Friday, August 29, 2014

RONALDO AMTABIRIA MAFANIKIO DI MARIA AKIWA UNITED.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo, amemtabiria mafanikio mchezaji mwenzake wa zamani Angel Di Maria katika klabu yake mpya ya Manchester United. Nyota huyo wa kimataifa wa argentina alifanikiwa kukamilisha usajili uliovunja rekodi nchini Uingereza Jumanne iliyopita baada ya kushindwa kufiti katika kikosi cha Carlo Ancelotti huku akipewa jezi namba saba ambayo imewahi kutimiwa na Ronaldo wakati akiwa United. Ronaldo ambaye alicheza misimu sita na United, anaamini kuwa uhamisho huo ndio Di Maria aliokuwa akihitaji na ana uhakika nyota huyo anaweza kuisaidia timu hiyo kubadili mwelekeo baada ya kuanza vibaya msimu mpya wa Ligi Kuu. Akihojiwa Ronaldo ambaye jana ametunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Ulaya katika sherehe zilizofanyika jijini Monaco, amesema Di Maria kwenda United ni jambo ambalo litamsaidia kwani anaamini amekwenda katika moja ya klabu bora duniani hivyo anamtakia mafanikio akiwa huko. Ronaldo aliendelea kudai kuwa amezungumza naye na kumwambia kuwa jezi namba aliyopewa ina majukumu makubwa lakini anadhani ataitendea haki jezi hiyo kwani ni mchezaji mahiri.

Thursday, August 28, 2014

RATIBA YA UEFA CHAMPIONS LEAGUE.


ROONEY NAHODHA MPYA UINGEREZA.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Manchester United, Wayne Rooney ametajwa kuwa nahodha mpya wa timu ya taifa ya Uingereza na kocha Roy Hodgson. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 amechukua beji hiyo kutoka kwa kiungo wa Liverpool Steven Gerrard ambaye alistaafu rasmi soka la kimataifa baada ya nchi hiyo kutolewa katika michuano ya Kombe la Dunia. Rooney amefunga mabao 40 katika mechi 95 za kimataifa na alitajwa kuwa nahodha wa United na kocha Louis van Gaal mapema mwezi huu. Rooney alithibitisha uteuzi huo katika mtandao wake na kudai kuwa ataitumikia nafasi hiyo kwa bidii na kujivunia huku akidai kuwa zilikuwa ndoto zake za muda mrefu. Rooney ataanza kuvaa beji rasmi akiwa na timu ya taifa Septemba 3 mwaka huu wakati Uingereza watakapoikaribisha Norway katika Uwanja wa Wembley kwa ajili ya mchezao wa kirafiki wa kimataifa.

MISRI YAJITOSA KINYANG'ANYIRO CHA AFCON.

CHAMA cha Soka nchini Misri nacho kimejitosa katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon mwaka 2017 baada ya kuandaa michuano hiyo mwaka 2006. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Libya viwalazimisha kujitoa katika mipango ya kujenga viwanja hatua ambayo imelilazimu Shirikisho la Soka Barani Afrika-CAF kutafuta mwenyeji mwingine wa michuano hiyo. Chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya EFA kimebainisha nia ya kutaka kuwa mwenyeji wa michuano hiyo lakini bado hawajafanya uamuzi wa mwisho kuhusiana na suala hilo. Makamu wa rais wa EFA Hassan Farid naye alithibitisha nia yao hiyo lakini amesema bado wanataka kuzungumza na baadhi ya wizara serikalini ili kupata ushirikiano wao. Misri ni mojawpao ya nchi chake barani Afrika zenye miundo mbinu mizuri ya kuandaa michuano mikubwa kama Afcon.

SANCHEZ ATATISHA ZAIDI - WENGER.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesema kiwango cha Alexis Sanchez alichoonyesha katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Besiktas imeinyesha kuwa ana ubora wa kumfanya afanikiwe katika Ligi Kuu nchini Uingereza. Nyota huo aliyesajiliwa kwa paundi milioni 35 akitokea Barcelona alifunga bao pekee katika mchezo huo na kuipa Arsenal ushindi mwembamba wa 1-0 katika Uwanja wa Emirates na kuwafanya kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo. Akihojiwa Wenger amesema Sanchez alionyesha mchezo mzuri kwani alikuwa akielewana vyema na wenzake na alikuwa akionyesha ari ya kupambana huku akiwa hatari anapokuwa katika lango la adui. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa ubora huo ndio unaotakiwa katika ligi. Bao hilo la kwanza kwa mchezaji huyo toka ajiunge na timu hiyo alilifunga muda mchache kabla ya mapumziko na kuingiza Arsenal katika ratiba ya makundi yaliyopangwa leo. Hata hivyo Wenger amekiri kuwa aliingiwa na woga kidogo wakati beki wake Mathieu Debuchy alipotolewa nje kwa baada ya kupewa kadi ya pili ya njano zikiwa zimebaki dakika 14 mpira kumalizika.

SFAXIEN YATAKA MCHEZO WAO WA DRC DHIDI YA VITA URUDIWE.

SHIRIKISHO la Soka la Tunisia-TFT, limetuma barua Shirikisho la Soka la Afrika-CAF kuwataka kuhamisha mchezo wao wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya klabu ya CS Sfaxien na AS Vita nje ya nchi ya jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC. Sfaxien walifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kumaliza kama vinara wa kundi B wakati klabu ya Vita wao walimaliza katika nafasi ya pili katika kundi A. Ofisa mkuu wa TFT Shafiq Jarraya amesema wamefikia uamuzi huo wa kuiomba CAF kuhamisha mchezo huo baada ya taarifa za kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa Ebola nchini humo. Jarraya amesema wana matumaini makubwa CAF watakubali maombi yao kwasababu timu itakuwa katika hatari ikienda huko.

BAYERN YANASA BEKI KUTOKA ROMA.

KLABU ya Bayern Munich imefanikiwa kumsajili beki wa kimataifa wa Morocco Mahdi Benatia kutoka klabu ya AS Roma ya Italia kwa ada ambayo haikuwekwa wazi. Beki huyo mwenye umri wa miaka 27 ambaye aliisaidia Roma kumaliza katika nafasi ya pili katika Serie A msimu uliopita alikuwa akihusishwa pia na tetesi za kutakiwa katika vilabu vua Chelsea na Manchester United. Bayern walikuwa wanatafuta beki baada ya nyota wa kimataifa wa Hispania Javi Hernandez kupata majeraha ya goti yatakayomuweka nje uwanjani mpaka mwakani. Roma tayari wameziba nafasi Benatia kwa kusajili beki wa klabu ya Olympiakos Kostas Manolas.

PUTIN AZINDUA UWANJA UTAKAOTUMIKA KATIKA YA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA 2018.

