Monday, October 31, 2016

PEPE KUKAA NJE YA UWANJA WIKI NNE.

BEKI wa Real Madrid, Pepe anaweza kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha mwezi mmoja baada ya kupata majeruhi ya msuli. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno alipata majeruhi na kutolewa nje katika kipindi cha kwanza cha mchezo ambao Madrid walishinda mabao 4-1 dhidi ya Alaves Jumamosi iliyopita. Taarifa kutoka katika mtandao wa klabu hiyo zinadai kuwa baada ya kufanyiwa vipimo zaidi leo, imegundulika kuwa Pepe anaweza kukaa nje kwa muda wa wiki tatu mpaka nne. Pepe mwenye umri wa miaka 33 sasa anatarajiwa kukosa mechi sita ukiwemo mchezo dhidi ya mahasimu wao Atletico Madrid utakaofanyika Novemba 19 mwaka huu.


ROBBEN KUREJEA PSV BAADA YA KUPITA MIAKA 14.

WINGA mahiri wa Bayern Munich, Arjen Robben anarejea PSV Eindhoven kwa mara kwanza baada ya kupita miaka 14 wakati timu hizo zitakapokwaana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho. Katika mchezo huo PSV wataikaribisha Bayern katika Uwanja wa Philips, mahali ambapo ndipo alipoibukia Robben. Robben mwenye umri wa mika 32 alionyesha mchezo wa kiwango cha juu katika ushindi wa mabao 3-1 iliyopata Bayern dhidi ya Augsburg, baada ya kufunga na kutoa pasi za mwisho mbili ambazo zilitumiwa vyema na Robert Lewandowski na kuwapata ushindi huo. Winga huyo alijiunga na PSV akiwa na umri wa miaka 18 na kufanikiwa kufunga mabao 21 katika mechi 75 alizoichezea klabu hiyo.

LOEW AONGEZA MKATABA UJERUMANI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Loew ameongeza mkataba mwingine mpya ambao utamalizika baada ya michuano ya Ulaya mwaka 2020. Chama cha Soka cha Ujerumani-DFB kilithibitihsa taarifa hizo mapema leo kuwa Loew ambaye alianza kuinoa Ujerumani mwaka 2006 amekubali kuongeza mkataba mwingine. Mkataba wa sasa wa kocha huyo ulikuwa unamalizika baada ya michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Urusi mwka 2018. Rais wa DFB, Reinhard Grindel amesema Loew amekubali kuongeza mkataba kwakuwa wana malengo yanayofanana ambapo mojawapo ni kutetea taji lao la Kombe la Dunia nchini Urusi na pia kushinda taji la Ulaya mwaka 2020.

WALCOTT, CAZORLA KUWAKOSA LUDOGORETS.

WINGA wa Arsenal, Theo Walcott mapema amefanya mazoezi tofauti na wachezaji wenzake wakati wakijiandaa na mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Ludogorets ya Bulgaria. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza anatarajiwa kukaa nje katika mchezo huo wa kesho kutokana na majeruhi madogo ya msuli wa paja, akiwa pia amekosa mchezo wa Jumamosi iliyopita ambao Arsenal walishinda kwa mabao 4-1 dhidi ya Sunderland. Hata hivyo, Walcott mwenye umri wa miaka 27 anakaribia kupona majeruhi hayo na anaweza kurejea katika mchezo wao wa derby ya kaskazini mwa London dhidi ya Tottenham Hotspurs Jumapili ijayo. Santi Cazorla na Nacho Monreal nao pia bado wanajiuguza na wanatarajiwa kukosa mchezo huo.

AC MILAN WAMNYATIA SCHWEINSTEIGER.

KLABU ya AC Milan inadaiwa kutaka kumuwania kiungo a Manchester United Bastian Schweinsteiger wakati wa kipindi cha dirisha dogo la usajili Januari mwakani. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani ameondolewa kabisa katika kikosi cha United huku taarifa za karibuni zikidai kuwa Jose Mourinho amemuondoa hata katika kikosi cha wachezaji wa akiba. Kufuatia hatua hiyo, sasa kuna uwezekano mkubwa wa kiungo huyo kutaka kuondoka Januari na Milan inaweza kuwa chaguo lake. Schweinsteiger pia amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda kucheza katika Ligi Kuu ya Marekani-MLS huku Los Angeles Galaxy ikitajwa kumuwania.

MAN UNITED NA SPURS ZAMNYIMA RAHA WENGER.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema mwezi Novemba ndio utakaompa picha nzuri kama kikosi chake kitaweza kushindania taji la Ligi Kuu msimu huu. Arsenal kwasasa wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi wakipishana na vinara Manchester City kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, kufuatia ushindi wa mabao 4-1 waliopata dhidi ya Sunderland. Hata hivyo, pamoja na kikosi chake kuonekana kufanya vyema lakini Wenger mwenyewe anadhani mwezi ujao ndio utakuwa kipimo sahihi kwani wanakabiliwa na mechi ngumu ikiwemo ile dhidi ya Tottenham Hotspurs na Manchester United. Akihojiwa Wenger amesema kufuatia mechi ngumu watakazokutana nazo anadhani mwishoni mwa mwezi ujao wanaweza kujua zaidi kuhusu hali yao.

Friday, October 28, 2016

MO BEJAIA NA TP MAZEMBE KATIKA FAINALI YA KOMBE LA SHIRIKISHO.

KLABU ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC inatarajiwa kukwaana na MO Bejaia katika mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Fainali hiyo itakayochezwa kwa mikondo miwili, itaanzia katika Uwanja wa Mustafa Tchaker huko Blida kwa mchezo wa mkondo utakaochezwa kesho usiku. Bejaia wao watakuwa wakiwania taji lao la kwanza katika michuano hiyo huku Mazembe wao wakiwa wazoefu wa michuano hiyo kwa kutwaa mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwemo la mwaka jana, moja la Kombe la Washindi na SuperCup tatu za CAF. Mchezo wa marudiano baina ya timu hizo unatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Mazembe jijini Lubumbashi, Novemba 6 mwaka huu.

PEREZ NJE WIKI NNE.

