Friday, October 24, 2014

PIRES ARIPOTIWA KUPIGWA NA KOCHA WA TIMU PINZANI INDIA.

MCHEZAJI mkongwe wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Robert Pires ameripotiwa kung’atwa na kupigwa usoni na kocha wa timu pinzani wakati wa muda wa mapumziko katika mchezo wa Ligi Kuu nchini India-ISL. Nguli wa zamani wa soka wa Brazil ambaye kwasasa anainoa klabu ya Fc Goa, Zico amedai kuwa Pires alimuambia kuwa alipigwa na kocha wa timu ya Atletico de Kolkata Antonio Lopez Habas wakati timu zikielekea katika vyumba vya kupumzikia baada ya kipindi cha kwanza kumalizika. ISL imekiri leo kupata taarifa hizo kutoka kwa timu zote mbili na kuwa wanazifanyia kazi ili kujua ukweli kuhusiana na hilo. Mmiliki mwenza wa Kolkata Utsay Parekh amesema hakuna yeyote aliyekuwepo wakati tukio hilo likitokea ndio maana waliiandikia ISL kuchunguza ili kubaini ukweli. Parekh aliendelea kudai kuwa kamera za CCTV zilikuwepo hivyo hadhani kama kutakuwa na ugumu wowote katika kutafuta ukweli. Katika mchezo huo Kolkata iliitandika FC Goa kwa mabao 2-1 hivyo kuendelea kuongoza ligi hiyo kujikusanyia alama 10 katika michezo minne waliyocheza mpaka sasa.

No comments:

Post a Comment