Friday, August 31, 2012

BOLT BLAKE WANG'ARA DIAMOND LEAGUE.

WANARIADHA nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt na Yohane Blake wameendelea kung’aa katika msimu wa mwishoni wa michuano ya Diamond League baada ya kushinda katika mbio za mita 100 na 200. Wawili hao hawajakimbia pamoja toka walipofanya hivyo katika michuano ya Olimpiki, walikwepana tena katika mbio hizo baada ya Bolt kushinda za mita 200 akitumia muda wa sekunde 19.66 na Blake kushinda za mita 100 akitumia muda wa sekunde 9.76. Akiongea kabla ya mbio hizo Blake ambaye ni mshindi wa medali ya fedha katika michuano ya olimpiki alisema kuwa anategemea kushangaza watu tena katika mbio hizo lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na hali ya hewa ya mvua iliyokuwepo. Blake alishinda kirahisi mbio hizo baada ya mpinzani wake mkubwa Tyson Gay kutoka Marekani kuondolewa baada ya kuanza kuchomoka kabla ya wenzake. Mkenya David Rudisha ambaye alivunja rekodi yake mwenyewe ya dunia aliyoweka katika mbio za mita 800 katika michuano ya olimpiki alishindwa kutamba katika mbio hizo baada ya kupitwa wakati wakumalizia mbio hizo na Mohammed Aman kutoka Ethiopia.

VALCKE ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA VIWANJA BRAZIL.

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Jerome valcke amesema kuwa maandalizi kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil yanaendelea vyema. Valcke amesema kuwa viwanja vyote vinajengwa kwa wakati huku miradi mingine nayo ikiendelea vizuri na kufikia kasi ambayo FIFA ilikuwa inahitaji ili viweze kukamilika kwa wakati. Kauli aliitoa baada ya kufanya ziara yake ya nne nchini humo kuangalia maendeleo ya maandalizi akipingana na kauli yake aliyoitoa Machi mwaka huu kuhusu maandalizi ya nchi hiyo na kuzua mtafaruku mkubwa na serikali ya nchi hiyo. Baadae valcke aliomba msamaha kuhusiana na kauli yake hiyo akidai watu walichukulia suala alilosema kwa ubaya kabla ya Rais wa FIFA kuomba radhi kuhusiana na suala hilo. Valcke alitembelea kuangalia maendeleo ya viwanja na miundo mbinu katika mji wa Manaus uliopo Kaskazini mwa nchi hiyo pamoja na mji wa Cuiaba ambao upo katikati mwa jimbo la Mato Grosso.

SERENA ATINGA RAUNDI YA TATU US OPEN.

MCHEZAJI wa tenisi nyota ambaye anashika namba nne katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanawake, Serena Williams amefanikiwa kutinga katika mzunguko wa tatu wa michuano ya wazi ya Marekani baada ya kumfunga Maria Jose Martinez Sanchez kutoka Hispania. Serena ambaye ni bingwa wa michuano ya Wimbledon na Olimpiki alitumia muda wa saa moja na dakika 22 kumfunga Sanchez kwa 6-2 6-4 na kufanikiwa kusonga mbele. Wakati nyota huyo akifurahia ushindi wake mambo hayakuwa mazuri kwa dada yake Venus Williams baada ya kuondoshwa katika michuano hiyo na Angelique Kerber kutoka ujerumani kwa 6-2 5-7 6-4. Katika michezo mingine iliyochezwa jana Agnieszka Radwanska alifanikiwa kupambana baada ya kupoteza seti ya kwanza na kufanikiwa kumfunga Carla Suarez Navaro wa Hispania kwa 4-6 6-3 6-0 wakati Ana Ivanovic wa Serbia naye pia alisonga mbele baada ya kumfunga Sofia Arvidsson kwa 6-2 6-2.

Thursday, August 30, 2012

ZAMALEK YAJIPANGA KUWALINDIA MASHABIKI WAKE HESHIMA PAMOJA NA KUTOLEWA CHAMPIONS LEAGUE.

Jorvan Vieira, Zamalek Coach.
KLABU kongwe ya soka nchini Misri, Zamalek inatarajiwa kuwa na mashabiki wake wakati watapoikaribisha timu ya Chelsea Berekum ya Ghana katika mchezo wa kundi A wa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika utakachezwa Jumamosi. Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imekubali kuruhusu mashabiki kuhudhuria mchezo huo wa ligi ya mabingwa kwa mara ya kwanza baada ya miezi saba kupita. Mashindano yote ya soka ya ndani nchini humo yamesimamishwa kufuatia vurugu zilizotokea huko Port-Said Februari mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 74 na wengine mamia kujeruhiwa. Katika mchezo huo Zamalek hawatakuwa na nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo lakini wataingia uwanjani ili kuwapa imani mashabiki wao baada ya kuwa na msimu usioridhisha kwenye ligi hiyo.

ROONEY AAPA KUBAKIA UNITED.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Manchester United, Wayne Rooney ameapa kubakia katika klabu hiyo na kuhakikisha anapambana ili kujihakikishia mstakabali wake katika kikosi hicho. Kuna tetesi zilizokuwa zimesambaa mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa kuna hali ya kutoelewana kati ya meneja wa United, Sir Alex Ferguson na mchezaji huyo wakati wakipindi cha kujiandaa kwa ajili ya msimu mpya wa ligi. Tetesi hizo ziliongezeka nguvu baada ya Ferguson kumuacha mchezaji huyo katika kikosi chake kilichocheza dhidi ya Fulham Jumamosi iliyopita na kuzua maswali mengi juu ya mstakabali wa mchezaji huyo katika siku za mbele. Lakini jana usiku mchezaji huyo alituma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa anazisikia habari hizo kutoka kwa watu na kukanusha kwamba sio za kweli. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 26 atakuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili baada ya kuumia wakati wa mchezo dhidi ya Fulham ambao aliingia kama mchezaji wa akiba. Ujio wa Robin van Persie ambaye ameajiliwa kutoka Arsenal kwa ada ya paundi milioni 22 unamaanisha kuwa Ferguson ana washambuliaji wa kutosha wakiwemo Danny Welbeck na Javier Hernandez hata kama Rooney akiamua kuondoka.

KAGAWA AITWA JAPAN.

KIUNGO wa kimataifa wa Japan na klabu ya Manchester United, Shinji Kagawa ni mmoja kati wachezaji 12 wa timu ya taifa ya Japan walioitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo. Mbali na Kagawa pia kiungo wa CSKA Moscow Keisuke Honda amejumuishwa katika kikosi hicho ambapo kitachuana na Iraq Septemba 11 mwaka huu katika Uwanja wa Saitamanchini humo. Kabla ya mchezo huo dhidi ya Iraq, timu hiyo itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE Septemba 6 mwaka huu. Katika ratiba ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 upande wa bara la Asia Japan imepangwa kundi B pamoja na Iraq, Australia na Jordan huku wao wakiwa vinara wa kundi hilo kwa alama tano.

RATIBA YA MAKUNDI UEFA CHAMPIONS LEAGUE KUPANGWA LEO.

KLABU ya Manchester City huenda ikapangwa kundi moja na timu za Ujerumani, Hispania na Italia katika ratiba ya makundi ya michuano ya Klabu Bingwa ya Ulaya inayotarajiwa kufanyika baadae leo. Mabingwa wa Ligi Kuu nchini Uingereza, City ambao walitolewa katika hatua ya makundi msimu uliopita wamewekwa katika chungu cha pili katika upangaji wa ratiba hizo na kuna uwezekano wakakutana na timu za Borussia Dortmund, Real Madrid na Juventus. Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Chelsea, Arsenal na Manchester United wenyewe watakuwa katika chungu cha kwanza katika uapngaji wa ratiba ya michuano hiyo. Ratiba hiyo itajumuisha timu 32 ambazo zitagawanywa katika vyungu vinne ambavyo vitawagawanya katika makundi makundi nane yatakayokuwa na timu nne kila kundi. Michezo katika hatua makundi inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 18 na 19 na kumalizika Desemba 4 na 5.

US OPEN: AZARENKA, SHARAPOVA WASONGA MBELE, CLIJSTERS NJE.