RAIS wa Urusi Vladimir Putin jana amefungua uwanja mpya wa Otkrytie uliopo jijini Moscow ambao utatumika kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018. Uwanja huo uliopo kaskazini-magharibi mwa mji mkuu huo, utakuwa ukitumiwa na klabu maarufu ya Spartak Moscow huku ukitarajiwa kutumika kwa baadhi ya mechi katika michuano hiyo. Putin alitua katika uwanja huo kwa helikopta akiwa ameongozana na waziri wa michezo wa Urusi Vitaly Mutko, meya wa jiji la Moscow Sergey Sabyanin na mmiliki wa Spartak ambaye ndiye aliyetoa fedha za ujenzi huo Leonid Fedun. Rais huyo alitembezwa sehemu mbalimbali za uwanja huo ambao kwasasa una uwezo wa kuingiza watazamaji 42,000 huku pia akikutana na wachezaji wakongwe pamoja na chipukizi wa Spartak. Uwanja huo uliochukua miaka saba kutengenezwa umegharimu kiasi cha dola milioni 415 huku pia ukiwa na uwezekano wa kuongezeka na kufikia uweo wa kuingiza watu 45,000.

FA WANA UHAKIKA WA WEMBLEY KUPATA NAFASI YA KUANDAA FAINALI YA EURO 2020.

CHAMA cha Soka nchini Uingereza, FA kina uhakika kuwa Uwanja wa Wembley una nafasi kuandaa fainali ya michuano ya Ulaya 2020 na pia hawajatoa uwezekano wa kuandaa michuano hiyo mwaka 2028. Katibu Mkuu wa FA Alex horne ana matumaini uwanja huo wa taifa wa Uingereza unaweza kuandaa mchezo wa nusu fainali na fainali katika kipindi cha miaka sita ijayo. Uwanja wa Allianz Arena uliopo jijini Munich ndio uwanja mwingine pekee unaogombani nafasi hiyo na Hornes anafikiri nafasi yao inaongezeka kutokana na Ujerumani kutilia mkazo nafasi yao ya kuandaa michuano ya Ulaya mwaka 2024. Michuano ya Ulaya mwaka 2020 itaandaliwa katika miji 13 tofauti huku mchezo wa fainali na nusu fainali ukiandaliwa katika uwanja mmoja huku miji iliyoshinda kupata nafasi hiyo ikitarajiwa kutangazwa Septemba 19 mwaka huu. Mara ya mwisho Uingereza kuandaa michuano mikubwa ya soka ilikuwa ni mwaka 1996 walipoandaa michuano ya Ulaya huku pia wakiwa wamewahi kuandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1966.

BAYERN NI BORA KULIKO CHELSEA NA MADRID - ROOBEN.

WINGA wa klabu ya Bayern Munich, Arjen Rooben amesisitiza kuwa klabu yake hiyo ni bora kuliko vikosi alivyowahi kucheza katika vilabu vya Real Madrid na Chelsea. Nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi aliwahi kuvaa jezi za Chelsea kati ya mwaka 2004 na 2007 kabla ya kuondoka na kwenda Santiago Bernabeu na baadae kutua Bayern kipindi cha kiangazi mwaka 2009. Robben amesema hajutii uamuzi wake wa kujiunga na mabingwa hao wa Bundesliga kwani anaamini ndio klabu bora aliyoitumikia katika maisha yake ya soka. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 aliendelea kudai kuwa toka ametua katika timu hiyo kiwango kimekuwa kikipanda huku akiamini mambo yataendelea kumnyookea katika siku zijazo pia.

PLATINI AMGWAYA BLATTER, ABAINISHA KUWA HATAGOMBEA URAIS FIFA KATIKA UCHAGUZI WA MWAKANI.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA, Michel Platini amebainisha kuwa hana mpango wa kugombea nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwani anataka kutilia mkazo kibarua chake cha sasa kuliko kushindana na Sepp Blatter katika uchaguzi ujao. Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa alikuwa akiaminika kuwa anafikiria kugombea nafasi nhiyo lakini alifafanua katika mkutano wa vyama 54 vya soka barani Ulaya uliofanyika huko Monte Carlo kuwa atabakia katika nafasi yake hiyo. Mjumbe wa kamati ya utendaji ya FIFA, Michel D’Hooge alikaririwa akidai kuwa ni ujumbe chanya uliotolewa na Platini na amefurahi kwani inamaanisha kuwa safari hii hakutakuwa na ushindani kati FIFA na UEFA. Platini amekuwa akimkosoa vikali Blatter kwa zaidi ya mara moja na mapema mwaka huu alieleza kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 78 amekwisha kama mtu sahihi wa kuiongoza FIFA. Blatter aliwahi kudai kuwa ataachia ngazi mwishoni mwa muhula wake huu wa nne lakini alibadili mawazo na uamuzi wake baadae na kuweka wazi kuwa atatetea tena kiti chake katika uchaguzi ujao. Blatter amekuwa akifanya kazi FIFA toka mwaka 1975 na alichaguliwa kwa mara ya kwanza kushika nafasi ya urais mwaka 1998.

BAYERN YATHIBITISHA KUMNASA XABI ALONSO.

KLABU ya Bayern Munich imetangaza kufikia makubaliano na Real Madrid juu ya uhamisho wa Xabi Alonso kwa ada ambayo haikuwekwa wazi huku nyota huyo wa kimataifa wa Hispania akisafiri leo kwenda Ujerumani kwa ajili vipimo vya afya. Mabingwa hao wa Bundesliga wamepania kuimarisha safu yao ya kiungo kwa kuongeza kiungo katika kikosi chao kutokana na majeruhi yaliyowaandama wachezaji wake kama Javi Martinez, Bastian Scheinsteiger na Thiago Alcantara. Mjumbe wa bodi wa Bayern Jan-Christian Dreesen alithibitisha kuwa ni kweli wamefanya mazungumzo na Madrid pamoja na Alonso na tayari wameshafikia makubaliano kilichoabaki ni vipimo vya afya. Alonso alisaini mkataba mpya na Madrid unaomalizika mwaka 2016 mwapema mwaka huu lakini amepoteza namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo huku kocha Carlo Ancelotti akipendelea kuwatumia zaidi viungo Luka Modric, Tony Kroos na James Rodriguez. Kiungo huyo ambaye ametangaza kustaafu soka la kimataifa wiki hiialianza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Real Sociedad na pia amewahi kuzicheza Eibar na Liverpool kabla ya kujiunga na Madrid katika majira ya kiangazi mwaka 2009.

REAL MADRID HAWAKUMPA HESHIMA ILIYOSTAHILI MWANANGU - BABA.

BABA yake winga mahiri Angel Di Maria ameiponda Real Madrid kufuatia uhamisho wa nyota huyo wa kimataifa wa Argentina kwenda Manchester United na kucheza pendekezo la mwabingwa hao wa Ulaya kumpa ofa mwanae ya kumlipa euro milioni 6 kwa mwaka. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 aliondoka Madrid kwa dili lililogharimu euro milioni milioni 75 mapema wiki hii baada ya kukataa ofa ya kuongeza mnkataba Santiago Bernabeu ambao ungegharimu kiasi hicho kilichoripotiwa. Hata hivyo mzee huyo Miguel Di Maria amesisitiza kuwa mwanae alikuwa anadhani hathaminiki kitu ambacho amedai ndio kilichochangia kuongezswa euro milioni 1.5 katika mshahara wake. Baba yake Di Maria aliendelea kudai kuwa mwanae alikuwa amechoka kuonyesha thamani yake kwani ni jambo amekuwa akilifanya kwa kipindi kirefu lakini hakupata heshima aliyostahili. Kwasasa Di Maria anafuraha United na wanamhudumia vizuri huku mshahara wake ukizidi ule ambao angepewa na Madrid. Usajili wa Di Maria unakuwa wan ne uliotumia fedha nyingi baada ya kuwasajili pia Ander Herrera, Luke Shaw na Marcos Rojo.

