Tuesday, January 31, 2017

AFCON 2017: WACHEZAJI CAMEROON WALILIA POSHO ZAO.

WACHEZAJI wa timu ya taifa ya Cameroon waligoma kufanya mazoezi jana huko Gabon kufuatia sakata la kutopewa posho zao. Kikosi hicho kinachojulikana kama Indomitable Lions kinataka posho hiyo iliyotokana na kiwango bora walichoonyesha katika mchezo wa robo fainali na kuiondoa Senegal iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri, kwa changamoto ya mikwaju ya penati 5-4. Taarifa kutoka katika kambi ya timu hiyo zinadai kuwa wachezaji hao wanaonolewa na kocha Hugo Broos wanalidai Shirikisho la Soka la Cameroon fedha zao za bakshishi kwa kufanikiwa kwao kutinga hatua ya nusu fainali. Wachezaji hao wanataka serikali kuingilia kati suala hilo na kulipwa fedha zao kabla ya kuanza tena mazoezi kwa ajili ya mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Ghana Alhamisi hii.

PATO AKAMILISHA USAJILI WAKE CHINA.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea na AC Milan, Alexandre Pato amekuwa mchezaji wa hivi karibuni kwenda China kufuatia kujiunga na klabu ya Tianjin Quanjian. Pato mwenye umri wa miaka 27 amehamia China baada ya kuichezea kwa kipindi kifupi Villarreal ambako amefunga mabao sita katika mechi 24 alizocheza katika mashindano yote. Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Brazil anajiunga na Tianjin ambayo inanolewa na beki nguli wa zamani wa Italia Fabio Canavaro na imepanda msimu huu katika Ligi Kuu ya nchi hiyo inayojulikana kama Chinese Super League. Pato alithibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akidai kuwa anafurahia kujiunga na familia hiyo mpya. Pato aliibuka katika klabu ya Internacional na baadae Milan kabla ya majeruhi ya mara kwa mara kumzuia kung’aa kama ilivyotegemewa.

LEVERKUSEN YANASA CHIPUKIZI WA GENK.

KLABU ya Bayer Leverkusen imekamilisha usajili wa winga chipukizi wa Genk anayetabiriwa kuja kung’aa sana siku za baadae, Leon Bailey. Chipukizi huyo wa kimataifa wa Jamaica amesaini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo ya Bundesliga. Bailey mwenye umri wa miaka 19 amekuwa akiwaniwa na vilabu kadhaa barani Ulaya huku Manchester United ikiwa mojawapo. Mwezi Novemba mwaka jana, Bailey aliweka wazi kuwa kama United wanamuhitaji na hawatamuhakikishia nafasi ya kucheza mara kwa mara atakaa kwenda huko. Liverpool pia waliwahi kuripotiwa kumuwania chipukizi huyo lakini nao walishindwa huku Ajax Amsterdam ikiwa klabu nyingine ya Ligi Kuu iliyokuwa ikimuwania.

N'ZONZI AJITIA KITANZI SEVILLA.

KIUNGO wa Sevilla, Steven N’Zonzi amesaini mkataba mpya ambao utamuweka klabu hapo mpaka Juni mwaka 2020. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Barcelona na Chelsea katika miezi ya karibuni lakini sasa amemaliza uvumi huko kwa kusaini mkataba mpya na Sevilla. Mkataba wake wa awali ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu 2018-2019, lakini sasa amepewa mkataba zaidi baada ya kuonyesha kiwango bora. Taarifa za N’Zonzi kuongeza mkataba mpya zilitangazwa katika mtandao wa klabu hiyo huku kukiwa na uwezekano wa kuongezwa msimu mmoja zaidi. N’Zonzi alijiunga na Sevilla akitokea Stoke City Julai 2015.

AFCON 2017: MAKOCHA WA ULAYA WAENDELEA KUTAMBA.


Duarte
MICHUANO ya Mataifa ya Afrika inayoendelea huko nchini Gabon imefikia hatua nusu fainali huku timu zilizofanikiwa kufika hatua hiyo zote zikiwa zinafundishwa na makocha wa kigeni kutoka bara la Ulaya. Baadhi ya timu zilizokuwa zikifundishwa na makocha wazawa akiwemo Callisto Pasuwa wa Zimbabwe, Baciro Cande wa Guinea Bissau, Florent Ibenge wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC na Aliou Cisse wa Senegal wote wakiwa wameshatolewa. Marehemu Stephen Keshi ndio kocha wa mwisho kupata mafanikio mwaka 2013 wakati Nigeria ilipotwaa taji la michuano hiyo huku kwa mwaka huu Ibenge na Cisse ndio makocha wazawa waliopata mafanikio kwa kuzifikisha timu zao robo fainali. Nguli wa soka wa zamani wa Cameroon, Rodger Milla amesema AFCON ni michuano migumu hivyo inahitaji makocha wa kiwango cha juu, na inafurahisha kuona makocha wazawa wakifanya vyema kiasi kwani hilo litawaongezea nafasi zaidi na pia kujifunza kutoka kwa wenzao wa Ulaya. Kocha wa Hector Cuper wa Misri, Avram Grant wa Ghana, Hugo Broos wa Cameroon na Paulo Duarte wa Burkina Faso ndio pekee walibakia katika michuano hiyo na wote wanatoka Ulaya.

ADEBAYOR ATIMKIA UTURUKI.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu za Arsenal na Tottenham Hotspurs, Emmanuel Adebayor anatarajiwa kukamilisha uhamisho wake kwenda Basaksehir ya Istabul baada ya kukamilihs avipimo vya afya na klabu hiyo. Nyota huyo wa kimataifa wa Togo alikuwa bila timu toka alipoondoka Crystal Palace Juni mwaka 2016 na sasa anatarajiwa kusaini mkataba wa miezi 18 na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Uturuki. Mapema leo Adebayor alituma picha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akifanyiwa vipimo vya afya na nyingine akiwa amevaa jezi ya klabu hiyo. Adebayor alikuwa akifanya mazungumzo na Lyon, lakini inaripotiwa kuwa uhamisho wake ulikwama kutokana na ushiriki wake katika michuano ya Mataifa ya Afrika akiwa na Togo. Akizungumza na wanahabari Adebayor alikiri dili lake la kujiunga na Lyon lilishindikana kwasababu ya ushiriki wake katika michuano hiyo.

MKWASA KATIBU MKUU MPYA YANGA.

