamuzi Denis Bitnel kumuonyesha kadi nyekundu ya moja kwa moja Luis Cavanda kwa kufanya madhambi ndani ya eneo la hatari. Wachezaji wa Trabzospor walimzonga mwamuzi kupinga kadi hiyo ambapo Dursun alimnyang’anya mwamuzi kadi aliyokuwa nayo na kumuonyeshea hatua ambayo ilipelekea na yeye kutolewa hivyo kuwafanya wenzake kucheza pungufu zaidi. Hii sio mara ya kwanza kwa klabu hiyo kuingia katika mizozo na waamuzi, kwani Novemba mwaka jana mwenyekiti wao Ibrahim Haciosmanoglu alifungiwa siku 280 baada ya kuwafungia waamuzi wanne uwanjani kwa kushindwa kutoa penati kwa timu hiyo.

BRAZIL WAFURAHIA KUNDI WALILOPANGWA COPA AMERIKA.

MKURUGENZI wa ufundi wa Shirikisho la Soka la Brazil, Gilmar Rinaldi amesema amefurahishwa na kundi walilopangwa katika michuano ya Copa America mwaka huu. Brazil ambao ni mabingwa mara nane wa michuano hiyo wamepangwa kundi B sambamba na timu za Ecuador, Haiti na Peru katika ratiba iliyopangwa jijini New York, Marekani jana. Akihojiwa mara baada ya upangwaji wa ratiba hiyo, Rinaldi amesema imekuwa ahueni kwao kwani wamepangwa kundi ambalo kidogo lina afadhali kulinganisha na mengine. Akizichambua timu walizopangwa nazo, Rinaldi amesema Ecuador kwasasa wanapitia kipindi kizuri kwani wanaongoza katika kundi katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018 hivyo ni timu yenye ushindani na wanapaswa kuwa heshimu. Rinaldi aliendelea kudai kuwa Peru walikuwa wakisuasua katika michuano hiyo iliyofanyika mwaka jana lakini tayari wameimarika. Mkurugenzi huyo amesema Haiti hawaifahamu sana hivyo watatuma wawakilishi wao kwenda kuipeleleza ili waweze kujiandaa vyema pindi watakapokutana nao.

RATIBA COPA AMERIKA: ARGENTINA WAPANGWA NA CHILE KUNDI MOJA.

MABINGWA watetezi Chile, wamepangwa katika kundi moja la D sambamba na Argentina, Bolivia na Panama katika michuano ya Copa Amerika 2016. Chile waliitandika Argentina kwa changamoto ya mikwaju ya penati mwaka jana na kushinda taji lao la kwanza kubwa katika historia. Michuno mikongwe kabisa ya kimataifa ambayo inatimiza miaka 100, itashuhudia wenyeji Marekani wakipambana na Colombia, Costa Rica na Paraguay wakivaana katika kundi A. Uruguay ambayo ndio timu iliyopata mafanikio zaidi katika michuano hiyo wenyewe wamepangwa na Jamaica, Mexico na Venezuela katika kundi C wakati mabingwa wa mwaka 2007 Brazil wao watakuwa na Ecuador, Haiti na Peru katika kundi B. Michuano hiyo ya mwaka huu imeongeza timu nne na imekuwa ya kwanza kufanyika nje ya Shirikisho la Soka la Amerika Kusini-COMNEBOL. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 3 kwa marekani kufungua dimba na Colombia huko Santi Clara, California huku fainali ikitarajiwa kuchezwa June 26 katika Uwanja wa MetLife uliopo East Rutherford, New Jersey.

Sunday, February 21, 2016

PICHA ZA PELE NA KIKOSI CHA BRAZIL KATIKA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA MWAKA 1966 NCHINI UINGEREZA.

