Wednesday, July 31, 2013

BARCELONA YAMPOTEZA NGULI WAKE WA ZAMANI.

KLABU ya Barcelona imetangaza katika mtandao wake kumpoteza mchezaji wake wa zamani Antoni Ramallets aliyefariki dunia Jumanne akiwa na umri wa miaka 89. Ramallets ambaye alikuwa golikipa aliichezea Barcelona mechi 400 kati ya mwaka 1946 na 1961, na kuisaidia timu hiyo kushinda mataji sita ya La Liga na mataji mengine matano ya Kombe la Mfalme. Rais wa Barcelona, Sandro Rosell alikaririwa na mtandao huo akitoa salamu zake za rambirambi kwa kumuelezea Ramallets kama mmoja wa makipa bora waliowahi kuichezea klabu hiyo hivyo siku ya jana ilikuwa siku ya masikitiko makubwa kwao kumpoteza. Wachezaji wa Barcelona walisimama kwa dakika moja katika mchezo wao wa kirafiki wa Jumanne dhidi ya Lechia Gdansk ili kumkumbuka golikipa huyo wa kimataifa wa Hispania.

SPURS YAKUBALI KUANZA MAZUNGUMZO NA MADRID.

HATIMAYE klabu ya Tottenham Hotspurs imeanza mazungumzo na klabu ya Real Madrid juu ya mauzo ya euro milioni 115 ya mshambuliaji wake Gareth Bale baada ya viongozi wa klabu hiyo kushawishika kwamba nyota huyo ataondoka katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi. Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy alikuwa amekomaa katika kipindi chote toka dirisha la usajili lilipofunguliwa akidai kuwa hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo kwa gharama yoyote. Hata hivyo kampeni za Madrid za kutaka kumsajili nyota huyo zilionyesha kuzaa matunda siku chache zilizopita baada ya kumuonya mchezaji huyo na washauri wake kuwa aombe kuondoka hivi sasa au waachane naye kabisa. Onyo hilo la Madrid limeonyesha kuzaa matunda baada ya Bale kukutana binafsi na Levy na kumuhabarisha kuwa anataka kwenda zake kwa vigogo hao wa soka nchini Hispania. Hatua hiyo imepelekea Levy ambaye msimamo wake wa kutomuuza Bale ulikuwa ukiungwa mkono na mmiliki wake Joe Lewis, kufungua mazungumzo na Madrid ambapo anatarajiwa kukutana na rais wake Florentino Perez Agosti 6 mwaka huu jijini Florida.

IAAF YAPANIA KUKOMESHA WANARIADHA KUTUMIA DAWA ZILIZOKATAZWA.

MAKAMUwa rais wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha-IAAF, Sebastian Coe amedai kuwa shirikisho hilo limejipanga kukomesha matumizi ya dawa za kuongeza nguvu baada ya wanariadha wawili nyota wa mbio fupi kukutwa na hatia ya kutumia dawa hizo mapema mwezi huu. Kauli hiyo ya Coe ameitoa jijini Moscow mji ambao ndio utakuwa mwenyeji wa mashindano ya riadha ya dunia baadae mwezi ujao baada ya Tyson Gay wa Marekani na Asafa Powell wa Jamaica kushindwa katika vipimo vyao walivyofanyiwa. Coe amesema kitu cha msingi kuhakikisha wanawafanyia wanaraidha vipimo vya mara kwa mara ili kuhakikisha mashindano ya hayo ya dunia yanafanyika katika hali salama ya bila mwanariadha yoyote kukutwa na dawa hizo zilizopigwa marufuku. Coe alikiri kuwa litakuwa ni suala lisilowezekana kwake kudai kuwa itafikia muda matukio kama hayo kuisha katika michezo lakini hivi sasa wanafuatilia suala hilo kwa karibu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo mwanzo. Mashindano ya raidha ya dunia yatakuwa ya kwanza makubwa kufanyika jijini Moscow toka mji huo ulioandaa michuano ya olimpiki mwaka 1980 na yatafanyika katika Uwanja wa Luzhniki ambao ndio zilizikofanyika sherehe za ufunguzi wa olimpiki mwaka huo.

HENRY AKABIDHIWA UNAHODHA KIKOSI CHA WACHEZAJI NYOTA WA LIGI YA MAREKANI.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Ufaransa, Thierry Henry ameteuliwa kuwa nahodha wa kikosi cha wachezaji nyota wa Ligi Kuu nchini Marekani-MLS kwa ajili ya mechi yao ya kirafiki dhidi ya AS Roma itakayofanyika jijini Kansas. Henry alikabidhiwa unahodha na kocha wa kikosi hicho Peter Vermes na kufuata nyayo za David Beckham ambaye aliwahi kuwa nahidha wa kikosi hicho katika mechi ya kirafiki dhidi ya Manchester United miaka miwili iliyopita. Henry ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza katika kikosi cha wachezaji nyota wa MLS ambapo United ilishinda kwa mabao 4-0 lakini mwaka mmoja baadae alikisaidia kikosi hicho kuigaragaza Chelsea kwa mabao 3-2. Kwa Roma hiyo itakuwa mechi yao ya kwanza kati ya nne watakazocheza wakati wakiwa huko Amerika Kaskazini kwa ajili ya maandalizi msimu mpya wa Ligi Kuu ya Soka nchini Italia.

NDOTO ZANGU ZIMETIMIA - NEYMAR.

MSHAMBULIAJI mpya wa klabu ya Barcelona, Neymar amebainisha kuwa anamhusudu Lionel Messi na kudai kuwa kucheza naye katika timu moja ni kama ndoto ambazo zimekuja kuwa kweli. Nyota wa kimataifa wa Brazil alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na klabu hiyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Lechia Gdansk akiingia dakika 15 za mwisho kuchukua nafasi ya Alexis Sanchez. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Neymar alikiri kuwa ndoto zake alizokuwa nazo katika kipindi kirefu zimeanza kuwa kweli baada ya kucheza mechi hiyo ya kwanza. Nyota mwenye miaka 21 anatarajiwa kukutana na klabu yake ya zamani ya Santos katika mechi ya kirafiki Agosti 2 mwaka huu.

HOENESS AFUNGULIWA MASHITAKA RASMI YA UKWEPAJI KODI.

MAHAKAMA ya jiji la Munich imemfungulia mashitaka jana rais wa klabu ya Bayern Munich, Uli Hoeness kwa kosa la ukwepaji kodi baada ya kukamilisha uchunguzi uliodumu kwa miezi kadhaa. Hoeness ambaye amekuwa kioo cha Bayern kwa miaka kadhaa, alitoa kauli ya kustusha April mwaka huu akidai kuwa aliijulisha mamlaka ya kodi Januari kukagua akaunti yake anayomiliki huko Switzerland. Msemaji wa mahakama hiyo Andrea Titz amesema mshitakiwa sasa amepewa wiki nne kujibu mashitaka yake ambao amepelekewa mapema jana. Hoeness ambaye anaweza kukabiliwa na kifungo jela lakini akiwa na mategemeo ya kupata msamaha baada ya kujisalisha mwenyewe, amesema akunti hiyo ya Switzerland iliyokutwa na matatizo haina uhusiano wowote na Bayern.

