Thursday, February 28, 2013

LIGI KUU NCHINI UINGEREZA KUTUMIA GOAL LINE TECHNOLOGY MSIMU UJAO.

LIGI kuu nchini Uingereza inatarajiwa kuanza kutumia mfumo wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli wakati msimu mpya wa ligi hiyo 2013-2014. Mfumo huo ulifanyiwa majaribio na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia iliyofanyika Desemba mwaka jana na tayari viongozi wa ligi hiyo wameshaanza mazungumzo na kampuni zilizopewa dhamana ya kufunga vifaa hivyo. Msemaji wa ligi hiyo Dan Johnson amesema mara msimu ujao utakapoanza klabu zote zitalazimika kuwa na mfumo huo zikiwemo klabu ambazo zitakuwa zimepanda daraja. Mifumo miwili ya Hawkeye na GoalRef ambayo ndio imepitishwa na FIFA yote ilitumika katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia kwa mafanikio. 

DJOKOVIC, FEDERER WATINGA NUSU FAINALI DUBAI.

WACHEZAJI nyota wa mchezo wa tenisi Novak Djokovic na Roger Federer wameendelea kung’ara katika michuano ya Dubai baada ya wote kutinga hatua ya nusu fainali. Djokovic ambaye anashika namba moja katika orodha za ubora duniani alifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kumfunga Andreas Seppi wa Italia kwa 6-0 6-3 na sasa anatarajiwa kukutana na Juan Martin del Porto wa Argentina. Federer anayeshika namba mbili katika orodha hizo anaye alimsambaratisha bila huruma Nikolay Davydenko kwa 6-2 6-2 na sasa nyota huyo raia wa Switzerland atakutana na Tomas Berdych wa Jamhuri ya Czech. Berdych alitinga hatua hiyo kwa kumfunga Dmitry Tursunov wa Urusi kwa 6-3 6-2 wakati Del Potro yeye alimfunga Daniel Brands wa Ujerumani kwa 6-4 6-2 na kuhakikisha nyota wanaoshika nafasi nne za juu kukutana katika hatua ya nusu fainali.

WAMBURA AMSHUKIA TENGA.

KATIBU wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini-TFF au FAT kama ilivyokuwa ikijulikana kipindi hicho, Michael Wambura amemshukia rais wa shirikisho akidai anapaswa kulaumiwa kama Tanzania ikifungiwa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Kauli hiyo ya Wambura imekuja baada ya serikali kufuta katiba mpya na kuiamuru TFF itumie katiba ya zamani ya mwaka 2006 katika kufanya mchakato wa uchaguzi. Wambura amesema TFF kama taasisi nyingine inapaswa kufanya kazi zake kwa kufuata misingi na sheria za nchi hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo la serikali. Wambura amesema kama FIFA ikiifungia Tanzania kushiriki michuano ya kimataifa kutokana na kauli hiyo ya Serikali lawama zote anapaswa kupewa Tenga kwani yeye ndio chanzo cha mgogoro huu unaondelea hivi sasa. 

UNITED KUFANYA ZIARA THAILAND.

KLABU ya Manchester United imetangaza kuwa itafanya ziara nchini Thailand kwa ajili maandalizi ya msimu mpya wa 2013-2014 wa Ligi Kuu nchini Uingereza. United ambao kwasasa wanaongoza msimamo wa ligi hiyo wanatarajiwa kuiva Singha All Star jijini Bangkok Julai 13 mchezo ambao utafanyika katika Uwanja wa Rajamangala. Klabu tayari imeshafanya ziara mara nne katika nchi hiyo lakini hawajacheza mechi yoyote kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita. Klabu hiyo pia katika maandalizi yake ya msimu ujao itacheza mechi za kujipima nguvu katika miji ya Sydney, Tokyo, Osaka na Hong Kong.

SIMBA KUTIMKA ALFAJIRI KUIFUATA LIBOLO.

KIKOSI kamili cha Simba kinaondoka jijini Dar es Salaam kesho kikiwa na msafara wa watu 18, wakiwamo wachezaji 18 na viongozi saba. Wachezaji wanaoondoka ni Juma Kaseja, Abel Dhaira, Nassor Said Masoud, Amir Maftah, Koman Bili Keita, Juma Nyoso, Shomari Kapombe, Salim Kinje, Ramadhani Chomboh, Amri Kiemba, Haruna Moshi, Kiggi Makasi, Abdallah Seseme, Amri Kiemba, Haruni Chanongo, Mrisho Ngassa, Felix Sunzu na Abdallah Juma. Viongozi ni Zacharia Hans Poppe, Muhsin Balhabou, Patrick Liewig, Jamhuri Kihwelo, Dk. Cosmas Kapinga, James Kisaka na Kessy Rajab. Simba inaondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) majira ya saa 11:10 alfajiri na inatarajiwa kufika Luanda, Angola majira ya saa nne asubuhi. Timu itafanya mazoezi ya mwisho jijini Dar es Salaam leo jioni kabla ya kuelekea kambini ambapo wachezaji watapumzika kusubiri muda wa safari. Mechi kati ya Simba na Libolo itachezwa Machi 3 (Jumapili ijayo) katika Uwanja wa Calulo uliopo katika mji wa Calulo jimbo la Kwanza Sul (Kwanza Kusini).

RENARD KUSAKA VIPAJI NCHI NZIMA.

KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya Zambia Herve Renard na benchi lake la ufundi wako katika ziara ya kuzunguka nchi nzima kutafuta wachezaji wenye vipaji ambao wataweza kujuishwa katika kikosi cha nchi hiyo ambacho kitashiriki michuano ya Challenge ya Cosafa na ile ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani-CHAN itakayofanyika Afrika Kusini 2014. Ziara ya kutafuta wachezaji hao ilianza wiki kadhaa nyuma katika mikoa yote 10 ya nchi hiyo ambayo wameigawanya katika kanda tano ili kuifanya kazi hiyo kuwa rahisi zaidi. Kazi kubwa ya benchi la ufundi litakuwa ni kutafuta wachezaji katika mikoa yote hiyo na baadae kuwapeleka katika kanda zilizoteuliwa kwa ajili ya usaili ambapo kila kanda itakuwa na wachezaji wapatao 44. Kanda zilizoteuliwa ni Ndola ambayo usaili wake utakuwa Machi mosi na 2 mwaka huu huku nyingine zilikiwa ni Kabwe, Lusaka, Livingstone na Chipata.

BADO TUNA UCHU WA KUICHAPA TENA BARCELONA - ARBELOA.

BEKI wa klabu ya Real Madrid, Alvaro Arbeloa amesema timu yake imepania mchezo wa La Liga dhidi ya mahasimu wao Barcelona kuliko mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester United utakaochezwa Jumanne ijayo. Madrid walifanikiwa kuwafunga Barcelona nyumbani kwao Camp Nou kwa ushindi wa kihistoria kwa mahasimu hao wa mabao mabao 3-1 na kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Mfalme. Barcelona mwishoni mwa wiki hii watasafiri kuelekea Santiago Bernabeu kwa ajili ya mchezo mwingine wa ligi dhidi ya Madrid ambapo utakuwa kama mchezo wa kulipiza kisasi baada ya kufungwa. Arbeloa amesema wataanza kufikiria mchezo dhidi ya United Jumapili baada ya kuhakikisha wamepata matokeo mengine mazuri dhidi ya Barcelona kama walivyofanya katika mchezo wa kwanza.

ARSENAL KUMTENGENEZEA BERGKAMP MWANASESERE.

KLABU ya Arsenal imebainisha kuwa ina mpango wa kumuenzi mshambuliaji nyota wa zamani wa klabu hiyo Dennis Bergkamp kwa kujenga sanamu lake nje ya Uwanja wa Emirates. Bergkamp atakuwa anafuata nyayo za wachezaji wenzake wa zamani Thierry Henry na Tony Adams pamoja na meneja nguli wa klabu hiyo Herber Chapman ambao tayari sanamu zao zenye rangi ya fedha ziko nje ya klabu hiyo yenye maskani yake kaskazini mwa jiji la London. Klabu hiyo ililazimika kuthibitisha mpango wake huo baada ya umbo la sanamu la Bergkamp kuonekana katika mtandao. Akihojiwa kuhusu mpango huo Bergkamp amesema ni heshima kubwa kwake na ana jivunia kwasababu kila mtu anajua kiasi gani anaipenda klabu hiyo na alikuwa na wakati mzuri kipindi chote alichocheza hapo. Katika kipindi chake akiwa klabuni hapo Bergkamp alifunga mabao 120 na kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu na mengine manne ya Kombe la FA katika kipindi cha miaka 11 ambayo ameitumikia klabu hiyo.

Horror Tackle - Diego Braghieri's 2-Footed Assault On Ronaldinho - Worst...

