Friday, October 31, 2014

MESSI NI FUNDI ZAIDI YA RONALDO - CAPELLO.

KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Fabio Capello amedai kuwa nyota wa Barcelona Lionel Messi ana kipaji zaidi ya mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo. Messi mwenye umri wa miaka 27 anatarajiwa kuwa mfungaji mwenye mabao mengi la Liga kama akifunga mabao mawili katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Celta Vigo hapo kesho. Ronaldo mwenye umri wa miaka 29 anashikilia nafasi ya 10 katika orodha hiyo. Capello amesema Ronaldo ni mchezaji mwenye nguvu mbinu nzuri lakini huwezi kulinganisha ujuzi wa kiufundi halisi alionao Messi. Messi ameshafunga mabao 250 katika mechi 284 alizoichezea Barcelona akiwa amebakisha bao moja kufikia rekodi ya nyota wa zamani wa Atletico Madrid telmo Zarra aliyoweka kati ya mwaka 1940 na 1950.

SUAREZ ALISTAHILI KUWEPO KATIKA ORODHA ZA BALLON D'OR - BARTRA.

BEKI wa kati ya klabu ya Barcelona Marc Bartra amesema ameshangazwa kwa kukosekana kwa Luis Suarez katika orodha ya kugombea tuzo za Ballon d’Or. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay alifunga mabao 31 katika mechi 33 akiwa na Liverpool msimu uliopita huku 12 kati hayo akiwa amefunga mwaka huu na kutoa pasi za kusaidia 11. Lakini pamoja na mafanikio hayo, Suarez anaonekana bado kuandamwa na mzimu wa kumng’ata Giorgio Chiellini wa Italia katika Kombe la Dunia nchini Brazil na kumfanya kufungiwa miezi minne adhabu ambayo aliimaliza wiki iliyopita. Bartra anaamini mshambuliaji huyo ambaye alitengeneza bao la Barcelona lililofungwa na Neymar katika mchezo wa El Clasico dhidi ya Madrid, alitakiwa kuwepo katika orodha hiyo. Akihojiwa beki huyo mwenye umri wa miaka 23 amesema maeshangazwa kwa Suarez kuachwa kwani anadhani alikuwa na mwaka wenye mafanikio.

TAJIRI LA CARDIFF LAWEKEZA TENA KATIKA SOKA MAREKANI.

MMILIKI wa klabu ya Cardiff City Vincent Tan na nguli wa zamani wa mpira wa kikapu wa Marekani Magic Johnson ni miongoni mwa kundi la wawekezaji ambao wamepewa klabu mpya ya soka katika Ligi Kuu ya Marekani-MLS ya Los Angeles FC. Kundi hilo la uwekezaji pia linamjumuisha mmiliki mwenza wa klabu ya Queens Park Rangers-QPR, Ruben Gnanalingam sambamba na mchezaji wa zamani wa soka la wanawake la nchi hiyo Mia Hamm. Timu hiyo mpya wa Los Angeles itasajiliwa rasmi MLS mwaka 2017 sambamba na timu nyingine kutoka Atlanta. Tan ambaye pia anamiliki timu ya TK Sarajevo ya Bosnia aliiambia BBC kuwa atakuwa mmiliki mwenye hisa nyingi zaidi katika klabu hiyo mpya.

GERRARD ADOKEZA KUIHAMA LIVERPOOL.

NAHODHA wa klabu ya Liverpool, Steven Gerrard amebainisha kuwa atajiunga na klabu nyingine kama timu hiyo ikishindwa kumpatia mkataba mpya. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye alijiunga katika shule ya soka ya Liverpool akiwa na umri wa miaka tisa, ameondoa uwezekano wa kustaafu soka wkati mkataba wake utakapomalizika Mei mwaka huu. Kiungo huyo amesema hana mpango wa kutundika daruga majira ya kiangazi kwani amepanga kuendelea kucheza soka zaidi. Gerrard aliendelea kudai kuwa kwasasa anasubiria kuona kama itakuwa ni Liverpool au mahali pengine, huo utakuwa uamuzi wa klabu hiyo. Nahodha huyo wa zamani wa Uingereza ambaye alitangaza kustaafu soka la kimataifa Julai mwaka huu ameichezea Liverpool karibu mechi 700, huku akicheza na washambuliaji mahiri wa zamani Robbie Fowler na Michael Owen.

POLISI YAKANUSHA KUKAMATWA KWA MUUAJI WA MEYIWA.

POLISI nchini Afrika Kusini wamekanusha taarifa kuwa watuhumiwa katika kesi ya mauaji ya nahodha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana, Senzo Meyiwa wamekamatwa katika daraja la Beit lililopo katika mkapa na Zimbabwe. Msemaji wa jeshi hilo Neville Malila amesema tetesi hizo kuwa kuna mtu amekamatwa sio za kweli ila uchunguzi kuhusiana na tukio hilo bado unaendelea. Mapema kulizuka taarifa kuwa mtuhumiwa mmojawapo wa katika mauaji hayo alikamatwa katika daraja hilo lililopo mpakani na Zimbabwe na kuwa alipelekwa Vosloorus mahali ambako alitenda kosa hilo. Meyiwa aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akiwa katika harakati za kumuokoa mpenzi wake Kelly Khumalo nyumbani kwake wakati majambazi walipovamia na kutaka kuwapora vitu vyao vya thamani.

Thursday, October 30, 2014

MESSI APIGWA BAO TENA, MASCHERANO ANYAKUWA TUZO YA MCHEZAJI BORA WA MWAKA WA BARCELONA.

KIUNGO mahiri wa Barcelona, Javier Mascherano amechaguliwa kuwa mchezaji wa mwaka wa klabu hiyo na kumshinda nahodha wake wa timu ya taifa ya Argentina na mchezaji bora wa zamani wa dunia Lionel Messi. Mascherano amekuwa akicheza kwa kiwango kikubwa wakati Barcelona wakikabiliwa na msimu mgumu aionyesha uwezo mkubwa wa kumudu nafasi ya beki wa kati na kiungo mkabaji. Messi ameshinda tuzo hiyo mara tatu katika kipindi cha miaka minne lakini amekosa tuzo hiyo ya msimu wa mwaka 2013-2014 kama alivyoikosa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa mwaka aliyochukua Cristiano Ronaldo. 
Mascherano aliwashukuru wale waliompigia kura kushinda tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kuonyesha jitihada zaidi kwa msimu mzima. Tuzo hiyo hupigiwa kura na wajumbe maalumu kutoka vyombo vya habari vya Catalan pamoja na maofisa wa juu wa klabu hiyo akiwemo rais wake Josep Maria Bartomeu.

JUVENTUS KUIVAA NAPOLI JIJINI DOHA KATIKA MCHEZO WA SUPERCUP.

MAOFISA wa Serie A nchini Italia wamethibitisha kuwa mtanange wa Supercup ambao utawakutanisha mabingwa wa ligi hiyo Juventus na mabingwa wa Kombe la Italia Napoli, utafanyika jijini Doha, Qatar Desemba 22 mwaka huu. Hii itakuwa mara ya saba kwa mtanange huo kufanyika nje ya Italia na waandaaji wanategemea mchezo wa kiungwana kuliko uliozikutasha timu hizo jijini Beijing miaka miwili iliyopita. Katika mechi hiyo Juventus walishinda kwa mabao 4-2 baada ya muda wa nyongeza huku wachezaji wawili wa Napoli wakipewa kadi nyekundu na baadae kukataa kuzungumza na wanahabari. Supercup ilianza kuchezwa nje ya Italia mwaka 1993 wakati AC Milan ilipokwaana na Torino jijini Washington, baadae ilikwenda nchini Libya mwaka 2002 na kurejea tena Marekani kwa kuchezwa katika Uwanja wa Giants mwaka 2003. Mtanange huo pia umewahi kuchezwa jijini Beijing mwaka 2009 na 2011.