Tuesday, July 30, 2013

NITAITUMIKIA DORTMUND KWA NGUVU ZANGU ZOTE PAMOJA NA YALIYOTOKEA - LEWANDOWSKI.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Borussia Dortmund, Robert Lewandowski ameahidi dhamiri yake ya kujitoa kwa dhati kwa klabu hiyo pamoja na kushindikana kwa uhamisho wake kwenda klabu ya Bayern Munich katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi. Lewandowski ambaye mkataba wake na Dortmund unamalizika 2014 alikataa kusaini mkataba mpya msimu uliopita akidai kuwa anategemea kuchagua klabu atakayokwenda mapema. Baada ya usajili kuanza na Lewandowski kutaka kuwa mchezaji wa pili kuchukuliwa na mahasimu wao Bayern baada ya Mario Goetze, Dortmund walizuia uhamisho wa nyota huyo ambao ungewaletea mamilioni ya euro. Lewandowski alikaririwa na gazeti moja nchini Ujerumani akidai kuwa atajitoa kwa nguvu zake zote kwa Dortmund haijalishi kitu gani kimetokea kwani aanapokuwa uwanjani huwa hafikirii mambo hayo. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Poland alimaliza msimu uliopita vyema kwa kufunga mabao 24 katika Ligi Kuu nchini Ujerumani na kuongeza mengine 10 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yakiwemo mabao manne aliyofunga katika mchezo mmoja dhdi ya Real Madrid.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MTIHANI WA UWAKALA WA WACHEZAJI, MECHI SEPT 26
Mtihani wa uwakala wa wachezaji (players agent) na uwakala wa mechi (match agent) wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Alhamisi ya Septemba 26 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Kutakuwa na jumla ya maswali 20 kwenye mtihani huo, 15 yanatoka FIFA kuhusiana na kanuni za kimataifa za mpira wa miguu na matano yatatoka TFF kuhusiana na kanuni mbalimbali zinazotawala mchezo huo nchini. Kwa ambao wangependa kufanya mtihani huo utakaokuwa katika lugha ya Kiingereza ambayo ni moja kati ya lugha nne rasmi za FIFA wanatakiwa kujisajili TFF kwa ada ya dola 50 za Marekani ambapo watapewa utaratibu na maeneo ambapo mtihani huo unalenga. Mtihani huo utafanyika saa 4 kamili asubuhi, na muda wa kufanya mtihani hautazidi dakika 90. Mpaka sasa Tanzania ina mawakala watano wa wachezaji wanaotambuliwa na FIFA. Mawakala hao ni John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully.WAAMUZI VPL KUFANYA MTIHANI WA UTIMAMU WA MWILI
Waamuzi wote wa daraja la kwanza (Class I) wanaotaka kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2013/2014 wanatakiwa kuhudhuria mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) utakaofanyika katika vituo viwili. Mtihani huo utafanyika Agosti 12,13 na14 mwaka huu katika vituo vya Dar es Salaam na Morogoro. Kituo cha Mwanza kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Manyara, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora. Kituo cha Dar es Salaam kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Njombe, Pwani, Ruvuma na Tanga. Washiriki wote wanakumbushwa kuwa ni lazima wafuate utaratibu huo wa vituo, na si vinginevyo. Pia waamuzi waliofungiwa (sio maisha) wanatakiwa kushiriki katika mtihani huo.RATIBA LIGI DARAJA LA KWANZA AGOSTI 14
Ratiba ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2013/2014 inayoshirikisha timu 24 zilizo katika makundi matatu zikicheza kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini) inatarajiwa kutolewa Agosti 14 mwaka huu. Kundi A linaundwa na timu za Burkina Moro ya Morogoro, JKT Mlale (Ruvuma), Kimondo SC (Mbeya), Kurugenzi Mufindi (Iringa), Majimaji (Ruvuma), Mkamba Rangers (Morogoro), Polisi (Iringa) na Polisi (Morogoro). African Lyon (Dar es Salaam), Friends Rangers (Dar es Salaam), Green Warriors (Dar es Salaam), Ndanda (Mtwara), Polisi (Dar es Salaam), Tessema (Dar es Salaam), Transit Camp (Dar es Salaam) na Villa Squad (Dar es Salaam) zinaunda kundi B. Timu za kundi C ni JKT Kanembwa (Kigoma), Mwadui (Shinyanga), Pamba (Mwanza), Polisi (Dodoma), Polisi (Mara), Polisi (Tabora), Stand United (Shinyanga) na Toto Africans (Mwanza). Tunapenda kukumbusha kuwa dirisha la usajili kwa madaraja yote ni moja ambapo usajili wa hatua ya kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti 3 mwaka huu wakati hatua ya pili ni Agosti 14 hadi 29 mwaka huu. Dirisha dogo litafunguliwa Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu.

AL MASRY WAONDOLEWA ADHABU YA KUFUNGIWA.

CHAMA cha Soka nchini Misri-EFA kimetangaza kuiondolea adhabu timu ya Al Masry kwa kuiruhusu kushiriki msimu mpya wa Ligi Kuu nchini humo ambayo inatarajiwa kuanza Agosti 22 mwaka huu. Al Masry walifungiwa mwaka mmoja na EFA baada ya vurugu zilizotokea Port Saied Februari mwaka jana ambapo mashabiki zaidi ya 72 wa Al Ahly waliuawa uwanjani. Msemaji wa EFA Azmy Megahed amesema Mahakama ya Usuluhishi wa Miechezo ya CAS imeiruhusu Al Masry kucheza na tayari wameshalipa ada yao ya ushiriki katika ligi hiyo. Hata hivyo Al Masry watakabiliwa na tatizo la kutafuta uwanja mwingine wa kutumia katika mechi zao za nyumbani kutokana na adhabu ya kufungiwa miaka mitatu uwanja wao wa Port Saied ikiwa bado haijamalizika. Maofisa awa Al Masry wanataka mechi zao kuchezwa Al Ismailiya lakini majeshi ya ulinzi walikataa wazo hilo kwasababu za kiusalama.

GUARDIOLA APANGA KUTOA UHURU ZAIDI KWA WACHEZAJI WAKE.

