Friday, July 28, 2017

CHELSEA YATENGA PAUNDI MILIONI 50 KWA BARKLEY NA CHAMBERLAIN.

KLABU ya Chelsea inadaiwa kutenga kitita cha paundi milioni 50 kwa ajili ya kuwawania nyota wawili wa kimataifa wa Uingereza, Ross Barkley na Alex Oxlade-Chamberlain. Meneja wa Chelsea Antonio Conte anataka kuongeza idadi ya wachezaji wazawa kwenye kikosi chake kufuatia kwasasa kuwa na idadi ya wachezaji 17 wa kigeni kwenye kikosi cha wachezaji 25. Kwa kipindi kirefu Chelsea imekuwa ikimfuatilia Barkley anayekipiga Everton, huku kiungo huyo alibakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wake akikataa kuongeza mwingine. Meneja wa Everton Ronald Koeman tayari ameshamwambia Barkley kutafuta timu nyingine huku akihitaji kiasi cha paundi milioni 25. Kwa upande wa Chamberlain mwenye umri wa miaka 23 yeye pia amebakisha miezi 12 kwenye mkataba wake huku akiwa bado kupewa ofa mpya.

ROMA BADO HAWAJAKATA TAMAA KWA MAHREZ.

KLABU ya AS Roma inajipanga kutoa ofa mpya ya paund milioni 32 kwa ajili ya Riyad Mahrez ambaye ameendelea kluonyesha kiwango kikubwa katika mechi za maandalizi ya msimu mpya. Mahrez tayari ameshafunga mabao mawili kuelekea msimu mpya baada ya kuifungia Leicester City bao la ushindi kwenye mchezo wao dhidi ya Luton juzi usiku. Hilo linakuwa bao lake la pili mwezi huu baada ya pia kufunga kwenye mchezo dhidi ya West Bromwich Albion huko Asia. Lakini nyota huyo wa kimataifa wa Algeria anataka kuondoka Leicester baada ya kuwaambia mabingwa hao wa Ligi Kuu msimu wa 2015-2016 kuwa ataondoka msimu uliopita.

THOMAS LEMAR ANUKIA ARSENAL.

KLABU ya Arsenal inadaiwa kukaribia kunasa saini ya nyota wa AS Monaco Thomas Lemar kwa kitita cha paundi milioni 45. Arsenal wamekuwa wakihangaika kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa na taarifa zinadai kuwa hatimaye wamefanikiwa kufikia makubaliano. Tayari ofa kadhaa za Arsenal kwa ajili ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 zimekataliwa na Monaco ambao wenyewe wanataka paundi milioni 80 kwa mchezaji huyo waliyemsajili kutoka Caen miaka miwili iliyopita. Taarifa kutoka Uingereza zinadai kuwa mapema mwezi huu kuwa Lemar alishafikia makubaliano na Arsenal na kuwahabalisha mabingwa hao wa Ufaransa kuwa anataka kuondoka.

LACAZETTE KUCHEZA KWA MARA YA KWANZA MBELE YA MASHABIKI WA EMIRATES.

MSHAMBULIAJI mpya wa Arsenal, Alexandre Lacazette anatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza mbele ya mashabiki wa nyumbani mwishoni mwa wiki hii katika mechi ya Kombe la Emirates. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger aliweka rekodi ya klabu kwa kutoa kitita cha paundi milioni 52 kumsajili Lacazette kutoka Olympique Lyon na mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa anatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza Uwanja wa Emirates wakati klabu hiyo itakapocheza na Benfica Jumamosi hii. Michuano hiyo ya kirafiki inayoshirikisha timu nne ni muhimu kwa Lacazette kujiweka fiti kabla ya Arsenal haijaanza kampeni zake za Ligi Kuu kwa kucheza na Leicester City Agosti 11 baada ya kuwa tayari wamecheza mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya Chelsea wiki ijayo. Akizungumza na wanahabari, Lacazette amesema Arsenal ni klabu kongwe na katika kipindi chote cha utotoni amekuwa na ndoto ya kuichezea kutokana na nyota kadhaa wa Ufaransa waliowahi kupitia hapo akiwemo Thierry Henry.

WEST HAM KUMKOSA ANTONIO MECHI DHIDI YA UNITED.

KIUNGO wa West Ham United, Michail Antonio bado ameendelea kujiuguza kufuatia kufanyiwa upasuaji wa msuli wa nyuma ya paja lakini anatarajiwa kukosa mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Manchester United. Antonio ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa klabu msimu uliopita, amekuwa akijiuguza majeruhi hayo yaliyokatisha kampeni zake Aprili mwaka huu kwenye ushindi wa bao 1-0 waliopata dhidi ya Swansea Cioty. Antonio sambamba na mchezaji mwenzake Andy Carroll ambaye pia amekuwa nje kwa majeruhi ya kipindi kirefu, waliachwa kwenye kikosi cha timu hiyo ambacho kilifanya ziara ya maandalizi ya msimu mpya huko Austria na Ujerumani. Meneja wa klabu hiyo Tony Bilic alithibitisha taarifa hizo wakati akizungumza na wanahbari nchini Ujerumani na kuongeza kuwa Antonio atakosa mechi moja dhidi ya United.

GUARDIOLA ANATAKA KUENDELEA KUBAKI cITY KWA KIPINDI KIREFU ZAIDI.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola atakuwa tayari kuongeza mkataba mwingine kufuatia kutaka kuendelea kubakia kwa kipindi kirefu iwezekanavyo katika klabu hiyo. Guardiola alisaini mkataba wa miaka mitatu na City wakati alipoteuliwa kuchukua nafasi ya Manuel Pellegrini mwaka jana. Msimu wake wa kwanza Uingereza ulishuhudia kumaliza akiwa mikono mitupu bila taji lolote kwa mara ya kwanza toka aanze shughuli hiyo ya ukocha lakini usajili mkubwa unaofanywa na klabu hiyo hivi sasa una nia ya kusahihisha makosa kwenye msimu ujao wa 2017-2018. City imefanya usajili mkubwa katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi kwa kuwanasa nyota kadhaa akiwemo bernardo Silva, Kyle Walker, Danilo na Benjamin Mendy na Guardiola ana matumaini ya kukaa hapo kwa kipindi kirefu ili kuona mipango yake ikifanikiwa. Akizungumza na wanahabari, Guardiola amesema hafahamu litakalotokea huko mbele lakini angependa kuendelea kuinoa City kwa kipindi kirefu zaidi ili kuona inafanikiwa na kuendelea kukaa kwenye nafasi za juu.