Laura Robson.
NYOTA wa tenisi wanaoongoza kwa ubora katika orodha ya wachezaji wanawake wa mchezo huo, Victoria Azarenka na Maria Sharapova wamefanikiwa kutinga katika mzunguko wa tatu wa michuano ya wazi ya Marekani inayojulikana kama US Open. Azarenka ambaye katika orodha hizo anashika namba moja alifanikiwa kumfunga Kirsten Flipkens kutoka Ubelgiji kwa 6-2 6-2 wakati Sharapova ambaye anashika namba mbili yeye alitumia muda wa dakika 54 kumchapa Lourdes Dominguez Lino kwa 6-0 6-1. Bingwa mtetezi wa michuano hiyo Sam Stour pia alifanikiwa kusonga mbele baada ya kumfunga Edina Gallovits-Hall wa Romania kwa 6-3 6-0 wakati wachezaji wengine nyota kama Petra Kvitova na Li na nao walisonga mbele baada ya kushinda katika michezo yao. Laura Robson kutoka uingereza alifanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza mkubwa baada ya kumfunga mchezaji namba moja wa zamani Kim Clijsters katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo. Clijsters alitarajia kushinda taji hilo kabla ya kustaafu mchezo huo kama alivyotangaza awali lakini alishindwa kutamba mbele ya kinda Robson ambaye ana umri wa miaka 18 kwa kufungwa kwa 7-6 7-6 wakitumia dakika 126.

HD Real Madrid vs Barcelona 2-1 All Goals and Highlights Supercopa 2012

Wednesday, August 29, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF.

SERENGETI BOYS SASA KUIVAA MISRI
Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) sasa itaivaa Misri kwenye raundi ya pili ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 10 za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwakani nchini Morocco. Awali Serengeti Boys ilikuwa icheze raundi ya kwanza dhidi ya Kenya, mechi ya kwanza ikichezwa Septemba 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) jana lilituma taarifa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) likielezea kujitoa kwenye michuano hiyo. Serengeti Boys itaanzia nyumbani Oktoba 14 mwaka huu, wakati ya marudiano itachezwa nchini Misri kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu. Mshindi baada ya mechi hizo mbili ataingia raundi ya tatu ambayo ndiyo ya mwisho kabla ya kwenda Morocco. Katika raundi ya tatu ambayo mechi zake zitachezwa katikati ya Novemba na ya marudiano mwisho mwa mwezi huo, mshindi kati ya Tanzania/Misri atacheza na mshindi wa mechi ya Congo Brazzaville dhidi ya Msumbiji/Zimbabwe ambazo zinapambana katika raundi ya kwanza. Wachezaji wanaounda kikosi cha Serengeti Boys chini ya Kocha Jakob Michelsen ni makipa Abdallah Bakar (Mjini Magharibi), Hamad Juma (Azam) na Peter Manyika (JKT Ruvu). Mabeki ni Abdallah Salum (Mjini Magharibi), Basil Seif (Morogoro), Hassan Mganga (Morogoro), Ismail Gambo (Azam), Mgaya Abdul (Azam), Miraji Selemani (Polisi Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni), Mohamed Hussein (Azam), Pascal Matagi (Dodoma) na Paul James (Kinondoni). Viungo ni Farid Musa (Kilimanjaro), Hussein Twaha (Coastal Union), James Mganda (Kipingu Academy), Mbwana Ilyasa (Simba), Mohamed Haroub (Zanzibar), Mohamed Kapeta (Kinondoni), Mudathiri Yahya (Azam), Mzamiru Said (Morogoro) na Selemani Bofu (JKT Ruvu). Washambuliaji ni Abdallah Kisimba (Mwanza), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Joseph Lubasha (Azam), Kelvin Friday (Azam) na Salvatory Nkulula (Kipindu Academy).

MCHEZAJI AOMBEWA ITC UJERUMANI
Chama cha Mpira wa Miguu cha Ujerumani (DFB) kimetuma maombi ya kupatiwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Robert Makanja ili aweze kucheza mpira wa miguu nchini humo. DFB imetuma maombi hayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kumwezesha mchezaji huyo kuichezea timu ya TUS Ahausen, Hessischer FuBall-Verband ambayo hata hivyo haikuelezwa iko ligi ya daraja gani nchini humo. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mashindano wa DFB, Markus Stenger, Mtanzania huyo ameombewa hati hiyo kama mchezaji wa ridhaa kwa maelezo kuwa hakuwahi kusajiliwa na klabu yoyote nchini. TFF inafanyia kazi maombi hayo na hati hiyo itatolewa mara baada ya taratibu husika kukamilika ikiwemo kubaini kama kweli mchezaji huyo hakuwahi kusajili na klabu yoyote hapa nchini.

WALCOTT ACHOMOA MKATABA MPYA.

MSHAMBULIAJI wa pembeni wa klabu ya Arsenal, Theo Walcott amekataa kusaini mkataba mpya na klabu hiyo lakini mazungumzo bado yanaendelea baina yake na klabu. Nyota huyo mwenye miaka 23 ambaye mkataba wake unatarajiwa kuisha mwaka 2013 bado anataka kubakia klabuni hapo kama watamboreshea maslahi yake. Matajiri wa jiji la Manchester klabu ya Manchester City wanatambua kinachoendelea juu ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza na wanaweza kujaribu kumyakuwa kama Arsenal wakishindwa kumpa mchezaji huyo anachotaka. Kuna taarifa kwamba Arsenal ambao wamempa mkataba utakaomuwezesha kulipwa paundi 75,000 kwa wiki mchezaji huyo kama wakishindwa kufikia makubaliano watamuuza mchezaji kabla ya kufingwa kwa dirisha la usajili Agosti 31. Kama mchezaji huyo akiondoka atakuwa ni mchezaji watatu wakutegemewa wa klabu hiyo kuondoka baada ya Robin van Persie aliyekwenda Manchester United na Alex Song aliyekwenda Barcelona.

BLATTER APINGA KUWEPO SHERIA YA UMRI WA KUGOMBEA FIFA.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter anapinga vikali kuwepo kwa sheria ya umri wa kiongozi anayetakiwa kuongoza shirikisho hilo ingawa anajiandaa kukubali uwepo wa ukomo wa uongozi. Blatter ambaye ana umri wa miaka 76 pia alipinga suala la viwanja vya soka kuwa na sehemu ya kusimama ambapo suala hilo lilimyuingiza katika mgongano na Ligi Kuu nchini Ujerumani maarufu kama Bungasliga ambayo baadhi ya viwanja vyake vina sehemu ya kusimama. Akihojiwa Blatter aliliambia gazeti moja la michezo nchini Ujerumani kuwa anaunga mkono suala la uongozi wa shirikisho hilo kuwa na ukomo lakini anapinga suala la watu wenye umri mkubwa kutopewa nafasi ya kugombea uongozi FIFA. Blatter amesema kuwa hadhani kama umri wa mtu ukiwa mkubwa ndio unamzuia kugombea nafasi za uongozi kwani wapo viongozi wengi wenye umri mkubwa lakini akli zao zinafanya kazi kama vijana. Bosi huyo wa FIFA pia aliponda suala la viwanja kuwa na sehemu za watu kusimama badala ya wote kukaa chini kwani suala hilo linahatarisha usalama wa watazamaji haswa wanaokwenda uwanjani na familia zao.

VALCKE AZURU TENA BRAZIL.

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA, Jerome Valcke ametua nchini Brazil ikiwa ni safari yake nne katika ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi na miundo mbinu kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Valcke ambaye aliungana na nyota wa zamani wa soka wa nchi hiyo, Ronaldo de Lima na Bebeto ambao ndio wawakilishi wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo nchini humo walitembelea mji wa Manaus ambao uko Kaskazini mwa nchi hiyo ili kuangalia maendeleo ya ujenzi wa uwanja ambao utatumika 2014. Uwanja huo unaoitwa Arena Amazonia unajengwa kwa gharama ya kiasi cha dola milioni 260 na utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 44,000 ambao mpaka sasa ukiwa umekamilika kwa asilimia 42 pekee huku ukitarajiwa kukamilika kabisa June mwakani. Mapema leo Valcke alitarajiwa kutembelea uwanja mwingine uliopo katika mji wa Cuiaba ambao unajengwa kwa gharama ya dola milioni 254 na mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 46 pekee. Valcke akimaliza ziara katika miji hiyo anatarajiwa kukutana na maofisa kamati ya maandalizi na kufanya mkutano na waandishi wa habari ili kuzungumzia maendeleo ya maandalizi ya michuano hiyo.

LAMPARD ATAKA KUINOA CHELSEA.

KIUNGO nyota wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Chelsea, Frank Lampard amesema kuwa anataka kuwa kocha wa klabu hiyo ambao ndio mabingwa wa vilabu barani Ulaya wakati atakapomaliza kipindi chake cha kucheza soka. Lampard ambaye ana umri wa miaka 34 amekuwa akicheza katika Ligi Kuu nchini Uingereza toka mwaka 2001 na hivi sasa yuko katika msimu wake wa mwisho katika mkataba wake. Akihojiwa kuhusu suala la mkataba wake Lampard amesema anachofikiri sasa ni kutafuta leseni ya ukocha lakini ni klabu moja tu ambayo angependa kufundisha nayo ni Chelsea. Lampard amesema anajua kuwa kauli yake hiyo inaweza kupondwa na wadau wengine wa mchezo wa soka lakini yeye hataki kuanzia kufundisha katika vilabu vidogo kama wengine. Kiungo huyo alikuwa nahodha wakati wa mchezo wa fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich na kukiongoza vyema kikosi hicho kunyakuwa taji lake la kwanza la michuano hiyo pamoja lile la FA.