MENEJA mpya wa klabu ya Bayern Munich, Pep Guardiola anapanga kuacha umiliki wa chumba cha kubadilishia nguo chini ya himaya ya wachezaji wake ili waweze kujisikia huru wakati wa mapumziko. Katika Uwanja wa Allianz Arena ambao unamilikiwa na klabu hiyo, kocha huwa anakuwa na ofisi yake ndogo karibu na mlango wa kuingilia katika chumba cha kubadilishia nguo ambapo mara chache kocha aliyeondoka Jupp Heynckes alikuwa akiitumia kwa ajili ya kubakia karibu na wachezaji wake. Hata hivyo Guardiola anapanga kuwapa nyota wake uwanja mpana zaidi wa kuzungumza kwa uwazi na hata kukosoana wenyewe kwa wenyewe bila ya woga ndio maana ameamua kuanzisha ofisi nyingine mbali na chumba hicho. Guardiola amesema ni muhimu kwa wachezaji kupewa nafasi kwani ni eneo lao ambapo hutaniana na kuzungumza chochote bila woga na hata kumponda. Bayern inatarajiwa kuanza kutetea taji lao la Bundesliga Agosti 9 mwaka huu wakati watakapochuana na Borussia Monchengladbach.

PAPARAZI AMSHITAKI MARADONA KWA KUMPIGA.

MPIGA mmoja wa gazeti la watu maarufu nchini Argentina, amemtuhumu nguli wa soka wa zamani wa nchi hiyo Diego Maradona kwa kumpiga teke la kiuno na kumfungulia mashitaka polisi kutokana na tuhuma hizo. Mpiga picha huyo wa gazeti la Gente aitwaye Enrique Medina amesema shambulio hiyo lilitokea nje ya nyumba ya Maradona Jumapili usiku wakati akisubiria kumpiga picha nyota huyo. Medina alidai kuwa wakati akiwa hapo nguli huyo alimkimbilia kama anataka kupiga mpira wa adhabu na kumpiga kiunoni pamoja na kwenye paja na kumsababishia maumivu makali. Mwandishi huyo aliendelea kudai kuwa teke alilopigwa halikuwa la mtu wa kawaida kwani lilitoka kwa mtu ambaye amezoea kufanya hivyo na alionekana kuwa na hasira nyingi. Maradona amekuwa akilalamika mara kwa mara vyombo vya habari kumfuatilia kwa karibu ambapo mwaka 1994 aliwahi kufanya tukio kubwa kwa kupiga risasi hewani kuwatimua waandishi waliokuwa wakimfuatilia ambapo bunduki yake ilifungiwa miaka miwili.

BECKHAM AVAMIA KAMBI MADRID KUSALIMIA.

KIUNGO mahiri wa zamani wa klabu ya Real Madrid, David Beckham amevamia kambi ya timu hiyo iliyopo jijini Los Angeles, Marekani kwa ajili ya kusalimiana na wachezaji wenzake wa zamani aliowahi kucheza nao. Madrid ambao hivi sasa wananolewa na meneja mpya Carlo Ancelotti wapo huko kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Hispania unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 18 mwaka huu. Kabla ya kuitembelea Madrid, Beckham alitembelea klabu yake ya zamani ya Los Angeles Galaxy kabla pia ya kuzitembelea Phoenix, Miami na Saint Louis. Beckham alipiga picha na Cristiano Ronaldo baada ya mazoezi na pia kusaini fulana na mipira kwa mashabiki waliobahatika kwenda kuwatizama Madrid wakiwa mazoezini.

CAF YATUPILIA MBALI OMBI LA AL AHLY KUSOGEZA MECHI YAO DHIDI YA ORLANDO PIRATES.

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika-CAF limetupilia mbali maombi ya Al Ahly waliotaka kusogeza mbele mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa ya Afrika dhidi ya Orlando Pirates iliyotakiwa kuchezwa Agosti 4 kwa ajili ya mfungo wa Ramadhan. Katika taarifa ya klabu hiyo iliyotumwa katika mtandao wake walithibitisha kupokea barua kutoka CAF ya kukataliwa ombi lao hilo. Mapema Jumapili iliyopita mkurugenzi wa michezo wa Al Ahly Sayed Abdel Hafiz aliviambia vyombo vya habari nchini Misri kuwa klabu hiyo imeomba mchezo huo kusogezwa mbele kwa siku tano ili kuepuka matatizo wachezaji wake waliyokutana nayo katika mchezo dhidi ya Zamalek. Hafiz alidai kuwa wachezaji wake walikabiliwa na wakati mgumu katika mchezo huo baada ya kukataa kufungua na kucheza mchezo huo katika kipindi cha mchana kilichokuwa na joto kali. Klabu hiyo pia imetakiwa kutafuta uwanja mwingine kwa ajili ya mchezo huo wa kundi A baada ya jeshi kuwakatalia uwanja wao wa Air Defence uliopo jijini Cairo kwasababu za kiusalama.

Monday, July 29, 2013

BOLT KUSHINDANA NA FARAH KATIKA MBIO ZA HISANI.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi, Usain Bolt amekubali kushindana na nyota wa mbio ndefu kutoka Uingereza Mo Farah katika mbio za hisani za mita 600. Farah ambaye alishinda medali za dhahabu katika mbio za mita 5,000 na 10,000 katika mashindano ya olimpiki yaliyofanyika London mwaka jana ndio wanariadha waliong’aa katika michuano hiyo sambamba na Bolt ambaye naye alishinda dhahabu katika mbio za mita 100 na 200. Akihojiwa Bolt amesema atajiandaa kwa ajili ya mbio hizo ingawa alikiri zitakuwa ngumu kwake kwakuwa amezoea kukimbia umbali mfupi na kwa kasi kubwa. Bolt ambaye anashikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 100 na 200 alidai kuwa kukimbia mita 600 akijiandaa vizuri ataweza lakini mita 1,500 ni suala ambalo halitawezekana kwake.

REINA ASONONESHWA NA LIVERPOOL KUMPELEKA KWA MKOPO NAPOLI.

GOLIKIPA wa klabu ya Liverpool, Pepe Reina ameeleza kusikitishwa kwake kwa timu hiyo kukubali kumpeleka kwa mkopo katika klabu ya Napoli ya Italia kabla ya kumwambia kwanza. Golikipa huyo wa kimataifa wa Hispania, mwenye umri wa miaka 30 alijiunga na Italia kwa mkpo wa msimu mmoja baada ya Liverpool kumsajili Simon Mignolet kutoka Sunderland. Katika barua yake aliyowaandikia mashabiki wa klabu hiyo, Reina amesema alikuwa bado anataka kuendelea kubakia Anfield baada ya mipango yake ya kwenda Barcelona kukwama. Reina amesema ameshangazwa na hatua iliyochukuliwa na klabu hiyo kumtoa kwa mkopo bila hata kushauriana naye lakini amemua kuelewa kwasababu muda mwingine maamuzi magumu lazima yatolewe katika soka.

MIPANGO YA USAJILI IKO POA - MOYES.

