Monday, June 30, 2014

KOMBE LA DUNIA 2014: RAIS WA URUGUAY AWATUSI FIFA.

RAIS wa Uruguay Joe Mujica amewatolea maneno ya kuwatusi viongozi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kutokana na kumfungia Luis Suarez kujishughulisha na shughuli zozote za kimichezo kwa miezi minne. Rais huyo mwenye umri wa miaka 79 aliielezea adhabu hiyo ambayo pia inahusisha kumfungia nyota huyo mechi tisa za kimataifa kuwa ya mabavu. Suarez alipewa adhabu hiyo ambayo ni kali zaidi katika historia ya Kombe la Dunia kwa kosa la kumng’ata beki wa Italia Giorgio Chiellini. Mujica anajulikana kwa tabia yake ya kuzungumza kile anachojikia mahali popote bila ya uoga. Rais huyo alitoa kauli hiyo katika luninga wakati wa mapokezi ya timu ya taifa ya nchi hiyo kufuatia kuondolewa katika hatua ya timu 16 bora na Colombia ambapo mara baada ya kutoa lugha hiyo ya matusi alishika mdomo lakini aliwaruhusu waandishi wa habari kuitoa kauli hiyo kama ilivyo.


AC MILAN YASIMAMISHA MATUMIZI YA JEZI NAMBA 4 KWA HESHIMA YA ZANETTI.

KLABU ya Inter Milan imeamua kusimamisha matumizi ya jezi yenye namba nne mgongoni kwa heshima ya Javier Zanetti na wanatarajia kumteua beki huyo wa kulia aliyestaafu hivi karibu kuwa makamu wa rais wa klabu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. Mkongwe huyo wa Argentina aliamua kutundika daruga zake rasmi mwaka huu baada ya kuitumikia Inter kwa kipindi cha miaka 19, ambapo alifanikiwa kushinda mataji matano ya Serie A, manne ya Kombe la Italia, taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia. Rais wa klabu hiyo Erick Thohir amebainisha kuwa sasa Inter itaondoa namba aliyokuwa akivaa nyota huyo kwenye jezi zake ili kumpa heshima kwa kipindi alichofanya kazi hapo pamoja na kumpa nafasi hiyo muhimu kwenye timu hiyo. Thohir amesema uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha bodi walichokutana kujadili jinsi ya kumuenzi mkongwe huyo kwa utumishi wake uliotukuka katika timu hiyo.

KOMBE LA DUNIA 2014: KLM YAOMBA RADHI MASHABIKI WA MEXICO KWA KUTUMA UJUMBE WA UTANI KWENYE AKAUNTI YAKE RASMI YA TWITTER.

SHIRIKA la Ndege la Uholanzi, KLM limeomba radhi kwa kutuma ujumbe kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwatania Mexico kutokana kipigo walichopata kutoka kwa Uholanzi kwenye michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Brazil. Ndani ya muda wa dakika chache kutoka Uholanzi ipate ushindi wa mabao 2-1 katika dakika za majeruhi, kulitumwa picha yenye bando la kuondoka huku kukiwa na kichwa cha habari kilichosomeka kwa lugha ya kireno Adios Amigos wakimaanisha Kwaherini Marafiki. Pembeni ya bango hilo la kuondokea kukawekwa picha wa mtu akiwa na mstachi pamoja na kofia kubwa aina ya sombrero ikieleza uhahilisia wa watu wa Mexico lakini muda mfupi baadae walifunta ujumbe huo. Mwigizaji maarufu wa Mexico Gael Garcia Bernal naye aliandika katika ukurasa wake wa twitter akiwahabalisha mashabiki zaidi ya milioni mbili wanaomfuata kuwa hatasafiri tena kwa ndege za shirika hilo na mamia ya watu kuonekana kulalamikia tukio hilo. Msemaji wa KLM Lisette Ebeling Koning baadae aliwaambia waandishi wa habari kuwa ujumbe ule ulikuwa ni wa utani lakini watu wengi wameochukulia tofauti. Koning aliendelea kudai haikuwa nia ya shirika hilo kuwaudhi watu wa Mexico ambao wanawahudumia kwa ndege ya kila siku ya shirika hilo kati ya Mexico City na Amsterdam na kuwaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.

KAKA KUJIUNGA NA SAO PAULO KABLA YA KWENDA ORLANDO CITY.

MAKAMU wa raia wa klabu ya Sao Paulo Ataide Gil Guerreiro amedai kuwa kiungo mahiri wa klabu ya AC Milan, Kaka anatarajiwa akujiunga na nao kwa mkopo kabla ya kuhamia katika timu ya Orlando City. Kaka alirejea Milan katika kipindi cha usajili cha majira ya kiangazi mwaka jana baada ya kukaa Real Madrid kwa miaka minne lakini kulikuwa na kipengele katika mkataba wake kinachomruhusu kuondoka kama timu hiyo ikishindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 sasa anapanga kurejea katika timu yake ya kwanza ya sao Paulo lakini kwa mkopo wa kipindi kifupi kabla ya kusaini mkataba wa muda mrefu na timu ya Orlando City inayoshiriki Ligi Kuu nchini Marekani-MLS mwaka 2015. Guerreiro amesema baada ya siku 60 za mazungumzo hatimaye wamefikia makubaliano lakini hakuna chochote rasmi kilichofanyika. Kaka aliibukia katika shule ya soka ya sao Paulo na kuifungia timu hiyo mabao 23 katika mechi 59 alizocheza katika timu hiyo kati ya mwaka 2001 na 2003 na baadae kwenda barani Ulaya kuichezea Milan ambapo aliitumikia kwa miaka sita akifanikiwa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa na Serie A.

KOMBE LA DUNIA 2014: MOURINHO AUNGA MKONO ADHABU YA WALIYOTOA FIFA DHIDI YA SUAREZ.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amedai kutokubaliana na adhabu ya kumfungia Luis Suarez kwenda uwanjani kufuatia nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay kumng’ata beki wa Italia Giorgio Chiellini. Mourinho amekubaliana na adhabu ya kutocheza kwa muda aliyopewa mshambuliaji huyo wa Liverpool lakini haoni tatizo kwa Suarez kuhudhuria uwanjani kutizama mechi. Akizungumza na mtandao wa Yahoo, Mourinho ambaye pia kuzinoa timu za Reala Madrid na Inter Milan amesema Suarez alistahili adhabu aliyopewa kutokana na kurudia tukio hilo mara kwa mara ila kitu ambacho hakikumfurahisha na kumfungia kwenda uwanjani kuangalia timu yake ikicheza.

KOMBE LA DUNIA 2014: MAPUMZIKO YA DHARURA YALINISAIDIA KUBADILISHA MBINU KATIKA KIKOSI CHANGU - VAN GAAL.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal amesema ametumia mapumziko ya kwanza kwa ajili ya kunywa maji katika Kombe la Dunia kubadilisha mbinu katika kikosi chake ambacho kilitoka nyuma na kuifunga Mexico kwa mabao 2-1. Mabao kutoka kwa Wesley Sneijder na Klaas Jan Hunterlaar katika dakika za majeruhi yalitosha kuisaidia Uholanzi kupata nafasi ya kucheza katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayoendelea nchini Brazil. Van Gaal amesema mara ya kwanza alibadilisha mfumo kutoka 4-3-3 na baadae kutengeneza nafasi nyingi. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa baada ya hapo alihamia katika mpango B na alifanya hivyo katika muda wa mapumziko ya kunywa maji, kwani ndio ilikuwa njia pekee sahihi ya kutumia mwanya huo.A

KOMBE LA DUNIA 2014: KOCHA WA ALGERIA AKWEPA KUULIZWA MASWALI YA MFUNGO WA RAMADHANI KWA WACHEZAJI WAKE.

