Wednesday, August 31, 2016

WILSHERE KWENDA PALACE AU BOURNEMOUTH.

KIUNGO wa Arsenal, Jack Wilshere anatarajiwa kujiunga na Crystal Palace au Bournemouth kwa mkopo wa msimu mzima ili aweze kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amekutana na meneja wa Palace, Alan Pardew na yule wa Bournemouth Eddie Howe jana kwa ajili ya mazungumzo. Wilshere ameichezea Uingereza mechi sita katika kipindi cha kiangazi zikiwemo mechi tatu za michuano ya Ulaya lakini ameachwa katika kikosi cha nchi hiyo kinachoongozwa na kocha mpya Sam Allardyce. Kutokana na Wilshere kuandamwa na majeruhi ya mara kwa mara, Arsenal waliamua kumnunua kiungo wa kimataifa wa Uswisi Granit Xhaka kwa kitita cha pauni milioni 35 kiangazi hiki.

BONY KWENDA STOKE.

KLABU ya Stoke City inadaiwa kukaribia kumsajili mshambuliaji wa Manchester City Wilfried Bony. Bony aliwasili katika uwanja wa mazoezi wa Stoke mapema leo ikiwa ni mchakato wa kukamilisha uhamisho wake kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, ingawa klabu hizo mbili zinadaiwa bado kufikia muafaka wa mwisho. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast bado hajacheza katika mechi yeyote msimu huu na City wamekuwa wakimtafutia klabu mpya katika wiki za karibuni. West Ham United, pamoja na kumnunua Simone Zaza mwishoni mwa wiki iliyopita nao walikuwa wakitajwa kumuwania Bony mpaka jana usiku lakini sasa wanaonekana kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho. Bony mwenye umri wa miaka 27 ni mmoja kati ya wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao wanategemewa kuondoka kabla ya dirisha la usajili kufungwa leo usiku, wengine ni Samir Nasri, Joe hart na Eliaquim Mangala.

CHELSEA YAMUWANIA TENA DAVID LUIZ.

KLABU ya Chelsea inadaiwa kuingia katika mzungumzo ya kumuwania David Luiz kutoka Paris Saint-Germain kwa kitita cha paundi milioni 32. Chelsea wamekuwa katika mazungumzo na Kia Joorabchian na Giuliano Bertolucci toka waliposhindwa kumsajili Kalidou Koulibaly kutoka Napoli. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 amesema yuko tayari kuondoka na alicheza kwa mafanikio wakati aliposajiliwa kwa mara ya kwanza Chelsea akitokea Benfica kwa kitita cha paundi milioni 21 Januari mwaka 2011. Hata hivyo, uhamisho huo utawezekana pale tu, PSG watakapofanikiwa kupata mbadala wa beki huyo.

ARSENAL WAPAISHA USAJILI WA LIGI KUU KUFIKIA ZAIDI PAUNDI BILIONI MOJA.

KLABU za Ligi Kuu sasa zimetumia zaidi ya pauni bilioni moja katika usajili wao waliofanya kipindi hiki cha kiangazi. Ligi hiyo ilikuwa tayari imeshavunja rekodi yake yenyewe ya usajili wiki iliyopita, wakati Manchester City walipomsajili kipa wa Barcelona Claudio Bravo na kupelekea kufikia kiasi cha paundi milioni 880 wakizidi paundi milioni 870 zilizotumika kiangazi mwaka jana. Arsenal kukamilisha usajili wa beki wa kimataifa wa Ujerumani Shkodran Mustafi kutoka Valencia aliyenunuliwa kwa ada ya pauni milioni 35 jana usiku kunapelekea jumla ya fedha zilizotumika katika usajili mpaka sasa kufikia zaidi ya paundi bilioni moja huku zikibaki saa chache kabla ya dirisha kufungwa leo usiku. Huu unakuwa msimu wa nne wa majira ya kiangazi kwa rekodi mpya kuwekwa katika usajili wa Ligi Kuu. Hull City imekuwa klabu ya 12 kuvunja rekodi yao ya usajili kiangazi hiki wakati walipomnyakuwa Ryan Mason kutoka Tottenham Hotspurs.

GUARDIOLA ADAI HAKUNA TIMU INAYOFIKIA KIWANGO CHA BARCELONA.

MENEJA wa Manchester City Pep Guardiola amemmwagia sifa Luis Enrique na Barcelona, akisisitiza hakuna yeyote katika ulimwengu wa soka anayecheza vizuri zaidi ya mabingwa hao wa La Liga kuelekea mchezo baina yao. Guardiola atapambana na klabu yake hiyo ya zamani baada ya City kupangwa kundi moja na Barcelona katika hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hiyo itakuwa mara ya tatu na nne kwa Guardiola kukutana na Barcelona toka alipoondoka mwishoni mwa msimu wa 2011-2012. Mara ya mwisho alikutana nao akiwa meneja wa Bayern Munich katika nusu fainali ya michuano hiyo misimu miwili iliyopita ambapo aliondoshwa kwa jumla ya mabao 5-3. Akihojiwa kuhusiana na hilo, Guardiola amesema kwa mara nyingine kucheza na Barcelona itakuwa jaribio gumu kwake haswa kutokana na safu imara ya ushambuliaji waliyonayo ambayo inaongozwa nyota watatu Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.

BENTEKE AMKUMBUKA RODGERS.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ubelgiji, Christian Benteke amesisitiza kuwa hakushindwa Liverpool, lakini anadhani muda wake ungekuwa na mafanikio zaidi kama klabu hiyo isingemtimua Brendan Rodgers. Benteke alinunuliwa kwa kitita cha pauni milioni 32.5 akitokea Aston Villa Julai mwaka 2015 wakati huo Liverpool ikiwa chini ya Brendan Rodgers. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25, alianza katika mechi sita za kwanza za ligi kabla ya Rodgers hajatimuliwa Octoba na nafasi yake kuchukuliwa na Jurgen Klopp. Kufuatia ujio wa meneja huyo mpya, Benteke hakufanikiwa kupata nafasi na badala yake Mjerumani huyo alipendelea kuwatumia zaidi Firmino na Divock Origi. Akihojiwa kufuatia uhamisho wake kwenda Crystal Palace uliogharimu kiasi cha pauni milioni 32, Benteke anaamini hakufanikiwa kufanya vizuri Liverpool lakini anadhani angefanya vyema zaidi kama angepewa nafasi ya kucheza.

Tuesday, August 30, 2016

DEAL DONE: MUSTAFI NA PEREZ.