MENEJA mpya wa klabu ya Manchester United, David Moyes amesisitiza kuwa mipango yake ya usajili katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi inakwenda vizuri pamoja na kushindwa kufanya usajili mkubwa mpaka sasa. United mpaka sasa wametuma ofa mbili kwa ajili ya kujaribu kumsajili Cesc Fabregas lakini wamekataliwa na Barcelona huku wakipigwa bao na Bayern Munich kwa kushindwa kupata saini ya Thiago Alcantara. Akihojiwa kuhusu mipango yake ya usajili, Moyes amesema usajili wa Fabregas sio pekee ambao anautegemea kwa msimu huu kwani anategemea katika muda uliobakia wa usajili atakuwa amepata wachezaji kadhaa. Mbali na Fabregas United pia wamekuwa wakihusishwa kutaka kuwasajili Maouane Fellaini na kiungo wa kati Yohan Cabaye ambaye anategemewa kuziba pengo la Paul Scholes.

HAMILTON AIBUKA KIDEDEA MASHINDANO YA HUNGARY GRAND PRIX.

DEREVA nyota wa mashindano ya langalanga, Lewis Hamilton wa timu ya Marcedes amefanikiwa kupanda ushindi wake wa kwanza akiwa na timu hiyo baada ya kuibuka kidedea katika mashindano ya Grand Prix ya Hungary. Hamilton alijituliza na kutumia kasi akiwashinda dereva Kimi Raikkonen wa timu ya magari ya Lotus aliyemaliza wa pili na Sebastien Vettel wa Red Bull aliyemaliza wa tatu. Mark Webber wa Red Bull alionyesha umahiri wake kwa kujikwamua kutoka nafasi ya kumi alikoanzia mashindano hadi kumpiku dereva wa Ferrari, Fernando Alonso. Kutokana na hali hio Raikkonen sasa anapanda kwa pointi moja mbele ya Alonso akishika nafasi ya pili kwa jumla ya pointi alizokusanya tangu kuanza kwa mashindano ya msimu huu wa 2013/2014 ingawa bado yuko nyuma ya kiongozi wa mashindano na mtetezi wa taji Sebastien Vettel kwa pointi 38.

Sunday, July 28, 2013

WACHEZAJI WAGENI WANAHATARISHA SOKA LA UJERUMANI - BIERHOFF.

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani, Oliver Bierhoff anaamini kuwa uchache wa wachezaji katika vilabu vya Bayern Munich na Borussia Dortmund ambao wanacheza katika timu ya taifa ya nchi hiyo unaweza kuwanyima nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Pamoja na mafanikio makubwa ambayo timu hizo mbili imeyapata katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu uliopita, Bierhoff ameonyesha wasiwasi wake kwa mwenendo wa timu ya taifa. Badala yake nguli huyo mwenye miaka 45 ametaka hatua za makusudi kwa vilabu vikubwa kuthamini vipaji vya vijana ili kuokoa soka la nchi hiyo lisije kuporomoka. Bierhoff amesema pamoja na Ujerumani kujivunia wachezaji nyota kama Mario Gotze, Mesut Ozil, Thomas Muller na Toni Kroos lakini nchi hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya kukosa washambuliaji pamoja na mabeki wa daraja la juu. Nguli huyo amesema kwasasa wanatakiwa kujipanga ili kuhakikisha wanaziba mapengo yaliyopo na kuendelea kubakia katika ushindani.

SEMENYA ASHINDWA KUFUZU MASHINDANO YA DUNIA.

MWANARIADHA nyota wa kike kutoka Afrika Kusini, Caster Semenya atashindwa kushiriki mashindano ya riadha ya dunia mwezi ujao baada ya kushindwa kufuzu katika mbio za mchujo zilizofanyika nchini Ubelgiji. Semenya alifanikiwa kushinda mbio za mita 800 katika mashindano hayo ya mchujo yaliyofanyika jijini Nivone kwa kutumia muda wa dakika 2 sekunde 01.86 lakini muda huo haukutosha kumfanya kufikia kiwango kilichohitajika ambacho ni dakika 2 sekunde 01.50. Katika mbio hizo Sanne Verstegen wa Uholanzi alimaliza katika nafasi ya pili akitumia muda wa dakika 2 sekunde 02.09. Hiyo ni mara ya kwanza kwa Semenya kushindana toka katika michuano ya olimpiki iliyofanyika jijini London mwaka jana baada ya kipindi kirefu kukaa kando kutokana na maumivu ya goti. 


AL AHLY YAOMBA MCHEZO WAO DHIDI YA PIRATES KUSOGEZWA MBELE KWA AJILI YA RAMADHAN.

KLABU ya Al Ahly ya Misri imeliomba Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kusogeza mbele mchezo wao dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini mpaka Agosti 9 mwaka huu. Mkurugenzi wa michezo wa Al Ahly Sayed Abdul Hafez alithibitisha timu hiyo kuandika barua rasmi kwa CAF ya kusogeza mbele mchezo huo mpaka Agosti 9 badala ya Agosti kama ulivyopangwa kwasababu ya mfungo wa mwezi wa Ranadhan ambapo wacheza wengi wa timu hiyo wanakuwa wamefunga. Hafez pia aliongeza kuwa Wizara ya mambo ya Ndani ya nchi hiyo imekataa kuwawekea ulinzi kwa ajili ya mchezo huo jijini Cairo au Alexandria hivyo wanatarajia mechi hiyo kuchezwa katika mji wa El Gouna au Aswan. Hafez amesema wamefikia hatua hiyo baada ya timu hiyo kucheza dhidi ya Zamalek mchana na wachezaji kukataa kufungulia ambapo wote waliathirika mpaka hivi sasa kutokana na kucheza kwenye jua kali huku wakiwa wamefunga. Naye kocha wa Pirates Roger De Sa ameonyesha wasiwasi wake wa kucheza na Al Ahly jijini Cairo kutokana na vurugu zinazoendelea lakini anaamini kuwa CAF itatoa uamuzi sahihi kuhusiana na mahali patakapochezwa mchezo huo.

MKONGWE DAVIDS AFANYA KITUKO.

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Edgar Davids ameamua kufanya kituko kwa kuamua kuvaa fulana yenye namba moja mgongoni msimu huu pamoja na ukweli kwamba yeye ni mchezaji wa kiungo. Davids ambaye ni kocha mchezaji wa klabu ya Barnet amesema ameamua kuvaa fulana yenye namba hiyo ingawa anajua ni utamaduni kwa namba moja kuvaliwa na golikipa. Baada ya namba hiyo kuchukuliwa na Davids sasa golikipa wa Barnet, Graham Stack anatarajiwa kuvaa fulana yenye namba 29 katika msimu mpya ambapo timu hiyo itakuwa ikipambana kujaribu kupanda daraja tena baada ya kushuka msimu uliopita. Stark amesema Davids alimfuata na kumuomba kuvaa fulana yenye namba moja msimu ujao na alimruhusu na kumwambia anaweza kumpa yoyote ile.

HEYNCKES ASIKITISHWA NA KIPIGO CHA BAYERN.