KOCHA wa timu ya taifa ya Algeria, Vahid Halilhodzic kubainisha ni wachezaji gani waislamu katika kikosi chake ambao watafunga mwezi mtukufu wa Ramadhani katika mchezo wa mtoano dhidi ya Ujerumani utakaochezwa baadae leo usiku. Siku thelathini za mfungo wa Ramadhani zimeanza jana na kocha huyo mwenye umri wa miaka 30 alionekana kukwepa maswali kuhisiana na suala hilo wakati wa mkutano wake na waandhisi wa habari. Kocha huyo raia wa Bosnia amesema suala hilo ni la binafsi zaidi na wakati ukiluliza swali hilo unakuwa unakosa heshima na maadili. Halilhodzic aliendelea kudai kuwa hawezi kuingilia imani ya mchezaji yeyote kwani wanaweza kufanya watakavyoataka. Kufunga Ramadhani kwa waislamu ni moja kati ya nguzo muhimu za dini hiyo, ingawa kuna baadhi ya watu kama wagonjwa, wajawazito, wasiojiweza na wazee ambao wanaruhisiwa kutokufunga. Nahodha wa Algeria Madjid Bougherra ameeleza kuwa atafunga mwezi huu mtukufu lakini kiungo wa Ujerumani Mesut Ozil na beki wa Ufaransa Bacary Sagna wote wamedai kuwa hawatafunga.

RIPOTI YABAINISHA PISTORIUS HAKUWA NA MATATIZO YOYOTE YA KIAKILI WA AKIFANYA MAUAJI YA MEPANZI WAKE.

KESI ya mauaji ya mwanariadha nyota mlemavu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius imeendelea tena leo baada ya kusimamishwa kwa muda ili aweze kufanyiwa vipimo vya akili kwa mara nyingine. Taarifa kutoka kliniki ya magonjwa ya akili alipokuwa akifanyiwa vipimo mwanariadha huyo imedai kuwa Pistorius hakuwa na tatizo lolote kiakili wakati akimuua mpenzi wake. Mawakili wake wa utetezi wamedai kuwa Pistorius hakuwa katika hali yake ya kawaida wakati alipomfyatulia risasi mpenzi wake. Mwanariadha huyo amekata shitaka la kumuua Reeva Steenkamp kwa makusudi na kudai kuwa ilikuwa bahati mbaya wakati alipoingiwa na hofu na kudhani kuwa alikuwa amevamiwa na majambazi. Pande mbili za mashitaka na utetezi zimekuwa taarifa hiyo. Steenkamp mwenye umri wa miaka 29 aliyekuwa mwanamitindo na mwanasheria, alipigwa risasi kipitia mlango wa bafuni katika nyumba ya Pistorius iliyopo jijini Pretoria katika siku ya wapendanao wamaka jana.

KOMBE LA DUNIA 2014: ROBBEN AKIRI KUJIRUSHA NA KUOMBA RADHI.

WINGA mahiri wa timu ya taifa ya Uholanzi, Arjen Robben ameomba radhi na kukiri kuwa alijirusha wakati nchi yake ikiitandika Mexico kwa mabao 2-1 katika hatua ya timu 16 bora kwenye michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Brazil lakini amedai hakujirusha walivyopewa penati. Klaas Jan Hunterlaar alifunga bao la ushindi la Uholanzi kwa penati kwenye muda wa majeruhi baada ya Robben kufanyiwa faulo. Kocha wa timu ya taifa ya Mexico Miguel Herrera alimtuhumu Robben kwa kujirusha mara tatu kwenye mchezo huo lakini winga huyo aliomba radhi kwa kujirusha katika kipindi cha kwanza. Robben aliendelea kudai kuwa penati waliyopewa dakika za mwisho ilikuwa halali kwasababu kweli alifanyiwa madhambi. Robben alifanyiwa faulo na nahodha wa Mexico katika dakika ya 94 ya mchezo huo lakini Herrera anadhani mchezaji huyo wa klabu ya Bayern Munich hakutakiwa kuwepo uwanjani kuweza kuipatia timu yake penati.

Friday, June 27, 2014

KOMBE LA DUNIA 2014: ALGERIA WAPANIA KULIPIZA KISASI CHA MWAKA 1982.

KOCHA wa timu ya taifa ya Algeria Vahid Halilhodzic amesisitiza kuwa Algeria hawajasahau utata uliopelekea kuenguliwa katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1982 wakati wakijiandaa na mchezo wao dhidi ya Ujerumani katika hatua ya timu 16 bora. Sare ya bao 1-1 dhidi ya Urusi jana iliiwezesha Algeria kufuzu hatua hiyo kwa mara ya kwanza toka waanze kushiriki michuano hiyo. Ushindi wa Ujerumani Magharibi waliopata dhidi ya Austria miaka 32 iliyopita uliruhusu timu hizo kufuzu hatua inayofuata na kuiacha Alegria. Katika michuano hiyo ya mwaka 1982 Algeria walimaliza mechi zao tatu za makundi wakiwa wameshinda mara mbili na kufungwa moja lakini mabo yalibadilika katika mchezo wa mwisho kati ya West Germain na Austria ambapo mpaka leo inahisiwa suala la upangaji matokeo lilifanyika ili kuzifanya timu hizo kufuzu. Kocha Halilhodzic amesema hawajasahau tukio hilo kwasababu kila mtu amekuwa akizungumzia kuhusu Algeria na Ujerumani toka mwaka 1982. Maofisa wa soka wa Algeria walipinga na kudai mechi hiyo ilipangwa lakini tuhuma zao hazikuwahi kuthibitishwa, hata hivyo matokeo ya utata huo ndio yaliyopelekea mechi za mwisho za makundu katika michuano hiyo kuchezwa muda mmoja ili kuepusha suala la kupanga matokeo.

WADHAMINI WAANZA KUMKIMBIA SUAREZ KWA UPUUZI WAKE.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Uruguay Luis Suarez amempoteza mmoja wa wadhamni wake baada ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa kumng’ata beki Giorgio Chiellini wa Italia. Kampuni ya kamari katika mtandao ya 888poker wamesema wameamua kusitisha mahusiano yao na mchezaji huyo kutokana na tukio lake hilo. Suarez mwenye umri wa miaka 27 ambaye pia ancheza katika klabu ya Liverpool amefungiwa miezi minne kujishughulisha na masuala ya soka kutokana na tukio hilo. Adhabu hiyo itamfanya Suarez kutocheza soka kwa nchi yake au klabu mpaka mwishoni mwa Octoba mwaka huu. Uruguay inatarajiwa kucheza na Colombia katika hatua ya timu 16 bora kesho baada ya kufuzu kutoka katika kundi B nyuma ya Costa Rica. Mbali na adhabu hiyo, FIFA pia imefungia mchezaji huyo mechi tisa za kimataifa huku akitozwa faini ya euro 82,000.

KOMBE LA DUNIA 2014: OBAMA ATIZAMA MECHI YA MAREKANI NA UJERUMANI KATIKA AIR FORCE ONE.

RAIS wa Marekani Barack Obama ameonyesha jinsi umuhimu wa michuano ya Kombe la Dunia ulivyo kwa Wamarekani kwa kuitizama nchi yake ikichuana na Ujerumani katika kundi G akiwa katika ndege yake ya Air Force One. Obama alikuwa akisafiri kutoka Maryland kuelekea Minnesota wakati Marekani ikicheza mechi yake hiyo muhimu na alihakikisha hataki kukosa chochote kutokana na mchezo huo kurushwa moja kwa moja katika Air Force One. Kikosi cha Marekani kinachonolewa na Jurgen Klinsmann kilifungwa bao 1-0 na Ujerumani lakini bado walifanikiwa kufuzu katika hatua ya mtoano kwa tofauti nzuri ya mabao ukilinganisha na Ureno ambao nao waliifunga Ghana kwa mabao 2-1 katika mchezo wa mwisho. Michuano hii ya Kombe la Dunia imegusa hisia za raia wengi wa Marekani ambapo zaidi ya mashabiki 15,000 wanadaiwa kukusanyika sehemu ya wazi jijini Chicago kuangalia mechi kati ya nchi hiyo na Ureno, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya mashabiki nchini humo kukusanyika kuangalia mechi ya Kombe la Dunia. Klinsmann ambaye ni mchezaji wa zamani wa ujerumani, aliandika barua ya wazi kwa raia wote wa Marekani kuwaomba kutenga muda wao kutazama mchezo huo barua ambayo ilijibiwa haraka na gavana wa New York Andrew Cuomo aliyetoa amri kwa waajiri wote kuongeza muda wa mapumziko ya chakula cha mchana kwa ajili ya kuangalia mchezo huo. Hii ni mara pili mfululizo kwa Marekani kutinga hatua ya timu 16 bora katika michuano ya Kombe la Dunia baada ya kumaliza mbele ya Uingereza katika michuano ya mwaka 2010.

