Friday, September 30, 2016

TERRY KUIKOSA SAFARI YA HULL.

KLABU ya Chelsea kwa mara nyingine itamkosa nahodha wake John Terry katika mchezo wao wa ugenini Jumamosi hii dhidi ya Hull City. Beki huyo mkongwe alirejea mazoezini wiki hii lakini alishindwa kukabiliana na athari za majeruhi ya kifundo cha mguu aliyopata wakati wa mchezo dhidi ya Swansea City mapema mwezi huu. Chelsea imepoteza mechi zote mbili ambazo walikuwa bila nahodha wao huyo, huku wakionyesha udhaifu katika safu yao ya ulinzi aktika mechi dhidi ya Liverpool na Arsenal. Akihojiwa kuelekea mchezo huo wa kesho, Conte amesema terry hatakuwepo kwakuwa bado anauguza majeraha ya kifundo cha mguu. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa beki huyo anaweza kurejea uwanjani baada ya mapumziko kupisha mechi za kimataifa.

IBRAHIMOVIC ALIKATAA EURO MILIONI 100 ILI AENDE UNITED - WAKALA.

WAKALA wa mshambuliaji wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic, Mino Raiola amedai mteja wake huyo alipewa ofa ya paundi milioni 100 na klabu ambayo hakutaja kuitaja ya China kipindi cha kiangazi.Nyota huyo wa kimataifa wa Sweden alitua Old Trafford akiwa mchezaji huru majira ya kiangazi baada ya mkataba mkataba wake Paris saint-Germain kumalizika. Ibrahimovic anaripotiwa kukunja kitita cha paundi 200,000 kwa wiki Old Trafford, lakini Raiola amedai mteja wake huyo angeweza kupata zaidi kama angeamua kwenda mashariki ya mbali. Akihojiwa Raiola amesema Ibrahimovic ni mchezaji bora kwani alikataa ofa ya euro milioni 100 kutoa China kwasababu alikuwa akihitaji ushindi zaidi kuliko fedha. Raiola aliendelea kudai kuwa siku zote amekuwa mtu mwenye bahati kwani amekuwa akiwawakilisha mabingwa ambao ni Ibrahimovic, Pavel Ndved na Maxwell ambao wamestaafu na sasa Blaise Matuidi na Gigio Donnarumma.

FABREGAS, MATA WAACHWA HISPANIA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Julen Lopetegui amewaacha Cesc Fabregas ba Cesar Azpilicueta katika kikosi chake ambacho kinajiandaa kwa ajili ya mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Italia na Albania. Fabregas ambaye ameshindwa kupata nafasi ya moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha Chelsea msimu huu hakujumuishwa pia katika kikosi cha kocha huyo mwezi uliopita. Mchezaji mwenzake wa Cheslea Azpilicueta mwenye umri wa miaka 27, alitajwa katika kikosi cha mwezi uliopita lakini safari hii naye ametemwa. Kwa upande mwingine nahodha Andres Iniesta amerejea katika kikosi hicho huku pia nyota Jose Callejon wa Napoli ambaye yuko katika kiwango kizuri msimu huu akiitwa.

KLOPP ATANGAZA KUSTAAFU UKOCHA KABLA YA KUFIKISHA MIAKA 60.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp tayari ameshaanza kufikiria kuhusu maisha baada ya soka na ameweka wazi amepanga kustaafu kabla ya kufikisha miaka 60. Meneja huyo mwenye umri wa miaka 49, alianza shughuli hizo katika klabu ya Mainz mwaka 2001 na pia kufanya kazi kwa mafanikio Borussia Dortmund kabla ya kutua Liverpool mwaka 2015. Klopp anafurahia maisha ya Anfield lakini amekiri haoni kama ataweza kuendelea na kazi zaidi ya kipindi cha miaka 10 ijayo. Akihojiwa Klopp amesema anafahamu itakuja siku ya kuamua kwamba kazi hiyo inatosha na kuna uwezekano mdogo sana wa kuendelea na kazi hiyo akiwa amefikisha umri wa miaka 60. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa atarejea zake nyumbani Ujerumani kwenda kuishi huko lakini hadhani kama atarudi akiwa kocha.

CONTE KUPEWA FUNGU JANUARI.

MMILIKI wa Chelsea, Roman Abramovic yuko tayari kumsaidia Antonio Conte baada ya kumwambia Muitaliano huyo kuwa ataruhusiwa kufanya usajili wa wachezaji kadhaa katika kipindi cha usajili wa Januari. Mkutano baina yao unatajwa kufanyika katika uwanja wa wa mazoezi wa Cobham wiki hii ambapo Conte aliwasilisha mapendekezo yake kwa mmiliki huyo akidai kupewa ruhusa ya kusajili. Taarifa kutoka ndani zinadai kuwa Abramovic anadhani Conte alirithi kikosi kilichopitwa na wakati ambacho kilitwaa taji la Ligi Kuu miaka miwili iliyopita lakini amefurahishwa kwa jinsi alivyokisuka na kukirejeshea makali yake. Conte anataka kukijenga upya kikosi hicho na imefahamika kuwa atapewa ushirikiano wowote ikiwemo wa kifedha na mmiliki huo.

WENGER AACHA MILANGO WAZI YA KWENDA KUINOA UINGEREZA.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema yuko tayari kuja kuinoa timu ya taifa ya Uingereza siku za usoni, lakini kwasasa mkazo wake uko katika klabu yake hiyo. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo, Wenger amesema siku moja kama atakuwa hana kazi anaweza kukubali kuinoa nchi hiyo. Meneja huyo raia wa Ufaransa atasheherekea miaka 20 ya kuwa na Arsenal Octoba mosi mwaka huu na mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwasasa kinatafuta meneja mpya kufuatia kuondoka kwa Sam Allardyce Jumanne iliyopita.

LUKAKU ATAMANI KUWAFIKIA KINA SUAREZ.

MSHAMBULIAJI wa Everton, Romelu Lukaku anatambua bado anahitaji kuimarika kama anataka kufikia kiwango cha nyota wa Barcelona Luis Suarez na washambuliaji wengine wakubwa. Lukaku alifunga mabao 18 katika mechi 37 za Ligi Kuu msimu uliopita, lakini Everton hawakuwa na msimu mzuri hatua iliyopelekea kumaliza wakiwa katika nafasi ya 11, jambo ambali lilipelekea kutimuliwa kwa Roberto Martinez. Akihojiwa Lukaku amesema anahitaji mechi nyingi zaidi za kushinda ili kufikia kiwango cha mchezaji kama Suarez. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa kwasasa anafunga mabao kama wao lakini anahitaji kutengeneza mabao kama wafanyavyo kina Sergio Aguero, Suarez, Karim Benzema, Roberto Lewandowski na wengineo.

ROONEY KUENDELEA KUWA NAHODHA WA UINGEREZA.