MSHAMBULIAJI wa Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuwa mshambuliaji wao Lucas Perez anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa wiki nane baada ya kuumia goti. Perez ambaye alijiunga na klabu hiyo akitokea Deportivo La Coruna Agosti mwaka huu alipata majeruhi hayo kufuatia kukwatuliwa na Denzell Gravenberch wa Reading katika kipindi cha pili cha mchezo wa Kombe la Ligi Jumanne iliyopita. Akihojiwa kuelekea katika mchezo wao wa kesho dhidi ya Sunderland, Wenger alithibitisha taarifa hizo na kudai kuwa watamkosa Perez kwa wiki kati ya sita mpaka nane. Pamoja na kumkosa Perez lakini Arsenal wamepata ahueni kufuatia taarifaz a kurejea kwa kiungo wake Aaron Ramsey. Wenger amesema Ramsey pamoja na Olivier Giroud wote wanatajiwa kuwepo katika kikosi chake kwa ajili ya mchezo huo wa kesho.

BABA YAKE NEYMAR ADAI KILICHOMPELEKA MWANAE BARCELONA NI MESSI.

BABA yake Neymar amesema Lionel Messi ndio sababu ya mwanae kuwepo Barcelona na kuthibitisha kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Argentina ndio anayemhusudu. Neymar alijiunga na Barcelona akitokea Santos kiangazi mwaka 2013, na haraka akafanikiwa kutengeneza ushirikiano mzuri na Messi uliosaidia klabu hiyo ya Catalan kutwaa mataji mawili ya La Liga, moja na Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja la Klabu Bingwa ya Dunia. Kufuatia Neymar kusaini mkataba mpya utakaomuweka Camp Nou mpaka mwaka 2021, Baba yake amesema kikubwa kilichochangia hilo ni kuwepo kwa Messi katika klabu hiyo. Mzee huyo amesema kijana wake Neymar siku zote amekuwa akimhusudu Messi na ndoto zake kubwa ni kucheza sambamba naye ndio maana yupo Barcelona.

MKHITARYAN AAPA KUPIGANIA NAFASI OLD TRAFFORD.

KIUNGO wa Manchester United, Henrikh Mkhitaryan ameapa kupigania nafasi katika kikosi cha kwanza pamoja na kutopangwa katika klabu yake hiyo mpya kwa wiki sita. Nyota huyo wa kimataifa wa Armenia alitua Old Trafford akitokea Borussia Dortmund majira ya kiangazi mwaka huu lakini hajaichezea United toka mechi yao ya Derby dhidi ya Manchester City Septemba 10. Mkhitaryan alipata majeruhi madogo ya msuli wakati wa mapumziko kupisha mechi za kimataifa Septemba, ingawa anadaiwa kuwa tayari alishapona majeruhi hayo kipindi kirefu. Lakini pamoja na kukosa nafasi ya kuchza, kiungo huyo amedai kuwa kamwe hawezi kukata tamaa ya kupambania nafasi yake katika kikosi cha Jose Mourinho.

PULIS AONGEZA MKATABA WEST BROM.

MENEJA wa West Bromwich Albion, Tony Pulis amesaini mkataba wa mwaka mmoja zaidi ambao utamuweka katika klabu hiyo mpaka mwishoni mwa msimu ujao. Katika taarifa yake, klabu hiyo imedai kuwa mkataba huo utaleta uhakika na mlinganyo baada ya kununuliwa na mfanyabiashara Guochuan Lai wa China kwenye lengo ya kuimarisha zaidi timu hiyo. Pulis alitua katika klabu hiyo Januari mwaka 2015 wakati wakiwa nje ya eneo la kushuka daraja na kufanikiwa kuipandisha mpaka kumaliza katika nafasi ya 13 na 14 katika Ligi Kuu. Akihojiwa Pulis amesema huu ni wakati wa mabadiliko makubwa kwa klabu hiyo na wakati hilo likitokea inahitaji muendelezo.

BARCELONA WAMSHITAKI RAIS WA LA LIGA.

KLABU ya Barcelona imemshitaki rais wa La Liga Javier Tebas kwa mahakama ya juu ya michezo nchini Hispania baada ya kuhoji tabi za wachezaji wao wakati wa mchezo walioshinda mabao 3-2 dhidi ya Valencia. Valencia litozwa faini ya euro 1,500 baada ya chupa za plastiki kurushwa kutoka katika majukwaa kwenda kwa wachezaji uwanjani. Lakini kamati ya nidhamu ya La Liga pia ilikosoa tabia iliyoonyeshwa na wachezaji wa Barcelona wakati wakishangilia bao lao la ushindi. Akihojiwa Tebas amesema suala la kutupa chupa lilipaswa kuchukuliwa hatua lakini baadhi ya wachezaji wa Barcelona nao walionyesha tabia zisizopendeza zilizowakwaza mashabiki wa Valencia. Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu, amesema kauli hiyo ya Tebas inaonyesha jinsi gani asivyowajibika kutokana na wadhifa alionao.

PLUIJM AREJEA YANGA.

HATIMAYE klabu ya Yanga imefanikiwa kumrejesha kocha wake Hans Van De Pluijm ambaye alijizulu nafasi yake hiyo mapema wiki hii. Kocha huyo alifikia hatua ya kujiuzulu kwa madai kuwa uongozi wa klabu ulikuwa ukifanya mambo bila kumshirikisha zikiwemo taarifa kuwa walikuwa wakipanga kuvunja benchi lote la ufundi. Taarifa za kuvunjwa kwa benchi la ufundi zilisambaa kufuatia ujio wa kocha wa timu ya Zesco United ya Zambia. Hata hivyo, baada ya vikao kadhaa ambavyo vilikuwa vikiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba hatimaye klabu hiyo imefanikiwa kumshawishi kocha huyo kuendelea na kibarua chake. Taarifa za kurejea kwa Pluijm zilithibitishwa na viongozi wa Yanga wenyewe pamoja na Waziri Mwigulu.