Wednesday, August 27, 2014

BAADA YA DI MARIA SASA MAN UNITED WAAMUA KUKOMAA NA VIDAL.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, Louis van Gaal na ofisa mkuu Ed Woodward sasa wamehamishia nguvu zao kumuwinda Arturo Vidal baada ya kumaliza kusajili Angel Di Maria jana. United imekuwa ikipinga kumuhitaji Vidal kwa kipindi kirefu kiangazi hiki lakini sasa wanadaiwa kuanza mazungumzo kama wanayoanya na Ajax Amsterdam kwa ajili ya kumsajili Daley Blind. Majeruhi ndio yalioonekana kumzuia Van Gaal kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Chile ambaye ana thamani ya paundi milioni 30 lakini kutokana na matokeo mabovu ya hivi karibuni klabu imeona hakuna jinsi bali kutumia fedha ili wajiimarishe. Upasuaji wa goti msimu uliopita ulimzuia Vidal kuitumikia Juventus toka mwishoni mwa Machi mwaka huu ingawa baadae alipona na kupata muda wa kuwepo katika kikosi cha Chile katika michuano ya Kombe la Dunia. Ujio wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 United kutasaidia kuimarisha safu ya kiungo ambayo imeonekana kuyumba na kupelekea kipigo cha mabao 4-0 jana dhidi ya timu ya daraja la pili ya MK Dons katika mcheo wa Kombe la Ligi. Kama United wakifanikiwa kumsajili Vidal watakuwa wamefikisha kiasi cha paundi milioni 150 walizotumia msimu huu kwa ajili ya usajili baada ya kufunja rekodi nchini Uingereza kwauhamisho wa Di Maria.

WENGER AMKINGIA KIFUA SANCHEZ.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amemkingia kifua Alexis Sanchez kwa kiwango bora alichoonyesha katika nafasi ya mshambuliaji wa kati katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Everton uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 Jumamosi iliyopita. Arsenal walipambana kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuhakikisha wanapata sare katika Uwanja wa Goodison Park ingawa nyota huyo aliyesajiliwa kwa euro milioni 42 msimu huu alitolewa baada ya mapumziko na nafasi yake kuchukuliwa na Olivier Giroud. Kuelekea katika mchezo wao wa leo dhidi ya besiktas katika Uwanja wa Emirates, Wenger amesema anadhani Sanchez alicheza vyema katika mchezo wa Jumamosi lakini bado anahitaji muda ili aweze kuzoea mikikimikiki ya ligi hiyo. Pamoja na Giroud kuumia katika dakika za mwisho za mchezo huo, Wennger amesema hana shaka katika hilo kwani ana washambuliaji wa kutosha katika kikosi chake. Arsenal walitoka sare ya bila ya kufungana na Besiktas katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa huko Instabul ikiwa ni mara ya kwanza kushindwa kushinda mechi za hatua hiyo mtoano ili waweze kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

MADRID WAMEPANIA KUWEKA HISTORIA - BALE.

WINGA mahiri wa Real Madrid, Gareth Bale amesisitiza kuwa wana nia ya kuweka historia na kuwa klabu ya kwanza kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Madrid waliitandika Atletico Madrid kwa mabao 4-1 baada ya muda wa nyongeza msimu uliopita na kushinda taji lao la 10 la michuano hiyo na nyota huyo wa zamani wa tottenham Hotspurs ana hamu ya kuongeza mataji zaidi katika msimu huu wa 2014-2015. Akihojiwa Bale amesema kushinda taji la 10 la Ulaya lilikuwa jambo bora kwa kila mtu na kufunga bao katika mchezo wa fainali ilikuwa ni moja kati ya ndoto zake hgivyo anadhani msimu uliopita ulikuwa mzuri kwao. Bale amesema kwasasa wanatakiwa kuangalia ya mbele na kujaribu kushinda taji hilo tena na kwa kufanya hivyo watakuwa wameweka historia ya kipekee. Madrid walianza vyema kwa kuichapa Sevilla mabao 2-0 mapema mwezi huu katika mchezo wa Super Cup ya Ulaya lakini walijikuta wakichapwa jumla ya mabao 2-1 na mahasimu wao Atletico katika mchezo wa ngao ya jamii kufunga pazia la La Liga.

BAYERN YATAKA KUSAJILI KINGA LA MONCHENGLADBACH.

MWENYEKITI wa klabu ya Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge ameiambia klabu ya Borussia Monchengladbach kukubali ofa yao kwa ajili ya Sinan Kurt au wahatarishe kumkosa kinda huyo kwa kusajiliwa kama mchezaji huru katika usajili wa kiangazi mwakani. Mabingwa watetezi wa Bundesliga wamepania kumsajili chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 18 lakini wameshindwa kufikia makubaliano ya klabu yake hiyo. Katika siku za karibuni Kurt amesema anataka kuendeleza soka lake Bayern ingawa klabu hiyo iko tayari kusubiri kwa mwaka mzima kama klabu yake itakataa kushusha bei wanayotaka. Rummenigge amesema mkurugenzi wa Monchengladbach, Max Eberl anataka fedha zaidi kuliko walizoahidi wakurugenzi wake Matthias Sammer na Michael Reschke. Mwenyekiti huyo aliendelea kudai kuwa hali hiyo ni ya kawaida lakini mkataba wa mchezaji unamalizika mwakani hivyo hawatakiwi kusahau kuwa kama wakikwamisha uhamisho huo mchezaji huyo anaweza kuondoka bure.

KUFUNGWA ILIKUWA HALALI - KOCHA CELTIC.

MENEJA wa klabu ya Celtic Ronny Deila amesema kikosi chake hakikuwa fiti baada ya kutandikwa bao 1-0 na Maribor ya Slovenia na kujikuta wakishindwa kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na Marcos Tavares akitumia vyema udhaifu wa mabeki na kuifanya Celtic kuangukia katika michuano ya Europa Leauge. Akihojiwa Deila amesema hawakufungwa kwasababu ya mabeki bali wamepoteza mchezo huo kwasababu wameshindwa kutengeneza nafasi za kufunga hivyo ni mategemeo yao watasimama katika nafasi hiyo msimu ujao. Mechi za kufuzu hatua ya makundi zinaendelea tena leo ambapo Arsenal watakuwa wenyeji wa Besiktas ya Uturuki katika Uwanja wa Emirates.

DI MARIA AWAAMBIA MASHABIKI WA MADRID KUWA HAKUONDOKA KWA MAPENZI YAKE.