Tuesday, August 28, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

SERENGETI BOYS, KENYA KUCHEZA AZAM COMPLEX
Mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 10 za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwakani nchini Morocco kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Kenya itachezwa Septemba 9 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Tayari Serengeti Boys chini ya Kocha Jakob Michelsen na Msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ikiwa na wachezaji 28 iko kambini jijini Dar es Salaam tangu jana (Agosti 27 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni. Wachezaji waliko kambini ni makipa Abdallah Bakar (Mjini Magharibi), Hamad Juma (Azam) na Peter Manyika (JKT Ruvu). Mabeki ni Abdallah Salum (Mjini Magharibi), Basil Seif (Morogoro), Hassan Mganga (Morogoro), Ismail Gambo (Azam), Mgaya Abdul (Azam), Miraji Selemani (Polisi Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni), Mohamed Hussein (Azam), Pascal Matagi (Dodoma) na Paul James (Kinondoni). Viungo ni Farid Musa (Kilimanjaro), Hussein Twaha (Coastal Union), James Mganda (Kipingu Academy), Mbwana Ilyasa (Simba), Mohamed Haroub (Zanzibar), Mohamed Kapeta (Kinondoni), Mudathiri Yahya (Azam), Mzamiru Said (Morogoro) na Selemani Bofu (JKT Ruvu). Washambuliaji ni Abdallah Kisimba (Mwanza), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Joseph Lubasha (Azam), Kelvin Friday (Azam) na Salvatory Nkulula (Kipindu Academy). Mechi ya marudiano itachezwa jijini Nairobi, Kenya kati ya Septemba 21, 22 na 23 mwaka huu. Timu itakayofanikiwa kusonga mbele itacheza raundi ya pili dhidi ya Misri. Mechi ya kwanza itachezwa nyumbani kati ya Oktoba 12, 13 na 14 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa kati ya Oktoba 26, 27 na 28 mwaka huu. Misri ni kati ya timu 17 zilizoingia moja kwa moja raundi ya pili. Nyingine ni Afrika Kusini, Algeria, Burkina Faso, Cameroon, Congo Brazzaville, Cote d’Ivoire, Gabon, Gambia, Ghana, Guinea, Mali, Rwanda, Senegal, Sierra Leone, Tunisia na Zambia.

KAMATI YA SHERIA KUPITIA USAJILI SEPT 2
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia usajili wa wachezaji kwa msimu wa 2012/2013. Usajili utakaopitiwa ni wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Lidi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo Kamati itapitia pingamizi zilizowasilishwa na klabu mbalimbali dhidi ya wachezaji waliosajiliwa na klabu zingine.

MADRID TUMBO JOTO MCHEZO WA KESHO DHIDI YA BARCELONA.

KLABU ya Real Madrid inatarajiwa kuikaribisha Barcelona katika mchezo wa pili wa Super Cup wakitambua kwamba wanahitaji ushindi ili kushinda taji lao la kwanza msimu huu. Kama klabu hiyo ikishindwa kuibuka kidedea katika mchezo huo itakuwa ni pigo kubwa katika kampeni yao ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo yao mitatu iliyotangulia. Mbali na kufungwa katika mchezo wao wa kwanza wa Super Cup na Barcelona kwa mabao 3-2 katika Uwanja wa Nou Camp, Madrid pia walipoteza mchezo wa La Liga dhidi ya Getafe kwa kufungwa mabao 2-1 na kuwapa nafasi mahasimu wao hao kuwaacha kwa alama tano wakiwa wameshinda michezo yao yote miwili. Meneja wa Madrid Jose Mourinho aliponda kikosi chake kwa mchezo waliocheza wakati akikataa kulaumu waamuzi wa mchezo huo kama alivyofanya katika mchezo dhidi ya Barcelona ambapo alidai bao la kwanza la timu hiyo lilikuwa la kuotea. Barcelona nao ambao msimu huu wameonekana kuanza vyema tofauti na msimu uliopita nao watakuwa wakisaka taji lao la kwanza msimu huu huku wakimkosa beki wao mahiri Carles Puyol ambaye aliumia katika mchezo wa Jumapili.

FA KUITOSA UMBRO NA KUINGIA MKATABA MPYA NA NIKE.

KAMPUNI kongwe ya vifaa vya michezo ya Marekani, Nike iko mbioni kusaini mkataba wa kuisambazia vifaa vya michezo timu ya taifa ya Uingereza. Nike inatarajia kuanza kuisambazia timu hiyo jezi mpya za kuchezea ugenini mapema mwaka ujao pamoja na ukweli kwamba mkataba wa timu hiyo na kampuni ya Umbro unatarajiwa kuisha mwaka 2018. Mkataba huo ambao utakiwezesha Chama cha Soka cha Uingereza-FA kuvuna mamilioni ya paundi, utaonekana kama mashindano kati ya kampuni hizo baada ya mahasimu wao wakubwa kampuni ya Adidas ya Ujerumani kutamba katika michuano ya olimpiki kwa kusambaza vifaa kwa timu ya kombaini ya Uingereza iliyoshiriki michuano hiyo. Wiki iliyopita maofisa wa FA walikuwa tayari kutangaza kuwa mkataba wao na Umbro kampuni ambayo ina maskani katika jiji la Manchester unaweza kuvunjika lakini maofisa hao waliacha kufanya hivyo mpaka watapokamilisha suala la mkataba mpya na Nike.

FERGUSON AWAZUIA MAKINDA WAKE KUENDESHA MAGARI YA KIFAHARI.


MENEJA wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson amewazuia wachezaji wake nyota wenye umri mdogo kuendesha magari ya kifahari ya kimichezo ya Chevrolet ambao ndio watakuwa wadhamini wao wapya. United imetiliana saini ya mamilioni paundi na kampuni kongwe ya magari ya nchini Marekani ambao jina lao litaonekana katika jezi za klabu hiyo mwanzoni mwa msimu wa mwaka 2014-2015. Kutokana na mkataba huo, kampuni hiyo ilitoa ofa kwa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha United kuchagua gari lolote la kifahari ambalo linatengenezwa na kampuni hiyo.  
Aina ya magari ya Chevrolet.
Hatahivyo kuna tetesi kuwa Ferguson aliingilia suala hilo kati na kudai kuwa wachezaji wote wenye umri wa miaka chini 23 hata kama atakuwepo katika kikosi cha kwanza hataruhusiwa kutoa oda ya kueletewa gari la kampuni hiyo. Hiyo itamaanisha kuwa mshambuliaji Danny Welbeck mwenye umri wa miaka 21, mabeki Phil Jones mwenye umri wa miaka 20, Chris Smalling miaka 22 na Rafael miaka 22 pia hawataruhusiwa kuendesha gari aina yoyote mpaka waruhusiwe na Ferguson. Hatua ya Ferguson imekuja ili kuwadhibiti wachezaji hao makinda wasijione kama tayari wamekuwa mastaa na kushindwa kucheza soka kwa kiwango cha juu.

MOJA YA AJALI MBALI KUWAHI KUTOKEA KATIKA MCHEZO WA KUTUPA MIKUKI HUKO ROME.

OFISA ACHOMWA NA MKUKI KOONI KATIKA MASHINDANO HUKO UJERUMANI.

OFISA mmoja katika michuano ya riadha iliyokuwa ikifanyika jijini Dusseldorf nchini Ujerumani amefariki dunia baada ya kuchomwa na mkuki katika koo wakati michuano hiyo ikiendelea. Ofisa huyo aliyejulikana kwa jina la Dieter Strack mwenye umri wa miaka 74 alikimbizwa hospitali mara baada ya tukio hilo lakini alifariki baadae kutokana na majeraha hayo. Taarifa kutoka vyombo vya habari vya nchi hiyo zinasema kwamba Strack alikumbwa na tukio hilo wakati akikimbia kwenda kupima umbali utakapotua mkuki uliotupwa lakini kabla ya mkuki huo kufika chini ulitua katika koo lake na kumjeruhi vibaya. Msemaji wa polisi katika mji huo Andre Hartwig amesema kijana aliyerusha mkuki huo ulioleta maafa ambaye ana umri wa miaka 15 alipelekwa kliniki ambako anapewa ushauri nafasa kutokana na tukio hilo. Matukio kama hayo katika michuano ya riadha hususani mchezo wa kurusha mkuki na kutupa tufe yamekuwa yakitokea lakini ni mara chache kusababisha kifo. Mwaka 2007 mwanariadha wa mbio za kuruka chini wa Ufaransa Salim Sdiri alichomwa na mkuki katika mashindano ya mchezo huo yaliyofanyika jijini Rome, Italia na kupelekwa hospitalini ambapo baadae alipona majeraha aliyopata.

