Wednesday, May 31, 2017

GRIEZMANN AMTUPIA MZIGO RAIS WA ATLETICO.

MSHAMBULIAJI wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann amesema anafurahia kuwepo klabu hapo na kuwa mustakabali wake uko mikononi mwa rais wa timu hiyo. Akizungumza na wanahabari, Griezmann amedai anajisikia furaha kuwepo hapo na wakala wake anazungumza na Atletico hivyo wataona kitakachotokea. Griezmann aliendelea kudai kuwa atafanya uamuzi wake majira haya ya kiangazi. Nyota huyo ambaye anahusishwa na tetesi za kwenda Manchester United, amesema tayari ameshazungumza na kocha na sasa suala lake liko mikononi mwa rais wa klabu.

DE ROSSI APEWA MKATABA MWINGINE ROMA.

MSHAMBULIAJI Daniele De Rossi amesaini mkataba mpya na AS Roma ambao utamuweka katika klabu hiyo mpak Juni mwaka 2019. Roma ilimuaga nguli wake Francesco Totti mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini sasa wamefanikiwa kumbakisha nyota mwingine. Mkataba wa De Rossi ulikuwa unamalizika mwezi ujao lakini sasa amesaini mwingine wa miaka miwili zaidi. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 aliibuliwa kutoka katika akademi ya klabu na amefanikiwa kucheza jumla ya mechi 561 katika mashindano yote toka aibukie katika kikosi cha kwanza mwaka 2001 na kufunga mabao 59. De Rossi amekuwa mchezaji muhimu msimu huu ambapo Roma imemalizika katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Serie A na kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

IBRAHIMOVIC KUBAKI LIGI KUU.

WAKALA wa Zlatan Ibrahimovic amedai kuwa mteja wake huyo anataka kubakia katika Ligi Kuu ya Uingereza lakini sio lazima kwamba atabakia Manchester United. Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Sweden, anakabiliwa na majeruhi ya muda mrefu baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti na mkataba wake na United unatarajiwa kumalizika mwezi ujao. Meneja wa United Jose Mourinho alishadokeza kuwa anataka mshambuliaji huyo abakie Old Trafford, lakini majeruhi yake yanafanya mambo kuwa magumu. Hata hivyo, Wakala wake Mino Raiola amesema kuna uwezekano wa Ibrahimovic kubakia Old Trafford lakini pia anaweza kuondoka kwani wameshapata ofa kadhaa.

WOLFSBURG YAANZA USAJILI KWA KISHINDO.

BEKI wa kimataifa wa Marekani, John Brooks ameondoka Hertha Berlin na kusajiliwa na Wolfsburg kwa ada inayoripotiwa kuvunja rekodi kwa raia wa Marekani. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amejiunga na Wolfsburg baada kupita misimu mitano akiwa hertha Berlin ambapo sasa amesaini mkataba unaomalizika mwaka 2022. Taarifa zinadai kuwa Wolfsburg imetoa kitita cha dola milioni 22.5 hivyo kuvunja rekodi iliyokuwepo ya dola milioni 13 wakati Jozy Altidore aliposajiliwa na Sunderland akitokea AZ mwaka 2013. Brooks ambaye ametokana na matunda ya akademi ya Hertha, ameichezea klabu hiyo mechi 24 na kuisaidia kumaliza katika nafasi ya sita kwenye Bundesliga msimu wa 2016-2017.

WENGER ATAKA TAJI LA LIGI KUU BAADA YA KULAMBA MIAKA MIWILI.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amedai kuwinda taji la Ligi Kuu msimu ujao baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili. Makubaliano hayo ya mkataba hayajajumuisha kipengele cha kuvunjwa na kama ukifanikiwa kukamilika anaweza kuongeza zaidi. Sio Arsenal wala Wenger mwenye umri wa miaka 67 wanaoona kama mkataba huu utakuwa wa mwisho. Akizungumza na wanahabari, Wenger amesema anaipenda Arsenal na yuko tayari kwa changamoto zilizopo mbele yao. Wenger aliendelea kudai kuwa wana kikosi imara na wakiongeza baadhi ya ya wachezaji wanaweza kupata mafanikio wanayotarajia msimu ujao.

LAUREN AUNGA MKONO WENGER KUONGEZWA MKATABA.

BEKI wa zamani wa kimataifa wa Cameroon na klabu ya Arsenal, Lauren anaamini kubaki kwa Arsene Wenger ni jambo zuri kwa timu hiyo. Meneja huyo ambaye alikuwa akikosolewa vikali msimu uliopita anatarajiwa kusaini mkataba mpya wa miaka miwili wakati wowote baada ya bodi kuafiki kumuongeza muda kocha huyo. Laureni aliyekuwa akicheza nafasi ya beki wa kulia katika kikosi cha Wenger kilichotwaa taji la Ligi Kuu msimu wa 2003-2004 bila kufungwa, anadhani ni jambo lenye tija kumbakisha kocha huyo. Lauren aliendelea kudai kuwa kikubwa anachotakiwa kufanya Wenger hivi sasa ni kuingia sokoni na kufanya usajili wa nguvu huku akihakikisha anawabakisha nyota wake akiwemo Alexis Sanchez na Mesut ozil.

CECH ATWAA TUZO NYINGINE NCHINI KWAO.

KIPA wa Arsenal, Petr Cech ametunukiwa tuzo ya Mpira wa Dhahabu ya kuwa mchezaji bora wa msimu wa 2016-2017 wa Jamhuri ya Czech. Hii ni mara ya 11 kwa golikipa huyo namba moja wa Arsenal kutwaa tuzo hiyo. Cech ameisaidia Arsenal kumaliza katika nafasi ya tano msimu huu na pia kutwaa taji la Kombe la FA kwa kuwafunga mabingwa Chelsea Jumamosi iliyopita. Tuzo hizo hutolewa kwa wanahabari wa michezo nchi humo kupiga kura na kuchagua wanasoka waliofanya vyema katika msimu husika.

Tuesday, May 30, 2017

MONACO YACHEMKA KA MAHREZ, ARSENAL NJIA NYEUPE.