UEFA YAMUWASHIA TAA YA KIJANI DROGBA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ivory Coast, Didier Drogba ameruhusiwa kuendelea kuichezea klabu ya Galatasaray katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya Shirikisho la Soka la bara hilo-UEFA kutupilia mbali madai ya klabu ya Schalke 04 ya Ujerumani. Drogba mwenye umri wa miaka 34 alicheza mchezo wake wa kwanza akiwa na Galatasaray katika michuano hiyo ya Ulaya dhidi ya Schalke Februari 20 katika hatua ya timu 16 bora ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1. Baada ya mchezo huo klabu ya Schalke ilipeleka malalamiko yake UEFA ikidai kuwa nyota huyo wa zamani wa UEFA hakusajiliwa kwa wakati ambao ungemuwezesha kucheza mechi za michuano hiyo. Hata hivyo UEFA ilitupilia mbali madai hayo ambapo kama Galatasaray wangekutwa na hatia ya kuchezesha mchezaji huyo kinyume cha sheria Schalke wangepewa ushindi wa mabao 3-0. Drogba amesajiliwa na Galatasaray kwa mkataba wa miezi 18 akitokea klabu ya Shanghai Shenhua ya China. 

FC Sevilla Vs Atletico Madrid 2-2 All Goals And Highlights 27.02.2013 Co...

David Beckham FULL DEBUT Highlights - PSG vs Marseille (2-0) Official *H...

Full HD middlesbrough vs chelsea 0-2 goals & highlights 27/02/2013

Bayern M√ľnchen Vs Borussia Dortmund 1-0 All Goals & Full Highlights 27.2...

Wednesday, February 27, 2013

MAPACHA HOSSAM NA IBRAHIM HASSAN WAPEWA KIBARUA CHA KIONOA MAKASA.

KLABU ya Misr Lel Makasa ya nchini Misri imewateua Hossam Hassan na pacha wake Ibrahim kuinoa timu hiyo msimu huu. Bodi ya klabu hiyo ilikutana na kuamua kumfukuza aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Mohammed Abd El Galel baada ya matokeo mabaya ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata katika ligi. 
Mwenyekiti wa Makasa Mohammed Abd El Salaam alithibisha uteuzi wa Hossam na Ibrahim kuinoa klabu hiyo ambapo wataanza kibaria hicho mapema wiki ijayo. Abd El Salaam alidai kuwa walianza mazungumzo na ndugu hao wiki iliyopita na kuafikiana na mpango huo na anawaamini wote wawili kama makocha wazuri na wanaweza kuikwamua timu hiyo na kuipeleka mbali. Mapacha hao ambao ni wachezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Misri walikuwa wakifundisha klabu ya Al Masry wakati maafa ya Port Saied yalipotokea mwaka 2011 na Zamalek katika msimu wa mwaka 2010. Mbali na timu hizo lakini pia waliisaidia timu ya taifa ya Misri kunyakuwa kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1998 nchini Burnina Faso chini ya Mahmoud Al Gouhary aliyekuwa akikinoa kikosi hicho wakati huo.

FRINGS ATUNDIKA DARUGA.

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani na nahodha wa klabu ya Toronto FC Torsten Frings ametangaza kustaafu soka akidai kuwa hawezi kurejea katika kiwango chake kufuatia kukoa msimu kutokana na kufanyiwa upasuaji wa nyonga. Frings ambaye ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mechi 79 na kucheza fainali mbili za Kombe la Dunia zikiwemo za mwaka 2002, ameitumikia Toronto kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu baada ya kucheza kwa mafanikio katika vilabu vya Bayern Munich, Werder Bremen na Borussia Dortmund. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 36 ndio alikuwa akilipwa zaidi katika klabu hiyo akichukua kitita cha dola milioni 2.43 lakini imebidi akatishe soka lake huko Marekani kutokana na majeruhi. Katika taarifa yake Frings amesema amgundua kuwa kupona kwake kutachukua muda mrefu kuliko alivyotegemea nay eye siku zote anataka kucheza kwa kiwango cha juu ili kuisasidia timu yake ndio maana ameamua kukaa pembeni ili aendelee kujiuguza taratibu.

TUNATAKIWA KUONGEZA BIDII ZAIDI - FABREGAS.

NYOTA wa zamani wa klabu ya Arsenal, Cesc Fabregas anadhani wachezaji wa timu yake ya Barcelona wanatakiwa kuongeza bidii zaidi uwanjani na kusahau machungu ya kufungwa waliyopata jana. Fabregas alisisitiza kwamba timu hiyo inatakiwa kujifunza kutokana na kipigo walichopata cha mabao 3-1 dhidi ya mahasimu wao Real Madrid jana usiku katika nusu fainali ya Kombe la Mfalme. Katika nusu fainali ya kwanza Barcelona walifanikiwa kupata matokeo ya sare ya bao 1-1 nyumbani kwa Madrid lakini walishindwa kutamba katika mchezo wao wa marudiano uliofanyka nyumbani kwao kwa kukubali kipigo hicho. Fabregas amesema wanatakiwa kujifunza kutokana na kipigo hicho ili kujipanga kuhakikisha wanashinda mchezo wao wa La Liga dhidi ya mahasimu wao hao Jumamosi kwani bado wana mataji ya kushindania. Barcelona katika mechi za karibuni imeonyesha kupunguza kasi yake waliyoanza nayo baada ya pia kukubali kipigo cha mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya AC Milan.

Tuesday, February 26, 2013

Full HD barcelona vs real madrid 1-3 goals & highlights 27/02/2013

INTER YATOZWA FAINI.

KAMATI ya nidhamu ya Ligi Kuu nchini Italia maarufu kama Serie A limeitoza faini ya euro 50,000 klabu ya Inter Milan baada ya mashabiki wake kukutwa na hatia ya kumfanyia vitendo vya kibaguzi mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo Mario Balotelli. Tukio lilitokea wakati Balotelli akiichezea kabla yake mpya ya AC Milan katika mchezo dhidi ya Inter ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1. Mashabiki wa Inter walikuwa wakipeperusha maganda ya ndizi katika mchezo huo lakini baadhi wachambuzi walidai pengine tukio hilo halikumlenga nyota huyo ambaye ameitumikia klabu hiyo kwa miaka minne. Balotelli ambaye ametokea Manchester City kabla ya kwenda AC Milan naye pia metozwa euro 10,000 kwa kuwaonyesha ishara ya matusi mashabiki hao. 

SHIRIKISHO LA SOKA LIBYA LAFANYA UCHAGUZI WA KWANZA TOKA MWAKA 1962.

SHIRIKISHO la Soka nchini Libya, FLF Jumatatu limemteua rais wa kwanza toka kuanzishwa kwa shirikisho hilo mwaka 1962. Anouer al-Tachan ndio jina lililoibuka kidedea katika uchaguzi huo ambao ulihudhuriwa na vilabu mbalimbali nchini humo. Katika mfumo wa zamani shirikisho hilo lilikuwa likimilikiwa na familia ya rais wa zamani wan chi hiyo Muammar Gaddafi haswa watoto wa kiume wa rais huyo Saadi na Mohammed. Mfumo mpya katika shirikisho hilo hivi sasa una wajumbe wakuchaguliwa wapatao 12 ambao kazi yao kubwa itakuwa kuratibu na kuweka mfumo mzuri wa uongozi katika kipindi cha mwaka mmoja watakachotawala. Ligi Kuu nchini humo bado haijachezwa toka kuanguka utawala wa zamani mwaka 2011 kutokana na harakati za kuhakikisha usalama unaimarika kwanza kabla ya kuanza.

BARCELONA BADO YAMNYATIA NEYMAR.

MAKAMU wa rais wa klabu ya Barcelona, Josep Bartomeu amebainisha kuwa klabu hiyo iko tayari kuanza mbio za kumsajili mshambuliaji nyota wa klabu ya Santos, Neymar mara watakapopata ishara kwamba nyota huyo yuko tayari kuondoka. Mshambuliaji huyo nyota wa kimataifa kutoka Brazil, anaendelea kuhusishwa na kuhamia vilabu vya Ulaya lakini mwenyewe amesisitiza mara kwa mara kuwa hana haraka ya kuondoka nchini kwake kabla ya Kombe la Dunia 2014 ambalo litafanyika katika ardhi yao. Hatahivyo pamoja na kauli ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 lakini klabu hiyo imeendelea kumfuatilia nyendo zake na wako tayari kumchukua wakati atakapoamua kuondoka Santos. Mkataba wa Neymar unamalizika baada ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014.

