Thursday, July 20, 2017

VIONGOZI WA SIMBA WAENDELEA KUSOTA RUMANDE.

KESI inayowakabili viongozi wa klabu ya Simba, rais Evans Aveva na makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ imeahirishwa tena mpaka Julai 31 mwaka huu itakapotajwa tena. Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka matano yakiwemo ya utakasishaji fedha, ambayo hayana dhamana na wote wako rumande gereza la keko toka Juni 29 mwaka huu. Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000. Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo. Kesi hiyo iliyotajwa mapema leo katika Mahakama ya hakimu Mkazi, Kisutu iliahirishwa na Hakimu Victoria Nongwa kutokana na uchunguzi kutokamilika. Aveva aliwasili mahakamani hapo akiwa mwenyewe kutokana na Kaburu kusumbuliwa na mardhi na yupo katika zahanati ndogo katika gereza hilo.

No comments:

Post a Comment