Thursday, October 27, 2016

HAKUNA UHASAMA BAINA YANGU NA MESSI - RONALDO.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amepuuza taarifa kuwa kuna uhasama baina yake na Lionel Messi, akisisitiza kuwa wanaheshimiana pamoja na kwamba sio marafiki wa karibu. Wawili hao wamekuwa wakitawala tuzo za Ballon d’Or katika kipindi cha miaka nane iliyopita na wamekuwa wakitajwa kama moja ya wachezaji bora kabisa kuwahi kutokea. Kumekuwa na mijadala mingi inayoendelea kuhusu ni nani bora haswa kati ya wawili hao, lakini Ronaldo amesema hakuna chuki yeyote baina yao. Akihojiwa Ronaldo amesema kumekuwa na hali ya kuheshimiana baina yake ya Messi, na hakuna uhasama wowote kama vyombo vya habari vinavyosambaza.

SABA WAKAMATWA KWA VURUGU MECHI YA WEST HAM NA CHELSEA.

POLISI jijini London limekamata watu saba kufuatia vurugu zilizozuka wakati wa mchezo wa Kombe la Ligi kati ya West Ham United na Chelsea jana. Chupa za plastiki, viti na sarafu vilikuwa vikirushwa wakati wa mchezo huo ambao West Ham walioshinda mabao 2-1 katika Uwanja wa London, kufuatia mashabiki kugombana mpaka kupelekea polisi kuingilia kati vurugu hizo. Hiyo ni mara ya pili kwa vurugu kuzuka katika uwanja huo mpya wa West Ham msimu huu. Meneja wa West Ham Slaven Bilic amechukizwa na tabi hiyo ya iliyoonyeshwa na mashabiki na kudai kuwa haikubaliki katika soka la sasa.

MDOMO WA MOURINHO WAMUINGIZA MATATANI TENA.

CHAMA cha Soka cha Uingereza-FA kimemfungulia mashitaka meneja wa Manchester United Jose Mourinho kwa kudai kuwa itakuwa vigumu kwa mwamuzi Anthony Taylor kufanya kazi yake kwenye mchezo wao dhidi ya Liverpool. Mourinho aliongeza kuwa kuchaguliwa kwa Taylor kwa ajili ya kuchezesha mechi hiyo ya Octoba 17 kumeongeza shinikizo kwa waamuzi wanaotoka jiji la Manchester. Sheria za FA zinakataza makocha kuzungumzia waamuzi ambao wanachezesha mechi zao. Mourinho amepewa mpaka Octoba 31 awe amejibu mashitaka hayo yanayomkabili.

NINGEWEZA KUJIUNGA NA NA WEST HAM - IWOBI.

WINGA mahiri wa Arsenal, Alex Iwobi amebainisha kuwa angeweza kujiunga na West Ham United kabla ya kuamua kutua Emirates. Nyota huyo wa kimataifa wa Nigeria, aliibuka katika kikosi cha kwanza cha Arsenal msimu uliopita na toka wakati huo amekuwa mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha meneja Arsene Wenger. Hata hivyo, Iwobi amekiri kuwa pia aliwahi kufanya mazoezi na West Ham kabla ya kuamua kujiunga na klabu kubwa ya Arsenal. Akihojiwa Iwobi amesema Arsenal na West Ham zote zilikuwa zikimuhitaji, hivuo alifanya mazoezini katika klabu zote mbili kwa miaka mitatu, kwasababu huwa wanatafutwa wakiwa na na miaka sita na hawawezi kusajiliwa mpaka wafikishe miaka tisa. Iwobi aliendelea kudai kuwa aliamua kujiunga na Arsenal kwasababu alikuwa akiwashabikiwa toka nyuma na mara zote alikuwa akiiona ni klabu kubwa.

KOMPANY ALIKUWA KACHOKA - GUARDIOLA.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema alimtoa nahodha Vincent Kompany wakati wa mapumziko katika mchezo wa Kombe la Lidi dhidi ya Manchester United, kwasababu beki huyo alikuwa amechoka. Kompany mwenye umri wa miaka 30, amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara hivi karibuni lakini alianza vyema katika mchezo huo wa jana bada ya kucheza kwa dakika 78 katika sare ya 1-1 waliyopata dhidi ya Southampton Jumapili iliyopita. Beki huyo alibadilishana na Aleksandar Kolarov wakati wa mapumziko katika mchezo huo wa Old Trafford huku Guardiola akidai kuwa alichoka na asingeweza kucheza kipindi cha pili. Guardiola pia aliamuacha nahodha huyo katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya waliofungwa mabao 4-0 na Barcelona na baada ya hapo akifafanua kuwa alimuacha kwsababu hakuwa fiti.

ROBO FAINALI EFL CUP: MAN UNITED VS WEST HAM, SOUTHAMPTON VS ARSENAL.

KLABU ya Manchester United wamepangiwa kucheza na West Ham United katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Ligi baada ya kuwang’oa mahasimu wao Manchester City. United iliitandika City bao 1-0 katika Uwanja wa Old Trafford, bao pekee ambalo lilifungwa na Juan Mata wakati West Ham wao walitinga hatua hiyo baada ya kuwang’oa Chelsea kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa London. Katika robo fainali nyingine, Hull City wataikaribisha Newcastke United, Liverpool itapambana na Leeds United wakati Southampton wao wakiwa wenyeji wa Arsenal. Mechi hizo zinatarajiwa kuchezwa kati ya Novemba 29 na 30 mwaka huu.

Tuesday, October 25, 2016

NYOTA 30 WATAKAOPIGANIA TUZO YA BALLON D'OR MWAKA 2016.

Sergio Aguero (Manchester City), Pierre-Emerick Aubameyang (Borussia Dortmund), Gareth Bale (Real Madrid), Gianluigi Buffon (Juventus), Cristiano Ronaldo (Real Madrid), Kevin de Bruyne (Manchester City), Paulo Dybala (Juventus), Diego Godin (Atletico Madrid), Antoine Griezmann (Atletico Madrid), Gonzalo Higuain (Juventus), Zlatan Ibrahimovic (Manchester United), Andres Iniesta (Barcelona), Koke (Atletico Madrid), Toni Kroos (Real Madrid), Robert Lewandowski (Bayern Munich), Hugo Lloris (Tottenham Hotspur), Riyad Mahrez (Leicester City), Lionel Messi (Barcelona), Luka Modric (Real Madrid), Thomas Muller (Bayern Munich), Manuel Neuer (Bayern Munich), Neymar (Barcelona), Dimitri Payet (West Ham), Pepe (Real Madrid), Paul Pogba (Manchester United), Rui Patricio (Sporting Lisbon), Sergio Ramos (Real Madrid), Luis Suarez (Barcelona), Jamie Vardy (Leicester City), Arturo Vidal (Bayern Munich).