KLABU ya Arsenal imekamilisha rasmi usajili wake wa wachezaji wawili kwa mpigo ambao umewagharimu zaidi ya paundi milioni 50. Nyota hao wawili waliosajiliwa ni mshambuliaji wa Deportivo La Coruna Lucas Perez na beki wa Valencia Shkodran Mustafi. Perez mwenye umri wa miaka 27 amesajiliwa kwa kitita cha paundi milioni 17.1 huku Mustafi yeye akisajiliwa kwa paundi milioni 35. Arsenal sasa inakuwa imesajili wachezaji sita kiangazi hiki bada ya Granit Xhaka na chipukizi Rob Holding, Takuma Asano na Kelechi Nwakali. Akimzungumzia Perez, meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema mshambuliaji huyo sio kwamba anaweza kufunga mabao pekee bali pia anaweza kucheza vyema na wenzake. Kwa upande wa Mustafi Wenger amesema yuko katika umri sahihi na ana uzoefu mzuri pamoja na utulivu mkubwa pindi anapokuwa na mpira.

ALCACER ATUA RASMI BARCELONA.

KLABU ya Barcelona imetangaza rasmi kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Hispania Paco Alcacer kutoka Valencia kwa mkataba wa miaka mitano. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye aliondolewa katika kikosi cha Valencia kilichoshinda bao 1-0 dhidi ya Eibar Jumamosi iliyopita, alifanyiwa vipimo vya afya Barcelona Jana kabla ya kukamilisha uhamisho wake huo uliogharimu euro milioni 30. Alcacer amefunga mabao 43 katika mechi 124 alizoichezea Valencia huku akiitwa mara 13 kukichezea kikosi chake cha timu ya taifa. Akihojiwa Alcacer amesema pamoja na kuwa anaondoka Valencia lakini siku zote itakuwa ni klabu ya moyo wake na kuwashukuru mashabiki kwa kipindi chote walichomuunga mkono.

ARSENAL KUMTOA WILSHERE KWA MKOPO.

KLABU ya Arsenal inadaiwa kuwa tayari kumuacha kiungo wa kimataifa wa Uingereza Jack Wilshere kuondoka kwa mkopo ili kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24, ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara, alifanikiw akucheza mechi tatu pekee kwa Arsenal msimu uliopita baada ya kuvunjika mfupa wa fibula. Wilshere ameichezea Uingereza mechi tatu kipindi cha kiangazi ikiwemo michezo mitatu ya michuano ya Ulaya lakini hajajumuishwa katika kikosi cha Sam Allardyce alichokitaja wiki hii. Kiangazi hiki Arsenal wamemsajili kiungo wa kimataifa wa Uswisi Granit Xhaka kwa kitita cha paundi milioni 35. Wilshere amebaki na saa 48 za kutafuta klabu ya kwenda kwa mkopo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili la kiangazi.

ROONEY KUSTAAFU SOKA LA KIMATAIFA BAADA YA URUSI.

MSHAMBULIAJI nyota na nahodha wa Uingereza Wayne Rooney anatarajia kustaafu soka la kimataifa baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 itakayofanyika nchini Urusi. Nyota huyo wa Manchester United alikuwa akizungumza na wanahabari kwa mara ya kwanza toka kocha mpya wa timu ya taifa ya Uingereza sam Allardyce athibitishe kuwa ataendelea kuwa nahodha. Akihojiwa Rooney ambaye amefunga mabao 53 katika mechi 115 kwa Uingereza, amesema pindi Kombe la Dunia la Urusi litakapomalizika anadhani wakati wake wa kuaga soka la kimataifa utakuwa umefika. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa michuano hiyo itakuwa nafasi yake ya mwisho kufanya kila kitu na Uingereza hivyo bado ataendelea kufurahia miaka miwili iliyobakia. Kama Rooney akicheza mchezo wa Jumapili hii wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Slovakia, atakuwa amevunja rekodi ya David Beckham ya kucheza mechi nyingi katika timu ya taifa.

AYEW, GYAN WAJITOLEA KUISAIDIA BLACK STARS KUFUATIA UKATA ULIYOIKUMBA.

MSUGUANO kati ya Wizara ya Michezo ya Ghana na Shirikisho la Soka la nchi hiyo-GFA umechukua sura mpya kufuatia wachezaji wa kikosi cha kwanza kuambiwa kujilipia nauli zao wenyewe. Kuelekea mchezo wao wa mwisho wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika Jumamosi hii, waziri wa michezo Nii Lante Vanderpuye ameiambia GFA kuwa hakutakuwa na fedha kwa ajili ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ambao wameitwa katika kikosi hicho cha Black Stars. Hatua hiyo imekuja kwa madai kuwa timu hiyo tayari imeshafuzu michuano hiyo itakayofanyika nchini Gabon mwaka 2017, hivyo wanaona ni upotevu wa fedha kuwasafirisha wachezaji kutoka Ulaya na kwingineko. Kutokana na hilo nahodha msaidizi wa Black Stars, Andre Ayew amejitolea kununua tiketi kwa baadhi ya wachezaji 21 kutoka nje walioitwa katika kikosi hicho kinachonolewa na Avram Grant kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Rwanda Septemba 3. Naye nahodha wa timu hiyo Asamoah Gyan pia atachangia chochote kwa kutoa baadhi ya tiketi kwa ajili ya wachezaji ambao hawataweza kumudu kununua tiketi.

MARADONA AMKUBALI MWANAE ALIYEZAA NA MCHEPUKO.

NGULI wa soka wa Argentina, Diego Maradona hatimaye amemkubali mtoto wake Diego Junior ambaye alikuwa naye mwishoni mwa wiki iliyopita huko Buenos Aires. Diego Junior alizaliwa nchini Italia mwaka 1986 kutoka katika mahusiano ya pembeni aliyokuwa nayo lakini hakuwahi kukubalika rasmi na baba yake, hata baada ya kulazimishwa kuwa analipa fedha za matumizi na jaji wa Italia mwaka 1992. Maradona mwenye umri wa miaka 55, sasa amemkubali rasmi mtoto wake huyo na kudai mbele ya wanahabari kuwa huyo ni mtoto wake wa kiume. Maradona pia aliendelea kudai kuwa anadhani Diego Junior anafanana na baba yake pamoja na kukaa kufanya vipimo vya DNA kwa miaka kadhaa kufuatia kutakiwa kufanya hivyo na mahakama. Naye Diego Junior aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa amefurahi hatimaye kukubaliwa na baba yake kwani walisubiria hilo kwa kipindi cha miaka 30.

BARCELONA YAANZA MAZUNGUMZO YA MKATABA MPYA NA MESSI.

RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amesema mazungumzo yameshaanza kwa ajili ya Lionel Messi kusaini mkataba mpya. Messi yuko chini ya mkataba mpaka mwaka 2018 lakini Barcelona wanataka kumpa ofa ya mkataba mpya kufuatia taarifa kuzagaa Julai mwaka huu kuwa walishakubaliana dili jipya. Akihojiwa kuhusiana na hilo, Bartomeu amesema Messi bado ana miaka miwili katika mkataba wake lakini watazungumza naye kwa ajili ya kumuongeza kwasababu wanataka kuendelea kuwa naye. Kwasasa Messi anasumbuliwa na majeruhi ya msuli wa paja wakati Argentina ikijiandaa kukwaana na Uruguay na Venezuela katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia.