MENEJA wa zamani wa klabu ya Bayern Munich, Jupp Heynckes amedai kutofurahishwa na matokeo ya timu hiyo kufungwa mabao 4-2 na Borussia Dortmund katika fainali ya Supercup iliyochezwa jana. Heynckes mwenye umri wa miaka 68 ambaye aliiongoza Bayern kushinda mataji matatu msimu uliopita alikuwepo katika Uwanja wa Signal Iduna Park kushuhudia mchezo huo uliokuwa na kila aina ya ushindani. Akihojiwa kocha huyo amesema hana shaka na Pep Guardiola kuipa mafanikio Bayern katika siku zijazo lakini kama ilivyokuwa kwa wengine na yeye pia amesikitishwa na kipigo hicho kwakuwa bado ni vijana wake. Guardiola alichukua nafasi ya Heynckes ambaye mkataba wake ulimalizika msimu uliopita lakini kocha huyo ambaye ni raia wa Ujerumani amesisitiza kuwa hajutii kustaafu. Heynckes amesema kuna mahala mtu unatakiwa kuamua kustaafu na hicho ndicho atakachofanya kwasasa, na kuwa anatizama Bundesliga akiwa ametulia kwenye kochi sebuleni kwake.

Saturday, July 27, 2013

MAREKANI YAWANIA TAJI LA TANO MICHUANO CONCACAF.

TIMU ya taifa ya Marekani inatarajiwa kujitupa uwanjani kuwania taji lao la tano la michuano ya Kombe la Dhahabu dhidi ya Panama, michuano ambayo hushirikisha nchi za Amerika kaskazini-CONCACAF. Katika fainali hiyo itakayopigwa baadae leo, Marekani inatarajiwa kuongozwa na mshambuliaji wake nyota Landon Donovan ambaye mpaka sasa amefunga mabao matano katika mechi sita za michuano hiyo alizocheza. Akihojiwa kuhusiana na mchezo huo Donovan amesema kuwa mashindano hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwao na ni mategemeo yao wataendelea kucheza kwa kiwango cha juu na kutawadhwa mabingwa wapya wa michuano hiyo. Marekani inanolewa na Mjerumani Jurgen Klinsmann imewahi kunyakuwa taji hilo mwaka 1991, 2002, 2005 na 2007 huku hii ikiwa ni fainali yake ya tano mfululizo.

LAMOUCHI KUMREJESHA DROGBA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Sabri Lamouch amesema anatarajia kumtumia nahodha wa timu hiyo Didier Drogba katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Mexico unaotarajiwa kuchezwa Agosti 14 mwaka huu. Mshambuliaji huyo anayekipiga katika klabu ya Galatasaray hajaitumikia timu yake ya taifa toka wapate matokeo mabay katika michuano ya Mataifa ya Afrika iliyofanyika nchini Afrika Kusini mapema mwaka huu. Kocha huyo amekuwa akidai amemuacha Drogba kutokana na kushuka kiwango chake kitu ambacho kimekuwa kikipingwa na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea lakini huku akiahidi kuongeza bidii ili kupata tena nafasi katika kikosi hicho. Ivory Coast tayari wamefuzu hatua ya mwisho kwa ajili ya kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia 2014 na wanatarajia kutumia mechi yao dhidi ya mexico kama maandalizi kwa ajili mchezo wao wa mwisho dhidi ya Morocco. Mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Mexico unatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa MetLife jijini New York, Marekani.

WENGER AVUNJA UKIMYA SUALA LA SUAREZ.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amevunja ukimya kuhusu klabu hiyo kutaka kumsajili Luis Suarez akidai kuwa klabu hiyo imejiandaa kusubiri ili iweze kupata saini ya mshambuliaji huyo wa Liverpool. Arsenal waliboresha ofa yao kufikia paundi milioni 40 kwa ajili ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay mapema wiki hii lakini mkurugenzi mtendaji wa Liverpool Ian Ayre alithibitisha kuwa ofa zote za klabu hiyo zilikataliwa. Akihojiwa na waandishi wa habari katika ziara yao ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi huko jijini Saitama, Japan Wenger amesema kwasasa hawako karibu kumsajili Suarez au mchezaji yoyote yule. Wenger amesema kwasasa ni ngumu kujua mambo yanavyoendelea kwa sababu kila mtu yuko katika ziara hivyo ni ngumu kufanya mawasiliano na watu hivyo baada ya ziara kumalizika anadhani wanaweza kujua kinachoendelea lakini kwasasa inabidi wasubiri.

ANCELOTTI AMPAMBA RONALDO.

MENEJA mpya wa klabu ya Real Madrid Carlo Ancelotti amemuelezea Cristiano Ronaldo kama mchezaji wa kipekee kuliko wote ambao amewahi kuwafundisha. Ancelotti amesema amefundisha wachezaji wengi wenye vipaji lakini Ronaldo ni tofauti kwasababu ana kipaji cha kipekee na nguvu, kila kocha lazima afurahie kumfundisha mchezaji huyo. Kocha aliendelea kudai kuwa Ronaldo ni mchezaji mwenye weledi na ana uhakika atakuwa na msimu wenye mafanikio katika kipindi cha 2013-2014. Ronaldo alimaliza katika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji kwenye La Liga msimu uliopita akiwa amefunga mabao 34 katika mechi 34 alizocheza akiwa amepitwa na mshindi wa tuzo ya Ballon r’Or Lionel Messi ambaye alifunga mabao 46.

BOLT ASHINDA KATIKA MASHINDANO YA LONDON ANNIVERSARY GAMES.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi ambaye ni bingwa mara sita wa michuano ya olimpiki, Usain Bolt kutoka Jamaica amefanikiwa kuweka rekodi ya muda bora msimu huu katika mbio za mita 100 za kuadhimisha mwaka mmoja toka kufanyika michuano olimpiki jijini London. Katika michuano ya olimpiki mwaka jana Bolt alifanikiwa kutetea medali zake za dhahabu katika mbuio za mita 100 na mita 200 huku pia akiweka rekodi katika mbio za mita 400 kupokezana vijiti. Mwanariadha nyota chipukizi wa Uingereza James Dasaolu ambaye alitegemewa kuleta upinzani kwa Bolt alijitoa kabla ya kuanza kwa mbio hizo kutokana na kuumia wakati akipasha misuli moto. Katika mbio za jana Bolt alianza taratibu kama ilivyo kawaida yake lakini aliongeza kasi na kuwapita wapinzani wake mwishoni mwa mbio hizo na kupelekea kushinda mbio hizo kwa kutumia muda wa sekunde 9.85. Nafasi ya pili katika mbio hizo ilishikiliwa na Michael Rodgers wa Marekani aliyetumia muda sekunde 9.98 akifuatiwa na Nesta Carter wa Jamaica aliyetumia sekunde 9.99 wakati Dwain Chambers Muingereza pekee aliyebakia katika mbio hizo baada ya Dasaolu kujitoa alishika nafasi ya tano kwa kutumia muda wa sekunde 10.10.

Thursday, July 25, 2013

TAIFA STARS YATUA UGANDA KUIVAA THE CRANES.