CLIJSTERS AANZA VYEMA US OPEN.

MCHEZA tenisi nyota Kim Clijsters ameanza vyema michuano yake ya mwisho mikubwa kabla ya kustaafu baada ya kumfunga Victoria Duval kutoka Marekani katika mzunguko wa kwanza wa michuano ya wazi ya Marekani. Clijsters ambaye ni bingwa wa michuano hiyo mwaka 2005, 2009 na 2010 alifanikiwa kushinda mchezo wake huo wa kwanza kwa 6-3 6-1 dhidi ya Duval ambaye anachipukia katika mchezo huo akiwa umri wa miaka 16. Mwanamama huyo ambaye ni raia wa Ubelgiji sasa atakutana na Laura Robson raia wa Uingereza katika mzunguko wa pili wa michuano inayoendelea jijini New York Marekani. Mbali na Clijsters michezo mingine iliyochezwa jana bingwa mtetezi wa michuano hiyo Sam Stosur raia wa Australia amefanikiwa kusonga mbele baada ya kumfunga Petra Martic wa Urusi kwa 6-1 6-1. Maria Sharapova kutoka urusi ambaye ni bingwa wa michuano hiyo mwaka 2006 naye alifanikiwa kuzonga mbele baada ya kumfunga Melinda Czink kutoka Hungary kwa 6-2 6-2 wakati bingwa wa michuano ya wazi ya Australia Victoria Azarenka pia alishinda mchezo wake kwa 6-0 6-1 dhidi ya Alexandra Panova.

Monday, August 27, 2012

BRAZIL KUCHEZA NA URENO.

TIMU ya taifa ya Brazil inatarajiwa kucheza michezo miwili ya nyumbani na ugenini ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Ureno mapema mwaka 2013 ikiwa kama sehemu ya maandalizi ya Kombe la Dunia mwaka 2014 ambayo nchi hiyo itakuwa mwenyeji. Mchezo wa kwanza wa kirafiki baina ya timu hizo unatarajiwa kuchezwa jijini Sao Paulo huku wa pili ukichezwa nchini Ureno katika tarehe ambazo zitatangazwa hapo baadae. Mbali na michezo hiyo miwili maofisa wa soka wan chi hiyo wamesema kuwa timu hiyo pia imejipanga kucheza mchezo mwingine wa kimataifa wa kirafiki na timu ya taifa ya Uingereza. Kabla ya michezo hiyo Brazil inatarajiwa kucheza na timu ya taifa ya Afrika Kusini-Bafana Bafana Septemba 7 mwaka huu mchezo ambao utafanyika jijini Sao Paulo kabla ya kucheza na China jijini Racife siku tatu baadae.

PUYOL AUMIA TENA.

NAHODHA wa klabu ya Barcelona, Curles Puyol amevunjika mfupa wa mguu wake wa kulia wakati wa mchezo baina ya timu yake na Osasuna ambao walishinda mabao 2-1. Katika taarifa yake klabu hiyo imesema kuwa mchezaji huyo inabidi afanyiwe vipimo zaidi vya xray ili kujua ukubwa wa tatizo hilo na muda gani atakuwa nje ya uwanja. Puyol mwenye umri wa miaka 34 anatarajiwa kukosa mchezo muhimu wa Super Cup baina ya timu yake na mahasimu wao Real Madrid utakaofanyika katika Uwanja wa Santiago Bernabeu Alhamisi ya wiki hii, ukiwa ni mchezo wa pili baada ya ule wa kwanza Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao 3-2. Mchezaji huyo aliumia katika dakika za majeruhi katika Uwanja wa Reyno de Navarra baada ya kugongana na mchezaji wa Osasuna Roland Lamah wakati akiwa katika harakati za kumzuia. Katika kipindi cha misumu ya hivi karibuni Puyol amekuwa akindamwa na majeruhi ya mara kwa mara ukiwemo upasuaji mguu wake wa kulia aliofanyiwa na kusababisha kushindwa kuichezea Hispania katika michuano ya Ulaya.

MADRID YANYAKUWA RASMI MODRIC.

KLABU ya Tottenham Hotspurs ya Uingereza imefikia makubaliano na klabu ya Real Madrid juu ya uhamisho wa mchezaji wake Luka Modric kwa ada ya paundi milioni 30. Kiungo huyo wa kimataifa kutoka Croatia mwenye miaka 26 anatarajiwa kusafiri kuelekea Hispania kwa ajili kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kusainishwa mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo. Tottenham pia katika taarifa yake iliyotuma katika mtandao wake wamesema kuwa mbali na kukubali kumuuza mchezaji huyo pia klabu hiyo imetangaza kuingia ubia na Madrid ambapo katika makubaliano ya ubio huo klabu hizo zitakuwa zikibadilishana mafunzo pamoja na uhusiano wa kibiashara. Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy amesema kuwa Modric amekuwa mchezaji wao kutegemewa na walikuwa hawahitaji kumuachia lakini wamefarijika kwamba amekwenda Madrid klabu ambayo katika siku mbeleni watakuwa na mahusiano nao mazuri kwa ajili ya maendeleo. Modric alijiunga na Tottenham mwaka 2008 kwa ada ya paundi milioni 16.5 akitokea klabu ya Dinamo Zagreb ya nchini kwake ambapo mpaka anaondoka amefunga mabao 17 katika michezo 150 aliyocheza katika timu hiyo.

CLIJSTERS ATARAJI KUSTAAFU TENISI NA TAJI LA US OPEN.

MCHEZAJI tenisi nyota ambaye ni bingwa mara tatu wa michuano ya wazi ya Marekani au US Open, Kim Clijsters anatarajia kustaafu mchezo huo kwa kushinda michuano hiyo ambayo imeanza leo jijini New York. Clijsters ambaye ana umri wa miaka 29 alitangaza nia yake ya kustaafu mchezo huo mara baada ya michuano ya US Open na amekuwa katika ziara ya kuaga katika kipindi chote cha msimu huu. Majeraha yaliyikuwa yakimkabili yalimzuia mchezaji kushiriki michuano mingi msimu huu lakini amesema kuwa hivi anajiamini na yuko vyema kwa ajili ya kutetea taji la michuano hiyo ambalo alilichukua mwaka jana. Clijsters alishindwa kutamba katika michuano ya michuano ya olimpiki iliyofanyika jijini London baada ya kukubali kipigo kutoka kwa Maria Sharapova katika mchezo wa robo fainali ya michuano hiyo. Mara ya kwanza Clijsters alitangaza kustaafu mchezo huo mwaka 2007 baada ya kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu lakini alibadilisha mawazo miaka miwili baadae na kurejea uwanjani na kushinda michuano ya US Open kabla ya kufanya hivyo tena mwaka 2010 na 2011.

MOURINHO AWAPONDA WACHEZAJI WAKE KUCHEZA HOVYO.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid Jose Mourinho amewalaumu wachezaji wake kwa kushindwa kucheza vizuri na kupelekea timu hiyo kuchapwa mabao 2-1 dhidi ya majirani zao Getafe katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga. Kipigo hicho kilimaliza ubabe wa Madrid ambao ni mabingwa watetezi kutofungwa katika michezo 24 ya ligi iliyopita huku pia ukiwa ni mchezo wa kwanza kupoteza katika kipindi cha miaka mitano katika La Liga baada ya kuongoza katika kipindi cha kwanza. Akihojiwa Mourinho amesema kuwa wachezaji wake hawakucheza mchezo mzuri kabisa na kwamba walistahili kufungwa katika mchezo lakini alikataa kumlaumu mchezaji mmoja mmoja na kusema kuwa wana kazi kubwa ya kufanya ili kurejea katika kiwango chao. Madrid ambao katika mchezo wa kwanza wa La Liga dhidi ya Valencia walitoka sare ya bao 1-1, kipigo hicho kinawaacha nyuma ya alama tano mbele mahasimu wao Barcelona ambao wameshinda katika michezo yao yote miwili. Mara ya mwisho Madrid kupoteza michezo yake miwili ya kwanza ilikuwa msimu wa mwaka 2001-2002 ambapo walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga na kupoteza mchezo wa fainali wa Kombe la Mfalme kwa Deportivo Coruna lakini walifanikiwa kushinda Kombe la Ligi ya mabingwa Ulaya wakiifunga Bayer Liverkusen katika mchezo wa fainali.

Osasuna VS Barcelona 1-2 All Goals & Match highlights 26/8/2012

Getafe vs. Real Madrid (2-1) All Goals & Full Highlights - 26/08/2012 - ...