KLABU ya Monaco inadaiwa kushindwa kinyang’anyiro cha kumsajili kiungo wa Leicester City, Riyad Mahrez na kuwaacha Arsenal wakipewa nafasi kubwa ya kumnasa. Mchezaji huyo bora Ligi Kuu msimu uliopita anafurahia kuishi Uingereza ambapo amekuwa mmoja kati ya mawinga bora duniani pamoja na kupoteza kiwango chake mwanzoni mwa msimu wa 2016-2017. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger alizungumza kwa simu na Mahrez mwaka jana ambapo alimuelezea nia yake ya kumsajili ingawa dili hilo halikufanikiwa. Leicester sasa wanaonekana kuwa tayari kumuachia winga huyo kama watapata ofa stahiki ya uhamisho wake. Leicester waliomaliza nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu msimu huu wana matumaini ya kupata kiasi cha paundi milioni 35 kwa kiungo huyo.

DORTMUND YAMTIMUA TUCHEL.

KLABU ya Borussia Dortmund imemtimua meneja wake Thomas Tuchel kufuatia taarifa za mgawanyiko katika vyumba vya kubadilishia nguo na kumaliza kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa Bundesliga. Klabu ilithibitisha kuondoka kwake kufuatia kuzagaa kwa madai kuwa uhusiano wa Tuchel na wachezaji wa Dortmund ulikuwa umevurugika kiasi ambacho hakiwezi kusawazishwa. Ingawa Dortmund walishinda taji la DFB Pokal Jumamosi iliyopita, lakini bado ilionekana uhusiano baina yake na wachezaji hautaweza kutengemaa. Nahodha wa klabu hiyo Marcel Schmelzer na mshambuliaji mwenye ushawishi Marco Reus wote walijiweka pembeni na kocha huyo mwenye umri wa miaka 43 ambaye atapokea kiasi cha euro milioni 2.9 kama kiinua mgongo chake. Tuchel alichukua nafasi ya Jurgen Klopp mwaka 2015 wakati kocha huyo alipondoka Signal Iduna Park baada ya Dortmund kumaliza msimu wakiwa nafasi ya saba.

WENGER AKUBALI MIAKA MIWILI ZAIDI ARSENAL.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amekubali kusaini mkataba mpya wa miaka miwili wa kuendelea kuinoa klabu hiyo aliyoiongoza kwa miaka 21. Wenger na mmiliki wa klabu Stan Kroenke walikutana jana ili kujadiliana mustakabali wake, huku uamuzi ukipelekwa kwa wakurugenzi kwenye kikao cha bodi kilichofanyika hii leo. Arsenal inapanga kutoa taarifa rasmi kuhusiana na suala hilo kesho. Klabu hiyo ilimaliza katika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu msimu huu, ikiwa ni mara ya kwanza kumaliza nje ya nne bora toka meneja huyo raia wa Ufaransa alipojiunga nao mwaka 1996. Arsenal walimaliza wakiwa alama 18 nyuma ya mabingwa Chelsea, lakini waliwachapa mabingwa hao kwa mabao 2-1 na kutwaa Kombe la FA katika Uwanja wa Wembley Jumamosi iliyopita.

AC MILAN YANASA BEKI WA VILLARREAL.


KLABU ya AC Milan imetangaza kumsajili beki wa kati Mateo Musacchio kutoka Villarreal kwa mkataba wa miaka minne. Beki huyo alifanyiwa vipimo vya afya wiki iliyopita na sasa ameshakamilisha uhamisho wake San Siro huku ikiaminika kuwa Milan wamelipa kiasi cha euro milioni 18. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, alianza soka lake katika klabu ya River Plate kabla ya kujiunga na Villarreal mwaka 2009. Akiwa Villarreal Musacchio amefanikiwa kucheza zaidi ya mechi 200 za mashindano yote lakini sasa atatua Serie A. Milan walimaliza katika nafasi ya sita kwenye Serie A msimu wa 2016-2017 na kufuzu michuano ya Europa League, lakini wanataka wamepanga msimu ujao kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

SOUTHGATE AELEZA SABABU ZA KUMUACHA ROONEY.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Gareth Southgate amesema hakuzungumza na nahodha Wayne Rooney kabla ya kufikia uamuzi wa kumuacha katika kikosi chake kwa ajili ya mechi za mwezi ujao dhidi ya Scotland na Ufaransa. Rooney ambaye ndio mfungaji bora wa wakati wote Uingereza ameanza katika mechi 15 pekee za ligi akiwa na Manchester United msimu huu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31, aliachwa pia katika kikosi kilichoitwa Machi mwaka huu kutokana na majeruhi. Akizungumza na wanahabari, Southgate amesema sababu kubwa iliyomfanya kumuacha Rooney kipindi hiki ni kiwango bora kilichoonyeshwa na wachezaji wengine wan chi hiyo.

MWENYEKITI WA CITY ADAI AGUERO HAENDI KOKOTE.

MWENYEKITI wa Manchester City, Khaldoon Al Mubarak amesema mustakabali wa Sergio Aguero hauna mashaka yeyote. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 28, ana mkataba na klabu hiyo unaomalizika mwaka 2020 lakini alipoteza nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza Februari mwaka huu mbele ya chipukizi mwenye umri wa miaka 19 Gabriel Jesus. Aguero ambaye alijiunga na City akitokea Atletico Madrid kwa kitita cha paundi milioni 38 mwaka 2011, alikaririwa Machi mwaka huu akidai kuwa hataki kuondoka katika klabu hiyo. Akiulizwa kuhusu mustakabali wa nyota huyo, Al Mubarak amesema ni mmoja kati ya wachezaji bora duniani hivyo lazima abakie.

Saturday, May 27, 2017

MAN CITY YAMMENDEA KIPA WA BENFICA.

KLABU ya Manchester City inaweza kumfanya kipa wa Benfica, Ederson kuwa kipa ghali zaidi katika historia ifikapo wiki ijayo. Taarifa kutoka nchini Ureno zinadai kuwa City wana uhakika wa kukamilisha taratibu za kumsajili kipa huyo mara baada ya kumalizika kwa fainali ya Kombe la Ureno kesho ambapo Benfica watacheza na Vitoria Guimaraes. City wanaweza kulazimika kulipa kiasi cha paundi milioni 35 kwa ajili ya kipa huyo mwenye umri wa miaka 35, kiasi ambacho kitapita kile cha paundi milioni 33 Juventus walizotoa kwa Parma kwa ajili ya kusajili Gianluigi Buffon mwaka 2001. Benfica wanamilika asilimia 50 pekee za haki ya Ederson hivyo watahitaji kiasi kikubwa cha ada ya usajili kwani watalazimika kugawana nusu kwa nusu na klabu yake ya zamani ya Brazil ya Rio Ave na wakala wa soka wa Gestifute. Jorge Mendes ambaye alikuwa jijini Manchester kusimamia uhamisho wa Bernardo Silva kwenda City ndiye wakala wa Ederson na mmiliki wa kampuni ya Gestifutre.