KOCHA wa muda wa timu ya taifa ya Uingereza, Gareth Bale amethibitisha kuwa Wayne Rooney ataendelea kuwa nahodha wa kikosi hicho. Southgate ambaye amechukua mikoba ya muda Jumanne hii kufuatia kuondoka kwa Sam Allardyce alizungumza na Rooney ambaye pia ndio nahodha wa Manchester United jana. Jumapili hii kocha huyo anatarajiwa kutaja kikosi chake ambacho kitajiandaa kwa ajili ya mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Malta na Slovenia. Mapema mwzi uliopita Allardyce alidai kuwa ni uamuzi rahisi kumuacha Rooney aendelee kuwa nahodha pamoja na kiwango kilichoonyeshwa na Uingereza katika michuano ya Ulaya mwaka huu.

Wednesday, September 28, 2016

KIPA WA MAURITIUS ADAKWA NA DAWA ZA KULEVYA.

GOLIKIPA wa kimataifa wa Mauritius, Joseph Kinsley Steward Leopold amekamatwa kwa tuhuma za kushughulika na madawa ya kulevya. Kikosi kazi cha kupambana na dawa hizo nchini humo, kilikwenda kupekua nyuma ya kipa huyo mwenye umri wa miaka 27 iliyopo huko Port Louis na kukuta pakiti 22 za dawa aina ya heroin. Vifaa vingine vinavyotumika kuandaa na kuhifadhi heroin vikiwemo viwembe na mizani pia vilikutwa katika nyumba ya kipa huyo. Leopold ni kipa chaguo la kwanza la timu ya ASPL 2000 inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo na pia alikuwa kipa wa akiba wa timu ya taifa katika mechi ya mwisho ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika.

MKUTANO MKUU MALUMU WA CAF WAIVA.

MAKAMU wa rais wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF, Seketu Patel amejitoa kutoka katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi mbili za Afrika katika Baraza la Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Hatua hiyo inafanya kubaki na wagombea watano katika uchaguzi huo ambao unatarajiwa kuteka sehemu kubwa ya Mkutano Mkuu Maalumu wa CAF utakaofanyika jijini Cairo kesho. CAF ilithibitisha taarifa hizo huku Patel mwenyewe akishindwa kutoa sababu zozote za kujitoa kwake kwenye kinyang’anyiro hicho. Rais wa Chama cha Soka cha Sudan Kusini, Chabur Goc Alei naye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho wiki iliyopita. Hatua hiyo sasa inamuacha makamu wa pili wa rais wa CAF Almamy Kabele Camara kutoka Guinea kuwa mgombea mwenye hadhi ya juu zaidi katika mbio hizo na mmoja kati ya wanaopigiwa upatu wa kukwaa nafasi mojawapo pamoja na mjumbe wa kamati ya utendaji ambaye pia ni raia wa Chama cha Soka cha Ghana Kwesi Nyantakyi. Wagombea wengine katika uchaguzi huo ni Ahmad wa Madagascar ambaye hutumia jina moja pekee katika utambulisho wake, Hamidou Djibrilla wa Niger na rais wa Chama cha Soka cha Senegal Augustin Senghor.

FA SASA KUMGEUKIA WENGER BAADA YA KUONDOKA ALLARDYCE.

CHAMA cha Soka cha Uingereza-FA kinadaiwa kuwa kitajaribu kumuwania kocha wa Arsenal, Arsene Wenger mwishoni mwa msimu huu ili awe kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo. Sam Allardyce aliachia wadhifa wake kama kocha wa nchi hiyo jana, ikiwa zimepita siku 67 toka alipoteuliwa kushika nafasi hiyo na kukiacha kikosi hicho kikitafuta kocha mpya. Wenger ambaye anasheherekea miaka 20 akiwa na klabu hiyo, anapewa nafasi kubwa kuchukua nafasi hiyo huku FA wakidaiwa kuwa tayari walishamfuata kabla ya kumchagua Allardyce. Hata hivyo, Arsenal haitarajiwi kumuachia kirahisi meneja wao huyo wa muda mrefu na mmiliki wa timu hiyo Stan Kroenke bado ana matumaini kuwa atakubali kuongeza mkataba.

SARE ZA MADRID ZAMCHANGANYA ZIDANE.

MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesema anahisi kukosa bahati baada ya timu yake kuruhusu bao la kusawazisha dakika za mwishoni jana na kupelekea kupata sare ya mabao 2-2 katika mchezo wao wa kundi F wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund. Katika mchezo huo Madrid walianza kuongoza kwa bao safi la kushtukiza la Cristiano Ronaldo kabla ya Dortmund hawajasawazisha kupitia kwa Pierre-Emerick Aubameyang aliyetumia vyema makosa yaliyofanywa na Keylor Navas. Madrid waliongeza bao lingine kupitia kwa Raphael Varane katikati ya kipindi cha pili lakini walishindwa kulinda ushindi huo baada ya Christian Pulisic aliyeingia akitokea benchi kusawazisha zikiwa zimebaki dakika tatu. Sare hiyo waliyopata jana Madrid inakuwa ya tatu baada ya zile mbili walizopata katika La Liga dhidi ya Villarreal na Las Palmas. Akihojiwa Zidane amesema anadhani wanakosa bahati kwani wanacheza vizuri na bidii lakini mwishoni wanashindwa kuzuia ushindi wanaokuwa nao.

VARDY AELEZA KULICHOMFANYA KUIKACHA ARSENAL.


MSHAMBULIAJI nyota wa Leicester City, Jamie Vardy amesema alikataa ofa ya kujiunga na Arsenal majira ya kiangazi ili ajaribu na kujenga mafanikio waliyopata kwa kutwaa taji la Ligi Kuu. Inadaiwa kuwa nyota huyo alikaribia kujiunga na Arsenal kufuatia klabu hiyo kutengua kitenzi katika mkataba wake cha paundi milioni 20, lakini Vardy mwenyewe alibadili maamuzi yake na kuamua kubakia King Power. Akihojiwa Vardy amesema kikubwa kilichombakisha Leicester sio uaminifu bali alitaka kuendelea kujenga kile walichokifanya na wachezaji wenzake. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa Leicester ni klabu inayokua na anafurahia kuwa sehemu ya makuzi ya klabu hiyo.

TEVEZ KUSTAAFU MWISHONI MWA MWAKA HUU.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Argentina, Carlos Tevez amelaumu vyombo vya habari kwa adhabu aliyopewa na kuongeza kuwa anaweza kuachana na soka itakapofika mwishoni mwa mwaka huu. Tevez mwenye umri wa miaka 32, ambaye kwasasa anacheza katika klabu ya nyumbani kwao ya Boca Juniors, alicheza kwa mafanikio barani Ulaya katika klabu za Manchester United, Manchester City na Juventus. Lakini nyota huyo ameeleza hisia zake kwa mambo kadhaa yanayotokea katika ligi ya nyumbani ikiwemo shinikizo kubwa lililowekwa kwa Boca na vyombo vya habari ambavyo amevilaumu kw akufungiw akwake mechi tatu. Akihojiwa Tevez amesema adhabu aliyopewa kwa kukosoa ni kama imetoka kwa waandishi na sio katika kamati. Tevez pia aliponda utaratibu wa upangaji ratiba fupifupi katika soka la nchi hiyo na kuongeza kuwa ni moja ya mambo ambayo yanamfanya afikirie kustaafu soka mwishoni mwa mwaka huu.

