Tuesday, January 17, 2017

SUALA LA MATIP LAMUUMIZA KICHWA KLOPP.


MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp ameeleza kuchoshwa kwake juu uwezekano wa kumtumia Joel Matip, akidai kuwa beki huyo anaweza kukosa mechi mpaka nane bila kufanya jambo lolote baya. Matip aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika , pamoja na kuweka wazi nia yake ya kuacha kuitumikia nchi yake. Beki huyo aliondolewa katika kikosi cha Liverpool katika mchezo waliotoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Manchester United mwishoni mwa wiki iliyopita na pia mchezo wao ujao wa Kombe la FA dhidi ya Plymouth Argyle wakati klabu hiyo ikisubiria kupewa ruhusa na kumtumia na FIFA. FIFA inadaiwa kushindwa kutoa mwongozo zaidi kwa Liverpool kufuatia sheria yake ambayo inaeleza kuwa “Mchezaji ambaye atakuwa ameitwa na nchi yake kwa ajili ya kuiwakilisha timu ya taifa, hataruhusiwa kucheza katika klabu yake katika kipindi chote atapokuwa akihitajika kwa majukumu yake kimataifa labda shirikisho husika likubaliane na klabu husika na taarifa zitolewe siku tano kabla”.

No comments:

Post a Comment