ETO'O APOKELEWA KISHUJAA GUINEA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o amepokelewa kishujaa na maelfu ya mashabiki jijini Conakry nchini Guinea kabla ya kukutana na rais wan chi hiyo Alpha Conde na baadhi ya mawaziri ka maongezi binafsi. Eto’o ambaye amewahi kunyakuwa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mara nne baadae alitembelea uwanja mpya wa Nongo wenye uwezo wa kuingiza watu 50,000 wilaya ya kaskazini mwa mji huo. Wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Shirikisho la Soka la Guinea, Eto’o alieleza sababu za yeye kutembelea nchi hiyo kuwa anataka kufanya mazungumzo kwa ajili ya shule ya soka kwa vijana wan chi hiyo. Nyota huyo ambaye amewahi kucheza katika vilabu vya Barcelona, Inter Milan na sasa Anzi Makhachkala ya Urusi tayari ameshafungua shule za soka nchini kwake Cameroon na Gabon ambapo wanafunzi wanasoma bure. Matunda ya shule hizo tayari yameshaanza kuonekana baada ya mshambuliaji mwenye umri wa miaka 16 Fabrice Olinga kutoka Cameroon kunyakuliwa na klabu ya Malaga inayoshiriki Ligi Kuu nchini Hispania akitokea katika shule hizo.

MCLAREN ATIMULIWA FC TWENTE.

KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Steve McClaren amejiuzulu wadhfa wake wa kuinoa klabu ya FC Twente ya Uholanzi siku moja baada ya kufanya mazungumzo na mwenyekiti wa klabu hiyo Joop Munsterman. Klabu hiyo haijashinda mchezo wowote wa ligi toka Desemba 21 na wapo katika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi wakiwa nyuma kwa ya PSV Eindhoven wanaoongoza ligi kwa alama sita. MacClaren amesema kuwa wamekubaliana na uongozi kwa lazima aondoke kwa manufaa ya klabu na anaondoka akiwa mtu anayejivunia baada ya kuiwezesha klabu hiyo kunyakuwa taji la ligi mwaka 2010. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 51 alijiunga na Twente baada ya kutimuliwa kibarua cha kuinoa Uingereza Novemba mwaka 2007 kufuatia nchi hiyo kushindwa kufuzu michuano ya Kombe la Ulaya mwaka 2008.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

KAMATI YA UTENDAJI TFF KUJADILI TAMKO LA SERIKALI
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepokea barua ya Serikali ikielezea uamuzi wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutengua uamuzi wa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kuidhinisha marekebisho ya Katiba ya TFF toleo la 2012.
Baada ya kupokea barua hiyo jana alasiri (Februari 25 mwaka huu), Sekretarieti iliwasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye ameagiza kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tamko hilo.Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitafanyika Jumamosi (Machi 2 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

KOCHA AZAM AFUNGIWA KWA KUCHOJOA BUKTA
Kocha Mkuu wa Azam, Stewart John Hall amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushusha bukta yake na kumlalamikia mwamuzi msaidizi wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Kagera Sugar iliyochezwa Januari 26 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za michuano ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali. Naye Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis Mwingira ametozwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa Manungu. Ally Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro naye ameangukiwa na rungu la Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu. Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na Kagera Sugar iliyochezwa Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Matukio ya aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya kujirudiarudia ambapo Oktoba 13 mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Morogoro aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu yake wacheze rafu. Naye Kocha wa timu ya Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya mechi dhidi ya Transit Camp iliyofanyika Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi. Pia Kocha wa Burkina Faso, Hasheem Mkingie amepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya FDL dhidi ya Mkamba Rangers. Kiongozi wa Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani baada ya mechi dhidi ya Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa miezi sita. Vilevile timu ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi kati yao na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka jana katika Uwanja wao wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Pia Coastal Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Nayo klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa timu yake kugoma kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana.
Timu ya Burkina Faso ya Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na kuonesha vitendo vya ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Oktoba 24 mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Faini ya ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya Pamba baada ya kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Nayo Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki wake kumtolea lugha chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), Hamis Semka na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa mjini Morogoro. Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kupotea. Pia klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao kuchelewa kufika uwanjani au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting). Klabu hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans, Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa, Moro United. Mchezaji Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal Union alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia kipa wa timu ya Transit Camp, Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka uzio na kwenda kupigana na washabiki. Kwa vile masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu yamepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

MWAMUZI FIFA, MAHAGI WAONDOLEWA VPL
Mwamuzi Msaidizi wa FIFA, Ferdinand Chacha ameondolewa kuchezesha mechi za VPL baada ya kupata alama za chini kwenye mechi kati ya African Lyon na Simba iliyochezwa mwezi uliopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Waamuzi wanaopata alama 6.5 au chini ya hapo kati ya 10 zinazohitajika pia wanaondolewa kwenye mechi za VPL na FDL. Waamuzi wengine walioondolewa kwa kutomudu mechi walizochezesha za VPL ni Mathew Akrama (Yanga vs Simba), Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba), Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa Sugar). Walioondolewa kwa kupata alama za chini ni Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu), Methusela Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar). Masoud Mkelemi aliyekuwa mwamuzi wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro United na Villa Squad ameondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting) na alichelewa kwa dakika tano kufika uwanjani.

MAKAMISHNA VPL/FDL WASIMAMISHWA, WAONYWA
Baadhi ya makamishna wa VPL na FDL wameondolewa na wengine kusimamishwa kusimamia mechi za ligi hizo kutokana na upungufu kwenye ripoti zao au kutowasilisha kabisa ripoti hizo TFF baada ya mechi. Kamishna Mohamed Jumbe aliyesimamia mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba ameondolewa kwenye orodha ya makamishna kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu. Makamishna wa mechi kati ya JKT Oljoro vs Yanga (Hakim Byemba), JKT Oljoro vs Kagera Sugar (Salum Kikwamba), Toto Africans vs African Lyon (Charles Komba), Coastal Union vs JKT Oljoro (Mohamed Nyange) wamesimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF. Kwa upande wa FDL makamishna waliosimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF ni wa mechi kati ya Kurugenzi vs Polisi Iringa, Morani vs Mwadui, Polisi Mara vs Pamba, Polisi Mara vs Mwadui, Morani vs JKT Kanembwa na Pamba vs Polisi Dodoma. Wengine ni Mwadui vs JKT Kanembwa, Polisi Tabora vs Morani, Polisi Dodoma vs Polisi Mara, Polisi Tabora vs Mwadui, Polisi Mara vs Morani, JKT Kanembwa vs Polisi Mara, Morani vs Rhino Rangers na Small Kids vs Mkamba Rangers. Kamati ya Ligi imewakumbusha makamishna wote kuwa ni jukumu lao kuhakikisha ripoti zao zimefika TFF na kurekebisha upungufu wa jinsi ya kuripoti matukio yanayotokea uwanjani. Licha ya kutuma nakala kwa njia ya email, wanatakiwa pia kuwasilisha ripoti halisi (original) TFF.

MECHI YA SIMBA, MTIBWA YAINGIZA MIL 62/-
Mechi namba 121 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi (Februari 24 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Mtibwa Sugar kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba imeingiza sh. 239,686,000. Watazamaji 10,669 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 14,577,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 9,467,694.92. Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 9,491 na kuingiza sh. 47,455,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 105 na kuingiza sh. 2,100,000. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,412,162.26, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,447,297.36, Kamati ya Ligi sh. 4,447,297.36, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,223,648.68 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,729,504.53.

VUMBI LA VPL KUENDELEA JUMATANO
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 27 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika viwanja tofauti. Vinara wa ligi hiyo Yanga wataikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000 (viti vya bluu na kijani), sh. 8,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 (VIP C na B) na sh. 20,000 (VIP A). Mechi nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union vs Ruvu Shooting (Mkwakwani, Tanga), Polisi Morogoro vs Mgambo Shooting (Jamhuri, Morogoro), JKT Ruvu vs Toto Africans (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar vs Tanzania Prisons (Manungu, Morogoro).

ARSENAL YATANGAZA FAIDA YA PAUNDI MILIONI 17 KATIKA KIPINDI CHA MIEZI SITA.

KLABU ya Arsenal imetangaza faida bila kutozwa ushuru kiasi cha paundi milioni 17 kwa kipindi cha miezi sita iliyoishia Novemba 30 kiasi hicho kikiwa kimepungua ukilinganisha kiasi cha paundi milioni 49 walichopata katika mwaka 2011. Katika taarifa yake iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo imesema kuwa kiasi cha paundi milioni 40.9 zilitumika kuwwasajili wachezaji Lukas Podolski, Santi Cazorla na Oliver Giroud na pia kuongeza mikataba kwa wachezaji Theo Walcott na Jack Wilshere. Mauzo ya mchezaji yalifikia kiasi cha paundi milioni 42.5 wakati mauzo ya tiketi yameshuka kutoka paundi milioni 113.5 mpaka paundi milioni 106 ikiwa ni matokeo ya kucheza michezo michache nyumbani kulinganisha na miaka iliyopita. Faida ya miezi sita ya Novemba mwaka 2011 pia ilinajumisha mauzo ya wachezaji Cesc Fabregas, Samir Nasri na Gael Clichy. Mwenyekiti wa klabu hiyo, Peter Hill-Wood amesema uwezo wao kushindana katika kiwango cha juu kwenye ligi ya nyumbani na Ulaya kunachagizwa kwa kiasi kikubwa na hali ya uchumi ambayo inaipa klabu nguvu na kujitegemea. Hata hivyo mashabiki wa Arsenal wamekuja juu baada ya timu hiyo kushindwa kunyakuwa taji lolote toka mwaka 2005 na kumtaka Wenger kutoa pesa zaidi kwa ajili ya kununua wachezaji wenye ubora kuziba pengo la Fabregas na Robin van Persie.