KLABU ya Yanga, imemtangaza kocha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa kuwa Katibu Mkuu mpya wa klabu hiyo. Mkwasa ambaye kabla ya kuinoa Taifa Stars aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Yanga, anachukua nafasi ya Baraka Deusdedit ambaye ametolewa na kupewa nafasi ya bwana fedha. Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa wanahabari na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Clement Sanga, Mkwasa amesema atajitahidi kufanya kazi kwa weledi wake wote kuhakikisha timu hiyo inafikia malengo waliyojiwekea. Mkwasa pia aliziasa klabu zingine kufuata nyayo za Yanga kwa kuteua viongozi ambao wanalifahamu soka kwa undani wake. Katika hatua nyingine Sanga aligusia suala la timu hiyo kugoma kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa Afrika Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao wameweka kambi nchini kwa ajili ya kujiwinda na mechi yao Super Cup dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo-DRC. Sanga amesema kikubwa kinachofanya wasikubali wito wa mechi hiyo ni kutokana na suala hilo kuja ghafla huku wakikabiliwa na mechi muhimu ya Ligi Kuu.

Monday, January 30, 2017

RATIBA YA 16 BORA KOMBE LA FA.

Uwanja wa Gander Green Lane wa klabu ndogo ya Sutton United wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 5,000 ambao ndio utatumika kwa ajili ya mechi yao ya Kombe la FA dhidi ya Arsenal. 

Burnley v Lincoln City
Fulham v Tottenham Hotspur
Blackburn Rovers v Manchester United
Sutton United v Arsenal
Middlesbrough v Oxford United
Wolverhampton Wanderers v Chelsea
Huddersfield Town v Manchester City
Millwall v Derby County/Leicester City

ELNENY KUIKOSA NUSU FAINALI YA AFCON.

KIUNGO wa kimataifa wa Misri na klabu ya Arsenal, Mohamed Elneny anatarajiwa kukaa nje katika mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Burkina Faso keshokutwa kutokana na majeruhi. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 bado anajiuguza majeruhi ya misuli ya kigimbi amayo ilimfanya kukosa pia mchezo wa robo fainali walioshinda bao 1-0 dhidi ya Morocco jana usiku. Kocha wa Misri Hector Cuper amesema Elneny bado anasumbuliwa na majeruhi na wanatarajia kutuma vipimo kwa klabu yake huku wakitumaini ataweza kupona na kucheza kama wakitinga hatua ya fainali. Misri wanatarajiwa kuchuana na Burkina Faso katika mchezo wa nusu fainali utakaochezwa katika mji wa Libreville.

BECKHAM ADAI ALIKATAA KWENDA BARCELONA KWA AJILI YA MADRID.

KIUNGO wa zamani wa Manchester United, David Beckham amebainisha jinsi gani klabu ilipofikia makubaliano ya uhamisho wake kwenda Barcelona wakati alipohamia Real Madrid mwaka 2003. Baada ya kutwaa mataji sita ya Ligi Kuu na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Beckham aliachana na United na kujiunga na Madrid kwa kitita cha euro milioni 35. Lakini beckham amesema kuwa United walikuwa tayari wameshaafikiana na Barcelona ingawa baadae aligoma kwasababu alikuwa akitaka kwenda Madrid. Akizungumza na kituo kimoja cha redio cha BBC, Beckham amesema ingawa alikuwa na hasira kwa wakati ule kwa jinsi United walivyotaka kumfanyia lakini hakuwahi kuwa na nia yeyote ya kulipiza kisasi. Beckham aliendelea kudai alichukizwa na kitendo kile cha kufanywa mambo bila yeye mwenyewe kujua wakati ndio kwanza walikuwa wametoka kushinda taji la Ligi Kuu.

CHAPECOENSE WASHINDA MECHI YAO YA KWANZA.

KLABU ya Chapecoense imefanikiwa kushinda mechi yake ya kwanza toka wachezaji wengi wafariki katika ajali ya ndege Novemba 29 mwaka jana. Watu 71, wakiwemo wachezaji 19 na viongozi walifariki dunia wakati timu hiyo ya Brazil ikisafiri kwenda Colombia kwa ajili ya mchezo wao wa fainali ya Copa Sudamericana. Toka wakati huo klabu hiyo imesajili wachezaji 22 wapya na kuteua meneja mpya. Katika mchezo huo Chapecoense iliwafunga Inter de Lages kw amabao 2-1 katika mashindano ya jimbo ambayo walishinda msimu uliopita, huku mabao yakifungwa na Niltinho na Wellington Paulista. Hiyo inakuwa mechi yao ya pili ya mashindano toka kutokee kwa ajali hiyo ambayo imeacha simanzi kubwa.

WENGER AKANUSHA KUMUWANIA BENZEMA.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amekanusha taarifa zilizozagaa kuwa klabu hiyo inamuwania mshambuliaji wa Real Madrid Karim Benzema. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwa kipindi kirefu amekuwa akihusishwa na tetesi hizo, lakini Wenger anaamini tetesi zinakuja kwasababu ya utaifa wake. Akizungumza na wanahabari Wenger amesema kwasasa safu yake ya ushambuliaji imekamilika na haoni nafasi ya kuongeza mshambuliaji mwingine. Wenger aliendelea kudai kuwa ana kikosi kikubwa na anaamini kilichokamilika hivyo haoni sababu ya kununua mshambuliaji.

BARCELONA WATAKA GOAL-LINE TECHNOLOGY LA LIGA.

KLABU ya Barcelona imetaka kuanza kutumika kwa mfumo wa kompyuta katika mstari wa goli kwenye La Liga baada ya kukataliwa bao lao la wazi katika sare ya bao 1-1 waliopata katika mchezo dhidi ya Real Betis jana. Baada ya Betis kupata bao la kuongoza katika kipindi cha pili kupitia kwa Alex Alegria, Barcelona walidhani wamesawazisha bao hilo wakati Aissa Mandi alipojaribu kuokoa mpira wa Jordi Alba ambao ulikuwa umevuka mstari. Hata hivyo mwamuzi Hernandez Hernandez hakulikubali bao hilo ingawa picha za video za marudio zilizonyesha wazi mpira ukiwa umetinga wavuni. Meneja wa Barcelona Luis Enrique alikataa kuwalaumu waamuzi kwa kukaa bao lile na badala yake ametaka kuletwa kwa teknologia hiyo ili kuwasaidia katika baadhi ya maamuzi.

KIPA WA KAGERA SUGAR AFARIKI DUNIA GHAFLA.