BARCELONA YAPATA AHUENI.

KLABU ya Barcelona imepata ahueni katika safu yao ya ulinzi kuelekea katika mchezo wao wa fainali ya Kombe la Mfalme baadae leo kufuatia taarifa za kuwepo kwa Gerard Pique, Javier Mascherano na Aleix Vidal. Pique alikosa mechi mbili za mwisho za La Liga za Barcelona kutokana na maumivu ya tumbo wakati Mascherano yeye alikosa mchezo walioshinda 4-2 dhidi ya Eibar kutokana na majeruhi ya msuli wa paja. Kurejea kwa Vidal ni jambo la kushangaza kidogo kwa hapo awali beki huyo wa kulia ilielezwa kuwa atakosa msimu wote uliosalia baada ya kupata majeruhi ya kifundo cha mguu katika mchezo walioshinda mabao 6-0 dhidi ya Alaves Februari mwaka huu. Mshambuliaji Luis Suarez na beki Sergi Roberto watakosa mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu wakati Jeremy Mathieu na Rafinha wao wakiwa nje bado kwa majeruhi. Barcelona watakuwa wakifukuzia rekodi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya 29 wakati watakapoivaa Alaves baadae leo huku pia ukiwa mchezo wa mwisho wa meneja Luis Enrique.

WATFORD WAPATA KOCHA MPYA.

KLABU ya Watford imemteua meneja wa zamani wa Hull City, Marco Silva kuwa meneja wao mpya kwa mkataba wa miaka miwili. Silva anakuwa meneja wa tisa wa Watford katika kipindi cha miaka mitano na nane toka familia ya Pozzo ya Italia ilipochukua umiliki wa timu hiyo mwaka 2012. Meneja huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 39 alichukua mikoba ya Mike Phelan Hull City Januari mwaka huu lakini alishindwa kuiwezesha kutoshuka daraja msimu huu na kujizulu Alhamisi iliyopita. Mwenyekiti wa Watford, Scott Duxbury amesema Silva ni mmoja kati ya makocha wazuri kwasasa kwenye Ligi Kuu na imani yao atawasaidia kwa ajili ya msimu ujao.

Friday, May 26, 2017

MAN CITY YANASA KIUNGO WA MONACO.

KLABU ya Manchester City imekubali kutoa kitita cha paundi milioni 43 kwa ajili ya kumsajili kiungo wa kushambulia Bernardo Silva kutoka kwa mabingwa wa Ufaransa Monaco. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 22, anatarajiwa kujiunga na City pindi dirisha la usajili la majira ya kiangazi likapofunguliwa Julai mosi mwaka huu huku klabu ikitarajiw akutangza usjaili huo Alhamisi ijayo. Silva amecheza mechi 58 akiwa na Monaco msimu huu zikiwemo mechi mbili dhidi ya City walizokutana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo amefunga mabao 11 na kusaidia mengine 12. Nyota huyo pia ameichezea Ureno mara 12 na kufunga bao moja.

SAMPAOLI KWENDA KUINOA ARGENTINA.

KLABU ya Sevilla imetangaza kufikia makubaliano na Chama cha Soka cha Argentina-AFA ili meneja wake Jorge Sampaoli aende kuwa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo. Sampaoli alijiunga na Sevilla kabla ya kuanza kwa msimu huu na kuwaongoza kushika nafasi ya nne katika msimamo wa La Liga, lakini mwishoni mwa kampeni kulizuka tetesi zilizomuhusisha kwenda kuinoa Argentina baada ya Edgardo Bauza kutimuliwa. Mwishoni mwa wiki iliyopita kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Chile alifafanua kuwa kuiongoza Argentina ni ndoto zake za kipindi kirefu na kwamba AFA inatakiwa kuzungumza na Sevilla kama wanamuhitaji. Katika taarifa yao iliyotumwa katika mtandao, Sevilla walithibitisha makubaliano baina yao kufikiwa na pande hizo mbili zitasaini makubaliano hayo Juni mosi mwaka huu. Kibarua cha kwanza cha Sampaoli kitakuwa mechi mbili za kirafiki ambazo Argentina inatarajiwa kucheza dhidi ya Brazil ,a Singapore mwezi ujao.

AUBAMEYANG MGUU NJE MGUU NDANI DORTMUND.

MSHAMBULIAJI wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang anataka kunyakuwa taji lake la kwanza akiwa na klabu hiyo kesho pamoja na tetesi kuwa mchezo huo wa fainali ya Kombe la Ujerumani unaweza kuwa wa mwisho kwenye timu hiyo. Dortmund wanatarajiwa kukwaana na Eintracht Frankfurt mchezo utakaofanyika katika Uwanja wa Olimpiki uliopo jijini Berlin. Dortmund wanataka kuondoa mkosi wa kufungwa katika fainali tatu zilizopita zilizochezwa jijini Berlin. Nahodha wa Dortmund, Marcel Schmelzer amesema kila wakati walipokuwa Berlin katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wamekuwa wakirejea nyumbani wakiwa mikono mitupu. Nahodha huyo aliendelea kudai safari hii watajirekebisha kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kuondoka na furaha. Naye Aubameyang amesema atazungumza na klabu hiyo na kufanya maamuzi baada ya fainali hiyo.

EVERTON KUJA DAR.

KLABU ya Everton inatarajiwa kuwa klabu ya kwanza inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza kucheza Tanzania wakati watakapokuja kwa ajili ya mchezo wa kirafiki kujiandaa na msimu mpya. Mchezo huo unaoratibiwa na kampuni ya ya kamari ya SportPesa unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Julai 13 mwaka huu. Klabu hiyo inatarajiwa kucheza na washindi wa SportPesa Super Cup, ambao unatarajiwa kushirikisha timu nne kutoka Kenya na nne kutoka Tanzania. Kampuni ya SportPesa yenye makao yake makuu nchini Kenya ndio wadhamini wapya wa jezi za Everton kuanzia msimu ujao.

