Friday, September 1, 2017

COUTINHO AITAKATISHA BRAZIL

TIMU ya taifa ya Brazil, imefanikiwa kujihakikishia nafasi ya kumaliza kinara katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia huko Amerika Kusini baada ya kuichapa Ecuador jana wakati Chile na Argentina zikiendelea kusuasua kwa mara nyingine. Brazil ilishinda mchezo huo kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na nyota wa Liverpool Philippe Coutinho ambaye usajili wake kwenda Barcelona ulikwama pamoja na Paulinho ambaye amesajili kipindi hiki cha kiangazi na Barcelona akitokea Shanghai Evergrande ya China. Ushindi huo unakuwa wa tisa mfululizo kwa Brazil na kuwapata mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia uhakika wa kumaliza kinara kutokana na tofauti ya alama 11 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine. Timu nne kutoka ukanda huo ndio zinafuzu moja kwa moja michuano hiyo ijayo inayofanyika nchini Urusi mwakani huku ile ya tano ikienda kucheza hatua ya mtoano. Katika michezo mingine iliyochezwa mapema leo Alfajiri, Colombia walitoka sare tasa na Venezuela, Peru waliididimiza Bolivia mabao 2-1, Paraguay ikaishughulikia Chile kwa kuitandika mabao 3-0 na Argentina walitoka sare ya bila kufungana na Uruguay.

No comments:

Post a Comment