HART KWENDA TORINO KWA MKOPO.

WAKALA wa Joe Hart amethibitisha kuwa mteja wake anatarajiwa kujiunga na klabu ya Torino ya Italia wakati akikaribia kuondoka Manchester City. Hart anaondoka City kufuatia kutomvutia meneja mpya Pep Guardiola ambaye tayari ameshamnunua Claudio Bravo kutoka Barcelona ili kuziba nafasi yake. Kipa huyo wa kimataifa wa Uingereza alicheza mechi yake ya mwisho na City katika mchezo wa kufuzu hatua ya makundi dhidi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Steaua Bucharest ya Romania. Akihojiwa kuhusiana na hilo wakala wa Hart, Jonathan Barnett alithibitisha kuwa mteja wake huyo amekubali kujiunga na Torino kwa mkopo wa msimu mzima. Barnett aliendelea kudai kuwa tayari City nao wameshatoa ruksa na sasa kinachosubiriwa ni vipimo vya afya kabla ya kukamilisha dili hilo.

Monday, August 29, 2016

SOUTHAMPTON YAVUNJA REKODI YAO USAJILI KWA NYOTA WA MOROCCO.

KLABU ya Southampton imevunja rekodi yake yenyewe kwa kumsajili kiungo wa kimataifa wa Morocco Sofiane Boufal kutoka klabu ya Lille ya Ufaransa kwa kitita cha paundi milioni 16. Boufal mwenye umri wa miaka 22, amefunga mabao 11 msimu uliopita na kuisaidia Lille kumaliza katika nafasi ya tano katika Ligue 1 na kufuzu michuano ya Europa League. Rekodi iliyokuwepo kwa Southampton ya kusajili mchezaji ghali ilikuwa ni paundi milioni 15 waliyomnunulia mshambuliaji wa Roma Dani Osvaldo mwaka 2013. Akihojiwa mara baada ya kukamilisha usajili huo, Boufal amesema klabu hiyo ni bora na anadhani itakuwa mahali pazuri kwake kukua zaidi kisoka.

SCHURRLE AACHWA KIKOSI CHA UJERUMANI.

WINGA wa Borussia Dortmund, Andre Schurrle amelazimika kuondolewa katika kikosi cha Ujerumani kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya kirafiki na kufuzu Kombe la Dunia kutokana na majeruhi. Schurrle alilalamika kuzumbuliwa na maumivu ya mgongo kufuatia ushindi wa mabao 2-1 waliopata Dortmund dhidi ya Mainz katika mchezo wao wa ufunguzi wa Bundesliga jana. Majeruhi hayo yanamaanisha kuwa Schurrle hatakuwepo katika mchezo wa kirafiki wa Ujerumani dhidi ya Finland ambao utafanyika huko Monchengladbach au ule wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Norway Septemba 4. Taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Ujerumani lilithibitisha taarifa hizo na kuongoza haijajulikana kama kocha Joachim Low ataamua kuita mchezaji mwingine ili kuziba nafasi yake. Katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Urusi, Ujerumani wamepangwa kundi C sambamba na Norway, Ireland Kaskazini, Jamhuri ya Czech, Azerbaijan na San Marino.

WENGER AMFANANISHA XHAKA NA EMMANUEL PETIT.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amepongeza ujio wa Granit Xhaka katika kikosi chake na kumfananisha na kiungo wa zamani wa timu hiyo Emmanuel Petit. Xhaka aliyesajiliwa kiangazi hiki alianza katika mechi zote dhidi ya Leicester City na Watford, huku kiwango chake kikiboreka zaidi katika mchezo wa juzi huko Vicarage Road. Wenger anaamini nyota huyo wa kimataifa wa Uswisi ana kila kitu ambacho kinafanana na Petit aliyetwaa taji la Ligi Kuu akiwa na Arsenal katika msimu wa 1997-1998. Akihojiwa Wenger amesema Xhaka huwa anakuwa mtulivu pindi awapo na mpira na kwa mbali anafanana na Petit ka aina ya soka lake.

HENRY APANIA KUWEKA HISTORIA NA UBELGIJI.

NGULI wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Arsenal, Thierry Henry anaamini Ubelgiji ina uwezo wa kuweka historia kufuatia kuteuliwa kwake kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya nchi hiyo. Henry atafanya kazi chini ya kocha mkuu Roberto Martinez baada ya kuteuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita. Nguli huyo sasa atafanya kazi na nyota wa Ubelgiji kama Eden Hazard, Kevin De Bruyne na Romelu Lukaku wakati Ubelgiji ikiwa inatafuta nafasi ya kufanikiwa zaidi kuliko ilivyokuwa katika michuano ya Ulaya ambayo walikwamia hatua ya robo fainali. Akihojia Henry amesema kibarua hicho kina changamoto kubwa lakini jambo moja mablo watakwenda kulifanyia kazi ni kuwajengea uwezo wachezaji watambue kuwa wana uwezo wa kuwa timu kubwa. Ubelgiji inatarajiwa kukwaana na Hispania katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Alhamisi hiii kabla ya mechi ya kwanza ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Cyprus siku tano baadae.

EMERY AJIPA MOYO PAMOJA NA KIPIGO.

MENEJA wa Paris Saint-Germain-PSG, Unai Emery amedai ana uhakika kikosi chake kitajifunza kutokana na uzoefu wa mechi zao za ugenini baada ya kupata kipigo cha kushtukiza kutoka kwa AS Monaco jana. Katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Louis II, PSG walitandikwa mabao 3-1 na mahasimu wao Monaco. Matokeo yanamaanisha PSG imeshuka mpaka nafasi ya tano katika msimamo wa Ligue 1, kufuatia kuanza msimu kwa ushindi. Akihojia Emery amesema walianza mchezo huo vyema lakini baada ya Monaco kuwafunga bao la kuongoza hali ilibadilika kwani walifanikiwa kuulinda ushindi wao vyema. Hata hivyo, Emery anaamini wachezaji wake wamejifunza kutokana na mchezo huo na watafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza.

MOURINHO KUMPA MAPUMZIKO ZAIDI IBRAHIMOVIC.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amesema Zlatan Ibrahimovic atapewa mapumziko zaidi kupisha mechi za kimataifa. Mshambuliaji huyo ameanza vyema msimu na klabu hiyo kwa kufunga bao katika mechi ya ngao ya hisani na baadae mabao mengine matatu katika mechi tatu za Ligi Kuu. Kufuatia kustaafu kuitumikia Sweden baada ya michuano ya Ulaya mwaka huu, nyota huyo hatakuwa na majukumu ya kimataifa mwishoni mwa wiki ijayo, lakini Mourinho bado anataka kumlinda zaidi. Akihojiwa Mourinho amesema ukiwa na umri wa miaka 34 huwezi kucheza mechi 70 kwa msimu hivyo ameapa wachezaji wengine ambao hawajachaguliwa na timu zao za taifa siku mbili za mapumziko huku Ibrahimovic akimpa siku nne.

