Saturday, November 30, 2013

CECAFA CHALENJI: KILI KUTPA KARATA YA PILI DHIDI YA SOMALIA.

TIMU ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars baadae leo inatarajia kutupa karata yake ya pili kwa kucheza na Somalia katika michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA. Stars ambayo inanolewa na kocha Kim Poulsen ilitoka sare ya bao 1-1 na timu mwalikwa ambayo ni Zambia hivyo ushindi katika mchezo wa leo utakuwa ni muhimu kwao ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo. Poulsen ambaye alilalamika tatizo la uwanja kujaa maji katika mechi ya kwanza hivyo kupelekea wachezaji wake kucheza chini ya kiwango amesema hawatapuuza mchezo wao dhidi ya Somalia ambao walibamizwa mabao 2-0 na Burundi. Katika mchezo wingine wa kundi B utakaochezwa leo Zambia watakwaana na Burundi mchezo ambao utafuata baada ya ule wa Stars kumalizika.

Picha kwa hisani ya Bin Zubery.

BAHRAIN GRAND PRIX KUFANYIKA USIKU MWAKANI.

MASHINDANO ya langalanga ya Bahrain Grand Prix mwakani ayanatarajiwa kufanyika usiku ili kusheherekea miaka 10 ya mashindano hayo nchini humo. Waandaaji wa mashindano hayo hivi wako katika pilikapilika za kufunga mfumo mpya wa taa ili mashindano hayo yaweze kufanyika kwa ufanisi na mafanikio. Ofisa Mkuu wa mashindano hayo nchini Bahrain Sheikh Salman bin Is Al-Khalida amesema hakuna njia nzuri zaidi ya kusherekea miaka 10 zaidi ya kufanya madereva washindane usiku. Bahrain itakuwa nchi ya pili kuandaa michuano hiyo usiku huku Singapore wao wakiwa wa kwanza kwa kuandaa mashindano hayo usiku toka mwaka 2008.

ETO'O NJE WIKI MBILI.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amesema mshambuliaji wake Samuel Eto’o atakaa nje ya kikosi cha timu hiyo kwa kipindi cha wiki mbili baada ya kutolewa nje katikati ya wiki katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya jijini Basle. Mourinho aliwaambia waandishi wa habari kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Cameroon alipata majeraha makubwa katika msuli wa nyuma ya paja. Kocha aliongeza kuwa beki David Luiz amerejea katika mazoezi jana baada ya kuumia mguu lakini mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Southampton Jumapili itakuwa ni mapema sana kwake kucheza. Chelsea ambao wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi, watacheza na Southampton nyumbani kabla ya kupepetana na Sunderland na Stoke City ugenini.

BILIONEA WA ARSENAL ATETEA MATAJIRI WA KIGENI KATIKA SOKA LA UINGEREZA.

BILIONEA wa Uingereza ambaye anamiliki hisa katika klabu ya Arsenal, Alisher Usmanov ametetea wageni wanaomiliki klabu za Ligi Kuu akidai kuwa ni jambo zuri kwa soka la nchi hiyo. Bilionea huyo amesema kuongeza kwa wamiliki kutoka nje ya nchi hiyo hakuna maana kuwa kutabadili muonekano wa soka la nchi hiyo. Na wakati akiisifia Arsenal kwa kuanza msimu vyema bilionea huyo amedai kuwa pia ana haki ya kukosoa bodi ya klabu hiyo kama ataona hawafanyi mambo kwa ufasaha. Bilionea huyo raia wa Urusi ambaye anakadiriwa kuwa na utajiri unafikia paundi bilioni 13, ametumia zaidi ya paundi milioni 200 kwa zaidi ya miezi ili kununua asilimia 30 ya hisa za klabu hiyo.

SAMATTA, ULIMWENGU KIBARUANI.

KLABU ya TP Mazembe leo ina kibarua kizito wakati watakapokuwa wenyeji wa timu ya CS Sfaxien ya Tunisia katika fainali ya mkondo wa pili ya Kombe la Shirikisho mchezo ambao utafanyika katika Uwanja wa Mazembe jijini Lubumbashi. Mazembe watatakiwa kushinda mabao 3-0 ili kuhakikisha wanatwaa taji hilo baada ya kufungwa mabao 2-0 katika fainali ya mkondo wa kwanza iliyofanyika katika Uwanja wa Olympique de Rades jijini Tunis wiki iliyopita. Hiyo itakuwa nafasi ya kipekee kwa wachezaji nyota wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza katika klabu hiyo kuandika historia ya kuvaa medali katika michuano mikubwa kabisa barani Afrika. Bingwa katika michuano hiyo ataibuka na kitita cha dola za kimarekani 625,000 wakati mshindi wa pili atachukua dola 432,000.

Friday, November 29, 2013

SIJUTI KUHAMIA MADRID - BALE.

WINGA mahiri Gareth Bale anafikiri kuwa Real Madrid ni klabu kubwa ulimwenguni na amedhamiria kushinda mataji akiwa hapo katika miaka mingi ijayo. Nyota huyo wa kimataifa wa Wales alijiunga na Madrid akitokea klabu ya Tottenham Hotspurs katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi kwa ada iliyovunja rekodi ya euro milioni 100 na amesisitiza kuwa hajuti kuhamia Santiago Bernabeu. Bale aliuambia mtandao wa klabu hiyo kuwa kwa mawazo yake anadhani klabu hiyo ni bora duniani, wana wachezaji bora na uwanja mzuri huku kila kitu hapo kikiwa sawa. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa anataka kufanya kila awezalo ili kuisaidia timu na kushinda mataji ili kumuonyesha kila mtu kwamba Madrid ni klabu kubwa. Bale mwenye umri wa miaka 24 pia alimpongeza nyota mwenzake Cristiano Ronaldo na kudai kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ureno yuko katika ligi yake ya kipekee. Amesema anadhani Ronaldo ni mchezaji bora duniani na ameonyesha hilo msimu huu tena akiwa chini ya shinikizo kama ilivyokuwa katika mchezo wa mtoano kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Sweden.

DRC KUTEUA KOCHA MPYA KABLA YA CHAN.

SHIRIKISHO la Soka la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limethibitisha kutaja jina la kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo kabla ya michuano inayokuja ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani yatakayofanyika nchini Afrika Kusini. Nchi imekuwa bila kocha toka alipoondoka Mfaransa Claude Le Roy ambaye aliondoka baada ya kushindwa kuiwezesha timu hiyo kufuzu hatua ya mtoano katika kusaka tiketi ya Kombe la Dunia 2014. Mwenyekiti wa shirikisho hilo Constant Omari alithibisha hilo na kudai kuwa watateua kocha mpya Desemba au mapema Januari kabla ya kuanza michuano hiyo. DRC ambao wameshinda michuano hiyo mwaka 2009, walikata tiketi baada ya kuiondosha Cameroon katika mechi za kufuzu.