Tuesday, July 25, 2017

BARCELONA YAITIA LIVERPOOL TUMBO JOTO KWA COUTINHO.

KLABU ya Barcelona imegoma kuacha mbio zake za kumuwania kiungo wa Liverpool Philippe Coutinho kufuatia maafisa wake kudaiwa kusafiri kuelekea jijini London kujaribu kufanikisha uhamisho huo. Taarifa kutoka nchini Hispania zinadai kuwa Barcelona inaamini dili hilo linaweza kufanikiwa kwa kutoa kitita cha paundi milioni 90. Meneja wa Liverpool amesisitiza Coutinho mwenye umri wa miaka 25 bado ataendelea kuwepo katika mipango yake kwa ajili ya msimu ujao na hana mpango wowote wa kumuachia nyota huyo wa kimataifa wa Brazil. Akizungumza na wanahabari mwishoni mwa wiki iliyopita, Klopp amesema kila mtu anafahamu kuwa Coutinho ni mchezaji muhimu kwao na mwenyewe anafahamu kuwa anajisikia vyema wakati wote anapokuwa katika klabu hiyo. Taarifa kutoka Hispania zimedai kuwa maafisa wa Barcelona walikutana na wawakilishi wa Liverpool na mawakala wanaofanya kazi kwa niaba ya Coutinho katika safari hiyo ya Uingereza. Coutinho alijiunga na Liverpool akitokea Espanyol kwa kitita cha paundi milioni 8.5 Januari mwaka 2013.

MBAPPE ANUKIA MADRID KWA ADA YA KUFURU.

TAARIFA kutoka nchini Hispania zimedai kuwa Real Madrid hatimaye wamefikia makubaliano na Monaco kwa ajili ya mshambuliaji Kylian Mbappe. Madrid wanadaiwa kukubali kutoa kitita cha paundi milioni 161 ka ajili ya chipukizi huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 18. Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti la Marca, Madrid wamekubali kulipa paundi milioni 145 kama ada ya awali kwa mchezaji huyo huku nyingine paundi milioni 16 wakija kuilipa baadae. Madrid wanataka kumnasa chipukizi huyo kufuatia kumuacha Alvaro Morata kwenda kujiunga na Chelsea. Monaco walikuwa wakitaka kumbakisha Mbappe katika klabu hiyo kipindi hiki cha kiangazi lakini ofa hiyo mpya ya Madrid ambayo itavunja rekodi ya dunia inaweza kuwashawishi kumuachia.

RONALDO AMALIZA UVUMI WA KUONDOKA MADRID.

TETESI za mustakabali wa Cristiano Ronaldo sasa zimefikia tamati kufuatia nyota huyo kuliambia gazeti moja nchini Hispania kuwa atabakia Real Madrid kwa ajili ya kushinda mataji zaidi. Akikaririwa na gazeti la Marca katika mahojiano huko Shanghai, Ronaldo amesema kushinda mataji muhimu na klabu na kwake binafsi msimu uliopita lilikuwa jambo zuri hivyo kufanya hivyo tena itakuwa fahari. Kufuatia kauli yake hiyo ni wazi kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Ureno anataka kubakia Santiago Bernabeu kwa msimu ujao pamoja na tetesi zilizozagaa kuhusu mustakabali wake kwa miezi kadhaa. Jumamosi iliyopita meneja wa Madrid Zinedine Zidane aliwahakikishia mashabiki wa klabu hiyo kuwa Ronaldo kwasasa yuko likizo na atarejea katika kikosi hicho Agosti 5 mwaka huu.

CHICHARITO NDANI YA WEST HAM.

KLABU ya West Ham United imefnikiwa kukamilisha usajili wa paundi milioni 16 wa mshambuliaji Javier Hernadez kutoka bayer Leverkusen ya Ujerumani. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United amepewa mkataba wa miaka mitatu na klabu hiyo ya Ligi Kuu. Mei mwaka huu Hernandez ambaye anajulikana zaidi kwa jina la utani la Chicharito, alifanikiwa kuwa mfungaji bora wa wakati wa kikosi cha timu ya taifa ya Mexico. Akizungumza na wanabahari, Hernandez amesema Ligi Kuu ya Uingereza ndio bora duniani na pindi nafasi ilipopatikana alifurahia sana kujiunga na klabu hiyo. Hernandez mwenye umri wa miaka 29, amefunga mabao 59 katika mechi 156 alizochezea United baada ya kutua Old Trafford mwaka 2010 kabla ya kujiunga na Leverkusen kwa kitita cha paundi milioni 7.3 Agosti mwaka 2015. Akiwa Leverkusen, Hernandez amefanikiwa kufunga mabao 39 katika mechi 76 alizoichezea klabu hiyo ya Bundesliga.

CHALSEA YAMRUDISHA NYUMBANI NYOTA WAKE KWA KAULI YA KIBAGUZI, WAPIGWA TATU NA BAYERN.

KLABU ya Chelsea imemrudisha nyumbani Kenedy kutoka katika ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya kufuatia kauli aliyotoa nyota huyo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kabla ya mchezo wao huko China. Klabu hiyo iliomba radhi baada ya mashabiki kumtuhumu nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 kwa ubaguzi na chuki dhidi ya wageni. Kenedy aliweka ujumbe huo kwenye ukurasa wake wa Instagram kabla ya mchezo walioshinda mabao 3-0 dhidi ya Arsenal, ambapo mashabiki walikuwa wakimzomea wakati wa mchezo. Kenedy baadae aliomba radhi lakini Chelsea waliamua kuchukua hatua zaidi kwa kumrejesha nyumbani na kumuondoa katika ziara yao. Mapema leo Chelsea ilitandikwa mabao 3-2 katika mchezo wao mwingine wa kirafiki dhidi ya Bayern Munich uliochezwa kwenye Uwanja wa taifa nchini Singapore.

WOLVES YANASA CHIPUKIZI KUTOKA ATLETICO.