BOLT YUKO TAYARO KUSHIRIKI JUMUIYA YA MADOLA.

BINGWA mara sita wa michuano ya olimpiki, Usain Bolt amesema atakuwepo kwa ajili ya mashindano ya Jumuiya ya Madola inayotarajiwa kufanyika jijini Glascgow, Scotland baadae mwaka huu. Bolt mwenye umri wa miaka 27 raia wa Jamaica amesema anaweza asishiriki michuano ya mmoja mmoja lakini anaweza kukimbia katika mbio za kupokezana vijiti. Nyota huyo ambaye ameshinda medali za dhahabu katika mbio za mita 100, 200 na mita 400 kupokezana vijiti katika mashindano ya olimpiki mwaka 2008 na 2012, amekuwa akijiuguza majeraha ya mguu. Bolt aliandika katika mtandao wake kuwa yuko tayari kwa ajili ya uchaguzi kwa ajili ya michuano ya Jumuiya ya Madola na ameshapeleka nyaraka zote zinazohitajika. Hata hivyo mwanariadha huyo hatakuwa fiti vya kutosha kushiriki mashindano ya kufuzu michuano hiyo itakayofanyika mwishoni mwa wiki hii nchini Jamaica ingawa mwenye ana matumaini ya kuchaguliwa katika mbio za mita 400 kupokezana vijiti. Bolt hajawahi kushiriki michuano ya Jumuiya ya Madola baada ya kuikosa ile iliyofanyika jijini Melborne mwaka 2006 na ile iliyofanyika Delhi miaka minne iliyopita.

KOMBE LA DUNIA 2014: NIGERIA NAO WAGOMA SABABU YA POSHO.

KIKOSI cha timu ya taifa ya Nigeria kimegoma kufanya mazoezi jana kufuatia kutoelewana juu ya posho zao za kuvuka hatua ya timu 16 bora katika michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Brazil. Wachezaji wa timu hiyo waliomba mkutano na viongozi ambapo walitaka sehemu ya pesa zao ambazo zitatolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa kuvuka hatua ya pili walipwe na Shirikisho lao la Soka la Nigeria. Kutokana na FIFA kuchelewa kutoa fedha hizo za bakshishi wachezaji wamesema shirikisho lao la soka linapaswa kuwalipa kabla ya hawajacheza mchezo wao dhidi ya Ufaransa Jumatatu. Wachezaji hao wameamua kufanya hivyo kwani wanajua wakitolewa katika michuano hiyo Jumatatu, itakuwa ngumu kupata fedha zao kutoka NFF kama ilivyokuwa katika michuano ya mwaka 2010. Migogoro ya fedha kwa timu za Afrika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu imekuwa suala la kawaida hatua ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa timu kukosa ari ya kujituma kutokana na kukosa haki zao. Timu za Cameroon na Ghana ambazo tayari zimeenguliwa katika michuano hiyo nazo zilikumbwa na migogoro kama hiyo ambayo ilipelekea wachezaji wa Cameroon kugoma kupanda ndege mpaka wapewe posho zao huku rais wa Ghana akilazimika kusafirisha fedha za ya dola milioni tatu kwa ndege ili kuzima mgomo uliotaka kutokea.

KOMBE LA DUNIA 2014: MARADONA AIPONDA TENA FIFA KWA ADHABU YA SUAREZ WALIYOTOA.

NGULI wa soka wa Argentina, Diego Maradona ameendeleza vita na Shirikisho la Soka Dunia-FIFA kwa kuponda adhabu waliyotoa dhidi ya Luis Suarez baada ya kukutwa na hatia ya kumng’ata Giorgio Chiellini wa Italia. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay na klabu ya Liverpool, amefungiwa miezi minne kujishughulisha na amsuala ya soka pamoja na kufungiwa mechi tisa za kimataifa kwa kutenda tukio hilo kwa mara ya tatu ndani ya miaka minne. Maradona ambaye alivaa fulana iliyokuwa na maandishi ya kumuunga mkono Suarez yaliyosomeka Luis tuko pamoja ameiponda FIFA na kudai kuwa wanamhukumu kama vile amefanya kosa kubwa sana. Maradona amesema uamuzi huo ni mkubwa na haelewi ni kwani kwani Suarez hajaua mpaka apewe adhabu kali kama hiyo. Maradona alihoji kuwa kama FIFA wanaona amefanya kosa kubwa sana kwanini wasimfunge pingu na kumpeleka katika gereza la wafungwa kigaidi la Marekani la Guantanamo Bay. Nguli huyo aliendelea kudai kuwa anakumbuka tukio la Zinedine Zidane alilofanya katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006 lakini FIFA badala ya kutoa adhabu kali waliishia kumpa tuzo ya mpira wa dhahabu. Maradona amesema amesikitishwa na jinsi Suarez anavyochukuliwa kama muhalifu kwa kusindikizwa kuondoka kambini akiwa chini ya ulinzi wa polisi ndio maana ameamua kumtetea katika vyombo vya habari kwani adhabu aliyopewa imekuwa kali sana.

SIJAONDOKA ARSENAL KWA AJILI YA PESA - SAGNA.

BEKI mahiri wa kimataifa wa Ufaransa, Bacary Sagna amejibu mapigo kwa mashabiki ambao wanamkosoa wakati alipoondoka Arsenal na kwenda Manchester City na kudai kuwa hakuondoka kwasababu ya fedha bali kuinua kiwango chake. Nyota huyo amejiunga rasmi na City baada ya miezi kadhaa ya mvutano kutokana na kukataa ofa ya mkataba mpya Arsenal, kutokana na huu wa sasa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Na baada ya kuisaidia Ufaransa kuvuka katika hatua ya timu 16 bora, Sagna amejibu tetesi kuwa kilichomfanya aondoke Arsenal ni mshahara na kudai kuwa kwa miaka sita ameitumikia timu hiyo kwa kiwango kimoja cha mshahara. Sagna amesema kwasasa yeye ni mchezaji wa City, lakini anataka kufafanua kuwa hakuondoka Arsenal kwa fedha kwani toka mwaka 2008 ameitumikia timu hiyo bila kuomba nyongeza ya mshahara. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa kilichomfanya kuondoka Arsenal ni kuhitaji mabadiliko ili aweze kujiongeza zaidi katika kazi yake hiyo ya soka.

KOMBE LA DUNIA 2014: HATUA YA MAKUNDI YAVUNJA REKODI KWA KUFUNGWA MABAO MENGI.

WAKATI Thomas Muller akifunga bao didi ya Marekani na kuipa ushindi Ujerumani wa 1-0 na kuifanya kuongoza kundi G, hakufikia idadi ya mabao manne ambayo yamefungwa na Lionel Messi na Neymar lakini pia ameweka rekodi mpya ya mabao katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Dunia kwa mwaka huu. Kufikia muda wa kundi H kumalizia mechi zake za mwisho huku Ubelgiji ikishinda bao 1-0 dhidi ya Korea Kusini na sare ya bao 1-1 kati ya Algeria na Urusi ilihitimisha idadi ya mabao 136 yaliyofungwa katika hatua hiyo ikiwa ni mabao sita zaidi ya yale yaliyofungwa katika michuano ya mwaka 2002 iliyofanyika Korea Kusini na Japan. Wachezaji wengine wanaowafuata kwa karibu kwa ufungaji nyota hao ni pamoja na Robin van Persie, Arjen Robben wote wa Uholanzi, Karim Benzema wa Ufaransa, Enner Valencia wa Ecuador, Rodriguez wa Colombia na Shaqiri wa Switzerland ambao wote wamefunga mabao matatu kila mmoja. Wengine waliofunga mabao mawili katika hatua hii ya kwanza ni pamoja na Tim Cahill wa Australia, Mario Mandzukic wa Croatia, Martinez wa Colombia, Dempsey wa Marekani, Wilfried Bony wa Ivory Coast, Andre Ayew wa Ghana, Asamoah Gyan wa Ghana, Musa wa Nigeria na Slimani wa Algeria.