Friday, February 22, 2013

MUAMBA KUKABIDHI KOMBE LA LIGI.

NYOTA wa zamani wa klabu ya Bolton Wanderers, Fabrice Muamba anatarajiwa kukabidhi Kombe la Ligi kwa nahodha wa timu ambayo itashinda katika mchezo wa fainali kati ya Bradford City na Swansea City katika Uwanja wa Wembley baadae leo. Muamba atakuwa mgeni rasmi katika mchezo huo na pia atatizama mechi hiyo upande maalumu kwa ajili ya wageni mashuhuri na kutambulishwa kwa pande zote mbili kabla ya mchezo huo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alilazimika kustaafu soka kabla ya muda baada ya kuzimia uwanjani wakati akichezea klabu ya Bolton kwenye robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham Hotspurs Machi mwaka jana. Muamba ambaye alikuwa akicheza nafasi ya kiungo moyo wake ulisimama kwa dakika 78 lakini kwasababu ya matibabu aliyopatiwa uwanjani wakati akianguka alifanikiwa kuzinduka na baadae kupona kabisa.

REAL MADRID WAINGIA MKATABA NA NIVEA.

KLABU ya Real Madrid na kampuni ya Beiersdorf AG wameingia mkataba wa udhamini kwa ajili ya kuitangaza klabu na kampuni hiyo ya vipodozi inayotengeneza mafuta ya Nivea kwa ajili ya kulinda ngozi. Rais wa Madrid Florentino Perez na ofisa mkuu wa kampuni hiyo walifikia makubaliano kwa mkataba ambao utaishia katikamsimu wa mwaka 2015-2016 katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo katika Uwanja wa Santiago Bernabeu jana. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya makubaliano hayo Pereza amesema Nivea itakuwa ni mojawapo wa wadhamini wao na watakuwa pamoja katika kuhakikisha wanajimiza malengo yao pamoja na changamoto zingine zitakazojitokeza. Kampeni mpya ya matangazo ya Nivea itawashirikisha nyota kadhaa wa klabu hiyo akiwemo Sergio Ramos, Marcelo, Gonzalo Higuain na Alvaro Arbeloa.

SHABIKI WA TOTTENHAM AHADITHIA WALIPOVAMIWA NA WAHUNI HUKO LYON.

MSHABIKI wa klabu ya Tottenham Hotspurs amedai alikuwa akihofia maisha yake wakati yeye na mwanae walipovamiwa na kikundi cha wahuni jijini Lyon, Ufaransa. Paul Eccles mwenye umri wa miaka 51 alipigwa ngumi na mateke katika tukio hilo na watu wapatao 20 ambao walivamia bar iliyokuwa na mashabiki wa Tottenham waliokwenda kuishangilia timu yao katika mchezo wa Europa League. Eccles ni mmoja kati ya mashabiki watatu ambao walikimbizwa hospitalia kwa ajili ya matibabu baada ya tukio hilo. Shabiki huyo amesema lilikuwa ni jambo la kuogopesha wakati yuko amelala chini huku akipigwa alikuwa akitegemea kuchomwa mgongoni kisu muda wowote na wahuni hao. Eccles anadai kuwa pamoja na kipigo hicho hawezi kuacha kusafiri kuishangilia timu yake ambapo sasa anapanga kwenda Italia kuishangilia timu hiyo ikicheza na Inter Milan mwezi ujao kama afya yake itamruhusu.

WENGER APANIA KUVUNJA BENKI MAJIRA KIANGAZI.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amedai kuwa anaweza kutoa kitita cha paundi milioni 80 kwa ajili ya kumsajili Radamel Falcao wakati timu hiyo ikijiandaa kubadilisha mfumo wake wa matumizi. Wenger ambaye yuko katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki baada ya kikosi chake kuchapwa na Bayern Munich katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya anatarajiwa kukabidhiwa kitita kikubwa kwa ajili ya usajili katika kipindi cha majira ya kiangazi. Wenger amedai kuwa wanaweza kufikia kiasi cha paundi milioni 40 kama Atletico Madrid itakuwa kumuuza Falcao na pia wanaweza kufikia kiwango cha mshahara atakachohitaji nyota huyo wa kimataifa kutoka Colombia. Kocha huyo anadai kuwa alikuwa na kitita cha kutosha katika kipindi cha dirisha dogo la usajili la Januari lakini alishindwa kusajili baada ya kukosa aina ya mchezaji ambaye anamuhitaji.

PISTORIUS APATA DHAMANA.

MWANARIADHA mlemavu Oscar Pistorius ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji ya rafiki yake wa kike amepewa dhamana baada ya kupita siku nne za usikilizaji wa kesi hiyo. Mwanariadha huyo ambaye ni bingwa wa michuano ya paralimpiki alikana tuhuma za mauaji akidai kuwa alimpiga risasi Reeva Steenkamp akidhani kuwa alikuwa jambazi. Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea tena June 4 mwaka huu, ambapo alitozwa kiasi cha dola 74,000 kwa ajili dhamana yake huku akitakiwa kuwasilisha pasi yake ya kusafiria, kutorejea katika nyumba yake ya Pretoria na kuripoti polisi kila Jumatatu na Ijumaa. Hakimu aliyekuwa akisimamia kesi hiyo Desmond Nair alitumia muda wa saa mbili kutoa maamuzi yake lakini hakimu huyo pia alidai anapata wakati mgumu kuelewa kwanini Pistorius alivyatua risasi nyingi kiasi hicho.

SIJAFIKIRIA KUACHIA NGAZI HATA SEKUNDE MOJA - WENGER.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesema hakuna hata sekunde moja aliyofikiria kuachia kibarua cha kuinoa klabu hiyo wiki hii. Kauli hiyo imekuja kutokana na nafasi finyu waliyonayo Arsenal kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza na kufuatiwa kutolewa pia katika mzunguko wa tano wa Kombe la FA na Blackburn Rovers. Wenger amedai kuwa wanatakiwa kuwa na umoja na nguvu na kuvurugwa na watu ambao wanakuwa na mawazo hasi baada ya timu kufanya vibaya katika mchezo mmoja. Kocha huyo amekuwa akipewa wakati mgumu na mashabiki wa klabu hiyo wengi wao wakitaka aachie nafasi hiyo baada ya kushindwa kuipa taji lolote Arsenal toka mwaka 2005 wakati walipoifunga Manchester United kwa matuta kwenye Kombe la FA. Lakini wakati akiulizwa swali hilo katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mchezo wao na Aston Villa utakaochezwa kesho Wenger amesema hajafikiria kujiuzulu wadhifa wake huo hata kwa sekunde moja kwani ana mkataba mpaka mwaka 2014 ndipo hatma yake itakapojulikana.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

YANGA, AZAM ZAPIGANIA USUKANI WA LIGI
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 23 mwaka huu) kwa mechi tatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu yatakuwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Uwanja huo wa kisasa utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na makamu bingwa Azam. Ingawa Azam imecheza mechi moja zaidi, lakini timu hizo zinatofautishwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kwenye msimamo wa ligi huku kila moja ikiwa na pointi 36. Pia vinara wa ufungaji kwenye ligi kwa sasa wanatoka katika timu hizo mbili. Kipre Tchetche aliyepachika mabao tisa hadi sasa ndiye anayeongoza akifuatiwa na Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye mabao manane. Iwapo timu yoyote itafanikiwa kuondoka na pointi tatu katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam, kasi ya mbio za kuwania ubingwa itaongezeka. Waamuzi wasaidizi watakuwa Hamis Chang’walu wa Dar es Salaam na John Kanyenye kutoka Mbeya wakati mezani atakuwepo Oden Mbaga. Mechi nyingine za kesho ni Mgambo Shooting dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Jumapili (Februari 24 mwaka huu), Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa katika hekaheka nyingine kwa Simba chini ya Mfaransa Patrick Liewig kuikabili Mtibwa Sugar inayonolewa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime.