KLABU ya Wolves imefanikiwa kumsajili chipukizi wa kimataifa wa Ureno Diogo Jota kwa mkopo wa msimu mzima kutoka Atletico Madrid. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20 alicheza kwa mkopo katika klabu ya FC Porto ambapo alicheza chini ya meneja Nuno Espirito Santo anayeinoa Wolves kwasasa. Jota alianza soka lake katika klabu ya nyumbani ya Pacos Ferreira na baadae kujiunga na Atletico kwa mkataba wa miaka mitano kiangazi mwaka jana. Akizungumza na wanahabari, Jota amesema hiyo nafasi nzuri wake kujiimarisha chini ya meneja ambaye anamuamini. Jota alifunga mabao tisa katika mechi 35 alizoichezea Porto msimu uliopita, likiwemo bao moja alilofunga katika ushindi wa mabao 5-0 waliopata kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Leicester City Desemba mwaka jana.

Monday, July 24, 2017

MORATTA APEWA NAMBA 9 CHELSEA.

KLABU ya Chelsea, imethibitisha kuwa nyota mpya Alvaro Morata aliyesajiliwa hivi karibuni atakuwa anavaa jezi yenye namba 9 katika msimu wa 2017-2018. Chelsea ilikamilisha usajili wa mshambuliaji huyo kutoka Real Madrid kwa kitita cha paundi milioni 70 Julai 21 mwaka huu na kumpa mkataba wa miaka mitano. Na sasa klabu hiyo imebainisha kuwa Morata atakuwa akivaa jezi namba 9 ambayo haikuwa ikivaliwa na mchezaji yeyote msimu uliopita. Mchezaji wa mwisho kuvaa jezi yenye namba hiyo alikuwa Radamel Falcao ambaye aliivaa msimu wa 2015-2016.

ANCELOTTI AKOMAA NA ARTURO VIDAL.

MENEJA wa Bayern Munich, Carlo Ancelotti amedai kuwa hakuna uwezekano wa Arturo Vidal kuondoka katika klabu hiyo lakini amekiri kuwa Renato Sanchez anaweza kuondoka. Kuna tetesi kuwa United ilikuwa ikiwawania viungo hao lakini Ancelotti amekanusha kuwa Vidal hatakwenda popote kipindi hiki cha majira ya kiangazi. Akizungumza na wanahabari kuhusiana na suala hilo, Ancelotti amesema hakuna uwezekano huo kwani Vidal ni mchezaji wao na ana uhakika na hilo. Kuhusu suala la Sanchez Ancelotti alikiri kuwa kuna uwezekano nyota huyo akabaki au akaondoka lakini kwa hivi sasa bado wako naye na anafanya mazoezi

CONTE ATOA HOFU HALI YA PEDRO.

MENEJA wa Chelsea, Antonio Conte amesema Pedro alipata majeraha kadhaa kufuatia kugongana na kipa wa Arsenal David Ospina kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika Jumamosi iliyopita lakini anatarajiwa kurejea mazoezi ndani ya siku 10 zihazo. Winga huyo mwenye umri wa miaka 29 alikimbizwa hospitalia kufuatia mchezo huo uliofanyika jijini Beijing, ambapo Chelsea walishinda mabao 3-0 na kulazwa kwa siku moja. Pedro pia alipata mtikisiko wa ubongo lakini alituma ujumbe akidai kuwa kila kitu kiko sawa kabla ya kusafiri kurejea jijini London. Pedro anatarajiwa kuvaa kitu cha kukinga uso wake wakati atakaporejea mazoezini. Kikosi cha Chelsea kilichosalia kwasasa kiko Singapore ambapo watacheza mechi mbili dhidi ya Bayern Munich kesho na Inter Milan Julai 29

MENDY RASMI MAN CITY.

BEKI wa Monaco Benjamin Mendy amekamilisha usajili wake wa paundi milioni 52 kwenda Manchester City. Beki huyo wa kushoto wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 23, ambaye alijiunga na Monaco akitokea Marseille kiangazi mwaka jana, amesaini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo. Mendy anakuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na City kipindi hiki cha usajili wa kiangazi na kupelekea klabu hiyo kutumia zaidi ya paundi milioni 200. Mendy ameichezea mechi 34 Monaco msimu uliopita na kuisaidia kushinda taji lao la kwanza la Ligue 1 baada ya kupita miaka 17. Mbali na Mendy nyota wengine waliosajiliwa na City mpaka sasa ni pamoja na nyota wa kimataifa wa Kyle Walker paundi milioni 45, kiungo wa kimataifa wa Ureno Bernardo Silva paundi milioni 43, kipa wa kimataifa wa Brazil Ederson Moraes paundi milioni 35 na kiungo Danilo kutoka Real Madrid paundi milioni 26.5.

VAN DIJK AACHWA KIKOSI CHA SOUTHAMPTON.

NAHODHA wa Southampton Virgil van Dijk ameondolewa katika kikosi cha timu hiyo ambacho kitakwenda kuweka kambi mazoezi nchini Ufaransa wiki hii. Beki huyo mwneye umri wa miaka 26, amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Liverpool, ingawa klabu hiyo ya Anfield ilidai mwezi uliopita kuwa wameshaacha kumfuatilia. Southampton tayari ilishaweka wazi kuwa hawana mpango wowote wa kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi. Wiki iliyopita meneja wa Southampton Mauricio Pellegrino amesema kuwa Van Dijk amekuwa akifanya mazoezi mwenyewe kwasababu anadhani mchezaji huyo hayuko sawa kwa asilimia 100. Van Dijk ambaye alijiunga na Southampton mwaka 2015 akitokea Celtic, alisafiri na kikosi cha timu hiyo kilichofanya ziara ya maandalizi ya msimu mpya huko Austria mapema mwezi huu lakini Pellegrino ameamua kumuacha kwenye safari yao ya Ufaransa.

Thursday, July 20, 2017

MAJERUHI YAMKOSESHA THIAGO ALCANTARA PRE-SEASON.

KIUNGO Thiago Alcantara anatarajiwa kukosa mechi kadhaa za Bayern Munich kujiandaa na msimu mpya dhidi ya AC Milan, Chelsea na Inter Milan kutokana na majeruhi ya misuli. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania hakuwepo katika kikosi cha Bayern kilichocheza mechi ya Kombe la Ubingwa wa Kimataifa dhidi ya Arsenal iliyofanyika huko Shanghai jana na anatarajiwa kurejea nchini Ujerumani kwa matibabu. Thiago alianza katika mechi 26 msimu uliopita akiwa na Bayern na kuisaidia kutwaa taji la tano mfululizo la Bundesliga ikiwa ni msimu wake mzuri kati ya minne aliyochezea timu hiyo. Meneja wa Bayern, Carlo Ancelotti amesema kwa pamoja yeye, madaktari na mchezaji wameamua ataendelea na kufanya mazoezi binafsi nyumbani wakati akijiuguza majeruhi yake hayo. Bayern wanatarajiwa kurejea katika mechi za ushindano Agosti 5 wakati watakapovaana na Borussia Dortmund katika mchezo wa DFL Supercup.