WINGA mpya wa klabu ya Manchester United, Angel Di Maria ameandika barua ya wazi kwa mashabiki wa Real Madrid akidai kuwa hakutaka kuondoka kwa wakongwe hao wa soka nchini Hispania. Nyota huyo alikamilisha usajili wake uliogharimu paundi milioni 60 jana huku United wakimpa mkataba wa miaka mitano. Lakini mwenyewe amesisitiza kuwa alikuwa yuko tayari kusaini mkataba mpya na mabingwa hao wa soka barani Ulaya. Katika barua yake iliyochapishwa katika gazeti la Marca la Hispania, Di Maria amesema anatakiwa kuondoka lakini anataka kuweka wazi kuwa haikuwa nia yake kufanya hivyo. Nyota huyo aliendelea katika barua hiyo kuwa baada ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa alikwenda katika Kombe la Dunia akiwa na matumaini ya kupewa mkataba lakini jambo hilo halikufanyika. Di Maria amesema kuna mambo mengi anayothamini na mengi kati ya hayo hayahusiani na masuala ya mshahara, ni mategemeo yake ataendelea kukua akiwa United moja ya klabu kubwa duniani na ana matumaini ya kuandika historia mpya akiwa hapo.

AFCON 2015: EBOLA YAZIDI KULETA BALAA, CONGO YAGOMA KWENDA NIGERIA.

SHIRIKISHO la Soka nchini Nigeria-NFF limedai kuwa halijapata taarifa yoyote rasmi kutoka Shirikisho la Soka la Afrika-CAF juu ya madai ya Congo Brazzaville kuelekea katika mchezo wao kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika utakaofanyika huko Calabar. Congo ambao watakuwa wageni wa Nigeria katika mchezo huo utakaochezwa Septemba 6 mwaka huu wametuma malalamiko CAF kueleza wasiwasi wao juu usalama katika mchezo huo. Congo wamesisitiza hawatakwenda katika mji wa Calabar au mji mwingine wowote nchini Nigeria kwa ajili ya mcjhezo huo kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Kumeguwa na wagonjwa wengi walioripotiwa katika baadhi ya sehemu za mji wa Liberia, Guinea, Sierra Leone na Nigeria ambavyo vifo vya watu 1,427 vimeripotiwa huku wengine zaidi ya 2,615 wakiambukizwa toka ugonjwa huo ulipolipuka Machi mwaka huu. Kocha wa timu ya taifa ya Congo, Claude Leroy amesema itakuwa ngumu na hatari kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo huo na kudai kuwa hata majirani zao Cameroon tayari wamefunga mipaka yao ili kuepusha maambukizi zaidi. Hata hivyo NFF wamesisitiza kuwa mchezo utafanyika kama ulivyopangwa katika Uwanja wa UJ Esuene uliopo mji wa Calabar.


PAMOJA NA KIPIGO CHA FEDHEHA, VAN GAAL ADAI HAJUTII CHOCHOTE.

KLABU ya Manchester United, Louis van Gaal amesema hana cha kujutia kutokana na mbinu na kikosi alichotumia jana kilichofungwa na timu ya MK Dons na kuondolewa katika michuano ya Kombe la Ligi. United walichapwa mabao 4-0 na timu hiyo ya daraja la pili yaliyofungwa na Will Grigg na Benik Afobe anayecheza kwa mkopo akitokea Arsenal, na kumuacha Van Gaal bila ushindi katika mechi tatu alizocheza toka akalie nafasi hiyo. Hata hivyo, Van Gaal hakuomba radhi kutokana na kipigo hicho na kusisitiza kuwa alikuwa sahihi kuchagua kikosi kilichotawaliwa na vijana na wachezaji wasio na uzoefu. Akihojiwa Mholanzi huyo amesema hajutii chochote kutokana na kupoteza mchezo huo kwani alipanga kikosi sahihi na mbinu alizotumia zilikuwa nzuri ila bahati haikuwa upande wao. Ila pamoja na hayo Van Gaal aliwaomba mashabiki wa klabu hiyo kuwa subira na kudai kuwa anahitaji muda ili kuigeuza timu hiyo kuwa ya ushindi.

Tuesday, August 26, 2014

WENGER ASUBIRIA VIPIMO VYA GIROUD WAKATI ARSENAL IKIENDELEA KUANDAMWA NA MAJERUHI.

KLABU ya Arsenal inasubiri matokeo ya ya vipimo vya kifundo cha mguu cha Olivier Giroud baada ya wasiwasi kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa anaweza kukaa nje kwa miezi mitatu. Giroud mwenye umri wa miaka 27 alipata majeruhi hayo katika mchezo dhidi ya Everton uliomalizika kwa sare vya mabao 2-2. Nyota huyo anatakiwa kufanyiwa vipimo kwa mara nyingine ili kujua ukubwa wa tatizo na muda ambao linaweza kupona. Kukosekana kwa Giroud kunamuacha meneja wa Arsenal Arsene Wenger kubakiwa na Alexis Sanchez, Joel Campbell, Yaya Sanogo na Lukas Podolski kama machaguo yake katika safu ya usambuliaji. Sanogo naye alikuwa nje kutokana na matatizo ya msuli na kuna hati hati akaukosa mchezo wa kesho wa kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Besiktas huku Sanchez yeye amekuwa akitumika kama winga toka atue akitokea Barcelona msimu huu.

GOMEZ AAPA KUPIGANIA NAFASI YAKE UJERUMANI.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Fiorentina ya Italia Mario Gomez ameapa kuwa atapigania nafasi yake katika kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani msimu huu. Nyota huyo wa zamani wa Bayern Munich alipatwa na majeraha mawili makubwa msimu uliopita na pamoja na kufanikiwa kurejea uwanjani kabla ya kumaliza kwa msimu wa 2013-2014, kocha wa Ujerumani Joachim Loew alimuacha katika kikosi cha kilichoshinda Kombe la Dunia nchini Brazil. Gomez tayari amekiri mara kadhaa kuwa ilikuwa ni jambo gumu kuishuhudia nchi yake huko Brazil bila uwepo wake lakini amesisitiza kuwa yote aliyokuwa akiwaza yanamlazimisha sasa alazimishe kurudi tena katika kikosi cha nchi hiyo kwa ajili ya michuano ya Ulaya 2016. Akihojiwa amesema suala la kurejea katika kikosi cha timu ya taifa lipo katika ndoto zake na ana matumaini makubwa kwamba atatizmiza malengo yake hayo.

BRENDAN RODGERS AMTAHADHARISHA BALOTELLI KUWA HIYO NI NAFASI YAKE YA MWISHO.

MENEJA wa klabu ya Liverpool, Bredan Rodgers amedai kuwa Mario Balotelli yuko katika nafasi yake ya mwisho baada ya kujiunga na Liverpool kwa kitita cha paundi milioni 16. Nyota huyo wa kimataifa wa Italia mwenye umri wa miaka 24 alikuwa jukwaani akiitizama timu yake hiyi mpya ikichapwa mabao 3-1 na klabu yake ya zamani ya Manchester City Jumatatu baada ya kutoka AC Milan kwa dili la miaka mitatu. Balotelli alikuwa na matukio kadhaa yenye utata akiwa City lakini wakati Rodgers akikiri usajili huo ni wa hatari pia amedai watatumia nafasi hiyo kumkuza kama mchezaji na kumsaidia kupata ukomavu. Rodgers amesema Balotelli ni kijana mwenye upeo na akili na anajua alipo katika soka lake hivi sasa kwani nafasi hiyo inaweza kuwa ya mwisho kung’ara. Liverpool ambao walimaliza wakiwa katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu msimu uliopita nyuma ya mabingwa City kwa alama mbili, walimuuza mshambuliaji anayeongoza kwa mabao Luis Suarez kwa kitita cha paundi milioni 75 kwenda Barcelona.

