Thursday, August 25, 2016

IHEANACHO HATIHATI KUIVAA TAIFA STARS.

NYOTA wa Manchester City, Kelechi Iheanacho yuko katika hatihati ya kuukosa mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2017 ambapo timu yake ya taifa ya Nigeria maarufu kama Super Eagles itakwaana na Tanzania, Taifa Stars huko Uyo, Septemba mwaka huu. Iheanacho aliitwa katika kikosi cha Super Eagles na kocha mpya Gernot Rohr wiki iliyopita, lakini sasa kuna uwezekano mkubwa wa mshambuliaji huyo kuukosa mchezo huo. Hatua hiyo inakuja baada ya nyota huyo kupata majeruhi katika mchezo wa City wa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Steaua Bucharest ya Romania katika Uwanja wa Etihad jana. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19, aliumia wakatia ijaribu kukimbiza mpira na haraka alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo wa kimataifa wa Brazil, Fernandinho katika dakika ya 76. Iheanacho ambaye alifunga mabao 14 kwa City katika mshindano yote msimu uliopita, bado hajawahi kufunga bao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

No comments:

Post a Comment