ZABALETA KWENDA WEST HAM UNITED.

BEKI Pablo Zabaleta anatarajiwa kusaini mkataba na West Ham United akiwa kama mchezaji huru pindi mkataba wake na Manchester City utakapomalizika mwishoni mwa mwezi ujao. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 32, anatarajiwa kujiunga na West Ham kwa mkataba wa miaka miwili kuanzia Julai Mosi. Zabaleta anaondoka City baada ya kuitumikia kwa miaka tisa na kumfanya kuwa mchezaji wa tatu aliyeitumikia klabu hiyo kwa kipindi kirefu baada ya Joe Hart na Vincent Kompany. Akizungumza na wanahabri, Zabaleta amesema kubwa lililomfanya kuondoka City ni kutafuta changamoto mpya na anamatumaini ya kuisaidia West Ham katika malengo yake ya msimu ujao. Zabaleta ambaye amecheza mechi 22 za mashindano yote msimu huu akiwa na City, alijiunga nao akitokea Espanyol kwa kitita cha paundi milioni 6.5 mwaka 2008 na kufanikiwa kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu, Kombe la FA na mataji mengine mawili ya Kombe la Ligi.

VALENCIA AONGEZA MKATABA UNITED.

WINGA wa Manchester United, Antonio Valencia amesaini nyongeza ya mwaka mmoja katika mkataba wake ambao utamuweka hapo mpaka mwaka 2019 huku kukiwa na kipengele cha kuongezewa tena. Valencia mwenye umri wa miaka 31 amecheza mechi 43 za mashindano yote za United msimu huu na kukiongoza kikosi cha timu hiyo kama nahodha wakati walipotwaa taji la Europa League mbele ya Ajax Amsterdam juzi. Nyota huyo wa kimataifa wa Ecuador alijiunga na United akitokea Wigan Athletic mwaka 2009. Akizungumza na wanahabari, Valencia amesema amefurahia sana mkataba huo kwani klabu hiyo imekuwa sehemu ya maisha yake toka alipojiunga nao mwaka 2009.

LEBRONE JAMES AIPITA REKODI YA MICHAEL JORDAN WAKATI CLEVELAND CAVALIERS IKITINGA FAINALI ZA NBA.

TIMU ya mpira wa kikapu ya Cleveland Cavaliers imefanikiwa kutinga hatua ya fainali za NBA kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuichabanga Boston Celtics kwa vikapu 135-102. Sasa Cavaliers watakutana tena kwa mara tatu mfululizo na mabingwa wa Ukanda wa Magharibi Golden State Warriors katika fainali hizo. Kyrie Irving na LeBrone James kwa pamoja wamefunga alama 79 katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa TD Gardens jijini Boston na kutwaa ubingwa wa Kanda Mashariki kwa kushinda 4-1 kati ya mechi saba zilizotakiwa kuchezwa. James mwenye umri wa miaka 32, alifanikiwa kuipita rekodi ya nguli wa Chicago Bulls Michael Jordan ya mfungaji kinara wa wakati wote kwenye mechi za mtoano. Jordan aliweka rekodi ya kufunga alama 5,987 katika mechi 179, rekodi ambayo imedumu kwa miaka 19 mpaka James alipoivuka kwa kufunga alama 5,995 katika mechi 212 za mtoano alizocheza. Mechi ya kwanza ya fainali kati ya Cavaliers na Warriors inatarajiwa kuchezwa Juni mosi mwaka huu katika Uwanja wa Oracle Arena jijini Oakland.

Wednesday, May 24, 2017

CHELSEA YAAHIRISHA SHEREHE ZA UBINGWA.

KLABU ya Chelsea imeahirisha maandamano ya kusheherekea ubingwa wao wa Ligi Kuu Jumapili hii kufuatia shambulio la kigaidi jijini Manchester ambapo watu 22 walipoteza maisha. Mlipuaji wa kujitoa muhanga alilipua bomu katika tamasha la muziki lilifanyika Manchester Arena juzi ambapo watu zaidi ya 59 walijeruhiwa. Chelsea ambao wanatarajiwa kukwaana na Arsenal katika fainali ya Kombe la FA Jumamosi hii, walitoa taarifa leo kuthibitisha mpango wao wa kuhahirisha maandamano ya kusherekea taji lao. Katika taarifa yao, Chelsea wamedai kuwa wanaungana na watu wote ambao kwa namna moja au nyingine wameguswa na tukio hilo katika kuomboleza hivyo wanadhani haitakuwa vyema kuendelea na mipango yao ya sherehe kipindi hiki. Arsenal nao wamethibitisha kuahirisha onyesho la moja kwa moja la mchezo huo kutoka Wembley, ambalo lilipangw akufanyika kwenye Uwanja wa Emirates, na kuongeza hakutakuwa na maandamano ya sherehe kama wakishinda taji hilo.

RUFANI YA MESSI YATUPILIWA MBALI.

MAHAKAMA Kuu nchini Hispania imetupilia mbali rufani ya Lionel Messi akipinga kukutwa na hatia ya kukwepa kodi. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina alihukumiwa miezi 21 jela mwaka jana kwa kushindwa kulipa kodi ya euro milioni 4.1 katika haki ya matumizi ya picha yake mwaka 2007, 2008 na 2009, na kulimwa faini ya euro milioni mbili. Baba yake Jorge Messi yeye pia alipewa adhabu kama hiyo ya kifungo jela na faini ya euro milioni 1.7. Ingawa Messi asingeweza kutumikia adhabu hiyo jela kwasababu hajawahi kukutwa na kosa kama hilo huko nyuma, alikata rufani katika kile mawakili wake walichodai kuwa ishara wa uthibitisho kwa mteja wao na kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu. Rufani hiyo imetupiliwa mbali, lakini Mahakama Mkuu imepunguza adhabu mpaka miezi 15, wakati faini imebaki euro milioni 1.3 na Jorge pia atalipa kiasi kama hicho.

SCHALKE ILIMWANIA PULISIC.