SIOGOPI KUPANGWA NA REAL MADRID WALA BARCELONA - PELLEGRINI.

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Manuel Pellegrini amesema haogopi kupangwa pamoja na timu kati ya Barcelona au Real Madrid katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Kikosi cha Pellegrini tayari kimefuzu hatua ya makundi lakini wanaweza kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa watetezi Bayern Munich ambao watacheza nao katika mechi ya mwisho katika hatua ya makundi. Hata hivyo, Pellegrini ambaye ni raia wa Chile amesema hawatakuwa na uoga kwa yoyote watakayepangwa nae katika hatua ya timu 16 bora na anaamini kuwa timu zingine nazo hazitataka kukutana na City. Pellegrini amesema Hispania ina timu ngumu haswa Barcelona na Real Madrid lakini pia Atletico Madrid nao wamekuwa na msimu mzuri lakini alitamba kuwa hawamuogopi yoyote watakayekutana naye kwasababu anaamini ana kikosi imara.

HATUNA MPANGO WA KUHAMISHA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA 2014 NJE YA BRAZIL.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amedai kuwa hawana mpango wa kuhamisha michuano ya Kombe la Dunia 2014 nje ya Brazil pamoja na tukio lilitokea wakati wa maandalizi ya michuano hiyo itakayochezwa kipindi majira ya kiangazi. Watu wawili walifariki baada ya crane kuanguka na kuharibu sehemu ya Uwanja wa Corinthians Arena uliopo jijini Sao Paulo. Brazil inatarajiwa kucheza mchezo wake wa ufunguzi katika uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza watazamani 65,000 katika siku zisizozidi 200. Pamoja na tukio hilo Blatter ameendelea kusisitiza kuwa hakuna mpango mwingine wowote kuhusiana na michuano hiyo kwasasa. Serikali ya Brazil imekiri kufanya jitihada ili kukamilisha viwanja 12 vitakavyotumika kwa ajili ya michuano hiyo lakini mpaka sasa ni viwanja sita pekee vilivyokuwa tayari huku vingine sita vilivyobakia vikiwa bado kumalizika.

LAHM NJE WIKI MBILI KWA MAUMIVU YA MSULI.

NAHODHA wa klabu ya Bayern Munich, Philipp Lahm anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili baada ya kuumia msuli wa paja katika ushindi wa mabao 3-1 iliyopata timu yake dhidi yake dhidi ya CSKA Moscow Jumatano iliyopita. Lahm mwenye umri wa miaka 30 alifanyiwa vipimo wakati timu hiyo iliporejea jijini Munich na anatarajiwa kukosa mechi mbili zijazo za Ligi Kuu nchini Ujerumani maarufu kama Bundesliga. Katika taarifa iliyotolewa katika mtandao wa klabu hiyo, Lahm atakosa mechi kati ya Bayern dhidi ya Eintracht Braunschweig utakaochezwa kesho na pia mchezo dhidi ya Augsburg. Mbali na Lahm, Bayern pia itawakosa nyota wake wengine kutokana na majeruhi wakiwemo Bastian Schweisteiger, Franck Ribery, Claudio Pizarro na Xherdan Shaqiri.

PAMOJA NA KUGONGA 40 MKONGWE GIGGS BADO ANATAKA KUENDELEA KUCHEZA.

KIUNGO mkongwe wa klabu ya Manchester United, Ryan Giggs hana mpango wowote wa kutundika daluga pamoja na kufikisha umri wa miaka 40 leo. Kiungo huyo wa kimataifa wa Wales amekuwa akiitumikia klabu hiyo yenye maskani yake Old Traford kipindi chote akiwa amecheza mechi 953 toka alipocheza katika kikosi cha kwanza cha United kwenye mechi dhidi ya Everton mwaka 1991. Giggs amesema anajisikia mwenye bahati kucheza katika klabu moja kwa kipindi chote hicho huku akiwa amezungukwa na wachezaji na pamoja na kocha mzuri. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa ingawa kunakuwa na vipindi vigumu muda mwingine lakini bado anafurahia kuwepo hapo kwa kipindi kirefu kadri kiwango chake kitakavyomruhusu. Amesema kama angekuwa anahama kutoka klabu moja kwenda nyingine angekuwa ameshakwisha hivi sasa kama ilivyo kwa wenzake walioanza pamoja kama David Beckham, Paul Scholes, Nick Butt, Gary Neville na Phill Neville.

UEFA YAMLIMA ADHABU YA MECHI TATU MBOKANI KWA KUMTUKANA MWAMUZI.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, Dieumerci Mbokani ametwangwa adhabu ya kufungiwa mechi tatu na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA baada ya kukutwa na kosa la kumtukana mwamuzi. Katika taarifa yake UEFA imesema Mbokani mwenye umri wa miaka 28 anayekipiga klabu ya Dynamo Kyiv alitumia maneno yasiyo ya kiungwana kwa mwamuzi wakati wa mchezo wa makundi wa michuano ya Europa League mapema mwezi huu. Dynamo Kyiv ilithibitisha adhabu hiyo jana lakini hawakuweka wazi kama wataka rufani kupinga adhabu hiyo kwa mchezaji wao. Mbokani amecheza misimu mitatu katika klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji, akicheza mechi 53 na kufunga mabao 34.

Thursday, November 28, 2013

TANZANIA YAKWEA VIWANGO FIFA.

TANZANIA imekwea kwa nafasi tano katika viwango vya soka vinavyoandaliwa kila mwezi na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Mwezi uliopita Tanzania ambayo imekuwa ikishuka na kupanda katika viwango hivyo iliporomoka mpaka nafasi ya 129 lakini katika viwango vilivyotolea leo imepanda tena mpaka katika nafasi ya 124. Kwa upande wa Afrika Ivory Coast imeendelea kuongoza kwa kushika nafasi ya 17 katika viwango vya dunia ikifuatiwa na Ghana waliopo katika nafasi ya 24 huku Algeria wakiwa nafasi ya tatu kwa kushika namba 26. Wengine ni Nigeria waliopo nafasi ya 36 na tano bora kwa upande wa Afrika inafungwa na Misri waliokwea kwa nafasi 13 moaka nafasi ya 38 katika viwnago hivyo.


WAWILI WAFA KATIKA AJALI KWENYE UWANJA WA KOMBE LA DUNIA BRAZIL.