KIPA wa timu ya Kagera Sugar David Burhan amefariki dunia mapema leo katika hospitali ya Bugando, Mwanza baadaya kuugua kwa muda mfupi. Kipa huyo ambaye ni mtoto wa mshambuliaji wa zamani wa Pan AfrikaAbdallah Burhan, aliugua ghafla wakati wakiwa njiani kuelekea Singida kwa ajili ya mchezo wa Azam Federation Cup (FA). Kocha wa Kagera Sugar, Mercy Mexime alithibitisha taarifa hizo na kuongeza kuwa Burhan alianza kuugua wakati wakielekea Singida lakini baadae alipata nafuu kabla ya hali yake kubadilika tena na kulazimika kulazwa Biharamulo kabla ya kuhamishishwa kupelekwa hospitali ya mkoa wa Kagera. Mexime aliendelea kudai kuwa mara baada ya kupata vipimo kipa huyo alipewa rufaa kwenda hospitali ya Bugando ambapo uongozi wa klabu hiyo ulimfanyiwa utaratibu wa haraka wa kumchukulia ndege kwenda Mwanza ambapo alifika jana kuanza matibabu kabla ya kufariki dunia mapema leo. Burhan alijiunga na Kagera Sugar msimu huu akitokea Maji Maji ya Songea, ambayo nayo ilimtoa Mbeya City.

Friday, January 27, 2017

BARCELONA NA ATLETICO KUKUTANA NUSU FAINALI KOMBE LA MFALME.

MABINGWA watetezi Barcelona wanatarajiwa kupambana na Atletico Madrid katika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mfalme, huku Alaves wakikwaana na Celta Vigo waliowaondosha Reak Madrid katika mashindano hayo. Baada ya kuindosha Real Sociedad katika robo fainali, Barcelona watasafiri kuifuata Atletico katika uwanja wao wa Vicente Calderone kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza Februari mosi kabla ya kurudiana tena katika Uwanja wa Camp Nou wiki moja baadae. Akizungumzia ratiba hiyo, kiungo wa Barcelona Serge Roberto amesema wanakutana na Atletico kwa mara nyingine wanawafahamu vyema hivyo anadhani utakuwa mchezo mgumu. Kiungo huyo aliongeza kuwa makosa kidogo yanaweza kuweka tofauti katika mechi kama hizo.

LEWANDOWSKI AMSIHI AUBAMEYANG KUBAKI BUNDESLIGA.

MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich, Robert Lewandowski anadhani itakuwa vyema kwa Bundesliga kama Pierre-Emerick Aubameyang atakabaki Borussia Dortmund. Nyota huyo wa kimataifa wa Gabon amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Real Madrid katika miezi ya karibuni na ofisa mkuu wa Dortmund Hans-Joachim Watzke akikiri wiki hii kuwa watafikiria itakayoanzia euro milioni 80. Pamoja na hayo, Lewandowski amemtaka mchezaji mwenzake huyo wa zamani kubakia Bundesliga. Lewandowski amesema amesikia taarifa kuwa Aubameyang anafurahia kuwepo Dortmund hivyo angependa klabu nayo ifikirie namna ya kumbakisha mshambuliaji huyo kwa faida ya Bundesliga.

KLABU ZA UINGEREZA ZAWEKA REKODI MPYA KATIKA USAJILI.

KLABU za Uingereza kwa mara nyingine zimeweka rekodi mpya kwa fedha walizotumia katika usajili msimu huu. Jumla klabu zote za soka zimetumia paundi bilioni 3.8 kwa mwaka 2016 ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.3 kulinganisha na mwaka 2015. Asilimia 82 ya kiasi chote kimetumiwa na nchi wanachama wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, lakini Uingereza ndio wanaongoza orodha hiyo. Mwaka jana kulishuhudiwa Paul Pogba akijiunga na Manchester United kwa kitita cha paundi milioni 89, wakati wachezaji kama Eric Bailly, Henrikh Mkhitaryan, Leroy Sane, John Stones, Granit Xhaka, Shkodran Mustafi na N’Golo Kante pia wakinunuliwa kwa bei kubwa. Klabu za Ligi Kuu ya Uingereza pekee zimetumia jumla ya paundi bilioni 1.03 mwaka jana ikiwa ni karibu nusu ya fedha zilizotumika kwa klabu zingine tano kubwa Ulaya.

SHANGHAI FA YAKANUSHA TAARIFA ZA ROONEY KUWINDWA CHINA.

CHAMA cha Soka cha Shanghai-SFA kimekanusha taarifa kuwa klabu za Shenhua na SIPG kutuma ofa kwa ajili ya kumuwania nahodha wa Manchester United Wayne Rooney. Rooney mwenye umri wa miaka 31 ambaye ni mfungaji bora wa wakati wote wa United amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia China baada ya meneja Jose Mourinho kubainisha kuwa hajamzuia nahodha huyo kama atataka kuondoka. Shenhua tayari imeshwanasa Carlos Tevez, Obafemi Martin, Fredy Guarin na Giovanni Moreno na sasa walikuwa wakihusishwa na tetesi za kumuhitaji Rooney pia. Hata hivyo, SFA imetupilia mbali tetesi hizo na kusisistiza klabu hizo haziwezi kufanya hivyo kutokana na sheria zinazidhibiti idadi ya wachezaji wa kigeni wanaopaswa kucheza katika kila mchezo. Sheria mpya iliyotolewa kwa Ligi Kuu ya China, klabu zinapaswa kutumia wachezaji wa kigeni wasiozidi watatu katika kila mchezo.

Wednesday, January 25, 2017

RONALDO ALAMBA TUZO NYINGINE.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ametunukiwa tuzo nyingine kwa mafanikio aliyopata mwaka 2016. Nyota huyo mwneye umri wa miaka 31, alishinda tuzo ya Ballon d’Or na tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa FIFA baada ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA Super Cup na Klabu Bingwa ya Dunia akiwa na Madrid pamoja Euro 2016 akiwa na Ureno. Ronaldo sasa ametwaa tuzo ya Mchezaji Mwenye Thamani Zaidi-MVP inayotolewa na Dongquidi, mtandao wa China unaomilikiwa na kampuni ya Suning Group, ambao ni wamiliki wa klabu ya Inter Milan. Nyota huyo wa zamni wa Manchester United ambaye amekuwa mchezaji soka wa kwanza kutajwa katika orodha za kugombea tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka, aliwahsukuru mashabiki waliomchagua na kushinda tuzo hiyo.

KALOU ASTAAFU SOKA LA KIMATAIFA.

MSHAMBULIAJI wa Ivory Coast, Solomon Kalou ametangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya mabingwa hao watetezi kuenguliwa mapema katika michuano ya Mataifa ya Afrika jana. Akizungumza na wanahabari mara baada ya kikosi chao kuchapwa bao 1-0 na Morocco, Kalou amesema anedhani wakati umefika wa yeye kupisha vijana wengine kutokana na umri wa miaka 31 aliofikia. Kalou aliendelea kudai kuwa hizo zimekuwa fainali zake za sita na amefanikiwa kufika fainali moja na kushinda mara moja. Nyota huyo ambaye kwasasa anakipiga katika klabu ya Hertha Berlin ya Ujerumani amesema kipindi hiki mambo hayakwenda sawa lakini kuna wachezaji chipukizi kama Franck Kessie na Wilfried Zaha ambao anadhani ndio hazina ya taifa hilo katika soka baadae.