UCHOVU WA SUPER CUP UMECHANGIA SARE YA ATLETICO - SIMEONE.

MENEJA wa klabu ya Atletico Madrid, Diego Simeone anaamini kuwa nguvu walizotumia katika mchezo wa Super Cup ziliwagharimu katika mchezo wao wa ufunguzi wa La Liga dhidi ya Rayo Vallecano ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana. Mabingwa hao watetezi wa La Liga walipambana na mahasimu wao Real Madrid mara mbili katika kipindi kisichozidi siku nne na Simeone anaamini kuwa uchovu ulichangia kikosi chake kutoa sare katika mchezo huo. Akihojiwa Simeone amesema walikuwa wametoka kucheza na Madrid Jumanne na Ijumaa na nguvu walizotumia katika siku hizo zilijionyesha katika kipindi cha pili cha mchezo wa jana. Hata hivyo Simeone alilaumu kikosi chake kwa kushindwa kutumia nafasi walizopata katika kipindio cha kwanza lakini anaamini wenyeji wao hao walikuwa bora zaidi yao katika kipindi cha pili.

CHAMPIONS LEAGUE: ARSENAL FITI KUIZAMISHA BESIKTAS.

KIUNGO mahiri wa Arsenal, Jack Wilshere ana uhakika kuwa sare waliyopata dhidi ya Everton itawasaidia katika mchezo wao muhimu wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Besiktas hapo kesho. Kikosi hicho kinachonolewa na Arsenal Wenger kinatarajia kuelekea katika mchezo wao huo wa mkondo wa pili wakiwa wametoshana nguvu na Waturuki hao baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Instabull wiki iliyopita. Hiyo inakuwa mara ya kwanza kwa Arsenal katika mechi 13 walizocheza za mtoano kushindwa kushinda. Lakini Arsenal sasa wanajisikia vyema baada ya kufanikiwa kutoka nyuma kwa kufungwa mabao 2-0 na kufanikiwa kutoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Everton Jumamosi iliyopita. Akihojiwa Wilshere amesema alama waliyopata dhidi ya everton ilikuwa ni muhimu kwani inawapa nguvu kwa ajili ya mchezo wao wa kesho.

WAZIRI NDIO AMENIOMBA NIISAIDIE SUPER EAGLES - KESHI.

KOCHA Stephen Keshi amethibitisha kuwa Waziri wa Michezo wa Nigeria Tammy Danagogo amewezesha yeye kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo kwa mechi mbili za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Congo Brazzaville na Afrika Kusini. Kumekuwa na mambo mengi yanayoendelea katika uongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo huku kukiwa na mipango ya kuandaa mkutanio mkuu na uchaguzi wa kamati mpya ya utendaji. Akihojiwa akiwa nyumbani kwake huko Califonia, Marekani, Keshi amesema kutokana na mambo yanayoendelea waziri amemuomba kusimamia mechi hizo mbili mpaka hapo hali itakapotulia NFF na anafurahi kuitumikia nchi yake. Toka kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil ambapo Nigeria ilitolewa katika hatua ya makundi, kumekuwa na migogoro ya hapa na pale katika NFF huku baadhi ya viongozi wake wakisimamishwa na kulifanya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kluingilia kati. Migogoro hiyo imesababisha Keshi ambaye mkataba wake ulimalizika baada ya michuano hiyo kushindwa kuanza mazungumzo ya mkataba kutokana na kutokuwa na uongozi unaoeleweka.

EVERTON YAMTENGEA ETO'O MKATABA WA MIAKA MIWILI.

KLABU ya Everton inakaribia kukubaliana mkataba wa miaka miwili kumsajili mshambuliaji Samuel Eto’o baada ya kuachwa na Chelsea mwishoni mwa msimu uliopita. Liverpool wamekuwa wakimtaka nyota huyo wa kimataifa wa camertoon mwenye umri wa miaka 13 lakini baada ya kukamilika kwa dili la Mario Balotelli aliyesajiliwa kwa paundi milioni 16 kunaacha njia nyeupe kwa Everton kuanza mazungumzo na Eto’o. Mazungumzo bado yanaendelea lakini Everton wanaweza kumsajili Eto’o kwa wakati ili aweze kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya timu yake ya zamani Chelsea Jumamosi hii. Everton tayari wameshamsajili Romelo Lukaku kwa ada ya paundi milioni 28 kutoka Chelsea kiangazi hiki na pia kumchukua Christian Atsu kwa mkopo kutoka hapohapo Chelsea. Mkataba wa Eto’o na Chelsea ulimalizika mwanzoni mwa Julai na kocha Jose Mourinho hakumuongeza mkataba mwingine. Eto’o ambaye amewahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika mara nne, alifunga mabao 12 katika mechi 35 baada ya kusajiliwa na Chelsea kwa mwaka mmoja akitokea Anzhi Makhachkala Agosti mwaka jana.

SIMEONE AFUNGIWA MECHI NANE KWA UTUKUTU.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Diego Simeone amefungiwa mechi nane na Shirikisho la Soka nchini Hispania-RFEF jana kufuatia kuitolewa na hatua za hasira alizochukua wakati wa mchezo wa Super Cup dhidi ya Real Madrid. Kocha huyo raia wa Argentina alifungiwa mechi nne kwa kosa la kumtandika kofi mwamuzi wa nne nyuma ya kichwa baada ya kuondolewa katika benchi lake ufundi Ijumaa iliyopita, adhabu ya mechi mbili ikiwa ni kwasababu ya kulalamika, moja ya kupinga uamuzi na nyingine kwa kutoa maelekezo katika benchi lake la ufundi akiwa jukwaani. Katika taarifa yake RFEF imedai kuwa Simeone alitolewa kwa kosa la kulalamika huku akinyoosha mikono yake hewani na kutoka nje ya eneo lake zaidi ya mara moja na kugoma kusikilisha maelezo ya mwamuzi wa nne. Tukio hilo lilitokea katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo dhidi ya Madrid katika Uwanja wa Calderon ambao Atletico walishinda kwa bao 1-0 hivyo kuwafanya kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 2-1 katika mechi wlaizokutana. Baadae Simeone alikiri kuwa alifanya makosa lakini Atletico wanatarajia kukata rufani ili adhabu hiyo iweze kupunguzwa kidogo.

DI MARIA ATUA RASMI MANCHESTER KUMALIZIA USAJILI WAKE ULIOWEKA REKODI MPYA UINGEREZA.