KOMBE LA DUNIA 2014; TIMU ZILIZOTINGA HATUA YA 16 BORA.

TIMU za Afrika zilizofuzu 16 Bora ya Kombe la Dunia nchini Brazil zitakutana na mabingwa wa zamani wa michuano hiyo katika hatua hiyo. Nigeria itamenyana na Ufaransa wakati Algeria itamenyana na Ujerumani ambapo kama wakifanikiwa kushinda watakuwa wameungana na Cameroon, Senegal na Ghana katika orodha ya timu za Afrika zilizowahi kufika robo fainali ya Kombe la Dunia. Mechi nyingine za Robo Fainali ni kati ya Brazil na Chile, Colombia na Uruguay, Uholanzi na Mexico, Argentina na Uswisi na Ubelgiji na Marekani. Michezo hiyo ya mtoano inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho ambapo wenyeji Brazil watakuwa wakipepetana na Chile mchezo ambao utachezwa saa moja usiku ukifuatiwa na mchezo kati ya Colombia na Uruguay utakaochezwa saa tano za usiku.

Thursday, June 26, 2014

KOMBE LA DUNIA 2014: SUAREZ AFUNGIWA MIEZI MINNE KUJISHUGHULISHA NA SOKA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Uruguay, Luis Suarez amefungiwa kujishughulisha na masuala yoyote yanayohusiana na soka kwa miezi minne kwa kumng’ata beki wa timu ya taifa ya Italia Giorgio Chiellini. Nyota huyo wa Liverpool mwenye umri wa miaka 27 pia amefungiwa kucheza mechi za kimataifa tisa, hivyo kumfanya kuikosa michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu. Hatua hiyo pia itamfanya kukosa mechi tisa za Ligi Kuu ya Uingereza msimu ujao. Tukio la kumng’ata Chiellini lililotokea Jumanne iliyopita katika mchezo wa kundi D ambao Uruguay ilishinda na kuvuka katika hatua ya timu 16 bora. Uruguay imepewa siku tatu za kukata rufani dhidi ya adhabu hiyo. Adhabu ni kubwa zaidi katika historia ya michuano ya Kombe la Dunia, ambapo imeizidi ile ya kufungiwa mechi nane aliyowahi kupewa Mauro Tassotti wa Italia kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Hispania Luis Enrique mwaka 1994.


KOMBE LA DUNIA 2014: MUNTARI, BOATENG WATIMULIWA KWA UTOVU WA NIDHAMU.

WACHEZAJI Sulley Muntari na Kevin-Prince Boateng wametimuliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ghana kufuatia tuhuma za utovu wa nidhamu. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa Chama cha Soka cha nchi hiyo-GFA, zimeeleza kuwa Boateng alitimuliwa kwa kutumia lugha ya kudhalilisha kwa kocha Kwesi Appiah wakati Muntari yeye alitishia kumpiga mjumbe wa kamati ya utendaji ya GFA. Taarifa hizo zimetoka muda mchache kabla ya mchezo wao dhidi ya Ureno ambao unaendelea hivi muda huu. Black Stars bado wana nafasi ya kufuzu hatua inayofuata kama wakifanikiwa kuifunga Ureno huku wakiomba Ujerumani iifunge Marekani katika mchezo mwingine ambao nayo unachezwa hivi sasa.

MAN CITY YANASA KIUNGO KUTOKA PORTO.

KLABU ya Manchester City imekamilisha usajili wa kiungo wa kimataifa wa Brazil Fernando kutoka klabu ya FC Porto ya Ureno. Porto ilitangaza taarifa hizo katika soko la hisa la Lisbon jana baada ya kukubali kuchukua kitita cha paundi milioni 12 kutoka City. City wamethibitisha uhamisho huo leo ingawa hawakueleza wamempa nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 mkataba wa miaka mingapi. Akihojiwa Fernando amesema amefurahishwa na usajili na atajitolea kwa nguvu zake zote kuisaidia klabu hiyo ya Manchester. Fernando amejiunga na Porto mwaka 2007 ambapo ameshinda mataji manne la Ligi pamoja na moja la Europa League mwaka 2011.

MAN UNITED BADO WAWEKA MATUMAINI KWA HERRERA PAMOJA NA KUKATALIWA OFA YAO YA KWANZA.

KLABU ya Manchester United bado ina matumaini ya kumsajili kiungo wa Athletic Bilbao Ander Herrera pamoja na ofa yao ya oaundi milioni 29 kukataliwa na timu hiyo. Inadaiwa kuwa United imefikia bei iliyowekwa katika mkataba wa Herrera lakini Bilbao bado wanaonekana kuhitaji fedha zaidi kwa ajili ya kumuuza mcezaji huyo. Mara ya kwanza United walishindwa kumnunua kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi mwaka jana lakini meneja mpya Louis van Gaal ameonekana kufufua upya suala hilo. Lakini pamoja na hayo United bado wana matumaini ya kumsajili kiungo huyo kabla ya kuanza kwa ziara ya zao za maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu zinazotarajiwa kuanza Julai 18 mwaka huu.

KOMBE LA DUNIA 2014: JAPAN YAANZA MCHAKATO WA KOCHA MPYA BAADA YA ZACCHERONI KUACHIA NGAZI.

CHAMA cha Soka nchini Japan, kimeanza mchakato wa kutafuta kocha mpya baada ya Alberto Zaccheroni kuamua kuachia ngazi kutokana na kushinda kuipa ushindi nchi hiyo katika michezo ya hatua ya makundi. Vyombo vya habari nchini Japan vimeripoti kuwa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Mexico Javier Aguirre ndiye anayepewa nafasi ya kuchukua mikoba hiyo. Taarifa hizo ziliendelea kudai kudai kuwa tayari JFA wameshaanza mazungumzo na kocha huyo mkongwe ambaye aliliongoza taifa lake kufika hatua ya timu 16 bora mara mbili katika michuano ya mwaka 2002 na 2010. Japan walikwenda katika michuano hiyo inayoendelea nchini Brazil wakia na matumani baada ya kufuzu kirahisi katika hatua ya makundi huku wakitabiriwa kufika hatua ya robo fainali lakini hayakwenda kama walivyotaraji kwani walijikuta wakiondolewa katika hatua ya mwanzo. Kipigo kutoka kwa Ivory Coast na Cololmbia pamoja na sare dhidi ya Ugiriki yalitosha kuifanya timu hiyo kuburuza mkia katika kundi C.

KOMBE LA DUNIA 2014: UBELGIJI KUWAKOSA KOMPANY NA VERMAELEN KATIKA MCHEZO WA LEO.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Marc Wilmots amedai kuwa watacheza mchezo wao wa mwisho wa mwisho wa kundi H dhidi ya Korea Kusini baadae leo bila ya kuwa na nahodha wake Vincent Kompany na Thomas Vermaelen. Wilmots aliwaambia waandishi wa habari kuwa kila kitu kilikuwa kinakwenda sawa lakini wana wachezaji wenye majeruhi madogo mdogo hivyo watawapumzisha katika mchezo dhidi ya Korea Kusini. Vermaelen alitegemea kuukosa mchezo huo baada ya kutolewa nje mapema katika mchezo wa Jumapili iliyopita walioshinda bao 1-0 dhidi ya Urusi wakati Kompany yeye alijitonesha maumivu ya msuli wakati akiwa katika mazoezi. Ubelgiji tayari wamefuzu hatua ya timu 16 bora lakini watahitaji kupata alama ili kujihakikishia nafasi ya kumaliza vinara katika kundi lao la G.