MUSTAFI AKIRI OZIL ALIMSHAWISHI KWENDA ARSENAL.

BEKI wa kimataifa wa Ujerumani, Shkodran Mustafi amebainisha kuomba ushauri kutoka kwa nyota wa Arsenal Mesut Ozil kuelekea uhamisho wake wa kwenda Emirates. Mustafi anatarajiwa kuthibitishwa rasmi kuwa mchezaji wa Arsenal wiki hii baada ya meneja Arsene Wenger kutangaza kuwa kilichobaki na kusaini mkataba ili kukamilisha uhamisho wake kutoka Valencia. Mustafi ambaye pia amewahi kucheza katika klabu ya Everton atakuwa akicheza sambamba na Mjerumani mwenzake Per Mertesacker katika safu ya ulinzi ya Arsenal. Akihojiwa Mustafi amesema hajaonana na Mertesacker kwa kipindi kirefu kwasababu alishastaafu soka la kimataifa lakini amekuwa akizungumza na Ozil na kumwambia kila anachohitaji kuhusu Arsenal. Mustafi aliendelea kudai kuwa kila kitua lichoambiwa kilimvutia hivyo haikuwa kazi kwake kukubali kujiunga nao kwani siku zote amekuwa akiipenda klabu hiyo.

NASRI AMUWEKA ROHO JUU GUARDIOLA.KIUNGO wa Manchester City, Samir Nasri amekiri kuwa bado anaweza kuondoka klabuni hapo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili kiangazi hiki. Kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 29, alidokezwa kuondoka hapo kufiatia kuwasili kwa Pep Guardiola lakini meneja huyo mpya alimpongeza kiungo huyo baada ya ushindi wa mabao 3-1 waliopata dhidi ya West Ham United jana. Nasri alicheza dakika 15 katika mchezo wa jana ikiwa ni kwanza kwake kwa msimu huu na Guardiola amesema kuwa kiungo huyo wa zamani wa Arsenal anaweza kubakia City.Akihojiwa kuhusiana na hilo, nasri amesema bado hajajua kama atabakia au ataondoka kiangazi hiki na hilo litategemea a baadhi ya mambo kama yatakaa sawa.

Saturday, August 27, 2016

PALERMO YATUMA OFA KWA BALOTELLI.

MAKAMU wa rais wa klabu ya Palermo na Italia, Guglielmo Micciche amesema wametuma ofa Liverpool kwa ajili ya Mario Balotelli na sasa wanasubiri kusikia kama ofa yao itakubaliwa. Balotelli ameondolewa kabisa katika mipango ya Liverpool na kuna uwezekano mkubwa wa kuondoka kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wiki ijayo. Akihojiwa Micceche amesema anafahamu ni jambo gumu lakini wameamua kujaribu kumuwania mshambuliaji huo. Micceche aliendelea kudai kuwa tayari wameshatuma ofa hivyo kazi imebaki kwa Liverpool waikubali au waikatae.

PSG YAKOMAA NA MATUIDI.

KLABU ya Paris Saint-Germain-PSG inajipanga kukataa ofa za kumuwania Blaise Matuidi kwa kumsainisha mkataba mpya kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 amekuwa akihusishwa na tetesi za kuwindwa na Juventus katika siku za karibuni. Hata hivyo, rais wa PSG Nasser Al Khelaifi ametupilia mbali tetesi hizo na kudai kuwa Matuidi anataka kubakia hapo na anatarajiwa kupewa mkataba mpya. Al Khelaifi alikaririwa na gazeti moja nchini Ufaransa akithibitisha kuwa nyota huyo hatauzwa kipindi hiki cha kiangazi. Matuidi alijiunga na PSG akitokea St Etienne mwaka 2011 na katika kipindi chote cha miaka minne wameshinda taji la Ligue 1.

PELLEGRINI ATIMKIA CHINA.

MENEJA wa zamani wa Manchester City, Manuel Pellegrini amejiunga na klabu ya Hebei China Fortune inayoshiriki Ligi Kuu ya China. City waliziba nafasi ya Pellegrini mwenye umri wa miaka 62 kwa kumchukua Pep Guardiola Juni mwaka huu pamoja na meneja huyo raia wa Chile kuwapa taji la Ligi Kuu mwaka 2014. Pellegrini anaungana na makocha wengine wenye majina makubwa waliokwenda China akiwemo Sven-Goran Eriksson na Luis Felipe Scolari. Kikosi cha Hebei kinawajumuisha nyota wa kimataifa wa Argentina Ezequiel Lavezzi, mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Gervinho na chipukizi wa zamani wa Chelsea Gael Kakuta. Klabu hiyo kwasasa inashikilia nafasi ya saba katika msimamo wa ligi huku kukiwa kumebaki michezo saba kabla ya msimu kumalizika.

LEWANDOWSKI AANZA KWA KISHINDO BUNDESLIGA.MSHAMBULIAJI nyota wa Bayern Munich, Robert Lewandowski jana ameanza vyema msimu wa Bundesliga kwa kufunga hat-trick wakati wakiilaza Werder Bremen kwa jumla ya mabao 6-0. Mabingwa hao wa Ujerumani walifunga bao la kuongoza kupitia kwa Xabi Alonso kabla ya Lewandowski hajafunga mawili baadae. Nahodha Philipp Lahm na Franck Ribery nao pia walifunga na Lewandowski kuja kufunga bao la tatu kwa penati kufuatia Thiago kufanyiwa madhambi. Thomas Muller yeye alitoa pasi za mwisho tatu kati ya sita zilizozaa mabao hayo katika Uwanja wa Allianz Arena. Beki Mats Hummels ambaye alijiunga na Bayern akitokea Borussia Dortmund kiangazi hiki alicheza dakika zote 90, wakati kiungo chipukizi mwenye umri wa miaka 19 Renato Sanchez aliyenunuliwa kutoka Benfica kwa kitita cha paundi milioni 27.5 hakutumika katika mchezo huo.

Friday, August 26, 2016

EUROPA LEAGUE: KINA SAMATTA WAPANGWA KUNDI MOJA NA ATHLETIC BILBAO.