ALLARDYCE AIACHA UINGEEREZA HUKU AKISIKITIKA.

ALIYEKUWA kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Sam Allardyce amesema amesikitishwa kuacha kibarua chake hicho baada ya kukitumikia kwa siku 67 pekee. Hatua hiyo imekuja baada ya gazeti moja nchini humo kutoa taarifa za uchunguzi wao kuwa, kocha huyo alitoa ushauri wa jinsi gani ya kukwepa mkono wa sheria katika suala la usajili. Allardyce aliomba radhi kutokana na hilo na kudai kuwa anafahamu kuwa baadhi ya kauli zake alizotoa huko nyuma zimesababisha aibu kubwa. Chama cha Soka cha Uingereza-FA kimeseam kauli ya kocha huyo sio ya kimaadili na kuongeza kuwa wameamua kusitisha mkataba wake kwa maelewano. Gareth Southgate sasa ndio amepewa mikoba ya muda kuingoza timu hiyo katika mechi zao nne zijazo, wakati mchakati mwingine ukifanyika.

Tuesday, September 27, 2016

KLOPP ATAKA TIMU YAKE KUIMARIKA ZAIDI.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema bado kuna nafasi ya kuimarika kama kikosi chake kinataka kupigania taji la Ligi Kuu msimu huu pamoja na kuanza vyema kampeni zao. Liverpool ambao mara ya mwisho kutwaa la ligi ilikuwa mwaka 1990, waliirarua Hull City kwa mabao 5-1 Jumamosi iliyopita na kukwea mpaka nafasi nne katika msimamo, wakiwa nyuma ya vinara Manchester City kwa alama tano. Liverpool wameshinda mechi ngumu za ugenini dhidi ya Arsenal na Chelsea huku wakiwababua mabingwa Leicester City kwa mabao 4-1 msimu huu, na mechi pekee waliyopoteza ni ile waliyofungwa na Burnley. Akihojiwa Klopp amesema ni kweli kwasasa wanacheza vizuri lakini bdo kuna nafasi ya kuimarika ili waweze kuendeleza wimbi lao la ushindi.

WENGER AMTETEA ALLARDYCE KUFUATIA KASHFA INAYOMKABILI.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kocha wa timu ya taifa ya Uingereza Sam Allardyce anahitaji kupewa nafasi ya kujitetea, kufuatia tuhuma zilizotolewa na gazetini. Uchunguzi wa gazeti la Daily Telegraph unadaiwa kung’amua kuwa Allardyce mwenye umri wa miaka 61 alitumia nafasi yake kufanya mazungumzo ya dili la paundi 400,000 na kutoa ofa ya ushauri wa jinsi gani wanaweza kukwepa sheria katika usajili wa mchezaji. Meneja huyo wa zamani wa Bolton Wanderers, Newcastle United na West Bromwich Albion pia amedaiwa kukikosoa Chama cha Soka cha Uingereza-FA, meneja aliyeondoka Roy Hodgson na msaidizi wake wa zamani Gary Neville. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo, Wenger amesema Allardyce anatakiwa kupewa nafasi ya kujitetea na matumani yake ni kwamba ataweza kusafisha jina lake. Allardyce mwenyewe bado hajajibu chochote kuhusiana na tuhuma hizo na amekuwa na mkutano na mwenyekiti wa FA Greg Clarke pamoja na ofisa mkuu Martin Glenn leo.

YAYA TOURE AIPONDA FIFA.

KIUNGO wa Manchester City, Yaya Toure amesema wachezaji na mashabiki wanaweza kuumia kufuatia hatua ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuvunja kikosi kazi kilichoundwa kwa ajili ya kupambana na vitendo vya kibaguzi katika soka. Toure mwenye umri wa miaka 33, alikuwa mmoja wa wajumbe wa kikosi kazi hicho kilichoundwa mwaka 2013 kusaidia kutokomeza ubaguzi. Katibu mkuu wa FIFA, Fatma Samba Diouf Samoura amesema kikosi kazi hicho kilikuwa na kazi maalumu ambayo tayari wameimaliza. Hata hivyo, hatua hiyo imekosolewa vikali na wadau mbalimbali, akiwemo Toure ambaye alifanyiwa vitendo vya kibaguzi na mashabiki wa CSKA Moscow Octoba mwaka 2013. Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Ivory Coast amesema hatua hiyo ya FIFA itaweza kuwaumiza mashabiki na wachezaji kama mipango sahihi isipowekwa.

ZIDANE AKANUSHA KUWEPO MPASUKO KATI YAKE NA RONALDO.

MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amepuuza tetesi kuwa kuwa kuna mpasuko kati yake na Cristiano Ronaldo kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund baadae leo. Zidane amedai kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Ureno ni mtu mwenye uelewa mzuri wa kujua kocha hufanya maamuzi kwa faida ya timu. Ronaldo amefunga mabao mawili katika mechi nne alizocheza msimu huu, likiwemo bao zuri la mpira wa adhabu alilofunga katika mchezo wao wa ufunguzi walioshinda mabao 2-1 dhidi ya Sporting Lisbon. Wakati alipotolewa mapema katika sare ya mabao 2-2 waliyopata dhidi ya Las Palmas, nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 alionyesha kukasirika. Hata hivyo, Zidane amesema kila kitu kikosi sawa katika kambi yao na sio jambo la kushangaza kwa mchezaji kuchukia akitolewa kwani hutokea mara kwa mara na sio kwa Ronaldo peke yake.

MO FARAH AAKA KUINOA ARSENAL.

MWANARIADHA nyota wa Uingereza na bingwa mara nne wa Olimpiki, Mo Farah amesema angependa kuja kuwa mwalimu wa mazoezi wa klabu ya Arsenal. Farah amekuwa shabiki wa Arsenal toka akiwa kijana mdogo na amesema yuko tayari kufanya kazi katika klabu hiyo inayotoka Kaskazini mwa London katika siku za usoni. Akihojiwa Farah ambaye ni mzaliwa wa Somalia amesema kitu kimoja anchokipenda kwa dhati ni soka na amekuwa na mahusiano mazuri na Arsenal. Farah aliendelea kudai kuwa alianza kuishabikia Arsenal toka alipowasili nchini Uingereza kwa mara ya kwanza akiwa mdogo kwasababu alipenda wanavyocheza. Kitu kingine kilichomvutia Farah ni kuwepo kwa wachezaji wengi wenye asili ya Afrika na siku moja angependa kuja kufanya nao kazi.

BARCELONA IKO POA BILA MESSI - ENRIQUE.