GRIEZMANN ATWAA TUZO YA MCHEZAJI BORA WA LA LIGA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa La Liga msimu uliopita. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa alitangazwa mshindi katika sherehe hizo zilizoandaliwa na viongozi wa ligi hiyo huko Valencia jana, iangawa mweneywe hakuwepo eneo la tukio. Klabu hiyo pia ilishuhudia meneja wake Diego Simeone akitwaa tuzo ya kocha bora wa msimu, beki bora akiwa Diego Godin na kipa bora Jan Oblak. Nyota wa Barcelona alishaguliwa kuwa mshambuliaji bora wa msimu huku Luka Modric wa Real Madrid akitwaa tuzo ya kiungo bora. Msimu uliopita Barcelona walitwaa taji la La Liga wakifuatiwa na Real Madrid nafasi ya pili na Atletico Madrid nafasi ya tatu.

PSG WALIKUWA TAYARI KUTOA PAUNDI MILIONI 170 KWA NEYMAR.

KLABU ya Paris Saint-Germain-PSG walikuwa tayari kutoa kitita cha paundi milioni 170 kwa ajili ya kumng’oa Neymar Barcelona majira ya kiangazi, lakini wwalikataa kulipa deni la paundi milioni 40 la nyota huyo wa kimataifa wa Brazil. Nyota huyo amekuwa akiandamwa na kesi za kukwepa kodi toka ahamie Barcelona na kushuhudia baadhi ya thamani na mali zake zikizuiwa na mamlaka husika. Inadaiwa kuwa Neymar alikuwa akitaka mshahara wa paundi milioni 22 kwa mwaka lakini pia pia aliwataka mabingwa hao wa Ufaransa kumlipia deni lake kama kweli wanataka aende Parc des Princes. Kufuatia PSG kukataa suala hilo, Neymar aliamua kusaini mkataba wa miaka mitano zaidi na Barcelona.

ARSENAL YAJIPANGA KUMBAKISHA WENGER.

KLABU ya Arsenal bado ina matumaini meneja wake Arsene Wenger ataendelea kuinoa timu hiyo baada ya kumalizika kwa msimu huu lakini wakaongeza kuwa hakuna haraka yeyote ya mazungumzo ya mkataba mpya. Meneja huyo mwenye umri wa miaka 67, anasheherekea miaka 20 ya kuinoa klabu hiyo lakini mkataba wa Mfaransa huyo unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Akihojiwa kuhusiana na mustakabali wa meneja huyo, mwenyekiti wa Arsenal Chips Keswick amesema kila mtu anafahamu mchango mkubwa aliotoa kocha huyo katika kipindi cha miaka 20 hivyo wana imani na uwezo wake wa kuwapeleka mbele. Mwenyekiti huyo aliendelea kudai kuwa watakaa na kuzungumza kuhusu mkataba mpya pindi wakati utakapofika. Arsenal inatarajiwa kuikaribisha klabu ya ligi daraja la pili ya Reading katika mzunguko wa nne wa michuano ya Kombe la Ligi baadae leo.

PEDRO AKIRI KUFANYA MAZUNGUMZO NA BARCELONA.

MSHAMBULIAJI wa Chelsea Pedro amebainisha kufanya mazungumzo ya kurejea Camp Noun a rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu majira ya kiangazi. Barcelona walikuwa wakitaka kuongeza nguvu katika safu yao ya ushambuliaji na waliona Pedro kama mchezaji anayefaa kwa nafasi hiyo kutokana na mafanikio yake kipindi cha nyuma. Hata hivyo, dili hilo halikufanikiwa na badala yake Barcelona walimsajili Paco Alcacer kutoka Valencia. Akihojiwa kuhusiana na hilo, Pedro alikiri kuzungumza na Bartomeu lakini mazungumzo hayo hayakufikia mbali sana baada ya klabu hiyo kupata chaguo lingine. Hata hivyo, Pedro aliendelea kudai kuwa kwasasa anafurahia maisha yake Chelsea kwani anapata muda wa kucheza jambo ambalo ndio lililomfanya kuondoka Barcelona.

SINA TATIZO NA MOURINHO - DE BRUYNE.

KIUNGO mahiri wa Manchester City, Kevin De Bruyne amesema hana tatizo lolote na Jose Mourinho katika kipindi ambacho alicheza chini ya Mreno huyo akiwa Chelsea. De Bruyne alishindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza akiwa Chelsea na kuamua kuamua kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji kwenda Wolfsburg. Mourinho alidai kuwa kiungo huyo hana uwezo wa kupambania nafasi yake katika kikosi cha kwanza, ingawa De Bruyne alikosoa madai ya meneja huyo kwa kuonesha uwezo mkubwa akiwa na Bundesliga na City. Akihojiwa De Bruyne amesema hana tatizo lolote na Mourinho, pamoja na kuwa ameshamuonyesha kuwa yote aliyosema kuhusu yeye yalikuwa sio sahihi.

Friday, October 21, 2016

DONE DEAL! NEYMAR ASAINI MKATABA WA NYONGEZA BARCELONA.

KLABU ya Barcelona imethibitisha rasmi kuwa mshambuliaji wao Neymar amesaini mkataba mpya utakaomalizika Juni 30 mwaka 2021. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil, amemaliza uvumi uliozagaa kuhusu mustakabali wake Camp Nou kwa kusaini mkataba mwingine wa miaka minne na nusu. Akihojiwa Neymar amesema amefurahi sana kuongeza mkataba wake kwani anajisikia kuwa nyumbani hapo. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa kabla ya kujiunga na Barcelona tayari alifahamu kuwa ni klabu kubwa.