TAIFA Stars imewasili salama hapa Kampala tayari kwa mechi ya marudiano ya mchujo dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini. Stars ambayo iliwasili ikitokea jijini Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakwenda Afrika Kusini mwakani imefikia hoteli ya Mt. Zion iliyoko eneo la Kisseka katikati ya Jiji la Kampala. Kocha Mkuu wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen ameridhishwa na kiwango cha hoteli hiyo, kwani ndiyo ambayo timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ilifikia Novemba mwaka jana ilipokuja Kampala kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA). Stars ambayo ilitiwa chachu na Rais Jakaya Kikwete alipokutana nayo Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati ikiondoka kuja Kampala, na kuitakia kila la kheri itafanya mazoezi yake ya mwisho kesho (Julai 26 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kujiandaa kwa mechi ya Jumamosi. Kocha Kim amesema ingawa mechi hiyo ni ngumu, lakini kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwani wachezaji wako wako vizuri na ari kwa ajili ya mechi iko juu. Wachezaji wote wako katika hali nzuri, isipokuwa Khamis Mcha aliyekuwa na maumivu ya goti, lakini kwa mujibu wa madaktari wa timu anaendelea vizuri kwani tayari wanampa mazoezi mepesi. Kikosi cha kamili cha Stars ilichoko hapa kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas. Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa. Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari siku ya Jumatatu (Julai 29 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

OFA YA ARSENAL KWA SUAREZ HAILINGANI NA THAMANI YAKE - RODGERS.

MENEJA wa klabu ya Liverpool Brendan Rodgers amedai kuwa ofa waliyotoa Arsenal hailingani na thamani aliyonayo mshambuliaji wake Luis Suarez. Liverpool imekataa ofa iliyovunja rekodi ya klabu hiyo ya paundi milioni 40 lakini Suarez anaonekana anataka kuzungumza na timu hiyo yenye maskani yake jijini London. Rodgers amesema kama Arsenal wanamtaka mchezaji huyo wanatakiwa watoe dau ambalo litalingana na thamani yake. Kwa maana hiyo Arsenal itatakiwa kuongeza dau zaidi baada ya ofa zake mbili kukataliwa na klabu hiyo. Suarez alionekana kwa mara ya kwanza uwanjani toka alipomng’ata mkono beki wa Chelsea Branislav Ivanovic msimu uliopita wakati alipotokea benchi katika mchezo wa kirafiki walioshinda kwa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Melbourne. Suarez alijiunga na Liverpool akitokea klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi mwaka 2011 kwa ada ya paundi milioni 22.7.

SHUTI LA RONALDO LAMVUNJA MKONO MTOTO WA MIAKA 11.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid ya Hispania amemvunja mkono mtoto wa miaka 11 kwa bahati mbaya wakati akipiga faulo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Bournemouth. Mtoto huyo aitwaye Charlie Silverwood alikuwa amekaa nyuma ya goli katika mchezo huo uliochezwa mwihoni mwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Goldsands wakati mpira huo uliopigwa na ronaldo ulipomfuata kwa kasi. Akihojiwa Silverwood amesema ilikuwa ni faulo ya kwanza kupigwa na Ronaldo katika mchezo huo na moja kwa moja mpira ulimfuata yeye hivyo alijaribu kuuzuia na kiganja cha mkono wake lakini kutokana na nguvu mpira huo uliusukuma mkono wake juu na kumvunja kiwiko chake. Kijana huyo aliendelea kudai kuwa kuiona Madrid ikicheza na klabu yake ya nyumbani ni bahati ambayo haiji mara mbili hivyo baada ya kuumia aliendelea kumalizia kutazama mchezo huo mpaka mwisho ingawa kwa maumivu na baada ya ndio akaelekea hospitali kupata matibabu. Madrid imemtumia salamu za pole kijana huyo na kumwambia kuwa fulana ya timu hiyo itakayokuwa imesainiwa na Ronaldo itatumwa kwake kama zawadi ya pole.

HIGUAIN, REINA WAFAULU VIPIMO VYA AFYA NAPOLI.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Argentina, Gonzalo Higuain na golikipa wa kimataifa wa Hispania Pepe Reina wanakaribia kukamilisha uhamisho wao wa kwenda Napoli baada ya kufaulu vipimo vya afya. Rais wa klabu ya Napoli, Aurelio De Laurentiis aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kimajii wa twitter kuwa wachezaji hao wawili walifaulu vipimo vyao na wanatarajiwa kujiunga na wenzao muda wowote. Higuain ambaye alikuwa akimendewa na klabu za Arsenal na Juventus, ameripotiwa kuigharimu Napoli euro milioni 37 wakati Reina yeye amejiunga na klabu hiyo kwa mkopo akitokea Liverpool. Mwishoni mwa wiki iliyopita Napoli ilimuuza mshambuliaji wake wa kimataifa wa Uruguay Edinson Cavani kwenda Paris Saint Germain kwa uhamisho ulioweka rekodi wa euro milioni 64.

POWELL APANIA KUTEREJEA UWANJANI BAADA YA KESI YAKE KUISHA.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi Asafa Powell kutoka Jamaica amesema anataka kurejea uwanjani mapema iwezekanavyo baada ya kushindwa kwenye vipimo vya dawa za kuongeza nguvu. Powell mwenye umri wa miaka 30 alikutwa na chembechembe za dawa ya oxilofrine ambazo zimekatazwa michezoni katika damu yake aliyochukuliwa katika michuano ya riadha ya Jamaica. Mara baada ya taarifa hizo kutoka, Powell alidai kuwa hakutumia dawa hizo kwa makusudi na kwamba atapokea adhabu yoyote itakayotolewa dhidi yake inga wa alikiri kuwa katika kipindi kigumu katika maisha yake ya mchezo huo. Powell na mwanariadha mwingine nyota wa mbio fupi kutoka Marekani Tyson Gay walishinda vipimo hivyo siku 10 zilizopita na sasa wote wanasubiri vipimo vingine ili kuthibitisha kabla ya kutolewa uamuzi wowote dhidi yao. Powell ndio alikuwa mwanariadha wa mwisho kushikilia rekodi ya mbio za mita 100 kabla ya Usain Bolt naye pia wa Jamaica kuja kufunja rekodi hiyo mwaka 2008.

MESSI AKIRI KUATHIRIWA NA KUONDOKA KWA VILANOVA.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Barcelona, Lionel Messi amekiri kuwa matatizo ya kiafya ya Tito Vilanova yamekuwa pigo kubwa kwao lakini ana uhakika kuwa timu hiyo itafanikiwa kupita katika kipindi hicho kigumu cha kuondoka kwa kocha huyo. Vilanova alitangaza kujiuzulu wiki iliyopita ili aweze kuendelea na matibabu yake ya saratani na Barcelona ikamteua kocha wa zamani wa Newell Old Boys, Gerardo Martino kuchukua nafasi yake. Messi amesema wamesikitishwa kwa kilichotokea kwa Vilanova lakini kikosi chao bado kipo imara na wataendelea kusonga mbele kwa heshima yake. Messi ambaye alicheza dakika 45 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Bayern Munich jana ambao walichapwa kwa mabao 2-0, amesema kwasasa yuko fiti na majeruhi yaliyokuwa yakimsumbua msimu uliopita yamekwisha.

