VALCKE AZURU TENA BRAZIL.
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA, Jerome Valcke ametua nchini Brazil ikiwa ni safari yake nne katika ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi na miundo mbinu kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Valcke ambaye aliungana na nyota wa zamani wa soka wa nchi hiyo, Ronaldo de Lima na Bebeto ambao ndio wawakilishi wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo nchini humo walitembelea mji wa Manaus ambao uko Kaskazini mwa nchi hiyo ili kuangalia maendeleo ya ujenzi wa uwanja ambao utatumika 2014. Uwanja huo unaoitwa Arena Amazonia unajengwa kwa gharama ya kiasi cha dola milioni 260 na utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 44,000 ambao mpaka sasa ukiwa umekamilika kwa asilimia 42 pekee huku ukitarajiwa kukamilika kabisa June mwakani. Mapema leo Valcke alitarajiwa kutembelea uwanja mwingine uliopo katika mji wa Cuiaba ambao unajengwa kwa gharama ya dola milioni 254 na mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 46 pekee. Valcke akimaliza ziara katika miji hiyo anatarajiwa kukutana na maofisa kamati ya maandalizi na kufanya mkutano na waandishi wa habari ili kuzungumzia maendeleo ya maandalizi ya michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment