Wednesday, February 20, 2013

BFT YAANDAA KOZI MAALUMU YA MAKOCHA WA NGUMI.

Shirikisho la ngumi za ridhaa Tanzania BFT katika kutekeleza majukumu yake ya kuendeleza mchezo wa ngumi kwa vitendo limeandaa kozi maalum ya awali kwa makocha wote waliokuwa wanafundisha mchezo wa ngumi bila ya kuwa na vyeti au mafunzo ya kuwawezesha kufundisha kwa misingi ya kitaaluma. Kozi hiyo ilianza tarehe 4/2/2013 mara tu baada ya kumalizika kwa mashindano ya klabu bingwa ya Taifa. Kozi hiyo inahudhuriwa na jumla ya makocha 14 ambao wanaendelea vizuri na mafunzo na leo tarehe 19/2/2013 wamefikia hatua ya mtihani watakayoendelea nayo hadi kesho. Kwa ujumla kozi hiyo ilikuwa ya nadharia na vitendo katika nadharia wamefundishwa namna ya kuwatambua wanafunzi wenye vipaji, mbinu na ujanja wa kucheza, namna ya kupanga ratiba za mazoezi,namna ya kupata pointi kwa kutumia komputa, vyakula vinavyofaa kwa wachezaji, upangaji wa ratiba za mashindano na huduma ya kwanza .Katika vitendo wamefundishwa kupigisha pad, kupiga bagi la mazoezi, namna yakuanzisha, kuendeleza na kumaliza  mazoezi kwa siku, namna ya kucheza ngumi na mengine mengi. Kozi hiyo imefundishwa na wakufunzi wa BFT waliopata mafunzo katika vyuo mbalimbali vya kimataifa major mstaafu Michael Changarawe na Mohamed Kasilamatwi. Kozi hiyo inatazamiwa kufungwa Alhamisi ya tarehe 21/2/2013 saa 3.00 asubuhi. Mgulani JKT katika bwalo la maofisa Mgeni rasmi wa kufunga kozi hiyo tunategemea kuwa ni mkuu wa kikosi cha Mgulani Major Charles Mbuge. Kwa taarifa hii tunaviomba vyombo vyote vya habari kuhudhuria katika tukio hilo kwa maendeleo ya ndondi Tanzania.

No comments:

Post a Comment