MKATABA MPYA WAMFANYA COUTINHO KUWA MCHEZAJI ANAYELIPWA ZAIDI LIVERPOOL.

KIUNGO Philippe Coutinho amesaini mkataba mpya na Liverpool ambao utamuweka hapo mpaka mwaka 2022 na kumfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi na klabu hiyo kwasasa. Uamuzi wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kusaini mkataba huo mpya na klabu hiyo mapema leo na kuzima tetesi za kuwaniwa na klabu za Barcelona na Paris Saint-Germain-PSG. Akizungumza na tovuti na klabu hiyo, Coutinho amesema amefurahi kusaini mkataba huo na kuishukuru klabu hiyo pamoja na mashabiki kwa kumfanya kujisikia yuko nyumbani. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa atajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kulipa wema na imani kubwa iliyoonyeshwa kwake.

Tuesday, January 24, 2017

SUNDERLAND WAMCHUKUA LESCOTT.

KLABU ya Sunderland imefanikiwa kukamilisha usajili wa Joleon Lescott aliyekuwa mchezaji huru kwa mkataba mfupi wa mpaka mwishoni mwa msimu huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza amekuwa bila timu toka mkataba wake ulipositishwa na AEK Athens Novemba mwaka jana na ameitwa Sunderland ili kuiokoa isishuke daraja. Lescott ambaye amewahi kushinda taji la Ligi Kuu akiwa na Manchester City katika vipindi viwili tofauti, amekuwa akifanya majaribio na Sunderland wakati meneja David Moyes akijipanga kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji. Moyes amewahi kumfundisha Lescott wakati wote wakiwa Everton na sasa anaungana na wachezaji wenzake wa zamani wa klabu hiyo akiwemo Steven Pienaar na Victor Anichebe waliopo katika kikosi cha Sunderland.

KOCHA WA ALGERIA AJITOA KAFARA BAADA YA KUTOLEWA AFCON.

KOCHA wa timu ya taifa ya Algeria, Goorges Leekens amejiuzulu wadhifa wake huo kufuatia kikosi chake kutolewa mapema katika michuano ya Mataifa ya Afrika. Algeria wanajulikana kwa jina la utani kama Mbweha wa Jangwani walikuwa wakipewa nafasi kubwa katika michuano hiyo lakini walijikuta wakienguliwa jana usiku baada ya kushindwa kupata ushindi wowote huko Gabon. Leekens aliiambia tovuti ya Shirikisho la Soka la nchi hiyo kuwa ameamua kuchukua uamuzi huo kwa faida ya wote. Kocha huyo alimalizia kwa kuitakia timu hiyo mafanikio katika mshindano yote yajayo.

TOURE AWAPONDA NYOTA WENZAKE WANAOKIMBILIA CHINA.

KIUNGO wa Manchester City, Yaya Toure amewaponda wachezaji wenzake ambao wanakimbilia China, akidai kuwa angependelea zaidi kufuata nyayo za mshambuliaji wa Manchester United Zlatan Ibrahimovic na kubaki katika ligi yenye ushindani. Klabu za Ligi Kuu ya China zimewanasa nyota kadhaa wenye majina makubwa hivi karibuni akiwemo kiungo wa kimataifa wa Brazil na Chelsea Oscar aliyenunuliwa kwa kitita cha euro milioni 60 na klabu ya Shanghai SIPG. Mahasimu wa SIPG, klabu ya Shanghai Shenhua wao wamemsajili nyota wa kimataifa wa Argentina Carlos Tevez kwa kitita cha euro milioni 84, lakini Toure amesema kwake pesa sio kila kitu. Akizungumza na wanahabari Toure amesema yeye kwa upande wake hachezi soka ili apate pesa bali anacheza kwasababu anafurahia mchezo huo.

Monday, January 23, 2017

AFCON 2016: BAADA YA KUIFUNGISHA VIRAGO ALGERIA, SENEGAL SASA KUIVAA CAMEROON.

TIMU ya taifa ya Algeria imeenguliwa katika michuano ya Mataifa ya Afrika kwenye hatua ya makundi baada ya kushindwa kupata ushindi wowote huko Gabon. Algeria waliingia katika michuano hiyo wakipewa nafasi kubwa kufanya vyema haswa kutokana na kikosi chake kilichosheheni nyota kadhaa akiwemo mchezaji bora wa mwaka wa Afrika Riyad Mahrez. Hata hivyo, katika hali isiyotegemewa wamejikuta wakitolewa baada ya kung’ang’aniwa sare ya mabao 2-2 na vinara wa kundi B Senegal iliyohitimisha safari yao. Senegal sasa anatarajiwa kucheza na Cameroon katika hatua ya robo fainali Jumamosi hii huku mshindi wa pili kwenye kundi hilo Tunisia ambao waliigaragaza Zimbabwe kwa mabao 4-2, wao wakicheza na Burkina Faso.

AUBAMEYANG ALIA NA MAANDALIZI MABOVU KUFUATIA KUTOLEWA MAPEMA KWA WENYEJI GABON.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang anaamini kutokuwa na maandalizi ya kutosha ndio kitu kilichochangia kuenguliwa mapema katika hatua ya makundi ya michuano ya mataifa ya Afrika. Gabon walikuwa wanatakiwa kuwafunga Cameroon jana ili waweze kusonga mbele lakini badala yake waliambulia sare ya bila kufungana. Aubameyang amesema ni jambo linalomkera kwasababu walikuwa na nafasi lakini anasikitika mambo hayakwenda kama walivyotarajia. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa wamehuzunika lakini pia hawakupata muda wa kutosha wa kufanya maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo. Burkina Faso walitinmga hatua hiyo wakiwa vinara wa kundi A wakifiatiwa na Cameroon waliomaliza katika nafasi ya pili.

ZIDANE ALIA NA MAJERUHI BAADA YA MODRIC NA MARCELO KUUMIA.

KLABU ya Real Madrid imethibitisha mapema leo kuwa nyota wake Luka Modric na Marcelo wote wamepata majeruhi ya msuli wa paja. Nyota hao walitolewa katika mchezo dhidi ya Malaga ambao Madrid walishinda mabao 2-1, ikiwa ni ushindi wao wa kwanza baada ya kupoteza mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Sevilla na Celta Vigo. Hata hivyo ushindi huo umekuja kwa gharama baada ya nyota hao wawili kongeza idadi ya majeruhi katika kikosi hicho ambapo tayari inawajumuisha Gareth Bale, James Rodriquez, Dani Carvajal, Pepe, Danilo na Fabio Coentrao. Akizungumza na wanahabari Zidane amesema suala la majeruhi kidogo linamchanganya kwani wana mechi kubwa Jumatano ijayo. Madrid inakabiliwa na mchezo mgumu wa robo fainali wa mkondo wa pili wa Kombe la Mfalme dhidi ya Celta Vigo ambapo katika mchezo wa kwanza walipoteza kwa mabao 2-1.