KOCHA WA BENFICA AHOJI VIGEZO VILIVYOTUMIKA KUTEUA ORODHA YA MAKOCHA WATAOGOMBEA TUZO YA KOCHA BORA WA MWAKA.

MENEJA wa klabu ya Benfica, Jorge Jesus amesisitiza kuwa alipaswa kujumuishwa katika orodha ya makocha 10 watakaogombea tuzo ya kocha bora wa mwaka, akidai kuwa baada ya walioukuwemo katika orodha hiyo wamepata mafanikio madogo kuliko yeye. Akihojiwa Jesus ambaye aliiongoza Benfica kushinda mataji matatu ya nyumbani msimu uliopita huku akifika fainali ya michuano ya Europa League amesema hajui ni vigezo vipi vilivyotumika kuteua orodha hiyo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kuna baadhi ya makocha walioteuliwa wamepata mafanikio kiduchu kuliko yeye la anashangaa wamejumuishwa kwenye orodha hiyo. Jesus amesema kutokana na jinsi orodha hiyo ilivyo anadhani hata yeye alipaswa kuwemo kutokana na mafanikio aliyopata akiwa na Benfica msimu uliopita. Orodha hiyo makocha walioteuliwa na timu zao katika ni pamoja na Carlo Ancelotti (Real Madrid), Antonio Conte (Italy/Juventus), Pep Guardiola (Bayern Munich), Juergen Klinsmann (United States), Joachim Loew (Germany). Wengine ni Jose Mourinho (Chelsea), Manuel Pellegrini (Manchester City), Alejandro Sabella (Argentina), Diego Simeone (Atletico Madrid) andLouis van Gaal (Netherlands) were on the Fifa shortlist announced on Wednesday.

WINGA WA CELTIC AFUNGIWA MECHI SABA KWA UBAGUZI.

WINGA mahiri wa klabu ya Celtic, Aleksandar Tonev amefungiwa mechi saba kwa kosa la kumfanyia vitendo vya unaguzi wa rangi beki wa timu ya Aberdeen Shay Logan. Tonev mwenye umri wa miaka 24 alilimwa adhabu hiyo kufuatia tukio hilo na Logan ambaye ni raia wa Uingereza katika mechi ya Ligi Kuu nchini Scotland Septemba mwaka huu. Winga huyo wa kimataifa wa Bulgaria yuko kwa mkopo Celtic akitokea klabu ya Aston Villa. Celtic katika taarifa yake wamesema watakata rufani kupinga adhabu hiyo wakidai kuwa mchezo huyo siyo mbaguzi. Tukio hilo limetokea katika kipindi cha cha mchezo ambao Celtic waliifunga Aberdeen mabao 2-1 Septemba 13.

VILABU VIKUBWA ULAYA KUKUTANA KUJADILI MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA 2022 QATAR.

KLABU kubwa barani Ulaya zinatarajiwa kukutana wiki ijayo ili kutoa ombi kwa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuruhusu michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar kuchezwa kati ya Aprili 28 na Mei 29 wakati huo. Qatar ilishinda haki ya kuandaa michuano hiyo mwaka 2010 lakini kumekuwa na tume maalumu iliyoundwa kuangalia uwezekano wa michuano hiyo kuchezwa majira ya baridi kutokana na joto kali lililopo katika nchi hiyo majira ya kiangazi. Muungano wa vilabu vya Ulaya-ECA, ambao unajumuisha vilabu vya Manchester, Liverpool, Barcelona na Bayern Munich unataka kuwasilisha ombi hilo ikiwemo kuanza mechi za ligi ya msimu wa mwaka 2021-2022 wiki mbili mapema na kucheza mechi za mwisho za kombe la FA baada ya fainali hizo. Kama FIFA wakiruhusu michuano hiyo kuchezwa kipindi hicho, hatua hiyo itasababisha Kombe la FA la Uingereza kukamilika Juni. Muungano huo unaowakilisha timu 214 za bara Ulaya, unaamini muda huo huenda ukaathiri pia mashindano ya mataji ya nyumbani kwa nchi za Ufaransa na Hispania.

Wednesday, October 29, 2014

DORTMUND YASIMAMISHA MAZUNGUMZO YA MKATABA NA REUS.

MKURUGENZI wa michezo wa Borussia Dortmund, Michael Zorc amekiri kusimamisha mazungumzo ya mkataba mpya na Marco Reus ili kuweka mkazo katika kiwango chao uwanjani. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani ana mkataba na Dortmund unaomalizika kiangazi mwaka 2017 lakini kuna kipengele kinachomuwezesha kuondoka kama klabu inayomtaka itatoa kitita cha euro milioni 25 mwishoni mwa msimu huu. Dortmund walikuwa wakitaka kumuongeza Reus mkataba mwingine bila kuweka kipengele cha cha kuuzwa huku Bayern Munich nao wakimfuatilia nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 kwa karibu. Kwa sasa Dortmund wanaonolewa na Jurgen Klopp wako katika nafasi ya 15 katika msimamo wa Bundesliga wakiwa wameambulia alama saba katika mechi tisa walizocheza. Zorc amesema wamesimamisha mazungumzo hayo kutokana na hali ilivyo sasa katika timu hiyo kwani wanataka kutoka katika wakati mgumu waliokuwa nao.

NIGERIA YAPEWA MPAKA IJUMAA KABLA YA KUFUNGIWA.

NIGERIA imepewa hadi Ijumaa kubadili msimamo wake kuhusu uamuzi wa mahakama iliyotupilia mbali uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Soka nchini humo-NFF kabla ya FIFA kuwafungia kushiriki michuano ya kimataifa hadi Mei mwakani. Kwa mujibu wa barua iliyotumwa kwa NFF, agizo hilo la FIFA ni sharti litimizwe kufikia mchana wa tarehe 31 October. FIFA inataka bodi iliyochaguliwa Septemba 30 mwaka huu kurejeshwa madarakani haraka. Kama Nigeria ikifungiwa itapoteza nafasi ya kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika ambapo wao ni mabingwa watetezi. Tayari Nigeria imeshapigwa marufuku mara mbili mwaka huu kutokana na hatua ya serikali kuingilia masuala ya soka.

KLABU BINGWA YA DUNIA KUFANYIKA KAMA ILIVYOPANGWA - FIFA.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limedai kuwa maandalizi kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia itakayofanyika nchini Morocco itaendelea kama ilivyopangwa pamoja na wasiwasi juu ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Michuano hiyo ya siku 10 ambayo itashirikisha bingw wa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya Real Madrid inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 10 mwaka huu. FIFA imesema imefanya mawasiliano na mamlaka husika nchini Morocco na kupokea ushauri kutoka kwa Shirika la Afya Duniani-WHO mara kwa mara kuhusiana na suala hilo. Morocco pia inatarajiwa kuwa mwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika Januari mwakani. Katika taarifa yake FIFA imedai kuwa afya za wachezaji, maofisa na mashabiki wa soka ni jambo wanalolipa kipaumbele kama ilivyo kwa michuano yeyote ya kimataifa ya FIFA. Kwa mujibu wa taarifa ya WHO, Morocco haijpata mgonjwa yeyote wa Ebola hivyo maandalizi yanaweza kuendelea kama yalivyopangwa. Mlipuko wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi umeambukiza zaidi ya watu 10,000 na kuua zaidi 5,000 kwa mujibu wa takwimu za WHO.