RATIBA ya michuano ya Europa League imepangwa rasmi leo huku klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji anayocheza nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta ikipangwa katika kundi F sambamba na timu za Athletic Bilbao na Sassuolo za Hispania na Rapid Vienna ya Australia. Genk walitinga hatua hiyo ya makundi baada ya kuiondosha Lokomotiva Zagreb ya Croatia kwa jumla ya mabao 4-2 huku Samatta akifunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata katika mchezo wa jana. Katika hatua nyingine Manchester United waliopo kundi A wamepangwa kundi moja sambamba na Fenerbahce ya Uturuki, Feyenoord ya Uholanzi na Zorya Luhansk ya Ukraine. Katika mechi za kundi hilo United itakutana na mshambuliaji wake wa zamani Robin van Persie ambaye kwasasa anakipiga Fenerbahce. Mechi za Europa League zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 15 mwaka huu huku mechi za mwisho za makundi zikitarajiwa kuchezwa Desemba 8.

Ratiba kamili ya makundi:
KUNDI A: Man Utd, Fenerbahce, Feyenoord, Zorya Luhansk
KUNDI B: Olympiacos, Apoel Nicosia, Young Boys, Astana
KUNDI C: Anderlecht, St Etienne, Mainz, Qabala
KUNDI D: Zenit St Petersburg, AZ Alkmaar, Maccabi Tel-Aviv, Dundalk
KUNDI E: Plzen, Roma, Austria Vienna, FC Astra Giurgiu
KUNDI F: Athletic Bilbao, Genk, Rapid Vienna, Sassuolo
KUNDI G: Ajax, Standard Liege, Celta Vigo, Panathinaikos
KUNDI H: Shakhtar Donetsk, Braga, Gent, Konyaspor
KUNDI I: Schalke 04, FC Red Bull Salzburg, Krasnodar, Nice
KUNDI J: Fiorentina, PAOK Salonika, Liberec, Qarabag
KUNDI K: Inter Milan, Sparta Prague, Southampton, Hapoel Beer Sheva
KUNDI L: Villarreal, Steaua Bucharest, FC Zurich, Osmanlispor

THIERRY HENRY ALAMBA SHAVU UBELGIJI.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa na klabu za Arsenal na Barcelona Thierry Henry ameteuliwa kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ubelgiji. Henry anajiunga katika benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Roberto Martinez ambaye alichukua nafasi ya Marc Wilmots mwanzoni mwa mwezi huu. Martinez ambaye ni meneja wa zamani wa Everton, amesema Henry ni mtu muhimu na ataleta kitu tofauti katika kikosi hicho. Henry mwenye umri wa miaka 39, anatarajiwa kufanya kazi sambamba na Graeme Jones ambaye amekuwa akifanya kazi na Martinez katika klabu za Swansea City, Wigan Athletic na Everton.

UEFA YAFANYA MABADILIKO CHAMPIONS LEAGUE NA EUROPA LEAGUE.

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limefanya mabadiliko kidogo katika michuano yao wanayoandaa kuanzia msimu wa 2018-2019. Mabadiliko hayo yaliyofanywa ni kuruhusu ligi nne bora barani Ulaya kupata nafasi nne za moja kwa moja katika hatua za makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ligi hizo nne kwa mujibu wa viwango vya UEFA ni Hispania, Ujerumani, Uingereza na Italia. Chini ya mfumo wa sasa, Uingereza, Ujerumani na Hispania zote zina nafasi tatu za kufuzu moja kwa moja kasoro ile ya nne ambayo lazima igombaniwe ili kufuzu. Italia wao wana nafasi mbili pekee za kufuzu moja kwa moja katika hatua ya makundi huku moja ya tatu ikiingia katika mzunguko wa mtoano. UEFA pia imedai kuwa timu zinazofuzu nafasi ya kushiriki michuano ya Europa League nazo pia zitafuzu moja kwa moja hatua ya makundi katika mfumo huo mpya.

RANIERI AJIPA MOYO.

MENEJA wa Leicester City, Claudio Ranieri ana uhakika haitachukua muda mrefu kabla ya kikosi chake hakijarejesha makali yao yaliyowafanya kutwaa ubingwa wa Ligi kuu msimu uliopita. Leicester walianza vibaya msimu kwa kufungwa na Hull City waliopanda daraja msimu huu kabla ya kuja kutoa sare ya bila kufunga na Arsenal. Akihojiwa Ranieri amesema anadhani wachezaji wapya waliowasajili hatachukua muda mrefu kabla ya kuzoeana na wenzao. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa ana matumaini kikosi chake kitapata matokeo mazuri katika mchezo wao dhidi ya Swansea City kesho.

ARSENAL YAKARIBIA KUWANASA PEREZ NA MUSTAFI.

KLABU ya Arsenal, inadaiwa kukubali dili la kuwasajili mshambuliaji wa Deportivo La Coruna Lucas Perez na beki wa Valencia Shkodran Mustafi na wote wanatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya muda wowote kuanzia sasa. Maofisa wa Arsenal wamekuwa wakiumiza vichwa katika kipindi hiki cha usajili wa kiangazi kutokana na majeruhi waliyonayo katika safu ya ulinzi na kutokuwa na washambuliaji wa kutosha na hatimaye wamefikia makubaliano ya kuleta nyota wawili kutoka La Liga. Perez mwenye umri wa miaka 27, amefunga mabao 17 katika ligi msimu uliopita na amekuwa akifuatiliwa mara kadhaa na maskauti wa Arsenal ambao baadae waliamua kumtolea ofa Jamie Vardy. Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Leicester City alikataa uhamisho wa kwenda Emirates kwa kusaini mkataba mpya na klabu hiyo na kuacha Arsene Wenger akitafuta washambuliaji wengine. Jana usiku Deportivo walithibitisha kuwa Perez amepewa ruhusa ya kukosa mchezo wa Ijumaa wa La Liga dhidi ya Real Betis.

WEST HAM YSAJILI NYOTA KUTOKA USWISI.

KLABU ya West Ham United imetangaza kumsajili kiungo wa kimataifa wa Uswisi, Edimilson Fernandes. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 anejiunga na klabu hiyo ya Ligi Kuu akitokea FC Sion kwa mkataba wa miaka minne. Fernadez amefunga mabao sita katika mechi 66 alizoichezea mabingwa hao wa mara mbili wa Uswisi. Akihojiwa mara baada ya kusaini mkataba huo, Fernandez amesema kutua West Ham ni changamoto mpua kwake na sasa jukumu limebaki kwake kuhakikisha anafanya bidii ili kuja kuwa mchezaji mkubwa.

BARCELONA YAMKAZIA ALCACER.

KLABU ya Barcelona inadaiwa kukubali kuongeza ofa kwa ajili ya mshambuliaji wa Valencia Paco Alcacer mpaka kufikia euro milioni 30 baada ya kumuuza Claudio Bravo. Mabingwa hao wa Hispania wamefanikiwa kupata faida ya euro milioni tano kwa kumuuza Bravo Manchester City na kumleta kipa wa Ajax Amsterdam Jasper Cillessen kuja kuziba pengo lake. Huku wakiwa wamebaki na euro milioni 24 katika bajeti yao ya usajili, Barcelona sasa wako katika nafasi nzuri ya kufikia ada inayohitajika kwa ajili ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24. Deportivo inadaiwa kuwa itakubali kiasi cha kuanzia euro milioni 30 na 35 kwa ajili kumuachia Alcacer kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Jumatano ijayo.