COSTA ASABABISHA MAAFA KWA KIUNGO WA HULL CITY.

KIUNGO wa Hull City, Ryan Mason amefanyiwa upasuaji baada ya kuvunjika kwa fuvu la kichwa chake wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Chelsea jana. Masom mwenye umri wa miaka 25, aligongana kwa kichwa na beki wa Chelsea Gary Cahill katika dakika ya 13 ya mchezo huo. Baada ya kutibiwa kwa dakika nane uwanjani, Mason aliwekewa mashine ya kumsaidia kupumua na kutolewa nje akiwa amebebwa kwenda machela kabla ya kukimbizwa hospitali moja kwa moja. Taarifa kutoka kwa klabu hiyo zimedai kuwa kwasasa kiungo huyo yuko katika hali nzuri na anategemewa kuendelea kubakia hospitali kwa siku chache zijazo. Mabao ya Diego Costa na Cahill yalitosha kuipa Chelsea ushindi wa mabao 2-0 na kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa wa ligi kwa tofauti ya alama nane.

WENGER AOMBA RADHI KWA VURUGU ALIZOFANYA.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger ameomba radhi kwa tabia mbovu aliyoonyesha mwishoni mwa mchezo dhidi ya Burnley jana, ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1. Wenger alionekana wazi akizozana na mwamuzi wa akiba aliyemuamuru kutoka uwanjani na kwenda jukwaani kwa kumsukuma. Meneja huyo alitolewa katika benchi lake la ufundi kwa tabia aliyoonyesha baada ya Burnley kupewa penati katika dakika za nyongeza. Wenger amesema anajutia kila kitu kwani alipaswa kunyamaza na kuzuia hisia, hivyo anaomba radhi kwa tukio hilo. Hata hivyo, meneja huyo aliendelea kudai kuwa hakupata nafasi ya kuomba radhi moja kwa mwamuzi huyo Anthony Taylor na kuna uwezekano wa kupata adhabu zaidi kutoka FA kwa tukio hilo.

Sunday, January 22, 2017

WENYEJI GABON WAAGA AFCON MAPEMA.

TIMU ya taifa ya Gabon imeaga michuano ya Mataifa ya Afrika jana na kuwa nchi ya tatu mwenyeji kutolewa katika hatua ya makundi. Gabon wakiongozwa na mshambuliaji wake nyota anayekipiga katika klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani, waling’ang’aniwa sare ya bila kufungana na Cameroon ambao wametinga hatua ya robo fainali. Mara ya mwisho timu mwenyeji kutolewa katika hatua za mapema ilikuwa mwaka 1994 wakati Tunisia walipoaga michuano hiyo katika hatua makundi. Katika mchezo mwingine Burkina Faso walifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali wakiwa vinara wa kundi A baada ya kuichapa Guinea Bissau kwa mabao 2-0.

Friday, January 20, 2017

DEPAY ATUA RASMI LYON.

KLABU ya Manchester United imemuuza rasmi winga wa kimataifa wa Uholanzi Memphis Depay kwenda klabu ya Lyon ya Ufaransa. Taarifa zinadai kuwa ada uhamisho huo ni paundi milioni 16 inayoweza kupanda mpaka paundi milioni 21.7 kama Lyon wakifuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Depay akipewa mkataba mpya. United pia imekubaliana na Lyon kupewa kipaumbele kama klabu hiyo itaamua kumuuza mchezaji huyo. Depay mwenye umri wa miaka 22 amefunga mabao saba katika mechi 53 alizoichezea United toka ajiunge nao kwa kitita cha paundi milioni 25 akitokea PSV Eindhoven ya Uholanzi mei mwaka 2015.

FIFA YAAMRIWA KUMLIPA LASSANA DIARRA EURO MILIONI SITA.

MAHAKAMA nchini Ubelgiji imetoa hukumu kuwa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA na lile la Uholanzi-KBVB kulaumiwa kwa kushindikana kufanyika usajili wa Lassana Diarra kwenda Charleroi mwaka 2015 na sasa lazima wamlipe kiungo huyo euro milioni sita. Mahakama ya Charleroi iliamua kuwa FIFA walikiuka sheria ya Umoja wa Ulaya-EU kwa kuingilia uhuru wa kuhama baada ya kudai kuwa klabu yeyote itakayomsajili Diarra italazimika kulipa deni la euro milioni 10 anazodaiwa na klabu ya Lokomotiv Moscow. Kiungo huyo wa zamani wa Arsenal, Chelsea na Real Madrid alilimwa faini hiyo kubwa kwa kuvunja mkataba wake wa miaka minne na Lokomotiv, kwa kuondoka katika klabu hiyo ya Urusi baada ya kupita miezi 12 pekee. Kufuatia muongozo huo wa FIFA, klabu ya Charleroi ya Ubelgiji ilisitisha mazungumzo yake na Diarra Februari mwaka 2015 na baadae nyota huyo kujiunga na Marseille kufuatia kutocheza msimu mzima wa 2014-2015.

Thursday, January 19, 2017

SENEGAL YAWA YA KWANZA KUTINGA ROBO FAINALI AFCON, TUNISIA YAZINDUKA.

TIMU ya taifa ya Senegal imekuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika baada ya kuishindilia Zimbabwe kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kundi B uliochezwa jijini Franceville. Mabao ya Sadio Mane katika dakika ya tisa na lingine la mpira wa adhabu lilifungwa na Henry Saivet katika dakika ya 13 yalitosha kuwahakikishia nafasi ya kutinga hatua ya mtoano baada ya pia kushinda mabao 2-1 dhidi ya Tunisia katika mchezo wao wa kwanza. Katika mchezo wa awali Tunisia nao walifanikiwa kurekebisha makosa yao ya kupoteza mchezo wao wa kwanza kwa kuichapa Algeria mabao 2-1 na kufufua matumaini yao ya kusonga mbele. Timu hizo zinatarajia kucheza mechi zao za mwisho za kundi B Jumatatu ijayo ambapo Senegal watapepetana na Algeria jijini Franceville wakati Zimbabwe wakitafuta ushindi wao wa kwanza katika michuano hii kwa kuchuana na Tunisia huko Libreville.

SIMEONE APOZA TAARIFA ZA GRIEZMANN KUWANIA MAN UNITED.