BALOTELLI ATOA GUNDU.


MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Liverpool Mario Balotelli jana alitoa gundu na kufanikiwa kuisaidia timu yake hiyo kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Ligi. Nyota huyo alitokea benchi na kufanikiwa kuisawazishia timu yake bao kabla ya Dejan Lovren hajaongeza lingine na kuiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Swansea City. Kwa mujibu wa kocha msaidizi, Colin Pascoe, Balotelli alijiumiza wakati wakifanya mazoezi ya kupasha katika mchezo huo na kulazimika kumuona daktari kabla ya mchezo huo. Nyota huyo wa kimataifa wa Italia amekuwa akikosolewa kwa tabia yake pamoja na ukame wa kufunga mabao toka atue Anfield akitokea AC Milan Agosti mwaka huu.

MCHEZAJI WA ZAMANI WA SWEDEN AFARIKI KWA SARATANI.

KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Sweden na klabu ya Sheffield Wednesday, Klas Ingesson ambaye alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha timu yake ya taifa ambacho kilimaliza katika nafasi ya tatu katika Kombe la Dunia mwaka 1994 amefariki dunia kwa saratani akiwa na umri wa miaka 46. Akiwa mchezaji Ingesson alicheza katika vilabu kadhaa ikiwemo Gothenburg ya Sweden na Bolgona, Bari na Lecce zote za Italia kabla ya kuanza kuinoa timu ya Elfsborg ya nchini kwake. Sheffield Wednesday walituma salamu zao za rambirambi kwa mchezaji wao huyo wa zamani kupitia katika mtandao na kudai kuwa mawazo na fikra zao zipo pamoja na familia na marafiki wa Ingesson katika kipindi hiki kigumu. Ingesson aliwahi kuichezea Sweden mechi 57 huku akiiongoza vyema nchi yake kuitandika Bulgaria kwa mabao 4-0 na kuchukua nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika nchini Marekani. Nyota huyo aligundulika kuwa na saratani katika mifupa mwaka 2009.

URUSI YAZINDUA NEMBO YAO YA KOMBE LA DUNIA 2018.

NEMBO rasmi itakayotumika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi imezinduliwa jana katika Kituo cha Anga cha Kimataifa. Nembo hiyo ambayo imepambwa na rangi ya nyekundu na bluu ambazo ni rangi ya bendera ya taifa hilo huku ikionyesha utajiri wa asili na historia yake ya mafanikio na ugunduzi. Picha za nembo hiyo pia iliwekwa katika ukumbi maarufu wa Bolshoi jijini Moscow. Urusi ilishinda haki za kuandaa michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuzibwaga nchi za Uingereza, Hispania, Ureno, Uholanzi na Ubelgiji.

HAIWEZEKANI KUMNYAMAZISHA BLATTER - ANCELOTTI.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema haiwezekani kumnyamazisha Sepp Blatter baada ya rais huyo wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kudai golikipa wa Bayern Munich Manuel Neuer anastahili zaidi kushinda tuzo ya Ballon d’Or kuliko Cristiano Ronaldo. Blatter alitoa kauli hiyo mapema wiki hii akidai golikipa huyo wa kimataifa wa Ujerumani anastahili tuzo hiyo kutokana na mafanikio walipata katika michuano ya Kombe la Dunia lakini Ancelotti anadhani Ronaldo anastahili kuchukua tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo. Katika mkutano wake na wanahabari, Ancelotti amesema ameshangazwa na kauli ya Blatter lakini ana uhuru wa kusema atakacho hivyo hakuna ambacho wanaweza kufanya kuhusiana na hilo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa tuzo huwa zinazungumziwa sana miezi michache kabla ya kutolewa na kwa maoni yake hana shaka kwamba Ronaldo anastahili tuzo hiyo baada ya kushinda mataji akiwa na Madrid na kufunga mabao mengi. Orodha ya wachezaji 23 wanaogombea tuzo hiyo itapunguzwa na kubakia wagombea watatu Desemba mosi mwaka huu huku mshindi akitarajiwa kutangazwa Januari 12 mwakani.

RONALDO KUPUMZIKA KOMBE LA MFALME.

MABINGWA watetezi Real Madrid wanatarajia kumpumzisha mfungaji wao kinara Cristiano Ronaldo sambamba na wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Mfalme dhidi ya timu ya daraja la tatu ya Cornella. Ronaldo ambaye amefunga mabao 16 katika mechi nane za La Liga na matatu katika mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu anatarajiwa kupumzishwa sambamba na golikipa Iker Casillas, mabeki wa kati Sergio Ramos na Pepe sambamba na viungo Toni Kross na Luka Modric. Katika taarifa yake kwa wanahabari meneja wa Carlo Ancelotti amesema nafasi ya Casillas itazibwa na Keylor Navas na Javier Hernandez ambaye alichukuliwa kwa mkopo kutoka Manchester United anatarajiwa kuanza katika safu ya ushambuliaji sambamba na Karim Benzema. Madrid waliichapa Barcelona mabao 2-1 na kushinda taji hilo msimu wa 2013-2014. Mchezo huo wa leo utaikutanisha klabu tajiri ambayo wastani wa mapato yake kwa mwaka ni zaidi euro milioni 600, dhidi ya klabu ambayo bajeti yake kwa msimu mmoja haizidi kiasi cha euro milioni moja. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Espanyol kwasababu uwanja wa Cornella uliopo pembeni una uwezo wa kuingiza mashabiki 1,500 pekee.

MARTINS AONGEZWA MKATABA NA SOUNDERS.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Nigeria, Obafemi Martins amesaini mkataba mpya na klabu ya Seattle Sounders inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani. Pamoja na maafikiano katika mkataba huo kutowekwa wazi, Martins amekuwa akitarajiwa kupewa mkataba mpya kutokana na kiwango kikubwa alichoonyesha. Meneja wa klabu hiyo Adrian Hanauer alithibitisha Martins kusaini mkataba huo wa kuendelea kuitumikia timu hiyo aliyojiunga nayo mwaka jana. Msimu huu Martins amefanikiwa kuifungia Sounders mabao 17 na kusaidia mengine 13 na kusaidia kushinda taji la Ngao ya Mashabiki pamoja na Kombe la Wazi la Marekani.

CHELSEA CHUPUCHUPU KWA KITIMU CHA DARAJA LA PILI.

KLABU ya Chelsea jana imefanikiwa kupata bao katika dakika za mwisho kuepuka aibu ya kufungwa na timu ya daraja la pili ya Shrewbury na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Ligi. Kikosi cha Chelsea kilionekana kuhangaika kucheza vizuri katika nyasi zilizolowa za Uwanja wa Greenhous Meadow lakini walifanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wao mahiri Didier Drogba katika dakika ya 48 ya mchezo huo. Hata hivyo wenyeji walisawazisha bao hilo katika dakika ya 77 kupitia kwa Andy Mangan na kupelekea mchezo huo kuwa mgumu lakini katika dakika ya 81 Shrewsbury walijikuta wakijifunga bao kupitia kwa Jermaine Grandison aliyekuwa katika harakati za kuokoa. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo kocha wa Shrewbury Micky Mellon aliwapongeza wachezaji wake kuonyesha mchezo mzuri na kuwapa wakati mgumu wapinzani wao pamoja na tofauti kubwa kati yao zilizopo. Kwa upande wa meneja wa Chelsea Jose Mourinho alikiri kuwa na wasiwasi wakati wapinzani wao waliposawazisha lakini alimpongeza Drogba kwa kuonyesha kiwangi kikubwa ambacho kilisaidia wao kuibuka na ushindi huo muhimu.