KOMBE LA DUNIA 2014: KOCHA HONDURAS ABWAGA MANYANGA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Honduras, Luis Fernando Suarez ameamua kubwaga manyanga baada ya kushindwa kuipa ushindi nchi hiyo katika mechi zake zote tatu za hatua ya makundi za Kombe la Dunia. Kocha huyo raia wa Colombia ambaye aliivusha Ecuador katika hatua ya timu 16 bora katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006 iliyofanyika nchini Ujerumani amemua kuachia ngazi kufuatia vipigo vitatu alivyopata katika michuano hiyo inayoendelea nchini Brazil. Suarez ambaye amekuwa kocha Honduras toka Machi mwaka 2011 aliomba radhi mashabiki wa soka wa nchi hiyo kwa kushindwa kufanya vyema huku akidai amesikitika kwasababu alikuwa na ndoto katika michuano hii. Kipigo cha mwisho cha Honduras katika michuano hiyo walikipata jana usiku katika mchezo wao dhidi ya Switzerland uliochezwa katika Uwanja wa Amazoni ambapo walifungwa mabao 3-0, yote yakifungwa na Xherdan Shaqiri.

WOLFSBURG IMEKUZA KIWANGO CHANGU - GUSTAVO.

KIUNGO wa kimataifa wa Brazil, Luiz Gustavo amesema kuondoka kwake katika timu ya Bayern Munich na kwenda Wolfsburg kumemsaidia kwa kikubwa kuinua kiwango chake ambacho kilikuwa kikidorora. Gustavo amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Brazil katika michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea ambapo ametengeneza mojawapo ya mabao ambayo yameivusha nchi hiyo katika hatua ya timu 16 bora. Kiungo amesema anakumbuka mambo mengi mazuri wakati akiwa Bayern hivyo kuondoka na kuiacha klabu hiyo halikuwa jambo rahisi lakini ndio ulikuwa mwanzo kwani amekuja kuwa fiti zaidi. Gustavo alitua Bayern akitokea kwa mahasimu wao wa Bundesliga Hoffenheim Januari mwaka 2011 ambapo aliichezea klabu hiyo kwa miaka miwili na nusu kabla ya kocha mpya Pep Guardiola kumruhusu kuondoka katika majira ya kiangazi mwaka jana. Akizungumzia uamuzi wa Guardiola kumruhusu kuondoka, Gustavo amesema kila mtu ana mawazo yake lakini hivi sasa ana furaha mahali alipokuwepo.

KOMBE LA DUNIA 2014: MESSI ANATOKEA SAYARI YA JUPITER - KESHI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Nigeria, Steven Keshi amesema Lionel Messi ametokea sayari ya Jupiter baada ya Muargentina huyo kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 waliopata dhidi ya wawakilishi hao wa bara la Afrika. Messi mwenye umri wa miaka 27 alifunga mabao hayo ambayo yameifanya Argentina kumaliza kinara katika kundi F. Keshi amesema ni mmoja mchezaji wa kipekee, amejaaliwa kipaji na hakuna mtu anayeweza kuchukua hilo kutoka kwake. Pamoja na kufungwa Nigeria walifanikiwa kufuzu hatua inayofuata baada ya Iran kushindwa kutamba mbele ya Bosnia-Herzegovina na sasa mabingwa hao wa Afrika watachuana na vinara wa kundi E ambao ni Ufaransa katika hatua hiyo. Argentina wao wameangukia kwa Swizterland aliyemaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi E baada ya kuitandika Honduras kwa mabao 3-0.

Tuesday, June 24, 2014

RATIBA YA BUNDESLIGA YATOKA.

BAADA ya kutoka ratiba ya Ligi Kuu nchini Uingereza, sasa imekuwa zamu ya Ujerumani kwa kutoa ratiba yao Bundesliga kwa ajili ya msimu ujao wa 2014-2015. Mabingwa wa Bundesliga kwa misimu miwili mfululizo, Bayern Munich wanatarajiwa kuanza kutetea taji lao nyumbani huko Allianz Arena kwa kuchuana na Wolfsburg Agosti 22 mwaka huu. Mahasimu wao Borussia Dortmund wao watafungua dimba na Bayer Leverkusen wakati Schalke wao watasafiri kuifuata Hannover wakati timu zilizopanda daraja msimu huu Koln na Paderborn zenyewe zitapambana na Humburg na Mainz. Mechi ya kwanza itakayozikutanisha mahasimu wa jiji Dortmund na Schalke itachezwa mwishoni mwa wikiendi ya mwisho ya mwezi Agosti wakati Bayern wao wataikaribisha Dortmund mwishoni mwa mwezi Octoba huku ile ya marudiano ikitarajiwa kuchezwa kati ya Mei 4 au 5 mwakani. Msimu utakamalizika kwa mabingwa watetezi Bayern kumaliza na Mainz huku mahasimu wao Dortmund wao wakimaliza na Werder Bremen.


UNITED YAMTENGEA HERRERA PAUNDI MILIONI 30.

KLABU ya Manchester United inajipanga kutenga kitita cha paundi milioni 30 kwa ajili ya kumsajili Ander Herrera kutoka klabu ya Athletic Bilbao. United walishindwa kumsajili kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania mwenye umri wa miaka 24 katika muda wa mwisho wa usajili kiangazi mwaka jana. Lakini meneja mpya Loius van Gaal amemua kujaribu tena kumsajili kiungo huyo katika dili ambalo pengine likakamilika Jumanne ijayo. Herrera ambaye alikuwa katika kikosi cha Hispania kilichoshiriki michuano ya olimpiki iliyofanyika London mwaka 2012 anatarajiwa kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Van Gaal toka Mholanzi huyo alipochukua nafasi ya David Moyes Juni mwaka huu. Toka aliposajiliwa Marouane Fellaine kutoka Everton kiangazi mwaka jana, United walikuwa hawajasajili mchezaji anayecheza nafasi ya kiungo wakati kwa miaka sita.

YAYA TOURE AWASHAMBULIA VIONGOZI WA CITY KWA KUMKATALIA KWENDA KUMUONA NDUGUYE HOSPITALI.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Ivory Coast Yaya Toure amebainisha kusikitishwa na klabu ya Manchester City kumkatalia kumpa kibali ili kwenda kumuona mdogo wake alipokuwa amelazwa wakati alipokwenda Abu Dhabi. Ibrahim Toure ambaye alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani alifariki akiwa na umri wa miaka 28 wiki iliyopita wakati kama zake Yaya na Kolo wakiwa katika majukumu ya kimataifa na Ivory Coast katika michuano ya Kombe la Dunia. Kiungo huyo wa zamani wa Barcelona, hata hivyo amesema City hawakumpa ruhusa ya kwenda kumtembelea ndugu yake huyo hospitali muda mfupi baada ya kufanikiwa kunyakuwa taji la Ligi Kuu. Badala yake kikosi cha City kilisafiri kwenda Abu Dhabi kucheza na klabu ya Al-Ain ikiwa ni sehemu ya sherehe za ubingwa wao. Yaya amesema alikuwa akisikia vibaya kwenda kusheherekea taji la ligi wakati kaka yake afya ikizidi kudhoofika hata hivyo maofisa wa City walikuwa akijua hilo lakini hawakumpa ruhusa aliyohitaji.

OSCAR KUBAKIA CHELSEA MSIMU UJAO.

KIUNGO wa klabu ya Chelsea, Oscar amesema atabakia Stamford Bridge msimu ujao pamoja na kufanya mawasiliano na mabingwa wa Ufaransa Paris Saint-Germain-PSG. Kwa muda mrefu PSG imekuwa ikimhusudu nyota huyo wa kimataifa wa Brazil, huku meneja wake Laurent Blanc akisema wazi wazi na kumekuwa na tetesi kuwa kiungo huyo anaweza kumfuata David Luiz huko. Nafasi ya Oscar, Chelsea imekuwa mashakani kufuatia kuwasili kwa Cesc Fabregas wakati kumekuwa na mashaka pia ya kuporomoka kw akiwango cha kiungo huyo msimu uliopita. Lakini wakati Oscar akikiri kuwasilina na PSG, amesema hakuna maafikiano yoyote yaliyofikiwa hivyo ataendelea kuwepo Stamford Bridge msimu ujao.