MENEJA wa Barcelona, Luis Enrique amesema wana wachezaji wa kutosha ambao wanaweza kuziba pengo liliachwa na nyota wao Lionel Messi. Messi anatarajiwa kuukosa mchezo wa huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Monchengladbach utakaofanyika kesho kutokana na majeruhi ya nyonga. Jumamosi iliyopita Barcelona walionesha wanaweza kusonga mbele bila Messi baada ya kuitandika Sporting Gijon kwa mabao 5-0 katika mchezo wa La Liga. Barcelona wamefunga mabao 18 katika mechi nne toka walipotandikwa mabao 2-1 nyumbani na Alaves Septemba 10 mwaka huu huku Neymar na Luis Suarez wakiwa katika kiwnago kizuri. Akihojiwa Enrique amesema ana wachezaji wa kutosha ambao wanaweza kuicheza vyema na kuziba pengo la Messi ambaye anatarajiwa kukaa nje kwa kipindi cha wiki tatu.

Monday, September 26, 2016

NYOTA WA PARAGUAY AZITOA UDENDA KLABU ZA LIGI KUU.

KLABU za Swansea City na Sunderland zinadaiwa kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania saini ya Federico Santander. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Paraguay ambaye kwasasa anakipiga katika klabu ya Fc Copenhagen ya Denmark, atakuwa akitazamwa na maskauti wa klabu zote mbili katika mchezo wao wa Jumanne dhidi ya Club Brugge. Santander amefunga mabao sita katika mechi 17 kwenye mashindano yote msimu huu na anaweza kuvutiwa kuhamia Ligi Kuu. Taarifa pia zinadai Everton na Olympique Lyon nazo ni klabu zingine zinazomfuatilia kwa karibu mshambuliaji huyo.

MWENYEKITI WA BOURNEMOUTH AKANUSHA ARSENAL KUMTAKA MENEJA WAO.

MWENYEKITI wa Bournemouth, Jeff Mostyn amekanusha Arsenal kumfuata meneja wao Eddie Howe.  Meneja huyo wa Bournemouth amekuwa akihusishwa na tetesi za kuchukua mikoba ya Arsene Wenger msimu ujao kufuatia meneja huyo raia wa Ufaransa kumalizika mkataba mkataba wake kiangazi mwakani. Lakini Mostyn anaamini Howe bado ana mambo mengi ya kufanya katika Uwanja wa Vitality wakati klabu hiyo ikijaribu kujiimarisha katika Ligi Kuu. Akihojiwa Mostyn amesema ni jambo la fahari kuona meneja wao akitafutwa na klabu zingine ingawa hakuna yeyote aliyewasiliana nao rasmi kuhusu suala hilo. Mwenyekiti huyo aliendelea kudai kuwa bado wana kazi kubwa ya kufanya na Howe kwani wanahitaji kuimarisha klabu hiyo.

WABAGUZI KUKIONA - FIFA.

KATIBU mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Fatma Samoura amekingia kifua kikosi kazi cha kupambana na masuala ya ubaguzi akidai kuwa mpango imara unatarajiwa kuwekwa ili kutokomeza kabisa hali hiyo. Kumezuka wasiwasi juu ya uamuzi wa wa kubadilisha kikosi kazi hicho huku ikiwa imebaki miaka miwili kabla ya michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Urusi mwaka 2018. Lakini Samoura ambaye alikuwa akizungumza jijini Manchester amesisitiza kuwa pamoja na mabadiliko hayo bado kutakuwa na sera isiyoruhusu kabisa aina yeyote ya unyanyapaa kwa kikosi kazi kipya kutakachopewa majukumu hayo. Samoura amesema kikosi kazi kipya kitakachopewa kazi hiyo kitakuwa imara zaidi ya ilivyokuwa mara ya kwanza kwani wamepanga kutokomeza kabisa masuala yeyote ya unyanyapaa katika soka.

BEKI PSG AFUNGWA MIEZI MIWILI JELA.

BEKI wa Paris Saint-Germain-PSG, Serge Aurier amehukumiwa miezi miwili jela kwa tuhuma za kumshambulia ofisa wa polisi. Nyota huyo mwneye umri wa miaka 23 anatuhumiwa kumshambulia polisi huyo baada ya kusimamishwa Mei mwaka huu na kutakiwa kufanyiwa vipimo kama alikuwa na kilevi. Aurier ambaye alikuwa akituhumiwa kumpiga kiwiko kifuani ofisa huyo amedai kuwa aliteswa na polisi na kuna taarifa zinadai kuwa atakata rufani kupinga uamuzi huo wa mahakama. Akihojiwa Juni mwaka huu, Aurier amesema ilikuwa ni vurugu kwani polisi walitoka katika gari lao na kumnyanyapaa, kumtesa na kumpiga usoni. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa kinachomsikitisha ni kutuhumiwa kupiga kiwiko polisi kwani kama kweli alitaka kumgusa angeweza kumpiga ngumi usoni. Aurier pia ameamriwa kulipa kiasi cha euro 300 kama fidia kwa majeraha aliyosababisha, euro 300 nyingine kwa uharibifu wa kimaadili na euro 1,500 gharama za kesi.

TP MAZEMBE, MO BEJAIA KUVAANA FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO.

KLABU ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC inatarajiwa kukwaana na Mouloudia Bejaia ya Algeria katika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Timu hizo zote mbili zimepata nafasi ya kutinga hatua hiyo kwa sheria ya bao la ugenini ambapo Mazembe wao walitoka sare ya bila ya kufungana na Etoile de Sahel ya Tunisia jana jijini Lubumbashi na kusonga mbele kwa sare ya bao 1-1 waliyopata ugenini katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza. Kwa upande wa Mo Bejaia wao walisonga mbele baada ya kupata sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya FUS Rabat ya Morocco kufuatia timu hizo kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wao wa kwanza. Fainali ya michuano hiyo ambayo itapigwa kwa mikondo miwili inatarajiwa kufanyika Octoba na Novemba mwaka huu.

DE BRUYNE KUKAA NJE WIKI NNE.

KIUNGO wa Manchester City Kevin De Bruyne anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki nne kufuatia majeruhi ya msuli wa paja aliyopata katika ushindi wa Jumamosi dhidi ya Swansea City. De Bruyne alitolea kufuatia kupata majeruhi hayo katika dakika ya 81 ya mchezo ambao City ilishinda mabao 3-1 na sasa taarifa zinadai kuwa atakaa nje kwa kipindi cha mwezi mmoja. Hatua hiyo sasa inamaanisha De Bruyne atakosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Celtic Jumatano hiipamoja na mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya Tottenham Hotspurs na Everton wakati pia kukiwa na hatihati ya kukosa safari ya kuifuata Barcelona Octoba 19 mwaka huu. Nyota huyo pia atakosa mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia za Ubelgiji ambao watacheza dhidi ya Bosnia-Herzegovina na Gibraltar.