Tuesday, October 28, 2014

MOURINHO AMLAUMU DEL BOSQUE MAJERUHI YA COSTA.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amemlaumu kocha wa timu ya taifa ya Ureno, Vicente del Bosque kutokana matatizo ya majeruhi ya Diego Costa. Mourinho amesema majeruhi ya msuli kwa Costa yalitokana na kuchezwa mechi mbili katika muda wa siku tatu wakati akiwa katika majukumu ya kimataifa. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa yeye mwenyewe alikuwa akimtumia Costa kwa tahadhari lakini hali haikuwa hivyo wakati alipokuwa na Hispania. Akiulizwa kama anadhani Costa tatizo la Costa limekwisha, Mourinho alikubali lakini akadai kuwa nyota huyo bado atahitajika kuitumikia tena nchi yake Novemba mwaka huu.

BALOTELLI AEPUKA ADHABU.

POLISI nchini Uingereza hawatachukua hatua yeyote dhidi ya Mario Balotelli kuhusu tuhuma za mshambuliaji huyo wa Liverpool kumtishia mwanamke aliyekuwa akipiga picha gari lake. Balotelli alituhumiwa kumfuata binti wa mama huyo wakati akipiga picha gari lake la kifahari la Ferrari. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na polisi wa jiji la Manchester, imedai kuwa hakuna tukio lolote uvunjifu wa sheria lililogunduliwa kutokana na tuhuma hizo. Kutoka na hilo jeshi hilo halitachukua hatua yeyote kwa Balotelli kuhusiana na tuhuma hizo. Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kutolewa katika kipindi cha mapumziko wakati Liverpool ilipotandikwa mabao 3-0 dhidi ya Real Madrid katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki iliyopita. Balotelli ambaye alinunuliwa akitokea AC Milan kwa kitita cha paundi milioni 19 alishambuliwa kwa kubadilishana jezi na Pepe katika muda wa mapumziko.

TUTAINGA MKONO URUSI KW ASILIMIA 100 - BLATTER.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amesema shirikisho hilo linaunga mkono Urusi kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na kupongeza maandalizi yake. Akihojiwa Blatter amesema bila kusita FIFA linaiunga mkono Urusi kwa asilimia 100 kuandaa michuano hiyo kwasababu wanaiamini serikali ya nchi hiyo. Vyanzo vya kidiplomasia vilidai mwezi uliopita kuwa mataifa ya Ulaya yanajadili kuunga mkono mpango wa Uingereza kumsusia rais wa Urusi Vladimir Putin michuano hiyo kwasababu ya vita vinavyoendelea mashariki mwa Ukraine. Blatter amesema hadhani kama taarifa hizo za kususia zitaleta tija yeyote kwani Urusi ni taifa kubwa na soka haliwezi kuinganosha nchi hiyo pekee bali dunia nzima.

WAJERUMANI WATAWALA ORODHA Y BALLON D'OR.

WACHEZAJI wa timu ya taifa ya Ujerumani ndio wametawala orodha ya kinyang’anyiro cha kutafuta Mchezaji Bora wa Mwaka wa Dunia inayojulikana kama Ballon d’Or. Katika orodha ya wachezaji 23, sita kati yao wametoka Ujerumani huku pia wakiteuliwa makocha 10 ambao nao watagombea tuzo ya kocha bora wa mwaka. Jurgen Klinsmann ni mmoja wa makocha walioteuliwa katika orodha hiyo baada ya kuingoza Marekani kutinga hatua ya timu 10 bora katika Kombe la Dunia. Orodha hiyo ya makocha imezua maswali mengi baada ya kuachwa makocha kama Jorge Luis Pinto wa Costa Rica na Jose Pekerman wa Colombia ambao walizisaidia timu zao kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. Mbali na hao pia wapo Jorge Sampaoli ambaye naye aliushangaza ulimwengu wakati akiongoza Chile na kuwangoa mabingwa watetezi Hispania na kutinga hatua ya mtoano smbamba na kocha wa Vahid Halilhodzic ambaye aliisaidia Algeria kufikia hatua hiyo. Kwa upande mwingine orodha ya makocha imewajumuisha Pep Guardiola wa Bayern Munich pamoja na timu yake kuishia nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita kwa kutandikwa na Real Madrid mabao 4-0, pamoja na Jose Mourinho pamoja na Chelsea kushindwa kunyakuwa taji lolote msimu uliopita. Nyota wa Ujerumani waliojumuishwa katika orodha hiyo nia pamoja na Manuel Neuer, Thomas Mueller, Toni Kroos, Mario Goetze, Philipp Lahm and Bastian Schweinsteiger wakati Argentina waliomaliza katika nafasi ya pili katika michuano ya Kombe la Dunia wao wakiingiza wacheza wachezaji watatu akiwemo Lionel Messi, Angel Di Maria and Javier Mascherano.

Orodha kamili ya wachezaji na nchi wanazotoka: Mario Goetze (Ujerumani) Toni Kroos (Ujerumani) Philipp Lahm (Ujerumani) Thomas Mueller (Ujerumani) Manuel Neuer (Ujerumani) Bastian Schweinsteiger (Ujerumani) Angel Di Maria (Argentina) Javier Mascherano (Argentina) Lionel Messi (Argentina) Andres Iniesta (Hispania) Sergio Ramos (Hispania) Diego Costa (Hispania) Karim Benzema (Ufaransa) Paul Pogba (Ufaransa) Gareth Bale (Wales) Eden Hazard (Ubelgiji) Thibaut Courtois (Ubelgiji) Cristiano Ronaldo (Ureno) Zlatan Ibrahimovic (Sweden) Neymar (Brazil) Arjen Robben (Netherlands) James Rodriguez (Colombia) Yaya Toure (Ivory Coast)

Orodha ya makocha na timu wanazofundisha: Carlo Ancelotti (Real Madrid) Antonio Conte (Italy/Juventus FC) Pep Guardiola (Bayern Munich) Juergen Klinsmann (Marekani) Joachim Loew (Ujerumani) Jose Mourinho (Chelsea) Manuel Pellegrini (Manchester City) Alejandro Sabella (Argentina) Diego Simeone (Atletico Madrid) Louis van Gaal (Uholanzi)

JEZI NAMBA MOJA YA ORLANDO PIRATES YAFUNGIWA KWA HESHIMA YA MEYIWA.

KATIKA kumkumbuka nahodha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana Senzo Meyiwa, mwenyekiti wa klabu ya Orlando Pirates Irvin Khoza ametangaza kuipumzisha jezi namba moja ya timu hiyo. Khoza amesema hadhani kama kuna mtu yeyote anayeweza kuziba nafasi ya Meyiwa ndio maana wameamua jezi yake kutovaliwa na yeyote tena. Meyiwa mwenye umri wa miaka 27 alipigwa risasi na kufariki dunia wakati akimtembelea mpenzi wake huko Vosloorus, Ekurhuleni Jumapili usiku. Huyo anakuwa mchezaji wa pili wa kupewa heshima hiyo baada ya jezi namba 22 iliyokuwa ikitumiwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Lesley Manyathela kusimamishwa kwa heshima yake baada ya kufariki kwa ajali ya gari mwaka 2003. Meyiwa alikuwa akitarajiwa kuingoza Pirates katika mchezo wa nusu fainali wa Kombe la Ligi ambao ungewakutanisha na mahasimu wao wa jiji la Soweto Kaizer Chiefs Jumamosi hii lakini umehahirishwa kutokana na kifo hicho. Badala yake Jumamosi hii kutafanyika mazishi ya golikipa huyo nyumbani kwao Umlazi jijini Durban.