KOMPANY, AGUERO BADO WANA NAFASI CITY - GUARDIOLA.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema mshambuliaji Sergio Aguero na beki Vincent Kompany wote wana uhakika wa kazi yao katika klabu hiyo. Nyota wote wawili hawakuanza katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona juzi, huku Kompany akiwa hakuonekana hata katika benchi la wachezaji wa akiba na kufanya kuzuka kwa tetesi kuwa hawako katika mipango ya kocha huyo. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo, Guardiola amesema Kompany yuko fiti sasa na kuhusu Aguero alimuacha katika mchezo wa juzi kwasababu za kiufundi. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kama Aguero akiamua kuondoka itakuwa ni uamuzi wake mwenyewe. Guardiola alithibitisha Pablo Zabaleta na Bacary Sagna kuwa wote wanatarajia kukosa mchezo wa Ligi Kuu wa Jumapili hii dhidi ya Southampton kwasababu ya majeruhi.

MKATABA WANGU HAUWEZI KUATHIRI UWEPO WA OZIL NA SANCHEZ - WENGER.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger hadhani kama mustakabali wake unaweza kuathiri nyota wao Mesut Ozil na Alexis Sanchez kusaini mkataba mpya na klabu hiyo. Ozil na Sanchez wote wamebakisha chini ya miaka miwili katika mikataba yao ya sasa lakini mazungumzo ya mikataba mipya tayari imeshaanza huku Arsenal wakitaka kuwapata ile ya muda mrefu. Wenger yuko katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na amesisitiza kuwa hatajadili mkataba mpya mpaka mwishoni mwa msimu na kufanya kuacha maswali mengi ya nani haswa atakuwa meneja wa klabu hiyo msimu ujao. Akihojiwa Wenger hadhani kama mjadala wa mkataba wake una mahusiano na ile ya kina Ozil na Sanchez kwani anaamini nyota hao wanafurahia kuwepo katika klabu hiyo.

FUCHS APEWA MKATABA MPYA LEICESTER.

KLABU ya Leicester City imetangaza kumpa mkataba mpya Christian Fuchs ambao utamuweka hao mpaka mwaka Juni 2019. Nyota huyo wa kimataifa wa Austria ameshacheza mechi 45 toka ajiunge na Leicester akiwa mchezaji huru kabla ya kuanza kwa msimu uliopita. Akihojiwa Fuchs amesema amefurahishwa kusaini mkataba huo kwani amekuwa na muda mzuri toka ajiunge na klabu hiyo. Fuchs sasa anaungana na nyota wengine wa klabu hiyo akiwemo Jamie Vardy, Riyad Mahrez, Wes Morgan na Kasper Schmeichel ambao pia tayari wameshasaini mikataba mipya.

LIVERPOOL KUMUWEKEA KIGINGI GOMEZ JANUARI.

KLABU ya Liverpool inadaiwa kuwa itazuia ofa yeyote ya mkopo kwa Joe Gomez katika usajili wa dirisha dogo Januari mwakani. Inaaminika kuwa Bournemouth wanataka kumchukua beki huyo kutoka kwa Liverpool kwa makubaliano ya muda mfupi. Mbali na Bournemouth lakini pia klabu ya Huddersfield Town inayoshiriki ligi ya ubingwa ambayo inanolewa na msaidizi wa zamani wa Jurgen Klopp katika klabu ya Borussia Dortmund, David Wagner nayo pia imetajwa kumtaka beki huyo. Hata hivyo, Liverpool wanaonekana kutokuwa na mpango na kumuacha beki huyo kwani wanataka kuanza kumrejesha taratibu katika kikosi cha kwanza baada ya kukaa nje ya uwanja kwa mwaka mmoja kufuatia kuumia goti.

POGBA ANAHITAJI MUDA - MOURINHO.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amesema Paul Pogba anahitaji muda ili kuonyesha uwezo wake Uingereza baada ya kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-1 waliopata dhidi ya Fenerbahce. Pogba aliyevunja rekodi ya usajili ya dunia kwa kunyakuliwa kwa kitita cha euro milioni 89 kutoka Juventus, alifunga bao moja kwa penati na lingine kwa shuti la mbali jana katika mchezo wa makundi wa Europa League uliofanyika Old Trafford. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 bado hajarejea katika kiwango chake toka arejee United baada ya kukaa Turin kwa miaka minne lakini Mourinho anaamini taratibu nyota huyo atarejea katika ubora wake. Akihojiwa Mourinho amesema Pogba anahitaji muda ili kuonyesha ubora wake kwani anafahamu soka la Italia, timu za kule zinacheza soka tofauti na Ligi Kuu.

Thursday, October 20, 2016

PIQUE KUKAA NJE WIKI TATU.

BEKI wa Barcelona, Gerard Pique anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu kufuatia majeruhi ya kifundo cha mguu aliyopata katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Manchester City jana huko Camp Nou. Mara ya kwanza ilionekana kuwa beki huyo anaweza kukaa nje kwa siku 10 lakini baada ya vipimo sasa imebainika kuwa itakuwa wiki tatu. Kutokana na hilo sasa Pique anatarajiwa kukosa mechi za La Liga dhidi ya Valencia, Granada na Sevilla pamoja na ule wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya City. Kwa upande mwingine beki wa kushoto Jordi Alba naye anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa wiki mbili kufuatia kupata majeruhi ya msuli wa paja katika mchezo huohuo wa jana.

RODGERS AMTETEA TOURE.

MENEJA wa Celtic, Brendan Rodgers amesema hakuna yeyote duniani aliyeumia zaidi kuliko Kolo Toure baada ya kufungwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Monchengladbach. Beki huyo mkongwe wa kimataifa wa Ivory Coast makosa yake aliyofanya katika safu ya ulinzi ndio yalipelekea Lars Stindl na Andre Hahn kufunga mabao hayo mawili na kuipa timu hiyo ya Ujerumani ushindi wake wa kwanza katika hatua ya makundi. Toure mwenye umri wa miaka 35, naye pia anajilaumu kwa kipigo hicho. Akihojiwa, Rodgers amesema Toure ni mchezaji mkweli hivyo matukio ya jana lazima yamuumize. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa anamwamini Toure kama mpambanaji hivyo anadhani atasahau magumu hayo na kuendelea kucheza kwa ubora wake.