Saturday, September 24, 2016

POGBA AONA MWEZI WAKATI MAN UNITED ILIPOIDHALILISHA LEICESTER.KLABU ya Manchester United imerejesha makali yake ya ushindi katika Ligi Kuu kwa kuwachapa mabingwa Leicester City kwa mabao 4-1 katika Uwanja wa Old Trafford. Nahodha Wayne Rooney aliachwa katika benchi kwenye mchezo huo ambao Chris Smalling alifunga bao la kwanza dakika ya 22 kabla ya Juan Mata hajaongeza la pili dakika ya 37. Muda mchache baadae Mata akaja kutengeneza bao safi lilifungwa na Marcus Rashford dakika ya 40 na Paul Pogba alipigilia msumari wa mwisho kwa kufunga bao lake la kwanza kwa klabu hiyo dakika ya 42. Kipindi cha pili Leicester walijitahidi kurejea mchezoni na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 59 kupitia kwa Demarai Gray.

BABA YAKE YAYA TOURE AMUOMBEA MSAMAHA MWANAYE KWA GUARDIOLA.

BABA wa kiungo wa Manchester City Yaya Toure amemtaka meneja wa klabu hiyo Pep Guardiola kujishusha na kumpa mwanaye nafasi nyingine. Mapema wiki hii Guardiola amesema hatampanga Toure katika kikosi chake tena mpaka pale wakala wake Dimitri Seluk atakapokuja kumuomba radhi kwa kauli aliyotoa katika vyombo vya habari. Mzee huyo aitwaye Mory amesema ana wasiwasi kwani kuna tatizo na anamuomba Guardiola kusamehe na kumruhusu mwanaye kufanya kazi yake. Pamoja na Guardiola kutaka kuombwa radhi na Seluk, wakala huyo alijibu mapigo na kumtuhumu meneja huyo anajidai kuwa kashinda kila kitu hivyo anaweza kufanya chochote anachotaka.

Friday, September 23, 2016

MABADILIKO YA RATIBA LIGI KUU BARA.

BODI ya Ligi kupitia Shirikisho La Mpira wa Miguu Nchini TFF, limetangaza mabadiliko ya ratiba ya ligi na kutangaza tarehe ya mchezo namba 1 wa kiporo baina ya Mabingwa wa Ligi Kuu Vodacom Yanga na JKT Ruvu. Mchezo huo uliokuwa wa ufunguzi wa ligi ulishindikana kuchezwa Agosti 21 baada ya Yanga kuwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya TP Mazembe Nchini Kongo. Bodi ya ligi imeupeleka mchezo huo hadi Oktoba 26 ambapo hapo awali walisema kuwa watatangaza ni lini utachezwa, na katika hilo mchezo namba 57 baina ya Mwadui na Azam, mchezo namba 60 TZ Prisons na Simba utachezwa Novemba 09, mchezo namba 59 Yanga na Ruvu Shooting utapigwa Novemba 10. Mchezo namba 69, Yanga na Mtibwa utachezwa Oktoba 13, mchezo namba 97 Kagera na Azam utapigwa Oktoba 28 na katika mchezo namba 100 baina ya Yanga na Mbao , namba 102 Toto na Mtibwa Sugar utapigwa Oktoba 30, Mtibwa na Mbeya City mchezo namba 113 na namba 115 kati ya Mwadui na Majimaji zote zitapigwa Novemba 07.

ADEBAYOR AKANUSHA KUPOMBEKA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Togo, Emmanuel Adebayor amekanusha taarifa zilizozagaa kuwa uhamisho wake kwenda Olympique Lyon ulikwama kwasababu alivuta sigara na kunywa pombe wakati wa mkutano na meneja wa klabu hiyo. Adebayor amesema kwa kawaida huwa hatoi kauli kwa mazungumzo yeyote ya usajili au tetesi lakini safari hii ameona ni lazima aweke sawa suala hili. Akiwa nje ya mkataba toka alipomaliza kibarua cha katika klabu ya Crystal Palace msimu uliopita, Adebayor mwenye umri wa miaka 32 alisafiri kwenda Lyon Ijumaa iliyopitakukutana na meneja wa klabu hiyo Bruno Genesio. Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Arsenal, Manchester City na Tottenham Hotspurs alikuwa akitegemewa kusaini mkataba wa muda mfupi na klabu hiyo ya Ligue 1 lakini ilishindikana. Adebayor amesema Lyon walitaka kumsajili na walimtumia ndege binafsi kutoka Togo ili awahi kwenda kusaini kwa ajili ya mchezaji wao dhidi ya Marseille na kuongeza kuwa kila kitu kilikuwa tayari kilichobaki ni yeye kufanyiwa vipimo vya afya na kusaini. Nyota huyo aliongeza kuwa hata hivyo hakuwahi kufika kwa wakati kwa ajili ya mchezo huo hivyo badala yake wakaamua kumsajili mshambuliaji mwingine chipukizi.

KUFA NA KUPONA LIGI YA MABINGWA AFRIKA.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajiwa kuendelea tena mwishoni mwa wiki hii kwa timu nne kutafuta nafasi ya kutinga fainali ya michuano hiyo. Katika nusu fainali ya kwanza Zamalek ya Misri itakuwa kama inaenda kukamilisha ratiba itakapokwenda kukwaana na Wydad Casablanca ya Morocco kwa katika mechi ya mkondo wa kwanza mabingwa hao mara tano walishinda kwa mabao 4-0. Kama Wydad wakifanikiwa kuifunga Zamalek na kutinga fainali itakuwa timu ya kwanza kufanya hivyo baada ya kupita miaka 52 wakati timu ya Hafia ya Guinea ilipotoka nyuma ikiwa imefungwa mabao 3-0 na Asec Mimosas ya Ivory Coast na kuja kulipiza kisasi nyumbani kwa kushinda mabao 5-0 mwaka 1976. Katika nusu fainali nyingine Zesco United ya Zambia wataifuata Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini huku wakiwa kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-1 waliopata katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza. Mechi zote mbili za marudiano zitachezwa kesho ambapo Sundowns wataikaribisha Zesco jijini Pretoria na Wydad wakipepetana na Zamalek jijini Rabat.

WENGE APUUZA KITABU KIPYA CHA MOURINHO.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema hatasoma kitabu ambacho meneja wa Manchester United Jose Mourinho amekaririwa akisema atapasua sura ya Mfaransa huyo. Mourinho amekuwa akikwazana mara kadhaa na Wenger wakati akiinoa Chelsea ambapo kuna wakati aliwahi kumuita mtaalamu wa kushindwa. Akihojiwa kuhusiana na kitabu hicho, Wenger amesema yeye anazungumza kuhusu soka na sio jambo lingine lolote na kwasasa anazingatia mchezo wao muhimu wa kesho dhidi ya Chelsea. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kamwe hayuko katika hali kubomoa bali kujenga na amekuwa akimheshimu kila mtu katika mchezo huo wa soka. Wenger amesema kauli iliyotolewa na Mourinho katika kitabu hicho haihusiani na masuala ya soka ndio maana hana mpango wa kushughulika nayo.

QTARA YATIMUA KOCHA.