WATU wawili wamekufa katika ajali kwenye moja ya viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil mwakani. Vifo hivyo vimetokea wakati crane lilipoanguka na kuharibu sehemu ya Uwanja wa Corinthians Arena uliopo jiji Sao Paulo nchini humo. Brazil inatarajiwa kucheza mechi yake ya ufunguzi wa michuano hiyo katika uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza watu 65,000 Juni 12 mwakani. Msemaji wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA amesema waandaaji wa michuano hiyo watafanya uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo huku rais wa shirikisho hilo akituma salamu zake za rambirambi kwa ndugu waliofiwa na jamaa zao.

NGULI WA ZAMANI WA ARSENAL ALAZWA KWA MARADHI YA SARATANI.

BEKI na kocha msaidizi wa zamani wa klabu ya Arsenal, Pat Rice ambaye aliitumikia timu hiyo ya Ligi Kuu nchini Uingereza kwa miaka 44 amelazwa hospitali kutokana na matatizo ya saratani. Rice, aliyewahi kuwa meneja wa muda wa Arsenal, alijiunga na klabu hiyo mwaka 1964 kabla ya kustaafu mwaka uliopita akiwa msaidizi wa kocha Arsene Wenger. Akihojiwa na mtandao wa Daily Mail msemaji wa Arsenal, amesema kila mtu katika klabu hiyo anamtakia heri Rice huku mawazo na fikra zao zikiwa karibu na familia yake katika kipindi hiki kigumu wanachopitia. Rice mwenye umri wa miaka 64 amecheza mechi 528 katika misimu 14 aliyochezea Arsenal baada ya kujiunga na kikosi cha vijana kilichoshinda Kombe la FA mwaka 1971. Baada ya kustaafu soka akiwa katika klabu ya Watford, Rice alijiunga na Arsenal tena akiwa kama kocha wa vijana mwaka 1984 kabla ya kuongeza ujuzi na kupanda cheo mpaka kuwa msaidizi wa Wenger na kushinda vikombe saba wakiwa wote.

BAYERN YAFIKIA REKODI YA BARCELONA KATIKA CHAMPIONS LEAGUE.

MABINGWA watetezi wa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, Bayern Munich wameendeleza ubabe katika ligi hiyo baada ya kuicharaza CSKA Moscow ya Urusi kwa mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Khimki Arena. Mabao ya Bayern katika mchezo huo yalifungwa na Arjen Robben, Mario Gotze na Thomas Mueller aliyefunga kwa mkwaju wa penati. Huo unakuwa ushindi wa 10 mfululizo kwa Bayern kwenye michuano hiyo hivyo kuvunja rekodi ya mwaka 2002 iliyowekwa na klabu ya Barcelona. Bayern ambayo inanolewa na Pep Guardiola inakabiliwa na mchezo wa mwisho dhidi ya Manchester City ambao ndio utakaoamua nani atamaliza kinara katika kundi D.

OFISA WA NFF AFUNGIWA MIAKA 10 KWA KULA MLUNGULA.

SHIRIKISHO la Soka nchini Nigeria-NFF limetangaza kumfungia mmoja wa maofisa wake ambaye pia ni kiongozi wa klabu kwa miaka 10 kutokana na kujihusisha na masuala ya rushwa. NFF ilimfungia Olaleye Adepoju ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo kutokana na kosa la kupokea rushwa kutoka katika mojawapo ya vilabu vinashiriki Ligi Kuu nchini Nigeria. Kamati ya dharura ya NFF pia ilitoa adhabu kama hiyo kwa Dapo Lam-Adesina kutokana na tukio hilo ambapo wawili hawataruhusiwa kujishughulisha na mambo ya soka ili kupisha uchunguzi. Adepoju anatuhumiwa kupokea rushwa ya dola 9,400 kabla ya kusikilizwa kesi ya kinidhamu dhidi ya klabu ya Shooting Stars kutoka Ibadan ambao ni mji mkuu wa jimbo la Oyo.

VILLAS BOAS APUUZA TETESI ZA KUTIMULIWA.

MENEJA wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Andre Villas-Boas ameponda ripoti kuwa anatakiwa kufukuzwa na kusisitiza kuwa anaungwa mkono bodi ya timu hiyo. Tetesi hizo zimekuja kufuatia Spurs kuchabangwa mabao 6-0 na Manchester City Jumapili iliyopita ikiwa ni kipigo kikubwa zaidi kupata toka walipofungwa na mabao 7-1 na Newcastle mwaka 1996. Matokeo hayo ambayo Villas-Boas ameelezea kama ya aibu, yameifanya timu hiyo kucheza mechi tatu bila kupata ushindi. Villas Boas amesema ana uhakika na bodi pamoja na wachezaji katika kikosi chake kwamba watasahau matokeo hayo na kuhakikisha wanafanya vyema katika mechi zao nyingine. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa amefanya mkutano na bodi lakini hakuona dalili zozote za kutaka kumtimua kwakuwa bado wameonyesha imani kwake.

MADRID INAWEZA KUFANYA VYEMA BILA RONALDO - DI MARIA.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Real Madrid, Angel Di Maria anaamini kuwa timu hiyo imeonyesha kwamba inaweza kukua bila kuwa na nyota wao Cristiano Ronaldo baada ya kuigaragaza Galatasaray kwa mabao 4-1 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Ronaldo hakuwepo katika mchezo huo lakini hilo halikuwa kikwazo kwa kikosi hicho kinachonolewa na Carlo Ancelotti kupata ushindi ambao ambao umewavusha mpaka katika hatua ya mtoano ya michuano hiyo. Di Maria mwenye umri wa miaka 25, ambaye alifunga bao la tatu katika mchezo huo anafikiri mchezo huo ulikuwa muhimu kwao kwasbabu umewafanya kuongoza kundi B. Madrid walicheza sehemu kubwa ya mchezo huo wakiwa pungufu baada ya beki Sergio Ramos kutolewa kwa kadi nyekundu mapema. Madrid kwasasa wanaongoza kundi B wakiwa na alama 13, saba zaidi ya Juventus wanashika nafasi ya pili na tisa zaidi ya Galatasaray na Copenhagen wanaoshika nafasi ya tatu na nne.

Wednesday, November 27, 2013

ASAMOAH ATAMBA KUIFUNGIA GHANA MABAO KATIKA KOMBE LA DUNIA.

KIUNGO wa Juventus Kwado Asamoah ambaye hajawahi kuifungia bao lolote timu yake ya taifa ya Ghana amedai kuwa ameyatunza mabao yake kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Brazil. Nyota huyo anataka kuisaidia Ghana kwa kufunga mabao katika michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi katika majira ya kiangazi mwakani. Asamoah amesema lengo lao kubwa lilikuwa ni kuhakikisha wanafuzu kwenda Brazil na baada ya kufanya hivyo sasa ni wajibu wao kuhakikisha wanafanya vyema kwenye michuano hiyo. Amesema pamoja na kushindwa kufunga bao lolote katika hatua za kufuzu anadhani sasa nafasi hiyo ataipata akiwa na timu hiyo kwenye michuano hiyo.