KOCHA wa Atletico Madrid, Diego Simeone hajashangazwa na taarifa za Antoine Griezmann kuwaniwa na klabu nyingi ikiwemo Manchester United na kuongeza kuwa hatamzuia mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa kama akiamua kuondoka. Mapema wiki hii kumekuwa na taarifa kuwa mazungumzo kwa ajili ya nyota huyo kwenda Old Trafford yamefikia pazuri na United wanajiandaa kutoa kitita cha euro milioni 100 ili kuvunja mkataba wake na Atletico. Akizungumzia kuhusiana na taarifa hizo Simeone amesema hana mpango wa kuzuia mchezaji yeyote kwani anachofanya yeye ni kufanya kazi kwa ajili ya manufaa ya klabu. Simeone aliendelea kudai kuwa Griezmann amekuwa katika kiwnago cha juu huku akifunga mabao hivyo ni kawaida kwa klabu kubwa kumuwania.

NILIKATAA KUJIUNGA NA LYON KWASABABU YA AFCON.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Togo, Emmanuel Adebayor amedai kuwa alikataa uhamisho wa kwenda Lyon ili aweze kuitumikia nchi yake katika michuano ya Mataifa ya Afrika. Adebayor ambaye bila klabu toka alipoondoka Crystal Palace mwishoni mwa msimu uliopita, ndio nahodha wa Togo katika michuano hiyo inayoendelea nchini Gabon. Mshambuliaji huyo angekosa zaidi ya mwezi mmoja msimu wa Ligue 1 kama Togo watafanikiwa kufika fainali Februari 5 na Lyon hawakufurahishwa na suala hilo ndio maana uhamisho wake ukashindikana. Adebayor amesema alikataa ofa ya mkataba ya Lyon ili aweze kuiwakilisha nchi yake kwani moja ya msharti katika mkataba huo ilikuwa ni kutoshiriki michuano hiyo.

MALINZI AULA FIFA.

SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya soka ya FIFA kwa miaka minne ijayo. Uteuzi huo unaanza mwaka huu 2017 hadi 2021. Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Januari 18, 2017 iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Fatma Samoura inasema: “Tuna faraja kukufahamisha kuwa umeteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya FIFA. Tunachukua nafasi hii kukupongeza kwa uteuzi huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Taarifa hiyo ilifafanua kuwa Kamati hiyo inayoongozwa na Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Bara la Asia, ina majukumu ya kusimamia mipango ya maendeleo ya mpira wa miguu duniani kote. Wajumbe wengine wote watatangazwa kwenye tovuti ya FIFA ambayo ni www.FIFA.com. Huu ni mfululizo wa Tanzania kupata nafasi katika vyombo vikubwa vinavyoendesha soka FIFA na CAF. Mwishoni mwa mwaka jana, CAF – Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika lilimteua Rais Malinzi kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati maalumu inayoongozwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou ya kuboresha mfumo wa uongozi wa CAF. TFF inamshukuru Rais Gianni Infantino na kamati yake ya ushauri kwa kumteua Malinzi katika nafasi ya ujumbe katika kamati hiyo muhimu ya maendeleo ya soka ulimwenguni.

HATMA YA ZANZIBAR CAF KUJULIKANA MACHI 26.

KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limepitisha ombi la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) la Zanzibar kuwa mwanachama kamili wa CAF. Katika kikao chake cha Kamati ya Utendaji kilichoketi Januari 12, mwaka huu kiliamua kupitisha ombi hilo kuwa moja ya ajenda za Mkutano Mkuu wa CAF utakaofanyika Machi 16, 2017 huko Addis Ababa, Ethiopia. Hivyo sasa Mkutano Mkuu huo utapiga kura na kama Zanzibar itapata idadi ya kura theluthi mbili yaani 2/3 ya wanachama wote, itatangazwa kuwa mwanachama mpya kamili wa CAF ambako atakuwa na haki mbalimbali za kama mwanachama. Haki hizo ni pamoja na kushiriki michuano yote inayoandaliwa na kusimamiwa na CAF na hii ni pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), fainali za Afrika Wanawake (AWCON), fainali za vijana (AFCON U17 na AFCON 20)na pia kuhudhuria mikutano mbalimbali ya CAF kama mwanachama kamili, kupokea na kusimamia kozi mbalimbali za CAF nakadhalika. Pia itakuwa na fursa ya kupiga kura katika masuala muhimu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) tofauti na sasa ambako inapata fursa ya klabu zake zinazoshika nafasi ya juu katika Ligi Kuu ya Zanzibar kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa Mheshimiwa Nape Nnauye – Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano Tanzania pamoja na Mheshimiwa Rashid Ali Juma - Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanizbar (SMZ) kwa kufanikisha hatua hiyo. Pia, TFF inatoa shukrani kwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Ravia Idarus Faina pamoja na Rais wa Heshima wa TFF Leodegar Chilla Tenga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa CAF na Marais wa Heshima wa TFF Said Hamad El Maamry ambaye ni Mjumbe wa kudumu wa CAF na Mzee Muhiddin Ndolanga na wadau wote wa familia ya mpira wa miguu kwa mafanikio ya hatua hii. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa sasa linajikita kwenye kampeni nzito ya kuomba kura za kutosha kuhakikisha kwamba Zanzibar inapata nafasi hiyo ya uanachama kamili. Kadhalika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia viongozi wake wako kwenye mchakato wa kumfanyia kampeni Rais wa Heshima wa TFF, Bw. Leodegar Chilla Tenga kuhakikisha anashinda nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji (Council) ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Leodegar Tenga anawania nafasi hiyo kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya Kiingereza akishindana na Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Zambia, Kalusha Bwalya na Kwesi Nyantakyi wa Ghana. TFF inaomba Watanzania wote na wadau wote wa mpira wa miguu nchini kutuunga mkono katika juhudi na jitihada zetu za kuona Zanzibar inapata nafasi hiyo kadhalika Tenga anakuwa mjumbe kwenye baraza la ushauri huko FIFA.

MAN UNITED YAIPITA REAL MADRID KWA KUINGIZA MAPATO MENGI ZAIDI.

