Friday, January 20, 2017

DEPAY ATUA RASMI LYON.

KLABU ya Manchester United imemuuza rasmi winga wa kimataifa wa Uholanzi Memphis Depay kwenda klabu ya Lyon ya Ufaransa. Taarifa zinadai kuwa ada uhamisho huo ni paundi milioni 16 inayoweza kupanda mpaka paundi milioni 21.7 kama Lyon wakifuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Depay akipewa mkataba mpya. United pia imekubaliana na Lyon kupewa kipaumbele kama klabu hiyo itaamua kumuuza mchezaji huyo. Depay mwenye umri wa miaka 22 amefunga mabao saba katika mechi 53 alizoichezea United toka ajiunge nao kwa kitita cha paundi milioni 25 akitokea PSV Eindhoven ya Uholanzi mei mwaka 2015.

FIFA YAAMRIWA KUMLIPA LASSANA DIARRA EURO MILIONI SITA.

MAHAKAMA nchini Ubelgiji imetoa hukumu kuwa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA na lile la Uholanzi-KBVB kulaumiwa kwa kushindikana kufanyika usajili wa Lassana Diarra kwenda Charleroi mwaka 2015 na sasa lazima wamlipe kiungo huyo euro milioni sita. Mahakama ya Charleroi iliamua kuwa FIFA walikiuka sheria ya Umoja wa Ulaya-EU kwa kuingilia uhuru wa kuhama baada ya kudai kuwa klabu yeyote itakayomsajili Diarra italazimika kulipa deni la euro milioni 10 anazodaiwa na klabu ya Lokomotiv Moscow. Kiungo huyo wa zamani wa Arsenal, Chelsea na Real Madrid alilimwa faini hiyo kubwa kwa kuvunja mkataba wake wa miaka minne na Lokomotiv, kwa kuondoka katika klabu hiyo ya Urusi baada ya kupita miezi 12 pekee. Kufuatia muongozo huo wa FIFA, klabu ya Charleroi ya Ubelgiji ilisitisha mazungumzo yake na Diarra Februari mwaka 2015 na baadae nyota huyo kujiunga na Marseille kufuatia kutocheza msimu mzima wa 2014-2015.

Thursday, January 19, 2017

SENEGAL YAWA YA KWANZA KUTINGA ROBO FAINALI AFCON, TUNISIA YAZINDUKA.

TIMU ya taifa ya Senegal imekuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika baada ya kuishindilia Zimbabwe kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kundi B uliochezwa jijini Franceville. Mabao ya Sadio Mane katika dakika ya tisa na lingine la mpira wa adhabu lilifungwa na Henry Saivet katika dakika ya 13 yalitosha kuwahakikishia nafasi ya kutinga hatua ya mtoano baada ya pia kushinda mabao 2-1 dhidi ya Tunisia katika mchezo wao wa kwanza. Katika mchezo wa awali Tunisia nao walifanikiwa kurekebisha makosa yao ya kupoteza mchezo wao wa kwanza kwa kuichapa Algeria mabao 2-1 na kufufua matumaini yao ya kusonga mbele. Timu hizo zinatarajia kucheza mechi zao za mwisho za kundi B Jumatatu ijayo ambapo Senegal watapepetana na Algeria jijini Franceville wakati Zimbabwe wakitafuta ushindi wao wa kwanza katika michuano hii kwa kuchuana na Tunisia huko Libreville.

SIMEONE APOZA TAARIFA ZA GRIEZMANN KUWANIA MAN UNITED.

KOCHA wa Atletico Madrid, Diego Simeone hajashangazwa na taarifa za Antoine Griezmann kuwaniwa na klabu nyingi ikiwemo Manchester United na kuongeza kuwa hatamzuia mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa kama akiamua kuondoka. Mapema wiki hii kumekuwa na taarifa kuwa mazungumzo kwa ajili ya nyota huyo kwenda Old Trafford yamefikia pazuri na United wanajiandaa kutoa kitita cha euro milioni 100 ili kuvunja mkataba wake na Atletico. Akizungumzia kuhusiana na taarifa hizo Simeone amesema hana mpango wa kuzuia mchezaji yeyote kwani anachofanya yeye ni kufanya kazi kwa ajili ya manufaa ya klabu. Simeone aliendelea kudai kuwa Griezmann amekuwa katika kiwnago cha juu huku akifunga mabao hivyo ni kawaida kwa klabu kubwa kumuwania.