MARTINO APONDA KIWANGO CHA WACHEZAJI WAKE.

KOCHA wa klabu ya Barcelona, Gerardo Martino ameponda kiwango cha wachezaji wake walichokionyesha katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao walitandikwa mabao 2-1 na Ajax katika uwanja wa Amsterdam Arena. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Martino amesema katika kipindi cha kwanza wachezaji wake walikuwa wamepoteana kabisa hivyo kuwapa mwanya wapinzani wao kuwafunga mabao mawili. Martino aliendelea kudai kuwa katika kipindi cha pili walifanikiwa kubadilisha mchezo na kucheza walivyozoea lakini walikuwa wamechelewa kwani tayari walikuwa wako nyuma. Kocha huyo amesema pamoja na kuwakosa nyota wake kadhaa kutokana na majeruhi lakini walipaswa kumiliki mpira eneo la kati kama walivyozoea kitu ambacho walishindwa kukifanya kipindi cha hivyo kukaribisha mashambulizi yaliyowaletea madhara. Pamoja na hayo kocha huyo anaamini watayafanyia kazi makosa hayo yaliyojitokeza ili kuhakikisha wanafanya vyema katika mechi zao nyingine pamoja na balaa la majeruhi linalowakabili.

SCHALKE WALILAUMU GHANA JUU YA BOATENG.

VIONGOZI wa klabu ya Schalke ya Ujerumani wameilaumu Ghana baada ya kiungo wao mahiri Kevin-Prince Boateng kushindwa kuitumikia timu hiyo katika mchezo wa ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Akiwa anaiwakilisha nchi yake kwa mara ya kwanza toka atangaze kustaafu soka la kimataifa Boateng aliifungia Ghana bao katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Misri ambao uliwawezesha kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Pamoja na hayo kocha wa Schalke Jens Keller amesema toka mchezaji huyo aende Ghana wiki mbili zilizopita hawajaridhishwa na kiwango chake na hawajua ni kitu gani kimemsibu huko. Mbali na Keller kulalamikia hilo pia mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo Horst Heldt alidai kuwa safari ya mchezo huyo kwenda Ghana imemharibia badala ya kumjenga na andependa kama angeahirisha safari hiyo.

NDEGE YA MAN UNITED YASHINDWA KUTUA UJERUMANI.

NDEGE iliyobeba kikosi cha Manchester United imelazimika kuahirisha kutua ikiwa mita 400 juu ya barabara wakati wakielekea nchini Ujerumani kwa ajili mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Bayer Leverkusen. Hata hivyo ndege hiyo ilitua salama katika jaribio lake la pili katika Uwanja wa Ndege wa Cologne. Klabu hiyo ilikataa kutoa taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo. United itafanikiwa kufuzu hatua ya mtoano ya michuano hiyo kama wakifanikiwa kushinda mchezo wao huo utakaochezwa katika uwanja wa Bay Arena.

TUNATAKIWA KUMALIZA KAZI SIO KUBWETEKA - WENGER.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amewataka wachezaji wake kutobweteka na kumaliza kazi baada ya kukaribia kuvuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya hatua ya mtoano kwa kuigaragaza Olympique Marseille kwa mabao 2-0. Mabao mawili ya timu hiyo yalifungwa na kiungo mahiri Jack Wilshere katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Emirates na kuifanya Arsenal kufikisha alama 12 katika michezo mitano waliyocheza kwenye kundi F. Arsenal itatakiwa kuepuka kipigo wakati watakapoifuata Napoli nchini Italia kwenye mechi yao ya mwisho itakayochezwa katika uwanja wa San Paolo Desemba 11 mwaka huu. Akihojiwa Wenger amesema ni jambo la ajabu kushindwa kufuzu wakati umefikisha alama 12 lakini ndio ukweli wenyewe hivyo hawapaswi kubweteka kabla hawajamaliza kazi.

Tuesday, November 26, 2013

KOBE BRYANT KUENDELEA KUWA MCHEZAJI ANAYELIPWA ZAIDI NBA.

NYOTA wa mpira wa kikapu nchini Marekani, Kobe Bryant amekubali kusaini mkataba mpya wa miaka miwili utakaomfanya kuweka rekodi ya kuichezea Los Angeles Lakers kwa misimu 20. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 anakuwa mchezaji wa kikapu aliyecheza timu moja katika Ligi Kuu ya Kikapu nchini humo-NBA kama akisaini mkataba huo mpya. Kuna taarifa kuwa Bryant atakatwa kiasi cha paundi milioni 3.71 lakini ataendelea kubakia kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika ligi hiyo akiwa anakunja kitita cha paundi milioni 15 kwa mwaka. Mtendaji Mkuu wa Lakers, Mitch Kupchak amesema nia na madhumuni ya kumuongeza mkatba nyota huyo ni kuhakikisha anastaafu akiwa hapo. Bryant ambaye ameshinda taji la NBA maera tano akiwa na Lakers, hajacheza meci yoyote toka msimu huu uanze kutokana na majeruhi lakini tayari ameanza mazoezi.

TOURE ATAMBA KUIVUNJA REKODI YA MABAO YA CHELSEA.

KIUNGO wa klabu ya Manchester City Yaya Toure anaamini kuwa kikosi chao kinaweza kuvunja rekodi ya mabao ya msimu katika Ligi Kuu nchini Uingereza. Kiungo huyo mwenye nguvu amempa jeuri kocha Manuel Pellegrini juu ya uwezo wa kushambulia unaoleta matumaini ya taji kwa kusema rekodi ya Chelsea iko hatarini. Kocha Carlo Ancelotti akiwa na kikosi maridadi msimu wa 2009-2010 aliiwezesha Chelsea kufunga mabao 103 na kutwaa taji misimu minne iliyopita. Na baada ya timu ya Pellegrini kufikisha mabao 34 wakiifunga mabao 6-0 Tottenham Hotspurs Jumapili, Toure amesema lengo lao ni kuvunja rekodi hiyo.

DORTMUND HAKUNA MGOGORO - KLOPP.

MENEJA wa klabu ya Borussia Dortmund, Jurgen Klopp amekanusha kuwa timu yake iko katika mgogoro baada ya kupata vipigo katika mechi tatu mfululizo. Dortmund walianza na kipigo cha kushtusha kutoka kwa Wolfburg na baadae kuporomoka kwa alama saba mbele ya vinara wa Bundesliga Bayern Munich kwa kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa mahasimu wao hao huku wakifungwa bao 1-0 nyumbani na Arsenal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Hata hivyo, Klopp amesisitiza kuwa wachezaji wake hawajaathirtiwa chochote na vipigo hivyo mfululizo huku akitegemea kikosi chake kurejesha makali na kushinda katika mchezo wao dhidi ya Napoli baadae leo. Klopp amesema pamoja na timu yake kutofanya vyema katika mechi tatu zilizopita anaamini wachezaji wake watarejesha morali iliyopotea haswa ikizingatiwa wametoka kuzitumikia timu zao za taifa ya wengine wameshinda katika mechi zao. Kwasasa Dortmund wanashika nafasi ya tatu katika kundi F wakiwa na alama tatu nyuma ya Arsenal na Napoli.

WENGER AKANA KUTAKA KUMSAJILI HENRY KWA MARA YA TATU.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger ameondoa uwezekano wa kumsainisha nguli wa zamani wa klabu hiyo Thierry Henry kwa mara ya tatu baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa kuanza mazoezi na timu hiyo. Henry ambaye kwasasa anacheza katika klabu ya New York Red Bull ya Marekani na kiungo wa zamani wa Arsenal Robert Pires mwenye umri wa miaka 40 wamekuwa wakifanya mazoezi na timu hiyo yenye maskani yake kaskazini mwa jiji la London ili kujiweka fiti. Henry ambaye ni mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi wakati akiwa na klabu hiyo alijiunga nao kwa mkopo Januari mwaka jana lakini Wenger amesema hana mpango wa kuchukua nyota huyo kwa mkopo tena. Wenger amesema kwasasa Henry anaruhusiwa kufanya nao mazoezi wakati akiweza na akitaka lakini sio kumsajili kwani wana kikosi kilichokamilika na kinachweza kutoa upinzani kwa timu yoyote.

DESAILLY AWATABIRIA MAZURI IVORY COAST.

NGULI wa soka wa Chelsea, Marcel Desailly anaamini kuwa timu ya taifa ya Ivory Coast inaweza kwenda mpaka katika nusu fainali katika michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Brazil mwakani. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa alizungumza hayo wakati akiwa jijini Nairobi katika ziara na Kombe la Ligi Kuu nchini Uingereza. Desailly amesema ni jambo la kuhudhunisha kuona timu zitakazoliwakilisha bara la Afrika katika michuano hiyo karibu zote zimetokea Afrika Mgharibi na kudai kuwa Afrika Mashariki na Kusini zimeachwa nyuma kitu ambacho hakikutakiwa. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF ni lazima lihakikishe linachukua hatua za makusudi ili kukuza soka katika upande unaoonekana kuwa nyuma ili bara zima liweze kushiriki yanapokuja mashindano hayo. Akiulizwa timu anayoipa nafasi kati ya tano zilizofuzu michuano hiyo Desailly amesema anafikiri Ivory Coast wanaweza kufanya vyema na kufika nusu fainali katika michuano hiyo mwakani.


Monday, November 25, 2013

PACQUIAO SASA AMTAKA MAYWEATHER.

BONDIA Manny Pacquiao amedai kuwa yuko tayari kupambana na Floyd Mayweather lakini ni juu ya Mmarekani huyo kusema ni lini wapigane. Pacquiao ambaye ni raia wa Philippines alipata ushindi wake wa kwanza katika miaka miwili wakati alipomtandika Brandon Rioas katika pambano la uzito wa welter kugombea mkanda wa WBO lilifanyika Jumamosi iliyopita. Bondia huyo mwenye umri wa miaka 35 amesema kazi yake ni kupigana na yuko tayari kupambana na Mayweather hivyo ni juu yake kukubali au kumuogopa kwa kukataa. Migogoro katika matangazo na masuala mengine ndio yamekuwa kikwazo kwa wawili hao kupigana.


OLYMPIQUE MARSEILLE SIO WA KUBEZA - CAZORLA.

SAFARI ya Arsenal kuelekea katika hatua ya timu 16 bora katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya inaweza kuonekana kama rahisi kutokana na mchezo wa nyumbani dhidi ya Olympique Marseille baadae leo lakini wameonywa kuchukulia mchezo huo kwa umakini. Arsenal ndio wanaoongoza kundi F wakiwa na alama tisa katika mechi nne walizocheza, wakiwa sambamba na Napoli waliopo katika nafasi ya pili na Borussia Dortmund waliopo katika nafasi ya pili. Kama Arsenal ikifanikiwa kuifunga Marseille na Dortmund wakishindwa kuifunga Napoli, kikosi cha Arsenal Wenger kitakuwa kimekata tiketi ya kucheza hatua hiyo huku wakiwa wamebakiwa na mchezo mmoja. Pamoja na hayo kiungo wa Arsenal, Santi Cazorla ameonya kuwa hawapaswi kudharau mchezo hata kama Marseille hawataweza kufuzu hatua hiyo. Cazorla amesema hata kama Marseille hawajapata alama yoyote katika kundi lao lakini wataufanya mchezo huo kuwa mgumu kwao kwasababu hawana cha kupoteza.

ROONEY AKIRI KUMPIGA KIATU MUTCH WA CARDIFF CITY.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Manchester United, Wayne Rooney amekiri kufanya makosa wakati alipomkwatua Jordon Mutch katika mchezo dhidi ya Cardiff City ambao walitoka sare ya kufungana mabao 2-2 jana. Mwamuzi wa mchezo huo Neil Swarbrick aliamua kumpa kadi ya njano nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 badala ya kumpa kadi nyekundu kutokana na tukio hilo. Rooney aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akikiri kuwa baada ya kuangalia tukio hilo tena amekubali kwamba alimchezea vibaya Mutch. Naye kocha wa United, David Moyes pia alikiri Rooney kucheza faulo lakini akadai kwamba kadi ya njano aliyopewa alistahili na sio nyekundu kama wengine wanavyodai.

UZI MPYA WA BRAZIL HUU HAPA.

TIMU ya taifa ya Brazil, imezindua jezi mpya zilizotengenezwa na wadhamini wao kampuni ya Nike huku kocha Luis Filipe Scolari akitamba kuwa wako tayari kunyakuwa taji lao la sita la michuano ya Kombe la Dunia katika ardhi yao ya nyumbani mwakani. Nyota wa Barcelona, Neymar na kiungo wa Wolfsburg ya Ujerumani Luiz Gustavo ni mojawapo ya wachezaji waliopiga picha kuzitangaza jezi hizo mpya katika ufukwe maarufu wa Copacabana. Scolari amezionya timu pinzani katika michuano hiyo kwamba wapo tayari kuhakikisha wanaweka historia mpya kwa kunyakuwa taji hilo kwa mara ya sita. Kocha huyo pia alisifu mwonekano mzuri wa jezi hizo na kutania kuwa kilichokosekana katika jezi hizo ni nyota sita akimaanisha idadi ya mataji ya michuano hiyo waliyochukua. Uzinduzi wa nembo ya 2014 ni mwanzo wa kampeni za Nike ambapo jezi ya Brazil ndiyo huwapatia mauzo makubwa kimataifa.