HATIMAYE TEVEZ AITWA TENA ARGENTINA.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Juventus, Carlos Tevez ameteuliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Argentina kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka mitatu. Tevez mwenye umri wa miaka 30 ameitwa katika kikosi hicho cha Gerardo Martino kwa ajili ya michezo ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Croatia na Ureno baada ya kuachwa na kocha wa zamani wa timu hiyo Alejandro Sabella toka mwaka 2011 mpka mwaka huu. Mara ya mwisho Tevez kuitumikia nchi yake ilikuwa katika robo fainali ya michuano ya Copa Amerika mwaka 2011 wakati Argentina walipong’olewa katika hatua ya hiyo baada ya golikipa wa Uruguay Fernando Muslera kuzuia penati ya mchezaji huyo. Tevez ameanza msimu wa Serie A kwa kiwango kikubwa akiwa ameifungia Juventus mabao sita na mawili zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Nyota huyo pia amefunga mabao 13 katika mechi 64 alizoitumikia nchiyake kati ya mwaka 2004 mpaka 2011. Argentina inakabiliwa na mchezo dhidi ya Croatia utakaofanyika jijini London, Novemba 12 utakaofuatiwa na mchezo dhidi ya Ureno jijini Manchester siku sita baadae.

ZIDANE AFUNGIWA MIEZI MITATU.

MCHEZAJI nguli wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane amefungiwa miezi mitatu leseni ya ukocha kwa kosa la kufundisha timu bila vyeti vilivyoruhusiwa. Shirikisho la Soka la Ufaransa lilimfungiwa kiungo huyo wa zamani kwa kuingoza timu ya Real Madrid ya Castilla kikiwa ni kikosi cha pili cha timu hiyo. Msaidizi wa Zidane katika timu hiyo Santiago Sanchez naye pia amefungiwa miezi mitatu. Katika taarifa yake klabu hiyo imebainisha kuwa hawatakubaliana na uamuzi huo na wamepanga kukata rufani na kudai kuwa Zidane ana kibali cha Shirikisho la Soka la Ufaransa cha kufanya kazi kama kocha mkuu. Zidane aliteuliwa kuwa kocha wa kikosi cha pili katika majira ya kiangazi baada ya kufanya kazi kama msaidizi wa Carlo Ancelotti msimu uliopita ambao Madrid walinyakuwa taji la 10 la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Zidane amewahi kuichezea Madrid kwa misimu mitano baada ya kujiunga nao akitokea Juventus kwa kitita cha paundi milioni 45 mwaka 2001 ada iliyovunja rekodi kwa wakati huo.

NIGERIA YAKABILIWA NA TISHIO LA KUFUNGIWA MICHUANO YA KIMATAIFA.

NIGERIA inakabiliwa na tishio lingine la kufungiwa michuano ya kimataifa yakiwemo yale ya Mataifa ya Afrika yatakayofanyika mapema mwakani. Hatua inakuja kufuatia uamuzi wa mahakama kuu kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Shirikisho la Soka nchini humo-NFF. Mahakama kuu ya Jos ilifutilia mbali uchanguzi wa Amaju Pinnick kuwa rais wa shirikisho hilo. Hii ni mara ya pili Nigieria kupigwa marufuku kwa sababu ya serikali kuingilia masuala ya shirikisho hilo. Shirikisho la soka Duniani-FIFA limetoa onyo kuwa kuingiliwa kwa masuala ya soka kutasababisha Nigeria kupigwa marufuku hadi Mei mwakani.

Monday, October 27, 2014

BLATTER ATUMA SALAMU ZAKE RAMBIRAMBI KWA NAHODHA WA AFRIKA KUSINI ALIYEUAWA.

RAIS wa Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA, Sepp Blatter ametuma salamu zake za rambirambi kufuatia kifo cha golikipa na nahodha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Senzo Meyiwa. Meyiwa mwenye umri wa miaka 27 alipigwa risasi na kufariki wakati akijaribu kumlinda mpenzi wake Kelly Khumalo wakati walipovamiwa na majambazi nyumbani kwa mwanadada huyo ambayo ni mwanamuziki. Kwa mujibu wa taarifa za polisi nchini nchini humo majambazi hayo yalikuwa yakitaka simu na vitu vya thamani vilivyokuwepo nyumbani kwa Khumalo, na kuongeza kuwa golikipa huyo alifariki mara tu baada ya kufikishwa hospitalini. Katika barua yake kwa rais wa Chama cha Soka cha Afrika Kusini, Danny Jordaan, Blatter alitum salama zake hizo kwa niaba ya jumuiya ya soka ya kimataifa kufuatia kifo hicho cha Meyiwa ambaye pia alikuwa golikipa namba moja wa klabu ya Orlando Pirates. Blatter aliongeza kwa majonzi makubwa Meyiwa atakumbukwa kwa wachezaji wenzake na mashabiki wa klabu na timu ya taifa na kuwataka familia na jamaa wa karibu na subira katika kipindi hiki kigumu. Meyiwa alikuwa akikaa langoni ktika mechi nne za mwisho za Afrika Kusini walizocheza kwa ajili ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani na kufanikiwa kutofungwa bao hata moja katika mechi hizo. Nyota huyo pia aliisaidia timu ya Pirates kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Ligi nchini humo. Kitita cha randi 250,000 sawa na dola 23,000 kimetolewa kwa yeyote atakayetoa taarifa kuhusu majambazi hayo.

POGBA AJIFANANISHA NA YAYA TOURE.

KIUNGO wa klabu ya Juventus, Paul Pogba amefananisha aina ya uchezaji wake nay a nyota wa klabu ya Manchester City Yaya Toure. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa alisaini mkataba mpya na mabingwa hao wa Serie A ambao utamalizika mwaka 2019 Ijumaa iliyopita baada ya kuwa mchezaji muhimu kwa timu hiyo na nchi yake toka alipotua jijini Turin akitokea Manchester United kama mchezaji huru miaka miwili iliyopita. Meneja wa Juventus, Massilimiano Allegri amesema mwishoni mwa wiki kuwa Pogba bado ana kazi kubwa ya kufanya ili aweze kuja kuwa mchezaji bora wa dunia. Akihojiwa na mtandao wa FIFA.com, Pogba amesema anadhani bado kuna wachezaji wengi bora zaidi yake lakini atajitahidi kadri awezavyo ili afikie ubora unaotakiwa. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa kuna wachezaji wengi wa nafasi ya kiungo ambao anawahusudu akimtolea mfano Toure ambaye ana umbo na nguvu sawa kama yeye lakini amezidi uzoefu.

WAENDESHA MASHITAKA KUKATA RUFANI HUKUMU YA PISTORIUS.

WAENDESHA mashitaka nchini Afrika Kusini wamedai kuwa watakata rufani dhidi ya hukumu aliyopewa mwanariadha mlemavu Oscar Pistorius kwa kumuua mpenzi wake. Wiki iliyopita Pistorius alianza kutumikia adhabu yake ya miaka mitano jela aliyopewa kwa kosa kumuua bila kukusudia mpenzi wake Reeva Steenkamp ingawa anaweza kuachiwa katika kipindi cha miezi 10. Msemaji wa waendesha mashitaka hao amesema rufani hiyo itaegemea zaidi kuhoji vipengele vya sheria vilivyotumika kutoa hukumu hiyo. Familia ya mwanariadha huyo wenyewe wamesema hawatakata rufani kupinga adhabu aliyopewa mtoto wao. Pistorius pia alipewa adhabu ya kufungiw kutumia silaha kwa kipindi cha miaka mitatu kwa kufyatua risasi katika mgahawa.