Thursday, August 25, 2016

MAKUNDI LIGI YA MABINGWA.

Group A: Paris St-Germain (France), Arsenal (England), Basel (Switzerland), Ludogorets (Bulgaria).

Group B: Benfica (Portugal), Napoli (Italy), Dynamo Kiev (Ukraine), Besiktas (Turkey).

Group C: Barcelona (Spain), Manchester City (England), Borussia Monchengladbach (Germany), Celtic (Scotland).

Group D: Bayern Munich (Germany), Atletico Madrid (Spain), PSV Eindhoven (Netherlands), Rostov (Russia).

Group E: CSKA Moscow (Russia), Bayer Leverkusen (Germany), Tottenham (England), Monaco (France).

Group F: Real Madrid (Spain), Borussia Dortmund (Germany), Sporting Lisbon (Portugal), Legia Warsaw (Poland).

Group G: Leicester City (England), Porto (Portugal), Club Brugge (Belgium), FC Copenhagen (Denmark).

Group H: Juventus (Italy), Sevilla (Spain), Lyon (France), Dinamo Zagreb (Croatia).

SAMATTA ALIVYOIPELEKA GENK MAKUNDI EUROPA LEAGUE.MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta jana amefanikiwa kuingoza vyema klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Europa League. Katika mchezo huo Samatta alifunga bao muhimu la kuongoza katika dakika ya kwanza ya mchezo katika ushindi wa mabao 2-0 iliyopata Genk dhidi ya Lokomotiva Zagreb ya Croatia. Ushindi huo waliopata katika Uwanja wa Luminus Arena umewafanya kutinga hatua hiyo kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza uliofanyika huko Zagreb. Ratiba ya makundi ya michuano hiyo inatarajiwa kupangwa baadae leo huko jijini Monaco, Ufaransa.

BRAVO ATUA RASMI MAN CITY, BYE BYE JOE HART.

KLABU ya Manchester City imefanikiwa kukamilisha rasmi usajili wa kipa Claudio Bravo kutoka Barcelona. Bravo mwenye umri wa miaka 33, amehamia Itihad kwa mkataba wa miaka minne akichukua nafasi ya Joe Hart, ambaye anategemewa kuondoka kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili kiangazi hiki. Meneja wa City Pep Guardiola alikuwa akitafuta kipa ambaye ana uwezo mkubwa wa kutumia miguu yake kuzuia mipira na sasa amempata. Bravo alijiunga na Barcelona akitokea Real Sociedad mwaka 2014 na kuwasaidia mabingwa hao wa Hispania kutwaa mataji mawili ya La Liga na moja la Ligo ya Mabingwa Ulaya.

SAMATTA NJIANI KUANDIKA HISTORIA NA GENK.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta leo anatarajiwa kuingoza klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji katika mchezo wa marudiano wa mwisho kuwania nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Europa League dhidi ya Lokomotiva Zagreb ya Croatia. Katika mchezo huo Genk watakuwa katika Uwanja wao wa nyumbani wa Luminus Arena wakijaribu kutafuta matokeo ya kusonga mbele baada ya sare ya mabao 2-2 katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Maksimir jijini Zagreb. Katika mchezo uliopita Samatta ambaye pia ni nahodha wa Taifa Stars, alifunga bao katika sare hiyo iliyopatikana na wanakwenda katika mchezo huo wakiwa wametoka kushinda mchezo wao ligi ya Ubelgiji kwa mabao 3-0 Jumapili iliyopita huku Samatta akifunga mabao mawili kati ya hayo. Kama Genk wakifanikiwa kupata sare ya bila mabao au ushindi mwembamba kuanzia 1-0 moja kwa moja watakuwa wametinga hatua inayofuata ya makundi ambayo ratiba yake inatarajiwa kupangwa kesho.

DRINKWATER NAYE AFUATA NYAYO ZA KINA VARDY LEICESTER.

KIUNGO wa Leicester City, Danny Drinkwater amesaini mkataba mpya wa miaka mitano na mabingwa hao wa Ligi Kuu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha timu hiyo ambacho kiliushangaza ulimwengu chini ya meneja Claudio Ranieri kwa kutwaa ubingwa msimu uliopita. Akihojiwa mara baada ya kusaini mkataba huo utakaomalizika mwaka 2021, Drinkwater amesema anafuraha kubwa kwani anapenda kuitumikia timu hiyo na anaona ndio pekee inayomfaa kwasasa. Drinkwater anafuata nyayo za nyota wenzake wa timu hiy ambao wameongeza mikataba yao kiangazi hiki akiwemo Jamie vardy, Riyad Mahrez, Wes Morgan, Kasper Scheichel na Andy king.

KIKOSI CHA STARS DHIDI YA NIGERIA HIKI HAPA.

Makipa- Deogratius Munishi – Young Africans, Aishi Manula – Azam FCMabeki-Kelvin Yondani - Young Africans, Vicent Andrew - Young Africans, Mwinyi Haji - Young Africans,Mohamed Hussein – Simba SC Shomari Kapombe - Azam FC,David Mwantika - Azam FCViungo-Himid Mao - Azam FC, Shiza Kichuya – Simba SC, Ibrahim Jeba – Mtibwa Sugar, Jonas Mkude – Simba SC, Muzamiru Yassin – Simba SC, Juma Mahadhi - Young Africans , Farid Mussa Tenerif ya HispaniaWashambuliaji-Simon Msuva - Young Africans, Jamal Mnyate – Simba SC, Ibrahim Ajib – Simba SC , John Bocco - Azam F, Mbwana Samatta - CK Genk ya Ubelgiji

IHEANACHO HATIHATI KUIVAA TAIFA STARS.

NYOTA wa Manchester City, Kelechi Iheanacho yuko katika hatihati ya kuukosa mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2017 ambapo timu yake ya taifa ya Nigeria maarufu kama Super Eagles itakwaana na Tanzania, Taifa Stars huko Uyo, Septemba mwaka huu. Iheanacho aliitwa katika kikosi cha Super Eagles na kocha mpya Gernot Rohr wiki iliyopita, lakini sasa kuna uwezekano mkubwa wa mshambuliaji huyo kuukosa mchezo huo. Hatua hiyo inakuja baada ya nyota huyo kupata majeruhi katika mchezo wa City wa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Steaua Bucharest ya Romania katika Uwanja wa Etihad jana. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19, aliumia wakatia ijaribu kukimbiza mpira na haraka alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo wa kimataifa wa Brazil, Fernandinho katika dakika ya 76. Iheanacho ambaye alifunga mabao 14 kwa City katika mshindano yote msimu uliopita, bado hajawahi kufunga bao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

BLATTER KITANZINI.

