MSHAMBULIAJI nyota Luis Suarez anatarajiwa kuanza kuitumikia Barcelona kwa mara ya kwanza wakati vinara hao wa La Liga wataposafiri kuifuata Real Madrid katika mchezo wa kwanza wa el Clasico utakaochezwa kesho. Suarez alikuwa ameruhusiwa kucheza baadhi ya mechi za kirafiki kwa klabu ya nchi yake toka aliposajiliwa kwa kitita cha paundi milioni 75 akitokea Liverpool baada ya kufungiwa miezi minne kwa kosa la kumng’ata beki wa Italia Giorgio Chiellini katika Kombe la Dunia Juni mwaka huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay, anatarajiwa kucheza mechi yake hiyo ya kwanza katika Uwanja wa Santiago Bernabeu akiwa sambamba na Neymar na Lionel Messi. Ujio wa Suarez unaweza kufunikwa na Messi ambaye amebakisha bao moja kuifikia rekodi ya mabao 251 katika La Liga iliyowekwa na Telmo Zarra aliyechezea Atletico Bilbao kati ya mwaka 1940 mpaka 1955. Kiungo wa Barcelona, Andres Iniesta ana matumaini wachezaji wote hao wawili yaani Messi na Suarez wanatang’ara katika mchezo huo ili kuendeleza rekodi yao nzuri ya kushinda Bernabeu ambapo mpaka sasa wameshashinda mechi nne kati ya sita walizokutana katika uwanja huo.
No comments:
Post a Comment