MARK WEBBER ATAKUMBUKWA DAIMA KATIKA LANGALANGA - ALONSO.

DEREVA wa mashindano ya langalanga, Fernando Alonso amedai kuwa wapenzi wa mashindano hayo watamkumbuka Mark Webber kufuatia dereva huyo wa Red Bull kuamua kustaafu. Webber ambaye ni raia wa Australia alikamata nafasi ya pili katika mashindano ya Grand Prix ya Brazil nyuma ya dereva mwenzake wa Red Bull Sebastian Vettel pamoja na rafiki yake wa karibu Alonso ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu. Alonso ambaye ni dereva wa Ferrari amesema hawezi kusahau mashindano hayo ya Brazil jinsi walivyokuwa wakishindana ndio maana watamkumbuka siku zote. Mbali na Alonso nyota mwingine wa langalanga aliyetoa heshima zake kwa Webber ni pamoja na bingwa mara nne wa dunia wa michuano hiyo Vettel ambaye amedai kuwa watamkosa mmoja wa madereva hodari na mwenye haiba ya kipekee.

Friday, November 22, 2013

FAINALI ZA KLABU BINGWA YA DUNIA ZITAKUWA BORA,

ZIKIWA zimebaki wiki mbili kabla ya kuanza kutimua vumbi kwa michuano ya Klabu ya Bingwa, rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Sepp Blatter anaamini kuwa wenyeji Morocco wako tayari kwa ajili ya michuano hiyo. Blatter amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea hatua za mwisho za maandalizi ya michuano hiyo pamoja na timu zitakazoshiriki. Rais huyo amesema timu zitakazoshiriki michuano hiyo ni pamoja na Guangzhou Evergrade ya China ambao ni mabingwa wa Ligi ya Mabingwa barani Asia, Bayern Munich mabingwa wa Ulaya na Al Ahly mabingwa wa Afrika. Wengine ni Auckland City mabingwa Oceania, Monterrey mabingwa wa CONCACAF, Atletico Mineiro mabingwa wa Amerika Kusini na Raja Casablanca ambao wameingia katika michuano hiyo kama wenyeji.

ZIDANE ALIKUWA BORA KULIKO MESSI - PELE.

NGULI wa soka wa zamani wa Brazil, Pele amedai kuwa Zinedine Zidane alikuwa mchezaji bora kuliko alivyo Messi wakati akiwa katika kiwango cha juu lakini akabainisha kuwa angemchagua nyota huyo wa Barcelona badala ya Cristiano Ronaldo katika tuzo za Ballon d’Or. Zidane alifanikiwa kushinda taji la Kombe la Dunia na Ulaya wakati akiitumikia Ufaransa kipindi hicho pamoja na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na baadae Ballon d’Or wakati akiwa anacheza klabu ya Real Madrid. Pamoja na kwamba wadau wengi wa soka wakidai kwamba Messi ni mmoja wa wachezaji bora kabisa kuwahi kutokea akiwa ameshinda tuzo ya Ballon d’Or mara nne mfululizo, Lakini Pele ana mawazo tofauti kuhusiana na hilo. Pele amesema kwa juhudi binafsi anadhani Zidane alikuwa bora kuliko Messi, na ukilinganisha wachezaji aliokuwa akicheza nao kipindi hicho huwezi kuwalinganisha kwa kiwango sawa na wachezaji anaocheza nao Messi kama Xavi Hernandez na Andres Iniesta. Pele aliendelea kudai kuwa pamoja na hayo angemchagua Messi kushinda tuzo ya Ballon d’Or badala Ronaldo kwasababu ya mbinu za hali ya juu alizonazo anapokuwa uwanjani.

WALCOTT FITI KUIKABILI SOUTHAMPTON.

VINARA wa Ligi Kuu nchini Uingereza, klabu ya Arsenal imepata ahueni baada ya winga wao mahiri Theo Walcott kurejea tena katika kikosi cha timu hiyo katika mchezo dhidi ya Southampton utakaochezwa kesho katika Uwanja wa Emirates. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amepongeza uwepo wa nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza aliyejiunga na klabu hiyo akiwa na miaka 16 mwaka 2006 baada ya kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara msimu huu. Wenger amesema anapomkosa mchezaji kama Walcott huwa inakuwa tatizo katika kikosi chake kutokana na umahiri na umakini wake anakuwa karibu na lango la adui. Hata hivyo Wenger aliendelea kudai kuwa hawezi kumtumia nyota huyo moja kwa moja kwasababu ndio kwanza ametoka kwenye majeruhi hivyo ataangalia wakati unafaa kumtumia kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi.

BURKINA FASO WAFIKISHA MALALAMIKO FIFA.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA, limethibitisha kupata malalamiko kutoka Shirikisho la Soka la Burkina Faso kuhusiana na mchezo wao wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia ambapo nchi hiyo ilifungwa bao 1-0 na Algeria. Maofisa hao wa Burkinabe wameiandikia FIFA kulalamikia baadhi ya maamuzi yaliyofanywa na mwamuzi Badara Diatta wa Senegal wakati wa mchezo huo, maamuzi ambayo yalipelekea kukataliwa kwa bao lao katika kipindi cha kwanza. Shirikisho hilo pia limelalamikia kadi ya njano aliyopewa nahodha wa Algeria Madgid Bougherra wakidai kuwa alistahili kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi nahodha wa Burkinabe Charles Kabore katika eneo la hatari. Uamuzi wa FIFA unatarajiwa kuhusiana na tukio la mchezo huo unatarajiwa kutolewa Desemba 5, siku moja kabla ya ratiba kamili ya Kombe la Dunia.

AYEW KUFANYIWA UPASUAJI.

KLABU ya Olympique Marseille imedai kuwa mshambuliaji wake nyota wa kimataifa wa Ghana Andre Ayew atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi miwili kutokana na majeraha ya mguu yanayomkabili. Ayew alipata majeraha wakati wa mchezo wa mkondo wa pili hatua ya mtoano ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia ambapo Ghana ilifungwa kwa mabao 2-1 na Misri Jumanne. Pamoja na kipigo hicho Ghana ilifuzu michuano hiyo itakayofanyika mwakani kwa jumla ya mabao 7-3 katika mechi mbili walizocheza na Misri. Nyota huyo ambaye anatarajiwa kufanyiwa upasuaji Jumatatu atakosa safari ya kwenda jijini London ambapo Marseille itakwaana na Arsenal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Thursday, November 21, 2013

POULSEN ATAJA 23 WATAKAOIWAKILISHA BARA KATIKA CHALENJI.