KLABU ya Manchester United imekubali kutoa kitita kilichovunja rekodi ya usajili nchini Uingereza cha paundi milioni 59.7 kwa ajili ya kumsajili winga wa Real Madrid Angel Di Maria. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 26 tayari ameshatua jijini Manchester na ameshafanyiwa vipimo vya afya asubuhi ya leo na baadae atatambulishwa rasmi. Di Maria anaweza kucheza mechi yake ya kwanza ugenini wakati United watakapocheza na Burnley katika mchezo wa Ligi Kuu Jumamosi hii. 
Usajili huo unazidi paundi milioni 50 walizolipa Chelsea kwa ajili ya kumchukua Fernando Torres kutoka Liverpool mwaka 2011. Mara ya mwisho United kuvunja rekodi ya usajili nchini Uingereza ilikuwa mwaka 2002 wakati walipotoa kitita cha paundi milioni 29.1 kwa ajili beki Rio Ferdinand alitoa Leeds United. Mpaka sasa United wameshatumia kiasi cha paundi milioni 132 kwa ajili ya usajili wa majira ya kiangazi wakiwa tayari wameshawasajili beki Luke Shaw, kiungo Ander Herrera na Marcos Rojo.

Monday, August 25, 2014

RONALDO FITI KUIKABILI CORDOBA.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Real Madrid Cristiano Ronaldo anaweza kuanza katika mchezo wa ufunguzi wa La Liga dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Cordoba pamoja na kushambuliwa na majeruhi. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno alitokea benchi katika mchezo wa Super Cup uliochezwa Ijumaa iliyopita na kufungwa na Atletico Madrid. Meneja wa Madrid Carlo Ancelotti amesema Ronaldo amefanya mazoezi vyema hivyo anaweza kumpanga katika kikosi chake. Ancelottio alikiri kuwa wakati wa maandalizi ya msimu alikuwa akisumbuliwa na majeruhi hivyo anahitaji kufanya jitihada ili aweze kurejea katika kiwangop chake. Ronaldo mwenye umri wa miaka 29 ambaye anashikilia tuzo ya mchezaji bora wa dunia alipata majeruhi ya mgongo wakati timu hizo mbili zilipotoa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa mkondo wa kwanza.

UJERUMANI WANAWAKE NAO WANYAKUWA KOMBE LA DUNIA.

TIMU ya taifa ya wanawake ya Ujerumani imefanikiwa kunyakuwa Kombe la Dunia kwa wachezaji wanawake wenye umri chini ya miaka 20 kwenye michuano iliyokuwa inafanyika huko Montreal, Canada. Ujerumani walifanikiwa kuwazidi maarifa Nigeria katika mchezo wa fainali kwa kuwafunga bao 1-0 kama ilivyokuwa kwa timu ya wanaume iliyonyakuwa taji hilo katika michuano iliyofanyika nchini Brazil. Pamoja na kuonyesha mchezo mzuri huku wakimiliki vyema mpira, Nigeria walishindwa kabisa kupenya ngome ngumu ya wapinzania wao. Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na Lena Petermann ambaye alifunga katika dakika ya nane ya muda wa nyongeza baada ya timu hizo kushindwa kufungana katika muda wa kawaida. Mshambuliaji wa Nigeria na mfunmgaji bora wa mashindano hayo Asisat Oshoala alikosa nafasi kadhaa za wazi wakati golikipa wa Ujerumani Meike Kamper alitajwa kama mchezaji bora wa mechi hiyo.

SUPER MARIO KULAMBA PAUNDI 90,000 KWA WIKI ANFIELD.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Italia, Mario Balotelli anatarajiwa kuanguka mkataba wa miaka mitatu katika klabu ya Liverpool baada ya leo kuelekea katika mchezo wao Ligi Kuu dhidi ya Manchester City. Kikosi cha Liverpool kinachoongozwa na Brendan Rodgers kitapata morali kwa kutangazwa kwa Balotelli kuwa mchezaji wao kabla ya kuanza kwa mchezo huo. Balotelli mwenye umri wa miaka 24 ambaye ameondoka AC Milan kwa kitita cha paundi milioni 16 alitua katika uwanja wa mazoezi wa Melwood mchana wa leo kumalizia hatua za mwisho za usajili wake. Wiki iliyopita nyota huyo alikwenda Melwood kukamilisha vipimo vya afya na kukubali mkataba huo ambao utamuwezesha kuchukua kitita cha paundi 90,000 kwa wiki. Wakati akiwa Manchester City Balotelli alifanikiwa kufunga mabao 30 katika mechi 80 alizocheza huku akifunga mabao 18 katika mechi 41 alizoichezea Milan msimu uliopita.

ALGERIA YASIMAMISHA LIGI KUFUATIA KIFO CHA MCHEZAJI.

SHIRIKISHO la Soka nchini Algeria limesimamisha Ligi Kuu kufuatia kifo cha mchezaji wa Cameroon Albert Ebosse ambaye alipigwa na jiwe lililorushwa na mashabiki. Uamuzi huo umefikiwa jana katika kikao kilichofanyika jana. Ebosse mwenye umri wa miaka 24 alipigwa na jiwe kichwani wakati akitoka uwanjani baada ya timu yake ya JS Kabylie kufungwa na USM Alger huko Tizi Ouzou juzi. Tayari mamlaka inayohusika imeshaufungia Uwanja wa 1st Novemba 1954 kulikotokea tukio hilo. Shirikisho hilo pia limeamua kutoa ubani wa dola 100,000 kwa familia ya Ebosse kiwango ambacho kinaaminika angeweza kukipata katika kipindi cha mkataba wake huku wachezaji wa Kabylie nao wakitoa mishahara yao ya mwezi kama rambirambi ya kufariki kwa mwenzao. Imegundulika kuwa uwanja wa 1st Novemba 1954 ulikuwa katika matengenezo wakati wa mchezo huo na mashabiki walitumiwe mawe ya ujenzi yaliyokuwa yamewekwa maeneo hayo.

MAN UNITED KUVUNJA REKODI USAJILI WA DI MARIA.

KLABU ya Manchester United italazimika kuvunja rekodi ya usajili nchini Uingereza kwa ajili ya kumsajili winga mahiri wa klabu ya Real Madrid Angel Di Maria. Meneja wa Madrid Carlo Ancelotti amebainisha kuwa Di Maria mwenye umri wa miaka 26 tayari amekwishawaaga wachezaji wenzake kuelekea katika uhamisho wake huo. Inakadiriwa kuwa United italazimika kuilipa Madrid kitita cha paundi milioni 75 kama wanahitaji saini ya winga huyo. Kama kweli wakitoa kitita hicho watakuwa wamevunja rekodi ya usajili iliyowekwa na Chelsea wakati walipomsajili Fernando Torres kwa paundi milioni 50 kutoka Liverpool mwaka 2011. Usajili mkubwa uliowahi kuweka rekodi na kufanywa na United ulikuwa ni wa Rio Ferdinand ambaye alitua Old Trafford kwa paundi milioni 29.1 akitokea Leeds mwaka 2002. Di Maria alitua Madrid akitokea Benfica kwa ada ya paundi milioni 36 mwaka 2010 na kufanikiwa kushinda taji la La Liga mwaka 2012 na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.

VAN GAAL AKIRI ALAMA MOJA WALIYOPATA SUNDERLAND HAITOSHI.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, Louis van Gaal amekiri baada ya kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Sunderland kuwa alama moja katika mechi mbili za Ligi Kuu walizocheza hazitoshi. Akihojiwa kocha huyo raia wa Uholanzi amesema wamepata alama moja na jambo hilo sio zuri kwa klabu kama hiyo. Van Gaal amesema wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii zaidi kwani wacchezaji wamesikitishwa na sare hiyo baada ya mchezo kwasababu walikuwa na uhakika wa kushinda. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kwasasa wanahitaji walau kushinda mechi moja ili kurejesha hali ya kujiamini halafu wataona huko mbele watakavyokwenda.

RAIS WA BARCELONA AKIRI MAKOSA KATIKA USAJILI WA WACHEZAJI WALIO CHINI YA UMRI LAKINI ADAI WATAKOMAA MOAKA KIELEWEKE.

RAIS wa klabu ya Barcelona, Josep Maria Bartomeu amekiri kufanyika makosa katika usajili wa wachezaji walio chini ya umri lakini wanatarajia kukata rufani Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS kupinga adhabu ya kufungiwa kusajili misimu miwili. Shirikisho la Soka Duniani-FIFA lilitupilia mbali rufani ya Barcelona waliyowapa kwa kosa hilo hivyo kumaanisha kuwa hawataruhusiwa kusajili kuanzia dirisha dogo la usajili Januari na Julai hadi Agosti mwakani. Adhabu hiyo ilisimamishwa kwa muda kupisha kusikilizwa kwa rufani yao hivyo kuwapa nafasi ya kusajili katika kipindi hi9ki cha kiangazi ambapo wamefanikiwa kumnasa Luis Suarez lakini Bartomeu amesema sasa wanatarajia kupeleka rufani yao CAS ili wapunguziwe adhabu. Bartomeu amesema wanajua kuwa walifanya makosa lakini adhabu imekuwa kubwa sana hivyo wataandaa ushahidi mzuri ili wa kuupeleka CAS ili wapunguziwe adhabu hiyo.

CAF CHAMPIONS LEAGUE: NUSU FAINALI SASA KUZIKUTANISHA ES SETIF DHIDI YA MAZEMBE, AS VITA DHIDI YA CS SFAXIEN.

BAADA ya sare ya bila kufungana dhidi ya mahasimu wao AS Vita katika mchezo wa jana uliochezwa jijini Kinsasha, TP Mazembe wamekwenda katika nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika huku wakiwa vinara wa kundi A. Katika mchezo wa jana Vita walicheza bila ya mshambuliaji wao Dady Birori ambaye alisimamishwa na Shirikisho la Soka la Afrika-CAF kwa kutumia majina mawili tofauti katika klabu yake na timu ya taifa ya Rwanda. Sakata hilo la Birori limepelekea Rwanda kuondolewa katika makundi ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani. Timu zote hizo mbili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimemaliza katika zikiwa na alama 11 ila Mazembe wameongoza kundi hilo kwa kuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Sasa Mazembe watacheza mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ugenini dhidi ya ES Seif ya Algeria huku Vita wao wakiwakaribisha CS Sfaxien ya Tunisia ambapo mechi za mkondo wa kwanza zikitarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 19, 20 au 21.



First leg: September 19-21, second: September 26-28.

HAYATOU ATAKA ADHABU KWA WALIOSABABISHA KIFO CHA MCHEZAJI WA CAMEROON.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF, Issa Hayatou ameonya kuwa Afrika haitatumika kama chimbuko la utovu wa nidhamu. Hayatou ametoa kauli hiyo baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon Albert Ebosse anayecheza katika klabu ya JS Kabylie ya Algeria kupigwa na jiwe kichwani na kufariki dunia wakati wa mchezo wa ligi ya nchi hiyo. Hayatou ameagiza hatua kali za kisheria kuchukuliwa ilikukabiliana na utovu wa Usalama. Ebosee mwenye umri wa miaka 24, aligongwa kichwani baada ya timu yake kushindwa mabao 2-1 na USM Alger mjini Tizi Ouzou. Shiriklisho la Soka la Algeria limeagiza kufungwa kwa Uwanja wa 1st Novemba 1954 uliotumika kwa ajili ya mchezo huo. Ebosse alikuwa mfungaji bora msimu uliokamilika akiwa na jumla ya mabao 17 tangu awasili nchini humo kutoka Malaysia.

Friday, August 22, 2014

NEYMAR AUMIA TENA.

KLABU ya Barcelona imepata pigo kubwa kuelekea katika mchezo wao wa ufunguzi wa La Liga dhidi ya Elche utakaochezwa Jumapili kutokana na taarifa za kukosekana kwa Neymar katika mchezo huo wa Camp Nou kutokana na majeruhi. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil, ndio kwanza alikuwa ameruhusiwa kucheza na madaktari wa timu hiyo baada ya kupona majeruhi ya mgongo aliyopata katika Kombe la Dunia lakini sasa anakabiliwa na majeruhi mengine. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo, imedai kuwa Neymar alikuwa akilalamika maumivu katika kifundo chake cha mguu wa kushoto na baada ya vipimo imegundulika kuwa ana matatizo ambayo yatachukua muda kidogo kupona. Taarifa hiyo imeendelea kudai kuwa kurejea mazoezini kwa mchezaji huyo kutategemea kumalizika kwa maumivu hayo hivyo ni wazi hatakuwepo katika mchezo wa kesho. Neymar alicheza mechi 26 za La Liga msimu uliopita na kufunga mabao saba lakini msimu huu unaonekana tayari ameuanza vibaya kwa maumivu.

NEWCASTLE YAMUWINDA AYEW.

KLABU ya Newcastle United imeripotiwa kuwa inataka kumsajili kiungo wa kimataifa wa Ghana Andre Ayew. Ayew ameshawahi kukaririwa Mei mwaka huu akidai kuwa na hamu kubwa ya kucheza katika Ligi Kuu ambayo huwa inaangaliwa sana nchini kwao Ghana. Nyota huyo amesema huwa anapenda kila kitu kuhusiana na ligi hiyo, ikiwemo mechi, hali ilivyo, mashabiki na ushindani uliopo. Mabao mawili aliyofunga katika Kombe la Dunia akiwa na Ghana yameonyesha kumuweka juu pamoja na timu yake kushindwa kung’ara katika michuano hiyo.

PATASHIKA LIGI YA MABINGWA AFRIKA KESHO.

MPAMBANO wa kugombea nafasi ya juu ndio jambo la muhimu wakati tukielekea kufunga pazia la hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya mabingwa barani Afrika mwishoni mwa wiki hii. Ingawa nafasi za nusu fainali zikiwa tayari zimejulikana vita iliyobaki sasa ni kujua nani anamaliza katika nafasi juu katika makundi. Timu zilizovuka hatua inayofuata ni AS Vita na TP Mazembe zote za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC katika kundi na Entene Setif ya Algeria na CS Sfaxien ya Tunisia katika kundi B. Baada ya kuvuka sasa timu hizo zitakuwa zikigombea nafasi ya kuondoza kundi ambapo Jumapili Mazembe watavaana na mahasimu wao Vita ambao wameshangaza wengi baada ya kupenya katika kundi lililokuwa na timu kongwe kama Zamalek ya Misri na Al Ahly ya sudan. Kesho kutakuwa na mchezo mwingine wa kundi B ambapo Sfaxien wenyewe watakuwa wenyeji wa Setif huku leo kukiwa mchezo wa kundi A kati ya Al Ahly dhidi ya Zamalek. Mechi nyingine ya kundi B itachezwa Jumapili ambapo Esperance ya Tunisia wataivaa Ahly Benghazi ya Libya.