CHAMA cha Soka cha Qatar kimemtimua kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Jose Daniel Carreno raia wa Uruguay ikiwa imepita miezi 17 toka walipomteua kuiandaa timu hiyo kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi. Uamuzi huo umekuja kufuatia timu hiyo kupoteza mechi zake mbili za kufuzu dhidi ya Iran na Ezbekistan. Haijawekwa wazi ni nani haswa ambaye anaweza kuchukua nafasi ya Carreno lakini kocha mwingine wa Uruguay Jorge Fossati anapewa nafasi kubwa. Kocha mwingine anayepewa nafasi hiyo ni Djamel Belmadi wa Algeria ambaye aliinoa timu hiyo mwaka 2014 hado 2015 wakati Qatar ilipotwaa michuano ya Ubingwa wa Gulf. Kocha mpya atakabiliwa na kibarua kigumu cha kukiandaa kikosi kwa ajili ya mchezo mgumu wa kufuzu dhidi ya Korea Kusini Octoba 6 mwaka huu.

SPURS YAMUONGEZA MKATABA WALKER.

KLABU ya Tottenham Hotspurs, imetangaza kumsainisha mkataba mpya Kyle Walker ambao unatarajiwa kumalizika mwaka 2021. Mkataba wa sasa wa Walker ulikuwa umalizike Juni 2019, lakini klabu hiyo imemua kumuongeza mkataba mwingine kama ilivyofanya kwa nyota wengine wa kikosi cha kwanza akiwemo Christian Eriksen, Dele Alli, Eric Dier na Danny Rose. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, amekuwa akianza katika kikosi cha kwanza toka msimu wa 2011-2012 na ameisaidia Spurs kumaliza katika nafasi ya tatu chini ya meneja Mauricio Pochettino msimu uliopita. Akihojiwa kuhusiana na hilo, Walker amesema ni heshima kubwa kwake na amemshukuru mwenyekiti pamoja na meneja kwa kuwa na imani naye.

KLOPP AITETEA LIVERPOOL.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp ametetea suala la usajili katika kipindi cha nyuma baada ya taarifa kuonyesha kuwa klabu hiyo wamekuwa wauzaji wakubwa katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Taarifa hiyo imegundua kuwa Liverpool wameingiza kiasi cha euro milioni 442 kwa kuuza wachezaji katika kipindi cha miaka sita iliyopita huku Valencia wakishikilia nafasi ya pili kwa kuingiza kiasi cha euro 432 wakifuatiwa na Juventus nafasi ya tatu kwa kuingiza euro milioni 415. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Klopp amesema klabu hiyo kwasasa imebadilika sana na hakuna haja ya kuwa watu wa kuuza wachezaji. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kwasasa wanachofanya ni kuimarisha kikosi walichinacho na kuongeza wachezaji wengine kadri itakavyohitajika.

BARCELONA INAWEZA KUSHINDA BILA MESSI - INIESTA.

KIUNGO wa Barcelona, Andres Iniesta amedai kuwa klabu hiyo inaweza kusonga mbele bila kuwepo nyota wao Lionel Messi. Messi alitolewa kufuatia kupata majeruhi ya nyonga katika mchezo wa Jumatano iliyopita dhidi ya Atletico Madrid ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 na sasa anategemewa kukaa nje kw akipindi cha wiki tatu. Pamoja na umuhimu wa Messi katika kikosi cha Barcelona, Iniesta amesema wanaweza kusonga mbele bila yeye kama wakiungana na kucheza kama timu. Iniesta aliendelea kudai kuwa anafahamu kuwa kikosi chao ni imara wakiwa na Messi lakini ni kiosi kizima ndicho kinachoshinda mataji hivyo ni matumaini yake wataendelea kucheza kwa umoja ili kupata matokeo. Mesi akiwa hayupo, Barcelona itakabiliwa na mechi tatu za ugenini ambazo ni dhidi ya Sportinh Gijon, Borussia Monchengladbach na Celta Vigo. Pia nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 anatarajiwa kukosa michezo ya kufuzu Kombe la Dunia ambapo Argentina itacheza dhid ya Peru na Paraguay Octoba 6 na 11 mwaka huu.

Thursday, September 22, 2016

RASMI: BUSQUETS ASAINI MITANO MIPYA.


KIUNGO wa Barcelona, Sergio Busquets amesaini rasmi mkataba mpya wa muda mrefu na klabu yake hiyo ya utotoni. Makubaliano kati ya pande zote mbili yaani klabu na mchezaji mwenyewe yalikuwa yameshaafikiwa toka Mei mwaka huu na kilichobakia kilikuwa ni kuwekeana na saini. Busquets sasa atabakia Barcelona mpaka 2021, huku kukiwa na kipengele cha kuongezewa miaka mingine miwili mpaka 2023. Taarifa hizo zimekuwa kama ahueni kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye alitolea mapema katika kipindi cha pili baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Atletico Madrid jana usiku.

FALCAO BADO HALI TETE.

KOCHA wa AS Monaco, Leonardo Jardim amethibitisha Radamel Falcao bado ameendelea kubakia hospitali baada ya kupata mtikisiko wa ubongo katika mchezo wa Ligue 1 ambao walitandikwa mabao 4-0 na Nice. Falcao alianguka chini katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza baada ya kugongana vibaya na kipa wa Nice Yoan Cardinale na alikimbizwa hospitali kwa ajili ya vipimo zaidi. Jardim alimkosoa mwamuzi kwa kushindwa kutoa penati kwa mchezo mbaya ulioonyeshwa na Cardinale. Akihojiwa kuhusu hali ya Falcao, Jardim amesema bado yupo hospitali akiendelea kupatiwa matibabu kwa tukio lililomkuta jana. Jardim aliendelea kudai kuwa waamuzi wanapaswa kuyaangalia matukio hayo kwa ukaribu kwani anadhani kipa wa Nice alipaswa kupewa kadi nyekundu.

MOURINHO NA GUARDIOLA KUKUTANA TENA KOMBE LA LIGI.

MAHASIMU wa jiji la Manchester klabu za Manchester United na Manchester City zinatarajiwa kukwaana katika mzunguko wa nne wa michuano ya Kombe la Ligi, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford. United ilitinga hatua hiyo kwa kuitoa timu ya daraja la kwanza ya Northampton jana wakati City wao waliwatoa Swansea City kwa kuichapa mabao 2-1 na kupelekea timu hizo kukutana kwa mara ya pili msimu huu baada ya ile derby ya Septemba 10. Mechi zingine za hatua hiyo, West Ham United watakuwa wenyeji wa Chelsea, Tottenham Hotspurs wao watasafiri kuifuata Liverpool, Newcastle United watakwana na Preston huku Norwich City wakiivaa Leeds United. Wengine ni Hull City watakaocheza Bristol City, Southampton dhidi ya Sunderland na Arsenal wao watapambana na Reading. Mechi hizo zote zinatarajiwa kuchezwa wiki ya kuanzia Octoba 24 mwaka huu.

MESSI NJE WIKI TATU.


MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki tatu baada ya kupata majeruhi ya nyonga katika sare ya bao 1-1 waliyopata dhidi ya Atletico Madrid. Nyota huyo alitolewa katika dakika ya 59 ya mchezo huo baada ya kukwatuliwa na Diego Godin. Messi alilazimika kukosa mchezo wa Argentina wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Venezuela mapema mwezi huu kutokana na matatizo kama hayo lakini amefanikiwa kucheza mechi zote za La Liga msimu huu. Kama hali ikiendelea vyema Messi anatarajiwa kurejea katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City Octoba 19 maka huu.

Wednesday, September 21, 2016

UEFA YAZINDUA LOGO MPYA YA EURO 2020.

RAIS mpya wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, Aleksander Ceferin amebainisa logo mpya itakayotumika katika michuano ya Ulaya 2020 katika sherehe zilizofanyika jijini London mapema leo. Logo hiyo inaonekana ikiwa katika rangi tofauti huku picha za mfano wa mashabiki wakiwa pande zote kulizunguka kombe la michuano hiyo ikiwakilisha uhusiano wa nchi 13 wenyeji. Michuano hiyo ya 2020 itafanyika katika miji 13 tofauti barani Ulaya ili kusheherekea miaka 60 toka kuanzishwa kwake, huku nusu fainali na fainali zikitarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Wembley nchini Uingereza. Akizungumza katika sherehe hizo, Ceferin amesema UEFA inataka michuano ya 2020 kuwa ya kweli kushangilia mafanikio ya mchezo huo unaopendwa na kutukuzwa. Mechi zingine za michuano hiyo pia zitachezwa katika nchi za Azerbaijan, Ubelgiji, Denmark, Ujerumani, Hungary, Ireland, Italia, Uholanzi, Romania, Urusi, Scotland na Hispania.

KLOPP AWAPA TANO WACHEZAJI WAKE.MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amepongeza ushindi wa mabao 3-0 waliopata katika mchezo wa mzunguko wa tatu wa Kombe la Ligi dhidi ya Derby County jana usiku lakini amesisitiza kuwa bado kuna nafasi ya kuimarika zaidi. Liverpool wametinga hatua ya 16 bora ya michuano hiyo kwa mabao yaliyofungwa na Ragnar Klavan, Philippe Coutinho na Divock Origi katika mchezo uliofanyika katika Uwanaj wa iPro. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Klopp alikipongeza kikosi chake kwa uwezo mkubwa walioonyesha na kuamini kuwa wanaweza kuimarika zaidi ya ilivyo hivi sasa. Klopp amesema walikuwa bora na walistahili kushinda kwa jinsi walivyotengeneza nafasi kufunga na kuzitumia. Pamoja na ushindi huo Klopp anaamini bado kuna mapungufu kadhaa ya kufanyia kazi ili waweze kuimarika zaidi.

CONTE AKATAA KUMUHAKIKISHIA FABREGAS.MENEJA wa Chelsea, Antonio Conte amesifu mabao mawili yaliyofungwa na Cesc Fabregas lakini amesisitiza sifa hizo hazimaanishi chochote baada ya kutoka nyuma na kuichapa Leicester City jana. Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania alifunga mabao hayo katika muda wa nyongeza baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 katika muda wa kawaida katika mchezo huo wa mzunguko wa tatu wa Kombe la Ligi na kuwafanya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2. Fabregas bado hajapata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu chini ya Conte huku mchezo pekee mwingine alioanza ulikuwa ni ule wa Kombe la Ligi dhidi ya Bristol City mwezi uliopita. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Conte amesema anataka ushindi na chaguo la kikosi chake hufanyika ili kupata ushindi na huwa hajali majina yao. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kwa upande wake jambo muhimu wakati anapomwita mchezaji ni kumuonyesha kuwa hajafanya kosa kufanya hivyo.

WENGER AMMWAGIA SIFA PEREZ.MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amependa alichokiona kutoka kwa mshambuliaji wake mpya Lucas Perez katika ushindi waliopata katika mchezo wa Kombe la Ligi dhidi ya Nottingham Forest jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alifunga mabao yake mawili ya kwanza katika klabu kwenye ushindi wa mabao 4-0 iliyopata Arsenal jana. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Wenger alimsifu mshambuliaji huyo kwa kiwango kikubwa alichoonyesha haswa bao la pili alilofunga. Wenger amesema bao la pili alilofunga Perez limeonyesha ubora wake kiufundi, nia na morali ya kupambana.

Tuesday, September 20, 2016

BALE, RONALDO WAREJEA KIKOSI CHA MADRID.

MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amethibitisha kuwa Cristiano Ronaldo na Gareth Bale watakuwepo katika dhidi ya Villarreal utakaochezwa kesho. Nyota hao wawili walikosa mchezo wa Jumapili iliyopita dhidi ya Espanyol kutokana na majeruhi na maradhi. Hata hivyo, haikuwadhuru sana Madrid kwani walishinda mchezo huo kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na James Rodriguez na Karim Benzema na kuendeleza rekodi yao nzuri ya ushindi. Akihojiwa kuelekea katika mchezo huo, Zidane amesema Bale na Ronaldo wako tayari hivyo atawatumia katika kikosi chake. Hata hivyo, Madrid watamkosa beki wao Pepe ambaye hakufanya mazoezi leo lakini mabeki wengine wanne waliobakia wako fiti.

GUARDIOLA ATAKA KUOMBWA RADHI ILI AMPE NAFASI YAYA TOURE.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema Yaya Toure ataichezea timu hiyo tena pale tu atakapopokea msamaha kwa kauli iliyotolewa na wakal wa mchezaji huyo. Hata hivyo, haiku wazi kama Guardiola anataka msamaha kutoka kwa kiungo huyo au wakala wake. Wakala wa Toure, Dimitri Seluk amedai mteja wake alidhalilishwa kwa nje ya kikosi cha klabu hiyo kinachoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuongeza Guardiola anapaswa kumuomba radhi kama City wakishindwa kutwaa taji hilo. Akiongea na wanahabari mapema leo, Guardiola amesema anapaswa kuwaomba radhi wachezaji wenzake na klabu na kama hatafanya hivyo hatacheza. Wakati huohuo, Toure mwenyewe ametanagza kustaafu soka la kimataifa baada ya kuitumikia Ivory Coast kwa miaka 12. Toure mwenye umri wa miaka 33 ambaye alianza kuitumikia nchi hiyo mwaka 2004, amesema anadhani wakati umefika wa kuacha nafasi kwa vijana wengine wanaochipukia nao kupata nafasi ya kuliwakilisha taifa lao.

SIMEONE AMMWAGIA SIFA NEYMAR.

MENEJA wa Atletico Madrid, Diego Simeone amemsifia neymar kuelekea mchezo wao dhidi ya Barcelona utakaochezwa kesho. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akisolewa vikali aina ya maisha huku wengine wakienda mbali kwa kumwambia hajitumi akiwa na Brazil wakati alipoonekana akijirusha sehemu mbalimbali wakati wa michuano ya Copa America. Hata hivyo, Neymar aliwajibu wakosoaji hao uwanjani kwa kuiongoza nchi yake kutwaa medali ya dhahabu ya Olimpiki Agosti mwaka huu. Akihojiwa kuhusiana na Neymar, Simeone amesema nyota huyo ni aina ya wachezaji ambao anawapenda kwani aina ya uchezaji wake ni wa kipekee. Neymar ni mmoja ya wachezaji wanaopewa nafasi ya kutwaa tuzo ya Ballon d’Or sambamba na Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Antoine Griezmann.