Sunday, August 26, 2012

ABBAS AMKINGIA KIFUA KOCHA MPYA ZAMALEK.

MWENYEKITI wa klabu ya Zamalek ya Misri, Mamdouh Abbas amesema kuwa hawana mpango wa kumtimua kocha wa klabu hiyo Jovran Vieira pamoja na matokeo mabovu waliyopata katika kipindi cha karibuni na kupelekea kuengiliwa katika Ligi ya mabingwa Afrika. Akihojiwa Abbas pia alikataa tetesi kuwa ameanza mazungumzo na mapacha Hossam na Ibrahim Hassan ili kuziba pengo na Vieira ambaye ni raia wa Brazil. Abbas amesema kuwa umepita mwezi mmoja toka wamwajiri Vieira hivyo hawana sababu ya kumfukuza kwasababu wanaamini uwezo wake na ataipeleka klabu hiyo mbali. Hossam na Ibrahim waliwahi kuinoa Zamalek katika msimu wa mwaka 2010-2011 kabla ya bodi ya klabu hiyo kuwatimua na kumwajiri Hassan Shehata ambaye aliondoka mwezi uliopita.

LIVERPOOL YAMNASA SAHIN KWA MKOPO.

KLABU ya Liverpool ya nchini Uingereza imefanikiwa kumsajili kwa mkopo kiungo Nuri Sahin kutoka klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania. Kiungo huyo wa kimataifa wa Uturuki ambaye ana umri wa miaka 23 anakuwa mchezaji wan ne kusajiliwa katika kikosi hicho ambacho kinanolewa na Brendan Rodgers ambaye pia amewasajili Joe Allen, Fabio Borin na Oussama Assaidi. Sahin ambaye pia alikuwa akiwindwa na klabu ya Arsenal amesema kuwa kiungo wa zamani wa klabu hiyo ambaye sasa anacheza Madrid Xabi Alonso ndiye aliyemshauri aende kujiunga na klabu hiyo. Akihojiwa mara baada ya kutua Anfield, Sahin amesema amekwenda katika klabu hiyo ili kuisaidia kushinda vikombe na kurejesha makali yake kama ilivyokuwa zamani. Mbali na ushauri aliopewa na Alonso lakini pia mchezaji huyo alishauriwa na kocha wa Madrid Jose Mourinho kuwa Ligi Kuu nchini Uingereza itakuwa nzuri kwake kukuza kiwango chake.

GALATASARAY YAJITOA MBIO ZA KUMWANIA KAKA.

RAIS wa klabu ya Galatasaray ya nchini Uturuki, Unal Aysal ameondoa uwezekano wa kumsajili kiungo wa klabu ya Real Madrid Kaka. Aysal mwenye umri wa miaka 71 mapema alidai kuwa klabu yake hiyo ambao ndio mabingwa wa Ligi Kuu nchini Uturuki inaweza kumsajili nyota huyo ambaye pia amewahi kukipiga katika klabu ya AC Milan ya Italia. Kaka ambaye ni raia wa Brazil amekuwa akihusishwa na suala la kuondoka katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi na kocha wa Madrid Jose Mourinho hakumjumuisha mchezaji huyo katika mchezo dhidi ya Barcelona uliochezwa katikati ya wiki iliyopita na Getafe ambao utachezwa baadae leo. Rais huyo amesema kuwa alizungumza na kocha wa klabu hiyo Fatih Terim na kumfahamisha kuwa kama anahitaji kuongeza katika kikosi hicho basi inabidi aongeze beki na sio Kaka ambaye anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji. Galatasaray inakabiliwa na mchezo mgumu wa mahasimu wao wa jijini Istabul timu ya Besiktas ambao unatarajiwa kupigwa baadae leo.

BOLT NDANI YA OLD TRAFORD.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt alikuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza kati Manchester United na Fulham uliochezwa katika Uwanja wa old Traford. 
Bolt ambaye ana medali sita za dhahabu za olimpiki ni mshabiki wa United kwa kipindi kirefu na katika siku za karibuni alikaririwa akisema kuwa anataka kuwa mchezaji wa klabu hiyo. Nyota huyo wa mbio fupi alitambulishwa mbele ya mashabiki waliohudhuria mchezo huo ambao walikuwa wakipiga kelele ya kumtaka Ferguson amsajili mwanaridha huyo ili kuimarisha safu yake ya ushambuliaji. 
Mshambuliaji mpya wa klabu hiyo Robin van Persie na mkongwe Ryan Giggs walipata nafasi ya kupiga picha ya pamoja na Bolt kabla ya kuanza kwa mchezo huo ambao United ilishinda kwa mabao 3-2.

ROONEY NJE YA UWANJA WIKI NNE.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Manchester United, Wayne Rooney anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja kufuatia majeraha aliyopata wakati timu yake ikiigaragaza Fulham kwa mabao 3-2 katika Uwanja wa Old Traford jana. Rooney alitolewa katika dakika za mwisho za mchezo huo huku mguu wake ukiwa umejaa damu baada ya kujiparua katika kiatu cha mshambuliaji wa Fulham Hugo Rodallega wakati akijaribu kumzuia mchezaji huyo asipige mpira langoni mwao. Picha za luninga zilionyesha jinsi mchezaji huyo alivyojiparua katika mguu wake wa kulia na meneja wa United Sir Alex Ferguson alithibitisha kuwa mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi hicho cha wiki nne. Kama Rooney hatapona haraka, anatarajiwa kukosa michezo mitatu ambayo timu yake itacheza na timu za Southampton, Wigan na Liverpool huku pia akikosa mchezo wa ufunguzi katika hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mbali na michezo hiyo pia kocha wa timu ya taifa ya Uingereza inabidi atafute mbadala wa mchezaji huyo katika michezo miwili ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Moldova na Ukraine mapema mwezi ujao.

Friday, August 24, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MICHUANO YA KOMBE LA TAIFA 2012
Michuano ya Kombe la Taifa (Taifa Cup) inayoshirikisha kombaini za mikoa ya Tanzania Bara haitakuwepo mwaka huu kutokana na kukosekana kwa udhamini. Licha ya kukosekana kwa udhamini, awali tulifikiria kuendesha mashindano hayo kwa michango ya wanachama wetu (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa) na Serikali za mikoa kugharamia timu zao. Lakini baadhi ya wanachama wetu na Serikali za mikoa walitushauri kuwa ni ngumu kuendesha mashindano hayo kwa sasa kutokana na shughuli za kitaifa zinazoendelea hivi sasa ikiwemo maandalizi ya sensa ya watu na makazi. Kwa mujibu wa Kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mashindano ya Kombe la Taifa yalitakiwa kufanyika kuanzia Julai 23 hadi Agosti 6 mwaka huu. Michuano ya Kombe la Taifa msimu uliopita ilidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambapo Mbeya iliibuka mabingwa katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.

WACHEZAJI 11 KUTOKA NJE WAPATA ITC
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji 11 wa nje kati ya 14 walioombea usajili na klabu mbalimbali za Ligi Kuu. Wachezaji walioombewa usajili Yanga na tayari ITC zao zimepatikana ni Nizar Khalfan kutoka Vancouver Whitecaps ya Canada, Didier Kavumbagu (Atletico Olympic- Burundi) na Mbuyu Twite kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Kwa upande wa Simba ni Musa Mude (Sofapaka, Kenya) na Daniel Akuffor (Stella Abidjan, Ivory Coast) wakati Mtibwa Sugar ni Shabani Kisiga timu ya El Itihad ya Oman. Waliopata ITC kwa upande wa Kagera Sugar ni Wilfred Ojodale Ame na Benjamin Efe Ofuyah wote kutoka FC Abuja ya Nigeria. Wengine ni Deangelis Silva kutoka New Road ya Nepal kwenda Coastal Union, George Odhiambo kutoka Randers FC ya Denmark kwenda Mtibwa Sugar na Jerry Santo kutoka Tusker, Kenya kwenda Coastal Union. Wachezaji ambao wameombewa usajili na ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng wa AFC Leopards, Kenya kwenda Simba na Ayoub Hassan Isiko kutoka Bull FC, Uganda kwenda Mtibwa Sugar. Bado klabu ambazo hazijakamilisha usajili na kupata ITC zina fursa ya kufanya hivyo hadi Septemba 4 mwaka huu ambapo dirisha litafungwa. Pia TFF imetoa ITC kwa wachezaji wanane walioombewa kwenda kucheza mpira wa miguu katika nchi za Kenya na Msumbiji kutoka katika klabu mbalimbali za hapa nchini. Wachezaji hao na klabu wanazokwenda katika mabano ni Abdallah Ally Abdallah (CD Madchegde, Msumbiji), Almasi Khatib Mkinda (Ferroviario da Beira, Msumbiji), David Naftali (Bandari, Kenya) na Hassan Hassan Mustafa (CD Madchegde, Msumbiji). Wengine ni Meshack Abel (Bandari, Mombasa), Mohamed Banka (Bandari, Kenya), Thobias Davis Silas (CD Madchegde, Msumbiji) na Thomas Maurice (Bandari, Kenya).