FDL YAENDELEA KUSHIKA KASI
Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea wikiendi hii kwa mechi kumi na moja katika viwanja tofauti. Timu hizo zinapambana kutafuta hadhi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao 2013/2014. Kesho (Februari 23 mwaka huu) kundi A litakuwa na mechi moja itakayozikutanisha timu za Mkamba Rangers na JKT Mlale itakayochezwa Uwanja wa Ruaha mkoani Morogoro. Kundi B lenyewe litakuwa na mechi mbili; Tessema itacheza na Ashanti United katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam wakati Ndanda itaikaribisha Polisi Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara. Raundi ya 12 ya ligi hiyo kundi A itashuhudia timu zote nane zikiwa viwanjani; Pamba vs Mwadui (CCM Kirumba), Polisi Tabora vs Polisi Mara (Ali Hassan Mwinyi), Polisi Dodoma vs Morani (Jamhuri) na JKT Kanembwa vs Rhino Rangers (Lake Tanganyika). Jumapili (Februari 24 mwaka huu) kundi A litakuwa na mechi kati ya Burkina Faso dhidi ya Kurugenzi (Jamhuri), Majimaji vs Polisi Iringa (Majimaji) wakati kundi B ni Transit Camp vs Villa Squad (Karume), na Green Warriors vs Moro United (Mlandizi).

FIFA KUSIKILIZA MADAI YA ASAMOAH DHIDI YA YANGA
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limesema linapeleka rasmi madai ya mchezaji wa zamani wa Yanga, Kenneth Asamoah kwenye chombo chake cha utatuzi wa migogoro (Dispute Resolution Chamber) baada ya klabu hiyo kutojibu chochote. Awali FIFA ilipokea malalamiko ya Asamoah kuwa anaidai Yanga dola 5,000 za Marekani ambapo ilikuwa ni sehemu ya malipo yake (signing fee) baada ya kujiunga na klabu hiyo. Desemba mwaka jana FIFA iliiandikia barua Yanga kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikitaka maelezo yake kuhusu madai hayo ya Asamoah, lakini hadi sasa haijajibu madai hayo. Kwa mujibu wa FIFA, hatua ya uchunguzi wa suala hilo umekamilika, na sasa linapelekwa rasmi katika chombo chake cha utatuzi wa migogoro (Dispute Resolution Chamber) kwa ajili ya kufanya uamuzi.

CASILLAS KUREJEA BAADA YA WIKI NNE.

GOLIKIPA wa kimataifa wa Hispania na klabu ya Real Madrid, Iker Casillas amesema anatarajia kurejea tena uwanjani baada ya wiki nne zijazo. Casillas alivunjika kidole gumba katika mchezo wa Kombe la Mfalme dhidi ya Valencia Januari mwaka huu na baadae kufanyiwa upasuaji ili kurekebisha tatizo hilo. Upasuaji huo umepelekea nahodha huyo wa Madrid kuwekewa skrubu mbili katika kidole gumba chake zoe zilikiwa na urefu wa milimita 17 na upana wa milimita mbili. Casillas amesema anategemea kurejea uwanjani baada ya mwezi mmoja baada ya madaktari kumhakikishia hivyo na tayari ameanza kufanya mazoezi mepesi na anaweza kuchezesha kidole chae kilichofanyiwa upasuaji. Hatahivyo, Casillas atatakiwa kupigania nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza baada ya kupona kidole chake baada ya Jose Mourinho kumuengua katika kikosi chake kutokana na majeruhi huku kukiwa na ujio wa golikipa mpya Diego Lopez kutoka Sevilla.

SERIKALI IKO NUMA YENU - NAMWAMBA.

Ababu Namwamba.
WAZIRI wa Vijana na Michezo nchini Kenya, Ababu Namwamba amelihakikishia Shirikisho la Soka la nchi hiyo-FKF kwamba serikali inawaunga mkono katika jitihada zao za kuomba kuandaa michuano ya Afrika kwa vijana itakayofanyika 2017 pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika-Afcon yatakayofanyika mwaka 2019. Akizungumza wakati wa sherehe za kumtambulisha kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo maarufu kama Harambee Stars, Adel Amrouche waziri huyo amesema kuwa alimueleza rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF Issa Hayatou ni ya Kenya kutaka kuandaa michuano inayokuja walipokutana jijini Kampala. Namwamba aliendelea kudai kuwa mojawapo ya sheria za CAF ili nchi ipewe uenyeji wa kuandaa Afcon lazima iwe kwanza imeandaa mojawapo ya michuano ya vijana na wao wanataka kuanzia kwa kuandaa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17. Kenya inakabiliwa na changamoto nyingi haswa suala la miundo mbinu lakini waziri huyo alidai kuwa tayari wameshazungumza na nchi marafiki kama Qatar na China ambao wako tayari kuwasaidia kama wakipata nafasi ya kuandaa michuano hiyo.

HATUKUCHEZA VIBAYA SANA - XAVI.

KIUNGO nyota wa klabu ya Barcelona, Xavi Hernandez amekataa kuwa kipigo cha mabao 2-0 walichokipata kutoka kwa AC Milan Jumatano iliyopita kilitokana na kucheza kwa kiwango kibovu kabisa toka msimu umeanza. Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania ni mchezaji pekee wa Barcelona aliyemudu kupiga shuti lililokwenda langoni mwa wapinzani katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa San Siro lakini bado anajiamini kuwa kikosi hicho kinaweza kumudu kutotolewa katika hatua ya timu 16 bora kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Xavi anakiri kuwa hawakucheza vizuri katika mchezo huo kwasababu hawakutumia vyema nafasi za upande wa pembani zilizokuwepo na pia kushindwa kujaribu mashuti ya mbali lakini anadhani wanaweza kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza na kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo wao marudiano. Maandalizi ya Barcelona katika mchezo wao wa ligi dhidi ya Sevilla mwishoni mwa wiki hii yanaonekana kuwa magumu zaidi kwa ukweli kwamba wanakabiliwa na mchezo wa marudiano ya Kombe la Mfalme dhidi ya Real Madrid Jumanne inayokuja.

CORINTHIANS HAIPASWI KULAUMIWA - RAIS.

RAIS wa klabu ya Corinthians ya Brazil, amesema kuwa kifo cha kijana wa miaka 14 kilichotokea wakati wa mchezo wao waliocheza nchini Bolivia kilikuwa ni bahati mbaya hivyo timu na mashabiki wake sio wakulaumiwa kutokana na tukio hilo. Kijana huyo Kevin Beltran raia wa Bolivia alifariki baada ya kupigwa na fataki usoni lililokuwa limerushwa na mmoja wa mashabiki wa Corinthians wakati wa mchezo wao wa Copa Libertadores uliochezwa Jumatano na kupelekea mashabiki 12 wa timu hiyo kukamatwa jijini Oruro. Rais wa klabu hiyo Mario Gobbi amesema kuwa hadhani kama Corinthians au mashabiki wake wanapaswa kulaumiwa kutokana na tukio hilo ambalo Shirikisho la Soka la Amerika Kusini limedai kuwa litafanyia uchunguzi. 
Waziri wa Michezo wa Brazil, Aldo Rebelo alitoa taarifa akiwa kuwa fujo za mashabiki hao hazikubaliki na kutaka mamlaka husika kuwapa adhabu wale wote waliohusika na vurugu hizo. Thursday, February 21, 2013

MASHABIKI TOTTENHAM WASHAMBULIWA UFARANSA.

MASHABIKI wa klabu ya Tottenham Hotspurs wameshambuliwa katika bar huko jijini Lyon nchini Ufaransa kabla ya mchezo wao wa Europa League dhidi ya Olympique Lyon utakaochezwa baadae leo. Mashabiki watatu walikimbizwa hospitali baada ya kundi la watu kuvamia na kuvunja madirisha ya vioo katika bar hiyo ambapo mashabiki wengine wakiumizwa na vioo vilivyokuwa vikiruka. Ofisa wa mambo ya nje alithibitisha kuwa wanalifanyia uchunguzi tukio ambalo limetokea saa 24 kabla ya mtanange baina ya timu hizo katika hatua ya timu 32 bora kwenye michuano hiyo. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Uingereza katika Uwanja wa White Hart Lane Alhamisi iliyopita Tottenham walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. 

DEL PIERO AONGEZA MKATABA SYDNEY.

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa kimataifa wa Italia na klabu ya Juventus, Alessandro Del Piero amesaini mkataba mwingine wa msimu mmoja katika klabu ya Sydney FC inayoshiriki Ligi Kuu nchini Australia maarufu kama A-League. Del Piero mwenye umri wa miaka 38 alitangaza uamuzi wake huo leo kabla ya muda wa klabu hiyo kufanya mkutano wa waandishi habari. Nyota huyo ambaye alijunga na Sydney msimu wa 2012-2013 ameshafunga mabao 11 katika mechi 18 za A-League alizocheza na tayari ameshaweka rekodi katika klabu hiyo kwa kufunga mabao mengi zaidi katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo. Mwenyekiti wa Sydney Scott Barlow amesifu wazo la kumsajili nyota huyo kwamba lilikuwa sahihi kwani hajawaangusha na amekuwa akionyesha kiwango bora zaidi kadri siku zinavyozidi kusonga mbele.

