MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Togo, Emmanuel Adebayor amekanusha taarifa zilizozagaa kuwa uhamisho wake kwenda Olympique Lyon ulikwama kwasababu alivuta sigara na kunywa pombe wakati wa mkutano na meneja wa klabu hiyo. Adebayor amesema kwa kawaida huwa hatoi kauli kwa mazungumzo yeyote ya usajili au tetesi lakini safari hii ameona ni lazima aweke sawa suala hili. Akiwa nje ya mkataba toka alipomaliza kibarua cha katika klabu ya Crystal Palace msimu uliopita, Adebayor mwenye umri wa miaka 32 alisafiri kwenda Lyon Ijumaa iliyopitakukutana na meneja wa klabu hiyo Bruno Genesio. Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Arsenal, Manchester City na Tottenham Hotspurs alikuwa akitegemewa kusaini mkataba wa muda mfupi na klabu hiyo ya Ligue 1 lakini ilishindikana. Adebayor amesema Lyon walitaka kumsajili na walimtumia ndege binafsi kutoka Togo ili awahi kwenda kusaini kwa ajili ya mchezaji wao dhidi ya Marseille na kuongeza kuwa kila kitu kilikuwa tayari kilichobaki ni yeye kufanyiwa vipimo vya afya na kusaini. Nyota huyo aliongeza kuwa hata hivyo hakuwahi kufika kwa wakati kwa ajili ya mchezo huo hivyo badala yake wakaamua kumsajili mshambuliaji mwingine chipukizi.
No comments:
Post a Comment