WEST HAM YAKARIBIA KUMNASA CHICHARITO.

KLABU ya West Ham United inakaribia kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Mexico Javier Hernandez kutoka Bayer Leverkusen. Klabu hiyo ina uhakika wa kusamjili mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United mwenye umri wa miaka 29, ingawa hakuna ada yeyote iliyowekwa wazi. Kwa upande mwingine, mshambuliaji wa Austria Marko Arnautovic anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya katika muda wa saa 48 zijazo baada ya West Ham kufikia makubaliano na Stoke City. Ofa mbili za West Ham zilikataliwa lakini inaaminika kuwa sasa Stoke wamekubali kupokea ada inayokadiriwa kufikia paundi milioni 24.

MILAN YATHIBITISHA KUMNASA BONUCCI.

KLABU ya AC Milan imethibitisha rasmi kumnasa beki Leonardo Bounucci kutoka Juventus ya Italia. Milan imemnasa nyota huyo wa kimataifa wa Italia kwa mkataba wa miaka na ada inayokadiriwa kufikia euro milioni 42. Milan ilithibitisha Ijumaa iliyopita kuwa wamefikia makubaliano ya kumsajili Bonucci mwenye umri wa miaka 30, wakisubiri vipimo vyake vya afya. Lakini sasa Milan chini ya meneja Vincenzo Montella amebainisha kuwa usajili huo umekamilika.  Meneja wa Milan, Montella amesema Bonucci ni mchezaji mwenye uzoefu wa kimataifa na kiufundi anadhani yeye pamoja na Sergio Ramos ndio mabeki bora wa kati duniani.

JUVENTUS YANASA BEKI WA AC MILAN.

KLABU ya Juventus imefanikiwa kumnasa beki wa kimataifa wa Italia Mattia De Sciglio kwa kitita cha euro milioni 12 kutoka AC Milan. Beki huyo amesajiliwa kwa mkataba wa miaka mitano na mabingwa hao wa Serie A na hatakuwa sehemu ya mabadiliko ya Milan chini meneja wake Vincenzo Montella. Beki huyo wa kulia anategemewa kuchukua nafasi ya Dabi Alves, baada ya nyota huyo wa kimataifa wa Brazil kutimkia Paris Saint-Germain-PSG kufuatia kukaa msimu mmoja jijini Turin. Ujio wa De Sciglio umekuja siku moja baada ya Juventus kumsajili Wojciech Szczesny kutoka Arsenal na kuongeza idadi ya wachezaji waliosajili akiwemo Rodrigo Bentancur na Douglas Costa.

MORATA AFURAHIA KUUNGANA TENA NA CONTE.

MSHAMBULIAJI Alvaro Morata amefurahishwa kwenda kuungana na Antonio Conte katika klabu ya Chelsea, akidai kuwa meneja huyo wa Italia ndiye aliyeonyesha kumuamini zaidi katika soka lake. Real Madrid na Chelsea zilifikia makubaliano juu ya uhamisho wa nyota huyo wa kimataifa wa Hispania jana, kwa ada inayoaminika kufikia paundi milioni 70. Mara kadhaa Morata amewahi kukiri kuwa deni kwa Conte, ambaye ndiye aliyemchukua akiwa chipukizi Juventus, lakini hakuwahi kumfundisha kufuatia kuchukua kibarua cha kuinoa timu ya taifa ya Italia. Kufuatia kufunga mabao 15 katika mechi 14 pekee za La Liga alizocheza akiwa na Madrid msimu uliopita, Morata anaamini hatimaye chini ya Conte anaweza kumsaidia kuimarika zaidi. Akizungumza na wanahabari nchini Hispania kabla ya kwenda London, Morata amesema anakwenda kwenye timu ambayo inanolewa na kocha ambaye alimuamini na hilo ni jambo kubwa kwake.

MOURINHO ALIA NA USAJILI MGUMU.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amesema anaweza kufanya usajili wa mchezaji mmoja zaidi kwasababu ya ugumu wa dirisha la usajili kipindi hiki cha majira ya kiangazi. Mourinho amedai kuwa klabu nyingi zinahitaji kiasi walichoweka kwa ajili ya wachezaji. Akizungumza na wanahabari kuhusiana na suala hilo, Mourinho ambaye ameshasajili wachezaji wawili kati ya wanne aliohitaji amesema United sio klabu iliyoko tayari kulipa kiasi ambacho klabu zinataka. Mourinho aliendelea kudai kuwa amezoea klabu zinazotoa fedha nyingi kwa wachezaji wakubwa, sasa kila mtu analipa fedha nyingine kwa mchezaji mzuri. United imetumia kitita cha paundi milioni 75 kwa ajili ya mshambuliaji wa Everton Romelu Lukaku na kiasi cha paundi milioni 31 kwa ajili ya beki wa Benfica Victor Lindelof.

VIONGOZI WA SIMBA WAENDELEA KUSOTA RUMANDE.

KESI inayowakabili viongozi wa klabu ya Simba, rais Evans Aveva na makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ imeahirishwa tena mpaka Julai 31 mwaka huu itakapotajwa tena. Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka matano yakiwemo ya utakasishaji fedha, ambayo hayana dhamana na wote wako rumande gereza la keko toka Juni 29 mwaka huu. Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000. Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo. Kesi hiyo iliyotajwa mapema leo katika Mahakama ya hakimu Mkazi, Kisutu iliahirishwa na Hakimu Victoria Nongwa kutokana na uchunguzi kutokamilika. Aveva aliwasili mahakamani hapo akiwa mwenyewe kutokana na Kaburu kusumbuliwa na mardhi na yupo katika zahanati ndogo katika gereza hilo.