NILIKATAA KUJIUNGA NA LYON KWASABABU YA AFCON.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Togo, Emmanuel Adebayor amedai kuwa alikataa uhamisho wa kwenda Lyon ili aweze kuitumikia nchi yake katika michuano ya Mataifa ya Afrika. Adebayor ambaye bila klabu toka alipoondoka Crystal Palace mwishoni mwa msimu uliopita, ndio nahodha wa Togo katika michuano hiyo inayoendelea nchini Gabon. Mshambuliaji huyo angekosa zaidi ya mwezi mmoja msimu wa Ligue 1 kama Togo watafanikiwa kufika fainali Februari 5 na Lyon hawakufurahishwa na suala hilo ndio maana uhamisho wake ukashindikana. Adebayor amesema alikataa ofa ya mkataba ya Lyon ili aweze kuiwakilisha nchi yake kwani moja ya msharti katika mkataba huo ilikuwa ni kutoshiriki michuano hiyo.

MALINZI AULA FIFA.

SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya soka ya FIFA kwa miaka minne ijayo. Uteuzi huo unaanza mwaka huu 2017 hadi 2021. Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Januari 18, 2017 iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Fatma Samoura inasema: “Tuna faraja kukufahamisha kuwa umeteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya FIFA. Tunachukua nafasi hii kukupongeza kwa uteuzi huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Taarifa hiyo ilifafanua kuwa Kamati hiyo inayoongozwa na Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Bara la Asia, ina majukumu ya kusimamia mipango ya maendeleo ya mpira wa miguu duniani kote. Wajumbe wengine wote watatangazwa kwenye tovuti ya FIFA ambayo ni www.FIFA.com. Huu ni mfululizo wa Tanzania kupata nafasi katika vyombo vikubwa vinavyoendesha soka FIFA na CAF. Mwishoni mwa mwaka jana, CAF – Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika lilimteua Rais Malinzi kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati maalumu inayoongozwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou ya kuboresha mfumo wa uongozi wa CAF. TFF inamshukuru Rais Gianni Infantino na kamati yake ya ushauri kwa kumteua Malinzi katika nafasi ya ujumbe katika kamati hiyo muhimu ya maendeleo ya soka ulimwenguni.

HATMA YA ZANZIBAR CAF KUJULIKANA MACHI 26.

KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limepitisha ombi la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) la Zanzibar kuwa mwanachama kamili wa CAF. Katika kikao chake cha Kamati ya Utendaji kilichoketi Januari 12, mwaka huu kiliamua kupitisha ombi hilo kuwa moja ya ajenda za Mkutano Mkuu wa CAF utakaofanyika Machi 16, 2017 huko Addis Ababa, Ethiopia. Hivyo sasa Mkutano Mkuu huo utapiga kura na kama Zanzibar itapata idadi ya kura theluthi mbili yaani 2/3 ya wanachama wote, itatangazwa kuwa mwanachama mpya kamili wa CAF ambako atakuwa na haki mbalimbali za kama mwanachama. Haki hizo ni pamoja na kushiriki michuano yote inayoandaliwa na kusimamiwa na CAF na hii ni pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), fainali za Afrika Wanawake (AWCON), fainali za vijana (AFCON U17 na AFCON 20)na pia kuhudhuria mikutano mbalimbali ya CAF kama mwanachama kamili, kupokea na kusimamia kozi mbalimbali za CAF nakadhalika. Pia itakuwa na fursa ya kupiga kura katika masuala muhimu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) tofauti na sasa ambako inapata fursa ya klabu zake zinazoshika nafasi ya juu katika Ligi Kuu ya Zanzibar kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa Mheshimiwa Nape Nnauye – Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano Tanzania pamoja na Mheshimiwa Rashid Ali Juma - Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanizbar (SMZ) kwa kufanikisha hatua hiyo. Pia, TFF inatoa shukrani kwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Ravia Idarus Faina pamoja na Rais wa Heshima wa TFF Leodegar Chilla Tenga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa CAF na Marais wa Heshima wa TFF Said Hamad El Maamry ambaye ni Mjumbe wa kudumu wa CAF na Mzee Muhiddin Ndolanga na wadau wote wa familia ya mpira wa miguu kwa mafanikio ya hatua hii. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa sasa linajikita kwenye kampeni nzito ya kuomba kura za kutosha kuhakikisha kwamba Zanzibar inapata nafasi hiyo ya uanachama kamili. Kadhalika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia viongozi wake wako kwenye mchakato wa kumfanyia kampeni Rais wa Heshima wa TFF, Bw. Leodegar Chilla Tenga kuhakikisha anashinda nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji (Council) ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Leodegar Tenga anawania nafasi hiyo kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya Kiingereza akishindana na Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Zambia, Kalusha Bwalya na Kwesi Nyantakyi wa Ghana. TFF inaomba Watanzania wote na wadau wote wa mpira wa miguu nchini kutuunga mkono katika juhudi na jitihada zetu za kuona Zanzibar inapata nafasi hiyo kadhalika Tenga anakuwa mjumbe kwenye baraza la ushauri huko FIFA.