VIPIMO VYA TIBA KWA WACHEZAJI
Klabu zote zilizowasilisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) maombi ya usajili kwa wachezaji wao zinatakiwa pia kuwasilisha nakala za hati zao za vipimo vya afya (medical certificate) kwa mujibu wa kanuni za usajili.

Yohan Blake 9.69 100M Men Lausanne Diamond League HQ.

Usain Bolt 19.58 200M Lausanne - Diamond League 2012 HD

UWANJA WA BOMBONERA WAFUNGIWA KWA VURUGU.

MAOFISA wa usalama wa Serikali nchini Argentina wameufungia uwanja wa Boca Juniors ikiwa kama adhabu kwa vurugu zilizofanywa na mashabiki wa klabu hiyo baada ya kumalizika kwa mchezo wa Klabu Bingwa ya Amerika Kusini maarufu kama Copa Sudamericana dhidi ya Independiente. Ofisa Mkuu wa Usalama nchini humo Dario Ruiz amesema kuwa uwanja huo unatumiwa na Boca ambao unaitwa Bombonera utafungiwa kuchezewa mchezo wa Ligi Kuu nchini humo. Vurugu zilitokea baada ya Independiente kusawazisha bao kwa penati ya dakika za mwisho na kupelekea timu hizo kutoka sare ya mabao 3-3 ambapo mashabiki waliokuwa wamekaa karibu na benchi la Independiente walivunja uzio uliokuwepo na kuingia uwanjani. Msemaji wa Boca amesema katika taarifa yao waliyotuma katika mtandao kuwa wameshawagundua mashabiki wanne waliohusika na vurugu hizo na wanatarajia kuwafungia kuingia katika uwanja huo. Vurugu zimekuwa tishio katika mechi nyingi za soka nchini Argentina kutokana na vikundi vya wahuni kutawala katika maeneo ya karibu na viwanja nchini humo.

MTANANGE WA AL AHLY NA ZAMALEK KUPIGWA SEPTEMBA 16.

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika-CAF limepanga mchezo wa mzunguko wa mwisho wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika kati ya timu ya Al Ahly na Zamalek ambao ni mahasimu kuchezwa Septemba 16 mwaka huu. Mkurugenzi wa Al Ahly Sayed Abd Al Hafez alithibisha kuwa wamepokea taarifa hizo kutoka CAF ambapo pia mchezo kati TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC na Chelsea Berekum ya Ghana nao utapigwa tarehe kama hiyo na muda mmoja. Mchezo wa klabu hizo kongwe na mahasimu nchini unatarajiwa kupigwa katika Uwanja wa Kijeshi na bila ya uwepo wa mashabiki. Al Hafez amesema kuwa ameamua kusafiri mapema kuelekea nchii DRC kutafuta hoteli nzuri na sehemu ya kufanyia mazoezi kwa ajili ya timu yake wakati itakaposafiri kwenda kucheza na Mazembe ili kuepuka adha waliyopata wakati walikwenda Ghana kucheza na Chelsea. Al Ahly ndio wanaoongoza kundi B wakiwa na alama 10 baada ya kushinda michezo mitatu na kutoa sare mmoja na sasa watakwenda Lubumbashi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mazembe utakaochezwa Septemba 2 mwaka huu.

BOLT, BLAKE WANG'ARA DIAMOND LEAGUE.

MKIMBIAJI nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Yohane Blake amefanikiwa kuweka rekodi katika mbio za mita 100 na kuwa mtu wa tatu mwenye kasi zaidi huku mjamaica mwenzake Usain Bolt naye akishinda kirahisi mbio za mita 200 katika michuano ya Diamond League iliyofanyika jijini Lausanne. Blake ambaye alishinda medali ya fedha katika mbio za mita 100 na 200 katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika jijini London, katika mbio hizo alitumia muda wa sekunde 9.69 Ni Bolt pekee ambaye alinyakuwa medali ya dhahabu katika mbi za mita 100, 200 na 400 kupokezana vijiti, ndio mwenye rekodi ya kukimbia kwa kasi zaidi katika mbio fupi. Akihojiwa mara baada ya mbio hizo Blake amesema kuwa amefurahishwa na muda aliotumia na ana mategemeo ya kufanya vizuri zaidi katika siku zijazo kama ataepuka majeruhi.

FC Barcelona Vs Real Madrid 3-2 All Goals And Highlights (Spanish Superc...

Thursday, August 23, 2012

WIZARA MISRI KUANZA KUWARUHUSU MASHABIKI.

WIZARA ya Mambo ya Ndani nchini Misri inatarajiwa kuwaruhusu baadhi ya mashabiki wa soka nchini humo kuhudhuria baadhi ya mechi ikiwa kama sehemu ya majiribio kwa wizara hiyo. Wizara hiyo inatarajiwa kuwaruhusu mashabiki kuhudhuria baadhi ya michezo ikiwemo mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Zamalek na Chelsea Berekum . Taarifa kutoka katika wizara hiyo inaendelea kusema kuwa michezo ambayo inawakutanisha timu mahasimu bado mashabiki wataendelea kuzuiwa ikiwemo mchezo wa mzunguko wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Al Ahly na Zamalek. Mechi zote zilizochezwa nchini Misri katika kipindi cha miezi sita iliyopita zilichezwa bila ya mashabiki baada ya wizara kuzuia kutokana na vurugu zilizotokea jijini Port Said. Zamalek itamenyana na Chelsea ya Ghana mwezi ujao katika michuano hiyo wakati Al Ahly itasafiri kwenda Lubumbashi ambapo watakutana na TP Mazembe katika mchezo ambao unatarajiwa kuwa mkali.

CRUYFF AMPONDA MOURINHO KUJIITA "THE ONLY ONE".

NYOTA wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya Barcelona Johan Cruyff amemtaja meneja wa Real Madrid Jose Mourinho kama mtu ambaye alifeli akiwa kama mchezaji. Cruyff alitoa kauli hiyo kwa kucheka baada ya Mourinho ambaye ni raia wa Ureno kujipachika jina la “the only one” akimaanisha kwamba ni yeye pekee. Akihojiwa kuhusiana na kauli hiyo ya Mourinho Cruyff amesema kuwa si kweli Mourinho kafanya mambo makubwa mpaka ajiite hivyo kwasababu hakuwa na chochote cha kujisifu wakati akiwa mchezaji. Mbali na kumshabulia Mourinho, nyota huyo wa zamani pia alimponda rais wa Barcelona Sandro Rosell kuhusu sera za uhamisho wa klabu yake hiyo ya zamani kuwa zinahitaji marekebisho. Cruyff amesema kuwa sera nzuri ni kutengeneza wachezaji na sio kununua kama anavyofanya Rosell ambapo hivi karibuni alimnunua Alex Song kutoka Arsenal ili aje kuongeza nguvu katika klabu hiyo. Cruyff pia amesema kocha wa sasa wa klabu hiyo Tito Vilanova ana kazi kubwa ya kufanya ili kufikia mafanikio aliyopata Pep Guardiola wakati akiinoa klabu hiyo.

SCHMEICHEL KUHUDHURIA FAINALI YA AIRTEL RISING STARS NAIROBI.

GOLIKIPA nyota wa zamani wa kimataifa wa Denmark na klabu ya Manchester United, Peter Schmeichel anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika fainali ya michuano ya Airtel Rising Stars itakayofanyika Jumamosi jijini Nairobi, Kenya. Katika shughuli hiyo Schmeichel atapata nafasi ya kutaja majina katika orodha ya wachezaji ambao wamechaguliwa kwenda kuweka kambi katika klabu za Arsenal na Manchester United nchini Uingereza. Makamu wa rais wa Airtel Afrika Achieng Butler alidokeza sababu kubwa ya kumleta nyota huyo nchini humo ni kuwapa vijana motisha na uchu wa kufikia mafanikio katika maisha yao ya soka. Michuano hiyo ya Airtel Afrika ilifunguliwa rasmi Jumatatu na Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga katika Uwanja wa Jiji uliopo Nairobi na fainali inatarajiwa kuchezwa katika uwanja huohuo.

CHELSEA YAKATAA PAUNDI MILIONI 30 ZA MAN CITY KWA AJILI YA LUIZ.

KLABU ya soka ya Chelsea imekataa kitita cha paundi milioni 30 kutoka kwa klabu ya Manchester City ili wawauzie beki wao David Luiz. Meneja wa City Roberto Mancini alikuwa akihaha kutafuta beki wa kuziba pengo la Micah Richards ambaye ni majeruhi na atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki 10. Luiz hakuwemo katika kikosi cha Chelsea ambacho kilishinda mabao 4-2 dhidi ya Reading wakati pande zote zikifanya mazungumza kuhusu mchezaji huyo ingawa hata hivyo beki huyo wa kimataifa wa Brazil alidai katika mtandao wa kijamii wa twitter kwamba alikuwa na majeraha ya goti. Ujumbe huo aliotuma twitter ulionyesha kumkera meneja wa Chelsea Roberto Di Matteo na kudai kuwa ataangalia uwezekano wa kuzuia masuala mengine kwa wachezaji wake wasiyaweke wazi katika mitandao hiyo. Luiz mwenye umri wa miaka 25 aliwasili Stamford Bridge kwa ada ya paundi milioni 21 kutoka klabu ya Benfica ya Ureno na toka kipindi hicho amekuwa kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo kutokana na umahiri wake wa kukaba na kushambulia alionao.

BOLT, BLAKE KUKUTANA DIAMOND LEAGUE, USWIS.

BAADA ya kumalizika kwa michuano ya Olimpiki iliyofanyika jijini London, wanariadha walioshiriki michuano hiyo duniani kote wanakutana tena baadae usiku michuano ya Diamond League itakayofanyika nchini Switzerland.
Mkimbiaji nyota wa mbio fupi Usain Bolt anatarajiwa kukimbia mbio za mita 200 zitakazofanyika jijini Lausanne, lakini ni kama anakuwa anamkwepa Mjamaica mwenzake Yohan Blake ambaye atakimbia mbio za mita 100. Katika michuano ya olimpiki nyota hao walishiriki mbio zote mbili za mita 100 na 200 kwa pamoja ambapo Bolt alishinda zote kabla ya kuunganisha nguvu kwa pamoja na kukimbia mbio za kupokezana vijiti za mita 400 na kuvunja rekodi ya dunia. Akihojiwa Blake amesema kuwa anapenda kukimbia kushindana na Bolt lakini inabidi uamuzi huo amuachie meneja wake kwakuwa yeye ndiye anafahamu anachokifanya. Wawili hao pia hawatakutana katika katika michuano ya Diamond League itakayofanyika jijini Zurich na Brussels kabla ya kumaliza msimu wao.

Wednesday, August 22, 2012

SENEGAL YATAKA MCHEZO BAINA YAO NA IVORY COAST UCHEZWE NEUTRAL GROUND KUTOKANA NA MACHAFUKO JIJINI ABIDJAN.

KUFUATIA matukio ya kivita yanaoendelea nchini Ivory Coast, Shirikisho la Soka la Senegal-FSF limesema kuwa linaweza kuomba kubadilishiwa eneo la mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2013 ambao ulikuwa uchezwe jijini Abidjan Septemba 8 mwaka huu. Rais wa FSF, Augustin Senghor amesema kuwa kutokana na hali ilivyo nchini Ivory Coast atalazimika kuomba Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kuhamishia mchezo huo katika nchi yoyote jirani kwa ajili ya usalama wa wachezaji wake. Senghor aliendelea kusema kuwa hata CAF wenyewe hawataweza kukubali mchezo huo kuchezwa jijini Abidjan ambapo kuna matukio ya kurushiana risasi yanayoweza kuathiri wachezaji wakati wa mchezo baina ya timu hizo. Watu wasiojulikana waliokuwa na silaha walianzisha mapigano jijini humo wiki mbili zilizopita dhidi ya kambi za kijeshi, vituo vya polisi na kwenye vizuizi katika mji huo na kusababisha vifi vya watu wapatao 15 na pia kufunja magereza na kuwaachia wafungwa waliokuwemo ndani. Hatahivyo Wizara ya Ulinzi nchini Ivory Coast imewahakikishia wananchi kuwa wamefanikio kudhibiti tukio hilo na wameweka askari wa kutosha ili kulinda eneo ilipotokea machafuko hayo.

SIX AFURAHISHWA NA KUREJEA KWA ADEBAYOR KATIKA KIKOSI CHA TOGO.

KOCHA wa timu ya taifa ya Togo, Didier Six amewaambia waandishi wa habari jijini Lome kuwa amefurahishwa na kitendo cha mshambuliaji nyota wa klabu hiyo Emmanuel Adebayor kurejea katika kikosi chake baada ya kukataa kufanya hivyo kwa kipindi kirefu. Six aliendelea kusema kuwa Adebayor mwenye umri wa miaka 28 alimfuata wakati akiwa mapumzikoni ambapo Togo ilikuwa ikicheza mchezo wa kirafiki na Burkina Faso nchini Ufaransa na kumuomba ampange katika kipindi cha pili. Ingawa walipoteza mchezo huo kwa mabao 3-0 lakini kocha huyo amesema kuwa alifarijika na kiwango pamoja na morali waliyoonyesha wachezaji wake pindi Adebayor alipoingia uwanjani. Kocha huyo amesema kuwa kikosi chake kina morali ya kutosha tayari kwa mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2013 dhidi ya Gabon na lazima atamjumuisha Adebayor katika kikosi chake hicho. Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester City ambaye amehamia moja kwa moja katika klabu ya Tottenham Hotspurs alipokuwa akicheza kw mkopo alikataa kuichezea timu ya taifa ili kuwashinikiza viongozi wa soka nchini kwake kuwahakikishia wachezaji wa timu hiyo usalama, usafiri wenye uhakika na malazi bora.

SANTOS AKABILIWA NA KIFUNGO KWA KUENDESHA MWENDO KASI.

MCHEZAJI nyota wa klabu ya Arsenal Andre Santos huenda akakabiliwa na adhabu ya kifungo jela baada ya polisi kumtuhumu kukimbiza gari lake kwa spidi kubwa inayofikia kilometa 130 kwa saa. Beki huyo wa kimataifa wa Brazil alifanya tukio hilo wakati akielekea mazoezini kwenye klabu yake hiyo ambapo alikuwa gari lake la kifahari aina ya Maserati GranTurismo alilonunua kwa paundi 110,000. Polisi wanadai kuwa mchezaji huyo alipita kwa mwendo kasi huo na kuwakimbia polisi ambapo anaweza kufungwa jela kama akipatikana na hatia ya kuendesha mwendo wa hatari. Polisi waliendelea kudai kuwa walimsimamisha mchezaji huyo lakini hakusikia lakini alifanikiwa kumsimamisha akiwa amekaribia kabisa sehemu ya kufanyia mazoezi ya klabu yake umbali wa mita 500.

Tuesday, August 21, 2012

ADEBAYOR AKUBALI KUKATWA MSHAHARA ILI AENDE MOJA KWA MOJA CITY.

MSHAMBULIAJI nyota wa Manchester City ambaye anacheza kwa mkopo katika klabu ya Tottenham Hotspurs anatarajiwa kukamilisha mkataba wake wa moja kwa moja kuhamia klabu hiyo yenye maskani yake jijini London. City na Spurs tayari zilishafikia makubaliano ya kuuziana mchezaji huyo kwa ada ya paundi milioni tano wiki sita zilizopita lakini uhamisho huo ulikwamishwa kutokana na kushindwa kufikia maelewano ya mambo binafsi ya mchezaji huyo na klabu hiyo. Lakini hatimaye mchezaji huyo amekubali kukatwa kiasi kikubwa cha mshahara wa paundi 170,000 ambacho alikuwa akilipwa wakati akiwa katika klabu ya City alipojiunga nayo katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka 2009. Hata hivyo City nao watakuwa wamepata hasara kubwa kwa mchezaji huyo wa kimataifa kutoka Togo ambaye walimnunua kutoka klabu ya Arsenal kwa ada ya paundi milioni 25. Kwasasa meneaj wa City anajipanga kutumia mwanya wa kumuuza Adebayor kujaribu kumnyakuwa kiungo Javi Martinez ambaye anataka kwenda klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani akitokea klabu ya Athletic Bilbao ya Hispania.

KLABU YA MACEDONIA YAFUNGIWA MIAKA MINNE BAADA YA WACHEZAJI KUPIMWA NA KUKUTWA POSITIVE NA MADAWA YALIYOKATAZWA MICHEZONI.

SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA limeifungia klabu ya Rabotnicki ya Macedonia miaka minne kushiriki michuano inayoandaliwa na bara hilo baada ya wachezaji wake wawili kupimwa na kukutwa wametumia madawa yaliyokatazwa michezoni. Klabu hiyo pia imetozwa faini ya euro 30,000 baada ya wachezaji hao Milovan Petrovic na Dino Najdoski kukutwa wakiwa wametumia dawa hizo zilizokatazwa kufuatia kipigo cha mabao 6-0 walichopata kutoka kwa Lazio ya Italia katika mchezo wa mtoano wa michuano ya Ligi ya Ulaya maarufu kama Europa League. Mbali na kufungiwa kwa klabu hiyo, wachezaji hao pia walifungiwa mwaka mmoja kila mmoja wakati daktari wa timu hiyo Mihajlo Ivanovski na mwalimu wa viungo Darko Velcevski nao walifungiwa kujishughulisha na masuala ya michezo kwa kipindi cha miaka mitatu kila mmoja. Mbali na adhabu hizo UEFA pia imetuma maombi Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuidhinisha adhabu hiyo ili wasiweze kushiriki mashindano yoyote duniani.

FUNNY Mario Balotelli v City Photographer

LIGI KUU TANZANIA BARA YAPIGWA KALENDA.

Angetile Osiah.
Kumekuwepo na taarifa tofauti kuhusu kuanza kwa Ligi Kuu ya Bara ambayo kwa mujibu wa kalenda ya Shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), inatakiwa kuanza Septemba 01, 2012. Baada ya kikao cha pamoja baina ya TFF na viongozi wa klabu za Ligi Kuu kilichofanyika Jumatatu ya Agosti 20, 2012 kwenye ofisi za TFF, TFF inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:

1. Baada ya kikao cha pamoja baina ya TFF, Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu zote za Ligi Kuu, ilionekana kuwa kutokana na kutokamilika kwa mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na mdhamini wa sasa, yaani Vodacom, mwanzo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa Septemba 15, 2012. Hii inatokana na ukweli kwamba kukamilika kwa mazungumzo baina ya pande husika, ndio kutatoa picha halisi ya Ligi Kuu ya msimu ujao.

2. Mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na Vodacom yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii kwa kuwa yameshafikia hatua nzuri na hivyo mkataba unaweza kusainiwa wakati wowote baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.

3. Kukamilika kwa mazungumzo hayo ni muhimu kwa kuwa kutasaidia Ligi Kuu kuanza bila ya matatizo yoyote kwa klabu zinazoshiriki, TFF na Kamati ya Ligi hasa kutokana na ukweli kuwa baadhi ya mambo yatakayokubaliwa yatalazimika kuingizwa kwenye Kanuni za Ligi; yatasaidia upatikanaji wa fedha kwa muda muafaka; upatikanaji wa vifaa kwa muda muafaka na masuala mengine muhimu.

4. Ratiba ya Ligi Kuu sasa inatarajiwa kutangazwa mapema wiki ijayo pamoja na tarehe rasmi ya kuanza kwa Ligi Kuu

5. Kutokana na kusogwezwa mbele kwa tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu, mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya mabingwa wa Tanzania Bara na washindi wa pili, nao sasa utapangiwa tarehe nyingine ambayo ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu. Kwa maana hiyo mchezo huo utachezwa katika siku itakayotangazwa baadaye.

6. Kuhusu chombo kitakachoongoza Ligi Kuu, TFF ilitoa mapendekezo ya Kamati ya Utendaji kwa Kamati ya Ligi na baadaye kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu kuhusu muundo wa chombo hicho kulingana na mwongozo wa Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) na Katiba ya TFF na suala hilo kwa sasa linajadiliwa na klabu za Ligi Kuu kwa ajili ya hatua za mwisho.


IMETOLEWA NA KATIBU MKUU TFF, ANGETILE OSIAH.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

SEMINA KWA AJILI YA MAKAMISHNA, WAAMUZI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa semina kwa ajili ya makamishna (match commissioners), watathmini wa waamuzi (referees assessors) na waamuzi wa daraja la kwanza (class one) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Ligi Kuu inayotarajia kuanza baadaye mwezi ujao. Kwa upande wa makamishna na watathmini wa waamuzi, semina itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 29-30 mwaka huu. Washiriki wanatakiwa kujigharamia kwa kila kitu; usafiri, malazi na chakula wawapo kwenye semina. Semina kwa waamuzi itafanyika katika vituo vya Dar es Salaam na Mwanza kuanzia Agosti 31- Septemba 2 mwaka huu. Pia nao watajigharamia kwa kila tu. Waamuzi watakaoshiriki semina hiyo ni ambao hawakushiriki ile iliyofanyika Juni mwaka huu na wale walioshiriki lakini hawakufaulu mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test). Waamuzi wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) hawashiriki kwa vile wao wamekukuwa wakishiriki semina zao zinazoandaliwa na FIFA kila baada ya miezi mitatu.

TENGA AKATAA KUJIUZULU KWA RAGE
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amekataa barua ya kuomba kujiuzulu ya mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Ismail Aden Rage. Rage ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Simba alimuandikia Rais Tenga barua ya kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichosema ‘kamati hiyo kushindwa kwa makusudi kusimamia sheria na kanuni za uendeshaji wa mpira Tanzania zinavyoeleza.’ Amekataa ombi hilo kwa maelezo kuwa kama Rage amehisi kuwepo udhaifu wa kutosimamia sheria na kanuni kama inavyotakiwa, ni vyema akaendelea kuwemo kwenye kamati hiyo ili kuisaidia kusimamia sheria na kanuni hizo kama inavyotakiwa badala ya kujiuzulu. “Kutokana na uzoefu na uwezo ambao Rage anao katika uongozi wa mpira wa miguu, ni vyema akautumia kuisaidia kamati kutekeleza wajibu wake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ili kusaidia kusukuma mbele gurudumu za maendeleo ya mpira wa miguu,” amesema Rais Tenga. Pia Rais Tenga amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mpira wa miguu kuongozwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo, rai ambayo imetoa kwa kamati zote za TFF ili kuhakikisha kuwa mpira wa miguu unaongozwa bila kuonea wala kupendelea upande wowote. Rais Tenga amesisitiza kuwa kamati hazina budi kuchukua hatua zinazostahili bila woga pale kanuni zinapotaka hatua kuchukuliwa. Amezitaka kamati zisisite kwa namna yoyote ile kuchukua hatua kwa vile kwa kufanya hivyo, uwezekano wa kutokea upendeleo au uonevu utapungua, hivyo mpira wa miguu kuongozwa kwa sheria na haki.

WACHEZAJI HAMKUTUMIA VYEMA VAN PERSIE - FERGIE.

MENEJA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amesema kuwa kikosi chake kilishindwa kumtumia ipasavyo mshambuliaji nyota mpya wa klabu hiyo aliyesajiliwa hivi karibuni Robin van Persie. Bao la kichwa lililofungwa na Marouane Fellaini katika kipindi cha pili lilitosha kuipa ushindi Everton waliokuwa wakicheza katika uwanja wao wa nyumbani dhidi ya United ambayo ilicheza bila kuwepo kwa mabeki wake wanne ambao ni majeruhi. Van Persie ambaye alisajiliwa na United kwa ada ya paundi milioni 24 aliingia akitokea benchi la wachezaji wa akiba katika kipindi cha pili lakini alishindwa kupata bao katika mchezo huo kama mashabiki wengi wa klabu hiyo walivyokuwa wakitegemea. Ferguson amesema kuwa tatizo kubwa la mchezaji kushindwa kufunga ni upande wa pembeni ambao alikuwa akimchezesha kwenye mchezo huo tofauti na ile nafasi ya katikati ambayo amezoea kucheza wakati akiwa Arsenal. Van Aliingia katika dakika ya 68 akichukua nafasi ya Danny Welbeck ambaye alianza katika mchezo huo lakini hakuweza kuiokoa timu hiyo kuepuka kipindi cha kwanza toka mwaka 2004 katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi kuu nchini Uingereza.

PARDEW KUKUBALI KUFUNGIWA MECHI MBILI NA FA.

MENEJA wa klabu ya Newcastle United Alan Pardew hatopinga adhabu atakayopewa na Chama cha Soka nchini Uingereza-FA kwa kosa la kumsukuma mwamuzi msaidizi wakati wa mchezo baina ya timu yake na Tottenham Hotspurs ambao ulimaliza kwa ushindi wa mabao 2-1. Pardew alitolewa katika benchi la ufundi la klabu hiyo na kuamriwa kwenda kukaa jukwaani na mashabiki baada ya kumsukuma mshika kibendera Peter Kirkup wakati akidai mpira uliokuwa umetoka nje nakuamriwa kurushwa katika lango lao. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 51 amepewa muda wa mpaka alhamisi awe amekata rufani lakini hatahivyo inaaminika kuwa atakubali uamuzi utakaotolewa na FA uamuzi ambao unatarajiwa kuwa ya kufungiwa michezo miwili. Pardew aliomba radhi kwa mwamuzi wa mchezo huo Martin Atkinson na pia mbele ya vyombo vya habari kwa kitendo alichofanya lakini mwamuzi Atknson aliamua kutaja tukio hilo katika ripoti yake aliyowasilisha kuhusu mchezo huo.