MKURUGENZI wa Schalke 04, Oliver Ruhert amebainisha klabu hiyo ilitaka kumsajili Christian Pulisic kabla ya hajaimarika kimataifa kwa mahasimu wao Borussia Dortmund. Pulisic amewateka mashabiki wa Dortmund toka alipohamia hapo akitokea Marekani na kupelekea kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha meneja Thomas Tuchel msimu huu. Pulisic mwenye umri wa miaka 18 amefunga mabao matano katika mechi 42 alizocheza katika mashindano yote na kuiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Bundesliga. Hata hivyo, angeweza kugeuka adui wa timu yake ya sasa wakati Schalke walipomuwania lakini walichelewa kwani mustakabali wake tayari ulishaamuliwa. Ruhert amesema tayari walikuwa wameshaanza mazungumzo na wakala wake kuhusu kumsajili lakini waliambiwa kuwa tayari walikuwa wameshakubali ofa ya Dortmund.

FIFA WAIPONGEZA YANGA KUTWAA UBINGWA.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Gianni Infantino ametuma salama za pongezi kwa klabu ya Yanga kufuatia kutwaa taji la la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo mwishoni mwa wiki iliyopita. Taarifa hizo za pongezi zimetolewa kupitia barua yake aliyotuma kwa Shirikisho la Soka nchini-TFF kwenda kwa Katibu Mkuu wa Yanga Boniface Mkwasa. Rais wa TFF, Jamal Malinzi alithibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kudai kuwa barua rasmi kutoka FIFA atakabidhiwa Mkwasa. Yanga walitawadhwa mabingwa kwa mara nyingine Jumamosi iliyopita kwa kuwazidi mahasimu wao Simba kwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga baada ya kulingana alama wote wakiwa na alama 68 katika michezo 30.

TOFAUTI YA MAN UNITED NA AJAX.

KLABU ya Manchester United imetumia fedha nyingi zaidi kwenye usajili katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuliko mpinzani wa fainali ya Europa League Ajax Amsterdam alivyosajili toka kumalizika kwa Vita Kuu vya Pili vya Dunia. Klabu hizo mbili zinatarajiwa kuvaana baadae leo katika fainali ya michuano hiyo itakayofanyika katika Uwanja wa Friends Arena jijini Stockholm, Sweden huku kukiwa na tofauti kubwa baina yao kwenye soko la usajili. Katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita United imetumia jumla ya paundi milioni 455 kwa usajili wa wachezaji wakati kwa upande wa Ajax wao wametumia kiasi cha paundi milioni 379 kwa usajili wa wapya toka mwaka 1945. Usajili uliovunja rekodi wa Paul Pogba wa paundi milioni 89.3, Angel Di Maria paundi milioni 59.7 na Antony Martial paundi milioni 36 unaonyesha kiasi gani United wana uwezo wa kutumia fedha nyingi kwenye usajili. Kwa upande wa Ajax wao hawajawahi kutumia zaidi ya paundi milioni 14 kusajili mchezaji mmoja katika historia yao pamoja na nyota kadhaa akiwemo Luis Suarez na Zlatan Ibrahimovic kupita katika mikono yao.

ARSENAL KUMKOSA GABRIEL KOMBE LA FA.

BEKI wa Arsenal, Gabriel anatarajiwa kukosa mchezo wa Jumamosi hii wa Kombe la FA dhidi ya Chelsea utakaofanyika katika Uwanja wa Wembley kufuatia madaktari kuthibitisha kuwa anaweza kuwa fiti baada ya wiki nane au zaidi. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 alibebwa katika machela katika mchezo wa Jumapili hii dhidi ya Everton baada ya kuumia goti. Beki mwenzake Laurent Koscielny pia anatarajiwa kukosa mchezo huo baada ya Chama cha Soka cha Uingereza kutupilia mbali rufani yake kupinga kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo dhidi ya Everton. Beki mwingine anayecheza nafasi ya kati Shkodran Mustafi naye yuko katika hatihati kufuatia kupata mtikisiko wa ubongo kufuatia kugongwa kichwani katika mchezo dhidi ya Sunderland wiki iliyopita.

YAYA TOURE ATOA MSAADA KWA WAHANGA WA MANCHESTER.

KIUNGO wa Manchester City, Yaya Toure na wakala wake kila mmoja anatarajiwa kutoa kitita cha paundi 50,000 sawa na zaidi ya milioni 145 za kitanzania, kwa ajili ya wahanga wa shambulio la bomu la kujitoa muhanga jijini Manchester. Mlipuko huo uliotokea katika Ukumbi wa Manchester Arena juzi uliacha watu 22 wakipoteza maisha huku wengine zaidi ya 59 wakijeruhiwa wakati wakihudhuria tamasha la Ariana Grande. Akizungumza na wanahabari wakala wa Toure, Dimitri Seluk amesema taarifa za binti wa miaka nane aliyekwenda kumtizama mwanamuziki aliyempenda halafu hakurudi nyumbani ni jambo la kuhuzunisha kwa kiasi kikubwa. Seluk aliongeza kuwa Toure na yeye wanataka kusaidia na njia pekee wanayoona inafaa kwasasa ni kutoa kiasi hicho cha fedha kusaidia wahanga na haijalishi kama wote wanatoka Manchester au la.

CAVALIERS WAPIGA HATUA MOJA KUELEKEA FAINALI YA NBA.

TIMU ya mpira wa kikapu ya Cleveland Cavaliers imebakisha ushindi katika mechi moja ili waweze kutinga katika fainali za NBA kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuichapa Boston Celtics kwa vikapu 112-99. Cavaliers sasa wanaongoza kwa 3-1 kati ya mechi saba za fainali ya Kanda ya Mashariki. Golden State Warriors tayari wameshatinga kwenye fainali hizo kwa kushinda mechi 4-0 dhidi ya San Antonio Spurs kwenye fainali ya Kanda ya Magharibi. Warriors walitawadhwa mabingwa wa NBA mwaka 2015 lakini walitandikwa mwaka jana na Cavaliers waliokata kiu yao ya kulikosa taji hilo kwa miaka 52. Nyota wa Cavaliers Kyrie Irving na LeBron James kwa pamoja walifunga alama 76 nyumbani kwa Celitcs, ambao walikuwa bila nyota wao Issaiah Thomas aliyekuwa majeruhi. Mchezo wa tano unatarajiwa kufanyika jijini Boston kesho.

Tuesday, May 23, 2017

MANJI ATUNDIKA DARUGA YANGA.

MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Yussuf Manji, amejiuzulu wadhifa huo akidai kuwa anatoa nafasi kwa watu wengine kuiongoza.  Kupitia barua yake iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, MANJI, amesema anaondoka akiamini ameiacha Yanga ikiwa timu yenye mafanikio makubwa ya kisoka hapa nchini. Licha ya taarifa yake hiyo, pia akizungumza kwenye kwenye mahojiano na Kituo Kimoja cha Radio jijini Dar es salaam, MANJI amekiri kujiuzulu wadhifa huo. Kwa mujibu wa barua ya MANJI iliyoisaini Mei 22, mwaka huu, amejiuzulu Uenyekiti na sasa majukumu yote hadi pale uchaguzi mpya utakapofanyika wa kujaza nafasi yake majukumu yote ya Timu yatakuwa chini ya Makamu wa Rais, Sanga. SANGA amethibisha kupokea barua ya MANJI kujiuzulu akisema ni kweli amepokea barua hiyo ya mwenyekiti juu ya uamuzi wake wa kupumzika kwa sasa.


HAKUNA TISHIO FAINALI YA EUROPA LEAGUE - UEFA.

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limedai kuwa hakuna taarifa zozote za kiintelejensia zinazoonyesha kuwa fainali ya Europa League inaweza kuwa mlengwa wa shambulio kufuatia tukio lililotokea jijini Manchester. Watu wapatao 22 waliuawa na wengine 59 kujeruhiwa, wakiwemo watoto katika mlipuko uliotokea mwishoni mwa tamasha kwenye Ukumbi wa Manchester Arena jana. Polisi nchini Uingereza wamekuwa wakilichukua tukio kama la kigaidi huku Waziri Mkuu wake Theresa May akilaani vikali wote waliohusika. Tukio hilo limetokea ikiwa zimebaki saa chache kabla ya mchezo wa fainali ya Europa League kati ya Manchester United dhidi ya Ajax Amsterdam utakaofanyika jijini Stockholm, Sweden kesho. Kufuatia hofu hiyo, UEFA imewahakikishia mashabiki waliopanga kuhudhuria mchezo huo kuwa hali ya kiusalama ni shwari kabisa na hakuna tishio lolote lililoripotiwa mpaka sasa.

GOLDEN STATE WARRIORS WATINGA FAINALI ZA NBA.

TIMU ya mpira wa kikapu ya Golden State Warriors imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya NBA kwa mara ya tatu mfululizo kufuatia ushindi wa vikapu 129-115 dhidi ya San Antonio Spurs. Nyota wa Warriors Stephen Curry alifunga alama 36 na Kevin Durant alama 29 ambazo ziliisaidia kukamilisha ushindi wa 4-0 kati ya mechi saba za fainali ambazo zilipaswa kuchezwa katika Kanda ya Magharibi. Sasa Warriors wanasubiri bingwa mtetezi Cleveland Cavaliers au Boston Celtic ili waje kucheza naye fainali za NBA kuanzia Juni mosi mwaka huu. Cavaliers mpaka sasa wanaongoza kwa mechi 2-1 kwenye fainali ya Kanda ya Mashariki.

RAIS WA ZAMANI WA BARCELONA AKAMATWA.

RAIS wa zamani wa Barcelona, Sandro Rosell amekamatwa ikiwa ni sehemu ya uchunguzi kuhusiana na tuhuma za kutakatisha fedha. Watu kadhaa pia wamekamatwa na polisi kufuatia tuhuma hizo kaskazini mashariki mwa mji wa Barcelona. Polisi wamesema kukamatwa huko ni sehemu ya uchunguzi kuhusiana na haki za mauzo zinazohusiana na Brazil. Rosell alikuwa rais wa Barcelona kuanzia mwaka 2010 mpaka 2014, wakati alipojiuzulu kufuatia uamuzi wa mahakama ya Hispania kufanyia uchunguzi usajili wa nyota wa kimataifa wa Brazil Neymar mwaka 2013. Juni mwaka 2016, Barcelona ililipa faini ya euro milioni 5.5 juu ya uhamisho wa Neymar mwenye umri wa miaka 25 kutoka Santos. Mke wa Rosell ni miongoni mwa watu waliokamatwa katika sakata hilo la leo.

CONTE ATWAA TUZO YA KOCHA BORA WA LMA.

MENEJA wa Chelsea, Antonio Conte ameshinda tuzo ya kocha bora wa msimu inayotolewa na Chama cha Makocha wa Ligi Kuu ya Uingereza-LMA. Meneja huyo raia wa Italia ametwaa tuzo hiyo kufuatia kuiongoza Chelsea kushinda taji la ligi katika msimu wake wa kwanza Stamford Bridge. Meneja wa klabu ya Brighton, Chris Hughton ameshinda tuzo ya kocha bora wa msimu wa Ligi ya Ubingwa kufuatia kuipandisha daraja timu hiyo. Meneja wa Sheffield United Chris Wilder na Paul Cook wa Portmouth nao wametwaa tuzo kufuatia kuziwezesha timu zao kupanda katika Ligi ya Ubingwa kutoka ligi daraja la kwanza. Conte ambaye timu yake imeweka rekodi ya kushinda mechi 30 za Ligi kuu, anaweza kutwaa taji la pili Jumamosi hii wakati watakapocheza na Arsenal katika fainali ya Kombe la FA.

Monday, May 22, 2017

SAFU YA ULINZI YA ARSENAL UTATA.

KLABU ya Arsenal inakabiliwa na tatizo kwenye safu yake ya ulinzi kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea Jumamosi hii, kufuatia Shkodran Mustafi kuwa katika hatihati ya kutocheza kutokana na majeruhi. Beki huyo mwenye umri wa miaka 25 alijigonga kichwani katika mchezo dhidi ya Sunderland uliochezwa Jumanne iliyopita. Mustafi alimaliza kwenye mchjezo huo lakini alipata dalili za mtikisiko kwenye ubongo hatua ambayo ilipelekea kuachwa kwenye mchezo wa jana dhidi ya Everton. Beki mwingine Laurent Koscielny atakosa fainali hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Wembley akitumikia adhabu wakati Gabriel naye alitolewa nje kwa machela jana. Mustafi alijiunga na Arsenal kwa kitita cha paundi milioni 35 majira ya kiangazi na amefanikiwa kucheza mechi 37 katika klabu hiyo msimu huu.