KLABU ya Manchester United imetajwa kupata mapato makubwa zaidi kuliko klabu yeyote duniani msimu uliopita kwa mujibu ya taarifa iliyochapishwa na jarida la Deloitte. United imeipita Real Madrid ambayo imekuwa ikiongoza orodha hiyo kwa miaka 11, baada ya kuweka rekodi ya kupata mapato ya kiasi cha paundi milioni 515 wakati wa msimu wa 2015-2016. Klabu hiyo ya Ligi Kuu imeshuhudia mapato yake kibiashara yakiongezeka kwa paundi milioni 71. Hiyo inakuwa mara ya kwanza kwa United kuongoza orodha hiyo ya mwaka ya Deloitte Football Money League toka msimu wa 2003-2004. Madrid wamshuka mpaka nafasi ya tatu nyuma ya mahasimu wao Barcelona ambao wamebaki katika nafasi ya pili nao Bayern Munich na Manchester City zote zimepanda katika nafasi ya nne na tano ikiwa ni mara ya kwanza kupanda kwenye tano bora. Mabingwa wa Uingereza Leicester City wameingia katika orodha hiyo kwa mara ya kwanza wakishika nafasi ya 20 huku Arsenal, Chelsea, Liverpool na Tottenham Hotspurs zote zimebaki kwenye nafasi zao za saba, nane, tisa na 12.


Tuesday, January 17, 2017

SUALA LA MATIP LAMUUMIZA KICHWA KLOPP.


MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp ameeleza kuchoshwa kwake juu uwezekano wa kumtumia Joel Matip, akidai kuwa beki huyo anaweza kukosa mechi mpaka nane bila kufanya jambo lolote baya. Matip aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika , pamoja na kuweka wazi nia yake ya kuacha kuitumikia nchi yake. Beki huyo aliondolewa katika kikosi cha Liverpool katika mchezo waliotoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Manchester United mwishoni mwa wiki iliyopita na pia mchezo wao ujao wa Kombe la FA dhidi ya Plymouth Argyle wakati klabu hiyo ikisubiria kupewa ruhusa na kumtumia na FIFA. FIFA inadaiwa kushindwa kutoa mwongozo zaidi kwa Liverpool kufuatia sheria yake ambayo inaeleza kuwa “Mchezaji ambaye atakuwa ameitwa na nchi yake kwa ajili ya kuiwakilisha timu ya taifa, hataruhusiwa kucheza katika klabu yake katika kipindi chote atapokuwa akihitajika kwa majukumu yake kimataifa labda shirikisho husika likubaliane na klabu husika na taarifa zitolewe siku tano kabla”.

UNITED YAMUONGEZA VALENCIA MWAKA MMOJA ZAIDI.

WINGA wa Manchester United Antonio Valencia amesaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja zaidi ambayo utamuweka Old Trafford mpaka Juni 2018. Wiki iliyopita klabu hiyo ilitangaza kumuongeza mkataba Marouane Fellaini kwa miezi 12 zaidi na sasa Valencia amefuata nyayo hizo leo. Nyota huyo wa kimataifa wa Ecuador alijiunga na United akitokea Wigan Athletic mwaka 2009 na kufanikiwa kucheza mechi 271 na kufunga mabao 21.

USAJILI WA JUVENTUS UNATOSHA - NEDVED.

MAKAMU wa rais wa Juventus, Pavel Nedved amedai kuwa hadhani kama klabu hiyo itafanya usajili mwingine katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo la Januari. Mabingwa hao wa Serie A waliongeza nguvu katika safu yao ya kiungo kwa kumsajili Tomas Rincon kutoka Genoa, wakati pia walimsajili Mattia Caldara ambaye atabakia kwa mkopo Atalanta mpaka mwishoni mwa msimu wa 2017-2018. Nedved amesema kwasasa waemridhishwa na kikosi walichonacho hivyo itakuwa hatihati kuongeza mchezaji mwingine katika kipindi hiki. Nedved aliendelea kudai kuwa siku zote wamekuwa wakiangalia hali waliyonayo sasa na pia baadae ndio maana anaamini hawahitaji kuongeza mchezaji mwingine. Juventus kwasasa ndio wanaongoza msimamo wa Serie A wakitofautiana na AS Roma kwa alama moja.

SAGNA ALIMWA FAINI KWA UJUMBE ALIOTUMA INSTAGRAM.

CHAMA cha Soka cha Uingereza-FA kimemlima faini ya paundi 40,000 beki wa Manchester City Bacary Sagna kwa ujumbe wake aliotuma katika mtandao wa kijamii akihoji uwezo wa mwamuzi Lee mason katika ushindi wa mabao 2-1 waliopata katika Ligi Kuu dhidi ya Burnley mapema mwezi huu. City walipata ushindi huo kwa mabao yaliyofungwa na Gael Clichy na Sergio Aguero pamoja na kucheza wakiwa pungufu baada ya Fernandinho kulimwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Johann Gudmundsson. Katika ujumbe wake aliotuma katika mtandao wa Instagram, Sagna alindika kuwa walicheza 10 dhidi ya 12 lakini bado walipambana na kushinda mchezo kama timu. Baadae nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa alirekebisha ujumbe wake huo kwa kuondoka maneno ya 10 kwa 12 lakini bado FA waliamua kumlima adhabu kwa kukiuka sheria zake.

NEYMAR NDIYE MCHEZAJI MWENYE THAMANI ZAIDI KWASASA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Neymar ametajwa kuwa mchezaji ghali zaidi duniani akiwapita nyota wengine ambao wanatajwa kuwa wakubwa zaidi yake akiwepo mchezaji mwenzake wa Barcelona, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambaye hivi karibuni ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa 2016 FIFA. Taarifa hizo za Neymar kuwa mchezaji ghali duniani zimejulikana kupitia utafiti ambao umefanywa na kampuni ya tafiti za soka ya CIES Football Observatory ambayo imesema kwasas a Neymar ana thamani ya Euro milioni 246.8. Katika utafiti huo, Lionel Messi ameshika nafasi ya pili akiwa na thamani ya Euro milioni 170.5 na Paul Pogba akishika nafasi ya tatu kwa kuwa na thamani ya Euro milioni 155.3 huku Cristiano Ronaldo akiwa katika nafasi ya saba kwa kuwa na thamani ya Euro Milioni 126. Aidha CIES walisema vigezo walivyotumia kuchagua wachezaji hao ni uwezo wa mchezaji uwanjani, msaada anaotoa kwa timu yake, magoli anayofunga na dakika anazocheza pia kuangalia umri na mkataba alionao katika klabu anayoichezea.

MMILIKI WA TIANJIN AKIRI KUMUWANIA COSTA.

MMILIKI wa klabu ya Tianjin Quanjian, Shu Tuhui amethibitisha kuwa alikuwa na mipango ya kuwasajili Diego Costa, Karim Benzema, Edinson Cavani na Radamel Falcao mpaka pale Chama cha Soka cha China-CFA kilipobadili sheria ya idadi ya wachezaji wa kigeni. Wakiwa tayari wameshamnasa nyota wa kimataifa wa Ubelgiji Axel Witsel, klabu hiyo inayonolewa na beki wa zamani wa Real Madrid na Juventus Fabio Canavaro, imekuwa ikihusishwa na tetesi za kutaka kuwasajili Costa na wenzake. Yuhui amebainisha kuwa Tianjin ilikuwa katika mazungumzo na Costa, Benzema, Cavani na Falcao kabla ya CFA hawajatangaza sheria mpya ambapo timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya China zitalazimika kutumia wachezaji watatu pekee wa kigeni kwa mchezo. Akihojiwa Yuhui amesema klabu yao ilikuwa na mipango mikubwa ya uwekezaji kwa ajili ya msimu mpya lakini wamebanwa na sheria hiyo mpya.