WAKALA WA NEYMAR AMSHAMBULIA PELE.

WAKALA wa mshambuliaji nyota wa Brazil Neymar amesema kuwa shutuma za hivi karibuni alizotoa nguli wa soka wa nchi hiyo Pele kwa nyota huyo zinatokana na wivu. Wakala huyo alidai kuwa Pele angekuwa mchezaji dhaifu katika kikosi cha nyota wa Brazil kama angekuwa anacheza kipindi hiki baada ya nguli huyo ambaye amenyakuwa Kombe la Dunia mara tatu akiwa na kikosi cha nchi hiyo, kuponda kiwango cha Neymar kwenye timu ya taifa. Wakala wa nyota huyo aliendelea kurusha makombora kwa Pele akidai kuwa kama nguli huyo angekuwa akicheza katika miaka ya hivi sasa asingeweza kumfikia kiwango cha Neymar kwasababu mabeki kipindi hicho walikuwa wanacheza taratibu tofauti na hivi sasa. Ni mwaka mmoja uliopita ambapo Pele mwenye umri wamiaka 72 alimsifia nyota huyo kwamba ni moja wa wachezaji bora kabisa duniani lakini heshima hiyo inaonekana kutetereka kati ya wawili hao baada ya shutuma alizotoa pele karibuni.

BODI KUMHAKIKISHIA WENGER NAFASI YAKE.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anatarajiwa kuhakikishiwa nafasi yake katika kikao cha bodi kitakachokutana pamoja na mmiliki wa klabu hiyo Stan Kroenke baadae leo. Klabu hiyo ilithibitisha katika mtandao wake kuwa Wenger atakutana na Kroenke ambaye aliwasili jijini London kuangalia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao Arsenal ilichapwa kwa mabao 3-1 na Bayern Munich, baada ya muda wa mazoezi. Arsenal sasa inapigana ili isipate aibu nyingine ya kufungwa huko jijini Munich katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Machi 13 na kuhakikisha inamaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza. Wenger anakabiliwa na kibarua kingine kigumu Jumamosi wakati timu hiyo itakapoikaribisha Aston Villa katika mchezo wa ligi huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo wanaomtaka aondoke baada ya kukosa vikombe kwa kipindi cha miaka nane.

Wednesday, February 20, 2013

AC Milan vs Barcelona 2-0 2013 All Goals & Highlights (20/02/2013)

Full HD galatasaray vs schalke 04 1-1 goals 20/02/2013

BFT YAANDAA KOZI MAALUMU YA MAKOCHA WA NGUMI.

Shirikisho la ngumi za ridhaa Tanzania BFT katika kutekeleza majukumu yake ya kuendeleza mchezo wa ngumi kwa vitendo limeandaa kozi maalum ya awali kwa makocha wote waliokuwa wanafundisha mchezo wa ngumi bila ya kuwa na vyeti au mafunzo ya kuwawezesha kufundisha kwa misingi ya kitaaluma. Kozi hiyo ilianza tarehe 4/2/2013 mara tu baada ya kumalizika kwa mashindano ya klabu bingwa ya Taifa. Kozi hiyo inahudhuriwa na jumla ya makocha 14 ambao wanaendelea vizuri na mafunzo na leo tarehe 19/2/2013 wamefikia hatua ya mtihani watakayoendelea nayo hadi kesho. Kwa ujumla kozi hiyo ilikuwa ya nadharia na vitendo katika nadharia wamefundishwa namna ya kuwatambua wanafunzi wenye vipaji, mbinu na ujanja wa kucheza, namna ya kupanga ratiba za mazoezi,namna ya kupata pointi kwa kutumia komputa, vyakula vinavyofaa kwa wachezaji, upangaji wa ratiba za mashindano na huduma ya kwanza .Katika vitendo wamefundishwa kupigisha pad, kupiga bagi la mazoezi, namna yakuanzisha, kuendeleza na kumaliza  mazoezi kwa siku, namna ya kucheza ngumi na mengine mengi. Kozi hiyo imefundishwa na wakufunzi wa BFT waliopata mafunzo katika vyuo mbalimbali vya kimataifa major mstaafu Michael Changarawe na Mohamed Kasilamatwi. Kozi hiyo inatazamiwa kufungwa Alhamisi ya tarehe 21/2/2013 saa 3.00 asubuhi. Mgulani JKT katika bwalo la maofisa Mgeni rasmi wa kufunga kozi hiyo tunategemea kuwa ni mkuu wa kikosi cha Mgulani Major Charles Mbuge. Kwa taarifa hii tunaviomba vyombo vyote vya habari kuhudhuria katika tukio hilo kwa maendeleo ya ndondi Tanzania.

WENGER HAPASWI KULAUMIWA - WILSHERE.

KIUNGO wa klabu ya Arsenal, Jack Wilshere amesema nafasi ya kocha wa klabu hiyo Arsene Wenger haipaswi kuhojiwa na wachezaji wa timu hiyo wanapaswa kuwajibika kwa matokeo mabaya. Matumaini ya Arsenal kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yamekuwa finyu baada ya kukubali kipigo nyumbani cha mabao 3-1 kutoka kwa Bayern Munich ya Ujerumani. Jumamosi iliyopita Arsenal ilipata pigo lingine baada ya kubanduliwa katika Kombe la FA kwa kufungwa bao 1-0 na Blackburn Rovers. Wilshere amesema Wenger ameifundisha klabu hiyo kwa miaka 16 na amekuwa akifanya kazi nzuri hivyo hauwezi kuhoji kuhusu uwezo wake. Arsenal kwasasa inashika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza wakiwa nyuma ya Tottenham Hotspurs kwa alama nne hivyo wana kibarua kingine cha kuhakikisha wanamaliza katika nafasi nne za juu ili waweze kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

MOURINHO NI MKALI ZAIDI - DEL BOSQUE.

KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente Del Bosque ameweka wazi ufananisho kati yake na kocha wa klabu ya Reala Madrid, Jose Mourinho na kudai kuwa mreno huyo huwa anakuwa mkali zaidi wakati akifundisha. Del Bosque ambaye ameiwezesha nchi hiyo kunyakuwa Kombe la Dunia 2010 pamoja na kutetea taji lao la Ulaya mwaka jana anadai huwa anakuwa mtulivu zaidi wakati akifundisha kuliko mwenzake Mourinho. Madrid ambao ni mabingwa watetezi wa La Liga kwasasa wapo katika nafasi ya tatu mwa msimamo wa ligi hiyo wakipishana kwa alama 16 na mahasimu wao Barcelona ambao wameshikilia usukani kitu ambacho watu wameanza kuhoji juu ya ufundishaji wa kocha huyo. Del Bosque mwenye umri wa miaka 62 aliendelea kudai kuwa kuna vitu vingi vya kuangalia kama sifa na utashi wa mtu ndio maana anajiona mtulivu zaidi ya Mourinho.

PARALIMPIKI ITAENDELEA NA HARAKATI ZAKE - CRAVEN.

RAIS wa Kamati ya Kimataifa ya Paralimpiki, Sir Philip Craven amesema kuwa michezo ya watu wenye ulemavu itaendelea kama kawaida baada ya mshituko wa kukamatwa kwa Oscar Pistorius kutokana na kesi ya mauaji. Pistorius mwenye umri wa miaka 26 ambaye ni bingwa mara mbili wa michuano ya paralimpiki alikana shitaka la kumuua kwa kukusudia mpenzi wake Reeva Steenkamp katika nyumba yake nchini Afrika Kusini. Craven aliiambia BBC kuwa tukio hilo litakwisha baada ya muda na wataendelea na harakati zao za kuitangaza paralimpiki na kuwashawishi wanariadha zaidi waweze kushiriki. Waendesha mashitaka wanamtuhumu Pistorius kwa kumuua Steenkamp mwenye umri wa miaka 29 kwa makusudi ingawa mwanariadha huyo aliiambia mahakama hiyo kupitia wakili wake kuwa hakudhamiria kumuua mpenzi wake kwenye tukio hilo.

MARADONA ATAMANI MWANAE ACHEZE ARGENTINA.

NGULI wa soka wa zamani wa kimataifa kutoka Argentina ameelezea ndoto zake za kumuona mwanae wa kiume aliyezaliwa karibuni Diego Fernando akiichezea nchi hiyo sambamba na watoto wa Lionel Messi na Sergio Aguero. Mpenzi wa zamani wa Maradona Victoria Ojeda alijifungua mtoto huyo mwishoni mwa wiki iliyopita huko jijini Buenos Aires wakati mtoto wa Messi aitwaye Thiago amefikisha miezi mitatu na nusu huku mtoto wa Aguero aitwaye Benjamin ametimiza miaka minne. Maradona aliiambia radio moja nchini Dubai kwamba ana ndoto kuona watoto hao wakiichezea Argentina siku huku akifafanua kuwa anadhani mtoto wa Messi atakuwa katika nafasi ya kiungo akiwalisha mipira Benjamini pamoja na Diego Fernando watakaokuwa wakicheza katika safu ya ushambuliaji. Maradona ambaye ni babu wa Benjamini Aguero amesema mapema wakati majukumu yake ya kibiashara yatakapomalizika atasafiri kwenda Argentina kumuona mwanae huyo aliyezaliwa. Nyota huyo ambaye ana mkataba jijini Dubai pia ana watoto wawili wa kike Dalma na Giannina ambao alizaa na mke wake wa zamani Claudia Villafane.