KOMBE LA DUNIA 2014: DEL BOSQUE AFIKIRIA KUACHIA NGAZI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque amesema anaweza kuamua mustakabali wake katika siku chache zijazo baada ya kumaliza ushiriki wao wa michuano ya Kombe la Dunia kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Australia. Mabingwa hao wa dunia wamemaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi B, baada ya kupata kipigo cha kushangaza kutoka kwa Uholanzi na Chile. Akiulizwa kuhusu mustakabali wake mara baada ya mchezo huo, Del Bosque amesema ataamua suala hilo katika siku chache zijazo au wiki ijayo kwani hana haraka na hilo. Hispania wameshinda Kombe la Dunia mwaka 2010 na michuano ya Ulaya mwaka 2012 wakiwa chini ya Del Bosque mwenye umri wa miaka 63. Kocha huyo amesema yeye pamoja na rais, katibu mkuu wa shirikisho la Soka la Hispania watazungumza kutafuta suluhisho zuri na watafanya kitu ambacho kitakuwa kizuri kwa maendeleo ya soka la nchi hiyo.

KOMBE LA DUNIA 2014: ALVES AWAONYA WACHEZAJI WENZAKE KUTOBWETEKA.

BEKI mahiri wa timu ya taifa ya Brazil, Dani Alves amewaonya wachezaji wenzake kuwa baada ya kumaliza hatua ya makundi sasa michuano ya Kombe la Dunia ndio inaanza rasmi. Baada ya Brazil kuigaragaza Cameroon kwa kufunga mabao 4-1 jana na kumaliza kiongozi wa kundi A, beki huyo wa klabu ya Barcelona amesema hawatakiwi kufanya makosa kama waliyofanya katika mchezo huo ambapo yalipelekea Cameroon kusawazisha bao. Alves amesema sasa Kombe la Dunia linaanza baada ya kupita hatua ya makundi ambapo makosa yoyote yanaweza kufanyika yanaweza kuigharimu timu kuenguliwa katika michuano hiyo. Pamoja na hayo Alves amesema ushindi wlaiopata jana ulikuwa muhimu kwa kuwajenga wajiamini zaidi kwa ajili ya hatua ya inayoafuata ya mtoano. Brazil watakwaana na Chile katika hatua hiyo ya mtoano katika mchezo utakaochezwa Juni 28 mwaka huu huku washindi wa pili katika kundi lao Mexico wenyewe wkichuana na Uholanzi.

COSTA ACHOMOA KUIFUNDISHA CLERMONT.

KLABU ya Clermont Foot ya Ufaransa, imedai kuwa Helena Costa ameamua kutochukua mikoba ya kuifundisha timu hiyo msimu ujao. Costa mwenye umri wa miaka 36 raia wa Ureno amekuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kufundusha timu ya wanaume barani Ulaya wakati alipoteuliwa kuchukua wadhifa huo Mei mwaka huu. Lakini rais wa klabu hiyo Claude Michy amesema mwanamama huyo ameamua kutoyatukuza majukumu yake na kuongeza kuwa uamuzi huo umekuwa wa ghafla na wa kushangaza. Sababu za Costa kukataa kibarua hicho bado hazijalikana. Kabla ya kukubali kibarua hicho cha kuinoa timu hiyo ya daraja la pili, Costa alikuwa kocha wa timu ya taifa ya wanawake ya Iran na pia likuwa akifanya kazi kama mng’amuzi wa vipaji wa klabu ya Celtic na kocha wa vijana wa Benfica ya Ureno.

SINA UHAKIKA NA KUMSTAKABALI WANGU MADRID - DI MARIA.

WINGA Angel Di Maria amekiri kuwa hana uhakika na mstakabali wake katika klabu ya Real Madrid, kufuatia timu za Ligi Kuu kuonyesha nia ya kumsajili. Winga huyo mwenye umri wa miaka 26 aekuwa akihusishwa na tetesi za kuhama baada ya kuwa na msimu mzuri Madrid ambapo amefunga mabao 11 na kusaidia mengine 26 hivyo kuingoza timu hiyo kunyakuwa taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Arsenal na Manchester United zimeonekana kufuatilia kwa karibu kiwango cha winga huyo katika michuano ya Kombe la Dunia akiwa na timu yake ya taifa ya Argentina ambapo amecheza katika mechi zote mbili dhidi ya Bosnia na Iran. Hata hivyo, Di Maria amesema kwasasa amehamishia mawazo yake kwa nchi yake kwenye michuano hiyo lakini akakiri kuwa hana uhakika na mustakabali wake Madrid. Akihojiwa Di Maria amesema hajui kitakachotokea kwasasa na hana uhakika wa maisha yake ya soka huko mbele kwasababu nguvu na mawazo yake ameyaweka katika timu yake ya taifa ila baada ya michuano hiyo ndio atajua kitakachotokea.

KOMBE LA DUNIA 2014: NEYMAR NI MUHIMU KWETU KAMA ILIVYO KWA MESSI ARGENTINA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luiz Felipe Scolari amekiri Neymar ni mchezaji muhimu katika kikosi chake kama ilivyo kwa Lionel Messi katika kikosi cha Argentina baada ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 4-1 waliopata kutoka kwa Cameroon. Nyota huyo wa Barcelona aliifungia Brazil bao la kuongoza katika dakika ya 17 akimalizia krosi ya chini iiyopigwa na Luiz Gustavo na kufunga bao lake la nne katika michuano hiyo kwa juhudi binafsi baadae katika kipindi cha kwanza. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Scolari alikiri kuwa Brazil inamtegemea Neymar kama ilivyo kwa Argentina na Messi. Scolari amesema wachezaji hao wawili ni tofauti na wanaweza kubadilisha matokeo katika timu zao wakati ambapo wanahitajika kufanya hivyo. Brazil imefanikiwa kuikwepa Uholanzi katika hatua ya timu 16 bora na sasa watachuana na Chile ambao wote wanatoka bara moja la Amerika Kusini lakini Scolari amesema kama angeambiwa achague basi angechagua timu nyingine. Scolari aliendelea kudai kuwa ni ngumu kucheza na mpinzani anayetoka Amerika ya Kusini kwasababu Chile wana wachezaji wengi wenye uwezo na wanacheza kwa umoja.

RIO FERDINAND KUTUA QPR MSIMU UJAO.

BEKI wa zamani wa klabu ya Manchester United, Rio Ferdinand amekubali dili la kusajiliwa katika klabu ya Queens Park Rangers-QPR ambao wamepanda daraja msimu huu. Beki huyo mwenye umri wa miaka 35 ameshawishika kupunguziwa mshahara wake baada ya kusikia mipango ya Harry Redknapp ya jinsi gani anaweza kuisaidia klabu hiyo yenye maskani yake jijini London kujiimarisha katika Ligi Kuu. Inaaminika kuwa mshahara wa nyota huyo umepunguzwa mara tatu ya ule wa paundi 200,000 kwa wiki aliokuwa akiupata Manchester United huku pia akikataa ofa ya kufanya kazi katika vyombo vya habari ambapo BT na BBC walikuwa wakitaka kumuajiri. Usajili huo wa Ferdinand unatarajiwa kuthibitishwa na klabu hiyo siku chache zijazo. Kwasasa Ferdinand ambaye anafanya kazi na BBC nchini Brazil, ni mchezaji huru baada ya kuachwa na United kufuatia miaka 12 aliyoitumikia. Redknapp mwenye umri wa miaka 67 ndiye aliyempa nafasi ya kucheza Ferdinand wakati akiwa West Ham United mwaka 1996 kuja kuwa mmoja wa mabeki ghali zaidi duniani wakati akihamia Leeds kwa paundi milioni 18 miaka mitano baadae.

Sunday, June 22, 2014

KOMBE LA DUNIA 2014: FIFA KUCHUNGUZA TUHUMA ZA UBAGUZI KWA MASHABIKI WA UJERUMANI.