GATTUSO ABADILI MAWAZO YA KUJIUZULU.

KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Italia na klabu ya AC Milan, Gennaro Gattuso ametangaza kujiuzulu na kisha kubadili uamuzi wake huo baadae kuifundisha timu ya OFI Crete inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ugiriki baada ya kuongoza mechi saba pekee. Gattuso mwenye umri wa miaka 36 alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo Juni mwaka huu lakini alitangaza kujiuzulu ghafla kufuatia kipigo walichoapata nyumbani cha mabao 3-2 kutoka kwa Asteras Tripolis. Katika mkutano wake na wanahabari, Gattuso amesema amekuwa akiifanya kazi hiyo kwa mapenzi na nguvu zake zote lakini hawezi kuwa pekee ambaye anapaswa kutatua matatizo ya timu hiyo kwani yeye sio rais na kazi yake inapaswa kuwa soka pekee. Lakini baada ya mazungumzo ya kina na uongozi wa klabu hiyo na jinsi mashabiki walivyomuunga mkono Gattuso aliamua kubadili uamuzi wake. Gattuso ambaye aliichezea Italia mechi 73 na kuisaidia kushinda Kombe la Dunia mwaka 2006 sambamba na kushinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Milan, alichukua nafasi ya Ricardo Sa Pinto kutoka Ureno ambaye aliingoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi msimu uliopita.

ZIDANE NI MFALME WA SOKA - MOURA.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG Lucas Moura amesema nyota wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa Zinedine Zidane ndiye mfalme wa soka. Zidane mwenye umri wa miaka 42 amewahi kushinda Kombe la Dunia, michuano ya Ulaya, mataji mawili ya Serie A akiwa na Juventus na taji moja la ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Madrid huku pia akitunukiwa tuzo ya Ballon d’Or mwaka 1998. Winga huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 22 amesema kupata nafasi ya kukutana na Zidane ililikuwa kama ndoto kwake kwani ndiye anayemhusudu sana toka akiwa mdogo. Moura amesema kwake Zidane ndiye mfalme wa soka na siku zote amekuwa akitamani kufikia mafanikio yake.

MOURINHO ALIA NA MWAMUZI MECHI YAO NA MAN UNITED.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho anadhani baadhi ya maamuzi yalikwenda kinyume kwa timu kwa timu yake wakati Manchester United walipofanikiwa kusawazisha katika mwisho na kupata sare katika mchezo baina ya timu hizo uliochezwa Old Trafford. Chelsea walianza kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Didier Drogba kabla ya Robin van Persie hajasawazisha katika dakika za majeruhi baada ya Branislav Ivanovic kutolewa kwa kadi nyekundu. Akihojiwa Mourinho amesema aliona kadi hiyo ikimnyemelea beki wake huo lakini akaongeza kuwa kama atataka kuongelea kuhusu hilo lazima azungumzie penati ya Ivanovic ambayo hakupewa. Chelsea sasa inakabiliwa na adhabu ya faini ya paundi 25,000 kwa wachezaji wake kupata kadi za njano zaidi ya sita katika mchezo mmoja. United wao walishawahi kuadhibiwa kwa kosa kama hilo mwaka 2008 kwa kupata kadi za njano saba katika mchezo baina ya timu hizo katika Uwanja wa Stamford Bridge.

VIJEBA VYAIPONZA GHANA U-17.

TIMU ya taifa ya Ghana ya vijana chini ya umri wa miaka 17 imeondolewa katika michuano ya vijana wa umri huo mwakani kwasababu ya kudanganya umri. Timu hiyo inayojulikana kama Black Starlets iliitandika Cameroon katika mechi zao mbili za kufuzu michuano hiyo itakayochezwa Niger lakini nchi hiyo iliituhumu Ghana kwa kudanganya umri kwa baadhi ya wachezaji wake. Chama cha Soka cha Ghana-GFA kimethibitisha kupata barua kutoka Shirikisho la Soka la Afrika-CAF ya kuenguliwa baada ya kuthibitika kuwa tuhuma hizo za kudanganya umri zilikuwa za kweli. Cameroon walipeleka malalamiko yao dhidi ya wachezaji saba wa Ghana baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wao mkondo wa kwanza. Kamati ya kitabibu ya CAF ilitoa taarifa ya uchunguzi wake kuhusu tuhuma hizo kuwa kuthibitisha kuwa ni kweli wachezaji hao walizidi umri lakini Ghana wenyewe wamesema watapinga uamuzi huo.

LENGO LA MILAN NI KUCHEZA LIGI YA MABINGWA ULAYA MSIMU UJAO - DE JONG.

MCHEZAJI nyota wa AC Milan, Nigel de Jong amesisitiza kuwa suala la kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya bado lipo katika malengo yao kufuatia kung’ang’aniwa sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Fiorentina jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi aliifungia Milan bao la kuongoza kabl ya mapumziko lakini Josip Ilicic alivuruga sherehe yao kwa kusawazisha bao hilo katika kipindi cha pili. De Jong amesema Fiorentina walipata nafasi moja lakinib aliitumia vyema ila kwa upande walionekana kuchoka ndio maana wakaambulia alama hiyo moja. De Jong aliendelea kudai kuwa pamoja na hayo bado hawajakata tamaa katika kuhakikisha wanamaliza katika nafasi tatu za juu ambazo zitawapa tiketi ya kushiriki michuano hiyo mwakani. Kwasasa Milan wako katika nafasi ya sita katika msimamo wa Serie A wakiwa na alama 15 katika mechi nane walizocheza.

FAINALI YA KWANZA LIGI YA MABINGWA YAMALIZIKA KWA SARE.

MECHI ya mkondo wa kwanza ya fainali ya michuano ya Klabu ya Afrika baina ya timu za Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC na Entente Setif ya Algeria imechezwa jana kwa timu hizo kutoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2 jijini Kinshasa. Katika mchezo huo uliochezwa katika uwanja marufu wa Tata Raphael wageni Setif ndio walionza kufunga bao la kuongoza katika dakik ya 17 kupitia kwa Ndombe Mubele kabla ya bao hilon kusawazishwa na Chikito Lema Mabidi na kupelekea timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare. Katika kipindi cha pili Setif walicharuka tena na kupata bao katika dakika ya 58 kupitia kwa Akram Djahnit lakini Mabidi aliisawazishia Vita tena kwa shuti la umbali wa mita 30. Uwanja huo wa Tata Raphael ni maarufu kwani uliwahi kuchezwa kwa pambano la ngumi maarufu duniani lililopewa jina la Rumble ni the Jungle miaka 40 kati ya Mohammad Ali na George Foreman wote wa Marekani. Mubele sasa anaongoza katika orodha ya wafungaji katika michuano hiyo akiwa amefikisha mabao sita kuelekea mchezo wao marudiano utakaochezwa nchini Algeria, Novemba mosi mwaka huu. Mshindi katika fainali hiyo atajinyakulia kitita cha dola milioni 1.5 na nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la Vilabu nchini Morocco Desemba mwaka huu.

Friday, October 24, 2014

KAMA KAWAIDA YAKE, BALOTELLI MATATANI TENA.