SIWEZI KUBADILI FALSAFA ZANGU - GUARDIOLA.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema kamwe hawezi kubadili falsafa yake pamoja na kikosi chake kufumuliwa mabao 4-0 na klabu yake ya zamani wa Barcelona. Lionel Messi alifunga hat-trick dhidi ya City huku kipa Claudio Bravo akitolewa kwa kushika mpira nje ya eneo lake. Akihojiwa Guardiola amesema hakuna mabadiliko atakayofanya na ataendelea kutumia falsafa hiyohiyo. Akizungumza kuhusu Bravo, Guardiola amesema ni kipa mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka kumi hivyo hana shaka naye pamoja na kosa alilofanya. Barcelona wanaongoza kundi C wakiwa na alama tisa, tano zaidi ya City.

NINGEKUWA MAN UNITED KAMA FERGUSON ANGEKUWEPO - VAN PERSIE.

MSHAMBULIAJI nyota wa Fenerbahce Robin van Persie amesema angeweza kuwepo katika kikosi cha Manchester United katika mchezo wa leo wa Europa League kama Sir Alex Ferguson angekuwa bado yupo Old Trafford. Van Persie alichaguliw akuwa mchezaji bora wa mwaka wa United katika msimu wake wa kwanza Old Trafford 2012-2013 ambapo pia walitwaa taji la Ligi Kuu. Akihojiwa kama anadhani angeweza bado kuwa United ikiwa Ferguson angeendelea kubakia, Van Persie amesema anadhani bado angekuwa yuko United. Van Persie aliendelea kudai kuwa wakati akisajiliwa United kulikuwa na mipango ya Ferguson kubakia kwa miaka michache zaidi lakini hilo halikutokea.

SIMEONE AVIMBA KICHWA NA KIKOSI CHAKE.

MENEJA wa Atletico Madrid, Diego Simeone amesema amefurahishwa na jinsi timu yake ilivyomiliki mchezo katika ushindi waliopata katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Rostov jana. Ushindi huo umeifanya Atletico kuongoza kundi D na Simeone amewapongeza wachezaji wake kwa mchezo mzuri. Simeone amesema ulikuwa mchezo mgumu lakini waliwafahamu wapinzani wao na jinsi wanavyocheza. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa wapinzani wao walikuwa wakijilinda kwa kipindi kirefu lakini hilo halikuwakatisha tama wachezaji wake kutengeneza nafasi chache na kutumia waliyopata na kuondoka na alama zote tatu.

MICHO AJITUTUMUA PAMOJA NA UGANDA KUPANGWA KUNDI LA KIFO AFCON.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uganda, Milutin Sredojevic maarufu kama Micho, amesema kuwa hakuna kinachoshindikana baada ya kupangwa kundi moja na Ghana, Mali na Misri katika ratiba ya michuano ya Mataifa ya Afrika iliyopangwa jijini Libreville, Gabon jana jioni. Akihojiwa mara baada ya upangwaji wa ratiba hiyo, Micho alieleza kuwa wakipata maandalizi mazuri wana uwezo wa kupata matokeo mazuri dhidi ya timu kubwa walizonazo katika kundi D. Micho amesema siku zote hakuna linaloshindikana na ili uwe bora ni lazima upambane na walio bora ili kuonyesha uwezo wako. Kocha huyo alienndelea kudai kuwa kundi lao ni gumu na lenye ushindani lakini anawaamini wachezaji wake pamoja na uongozi wa Shirikisho la Soka la nchini hiyo-FUFA. Uganda wataanza kampeni zao za Afcon kwa kucheza na Ghana Januari 17, Misri Januari 21 mechi zote zikifanyika huko Port Gentil kabla ya kuivaa Mali katika mchezo wao wa mwisho wa kundi Januari 25 huko Oyen.

Wednesday, October 19, 2016

MAN UNITED IMEONGEZA MASHABIKI MILIONI NANE.

WINGA wa zamani wa Manchester United, Jasper Blomqvist anaamini klabu hiyo imejiongezea mashabiki milioni nane wa Paris Saint-Germain-PSG kufuatia kumsajili Zlatan Ibrahimovic majira ya kiangazi. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden alicheza kwa miaka minne Parc des Princes, akishinda mataji 11 na klabu hiyo kabla ya kuondoka kiangazi kufuatia kumaliza mkataba wake. Akihojiwa Blomgvist amesema kutokana na umaarufu mkubwa wa Ibrahimovic nchini Sweden anadhani PSG watakuwa wamepoteza mashabiki wengi nchini humo wanaoweza kufikia hata milioni nane. Mkongwe huyo aliendelea kudai kuwa Ibrahimovic ana jina kubwa Sweden yuko kila mahali hata mpaka kipindi hiki ambacho ameacha kucheza soka.

MASHABIKI WAIPONZA COPENHAGEN.

MASHABIKI wa klabu ya FC Copenhagen waliwafurahisha watazamaji duniani kote kwa miwako na mafataki kuelekea mhezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Leicester City jana lakini walijisababishia matatizo kwa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA. Kueleka kuanza kwa mchezo huo uliofanyika Uwanja wa King Power, mashabiki wa Copenhagen waliosafiri kuishangilia timu yao waliwasha mafataki wakati wimbo wa mashindano hayo ukiimbwa muda ambao wachezaji wanaingia uwanjani. Hata hivyo, klabu hiyo sasa imeingia matatizoni kwa mashabiki hao kuvunja sheria kwa kuwasha mafataki hayo ambayo tayari yalishapigwa marufuku. Katika taarifa yake UEFA imedai kuwa kesi hiyo itashughulikiwa na kamati ya nidhamu ambayo itakutana Novemba 17 mwaka huu.

