Friday, June 27, 2014

KOMBE LA DUNIA 2014: OBAMA ATIZAMA MECHI YA MAREKANI NA UJERUMANI KATIKA AIR FORCE ONE.

RAIS wa Marekani Barack Obama ameonyesha jinsi umuhimu wa michuano ya Kombe la Dunia ulivyo kwa Wamarekani kwa kuitizama nchi yake ikichuana na Ujerumani katika kundi G akiwa katika ndege yake ya Air Force One. Obama alikuwa akisafiri kutoka Maryland kuelekea Minnesota wakati Marekani ikicheza mechi yake hiyo muhimu na alihakikisha hataki kukosa chochote kutokana na mchezo huo kurushwa moja kwa moja katika Air Force One. Kikosi cha Marekani kinachonolewa na Jurgen Klinsmann kilifungwa bao 1-0 na Ujerumani lakini bado walifanikiwa kufuzu katika hatua ya mtoano kwa tofauti nzuri ya mabao ukilinganisha na Ureno ambao nao waliifunga Ghana kwa mabao 2-1 katika mchezo wa mwisho. Michuano hii ya Kombe la Dunia imegusa hisia za raia wengi wa Marekani ambapo zaidi ya mashabiki 15,000 wanadaiwa kukusanyika sehemu ya wazi jijini Chicago kuangalia mechi kati ya nchi hiyo na Ureno, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya mashabiki nchini humo kukusanyika kuangalia mechi ya Kombe la Dunia. Klinsmann ambaye ni mchezaji wa zamani wa ujerumani, aliandika barua ya wazi kwa raia wote wa Marekani kuwaomba kutenga muda wao kutazama mchezo huo barua ambayo ilijibiwa haraka na gavana wa New York Andrew Cuomo aliyetoa amri kwa waajiri wote kuongeza muda wa mapumziko ya chakula cha mchana kwa ajili ya kuangalia mchezo huo. Hii ni mara pili mfululizo kwa Marekani kutinga hatua ya timu 16 bora katika michuano ya Kombe la Dunia baada ya kumaliza mbele ya Uingereza katika michuano ya mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment