KLABU ya Manchester United imetumia fedha nyingi zaidi kwenye usajili katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuliko mpinzani wa fainali ya Europa League Ajax Amsterdam alivyosajili toka kumalizika kwa Vita Kuu vya Pili vya Dunia. Klabu hizo mbili zinatarajiwa kuvaana baadae leo katika fainali ya michuano hiyo itakayofanyika katika Uwanja wa Friends Arena jijini Stockholm, Sweden huku kukiwa na tofauti kubwa baina yao kwenye soko la usajili. Katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita United imetumia jumla ya paundi milioni 455 kwa usajili wa wachezaji wakati kwa upande wa Ajax wao wametumia kiasi cha paundi milioni 379 kwa usajili wa wapya toka mwaka 1945. Usajili uliovunja rekodi wa Paul Pogba wa paundi milioni 89.3, Angel Di Maria paundi milioni 59.7 na Antony Martial paundi milioni 36 unaonyesha kiasi gani United wana uwezo wa kutumia fedha nyingi kwenye usajili. Kwa upande wa Ajax wao hawajawahi kutumia zaidi ya paundi milioni 14 kusajili mchezaji mmoja katika historia yao pamoja na nyota kadhaa akiwemo Luis Suarez na Zlatan Ibrahimovic kupita katika mikono yao.
No comments:
Post a Comment