JUVENTUS YAMUWANIA KEITA

MKURUGENZI mkuu wa Juventus, Giuseppe Marotta amethibitisha kuwa mabingwa hao wa Serie A wanamuwania mshambuliaji wa Lazio Balde Keita, lakini amedai hakuna makubaliano yeyote yaliyofikiwa. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23, amekuwa na msimu mzuri kufuatia kufunga mabao 16 katika mechi 31 za ligi alizoichezea Lazio. Kiwango chake hicho hakijaivutia Juventus pekee bali pia Manchester United na Chelsea lakini suala la usajili bado linaonekana kuwa mbali kwasasa. Akizungumza na wanahabari, Marotta amesema hakuna makubaliano yeyote yaliyoafikiwa juu ya Keita hivyo bado ni mchezaji wa Lazio na ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi. Marotta aliendelea kudai kuwa wanamfuatilia Keita kwa karibu kwani wanataka kumsajili lakini kwasasa wametulia.

MMILIKI WA ARSENAL AKANUSHA KUTAKA KUUZA HISA ZAKE.

MWANAHISA mkubwa wa Arsenal, Stan Kroenke amesema hajwahi kutaka kuuza hisa zake anazomiliki kwenye klabu hiyo. Kampuni ya Kroenke inayojihusisha na masuala ya michezo na burudani ilitoa kauli hiyo mapema leo kufuatia taarifa kuwa Alisher Usmanov ametoa ofa ya paundi milioni moja kwa ajili ya kuchukua umiliki wa klabu hiyo. Katika taarifa yake kampuni hiyo ya Kroenke imeiongeza kuwa wamepanga kuwekeza Arsenal kwa kipindi kirefu na wanatarajia kubakia hivyo. Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya Arsenal kushindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 20. Kroenke anamiliki hisa asilimia 67 Arsenal, huku Usmanov yeye akimiliki hisa asilimia 30 lakini hashiriki vikao vya bodi au kutoa maamuzi ya klabu.

TOURE ATAKA KUSTAAFU AKIWA CITY.

KIUNGO wa Manchester City, Yaya Toure amesema anataka kumaliza soka lake akiwa na klabu hiyo na kuongeza kuwa itakuwa vigumu kuvaa jezi ya timu nyingine. Mkataba wa Toure unatarajiwa kumalizika Julai mwaka huu na sio yeye wala meneja Pep Guardiola aliyeweza kudokeza kama nyota huyo wa kimataifaw a Ivory Coast atapewa ofa ya mkataba mwingine. Beki Pablo Zabaleta aliagwa katika mchezo wa mwisho wa City kucheza nyumbani wiki iliyopita baada ya kuihabalisha klabu kuwa hataongeza mkataba mwingine pindi huu wa sasa utakapomalizika majira ya kiangazi. Akizungumza na wanahabari mara baada ya ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Watford jana, Toure amesema bado anahitaji kucheza zaidi kwani anaona bado ana uwezo wa kuisaidia City kupata mataji zaidi.

Friday, May 19, 2017

24 WAITWA TAIFA STARS.

KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ataja kikosi cha wachezaji 24 watakaoweka kambi kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wao wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2019, dhidi ya Lesotho Juni 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

KALOU AITWA TENA IVORY COAST.

KOCHA mpya wa Ivory Coast, Marc Wilmots ametaja kikosi chake kwanza toka alipoteuliwa kuchukua kibarua hicho machi mwaka huu. Ivory Coast inakabiliwa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Uholanzi Juni 4 na mchezo mwingine wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika siku tano baadae dhidi ya Guinea. Katika kikosi hicho cha wachezaji 27, Wilmots amemjumuisha winga wa Hertha berlin Salomon Kalou ambaye anaonekana bado ataendelea kucheza soka la kimataifa. Kalou alikuwa akifikiria mustabali wake ujao kwa soka la kimataifa baada ya Ivory Coast waliokuwa mabingwa watetezi walipoenguliwa katika michuano ya Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu. Wilmots ambaye kabla ya kutua Ivory Coast alikuwa akiinoa Ubelgiji, pia amemjumuisha mshambuliaji aliyekosekana kwa kipindi kirefu Seydou Doumbia.

WENGER KUFAHAMU MUSTAKABALI BAADA YA KOMBE LA FA.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema mustakabali wake katika klabu hiyo utaamuliwa katika kikao cha bodi baada ya fainali ya Kombe la FA Mei 27 mwaka huu. Meneja huyo raia wa Ufaransa, mwenye umri wa miaka 67 amekuwa na Arsenal toka mwaka 1996 na mkataba wake unamalizika kipindi hiki cha majira ya kiangazi. Wenger amekuwa akikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo wengi wao wakimuhitaji aachie ngazi. Akizungumza na wanahabari, Wenger amesema kuna mambo yatajadiliwa katika mkutano huo wa bodi na moja kati yake ni juu ya kitakachotokea kwa meneja. Wenger aliendelea kudai kuwa yeye mwenyewe atakuwepo kwenye kikao hicho, lakini kwasasa wamehamishia nguvu zao katika mechi zao za mwisho. Arsenal watavaa na mabingwa wa Ligi Kuu Chelsea katika Uwanja wa Wembley.

GRIEZMANN ATAJA ATAKAENYAKUA TUZO YA BALLON D'OR LAKINI SIO RONALDO.

MSHAMBULIAJI nyota wa Atletico Madrid, Antonio Griezmann hategemei kama mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo atashinda tuzo ya Ballon d’Or mwakani. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita tuzo hizo zimekuwa zikitawaliwa na nyota wawili Ronaldo na mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi huku Griezmann akiikaribia tuzo hiyo kwa kushika nafasi ya tatu mwaka jana. Lakini pamoja na wadau wengi kumpigia chapuo Ronaldo kutwaa tuzo hiyo baada ya kufunga mabao matano katika mechi za mikondo miwili dhidi ya Bayern Munich kabla ya kuja kufunga hat-trick dhidi ya Atletico na kutinga fainali, bado Griezmann haoni kama nyota huyo ataitwaa tuzo hiyo. Akizungumza na wanahabari, Griezmann amesema kwa mawazo anadhani Juventus ndio watakaotwaa taji la Ligi ya Mabingwa na Ulaya na kipa wao Gianluigi Buffon ndio atayetwaa tuzo hiyo badala ya Ronaldo.

POCHETTINHO AMMWAGIA SIFA KANE BAADA YA KUPIGA NNE.