TEKNOLOGIA YA KOMPYUTA KUTUMIKA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limethibitisha kuwa mfumo wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli unatarajiwa kutumika katika michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Brazil 2014. Mfumo huo ulitumika kwa mafanikio katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia iliyofanyika Desemba mwaka jana na pia itatumika katika michuano ya Kombe la Shirikisho itakayofanyika Juni mwaka huu. Rais wa FIFA mara kwa mara amekuwa akipigia debe mfumo huo toka alipoona bao halali alilofunga kiungo wa Uingereza Frank Lampard likikataliwa na kupelekea nchi hiyo kufungwa na Ujerumani katika michuano ya Kombe la Dunia 2010. FIFA katika mkutano wake wa mwaka jana ilipitisha mifumo miwili ya Goalref na Hawkeye ambayo yote kwa pamoja ilitumika katika michuano ya klabu bingwa ya dunia.

Tuesday, February 19, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

FIFA YASITISHA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF
SHIRIKISHO la Kimaifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeahirisha uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mkanganyiko uliojitokeza katika mchakato wa uchaguzi huo. Akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za TFF jijini Dar es Salaam leo mchana (Februari 19 mwaka huu), Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema FIFA imetuma barua ikiagiza mchakato wa uchaguzi usimame baada ya kupata malalamiko. Amesema kutokana na mkanganyiko huo, FIFA katika barua yake ya leo (Februari 19 mwaka huu- imeambatanishwa) imeagiza mkutano wa uchaguzi wa TFF ambao awali ulipangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu uahirishwe hadi hapo itakapotuma ujumbe wake nchini. Ujumbe huo wa FIFA unatarajiwa kufika nchini katikati ya mwezi ujao (Machi) ambapo utafanya tathimini ya hali hivyo, kutuma ripoti yake katika shirikisho hilo na baadaye kutoa mwongozo wa nini kifanyike. Rais Tenga amewaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na uamuzi huo wa FIFA, hivyo kwa sasa hakutakuwa tena na mkutano huo mpaka hapo watakapopewa taarifa nyingi. Amesema TFF inakaribisha kwa mikono miwili uamuzi huo wa FIFA kwa sababu ni chombo ambacho cha juu kimpira duniani, na hatua hiyo ina lengo la kuhakikisha kuwa kila mhusika katika mchakato huo wa uchaguzi anapata haki yake. “Nia yetu ni kuona watu wanatendewa haki, na nia ya FIFA ni kutafuta ukweli. Hivyo wahusika (waathirika) wajiandae, watumie wakati huu kuandaa hoja zao ili FIFA wakifika wawasikilize, wapate maelezo ya kina kuhusu utaratibu na malalamiko yaliyotolewa,” alisema Tenga. Rais Tenga amesema timu hiyo ya FIFA itakapofika yenyewe ndiyo itakayopanga izungumze na nani kwa wakati gani, hivyo ni vizuri waathirika na vyombo vyote vilivyohusika na mchakato wa uchaguzi wakajiandaa. Amesema ilikuwa ni muhimu suala hili likatatuliwa katika ngazi ya FIFA kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi utakapofanyika TFF inaendelea kuwa chombo kimoja badala ya kurudi katika migogoro iliyokuwepo huko nyuma. “Nataka tubakie kama tulivyokuwa. Malumbano yaishe. Pangeni hoja, wakija hao waheshimiwa (FIFA) muwaambie. FIFA ni chombo cha juu, nafurahi wamekubali kuingia katika hili, kwani wana shughuli nyingi wangeweza kukataa,” amesema.Kuhusu fursa ya kufanya marejeo (review) kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inayoongozwa na Idd Mtiginjola ambayo aliielezea Jumamosi, Rais Tenga amesema kwa vile hicho ndicho chombo cha mwisho nchini katika masuala ya uchaguzi alishauriwa kuwa kingeweza kufanya review. “Kwa vile hakuna chombo kingine, nikashauriwa kuwa kinaweza kufanya review. Katika utaratibu wa kutoa haki, uamuzi ni lazima uwe wa wazi kwa kutoa sababu. Nilidhani hilo linawezekana, kwani Mahakama Kuu hufanya hivyo. Kwa hili uamuzi wa Mtiginjola ni sahihi,” amesema Rais Tenga. Kamati ya Mtiginjola iliyokutana jana (Februari 18 mwaka huu) ilitupa maombi ya review yaliyowasilishwa mbele yake na waombaji uongozi watano kwa vile hakuna kipengele chochote kwenye Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi kinachotoa fursa hiyo. Waombaji hao walikuwa Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board). Wengine ni walioomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye mabano; Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu).

NI KIBARUA PRISONS, SIMBA JIJINI MBEYA
BAADA ya sare mbili mfululizo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Simba kesho (Februari 20 mwaka huu) wanashuka Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya wakiwa wageni wa Tanzania Prisons. Katika mechi zake mbili zilizopita, Simba iliondoka pointi mbili tu kati ya sita ilizokuwa ikizipigania. Ilitoka sare na timu za JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na baadaye sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Oljoro JKT. Hiyo itakuwa mechi ya nne kwa Mfaransa Patrick Liewig tangu aanze kuinoa Simba huku akifanikiwa kuondoka na ushindi katika mechi moja dhidi ya African Lyon inayokamata mkia kwenye ligi hiyo. Simba iliilaza Lyon mabao 3-1. Kwa upande wa kocha Jumanne Chale anashusha kikosi chake uwanjani kesho akiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya African Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja huo huo Februari 9 mwaka huu. Hekaheka nyingine itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 25,000 utakapokuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans na African Lyon. Wakati Lyon ikikamata mkia, Toto Africans yenye pointi 14 inashika nafasi ya 12 katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 14. Mwamuzi Simon Mberwa wa Pwani atakuwa shuhuda wa mechi kati ya Coastal Union ya Tanga na Oljoro JKT ya Arusha itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na uimara wa timu zote mbili. Nayo JKT Ruvu ambayo haijafanya vizuri msimu huu kulinganisha na minne iliyopita itacheza Azam kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam. JKT Ruvu chini ya kocha Charles Kilinda inakamata nafasi ya nne kutoka chini ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi 15. Iwapo itafanikiwa kushinda mechi hiyo, Azam itaendelea kujiimarisha katika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga. Azam ambayo ni moja ya timu zenye safu kali ya ushambuliaji katika ligi hiyo ikiwa imefunga mabao 27 ina pointi 33.

PISTORIUS AKIRI KUMPIGA RISASI MPENZIWE.

MWANARIADHA mlemavu Oscar Pistorius ametoa maelezo ya kuogofya kuhusu usiku aliompiga risasi rafiki yake wa kike na kumuua akidai kuwa alidhani ni mwizi wakati alipoamka katikati ya usiku wa manane. Katika taarifa iliyosomwa mbele ya mahakimu wa mahakama ya jijini Pretoria, mwanariadha huyo alidai kuwa alikuwa upande wa juu wa nyumba yake wakati aliposikia kelele kutoka bafuni. Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa Pistorius akiamini kuwa mpenzi wake Reeva Steenkamp bado yuko kitandani kalala alichukua bastola yake na kupiga kelele kutoa onyo kabla ya kufyatua risasi nne kupitia mlangoni. Baada ya kufyatua risasi ndipo Pistorius anadai aligundua Steenkamp hakuwepo kitandani ikabidi akavunje mlango wa bafu hilo na kujaribu kumsaidia lakini alifia kwenye mikono yake. Pistorius ataendelea kubakia rumande mpaka kesi hiyo itakapoendelea tena leo baada ya mahakimu kuisimamisha kutokana na mtuhumiwa kushindwa kuwa katika hali yake ya kawaida.

Monday, February 18, 2013

WAFANYAKAZI MARICANA WATISHIA KUGOMA TENA.