KOCHA Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 23 watakaoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayofanyika nchini Kenya kuanzia Novemba 27 mwaka huu. Kilimanjaro Stars iliyotwaa kombe hilo mara ya mwisho mwaka 2010 chini ya Kocha Jan Poulsen, na ambayo imepangwa kundi B katika michuano ya mwaka huu itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos. Wachezaji wanaounda kikosi hicho cha Tanzania Bara ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam). Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam). Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC). Kilimanjaro Stars inatarajia kuondoka Jumatatu (Novemba 25 mwaka huu) kwenda Nairobi kushiriki michuano hiyo itakayoanza Novemba 27 mwaka huu na kumalizika Desemba 13 mwaka huu.MECHI DHIDI YA STARS, ZIMBABWE YAINGIZA MIL 50/-
Mechi ya kirafiki ya kimataifa ya FIFA Date kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (The Warriors) iliyochezwa juzi (Novemba 19 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 50,980,000 kutokana na watazamaji 7,952. Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000. Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 7,776,610.17 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 3,682,560. Asilimia 15 ya uwanja sh. 5,928,124, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 7,904,166 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 1,976,041. Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 17,784,373 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 889,219 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.

BARCELONA KUWAKOSA MESSI NA VALDES MWAKA HUU.

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu nchini Hispania, Barcelona italazimika kucheza mechi zao nane zilizosalia kwa mwaka huu kuanzia mechi ya Jumamosi dhidi ya Granada bila ya mshambuliaji wake mahiri Lionel Messi na golikipa Victor Valdes. Messi yuko kitandani akiuguza msuli wa nyuma ya paja la mguu wake wa kushoto wakati Valdes ambaye amekuwa katika kiwango cha juu msimu huu naye amechanika msuli wa mguu wake wa kulia. Kama hiyo haitoshi, kuingo mchezeshaji wa timu hiyo Xavi Hernandez naye kuna hati hati ya kuukosa mchezo wa Jumamosi kutokana na majeraha ya msuli wa kigimbi na Jordi Alba naye bado yuko kitandani akijiuguza. Hata hivyo majeruhi hayawezi kuibabaisha klabu hiyo kutokana na historia ya nyuma kwani Valdes na Messi wamewahi kukosekana katika kikosi kwa muda unaofanana mwaka 2007 na timu hiyo kufanikiwa kushinda mechi 13 kati ya 16 walizocheza bila yao.

GUARDIOLA APATA AHUENI BAADA YA BOATENG KUWA FITI TAYARI KWA DORTMUND.

KOCHA wa klabu ya Bayern Munich Pep Guardiola amepata habari njema kutoka katika meza ya madaktari wa timu hiyo kuelekea katika mchezo wa mwishoni mwa wiki dhidi ya mahasimu wao Borussia Dortmund. Madaktari wa timu hiyo wamemhakikishia kocha huyo kwamba beki wake tegemeo Jerome Boateng anatakuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo muhimu wa Bundesliga. Beki huyo wa kati aliumia kisigino wakati akiitumikia Ujerumani katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Uingereza ambao walishinda kwa bao 1-0 na Bayern walikuwa na hofu nyota huyo kukosekana katika mchezo huo wa Jumamosi. Hata Hivyo, Boateng mwenye umri wa miaka 25 alithibitisha kuwa atakuwepo katika mchezo huo utakaopigwa katika Uwanja wa Signal Iduna Park jijini Dortmund. Katika mchezo huo Bayern watakuwa wakisaka ushindi ili kuongeza pengo la alama kufikia nne katika msimamo wa Bundesliga wakati wapinzani wao watakuwa wakipambana ili kuhakikisha wanabakisha pengo la alama moja baina yao.

ALVES AMFAGILIA RONALDO KUCHUKUA BALLON D'OR.

BEKI mahiri wa klabu ya Barcelona, Dani Alves amekiri kuwa mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo yuko katika kiwango bora kuliko hasimu wake katika tuzo za Ballon d’Or Lionel Messi na Franck Ribery lakini anafikiri kukosa taji lolote kwa Ronaldo msimu huu kunaweza kumgharimu kuikosa tuzo hiyo. Ronaldo mwenye umri wa miaka 28 amekuwa katika kiwango cha juu toka kuanza kwa msimu wa 2013-2014, akiwa amefunga mabao 24 katika mechi 17 alizocheza huku akifunga mabao mengine manne yaliyoiwezesha Ureno kukata tiketi ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Wakati akikiri kiwango kikubwa cha nyota huyo, Alves anaamini kuwa kukosa taji lolote kwa Madrid katika msimu wa 2012-2013 kutamuweka katika nafasi mbaya kwenye tuzo hizo. Alves amesema karata yake inakwenda kwa Messi au Ribery na kama sio Messi basi anayestahili tuzo hiyo ni Ribery kwasababu ameshinda kila na alikuwa mhimili muhimu kwa timu ya Bayern Munich.

ORODHA KAMILI YA TIMU 32 ZILIZOFUZU KOMBE LA DUNIA 2014.

URUGUAY imekuwa taifa la mwisho kukata tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 zitakazopigwa nchini Brazil baada ya kutoka sare ya 0-0 na Jordan katika mchezo wa mkondo wa pili hatua ya mtoano. Uruguay katika mchezo wa kwanza walipata ushindi wa mabao 5-0 na katika mchezo huo wa pili uliopigwa jijini Montevideo walitawala sehemu kubwa ya mchezo na walikaribia kufunga baada ya kichwa kilichopigwa na Diego Godin kugonga mlingoti. Nchi hiyo ya America Kusini ambao kwasasa wanakamata nafasi ya sita kwenye ubora wa viwango vya dunia walishinda taji hilo 1930 na 1950 na wakafika nusu fainali kwenye fainali zilizopigwa nchini Africa Kusini 2010. Orodha kamili ya timu 32 zitakazoshiriki michuano hiyo kwa upande wa bara la Afrika ni Algeria, Cameroon, Ghana, Ivory Coast, Nigeria, bara la Asia ni Australia, Iran, Japan na Korea Kusini wakati Ulaya itawakilishwa na Ubelgiji, Bosnia-Hercegovina, Croatia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Ugiriki, Italia, Uholanzi, Ureno, Urusi, Switzerland na Hispania. Nyingine ni Costa Rica, Honduras, Mexico na Marekani ambazo zinawakilisha nchi za Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean huku bara la Amerika Kusini likiwakilishwa na Argentina, Brazil ambao ni wenyeji, Colombia, Ecuador, Chile na Uruguay.