PICHA za kipekee za Pele na kikosi cha Brazil kilichoshinda kombe la dunia la mwaka wa 1966 zimetolewa kwa mara ya kwanza. Picha hizo zinaonesha kikosi hicho kinachomjumuisha gwiji wa kandanda Pele wakibarizi nje ya mgahawa wa kifahari huko Cheshire Uingereza . 
Picha hizo ni sehemu ya onyesho moja katika mgahawa wa Lymm. Hoteli hiyo ya Lymm ndio iliyokuwa makao ya kikosi hicho wakati wa mchuano huo yapata miaka 50 iliyopita. Moja wa wachezaji nyota katika enzi hizo Pele na Garrincha wanaonekana wakijivinjari. Baadhi ya picha hizo zilipigwa na meneja wa magahawa huo Roger Allen. 
Meneja wa sasa wa hoteli hii ya Lymm, Jamie McDonald, anasema: "Babu yangu hakuisha kuzungumzia uwezo wa gwiji Pele. ''Alinieleza kuwa wakati huo wachezaji walikuwa wanyenyekevu mno ,hata wengine waliomba wenyeji baiskeli ilikupasha misuli moto'' Pele,wakati huo ndiye aliyekuwa ameuteka ulimwengu kwa miondoko yake na ilikumzuia asisumbuliwe na wapiga picha iliwabidi kukodishiwa hoteli ya kipekee yenye uwezo wa kuwalinda. 
Glenda Bowers, alikuwa na miaka 15 wakati huo. "mimi na mwenzangu tulikuwa wachanga kwa hivyo tuliruhusiwa kukutana na wachezaji hao'' Baadhi ya bidhaa zinazooneshwa ni pamoja na soksi na viatu zilizokuwa za Pele. "alimpatia mhudumu wa ndani aliyekuwa akifua nguo zao ikiwemo suruali fulana na hata sare moja.'' Pia kunapicha ambayo pele alipigwa pamoja na muhudumu wa baa bi Bessie Vale. 
Wakati huo Pele alikuwa ameapa kutocheza tena katika kombe la dunia akidai wachezaji weupe walimpiga mateke mengi mno katika uwanja wa Goodison Park. Uwanja huo wa Goodison Parkndio unaotumika na klabu inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza ya Everton. Onyesho hilo lenye nembo ya ''BrazilLymm66'', litaendelea kwa siku nne.

ROBO FAINALI FA: CHELSEA KUIVAA EVERTON.

KLABU ya Chelsea itasafiri kuwafuata mahasimu wao wa Ligi Kuu Everton katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA. Chelsea jana walifanikiwa kuirarua Manchester City kwa mabao 5-1 katika mchezo wa mzunguko wa tano uliofanyika katika Uwanja wa Stamford Bridge. Manchester United na Shrewsbury inayoshiriki ligi daraja la kwanza wao watacheza mchezo wao baadae leo ambapo mshindi atakuwa mwenyeji wa West Ham United. Mechi za robo fainali ya FA itazikutanisha Reading dhidi ya Crystal Palace wakati Watford wanasubiri mshindi katika mchezo wa marudiano kati ya mabingwa watetezi Arsenal dhidi ya Hull City. Mechi za robo fainali zinatarajiwa kuchezwa mwishoni mwa wiki ya Machi 11 na 14 mwaka huu.

JINSI MAN CITY WALIVYOFEDHEHESHWA NA CHELSEA KWENYE FA.

Friday, February 19, 2016

TETESI MBALIMBALI ZA USAJILI ZILIZOJIRI HUKO MAJUU.

PEP Guardiola anaripotiwa kumtaka kiungo wa Real Madrid Toni Kroos kwenda Manchester City ili kuchukua nafasi ya Yaya Toure, ingawa anaweza kukabiliwa na upinzani kutoka Manchester United.
Chanzo: AS

KIUNGO wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes anataka nafasi ukocha Old Trafford.
Chanzo: Manchester Evening News

IlKay Gundogan anatarajia kuikacha Barcelona na kwenda kusajiliwa Manchester City kutokana na mkanganyiko uliopo katika suala la usajili wake Camp Nou.
Chanzo: Sport

MSHAMBULIAJI wa Real Madrid Karim Benzema natarajia kukutana na Mathieu Valbuena kabla ya Machi 4 ili kuzungumzia kesi ya kutishia inayomkabili Benzema. Haijajulikana kama wawili hao watakutana binafsi au chini ya uangalizi wa Shirikisho la Soka la Ufaransa.
Chanzo: RMC

KOCHA wa Italia, Antonio Conte anataka kumpeleka kiungo wa AS Roma Radja Nainggolan Chelsea kama atafanikiwa kupewa kibarua cha kuinoa timu hiyo.
Chanzo: gianlucadimarzio.com

TAARIFA zinadai kuwa Jose Mourinho amepania kumpeleka mshambuliaji wa Juventus Alvaro Morata katika klabu ya Manchester United majira ya kiangazi ingawa kuna uwezekano wa kupata upinzani kutoka kwa Real Madrid.

Chanzo: La Stampa

MENEJA wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino anatajwa kuwa miongoni mwa makocha watano katika orodha iliyotengwa na Chelsea wengine wakiwa Diego Simeone, Jorge Sampaoli, Antonio Conte na Massimiliano Allegri.
Chanzo: ESPN

KLABU ya Paris Saint-Germain inajiandaa kuwawania mshambuliaji wa Everton Romelu Lukaku na Gonzalo Higuaini wa Napoli.
Chanzo: transfermarketweb.com

GOLIKIPA wa Arsenal, David Ospina anadaiwa kutaka kuondoka Arsenal baada ya kushindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.
Chanzo: Evening Standard