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter ameapa kuwa atakubali hatma yake katika maamuzi yatayotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS juu ya rufani yake kupinga kufungiwa miaka sita kujishughulisha na masuala ya soka. Akihojiwa nje ya ofisi za makahama hiyo huko Lausanne, Uswisi, Blatter mwenye umri wa miaka 80 amesema takubaliana na uamuzi wowote utakaotolewa. Blatter aliongeza kuwa ana matumaini uamuzi utakaotolewa utakuwa mzuri kwa upande wake lakini akiwa kama mwanasoka amejifunza kuwa kuna kushinda na wakati mwingine kushindwa pia. Rais huyo mkongwe alikumbwa na adhabu hiyo kutoka FIFA kufuatia kukutwa na hatia ya kufanya malipo ya dola milioni mbili kwenda kwa rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Michel Platini mwaka 2011. Mara ya kwanza FIFA ilimlima adhabu ya kumfungia miaka minane Blatter pamoja na Platini lakini adhabu hiyo ilipunguzwa mpaka miaka sita baada ya kukata rufani.

KOMBE LA LIGI: CITY VS SWANSEA, LEICESTER VS CHELSEA.

KLABU ya Manchester United inatarajiwa kupambana na timu ya League One ya Northampton Town katika mzunguko wa tatu wa michuano ya Kombe la Ligi wakati timu ya League Two ya Accrington Stanley wao wakiwa wageni wa West Ham United. Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Manchester City wao watasafiri kuifuata Swansea City, huku Liverpool waliofungwa katika hatua ya fainali nao wakiwa wageni wa Derby Count. Mabingwa wa Ligi Kuu Leicester City wataikaribisha Chelsea, wakati Southampton nao wakiwa wenyeji wa Crystal Palace na Hull City wakiifuata Stoke City katika mechi zitakazokutanisha timu za Ligi Kuu. Kwa upande mwingine Arsenal wao watakuwa wageni wa Nottingham Forest huku Queens Park Rangers-QPR wakiikaribisha Sunderland. Mzunguko wa tatu wa michuano hiyo unataajiwa kuchezwa wiki inayoanzia Septemba 19 mwaka huu.

JOE HART AACHA KITENDAWILI CITY.

KIPA wa Manchester City, Joe Hart amesema kuisaidia timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika mchezo ambao unaweza kuwa wa mwisho kwake kuitumikia klabu hiyo, ni jambo ya kipekee. Hart ambaye anategemewa kuondoka kufuatia Claudio Bravo kukaribia kukamilisha usajili wake, alikuwa akipigiwa kelele na mashabiki wakati wote wa mchezo huo wa marudiano ambao City ilishinda bao 1-0 dhidi ya Steaua Bucharest. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo ambao City walizonga mbele kwa jumla ya mabao 6-0, Hart amesema wana meneja bora ambaye atakuwa na mawazo tofauti katika maamuzi yake. Naye meneja wa City Pep Guardiola amesema anafahamu kuwa kipa huyo ni nguli katika klabu hiyo.

Tuesday, August 23, 2016

BRAVO ATUA UINGEREZA KUKAMILISHA UHAMISHO WAKE MAN CITY.

KIPA wa Barcelona, Claudio Bravo anadaiwa kutua nchini Uingereza mapema leo kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wake kwenda Manchester City. Meneja wa City Pep Guardiola amemtaja Bravo kama kipa wake namba moja kwa msimu huu baada ya kuamua kumtema Joe Hart katika mipango yake. Taarifa zinadai kuwa Bravo atakaribia kulipwa mara ya mbili mshahara wake wa sasa wakati atakaposaini mkataba wake na City. Kipa huyo wa kimataifa wa Chile ambaye alishinda taji la Copa America akiwa na nchi yake mara mbili mfululizo katika miaka miwili iliyopita, alikuwa akilipwa euro milioni 3.5 na Barcelona lakini sasa anaweza kupata kiasi cha euro milioni sita kwa City.

PRINCE BOATENG AANZA KWA KISHINDO LAS PALMAS.

KIUNGO wa kimataifa wa Ghana, Kevin-Prince Boateng amefunga bao lake la kwanza La Liga katika ushindi wa mabao 4-2 iliyopata timu yake mpya ya Las Palmas dhidi ya Valencia huko Mestalla. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29, alijiunga na Las Palmas kwa mkataab wa mwaka mmoja mwezi huu akiwa kama mchezaji huru baada ya AC Milan kumtema. Boateng ameilipa Las Palmas kwa kuonyesha kuwa mchezaji muhimu wa kigeni kwa kufunga bao hilo katika dakika ya 31 ya mchezo. Mara baada ya mchezo huo nyota huyo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akieleza furaha yake ya kufunga mabao katika ligi zote nne kubwa alizowahi kucheza. Kabla ya kwenda Las Palmas, Boateng amewahi kucheza klabu za Hertha Berlin, Tottenham Hotspurs, Borussia Dortmund, Portmouth, Milan na Schalke.

LYON YAIZODOA ARSENAL KWA LACAZETTE.

RAIS wa Lyon, Jean-Michel Aulas amesisitiza kuwa Alexandre Lacazette ataendelea kubakia katika klabu hiyo na pia kumtaka Rachid Ghezzal kuongeza mkataba baada ya winga huyo kukaa uhamisho wa kwenda Everton. Mwezi uliopita Lyon ilidai kukataa ofa ya euro milioni 35 za Arsenal kwa ajili ya Lacazette, ingawa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amesema yuko tayari kuondoka mwezi huu kama klabu itapokea ofa ambayo hawataweza kuikataa. Lacazette ameshafunga mabao matano katika mechi mbili za kwanza za ligi msimu huu na Aulas ameonyesha kuwa na uhakika wa nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa kubakia hapo mpaka mwishoni mwa msimu huu. Akihojiwa kuhusiana na hilo Aulas amesema Lacazette ni mchezaji muhimu katika kikosi chao hivyo hawana mpango wowote wa kumuachia kiangazi hiki.

AC MILAN YAITOLEA NJE CHELSEA KWA ROMANGNOLI.

KLABU ya AC Milan imethibitisha kukataa mazungumzo na Chelsea kwa ajili ya kumuwania beki wake Alessio Romagnoli. Klabu hiyo ya Serie A imedai Chelsea walitoa ofa ya euro milioni 35 kwa ajili ya nyota huyo wa kimataifa wa Italia mwenye umri wa miaka 21, lakini wamekataa ofa hiyo. Meneja mpya wa Chelsea emapania kuimarisha safu ya ulinzi ya Chelsea kabla ya kufungw akwa dirisha la usajili wa kiangazi baada ya kutofurahishwa na jinsi safu hiyo ilivyo sasa. Baada ya kuchemka kumsajili beki wa Napoli Kalidou Koulibaly, Chelsea waliamua kuhamishia nguvu zao kwa Romangnoli ambaye anafananishwa na nguli wa zamani wa Milan Alessandro Nesta.