Tuesday, July 18, 2017

STARS YAIFUATA MAPEMA AMAVUBI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga ametangaza mabadiliko kidogo katika mipango yake ya kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi Rwanda unaotarajiwa kufanyika Jumamosi hii. Awali Stars walikuwa wafanye mazoezi kwa muda wa siku tatu jijini Mwanza yaani Jumatatu, Jumanne na Jumatano kabla ya kuanza kufunga safari kuelekea jijini Kigali kwa ajili ya mchezo wao huo. Akizungumza na wanahabari mapema leo, Ofisa habari wa Shirikisho la Soka nchini-TFF, Alfred Lucas amesema Stars sasa haitafanya tena mazoezi kesho na badala yake watasafiri kurejea jijini Dar es Salaam na kuunganisha moja kwa moja mpaka Kigali. Lucas amesema sababu kubwa na kocha Mayanga kufanya hivyo ni kutoa nafasi zaidi kwa kikosi cha Stars kuzoea mazingira na hali ya hewa ya huko kabla ya mchezo wao huo muhimu wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani-CHAN. Kwenye mchezo wa kwanza Stars walitoka sare ya ya bao 1-1 dhidi ya Rwanda na sasa wanahitaji ushindi wa aina yeyote au sare ya mabao kuanzia 2-2 ili waweze kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu michuano hiyo.

SZCZESNY ATUA TURIN KUMALIZIA UHAMISHO WA JUVENTUS.

KIPA wa Arsenal, Wojciech Szczesny anakaribia kusajiliwa rasmi na Juventus kufuatia mabingwa wa Serie A kutangaza kutuma ujumbe wa ujuo wake katika ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa Twitter. Klabu hiyo iliandika ujumbe kwenye ukurasa huo sambamba na picha ukiwahabalisha mashabiki wao ujuio wa kipa huyo. Vyombo vya habari nchini Uingereza vilitoa taarifa jana kuwa Arsenal wamekubali kitita cha euro milioni 10 kwa ajili ya kumuachia Szczesny ambaye misimu miwili iliyopita amekuwa akicheza kwa mkopo AS Roma. Msimu uliopita Szczesny alicheza mechi zote 38 za Serie A akiwa na Roma na kumaliza akiwa hajafungwa katika mechi 14 kati ya hizo. Kipa huyo mwenye umri wa miaka 27, amekubali kwenda kuwa kipa namba mbili Juventus nyuma ya mkongwe Gianluigi Buffon.

LUKAKU AFUNGUA PAZIA LA MABAO UNITED, MOURINHO AMFAGILIA.

MSHAMBULIAJI Romelu Lukaku amefunga bao lake la kwanza akiwa Manchester United kufuatia ushindi wa mabao 2-1 waliopata katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Real Salt Lake uliofanyika huko Utah mapema leo Alfajiri. Lukaku ambaye amejiunga na United akitokea Everton kwa kitita cha paundi milioni 75 wiki iliyopita, alifunga bao hilo dakika ya 38 akimalizia pasi murua ya Henrikh Mkhitaryan. Nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 24 pia alihusika katika bao la kusawazisha lililofungwa na Mkhitaryan dakika ya 29 baada ya Luis Silva kuifungia Salt Lake bao la kuongoza. Akizungumza na wanahabari kuhusiana na hilo, meneja wa United Jose Mourinho amesema bao hilo la Lukaku ni muhimu kwake na alishamwambia kabla ya mchezo huo kuwa anapenda kila kitu anachofanya. Ijumaa hii United inatarajiwa kuchuana na Manchester City kwenye mchezo mwingine wa kirafiki utakaofanyika jijini Houston.

POLISI WAMSHIKILIA "MALINZI" WA HISPANIA KWA TUHUMA ZA UBADHILIFU.

POLISI nchini Hispania imedai kumshikilia rais wa Shirikisho la Soka la Hispania na mtoto wake wa kiume ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa masuala ya rushwa. Rais huyo Angel Maria Villar Llona mwenye umri wa miaka 67 alikamatwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha. Villar ambaye amewahi kuwa mchezaji wa zamani wa nchi hiyo, amekuwa rais wa shirikisho hilo toka mwaka 1988. Mwanaye Gorka pia ni miongoni mwa watu kadhaa wengine waliokamatwa wakati wa msako huo uliofanyika mapema leo.

STURRIDGE YUPO FITI - KLOPP.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema mshambuliaji Daniel Sturridge yuko katika hali bora kuliko wakati wote aliokuwepo hapo. Majeruhi ya mara kwa mara yalimfanya nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 kucheza mechi 46 pekee katika miezi mitatu iliyopita. Klopp ambaye alichukua mikoba ya kuinoa Liverpool Octoba mwaka 2015, amesema Sturridge yuko katika hali njema na anaweza kucheza mechi zote za maandalizi ya msimu mpya. Liverpool pia imekuwa ikihusishwa na tetesi za kumuwania kiungo wa RB Leipzig Naby keita lakini Klopp amesema kwasasa hawezi kusema lolote kuhusiana na nmyota huyo wa kimataifa wa Guinea.

LEICESTER HAIJAPATA OFA KWA MAHREZ - SHAKESPEARE.

MENEJA wa Leicester City, Craig Shakespeare amedai kuwa hawajapokea ofa yeyote kwa ajili ya Riyad Mahrez pamoja na winga huyo kuhusishwa na tetesi za kuwania na Arsenal na AS Roma. Mustakabali wa Mahrez bado haujajulikana toka Leicester watwae taji la Ligi Kuu msimu wa 2015-2016 ambapo nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 aliamua kubakia msimu uliopita ili aweze kuwa sehemu ya kikosi katika kampeni zao za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Baada ya Leicester kumaliza katika nafasi ya 12 msimu wa 2016-2017, Mahrez alithibitisha nia yake ya kuondoka Uwanja wa King Power kwa kutoa taarifa hiyo Mei mwaka huu lakini mpaka sasa bado amebakia kuwa mchezaji wa Leicester. Roma wana matumaini ya kumsjaili nyota huyo wa kimataifa wa Algeria na kuna taarifa kuwa anaweza kukubali kwenda Italia kama Arsenal wasipomtafuta. Akizungumza na wanahabari, Shakespeare amesema anadhani Mahrez aliweka wazi msimu wake lakini mpaka sasa hakuna timu yeyote iliyotuma ofa rasmi hivyo ataendelea kuwa mchezaji wao.