SANCHEZ, OZIL WAMNYIMA USINGIZI WENGER.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini ushindano wao wa mataji unaweza kuwasaidia kuwashawishi winga Alexis Sanchez na kiungo Mesut Ozil kusaini mikataba mipya ya muda mrefu na klabu hiyo. Ozil na Sanchez wameingia katika miezi 20 ya mwisho katika mikataba yao ya sasa kwenye klabu hiyo na wanatarajiwa kusaini mikataba mipya minono ambayo itawafanya kubakia Emirates zaidi ya 2018. Wenger amekiri kuwa wakati majadiliano kuhusu masuala ya fedha yakiwa jambo muhimu, maendeleo ya timu uwanjani yanaweza kuchukua nafasi kubwa. Meneja huyo amesema wachezaji kama Sanchez na Ozil huwa hawaangalii sana masuala ya kifedha kwasababu tayari ni matajiri, hivyo jambo la muhimu litakuwa na maendeleo ya timu na jinsi inavyoshindania mataji. Arsenal kwasasa wanaongoza msimamo wa kundi lao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na wanatarajiwa kucheza na wakaribisha Ludogorets Razgrad ya Bulgaria leo.

GUARDIOLA AKANUSHA KUMTAKA MESSI.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amekiri alijaribu kumsajili kipa wa Barcelona Marc-Ander ter Stegen majira ya kiangazi kabla ya kuamua kumchukua Claudio Bravo. Lakini Guardiola amekanusha taarifa kuwa alijaribu kuwachukua wachezaji wake wanne wa zamani wa Barcelona na kuwaleta Etihad akiwemo Lionel Messi. Guardiola alikuwa akihitaji kipa mpya City ambaye anaweza kucheza vyema mipira ya miguu na alikwenda Camp Nou ambako walikuwa Ter Stegen na Bravo waliokuwa wakishirkiana katika majukumu ya kipa namba moja. Akihojiwa Guardiola amesema alifahamu kuwa Ter Stegen alikuwa akitaka kucheza wakati wote hivyo aliwasiliana naye lakini iliposhindikana ndio maana alihamia kwa Bravo kwani wote wawili wanashabihiana. Meneja huyo amesisitiza kuwa kamwe hakujaribu kumsajili yeyote zaidi kutoka katika klabu hiyo ambayo ameifundisha kwa miaka minne.

MATOKEO YA LIGI KUU YAMNYIMA RAHA RANIERI.MENEJA wa Leicester City, Claudio Ranieri amesisitiza bado ana hasira na kikosi chake pamoja na kufanikiwa kupiga hatua kubwa kuelekea hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bao pekee la Riyad Mahrez lilitosha kuipa ushindi wa bao 1-0 Leicester dhidi ya FC Copenhagen ya Denmark na kuendelea rekodi yao ya ushindi wa asilimia 100 Ulaya na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa kundi G. Kama wakifanikiwa kupata ushindi katika mchezo wao wa marudiano dhidi ya Copenhagen Novemba 2, moja kwa moja watakuwa wametinga hatua hiyo baada ya kuwa tayari wameshawafunga Club Brugge na FC Porto. Leicester wamepata alama nyingi zaidi katika mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko mechi nane za Ligi Kuu walizocheza na Ranieri amekiri kutofurahishwa na hali inavyoendelea. Ranieri anafurahia kwa upande mmoja lakini upande anachukizwa kutokana na hali ilivyo kwani katika mechi nane za ligi wameambulia alama nane pekee.

Real Madrid vs Legia Warszawa 5-1 All Goals & Full Highlights Champions ...

Tuesday, October 18, 2016

MODRIC ASAINI MKATABA MPYA MADRID.

KLABU ya Real Madrid imetangaza kumsainisha mkataba mpya Luka Modric ambao utamuweka Santiago Bernabeu mpaka Juni mwaka 2020.  Mkataba wa sasa wa nyota huyo wa kimataifa wa Croatia ulikuwa unamalizika mwaka 2018, lakini sasa amekubali kusaini miaka miwili zaidi. Modric alijiunga na mabingwa wa Ulaya akitokea Tottenham Hotspurs Agosti mwaka 2012 na toka wakati ameimarika na kuwa mchezaji wa kutegemewa Madrid. Kiungo huyo mwneye umri wa miaka 31 ameichezea Madrid mechi 18o za mashindano yote mpaka sasa na kufanikiwa kutwaa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mawili ya Super Cup ya UEFA, Kombe la Mfalme, Klabu Bingwa ya Dunia na Supercopa de Espana.

LEICESTER WAKOMALIA CHAMPIONS LEAGUE.


MENEJA wa Leicester City, Claudio Ranieri amesema timu yake imetoa kipaumbele kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwasababu wana kipindi kirefu cha kuimarisha kiwango chao katika Ligi Kuu. Leicester watakuwa wenyeji wa FC Copenhagen katika Uwanja wa King Power baadae leo, huku wakiwa tayari wameshinda mechi zao mbili za kwanza za kundi G. Lakini mabinga hao wa Ligi Kuu wameambulia alama nane pekee katika mechi zao nane za ligi msimu huu. Akihojiwa Ranieri amesema katika Ligi Kuu watakuwa salama ifikapo mwishoni mwa mwaka ila kwasasa nguvu zao zipo katika Ligi ya Mabingwa. Leicester wlianza michuano hiyo kwa kuilaza Club Brugge kwa mabao 3-0 kabla ya kuja kupata ushindi wa bao 1-0 kwa Porto.

TAJIRI WA MAREKANI AINUNUA MARSEILLE.

MFANYABIASHARA tajiri wa Marekani, Frank McCourt amefanikiwa kuinunua klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa kwa kitita cha euro milioni 45. McCourt ambaye anamiliki Los Angeles Dodgers, amepanga kuwekeza kiasi cha euro milioni 200 katika klabu hiyo kwa kipindi cha miaka minne. Marseille mabingwa wa Ligue 1 mara tisa, ambao walimaliza katika nafasi ya 13 msimu uliopita, kwasasa wanashikilia nafasi ya 12 katika msimamo baada ya kucheza mechi nane. Akihojiwa McCourt mwenye umri wa miaka 63, amesema anataka kufungua ukurasa mpya katika klabu hiyo yenye historia kubwa na kuirejesha njia ya mafanikio.

MAN CITY YAINGIZA FAIDA KWA MSIMU WA PILI MFULULIZO.