MENEJA wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino amesema Harry Kane ni mmoja kati ya washambuliaji bora duniani na kusisitiza kuwa klabu hiyo inaweza kuwabakisha wachezaji wake bora kwa ajili ya msimu ujao. Kane mwenye umri wa miaka 23, alifunga mabao manne katika ushindi wa mabao 6-1 waliopata Spurs dhidi ya Leicester City katika Uwanja wa King Power na kukwea mpaka kileleni kwenye orodha ya wafungaji bora akiwapita Romelu Lukaku na Alexis Sanchez. Akizungumza na wanahabari, Pochettino amesema Kane ni mchezaji muhimu na anayependa kuitumikia Spurs. Pochettino aliendelea kudai kuwa wachezaji wote wanaowahitaji watakuwepo kwa ajili ya msimu ujao na kama mchezaji yeyote ataondoka itakuwa ni juu ya klabu yenyewe. Kane aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita kwa kufunga mabao 25, msimu huu tayari ameshafikisha mabao 26 huku kukiwa kumebaki mechi moja msimu kumalizika.

MSIMU UJAO SITAFANYA MAKOSA - MOURINHO.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amesisitiza hatafanya makosa katika msimu wake wa pili Old Trafford haswa ikizingatiwa kuwa kwasasa anaifahamu vyema klabu hiyo kwa undani. Mourinho bado anaweza kumaliza msimu wake wa kwanza kwa kushinda mataji mawili kama akifanikiwa kuichapa Ajax Amsterdam katika fainali ya Europa League wiki ijayo baada ya kuwa tayari wameshatwaa taji la Kombe la Ligi. Lakini walishindwa kutamba katika Ligi Kuu na wanatarajiwa kumaliza katika nafasi ya sita katika msimamo pamoja na matokeo yeyote watakayopata katika mechi ya mwisho dhidi ya Crystal Palace Jumapili hii. Hiyo inamaanisha kuwa Europa League ndio nafasi yao ya pekee iliyobaki ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Akizungumza na wanahabari, Mourinho amesema msimu wa kwanza ulikuwa mgumu lakini anadhani atafurahia msimu wa pili kwakuwa anajua hataweza kufanya makosa.

Thursday, May 18, 2017

BENZEMA AACHWA TENA UFARANSA, DESCHAMPS ATOA SABABU.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps amesema maelewano yaliyopo katika kikosi chake hawezi kuyahatarisha kwa kumuita tena mshambuliaji wa Real Madrid Karim Benzema. Benzema hajaitwa katika kikosi cha Ufaransa toka aliposhitakiwa na polisi kwa tuhuma za kujihusisha na genge la watu waliokuwa wakimuandama mchezaji mwenzake wa nchi hiyo Mathieu Valbuena, kesi ambayo bado haijafikishwa mahakamani. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 mwaka jana alikosa michuano ya Ulaya iliyofanyika katika ardhi yao ya nyumbani kutokana na tuhuma hizo, ingawa rais wa Shirikisho la Soka la Ufaransa-FFF, Noel Le Grael tayari alishatangaza Februari kuwa uamuzi wa Benzema kuitwa unabaki kwa Deschamps. Hata hivyo, Benzema kwa mara nyingine amekosa kwenye kikosi hicho ambacho kinatarajiwa kucheza mechi tatu dhidi ya Paraguay, Sweden na Uingereza Juni mwaka huu.

BAYERN WASINGEPATA URAHISI UINGEREZA - KLOPP.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema Bayern Munich wasingeweza kupata urahisi wa Bundesliga kama ingekuwa klabu ya Ligi Kuu ya Uingereza. Klopp bado ndio meneja pekee aliyezima utawala wa Bayern kwenye soka la Ujerumani kufuatia kuingoza Borussia Dortmund kutwaa mataji mawili mfululizo ya Bundesliga mwaka 2011 na 2012. Toka kipindi hicho Bayern imerejea katika utawala wake huku Dortmund, Wolfsburg na RB Leipzig zikishindwa kuizuia timu hiyo. Bayern waliirarua Arsenal kwa jumla ya mabao 10-2 msimu huu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa kuhusu nafasi ya Bayern kama ingekuwa klabu ya Uingereza, Klopp amesema haingekuwa rahisi kutwaa taji la ligi kama wanavyofanya kwenye Bundesliga.

VURUGU ZASABABISHA MCHEZO KUSITISHWA.

MECHI ya hatua ya mtoano kutafuta nafasi ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kati ya Panathinaikos na PAOK Salonika imelazimika kusitishwa kufuatia kutoka kwa vurugu. Mchezo huo ulishuhudia mwamuzi akitoa kadi nne nyekundu, mashabiki wakipigana wenyewe kwa wenyewe huku kocha wa PAOK Vladimir Ivic akipigwa na chupa ya maji kichwani na kukimbizwa hospitali. Panathinaikos ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 katika mchezo huo kabla ya mwamuzi kuamua kusitisha katika dakika ya 55. Kabla ya kusitisha mchezo huo kabisa mwamuzi Giorgos Kominos aliusimamisha kwa muda wakati kocha Ivic akipatiwa matibabu ya awali kabla ya kukimbizwa hospitali na kushonwa nyuzi kadhaa. PAOK, Panathinakos, AEK Athens na Panionios zote zipo kwenye hatua ya mtoano kutafuta mshindi mmoja ambaye ataungana na mabingwa wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, Olympiakos katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

MOURINHO ALIA NA WASIMAMIZI WA LIGI KUU.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amesema inakatisha tama kuwa Ligi Kuu ya Uingereza haijali kuhusu kuzisaidia timu za Uingereza zikiwa na mechi katika michuano ya Ulaya. United inatarajiwa kupambana na Crystal Palace katika mchezo wao wa mwisho wa ligi Jumapili hii, siku tatu kabla ya mchezo wao wa fainali ya Europa League. Ushindi dhidi ya Ajax Amsterdam jijini Stockholm Jumatano ijayo, utaifanya United kupata nafasi ya moja kwa moja katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Akizungumza na wanahabari, Mourinho amesema katika kila nchi duniani mechi ingechezwa Jumamosi, kwani wataendelea kubakia nafasi ya sita kwa matokeo yeyote watakayopata na Palace wako eneo salama. Mourinho aliendelea kudai kuwa katika kipindi cha miaka saba aliyokaa Uingereza hajabahatika kuona jitihada zozote za kujaribu kuzisaidia timu za hapo zinapokuwa katika mashindano ya Ulaya.