Monday, July 17, 2017

DIEGO COSTA APIGA PICHA AKIWA NA JEZI YA ATLETICO.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Hispania, Diego Costa amepiga picha za video akifurahia likizo yake huku akiwa amevaa jezi ya Atletico Madrid. Katika picha hizo za video kwenye mtandao wake wa Instagram, nyota huyo alivaa jezi ya timu yake hiyo ya zamani, huku akiandika ujumbe kwa mchezaji mwenzake Cesc Fabregas kuwa amkumbatie meneja wao Antonio Conte. Mustakabali wa Costa bado haujawekwa sawa toka nyota huyo alipobainisha kuwa Conte alimwambia kuwa hahitajiki tena kwenye klabu hiyo. Matokeo hayo yamemfanya Costa mwenye umri wa miaka 28 kuachwa katika kikosi cha Chelsea kilichoanza maandalizi ya msimu mpya huku kukiwa na matumaini ya kupata klabu mpya.

HART KUFANYIWA VIPIMO VYA AFYA WEST HAM.

KIPA Joe Hart anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya katika klabu ya West Ham United ili kukamilisha uhamisho wake wa mkopo kutoka Manchester City. West Ham walikuwa wakitafuta kipa mpya kipindi hiki cha majira ya kiangazi na wamefanikiwa kumshawishi kipa huyo wa kimataifa wa Uingereza. Mkataba wa Hart unatarajiwa kumalizika mwaka 2019 katika klabu ya City na inadaiwa kuwa tayari alishaambiwa atafute klabu mpya na meneja Pep Guardiola. City walimruhusu Hart aende kwa mkopo katika klabu ya Torino msimu uliopita na sasa anatarajiwa kuhamia Uwanja wa London huku Guardiola akiwa tayari kumlipa nusu ya mshahara wake.

Monday, July 10, 2017

ROONEY ADOKEZA ZIARA YA TANZANIA.

MSHAMBULIAJI mpya wa Everton, Wayne Rooney amesema anasubiri kwa hamu ziara ya Tanzania akiwa na klabu hiyo. Rooney aliyerejea Everton baada ya kupita miaka 13, anatarajiwa kuwa kwenye kikosi cha timu hiyo ambacho kitatua Tanzania kwa ajili ya mechi moja ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya. Akizungumza na luninga ya klabu hiyo, Rooney amesema anaisubiri kwa hamu ziara hiyo ya kwenda Tanzania kani anadhani itakuwa safari nzuri itakayomuwezesha kufahamiana vyema na wenzake. Rooney aliendelea kuwa ziara kama hizo huwa nzuri kwani ni vizuri kukaa hotelini na wachezaji, kujumuika nao na kuwafahamu zaidi. Rooney amesema hajawahi kufika Tanzania hivyo ana hamu kubwa ya kutua katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

COSTA AACHWA KIKOSI CHA CHELSEA KINACHOANZA ZIARA YA MAANDALIZI YA MSIMU MPYA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Hispania, Diego Costa hajajiunga na kikosi cha Chelsea kwa ajili ya mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya baada ya kupewa ruhusa ili aweze kukamilisha uhamisho wake kwenda Atletico Madrid. Atletico ndio imebaki chaguo pekee kwa Costa ambaye tayari alishahabalishwa na meneja Antonio Conte kwa njia ya ujumbe kuwa hahitajiki Stamford Bridge mwezi uliopita. Chelsea na Atletico tayari zimeanza mazungumzo lakini hawajafikia muafaka kuhusu ada na Costa anaonekana yuko radhi kukubali chochote atakachoambiwa na klabu yake hiyo ya zamani. Kufuatia kushindwa na Manchester United katika mbio za kumuwania Romelu Lukaku, Chelsea watalazimika kuingia sokoni tena kutafuta mbadala wa Costa kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa Ligi Kuu.

LUKAKU AAGA RASMI EVERTON.

MSHAMBULIAJI Romelu Lukaku ametuma ujumbe wa kuaga kwa klabu ya Everton wakati akijiandaa kukamilisha usajili wake kwenda Manchester United. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alifanyiwa vipimo vya afya mwishoni mwa wiki iliyopita na anatarajiwa kusajili na United kwa kitita cha paundi milioni 75, pamoja na klabu yake ya zamani ya Chelsea nayo kufikia kiwango hicho. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji akitua Everton akitokea Chelsea kwa kitita cha paundi milioni 28 Julai mwaka 2014 na ameshafunga mabao 68 katika Ligi Kuu. Lukaku alituma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram akiwashukuru watu wote waliofanya kazi pamoja Everton. Lukaku pia aliwashakuru mashabiki kwa kumuunga kwa muda wote wa miaka minne aliyokuwa nao pamoja na ni heshima kubwa kucheza mbele yao.

Thursday, July 6, 2017

RB LEIPZIG YAIBANIA LIVERPOOL KWA KEITA.

KLABU ya Liverpool imepata pigo lingine katika jitihada zao za kuwania kumsajili kiungo wa RB Leipzig, Naby Keita kufuatia klabu hiyo ya Bundesliga kuzizitiza hatamuuza kwa bei yeyote ile. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22, anawindwa kwa udi na uvumba na meneja Jurgen Klopp baada ya kuisaidia Ujerumani kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita juu ya Borussia Dortmund lakini wakiachwa kwa mbali kidogo na Bayern Munich. Taarifa zilikuwa zinadai Liverpool walihitajika kuvunja rekodi ya usajili Bundesliha kwa kutoa paundi milioni 66 katika mbio zao za kumuwania Keita lakini sasa ndoto hizo zinaonekana kuyeyuka. Akizungumza na wanahabari kuhusiana na suala hilo, afisa usajili wa Leipzig, Ralf Rangnick amesema hawana mpango wowote wa kuachia wachezaji wao muhimu kuondoka kipindi hiki. Liverpool wanataka kuongeza kiungo wa kati, beki wa kushoto na beki wa kati kabla ya kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu baada ya kuwa tayari wameshawasajili winga Mohamed Salah kutoka AS Roma na mshambuliaji Dominic Solanke kutoka Chelsea.

TANZANIA YAKWEA VIWANGO FIFA.