POLISI wanachunguza madai kuwa mshambuliaji nyota wa Liverpool, Mario Balotelli wamemtishia mwanamke ambaye alikuwa akipiga picha gari lake la kifahari aina ya Ferrari. Inadaiwa mwanamke anamtuhumu nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kumfuata binti yake ambaye alikuwa akilipiga picha gari hilo lililokuwa limeegeshwa pembeni. Polisi wa Manchester wamedai kupokea taarifa ya tishio na wanafanya uchunguzi kwa kuwahoji watu mbalimbali ambao walikuwa karibu na eneo hilo. Balotelli ameendelea kuandamwa na matukio baada ya juzi kupokea onyo kutoka katika kllabu yake kwa kubadilishana shati na beki wa Real Madrid Pepe wakati timu yake ikiwa nyumba kwa mabao 3-0 katyika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliofanyika katika Uwanja wa Anfield.

VAN GAAL AMPA SHAVU VALDES.

KLABU ya Manchester United imetangaza kuwa golikipa wa zamani wa klabu ya Barcelona, Victor Valdes anatarajiwa kuanza kufanya nao mazoezi. Valdes mwenye umri wa miaka 32 ambaye aliondoka Barcelona mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuitumikia timu hiyo katika kipindi chake chote kwasasa bado anapona majeruhi ambayo yalisababisha kushindwa kujiunga na Monaco ya Ufaransa. Golikipa huyo ambaye amecheza mechi 20 za kimataifa akiwa na Hispania aliumia goti lake la kulia Machi mwaka huu na kfanyiwa upasuaji ambao ulimuweka nje kwa msimu uliobakia pamoja na Kombe la Dunia. 
Valdes akiwa na Van Gaal mwaka 2002 katika mazoezi ya Barcelona.
Meneja wa United, Louis van Gaal amempa ofa Valdes nafasi ya kufanya mazoezi na kuhakikisha anapona kabisa goti lake katika timu hiyo. Katika taarifa ya klabu hiyo imedai kuwa Valdes ambaye ni mchezaji huru atakuwa akifanya mazoezi chini ya uangalizi wa madaktari wa United ili kuhakikisha anapona kabisa. Van Gaal ndiye aliyempa nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza Valdes wakati akiwa na umri wa miaka 20 mwaka 2002 lakini alikaa naye kwa kipindi cha miezi sita kabla ya kocha huyo hajaondoka Barcelona.

VILABU ULAYA VYAITAKA FIFA KUKUBALI KOMBE LA DUNIA 2022 KUCHEZWA MEI.

VILABU vikubwa barani Ulaya vinatarajia kulitaka Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kucheza michuano ya Kombe la Duniani mwaka 2022 nchini Qatar katika kipindi cha mwezi Mei. Qatar ilishinda haki za kuandaa michuano hiyo mwaka 2010 lakini mjadala wa kuhamisha michuano hiyo kutoka katika majira ya kiangazi kama ilivyozoeleka umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya mwaka. Chama cha Vilabu Ulaya-ECA ambacho kinajumuisha klabu za Manchester United, Liverpool, Barcelona na Bayern Munich vimejadili kuwa kipindi cha mwezi Mei mwaka 2022 kitakuwa muafaka kwa michuano hiyo. ECA wanaamini michuano hiyo kuchezwa katika kipindi cha majira ya machipuko kitasaidia kupunguza hatari iliyopo ya kucheza katika joto kali. Maswali yaliibuka haraka baada ya Qatar kupata haki ya kuandaa michuano hiyo kuhusu uwezekano wake kutokana na joto kali lililopo katika nchi hiyo ya jangwa katika kipindi June na Julai ambacho ndio Kombe la Dunia huchezwa. Ila mara zote Qatar wenyewe wamekuwa wakisisitiza wanaweza kuandaa michuano hiyo kiangazi kwa kutumia mpango wao wa vipoza hewa ili kupunguza joto nmdani ya viwanja na sehemu ambazo zitakuwa zimetengwa kwa ajili ya mashabiki.

SUAREZ KUANZA KUITUMIKIA BARCELONA KWA MARA YA KWANZA KATIKA EL CLASICO KESHO.

MSHAMBULIAJI nyota Luis Suarez anatarajiwa kuanza kuitumikia Barcelona kwa mara ya kwanza wakati vinara hao wa La Liga wataposafiri kuifuata Real Madrid katika mchezo wa kwanza wa el Clasico utakaochezwa kesho. Suarez alikuwa ameruhusiwa kucheza baadhi ya mechi za kirafiki kwa klabu ya nchi yake toka aliposajiliwa kwa kitita cha paundi milioni 75 akitokea Liverpool baada ya kufungiwa miezi minne kwa kosa la kumng’ata beki wa Italia Giorgio Chiellini katika Kombe la Dunia Juni mwaka huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay, anatarajiwa kucheza mechi yake hiyo ya kwanza katika Uwanja wa Santiago Bernabeu akiwa sambamba na Neymar na Lionel Messi. Ujio wa Suarez unaweza kufunikwa na Messi ambaye amebakisha bao moja kuifikia rekodi ya mabao 251 katika La Liga iliyowekwa na Telmo Zarra aliyechezea Atletico Bilbao kati ya mwaka 1940 mpaka 1955. Kiungo wa Barcelona, Andres Iniesta ana matumaini wachezaji wote hao wawili yaani Messi na Suarez wanatang’ara katika mchezo huo ili kuendeleza rekodi yao nzuri ya kushinda Bernabeu ambapo mpaka sasa wameshashinda mechi nne kati ya sita walizokutana katika uwanja huo.

PIRES ARIPOTIWA KUPIGWA NA KOCHA WA TIMU PINZANI INDIA.

MCHEZAJI mkongwe wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Robert Pires ameripotiwa kung’atwa na kupigwa usoni na kocha wa timu pinzani wakati wa muda wa mapumziko katika mchezo wa Ligi Kuu nchini India-ISL. Nguli wa zamani wa soka wa Brazil ambaye kwasasa anainoa klabu ya Fc Goa, Zico amedai kuwa Pires alimuambia kuwa alipigwa na kocha wa timu ya Atletico de Kolkata Antonio Lopez Habas wakati timu zikielekea katika vyumba vya kupumzikia baada ya kipindi cha kwanza kumalizika. ISL imekiri leo kupata taarifa hizo kutoka kwa timu zote mbili na kuwa wanazifanyia kazi ili kujua ukweli kuhusiana na hilo. Mmiliki mwenza wa Kolkata Utsay Parekh amesema hakuna yeyote aliyekuwepo wakati tukio hilo likitokea ndio maana waliiandikia ISL kuchunguza ili kubaini ukweli. Parekh aliendelea kudai kuwa kamera za CCTV zilikuwepo hivyo hadhani kama kutakuwa na ugumu wowote katika kutafuta ukweli. Katika mchezo huo Kolkata iliitandika FC Goa kwa mabao 2-1 hivyo kuendelea kuongoza ligi hiyo kujikusanyia alama 10 katika michezo minne waliyocheza mpaka sasa.

WACHEZAJI WA BAYERN WATEMBELEA KITUO CHA WAKIMBIZI.

WACHEZAJI wa klabu ya Bayern Munich, wametembelea kituo cha wakimbizi kilichopo kaskazini mwa Ujerumani katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo inakabiliwa na ongezeko la watu wengi wanaohitaji msaada. Wachezaji hao akiwemo Bastian Schweinsteiger na Holger Badstuber walitembelea kituo hicho ambacho kina mayatima 250 ambao hawana wazazi wala ndugu juzi baada ya timu hiyo kurejea kutoka Roma ambako pia walimtembelea Papa Francis huko Vatican. Rais wa klabu hiyo Karl-Heinz Rummenigge aliyeongoza ujumbe huo na kutoa msaada wa nguo na vifaa vya michezo amesema watoto hao hawana chopchote zaidi ya nguo walizovaa hivyo anadhani wana jukumu la kuwasaidia wao na wengine. Mwaka huu Ujerumani inategemea zaidi watu 200,000 wanaotafuta makazi katika mipaka yake kuzunguka nchi ikiwa ni ongezeko la asilimia 60 kulinganisha na mwaka jana. Makazi mapya ya wakimbizi yametengenezwa kuzunguka nchi ikiwemo kambi za zamani za jeshi na shule ili kuweza kukabiliana na ongezeko hilo la wakimbizi wengi wao wakiwa wametoka katika nchi za Syria na Iraq.