SHIRIKISHO la Soka Dunia-FIFA linatarajia kuchunguza tuhuma za ubaguzi zinazodaiwa kutolewa na mashabiki wa Ujerumani katika mchezo dhidi ya Ghana ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 huko Fortaleza. Picha zilionyesha baadhi ya mashabiki wakiwa wamejipaka rangi nyeusi katika nyuso zao katika mitandao ya kijamii, na kuzua mjadala kuwa mashabiki wa timu za Ulaya wanaonyesha tabia za kibaguzi. Kuongezea uzito madai hayo ni tukio la mshabiki mmoja, ambaye aliingia uwanjani akiwa na maandishi kuhusu Nazi wakati wa kipindi cha pili cha mchezo huo. Msemaji wa FIFA amesema siku zote wanachukua ushahidi wowote unaowasilishwa au kuonekana katika kamati yao ya nidhamu na wao ndio wanaokutana kuangalia kama wanaweza kufungua kesi na baadae tume ya nidhamu kutoa maamuzi.

KOMBE LA DUNIA 2014: VAN GAAL AILALAMIKIA FIFA KWA UPENDELEO.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal amelikosoa Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA kwa kushindwa kutoa usawa kwa kuwalazimisha kucheza mchezo wao wa mwisho wa kundi B kabla ya kujua mpinzani watakaekutana naye katika hatua inayofuata ya timu 16 bora. Uholanzi tayari wameshafuzu hatua hiyo ya mtoano kufuatia ushindi wao dhidi ya Hispania na Australia ambapo wanatarajia kuchuana na Chile katika mchezo wao wa leo utakaochezwa saa moja usiku kwa saa za hapa wakitegemea kuchukua uongozi wa kundi lao. Mpinzani wao watakayekutana naye hatua inayofuata atatoka katika kundi A, ambapo Brazil, Croatia na Mexico wanafukuzia nafasi ya kufuzu mechi ambazo zitachezwa kwa pamoja saa tano usiku. Kupangwa kwa mechi za kundi A kuchezwa baada ya mechi za kundi B kunaonekana kutompendeza Van Gaal ambaye amedai anaona kama wenyeji wao wanapendelewa. Van Gaal amesema katika kila mechi FIFA wanaonyesha mabango ya kutaka usawa katika mchezo huo wa soka lakini kwa jinsi wanafanya kwa kuwapendelea wenyeji katika ratiba haoni usawa wowote. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa watakachofanya wao na kuzingatia ushindi katika mchezo wao dhidi ya Chile hadhani kama hilo litaathiriwa kwasababu Brazil wanacheza baada yao, wanachotegemea ni kuwa watakuwa wanamichezo.

KOMBE LA DUNIA 2014: RONALDO AMPONGEZA KLOSE KUFIKIA REKODI YAKE YA MABAO.

MSHAMBUALIAJI nyota wa zamani wa Brazil, Ronaldo amempongeza Miroslav Klose baada ya Mjerumani huyo kufikia rekodi yake ya mabao 15 katika michuano ya Kombe la Dunia jana. Klose mwenye umri wa miaka 36 aliingia katika kipindi cha pili kwenye mchezo dhidi ya Ghana na kufunga bao la kusawazisha lililofanya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2. Ronaldo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akimkaribisha Klose na kumpongeza kwa mafanikio hayo makubwa aliyopata. Ronaldo alifunga mabao yake katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1998, 2002 na 2006.

KOMBE LA DUNIA 2014: KOLO NA YAYA TOURE WASHINDWA KUMZIKA NDUGU KWA AJILI YA TIMU YA TAIFA.

NDUGU wawili Yaya na Kolo Toure wameamua kubakia na timu yao ya taifa ya Ivory Coast katika michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Brazil baada ya kifo cha mdogo wao. Ibrahim Toure mwenye umri wa miaka 28 ambaye alikuwa akiugua maradhi ya saratani alifariki dunia Alhamisi iliyopita. Shirikisho la Soka la Ivory Coast lililotoa taarifa hiyo huku wakituma salamu za rambirambi kwa familia ya ndugu hao. Ivory Coast itachuana na Ugiriki katika mchezo wao wa mwisho wa kundi C Jumanne ijayo wakijua kuwa ushindi utawavusha katika hatua inayofuata ya timu 16 bora. Yaya Toure mwenye umri wa miaka 31 anayekipiga katika klabu ya Manchester City amecheza katika mechi zote mbili za Ivory Coast dhidi ya Japana na Colombia wakati beki wa Liverpool Kolo Toure mwenye umri wa miaka 33 bado ameendelea kusugua benchi katika michuano hiyo.

HODGSON KUMSHAWISHI GERRARD AENDELEE NA MAJUKUMU YA KIMATAIFA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson anatarajia kumshawishi Steven Gerrard kuendelea na kucheza soka la kimataifa mpaka 2016 na kumuacha nahodha huyo wan chi hiyo katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi kati ya kuhitajika kwake na klabu na timu ya taifa. Pamoja na Gerrard mwenye umri wa miaka 34 kushinda kung’aa katika michuano ya Kombe la Dunia, thamani ya uzoefu wake katika kikosi inamaanisha Hodgson atahitaji kiungo kuendelea ili wachezaji chipukizi waweze kuiga mfano wake. Huku Frank Lampard akikaribia kutundika daruga zake katika soka la kimataifa, Gerrard anabakia kuwa mmoja wa wachezaji wachache wakongwe waliobakia na Uingereza hatataka kumpoteza ili kutengeneza uwiano kwa kikosi cha wachezaji chipukizi kilichopo. Hata hivyo, Gerrard itabidi aangalie umuhimu wake katika klabu ya Liverpool ambayo ina ratiba ngumu msimu ujao baada ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na nyota amesema atatoa uamuazi baada ya kuzungumza na marafiki zake, familia na kocha wake Brendan Rodgers baada ya Kombe la Dunia.

KOMBE LA DUNIA 2014: DANI ALVES AMPONDA SHEARER.

BEKI mahiri wa kimataifa wa Brazil, Dani Alves amemshambulia Alan Shearer kwa kudai kauli ya mchambuzi huyo wa soka wa BBC kuhusu mshambuliaji Fred ni ya kipuuzi. Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Uingereza aliiambia luninga ya ESPN wiki iliyopita kuwa chaguo la kwanza la mshambuliaji wa kati wa Brazil hana kasi na hawezi kupiga mashuti hivyo anatakiwa kuondolewa katika kikosi cha kwanza cha nchi hiyo. Pamoja na kuwa na rekodi nzuri ya kufunga kwa Brazil mwaka uliopita, Fred ambaye anacheza katika timu ya Fluminense amekuwa kimya sana katika michuano hii kwa kushindwa kufumania nyavu katika mechi mbili walizocheza. Shearer amesema hajui kwanini Brazil bado wanaendelea kumpanga katika kikosi cha kwanza kwnai hana msaada wowote katika safu ya ushambuliaji. Lakini Alves alimshambulia vikali Shearer kwa kauli hiyo nakudai kuwa ni ya kipuuzi kwa mtu ambaye amecheza soka na anayejua ugumu wa suala ufungaji kwa mchezaji. Brazil kwasasa wanaongoza katika kundi A kuelekea mchezo wao mwisho dhidi ya Cameroon huku timu itakayoongoza kundi ikitarajiwa kupambana na aidha Chile au Uholanzi katika hatua ya timu 16 bora.

KOMBE LA DUNIA 2014: MARADONA AZIDI KUISHAMBULIA FIFA.