TANZANIA imekwea kwa nafasi 25 katika viwango vya ubora duniani vinavyotolewa kila mwezi na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Katika viwango vilivyopita ambavyo vilitolewa Juni mosi Tanzania ilishuka kwa nafasi nne mpaka nafasi ya 139 lakini kwenye viwango vipya vilivyotolewa mapema leo imekwea mpaka nafasi ya 114. Mbali na kukwea viwango hivyo duniani lakini pia kwa upande wa Afrika Mashariki nako wamepanda mpaka nafasi ya tatu baada ya kushika nafasi ya 30 kwa upande wa Afrika wakizidiwa na Uganda waliopo nafasi ya 74 duniani na 15 Afrika na Kenya waliopo nafasi ya 84 duniani na 18 Afrika. Nchi zingine za Afrika Mashariki ni Burundi waliopo nafasi 121 duniani na 35 kwa Afrika, Rwanda nafasi ya 127 duniani na 36 na Sudan Kusini ndio wa mwisho wakishika nafasi ya 143 duniani na 43 Afrika. Kwa upande wa Orodha za Afrika Misri ndio kinara akishika nafasi ya 24 duniani akifuatiwa na Senegal waliopo nafasi ya 27, jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC nafasi ya 28, Tunisia nafasi ya 34 na wa tano ni mabingwa wa Afrika Cameroon waliopo nafasi ya 36. Katika orodha za jumla mabingwa wa dunia na Kombe la Shirikisho Ujerumani wamerejea kileleni wakifuatiwa na Brazil katika nafasi ya pili, Argentina nafasi ya tatu, Ureno nafasi ya nne na Switzerland nafasi ya tano.

WENGER AELEZA SABABU ZA KUVUNJA BENKI KWA LACAZETTE.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amebainisha kitu alichokiona kwa Alexandre Lacazette na kwanini ana uhakika nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa ataweza kuisaidia timu hiyo kushindana katika kiwango cha juu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amesajiliwa Arsenal akitokea Olympique Lyon kwa mkataba wa miaka mitano huku ada ya paundi milioni 52 ikiweka rekodi mpya na kuizidi ile ya Mesut Ozil aliyosajiliwa kwa kitita cha paundi milioni 42.5 kutoka Real Madrid mwaka 2013. Lacazette pia anatarajiwa kulipwa kitita cha paundi 200,000 kwa wiki, kiasi cha ambacho kitamfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi Emirates. Wenger amesema amefurahishwa na nyota huyo kujiunga nao kwani kwa miaka mingi ameonyesha anaweza kufunga mabao na ni mshambuliaji mwenye ufanisi wa hali ya juu, sambamba na ufundi na tabia njema.

MAN UNITED YAKUBALI KUTOA PAUNDI MILIONI 75 KWA LUKAKU.

KLABU ya Manchester United inadaiwa kukubali kutoa kiasi kinachofikia paundi milioni 75 kwa ajili ya mshambuliaji wa Everton Romelu Lukaku. Nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 24 amefunga mabao 25 katika Ligi Kuu msimu uliopita. United ambao wamekuwa wakimfukuzia Lukaku zaidi kipindi hiki cha kiangazi, sasa hawadhaniwi kama watamuwania tena mshambuliaji wa Real Madrid Alvaro Morata. Uhamisho huo wa Lukaku hauhusiani na mazungumzo yaliyofanywa na mshauri wa Wayne Rooney pamoja na mwenyekiti wa Everton juu ya uwezekano wa nyota huyo kurejea tena katika timu hiyo. Meneja wa United, Jose Mourinho ana matumaini dili hilo litakalimika kwa wakati ili aweze kumjumuisha Lukaku katika kikosi chake kabla ya kuanza ziara ya maandalizi ya msimu mpya huko Marekani Jumapili hii.

BARCELONA WATOSWA KWA PAULINHO.

KLABU ya Barcelona imekataliwa ofa yao ya paundi milioni 20 kwa ajili ya kumuwania kiungo wa zamani wa Manchester City, Paulinho ambaye kwasasa anakipiga katika timu ya Guangzhou Evergrande. Klabu hiyo ya China imetoa taarifa mapema leo kuwa Barcelona walituma ofa yao rasmi kwa ajili ya nyota huyo wa kimataifa wa Brazil lakini wamekataa kwakuwa hawana mpango wa kumuuza. Taarifa hiyo ilidai kuwa Paulinho tayari alishaongeza mkataba Januari mwaka huu na ni mchezaji muhimu katika kikosi chao kwasasa hivyo hawawezi kumuacha. Klabu hiyo pia imetoa shukrani kwa Barcelona ambao wameonyesha kumuhusudu sana Paulinho.

RUDIGER AELEZA MAHABA YAKE KWA ARSENAL.

BEKI wa kimataifa wa Ujerumani, Antonio Rudiger anaweza kujiingiza katika bifu zito na mashabiki wa Chelsea kufuatia kauli yake aliyotoa kabla ya kujiunga na mabingwa hao wa Uingereza. Rudiger amekubali kujiunga na Chelsea na kwasasa inadaiwa tayari yuko jijini London kwa ajili ya vipimo vya afya kabla ya kukamilisha usajili huo unaodaiwa kufikia paundi milioni 36. Lakini pamoja na kwenda Chelsea, nyota huyo amekiri hadharani kuwa anaihusudu sana Arsenal na amekuwa akiifuatilia kwa kipindi kirefu. Rudiger amesema amekuwa akiifuatilia Arsenal toka enzi za kina Thierry Henry na Dennis Bergkamp na kwamba moyo wake unaipenda klabu hiyo. Beki huyo anatarajia kupewa mkataba wa miaka mitano na Chelsea.

Wednesday, July 5, 2017

TORRES AONGEZA MWAKA MMOJA ATLETICO.

MSHAMBULIAJI wa Atletico Madrid, Fernando Torres amesaini mkataba wa mwaka mmoja ambao utamuweka katika klabu hiyo mpaka Juni mwaka 2018. Akizungumza na tovuti ya klabu hiyo mara baada ya kusaini mkataba huo, Torres amesema amefurahishwa kuendelea kubakia hapo kwa mwaka mmoja zaidi. Baada ya kuibuka katika kikosi cha kwanza cha Atletico mwaka 2001, mshambuliaji huyo aliimarika na kuwa nahodha kabla ya kujiunga na Liverpool mwaka 2007. Torres ambaye ametwaa mataji mwili ya Ulaya na moja la Kombe la Dunia akiwa na Hispania, pia amecheza kwa vipindi vifupi Chelsea na AC Milan kabla ya kurejea Atletico mwaka 2015.

LACAZETTE ASAINI MIAKA MITANO ARSENAL.