ENYEAMA ATAKA CAF KUSITISHA AFCON.

GOLIKIPA na nahodha wa timu ya taifa ya Nigeria maarufu kama Super Eagles, Vincent Enyeama amelitaka Shirikisho la Soka la Afrika-CAF kusitisha michuano ya Mataifa ya Afrika-AFCON inayotarajiwa kufanyika Januari mwakani. Enyeama ambaye anakipiga katika klabu ya Lille amefafanua kuwa michuano hiyo inapaswa kusitishwa kutokana na wasiwasi juu ya ugonjwa wa Ebola kuongezeka. Golikipa huyo mwenye umri wa miaka 32 ameeleza woga wake kuwa ugonjwa huo ambao umeshaua zaidi ya watu 4,500 mpaka sasa utasambaa zaidi kufuatia mkusanyiko wa watu watakaokuwepo viwanjani. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa hatari ni kubwa kama AFCON itaandaliwa wakati huu ambapo bado ugonjwa huo haujadhibitiwa lakini amesema atashiriki kama nchi yake itafuzu michuano hiyo pamoja na hatari iliyopo.

ROGER MILLA AISHANGAA MOROCCO KUSITA KUANDAA AFCON.

NGULI wa soka wa zamani wa Cameroon, Roger Milla amekosoa ombi la Morocco la kuahirisha michuano ya Mataifa ya Afrika-AFCON kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia Januari 17 mwakani lakini Morocco wametaka kusogezwa mbele wakati serikali na taasisi za kiafya duniani kote wakihangaika kuzuia virusi hivyo kusambaa zaidi. Maofisa wa afya wa Morocco wameonya kuwa maelfu ya watu wanaotarajiwa kuhudhuria michuano hiyo ya wiki tatu wanaweza kuleta maambukizi ya ogonjwa huo katika nchi hiyo iliyopo kaskazini mwa bara la Afrika. Hata hivyo, Milla amesema anadhani Morocco wanajaribu kuficha ukweli halisi kuwa hawataki kuwa wenyeji wa michuano hiyo kwa kisingizio cha Ebola. Milla ambaye alikuwa shujaa wa Cameroon mwaka 1990 kwa kufunga bao akiwa na umri mkubwa zaidi wa miaka 40, aliendelea kudai kuwa amekuwa akifuatilia na kwa maoni yake anaona Morocco hawahofii Ebola bali wana ajenda yao ya siri ambayo hawataki kuiweka wazi. Nguli aliendelea kudai kuwa mpango wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF kutaka kuipeleka michuano hiyo mahali pengine hadhani kama wanatatua tatizo bali wanalihamisha. CAF inatarajiwa kukutana na maofisa wa Shirikisho la Soka la Morocco Novemba 2 jijini Algiers ili kuzungumzia suala hilo.

SERBIA YAPEWA USHINDI WA MEZANI NA UEFA.

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limeipa ushindi Serbia wa mabao 3-0 dhidi ya Albania baada ya mchezo wa kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016 uliofanyika jijini Belgrade kusitishwa kabla ya muda. Lakini pamoja na kupewa ushindi huo, Serbia wamekatwa alama tatu baada ya mchezo huo uliofanyika Octoba 14 mwaka huu kuvunjika wakati ndege isiyokuwa na rubani ilipopita uwanjani huku ikipeperusha bendera iliyokuwa na ujumbe wa kisiasa. Ndege hiyo isiyokuwa na rubani na bendera ilisababisha vurugu kwa mashabiki na rabsha baina ya wachezaji katika Uwanja wa Partizan. Mbali na adhabu hiyo Serbia pia watalazimika kucheza mechi zao mbili za nyumbani bila mashabiki huku vyama vyote vya soka Serbia na Albania vikitozwa faini ya euro 100,000. Nchi zote zimepewa nafasi ya kukata rufani kama hawataridhika na adhabu walizopewa. Serbia sasa wanatarajiwa kucheza mechi zake za kundi I dhidi ya Denmark na Armenia bila mashabiki.

SITAWEZA KUIFUNDISHA BARCELONA - ANCELOTTI.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti amedai kuwa anaheshimu uhasimu uliopo hivyo hawezi kwenda kuifundisha Barcelona badala yake atastaafu akiwa na hapohapo Santiago Bernabeu. Ni makocha wawili pekee ambao ni Radomir Antic na Enrique Fernandez ambao waliwahi kuzifundisha timu zote hizo mbili kwa nyakati tofauti katika kipindi cha nyuma. Ancelotti ambaye amewahi pia kuzinoa klabu za AC Milan ya Italia na Chelsea ya Uingereza, amesisitiza kuwa kuchukua mikoba ya kuinoa Barcelona ni jambo analiona halitawezekana. Akihojiwa kocha huyo amesema sasa anaifundisha Madrid na kamwe hataweza kuifundisha Barcelona kwasababu anaheshimu historia yake pamoja na historia ya vilabu hivyo. Akiulizwa kama angependa kukaa kwa muda mrefu Madrid kama ilivyokuwa kwa Sir Alex Ferguson katika klabu ya Manchester United, Ancelotti amesema hadhani kama itawezekana kukaa zaidi ya miaka 24 lakini angependa kustaafu akiwa hapo. Madrid wanatofautiana alama nne na Barcelona ambao ndio vinara wa la Liga kuelekea katika mchezo wao huo wa tisa kwa msimu huu.

KAMA ULI-MISS BAO TAMU LA MSIMU LILILOFUNGWA NA ERIK LAMELA WAKATI TOTTENHAM IKIIBUGIZA ASTERA MABAO 5-1 KATIKA EUROPA LEAGUE.

Thursday, October 23, 2014

HALI YA SCHUMACHER INATIA MATUMAINI - DAKTARI.

DAKTARI ambaye alikuwa akimtibu Michael Schumacher kwa karibu miezi sita baada ya kupata majeraha ya kichwani katika ajali ya kuteleza katika barafu amesema bingwa huyo wa zamani wa mashindano langalanga anaendelea vyema. Lakini Jean-Francois Payen ambaye ni daktari katika hospitali ya Grenoble ya Ufaransa ambayo Schumacher alitibiwa ameonya kuwa hali yake inaweza kuchukua muda mrefu kidogo wa kati ya mwaka mmoja mpaka mitatu. Schumacher mwenye umri wa miaka 45 alikuwa akiteleza katika barafu katika milima ya Ufaransa Desemba mwaka jana wakati alipoanguka na kugonga kichwa katika jiwe. Dereva huyo huyo bingwa wa langalanga kutoka Ujerumani aliwekwa katika hali ya kutojitambua ili kumsaidia ubongo wake kupona taratibu wakati akipatiwa matibabu Grenoble na baadae kuhamishiwa Lausanne, Switzerland. Schumacher sasa ameshaondolewa hali ya kutojitambua na amekuwa akipata uangalizi wa karibu nyumbani kwake ambapo Profesa Payen amekuwa akimtembelea kufuatilia maendeleo yake.