WAFANYAKAZI wanaofanya shughuli za ujenzi katika Uwanja wa Maracana nchini Brazil wametishia kugoma na kuwapa changamoto mpya waandaaji wa Kombe la Dunia ambao wanakimbizana na muda ili kumaliza uwanja huo kwa wakati. Wafanyakazi hao ambao wanadai nyongeza ya mshahara, vocha za chakula na bima binafsi ya afya kwa familia zao walisimama kufanya kazi kwa siku moja na kutishia kugoma kabisa kuanzia wiki ijayo. Uwanja huo maarufu ambao ulitumika katika baadhi mechi kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1950, unafanyiwa ukarabati kwa ajili ya kutumika katika michuano ya Kombe la Shirikisho na Kombe la Dunia mwakani ambapo utatumia kiasi cha dola milioni 458. Uwanja huo ulipangwa kufunguliwa rasmi katika mchezowa kimataifa wa kirafiki kati ya Brazil na Uingereza June 2 mwaka huu na kuandaa mchezo wa kwanza wa ushindani kati ya Mexico na Italy June 16 kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho. Ujenzi wa uwanja huo tayari umevuka muda wake ambapo ulitakiwa kuisha Desemba mwaka jana na sasa wameamua kufanya kazi bila kupumzika huku wafanyakazi wakipishana mara tatu kwa siku ili wamalize kabla ya tarehe ya mwisho ambayo ni April 15.

TUKIKUBALI KUFUNGWA SAN SIRO TUMENG'OKA - BOJAN.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Barcelona, Bojan Krkic anaamini kuwa kufungwa kwa klabu yake ya sasa ya AC Milan katika mchezo wa kwanza wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutakuwa kumefifisha matumaini yao ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo. Nyota huyo alielezea umuhimu wa Milan kuepuka kufungwa katika mchezo wa kesho usiku ambao wataikaribisha Barcelona katika uwanja wao wa nyumbani wa San Siro. Bojan amesema watakuwa wakicheza na timu bora duniani lakini wanashukuru kwakuwa wenyewe watakuwa na mashabiki watakaokuwa nyuma yao ambapo wanachotakiwa kufanya ni kupata angalau sare ili kuweka matumaini yao hai kwa mchezo wa marudiano. Bajan mwenye umri wa miaka 22 aliondoka Barcelona mwaka 2011 na kubainisha kuwa bado anawasiliana na wachezaji wenzake wa zamani ambao walimsaidia kwa namna moja au nyingine kufikia hapo alipo.

CITY WAANZA MBIO ZA KUMGOMBEA NEYMAR.

KLABU ya Manchester City yenye nguvu kubwa kifedha katika Ligi Kuu nchini Uingereza wamepiga hatua yao ya kwanza katika mbio za kumuwania mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Brazil, Neymar. Maofisa wa ngazi za juu wa klabu hiyo Ferran Soriano na Txiki Begiristain wametajwa kuanza mazungumzo ya awali na familia pamoja na mwakilishi wa nyota huyo katika Uwanja wa Wembley wakati wa mchezo wa kirafiki kati ya Uingereza na Brazil uliochezwa Februari 6 mwaka huu. Ofisa Mkuu Soriano na Begiristain ambaye ni mkurugenzi wa soka wa klabu hiyo walikuwa wageni waalikwa wa Chama cha Soka cha Uingereza-FA katika mchezo huo. Katika mchezo huo ambao Neymar hakung’ara sana baada ya Uingereza kushinda kwa mabao 2-1 maofisa hao walionekana wakijongea karibu na mahali familia ya Neymar ilipokuwa imekaa huku mara kwa mara wakiwa katika mazungumzo na baba wa nyota huyo.

MTANIKUMBUKA NIKIONDOKA - WENGER

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amewaonya mashabiki wa klabu hiyo wanaomponda kwamba watamkumbuka wakati akiwa ameondoka. Akizungumza kabla ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich Wenger alitetea rekodi yake toka aanze kuinoa klabu hiyo na kuwahakikishia kuwa lazima watamkumbuka wakati ataoondoka. Wenger alidai kuwa amekuwa akifundisha soka kwa kipindi cha miaka 30 na miaka 16 kati ya hiyo amefanya kazi Uingereza hivyo anastahili heshima kutokana na mafanikio mengi ambayo ameipa Arsenal katika kipindi chote. Katika kipindi cha karibuni Wenger amekataa kazi ya Kuzinoa timu za taifa za Uingereza, Ufaransa pamoja na klabu za Bayern Munich, Real Madrid na Paris Saint-Germain ambazo zote zilikuwa zikimuwania kutaka huduma yake. Baadhi ya mashabiki wa Arsenal wameonyesha kuishiwa na imani na kocha huyo baada ya miaka nane kupita bila ya kushinda taji lolote huku mara ya mwisho kufanya hivyo ikiwa ni mwaka 2005 waliponyakuwa Kombe la FA.

Sunday, February 17, 2013

ALVES ASIFU KIWANGO CHA MESSI.

BEKI wa klabu ya Barcelona, Dani Alves amesifu kiwango cha mshabuliaji nyota wa klabu hyo Lionel Messi kwa kudai kuwa hufanya kazi yao kuwa rahisi pindi awapo uwanjani. Alves alijiunga katika orodha ya watu wengi waliosifia kiwango cha nyota huyo wa kimataifa wa Argentina baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-1 waliopata ugenini dhidi ya Granada. Messi alifunga bao lake la 300 na 301 kwa klabu hiyo baada ya kuwa nyuma kwa bao lililofungwa katika kipindi cha kwanza na kufanikiwa kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga. Alves amesema kucheza na Messi kwenye timu moja kunafanya mambo yawe rahisi zaidi kutokana na kiwango cha hali ya juu alichonacho nyota huyo hivyo kufanya matokeo kuwa mazuri baada ya dakika 90. Messi amefikisha mabao 37 katika ligi msimu huu huku wakitofautiana kwa alama 15 na Atletico Madrid ambao wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo. 

VILANOVA YUKO KATIKA HALI NZURI - ZUBIZARRETA.

MKURUGENZI wa Michezo wa klabu ya Barcelona, Andoni Zubizarreta amesema kuwa meneja wa klabu hiyo Tito Vilanova yuko katika hali nzuri toka lianza matibabu yake huko jijini New York, Marekani. Zubizarreta alibainisha kuwa matibabu ya mionzi ili kutibu kansa ya koo inayomkabili Vilanova yanaendelea vyema na hivi karibuni anaweza kurejea kuendelea na kibarua chake kama kawaida. Vilanova mwenye umri wa miaka 44 alichukua kibarua cha kukinoa kikosi cha Barcelona katika kipindi ca majira ya kiangazi lakini kabla ya nusu ya msimu aligundulika kuwa na kansa ya tezi ambayo hivi anapatiwa matibabu yake huko New York. Zubizarreta amesema kocha huyo kwasasa amerejea katika hali yake ya kawaida baada ya mionzi huku akitizama soka katika luninga kila Barcelona inapokuwa uwanjani na anashukuru watu wote wanaomuombe katika kipindi hiki kigumu.

SABC YAJITETEA KUONYESHA KIPINDI CHA STEENKAMP.

TELEVISHENI ya SABC ya nchini Afrika Kusini imetetea uamuzi wake wa kuonyesha kipindi kilichorekodia na Reeva Steenkamp, rafiki wa kike wa mwanariadha mlemavu Oscar Pistorius ambaye anatuhumiwa kumuua mwanadada huyo. Muandaaji wa kipindi hicho, Samantha Moon aliliambia shirika la habari a BBC kuwa uamuzi wa kuonyesha kipindi hicho ulikuja baada ya kushauriana na familia ya mwanadada huyo ambaye aliwahi kuwa mwanamitindo. Kipindi hicho kiitwacho Tropika Island Treasure kilirekodiwa nchini Jamaica ambapo watu kadhaa hushindanishwa kugombea zawadi ya dola 113,500. Kwa upande mwingine mjomba wa Pistorius amesema jana kuwa mwanariadha huyo ambaye aliweka historia mwaka jana kwa kushiriki katika olimpiki ya watu wa kawaida pamoja na ile ya walemavu bado yuko katika mshituko na masikitiko makubwa kutokana na tukio hilo.

KENYA YAJIPANGA KUOMBA KUANDAA AFCON 2019.

KENYA inajipanga kuwa nchi ya tatu kwa upande wa Afrika Mashariki baada ya Sudan na Ethiopia kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2019. Shirikisho la Soka la Kenya-FKF limedokeza kuwa watatumia michuano ya Afrika ya Vijana watakayoandaa mwaka 2017 kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa kabisa barani humu. Katika taarifa iliyotolewa na shirikisho hilo ilidai kuwa FKF kwa kushirikiana na Wizara ya Vijana na Michezo nchini humo wanajipanga ili kutuma maombi ya kuandaa michuano ya Afcon 2019 pamoja na ile ya vijana itakayofanyika mwaka 2017. Taarifa hiyo ilidai kuwa serikali kwa kupitia wizara hiyo tayari imetoa ruhusa kwa FKF kuomba kuandaa michuano hiyo na sasa wanakabiliwa na upinzani kwa Algeria, Nigeria, Liberia, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC ambao nao wote wameomba kuandaa michuano ya kipindi hicho.