KLABU ya Arsenal imefanikiwa kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa Alexandre Lacazette kutoka Olympique Lyon kwa kitita kilichovunja rekodi ya klabu cha paundi milioni 46.5 na kupewa mkataba wa miaka mitano. Ada hiyo ambayo inaweza kufikia hadi paundi milioni 52.6 ukijumlisha na nyongeza nyingine, itaipita ile ya paundi milioni 42.4 Arsenal waliyolipa Real Madrid kwa ajili ya Mesut Ozil mwaka 2013. Akizungumza na wanahabari, Lacazette amesema Arsenal ni klabu inayocheza soka la kupendeza nchini Uingereza hivyo alihitaji sana kuja kuichezea. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 anatarajiwa kusafiri na kikosi cha timu hiyo mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki jijini Sydney wiki ijayo.

MADRID YAVUNJA MWIKO WA MIAKA 17 KWA KUNASA KINDA KUTOKA ATLETICO.

KLABU ya Real Madrid imefanikiwa kumsajili beki wa kushoto Theo Hermandez kutoka kwa mahasimu wao wa jiji Atletico Madrid na kumpa mkataba wa miaka sita. Hernandez anakuwa mchezaji wa kwanza katika kipindi cha miaka 17 kusajiliwa moja kwa moja kutoka Atletico baada ya kiungo wa kimataifa wa Argentina, Santiago Solari kufanya hivyo mwaka 2000. Chipukizi huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 19 alishindwa katika kikosi cha kwanza cha Atletico na kuutumia msimu uliopita kwa mkopo kwenye kikosi cha Alaves. Akiwa Alaves amecheza mechi 38 za mashindano yote ikiwemo fainali ya Kombe la Mfalme ambapo walifungwa na Barcelona. 
Katika hatua nyingine beki Fabio Coentrao amejiunga na klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno kwa mkopo wa mwaka mmoja. Coentrao alijiunga na Madrid akitokea kwa mahasimu wa Sporting, Benfica kwa kitita cha paundi milioni 27 mwaka 2011 na kufanikiwa kushinda taji moja la La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Tuesday, July 4, 2017

MONCHENGLADBACH YANASA BEKI WA DORTMUND.

KLABU ya Borussia Monchengladbach imefanikiwa kumsajili beki wa kimataifa wa Ujerumani Matthias Ginter kutoka Borussia Dortmund kwa kitita cha euro milioni 17. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 amesaini mkataba unaomalizika mwaka 2021 kuitumikia klabu hiyo. Ginter alikuwa sehemu ya kikosi cha Ujerumani kilichoitandika Chile bao 1-0 Jumapili iliyopita na kutwaa taji la michuano ya Kombe la Shirikisho. Mkurugenzi wa michezo wa Dortmund, Michael Zorc amesema Ginter alimueleza nia yake ya kuondoka kwasababu ya ushindani wa nafasi uliopo kwenye kikosi cha timu hiyo.

MWAMUZI ASHAMBULIWA KUFUATIA KUTOA PENATI YENYE UTATA.

CHAMA cha soka cha China-CFA kimethibitisha kuwa kundi la watu 10 limewashambulia waamuzi kufuatia sare yenye utata iliyopatikana katika mchezo wa Ligi Daraja la Pili nchini humo. Mwamuzi wa kati na wasaidizi wake walishambuliwa katika vyumba vya hoteli waliyofikia muda mfupi baada ya umeme kukatwa. Taarifa ya CFA imedai kuwa waamuzi hao waliachwa na majeraha ya kichwani, kiuno na miguu na tayari polisi wameanza uchunguzi wa tukio hilo. Tukio hilo limetokea kufuatia mchezo uliomalizika kwa utata kati ya Baoding Rongda na Wuhan Zall ambao ulicheza Jumamosi iliyopita.

MOURINHO ACHUKIZWA NA USJAILI WA UNITED.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amedaiwa kutofurahishwa na taratibu za klabu hiyo katika usajili wa kipindi hiki cha kiangazi. Baada ya United kutwaa taji la michuano ya Europa League Mei 24 mwaka huu, Mourinho amesema alimpa makamu mwenyekiti Ed Woodward orodha na wachezaji anawahitaji katika usajili. Taarifa za ndani zinadai kuwa orodha hiyo ilikuwa na mahitaji machache ya wachezaji watatu au wanne pekee. Kuna uwezekano kukawa na maendeleo mengine wiki hii lakini mpaka sasa ni mchezaji mmoja mpya aliyesajili ambaye ni beki wa Benfica, Victor Lindelof aliyetua Old Trafford kwa kitita cha paundi milioni 31. Inaaminika kuwa Mourinho anataka angalau mshambuliaji mmoja ili kuziba nafasi ya Zlatan Ibrahimovic pamoja na mchezaji wa nafasi ya kiungo wa ulinzi.

ARSENAL YASUBIRI VIPIMO KUKAMILISHA USAJILI WA LACAZETTE.

KLABU ya Arsenal inadaiwa kujipanga kumtangaza Alexandre Lacazette kuwa mchezaji wao mpya baada ya kufikia makubaliano ya kumsajili na Olympique Lyon. Arsenal wamekuwa wakimfukuzia mshambuliaji huyo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita na walikataliwa mara mbili na Lyon katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi mwaka jana. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger anadaiwa kwenda nchini Ufaransa mwezi uliopita lakini alikataliwa tena kabla ya taarifa ya makubaliano kutolewa wiki iliyopita. Taarifa kutoka nchini Ufaransa zinadai kuwa Lacazette sasa anaweza kusaini mkataba huo na Arsenal wakati wowote kutokea sasa.

KOREA KUSINI WAPATA KOCHA MPYA.

CHAMA cha Soka cha Korea Kusini, kimemteua Shin Tae-yong kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 46 ambaye enzi zake alikuwa akicheza nafasi ya kiungo, anachukua nafasi ya Uli Stielike wa Ujerumani aliyetimuliwa mwezi uliopita kufuatia kupata matokeo mabaya ambayo yamefanya kuhatarisha nafasi ya Korea Kusini kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Shin ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja, aliichezea kwa misimu 12 klabu ya Ilhwa Chunma ya nchi hiyo huku pia akicheza mechi 13 katika kikosi cha timu ya taifa. Shin amekuwa sehemu ya benchi la ufundi la kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya nchi hiyo toka mwaka 2015 na alikiongoza kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 kutinga hatua ya mtoano ya 16 kwenye michuano ya Kombe la Dunia iliyofayika kwenye ardhi yao mapema mwaka huu.