KLABU ya Manchester City imetangaza rekodi mpya ya mapato yao kufikia paundi milioni 391.8, huku wakitengeneza faida kwa mwaka wa pili mfululizo. Vinara hao wa Ligi Kuu walitoa taarifa yao ya mwaka wa fedha wakionyesha kutengeneza faida ya paundi milioni 20.5 kwa msimu wa 2015-2016. Mwaka jana, City walitangaza mapato yao ya kwanza toka Sheikh Mansour alipochukua umiliki wa klabu hiyo mwaka 2008 na kuanza kuwekeza katika kikosi cha kwanza. Klabu hiyo ilitangaza hasara ya paundi milioni 197.5 msimu wa 2010-2011 ikiwa ni hasara kubwa kuwahi kupata klabu za Uingereza na kufuatia na hasara zingine za paundi milioni 97.9 msimu wa 2011-2012, paundi milioni 51.6 msimu wa 2012-2013 kabla ya hatimaye kutangaza ongezeko ya paundi milioni 11 msimu uliopita. Mapato ya paundi milioni 391.8 ya City ni ongezeko la asilimia 11 kulinganisha ya yale ya paundi milioni 351.8 waliyopata mwaka jana. Mapato hayo yamechangiwa kwa kiasi kubwa na upanuzi wa Uwanja wa Etihad ambao kwasasa unabeba mashabiki 55,000 na pia uwekezaji wa asilimia 13 wa kampuni mama ya China Media Capital Holdings.

MOURINHO AIPONDA LIVERPOOL KUFUATIA SARE.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amesema Liverpool sio timu ya kwanza ya ajabu kama inavyoripotiwa na vyombo vya habari, baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana jana. Katika mchezo huo wa Anfield uliokuwa na nafasi chache, wenyeji Liverpool walionyesha kutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa kufuatia wapianzani wao muda mwingi kucheza kwa kujihami. Akihojiwa Mourinho amesema jambo la muhimu ni kuwa wamepata alama moja ambayo imewazuia wapinzani wao kupata alama tatu. Kwa upande wa meneja wa Liverpool Jurgen Klopp, yeye ameonyesha kutofurahishwa na kikosi chake kwani walikuwa wakitaka kucheza haraka na kupoteza umakini katika pasi zao. Matokeo hayo ynaiacha Liverpool katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na alama saba huku United wakiwa nyuma yao kwa tofauti ya alama tatu kwenye nafasi ya saba.

MISRI SASA MASHABIKI RUKSA VIWANJANI.

CHAMA cha Soka cha Misri-EFA kimetangaza kuwa kitaruhusu mashabiki 50,000 kuhudhuria mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia kati ya Misri na Ghana utakaofanyika jijini Alexandria. Mchezo huo unatarajiwa kufanyika Jumapili ya Novemba 13 katika Uwanja wa Borg El Arab. Kuzuiwa kwa mashabiki katika mechi nchini humo kuliwekwa toka mwaka 2012 wakati mashabiki 72 wa Al Ahly walipokufa kufuatia vurugu zilizotokea huko Port Said. EFA pia imetangaza kuwa mashabiki 40,000 wataruhusiwa kwnda kuangalia mchezo wa fainali ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo itafanyika jijini Alexadria. Katika mchezo huo Zamalek watakuwa wenyeji wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini Jumapili hii.

KICHUYA MCHEZAJI BORA WA MWEZI.

MSHAMBULIAJI Shiza Kichuya wa Simba SC amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa Septemba msimu wa 2016/2017. Kichuya aliwashinda nyota wengine wa VPL akiwemo Adam Kingwande wa Stand United na Omari Mponda wa Ndanda FC. Mchezaji aliisadia timu yake kwa mwezi huo kupata pointi zote 12 katika mechi nne ilizocheza, matokeo ambayo yameifanya Simba iendelee kuongoza Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16. Pia alifunga mabao matatu katika mechi mbili kati ya nne ilizocheza timu yake. Kwa kushinda tuzo hizo ya mwezi, Kichuya atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

Monday, October 17, 2016

KUFA NA KUPONA ANFIELD LEO.

MACHO na masikio ya wapenzi wa soka duniani baadae leo watakuwa luningani kushuhudia mchezo wa Ligi Kuu ambao utazikutanisa timu mahasimu Liverpool dhidi ya Manchester United. Mchezo huo utakaofanyika Anfield unakutanisha timu hizo zenye uhasimu wa kipindi kirefu nchini Uingereza ambapo klabu hizo kwa pamoja wametwaa jumla ya mataji 87, Liverpool 44 na United mataji 43. Liverpool inakwenda katika mchezo huo ikiwa katika kiwango kizuri kwa kushinda mechi zake zote nne zilizopita za ligi huku United wao wakiwa tayari wameshapoteza mechi mbili msimu huu na wako nyuma ya vinata Manchester City kwa alama tano. Hata hivyo, rekodi ya United wakikutana na Liverpool iko juu ambapo wameshinda mechi nne za ligi zilizowakutanisha huku mara ya mwisho ikiwa ni Januari mwaka huu wakati waliposhinda bao 1-0. Liverpool mara ya mwisho kuishinda United katika Uwanja wa Anfield ilikuwa katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Europa League msimu uliopita ambapo walishinda mabao 2-0.

NEYMAR KUSAINI MKATABA MPYA IJUMAA.

KLABU ya Barcelona imethibitisha kuwa mshambuliaji wake nyota Neymar anatarajia kusaini mkataba mpya Ijumaa hii. Barcelona walitangaza taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ataisaini mkataba mpya ambao utamuweka klabuni hapo mpaka mwaka 2021. Neymar amekuwa akihusishwa na tetesi kuwindwa vilabu kadhaa ikiwemo Paris Saint-Germain lakini sasa mshambuliaji huyo anajipanga kusaini mkataba mpya wa muda mrefu Camp Nou. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa katika kiwango bora msimu huu akiwa amefunga mabao manne katika mechi sita za La Liga alizocheza. Neymar alijiunga na Barcelona akitokea Santos mwaka 2013 na ameshinda mataji mawili ya la Liga na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.