FIFA KUTUMIA SPRAY MAALUMU KATIKA MICHUANO YA KLABU BINGWA YA DUNIA.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limepanga kutumia kutumia spray maalumu katika sehemu ya mstari wa ukuta kabla ya kupigwa adhabu kwenye michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia ili kuwarahisishia waamuzi. Katika taarifa yake FIFA imesema spray hiyo itatumika kwenye michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi December 11-21 nchini Morocco baada ya kufanyiwa majaribio kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 na 20. Spray hiyo ambayo hupotea baada ya dakika moja itakuwa inapulizwa uwanjani kuchora mstari wa kupanga ukuta wa timu inayopigiwa adhabu, kitu ambacho kitaondoa kadi za njano ambazo hupewa mchezaji anayekaidi maamuzi ya mwamuzi ya kuonesha sehemu ya kuweka ukuta wa kulinda lango lao. Klabu bingwa ya dunia ya vilabu itazihusisha Bayern Munich ya Ujerumani, Atletico Mineiro ya Brazil, Guangzhou Evergrande ya China, Al Ahly ya Misri, Monterrey ya Mexico, Auckland City ya New Zealand na Raja Casablanca ya Morocco.

Wednesday, November 20, 2013

DESCHAMPS APEWA MIAKA MIWILI ZAIDI BAADA YA KUIWEZESHA UFARANSA KWENDA BRAZIL.

RAIS Shirikisho la Soka la Ufaransa, Noel Le Graet ametangaza kumuongeza mkataba kocha watimu ya taifa ya nchi hiyo Didier Deschamps ambao utamalizika mwaka 2016. Mkataba wa sasa wa Deschamps ulikuwa unamalizika baada ya fainali ya Kombe la Dunia lakini Le Graet alithibitisha kumuongeza mkataba kocha huyo baada ya ushindi dhidi ya Ukraine katika Uwanja wa Stade de France na kuwahakikishia nafasi ya kwenda Brazil. Akizungumza mara baada ya mchezo huo Le Graet amesema anamuunga mkono kocha huyo kwa asilimia 100 ndio wameona wamuongeze mkataba mwingine wa miaka miwili. Deschamps alisema mapema kwamba angeachia ngazi kama Ufaransa ingeshindwa michuano hiyo lakini ushindi wa mabao 3-0 waliopata ulitosha kuwahakikishia nafasi hiyo kwa jumla ya mabao 3-2 katika mechi mbili walizokutana na Ukraine.

MAJERUHI WAZIDI KUIANDAMA BARCELONA.

KLABU ya Barcelona imekumbwa na balaa la majeruhi kwa wachezaji wake jana baada ya nyota wake watatu kupata majeruhi wakati wakiwa katika majukumu ya kimataifa. Nyota hao walioumia ni pamoja na Xavi Hernandez ambaye vipimo vilionyesha amepata majeruhi ya msuli nyuma ya paja, Victor Valdes aliyetolewa katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Afrika Kusini na Cristian Tello aliyeumia kifundo cha mguu katika mazoezi. Golikipa Valdes ambaye amekuwa katika kiwango kizuri msimu huu alilazimika kutolewa nje katika kipindi cha pili kwenye mchezo huo ambao Hispania walichapwa kwa bao 1-0 katika Uwanja wa Soccer City jijini Johannesburg na nafasi yake kuchukuliwa na Iker Casillas. Shirikisho la Soka nchini Hispania-REEF limetoa taarifa katika ukurasa wa twitter wa timu ya taifa ya nchi hiyo kuwa wanahofu Valdes alichanika msuli katika kigimbi cha mguu wake wa kulia hivyo wanasubiri vipimo ili kujua ukubwa wa tatizo hilo. Nayo klabu ya Barcelona katika mtandao wake imethibitisha kutokuwa na uhakika wa kuwatumia kiungo wake Xavi na Tello katika mchezo wa La Liga Jumamosi dhidi ya timu ya Granada.

UFARANSA YAENDA BRAZIL KWA STAILI, RONALDO AMFUNIKA IBRAHIMOVIC.

TIMU ya taifa ya Ufaransa imefanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil baada ya kufanikiwa kugeuza matokeo na kuiondosha Ukraine huku Cristiano Ronaldo naye akiihakikishia Ureno kwenda huko kwa kupiga mabao matatu peke yake. Timu hizo vigogo wa soka vya Ulaya zinaungana na Croatia, Ugiriki, Ghana na Algeria kuelekea katika fainali hizo zinazochezwa majira ya kiangazi mwakani baada ya kufanikiwa kushindwa mechi zao za mtoano za mkondo wa pili jana. Ufaransa wao waligeuza matokeo ya kufungwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza kwa kuibugiza Ukraine kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Mamadou Sakho, Karim Benzema na linguine la kujifunga la Oleg Gusey na kuifanya nchi hiyo kufuzu kwa jumla ya mabao 3-2. Kwa upande wa Ureno wao walifanikiwa kuigaragaza Sweden kwa mabao 3-2 na kufuzu kwa jumla ya mabao 4-2 katika mechi mbili za mtoano walizokutana.

ROBINHO AIPITA REKODI YA PELE.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Brazil, Robinho amefanikiwa kuifungia Brazil bao la ushindi akitokea benchi katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Chile na kumfanya nyota huyo kufikisha mabao tisa aliyowafunga wapinzani wao hao wa Amerika Kusini. Robinho ambaye sasa ameipita rekodi iliyoweka na Pele kwa kufunga bao moja zaidi yake dhidi ya Chile, aliitwa tena katika kikosi cha nchi hiyo mapema mwezi huu kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki baada ya kukaa nje kwa kipindi cha miaka miwili. Brazil inatarajiwa kucheza mechi moja zaidi ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini jijini Johannesburg Machi mwakani kabla ya kocha Luis Filipe Scolari hajatangaza kikosi cha mwisho cha Kombe la Dunia. Fainali za Kombe la Dunia mwakani zinaandaliwa na Brazil ikiwa ni mara ya kwanza toka mwaka 1950 walipofanya hivyo.

UHOLANZI YAMALIZA MWAKA BILA KUFUNGWA.

TIMU ya taifa ya Uholanzi imefanikiwa kumaliza mwaka bila kufungwa mechi hata moja baada ya kutoka sare ya bila ya kufungana na Colombia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jijini Amsterdam. Uholanzi ilifanikiwa kucheza pungufu na wachezaji 10 pekee kwa karibu saa moja baada ya Jeremain Lens kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 35 huku pia wakiwakosa Sien de Jong na Rafael van der Vaart walioumia kabla ya mapumziko. Kukosekana kwa wachezaji hao huku mmoja akitolewa nje moja kwa moja kuliwapunguza makali Uholanzi ambao walikuwa wakicheza nyumbani na kuwafanya kutumia muda mwingi wa mchezo kujilinda. Uholanzi ambayo ilitoka sare ya mabao 2-2 na Japan Jumamosi iliyopita, imeshinda mechi saba na kutoa sare tano katika mechi 12 walizocheza mwaka 2013.