KIPA WA CHELSEA ATAMANI KUREJEA HISPANIA.

KIPA wa Chelsea, Thibaut Courtois amekiri anataka kurejea La Liga na anaweza asiongeze mkataba mpya katika klabu hiyo ili kurahisisha kuhamia Hispania. Courtois alijiunga na Chelsea akitokea Genk mwaka 2011 na haraka alipelekwa kwa mkopo Atletico Madrid kwa kipindi cha misimu mitatu iliyofuata. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alicheza kwa mafanikio Atletico na kuisaidia kushinda taji la La Liga mwaka 2014 pamoja na Kombe la Mfalme mwaka 2013 na pia Europa League mwaka 2012. Akihojiwa kipa huyo amebainisha kuwa alilia wakati mkataba wake na klabu hiyo ulipomalizika na amepania kurejea tena Hispania katika siku za usoni.

Monday, September 19, 2016

RAIS WA LYON ADAI BENCHI LA UFUNDI NDIO LILIMPIGA CHINI ADEBAYOR.

RAIS wa Olympique Lyon, Jean-Michel Aulas amedai meneja Bruno Genesio na benchi lake la ufundi ndio walichukua uamuzi wa kumsajili Jean-Philippe Mateta badala ya Emmanuel Adebayor. Adebayor ambaye ni mchezaji huru alikuwa akitegemewa kujiunga na klabu hiyo ya Ligue 1 wiki iliyopita lakini dili hilo halikukamilika kama ilivyotarajiwa. Lyon ilieleza sababu za kumuacha mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 32 kuwa ni kukosekana kwake katika michuano ya Mataifa ya Afrika pamoja na kutoweza kushiriki hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Aulas amesema Mateta mwenye umri wa miaka 19 ambaye amechukuliwa kutoka Chateauroux, alionyesha ni mtu sahihi kusajiliwa kuliko mkataba wa kipindi kifupi ambao angepewa Adebayor. Aulas amesema kutokana na kuumia kwa Alexandre Lacazette walikuwa wakitafuta mchezaji wa safu ya ushambuliaji ili kuziba nafasi hiyo na walikuwa na machaguo mengi kabla ya kocha na benchi lake kuamua kumchukua Mateta.

ALLEGRI ATETEA HATUA YAKE YA KUMTEMA HIGUAIN KATIKA KIKOSI CHA KWANZA.

MENEJA wa Juventus, Massimiliano Allegri amekingia kifua uamuzi wake wa kumuacha katika kikosi cha kwanza Gonzalo Higuain katika mchezo waliofungwa mabao 2-1 na Inter Milan jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina alisajiliwa na mabingwa hao wa Serie A kwa ada iliyovunja rekodi ya klabu ya euro milioni 90 akitokea Napoli Julai mwaka huu na mpaka sasa ameshafunga mabao matatu katika mechi tatu za ligi alizocheza. Lakini katika mchezo wa jana nyota huyo aliachwa benchi na kushuhudia Juventus wakipata kipigo chao cha kwanza kwa msimu huu wa 2016-2017. Akihojiwa Allegri alitetea uamuzi wake akidai kuwa alitaka kucheza mchezo wa kutumia nguvu zaidi hivyo alimuhitaji wakati mchezo ukiwa unaendelea na sio mwanzo. Juventus ambao sasa wako nyuma ya vinara Napoli kwa tofauti ya alama moja wanakabiliwa na mchezo dhidi ya Cagliari Jumatano hii.

KLOPP ATAMBIA VIKOSI VYAKE.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amedai hana mpango wowote wa kuwapumzisha wachezaji wanaoonekana kuwa fiti wakati wa mchezo wao wa mzunguko wa tatu wa Kombe la Ligi dhidi ya Derby County. Klopp anaamini kuwa kila kikosi atakachokitumia msimu huu kitakuwa kiko vizuri. Liverpool wanatarajiwa kusafiri kwenda Pride Road kesho jioni kwa ajili ya mchezo huo ambapo watakuwa wakijaribu kuendelea rekodi yao nzuri ya kushinda mechi nne mfululizo zilizopita. Akihojiwa Klopp amesema kwa mawazo yake vikosi vyote alivyonavyo ni imara hivyo hana shaka na mchezo wao huo wa kesho.

Cuplikan Gol Watford vs Manchester United | 3 - 1

Friday, September 16, 2016

BALLON D'OR "KUSHNEY"

TAARIFA zinadai kuwa mwisho wa Ballon d’Or unakaribia kufuatia Shirikisho la Soka Duniani-FIFA na Shirikisho la Soka la Ufaransa-FFF kumaliza mkataba wao. FIFA Ballon d’Or ilitambulishwa mwaka 2010 kama jina rasmi la tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia kufuatia makubaliano na FFF. Hata hivyo, tuzo za mwaka huu zinaweza kuwa za mwisho za aina yake kufuatia Ufaransa kuchukua umiliki wa jina lao na kuhamisha mji mwenyeji kutoka Zurich. Kumalizika kwa mkataba huo kunamaanisha kuwa sasa tuzo hizo zitatumia jina lake halisi la Mchezaji bora wa Dunia huku rais wa FIFA Gianni Infantinho na maofisa wengine wakijaribu kutafuta jina muafaka kwa ajili ya sherehe hizo. Kutokana na hilo, FIFA imesema inaangalia uwezekano wa kuhamisha tukio hilo katika miji tofauti kila mwaka huku jiji la London likitajwa kuwa linaweza kuwa la kwanza kuandaa sherehe hizo.


NUSU FAINALI LIGI YA MABINGWA KUCHEZWA MWISHONI MWA WIKI HII.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajiwa kuendelea tena mwishoni mwa wiki hii kwa mechi za hatua ya nusu fainali kuchezwa katika viwnaja tofauti. Kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 15 michuano hiyo itashuhudia timu kutoka ukanda wa kusini mwa Afrika zikimenyana ambapo Zesco United ya Zambia itakwaana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Afrika Kaskzini imekuwa ikitawala michuano hiyo huku timu za Misri, Tunisia, Morocco na Algeria zikishinda taji hilo mara 28 kati ya 51 huku Afrika ya kati wakilitwaa mara 12 na Afrika Magharibi mara 10. Kutokana na utawala huo wa Afrika Kaskazini sio jambo la kushangaza kuona mchezo mwingine wa nusu fainali ya michuano hiyo ukihusisha timu zao ambapo mabingwa mara tano Zamalek ya Misri watakwanaa na Wydad Casablanca ya Morocco ambao wamewahi kutwaa taji hilo mara moja. Mchezo huo wa mkondo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa jijini Alexandria baadae leo huku ule wa Zesco na Sundowns ukitarajiwa kufanyika huko Ndola nchini Zambia kesho mchana.