NGULI wa soka nchini Argentina ameendeleza vita vya na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA baada ya shirikisho hilo kuwataka wachezaji saba wa Costa Rica kwenda kufanyiwa vipimo baada ya kuifunga Italia. Maradona amesema shirikisho hilo limeonyesha kushindwa kuheshimu sheria baada ya kusisitiza kufanywa ka vipimo hivyo. Wachezaji wawili pekee wa Italia ndio waliofanyiwa vipimo baada ya kufungwa na Costa Rica bao 1-0 Ijumaa na kuzima matumaini ya Uingereza ya kufuzu hatua ya makundi. Maradona mwneye umri wa miaka 53 alihoji kama FIFA wamewataka wachezaji saba wa Costa Rica kufanyiwa vipimo kwanini hawakufanya hivyo kwa wachezaji wa Italia. Nguli huyo aliendelea kudai kuwa anavyofahamu yeye ni wachezaji wawili katika kila timu wanaotakiwa kufanyiwa vipimo kama wametumia dawa za kuongeza nguvu baada ya mchezo husika lakini sio saba. Amedai hatua hiyo inaonyesha jinsi gani FIFA wanavyotapatapa kwa kuona timu vigogo zikiyaaga mashindano mapema hivyo kuwafanya kukosa mikataba minono ya matangazo.

KOMBE LA DUNIA 2014: ULIKUWA USIKU MZURI KWA TIMU AFRIKA - KESHI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Nigeria, Steven Keshi amesema ulikuwa usiku mzuri kwa timu za Afrika zinazotoka upande wa Magharibi baada ya kikosi chake kuichapa Bosnia-Herzegovina jana usiku na Ghana kutoa sare ya mabao 2-2 na Ujerumani. Akihojiwa Keshi amesema kila mtu ana furaha kwani Ghana wamepata matokeo waliyohitaji na wao wameshinda hivo ni jambo zuri kwa bara la Afrika. Keshi mwenye umri wa miaka 52 pia alipongeza kiwango cha timu yake walichoonyesha katika michuano hiyo kwa kuhakikisha wanalinda lango lao vyema hivyo kuwafanya kucheza mechi ya pili bila kufungwa. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa wanatakiwa kuendelea na juhudi hizo ili kuhakikisha wanafanikiwa kuvuka hatua inayoafuata kwani mchezo wao wa mwisho dhidi ya Argentina anajua hautakuwa rahisi.

KOMBE LA DUNIA 2014: MESSI IS A GENIUS - SABELLA.


KOCHA wa timu ya taifa ya Marekani, Alejandro Sabella amempongeza Lionel Messi kwa ujuzi wake baada ya kufunga bao dakika za majeruhi na kuindosha Iran katika michuano ya Kombe la Dunia. Iran waliichanganya Argentina kwa mchezo wao wa kupaki basi mpaka Messi alipotumia ujuzi binafsi kwa kufunga bao lake la pili katika michuano hiyo. Sabella amesema Iran walifanya maisha kuwa magumu katika mchezo huo lakini anashukuru kwakuwa na mtu mwenye ujuzi ambaye ni Messi aliyefanya mambo yawezekane. Kabla ya michuano hii Messi alikuwa amefunga bao moja katika mechi nane za Kombe la Dunia alizocheza lakini mambo yamebadilika safari hii baada ya kuonyesha uwezo wake katika mechi mbili zilizopita. Sabella amesema wachezaji wake wote walichangia kwa kiasi kikubwa ushindi lakini kwa shuti alilopiga Messi hata kama kungekuwa na magolikipa wawili wasingweza kulizuia.

KOMBE LA DUNIA 2014: BECKHAM NYUMA YA MWAMKO WA SOKA LA MAREKANI.

HILI ni Kombe la Dunia la kwanza kumkosa David Beckham baada ya kupita zaidi ya miaka 20, hata hivyo kazi yake kubwa aliyoifanya kulitangaza soka nchini Marekani itaonekana baadae leo usiku wakati nchi hiyo itakapoivaa Ureno.

Hakuna shaka kwamba Marekani hivi sasa wameanza kupagawa na mchezo wa soka huku mamilioni wakifuatilia kila hatua na mastaa wa Hollywood wakitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii ya twitter kuelezea mchezo wa soka.

Kunatarajiwa kuwa na mshabiki zaidi ya 10,000 wa Marekani huko Manaus katika tiketi 90,000 za Kombe la Dunia zilizouzwa kwa ajili ya michuano hiyo na kufanya kuwa nchi iliyonunua tiketi nyingi zaidi ukiacha wenyeji Brazil katika michuano hiyo.

Katika mchezo huo wa leo zaidi ya mashabiki milioni 20 wa nchi hiyo wanatarajiwa kutizama mchezo huo idadi ambayo inatarajiwa kuizidi ile ya mashabiki waliotizama mchezo wao pendwa wa fainali ya mpira wa kikapu ambapo San Antonio Spurs waliibuka kidedea wiki ijayo.

Kuhama kwa Beckham kutoka klabu ya Real Madrid kwenda Los Angeles Galaxy kumechangia kwa kiasi kikubwa nchi hiyo kupata hamasa ya mchezo huo baada ya utawala wa kipindi kirefu wa michezo ya mpira wa kikapu na baseball.

Mtoto wa kiume wa kocha wa wa Liverpool Kenny Dalglish aitwaye Paul ambaye amekaa Marekani kwa muda wa miaka nane anatoa ushuhuda wa jinsi Beckham alipoinua hamasa ya mchezo soka nchini Marekani katika kipindi cha miaka minne alipokuwepo huko.

Paul amesema Beckham alikuwa zaidi ya mchezaji, kwani wakati anafika Ligi Kuu ya Soka nchini humo maarufu kama MLS ilikuwa na timu 12 pekee lakini msimu ujao wa ligi hiyo unatarajiwa kuwa na timu ya 21.

Nyota mbalimbali akiwemo wa mpira wa kikapu LeBron James ambaye ana zaidi ya watu milioni 13 wanaomfuata katika mtandao wa twitter aliandika katika ukurasa wake kwa kuipongeza nchi hiyo kuanza vyema katika mchezo wa kwanza dhidi ya Ghana.

Nyota wengine walioipongeza nchi hiyo ni Justin Timberlake huku Ikulu ya Marekani nayo iituma salamu zake pamoja na kuwakilishwa na makamu wa rais Joe Badden katika mchezo wa kwanza dhidi ya Ghana.

KOMBE LA DUNIA 2014: KLOSE AIFIKIA REKODI YA RONALDO.

MSHAMBULIAJI mkongwe wa Ujerumani Miroslav Klose amefikisha idadi sawa ya mabao yaliyofungwa katika michuano ya Kombe la Dunia na aliyekuwa mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil Ronaldo de Lima. Klose alifunga bao lake la kumi na tano dhidi ya Ghana katika mechi iliyomalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2. Katika mchezo huo uliokuwa mkali na kusisimua Ujerumani ndio walioanza kupata bao la kuongoza katika kipindi cha pili kabla ya Ghana hawajasawazisha kupitia kwa Andre Ayew na baadae kuongeza la pili kupitia kwa Asamoah Gyan lakini Ujerumani nao wlaiswazisha kupitia kwa mkongwe Klose na kupelekea mchezo huo kumalizika kwa sare hiyo. Wawakilishi wengine wa Afrika Nigeria jana nao walijitoa kumasomaso kwa kuichapa Bosnia-Herzegovina kwa bao 1-0 hivyo kuweka hai matumaini yao ya kusonga mbele katika michuano hiyo kama wakifanikiwa kuifunga Argentina katika mchezo wao wa mwisho.

Thursday, June 19, 2014

26 WAITWA STARS SAFARI YA GABORONE.

WACHEZAJI 26 wa timu ya taifa ya Tanzania-Taifa Stars wanatarajiwa kuingia kambini Jumatatu ijayo kwa ajili ya safari ya Gaborone, Botswana. Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa Stars Salum Mayanga, amedai kuwa wachezaji hao wanatakiwa kuripoti katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa safari hiyo inayotarajiwa kuwa Juni 24 mwaka huu. Wachezaji hao ni wanaotakiwa kuripoti kambini ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Benedictor Tinoko, Kelvin Yondani, Said Moradi, Nadir Haroub, Joram Nason, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Edward Charles, Aggrey Morris na Pato Ngonyani. Wengine ni Frank Domayo, Amri Kiemba, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Said Juma, Haruna Chanongo, Himid Mao, John Bocco, Simon Msuva, Kelvin Friday, Ramadhan Singano, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa na Mwegane Yeya.