Friday, September 1, 2017

CHELSEA YAWANASA DRINKERWATER NA ZAPPACOSTA DAKIKA ZA MAJERUHI

MABINGWA wa Ligi Kuu Uingereza, Chelsea imekamilisha usajili uliokuwa na changamoto nyingi Alfajiri ya leo kwa kuwanasa kiungo Danny Drinkwater kutoka Leicester City na beki wa kulia wa kimataifa wa Italia Davide Zappacosta kutoka Torino. Meneja wa Chelsea Antonio Conte alishuhudia mawindo yake kadhaa yakishindikana katika muda wa mwishoni wa usajili wa kipindi hiki cha kiangazi lakini alifanikiwa kuimarisha kikosi chake kuelekea michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Drinkwater mwenye umri wa miaka 27 amesajiliwa kwa mkataba wa miaka mitano na ada inayokadiriwa kufikia paundi milioni 35, ambayo ilitangazwa saa mbili na nusu baada ya dirisha la usajili kufungwa jana usiku. Zappacosta mwenye umri wa miaka 25 amesajiliwa kwa mkataba wa miaka minne na Chelsea wametoa paundi milioni 23 kunasa saini ya beki huyo. Mbali na hao Chelsea pia ilifanikiwa kuwasajili mapema kipa Willy Caballero, beki Antonio Rudiger, kiungo Tiemoue Bakayoko na mshambuliaji wa kimataifa wa Hispania Alvaro Morata aliyejiunga nao kutoka Real Madrid kwa ada iliyovunja rekodi ya klabu ya paundi milioni 58.

No comments:

Post a Comment