VAN GAAL AAMUA KUSTAAFU RASMI SOKA.

KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi na klabu ya Manchester United, Louis van Gaal ametangaza kustaafu rasmi kibarua hicho baada ya kudumu kwa kipindi cha miaka 26. Van Gaal mwenye umri wa miaka 65 amekuwa bila kazi toka alipotimuliwa na United saa chache baada ya kushinda taji la Kombe la FA Mei mwaka jana. Van Gaal amesema mara ya kwanza alifikiria kuwa atasimama kwa muda lakini baada ya kufikiria kwa muda anadhani imetosha na hataweza tena kurejea kufundisha soka. Mbali na United Van Gaal pia amewahi kuzinoa klabu za Ajax Amsterdam, Barcelona, Bayern Munich na AZ. Van Gaal alitangaza uamuzi huo jana baada ya kupokea tuzo ya mafanikio ya maisha kutoka kwa serikali ya Uholanzi kutokana na mchango wake mkubwa katika soka.

Mataji aliyowahi kushinda.
National titles: Ajax (1993-94, 1994-95, 1995-96), Barcelona (1997-98, 1998-99), AZ Alkmaar (2008-09), Bayern Munich (2009-10)
Champions League: Ajax (1994-95)
Uefa Cup: Ajax (1991-92)
FA Cup: Manchester United (2015-16)

Monday, January 16, 2017

CHINA YAAMUA KUPUNGUZA IDADI YA WACHEZAJI WA KIGENI.

KLABU zinazoshiriki Ligi Kuu ya China zitaruhusiwa kutumia wachezaji watatu pekee wa kigeni katika mchezo katika msimu wao ujao wa ligi ambao utaanza Machi mwaka huu. Sheria hiyo ya mabadiliko imepunguza idadi ya wachezaji wa kigeni wanaohitajika hatua ambayo itapunguza wimbi la kusajiliwa wachezaji kwa fedha nyingi kutoka Ulaya. Mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa amekuwa akihusishwa na tetesi za kutimkia China huku taarifa zikidai atakuwa akilipwa paundi milioni 30 kwa mwaka kama dili hilo likikamilika. Klabu ya Tianjin Quanjiani ambayo mapema mwezi huu ilimsajili nyota wa kimataifa wa Ubelgiji Axel Witsel kwa mshahara wa paundi milioni 15 kwa mwaka ndio wanaidaiwa kumuwania Costa. Taarifa za kupunguzwa kwa idadi ya wachezaji wa kigeni itaigusa moja kwa moja klabu ya Shanghai Shenhua ambayo ina wachezaji sita wa kigeni wakiwemo Carlos Tevez, mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Demba Ban a mshambulaiji wa zamani wa Newcastle Obafemi Martins.

ROMA WAMUWANIA CHIPUKIZI WA CHELSEA.

MENEJA wa AS Roma, Luciano Spalletti amethibitisha klabu hiyo kumuwania chipukizi wa Chelsea Charly Musonda katika kipindi hiki cha usajili wa Januari. Nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 20 alikatishwa mkataba wake wa mkopo katika klabu ya Real Betis huku meneja wa Chelsea Antonio Conte akisisitiza kuwa anaweza kumpa nafasi katika kikosi chake cha kwanza. Lakini Spalletti amebainisha kuwa anataka sana kumleta Musonga Stadio Olimpico kabla ya mwishoni mwa mwezi huu. Meneja huyo raia wa Italia pia anataka kumuwania winga wa West Ham United Sofiene Feghouli ambaye ameshindwa kung’aa katika klabu hiyo toka asajiliwe akitokea Valencia kiangazi mwaka jana.

ROBBEN AFUATA NYAYO ZA RIBERY BAYERN.

WINGA mahiri wa Bayern Munich, Arjen Robben amefikia makubaliano na klabu hiyo ya kuongeza mkataba mpaka ambao utamuweka hapo mpaka Juni mwaka 2018. Nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi mkataba wake wa sasa unamalizika mwishoni mwa msimu huu, lakini ameamua kuongeza mkataba wa mwaka mmoja zaidi. Robben alijiunga na Bayern akitokea Real Madrid Agosti mwaka 2009 na toka wakati amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha timu hiyo. Winga huyo mwenye umri wa miaka 32 ameichezea Bayern zaidi ya mechi 200, na kushinda mataji matano ya Bundesliga, manne ya DFB Pokal, moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Klabu Bingwa Dunia. Robben amefuata nyayo za winga mwenzake Franck Ribery ambaye naye alisaini mkataba wa mwaka mmoja zaidi Novemba mwaka jana.

EL HADARY MBIONI KUWEKA HISTORIA AFCON.

SIKU mbili baada ya kusheherekea miaka 44 ya kuzaliwa kwake, kipa wa timu ya taifa ya Misri Essam El Hadary sasa anatarajia kuweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika inayoendelea huko nchini Gabon. El Hadary anacheza fainali zake za saba za michuano hiyo, akizidiwa moja na nguli wa zamani wa Cameroon Rigobert Song. Kipa huyo anatarajiwa kuwepo katika kikosi cha Misri kitakachokwaana na Mali katika mchezo wa kundi D utakaochezwa huko Port Gentil kesho. Kama El Hadary akipangwa katika mchezo huo atakuwa ameifunika rekodi ya Hossam Hassan aliyoweka katika michuano ya mwaka 2006 ambapo alikuwa na umri wa miaka 39.

Saturday, January 14, 2017

COSTA AACHWA KIKOSI CHA CHELSEA.

MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Diego Costa ameachwa katika kikosi cha timu hiyo kitakachokwaana na Leicester City baadae leo kufuatia mgogoro na kocha wake juu ya siha yake. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania hajafanya mazoezi kwa siku tatu na ameachwa katika kikosi cha timu hiyo kilichosafiri kwenda kukwaana na mabingwa hao wa Uingereza. Taarifa hizo zimekuja kufuatia tetesi kuwa ametengewa ofa nono kwenda China ambayo itamfanya kulipwa kitita cha paundi milioni 30 kwa mwaka. Costa mwenye umri wa miaka 28 amefunga mabao 14 na kutengeneza mengine matano msimu huu. Chelsea wenyewe walikanusha taarifa hizo zilizozagaa.