SIJUTII FABREGAS KWENDA CHELSEA - WENGER.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amekiri kuwa anaona tofauti anapomuona Cesc Fabregas akiichezea Chelsea katika fulana ya bluu lakini amesisitiza kuwa hajutii kutomsajili tena. Wenger aliwaambia waandishi wa habari kuwa kitu pekee anachojutia ni kuondoka kwa Fabregas mwaka 2011 kwenda Barcelona na kudokeza kuwa bado anataka kusajili kiungo mwingine kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania mwenye umri wa miaka 27 ambaye amecheza mechi zaidi ya 300 akiwa Arsenal alianza vyema katika timu yake mpya ya Chelsea wakati waliposhinda mabao 3-1 dhidi ya Burnley Jumatatu. Wenger amesema hajutii mchezaji huyo kujiunga na mahasimu wao ingawa anaona tofauti lakini inabidi ukubali kuwa ni kawaida kwa wachezaji wa kulipwa kuhama kutoka klabu moja kwenda nyingine. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kuondoka kwa Fabregas kulimpa nafasi nyota wa kimataifa wa Wales Aaron Ramsey mwenye umri wa miaka 23 kuibuka katika kikosi chake kwanza.

GALATASARAY YAMPOTEZEA PODOLSKI.

RAIS wa klabu ya Galatasaray amethibitisha kuwa timu hiyo haitatoa ofa yoyote kwa ajili mshambuliaji wa Arsenal, Lkas Podolski. Kumekuwa taarifa wiki hii zinazodai kuwa Arsenal wako tayari kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani ambaye ameshindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza toka atue katika Uwanja Emirates mwaka 2012. Lakini wakati bosi huyo Galatasaray Unal Aysal akikiri kufanya mazungumzo na meneja wake Cesare Prandelli kuhusu Podolski, amebinisha kuwa kocha huyo amemshauri kuachana na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29. Aysal amesema alimuuliza Prandelli kama anamtaka Podolski lakini alimjibu kuwa huo utakuwa usajili wa kifahari ambao hana shida nao kwa sasa.

FIFA YAKOMAA MICHUANO YA KLABU YA DUNIA IFANYIKE MOROCCO PAMOJA NA EBOLA.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA, limethibitisha kuwa michuano ya Klabu Bingwa ya dunia itakayoihusisha Real Madrid itafanyika nchini Morocco kama ilivyopangwa Desemba mwaka huu pamoja na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ulioathiri nchi kadhaa barani Afrika. Katika taarifa yake FIFA imedai kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani-WHO hakuna mgonjwa yoyote aliyepatikana Morocco hivyo hawaoni sababu ya kubadilisha sehemu. Virusi hivyo hatari vya Ebola tayari vimeua watu wapatao 1,350 katika nchi nne magharibi mwa Afrika zikiwemo Liberia, Guinea, Nigeria na Sierra Leone toka uanza kulipa Machi mwaka huu. Mabingwa wa Ulaya Madrid tayari wamefuzu michuano hiyo itakayoanza Desemba 10 hadi 20 wakiwa sambamba na timu za San Lorenzo kutoka Argentina, Cruz Azal kutoka Mexico, Auckland City kutoka New Zealand na wenyeji Moghreb Tetouan. Mabingwa kutoka bara la Afrika na Asia nao watashiriki michuano hiyo ambapo mwaka jana Bayern Munich ndio walioibuka kidedea katika michuano iliyofanyika hapohapo Morocco.

HUMMELS HATIHATI KUIVAA LEVERKUSEN.

KOCHA wa klabu ya Borussia Dortmund, Jurgen Klopp amedokeza kuwa Mats Hummels anaweza asicheze katika mchezo wa ufunguzi wa Bundesliga dhidi ya Bayer Leverkusen utakaochezwa kesho. Beki huyo wa kati alipata mapumziko marefu baada ya kushinda Kombe la Dunia akiwa na Ujerumani huko Brazil lakini bado hajawa fiti kwa asilimia 100 na Klopp hataki kumuharakisha kumrejesha uwanjani. Klopp amesema Mats anahitaji muda zaidi wa kufanya mazoezi na nafasi yake haimpi mashaka yoyote kwasababu wapo watu wanaoweza kuiziba kwa muda huu. Dortmund haitakuwa na wachezaji wake 10 wa kikosi cha kwanza katika mchezo huo dhidi ya Leverkusen baada ya kukumbwa na majeruhi ya hapa na pale. Wachezaji hao ambao hawatakuwepo ni pamoja na Oliver Kirch, Dong-Won Ji, Marcel Schmelzer. Nuri Sahin, Jakub Blaszczykowski, Adrian Ramos, Ikay Gundogan, Erik Durm na Roman Weidenfeller.

LIVERPOOL YAMTEGA ETO'O KWA MKATABA WA MWAKA.

KLABU ya Liverpool imemtengea ofa ya mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Samuel Eto’o ili aweze kutua Anfield. Liverpool ambao wanakaribia kumsajili Mario Balotelli kutoka AC Milan, pia wako tayari kumleta na Eto’o wakati meneja Brendan Rodgers akiwa katika mipango ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Eto’o ni mchezaji huru toka alipoondoka Chelsea mapema kiangazi na amekuwa akivivutia vilabu kadhaa barani Ulaya, Amerika na Mashariki ya Kati. Ila nyota huyo wa kimataifa wa Cameroon bado anataka kubakia nchini Uingereza baada ya kucheza kwa mafanikio msimu mmoja akiwa na Chelsea. Vilabu vya Ajax Amsterdam ya Uholanzi na Everton vimeonyesha nia ya kumtaka lakini inaonekana Liverpool sasa ndio wako katika nafasi nzuri ya kumchukua nyota huyo wa zamani wa Barcelona na Inter Milan.

MACKAY AOMBA RADHI.

KOCHA Malky Mackay ameomba radhi kwa ujumbe wa simu aliokuwa akituma na kukiri kuwa haikuwa na maudhui mazuri kwa tamaduni zingine. Kocha huyo wa zamani wa Cardiff City na mfanyakazi mwingine wa zamani wa timu hiyo Iain Moody wanatuhumiwa kutumiana ujumbe wa kudhalilisha matabaka fulani katika jamii ikiwemo masuala ya ubaguzi wa rangi, jinsia na ushoga. Lakini Mackay mwenye umri wa miaka 42 amesema ujumbe aliokuwa akituma ilikuwa ni sehemu ya utani kati yake na rafiki yake Moody. Chama cha makocha wa Ligi nchini Uingereza kilituma taarifa kuwa mackay ameomba radhi kama ujumbe wake ulidhalilisha matabaka mengine. Wawili hao walitimuliwa Cardiff msimu uliopita na klabu hiyo ya Wales wamewashitaki Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwa ajili ya hatua zaidi. Moody naye ambaye alikuwa amepata kibarua cha ukurugenzi wa michezo katika klabu ya Crystal Palace alijiuzulu wadhifa wake huo jana lakini hajatoa kauli yoyote kuhusiana na tuhuma hizo.