NEWELL'S OLD BOYS NA MATUMAINI YA KUMSAJILI MESSI.

KLABU ya Newell’s Old Boys bado ina matumaini ya kumsajili Lionel Messi kutoka Barcelona baada ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018. Messi alianza soka lake katika klabu hiyo ya Argentina kabla ya kuhamia katika akademi maarufu ya soka ya Barcelona inayoitwa La Masia. Toka wakati huo nyota huyo amekwenda kutwaa tuzo nne za Ballon d’Or na kuwa mmoja wachezaji bora kabisa kuwahi kutokea katika soka. Makamu wa rais wa Newell’s Cristian D’Amico ana matumaini ya kuona mshambuliaji huyo akirejea tena katika Uwanja wa Marcelo Biesla katika siku zijazo.

NEYMAR APEWA LIKIZO ZAIDI.

MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Neymar anatarajiwa kukosa mchezo dhidi ya Athletic Bilbao mwishoni mwa wiki hii na hatarejea Hispania mpaka baada ya mapumziko kupisha mechi za kimataifa mwanzoni mwa Septemba. Baada ya kufunga penati ya ushindi dhidi ya Ujerumani na kuiwezesha Brazil kutwaa medali yake ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki Jumamosi iliyopita, nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alitegemewa kurejea mazoezini kwenye klabu yake kesho. Hata hivyo, vyombo vya habari vya Hispania vimedai meneja wake Barcelona Luis Enrique amempa mapumziko nyota huyo ya kubakia Brazil mpaka Septemba. Neymar sasa anatarajiwa kurejea Catalonia kwa ajili ya mchezo wa Alaves ambao utafanyika Septemba 10 mwaka huu.

VALENCIA YAMKOMALIA MUSTAFI.

MENEJA wa Valencia, Pako Ayestaran wachezaji wake Shkodran Mustafi na Paco Alcacer hawatauzwa katika kipindi hiki cha usajili wa kiangazi. Mustafi amekuwa akihusishwa na tetesi za kujiunga na Arsenal wakati Alcacer anekuwa kitajwatajwa kuwindwa na Barcelona. Valencia wanahitaji kuuza wachezaji ili kuepuka kuvunja sheria za matumizi ya fedha, lakini meneja huyo amesisitiza kuwa wachezaji hao hawatakwenda popote kiangazi hiki. Akihojiwa mara baada ya kikosi chake kutandikwa mabao 4-2 nyumbani na Las Palmas jana, Ayestaran amesema Mustafi hatakwenda popote kiangazi hiki.

Monday, August 22, 2016

NEYMAR AJIVUA UNAHODHA BRAZIL.

MSHAMBULIAJI nyota wa Brazil, Neymar amesema anatarajia kuachia beji yake ya unahodha baada ya kufunga penati ya ushindi dhidi ya Ujerumani na kuipatia nchi yake medali ya kwanza ya dhahabu katika Olimpiki. Nyota huyo wa Barcelona aliteuliwa kuwa nahodha na Dunga katika michuano ya Kombe la Dunia ambayo walifungwa katika hatua ya nusu fainali na Ujerumani kw amabao 7-1, mchezo ambao Neymar aliukosa kwasababu ya majeruhi. Baada ya ushindi huo, Neymar amesema tayari ameshakuwa bingwa na ameamua kuachia beji yake ya unahodha kwani ametimiza kile alichokuwa kikiota wakati wote. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa anaivua beji hiyo ili kutoa nafasi kwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Brazil Tite kuchagua nahodha atakayemuhitaji.

OLIMPIKI YAMALIZIKA MAREKANI WAKIIBUKA WABABE.

MICHUANO ya Olimpiki imemalizika rasmi jijini Rio de Janeiro kwa sherehe kabambe ya kufunga na kuwakabidhi rasmi wenyeji wa michuano hiyo mwaka 2020 jiji la Tokyo. Sherehe hizo zilizopambwa na mambo mbalimbali ya tamaduni za watu wa Brazil zilidumu kwa muda wa saa tatu katika Uwanja wa Maracana kabla ya mwenge wa Olimpiki kukabidhiwa kwa wenyeji wajao Tokyo. Ofisa mkuu wa Kamati ya Kimataifa wa Olimpiki-IOC, Thomas Bach ameisifia Brazil kwa maandalizi mazuri ya michuano hiyo iliyochukua muda wa siku 16 kabla ya kutia nanga mapema leo alfajiri. Michuano hiyo ya 31 ilishirikisha jumla ya wanariadha 11,303 kutoka mataifa 206 na timu ya wakimbizi huku kukiwa na michezo 26 iliyokuw aikishindaniwa. Katika michuano ya mwaka huu Marekani ndio wameibuka wababe kwa kuzoa jumla ya medali 121, 46 zikiwa za dhahabu, 37 za fedha na 38 za shaba, wakifuatiwa na Uingereza waliozoa medali 67, 27 za dhahabu, 23 za fedha na 17 za shaba. Wengine wanaofuatia ni China waliobeba medali 70, 26 za dhahabu, 18 za fedha na 26 za shaba, Urusi wao wako nafasi ya nne wakiwa na medali 56, dhahabu 19, fedha 18 na shaba 19, Tano bora inafungwa na Ujerumani wlaiozoa medali 42, dhahabu 17, fedha 10 na shaba 15. Kwa upande wa Afrika, Kenya ndio wlaiofanikiwa zaidi kwa kuzoa medali 13, sita za dhababu, sita zingine za fedha na moja ya shaba, wakifuatiwa na Afrika Kusini waliochukua medali 10, mbili za dhahabu, sita za fedha na mbili zingine za shaba.

Wednesday, August 17, 2016

POGBA FITI KUIVAA SOUTHAMPTON.

KIUNGO mpya wa Manchester United, Paul Pogba anatarajiwa Ijumaa hii kuichezea kwa mara ya kwanza timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Southampton. Nyota huyo ambaye aliondoka kwa mlango wa nyuma mwaka 2012 kwenda Juventus kabla ya kurejea kwa ada ya paundi milioni 89 iliyovunja rekodi ya dunia, alishindwa kuanza katika mchezo uliopita dhidi ya Bournemouth kwasababu ya kutumikia adhabu ya mechi moja aliyotoka nayo Italia. Akihojiwa kuhusu mchezo wa kesho, Pogba amesema anajisikia yuko fiti na amekuwa akifanya mazoezi kwa siku 10 lakini itategemea meneja wake Jose Mourinho atakavyoona inafaa. Pogba aliendelea kudai kuwa ameshazoea hali hiyo kwani amekuwa akifanya mazoezi hata wakati alipokuwa likizo hivyo anajiona yuko sawa.