Wednesday, July 24, 2013

SIJUTII KUINUNUA QPR - FERNANDES.

MMILIKI wa klabu ya Queens Park Rangers, QPR, Tony Fernandes amesema hajutii kuinunua klabu hiyo pamoja na kushuka daraja na kudai kuwa ana mategemeo ya kuigeuza na kuwa klabu yenye mafanikio. Fernandes ambaye alitenga mamilioni ya paundi kwa ajili ya kuibakisha klabu hiyo ligi kuu amesema hana mpango wa kumiliki klabu kubwa kama Liverpool au Arsenal kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kununua mafanikio ya wengine. Bilionea huyo wa Malaysia ameamua kuchagua QPR ili aweze kuipa mafanikio kama zilivyo klabu nyingine kubwa nchini Uingereza na ana mategemeo ya kurejea tena ligi kuu katika kipindi cha muda mfupi ujao. Fernandes ambaye pia anamiliki timu ya Caterham ya langalanga amesema alikuwa akijua kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kushuka daraja wakati alipoinunua klabu hiyo mwaka 2011.

HIGUAIN KWENDA NAPOLI.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Argentina na klabu ya Real Madrid, Gonzalo Higuain inasemekana amekamilisha usajili wake kwenda Napoli ya Italia kwa mujibu ya magazeti ya nchini Hispania. Gazeti la Marca la nchi hiyo lilidai kuwa Napoli wamelipa kiasi cha euro 37 kwa ajili saini ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 25. Kama mpango huo ukikamilika Higuain atakuwa mchezaji wa tatu wa Madrid kuuzwa Napoli katika kipindi hiki cha uasajili majira ya kiangazi baada ya Raul Albiol na Jose Callejon kuwa tayari wameuzwa. Kwa mujibu wa taarifa za gazeti hilo pesa zitakazopatikana kwa mauzo ya Higuain zitatumika katika kutafuta saini za Gareth Bale wa tottenham na Luis Suarez wa Liverpool.

HAYATOU AMTEUA JORDAAN KUWA MSHAURI WAKE.

OFISA mkuu wa zamani wa kamati ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia 2010, Dr Danny Jordaan ameteuliwa kuwa mshauri wa rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF Issa Hayatou. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa CAF imeeleza kuwa uteuzi wa Jordaan umekuja kufuatia mchango wake anaoendelea kutoka katika kunyanyua soka la Afrika. huku Hayatou akiongeza kuwa anategemea mafanikio makubwa kwa kushirikiana vyema na Jordaan. Jordaan amewahi kufanya kazi kama Ofisa Mkuu wa Chama cha Soka cha Afrika Kusini-SAFA kati ya mwaka 1997 na 2001 na pia amefanya kazi kama mjumbe wa bodi ya masoko na luninga ya FIFA kati ya mwaka 1998 na 2003. Kwasasa Jordaan anafanya kazi kama mshauri maalumu wa FIFA wa michuano ya Kombe la Dunia 2014 itakayofanyika nchini Brazil.

MARTINO ATAPATA MAFANIKIO BARCELONA - CRUYFF.

NGULI wa soka wa zamani wa klabu ya Barcelona, Yohan Cruyff anaamini kuwa kocha mpya wa klabu hiyo Gerardo Martino anaweza kupata mafanikio kama ilivyokuwa kwa Frank Rijkaard na pep Guardiola pamoja nauzoefu mdogo alionao katika soka la Ulaya. Rijkaard alifanikiwa kushinda mataji matano kati ya kipindi cha mwaka 2003 na 2006 pamoja na kutoka kufundisha klabu ndogo ya Sparta Rotterdam wakati Guardiola ambaye alirithi mikoba yake yeye aliibuka kukota kikosi B cha klabu hiyo lakini naye alipata mafanikio makubwa. Barcelona walitangaza kumpa mkataba wa miaka miwili Martino huku akiwa hajafundisha timu yoyote barani Ulaya lakini Cruyff anaamini kocha mwenye umri wa miaka 50 ataleta mafanikio Camp Nou. Cruyff amesema hajui chochote kuhusu kocha huyo lakini Rijkaard na Guardiola walianza kuifundisha Barcelona wakiwa hawana mafanikio yoyote kama makocha hivyo hana shaka kwamba Martino naye anaweza kufanikiwa.

MARADONA AFANYIWA UPASUAJI WA MACHO.

NGULI wa soka nchini Argentina, Diego Maradona amefanyiwa upasuaji wa macho ambao umemalizika kwa mafanikio. Maradona mwenye umri wa miaka 52 alifanyiwa upasuaji huo ili kukwangua utandu uliokuwa katika macho yake ambao ulikuwa ukisumbua kutokuona sawasawa katika mji wa Mendoza uliopo magharibi mwa Argentina. Daktari aliyemfanyia upasuaji Roberto Zaldivar aliwaambia waandishi wa habari kuwa Maradona alikuwa akiendelea vyema na upasuaji huo ni wa kawaida kwa watu wenye umri kama wake. Maradona anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi kabla ya kurejea Buenos Aires na baadae kwenda Dubai ambako anafanya kazi kama balozi wa soka.

Tuesday, July 23, 2013

TUMEJIANDAA KUIKABILI UGANDA - KIM.

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwenye mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayochezwa Jumamosi jijini Kampala. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo, Kim amesema tangu kikosi chake kimeingia kambini Julai 14 mwaka huu, wachezaji wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mazoezi na wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo. “Uganda ni timu bora kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Mechi itakuwa ngumu, tunaamini tunakwenda kufanya vizuri. Tayari tunayo mikakati kwa ajili ya mechi hiyo, tunakwenda kuikamilisha Kampala,” amesema Kim. Hata hivyo, Kim amesema licha ya mwitikio mzuri wa wachezaji kwenye mazoezi lakini wanakabiliwa na changamoto ya wengi wa wachezaji kuwa wamefunga wakati wachezaji wanapokuwa kambini wanatakiwa kula, kunywa na kupumzika. “Hiki ni kipindi kigumu kwa mpira wa miguu, na suala la kufunga ni la kiimani ambapo hatuwezi kuwazuia wachezaji kufunga. Karibu nusu ya wachezaji wanafunga, hii ni changamoto ambayo tunaiheshimu,” amesema Kim na kuongeza kuwa ni wazi kikosi chake cha kwanza kitakuwa na mabadiliko baada ya beki Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio nchini Uholanzi. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaondoka Mwanza kesho (Julai 24 mwaka huu) saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 8.15 mchana. Wachezaji waliomo kwenye msafara huo ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas. Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.

MADRID YAMKOMALIA VILLAS-BOAS.

MENEJA wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Andre Villas-Boas kwa mara nyingine amesisitiza kuwa Gareth Bale hawezi kwenda popote katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi lakini gazeti la Marca la Hispania limedai kuwa tayari nyota huyo wa kimataifa wa Wales ameshakamilisha uhamisho kwenda Real Madrid. Gazeti hilo lilidai kuwa Madrid wako katika hatua za mwisho za kumsainisha Bale mkataba wa miaka sita ambao utakuwa na thamani ya paundi milioni 8.5 kwa mwaka. Mbali na taarifa hiyo gazeti hilo pia lilidai kuwa Bale tayari amewaambia viongozi wa Spurs kuwa anataka kuondoka kwenda Santiago Bernabeu. Akihojiwa katika ziara ya Spurs nchini Hong Kong, Villas-Boas kwa mara nyingine tena alikana tetesi hizo na kudai kuwa Bale haendi kokote lakini akithibitisha kuwa klabu hiyo ina mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Valencia Roberto Soldado.

FINIDI GEORGE KUVIFUNDISHA VITOTO VYA REAL MALLORCA.

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Finidi George ametajwa kuwa kocha mpya wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 16 ya Real Mallorca ya Hispania. Akihojiwa na mtandao wa Supersport, George amesema ni heshima kubwa kwake kupata nafasi hiyo na ni mategemeo yake wataweza kuwapandisha wachezaji watatu au wanne katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo. George amesema kwasasa ana leseni ya daraja la B ya ukocha inayotambuliwa na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA lakini kutokana na kazi hiyo aliyopata itakuwa kazi rahisi kwake kusomea kozi ya ukocha mwakani ili aweze kupata leseni daraja A. Mchezaji huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi ambacho kilinyakuwa taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya amesema jina zuri alilojitengenezea kipindi akicheza soka ndio linamemfanya kupata nafasi hiyo. Amesema anawakumbuka wachezaji wenzake wengi aliocheza nao wakati akiwa Ajax, Malorca na Real Betis ambao kwasasa ni makocha hivyo akifanya kazi hiyo kwa kujituma anadhani na yeye atakuwa katika nafasi kama za wenzake huko mbele.

MAJERUHI YAZIDI KUIANDAMA ARSENAL.

KLABU ya Arsenal imepata pigo lingine baada ya beki wake wa kushoto Nacho Monreal kuingia katika orodha ya wachezaji majeruhi baada ya kuumia mgongo wakati akiwa katika mapumziko yake. Monreal mwenye umri wa miaka 27 alipewa mapumziko ya ziada baada kushiriki katika ya Kombe la Shirikisho akiwa na timu ya taifa ya Hispania hatua iliyopelekea kukosa ziara ya kujiandaa na msimu mpya ya Arsenal nchini Japan. Lakini akiwa mapumzikoni Monreal aliumia mgongo na Wenger hafamu chanzo cha kuumia kwa beki huyo ambaye atakosa mechi za mwanzoni mwa msimu. Ukuta wa timu ya Arsenal unaweza kuwa dhaifu mwanzoni mwa msimu 2013-2014 baada ya Thomas Vermaelen, Laurent Koscielny na golikipa Wojciech Szczesny nao pia wakiwa majeruhi.

MARTINO KOCHA MPYA BARCELONA.

KLABU ya Barcelona imemteua Gerardo Martino kutoka Argentina kuwa kocha mpya wa klabu hiyo akichukua nafasi ya Tito Vilanova aliyejiuzulu kutokana na maradhi ya saratani yanayomsumbua. Martino mwenye umri wa miaka 50 amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuwafundisha Barcelona ambao ni mabingwa wa La Liga msimu uliopita. Makubaliano hayo yalifanyika mapema jana ambapo wasaidizi wake wanatarajiwa kuwa waargentina wenzake Elvio Paolorroso na Jorge Pautasso ambao alikuwa akifanya nao kazi katika klabu ya Newell Old Boys ya Argentina. Martino hajawahi kufundisha Ulaya kabla lakini amefundisha vilabu mbalimbali nchini Argentina ikiwemo timu ya taifa ya Paraguay na pia ni rafiki wa karibu wa nyota wa Barcelona Lionel Messi na baba yake Jorge kwasababu wanatoka katika mji mmoja wa Rosario. Kocha huyo anatarajiwa kutua nchini Hispania Jumatano kwa ajili ya kutambulishwa mbele ya waandishi wa habari na mashabiki kabla ya kuanza kibarua chake rasmi Alhamisi ya wiki hii.

GUARDIOLA USO KWA USO NA BARCELONA.

MENEJA mpya wa klabu ya Bayerm Munich, Pep Guardiola anatarajiwa kukutana na timu yake ya zamani ya Barcelona katika mchezo wa kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi barani Ulaya. Barcelona walitua jijini Munich bila kuwa na kocha wao mkuu baada ya Tito Vilanova kujiuzulu wadhifa wake Ijumaa iliyopita kwa matatizo ya kiafya huku klabu hiyo ikiwa katika mchakato wa kutafuta kocha mpya. Msadizi wa Vilanova Jordi Roura ndiye atachukua mikoba yake kwa muda katika mchezo huo wa kirafiki utakaofanyika Allianz Arena. Guardiola alichukua mikoba rasmi ya kuinoa Bayern mapema mwezi uliopita baada ya kuchukua mapumziko ya mwaka mzima toka alipoondoka Barcelona katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka jana.

FIFA YAITOLEA KITANZI CAMEROON.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetangaza kuondoa adhabu ya kuifungia Cameroon kushiriki mechi za kimataifa baada ya kuundwa kamati ya muda itakayoongozwa na Joseph Owona. Kwa maana hiyo klabu ya Coton Sport sasa inaweza kucheza na Sewe katika michuano ya Kombe la Shirikisho mwishoni mwa wiki hii huku pia timu ya taifa ya Cameroon nayo ikichuana na Cameroon katika mechi za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani-CHAN. FIFA ilifikia hatua ya kulifungia Shirikisho la Soka la Cameroon-Fecafoot baada ya kutokea mganganyiko katika uchaguzi wake ambao ulimrudisha madarakani Mohamed Iya ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi mahakamani ya matumizi mabaya ya fedha wakati akiwa kiongozi wa kampuni moja ya katani nchini humo. Katika barua iliyotumwa na FIFA katika mtandao wake imedai kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kuundwa kwa kamati hiyo itakayoliongoza shirikisho hilo kwa muda mpaka hapo utakapofanyika uchaguzi mwingine.

NFF YAWAFUNGIA MAISHA WACHEZAJI NA VIONGOZI.

SHIRIKISHO la Soka nchini Nigeria-NFF limewafungia maisha wachezaji na viongozi wote walioshiriki katika mechi mbili za mtoano kwa ajili ya kupanda daraja. Katika mechi hizo klabu ya Plateau United Feeders waliifunga Akurba FC kwa mabao 79-0 wakati timu ya Police Machine FC wenyewe waliigaragaza Bubayaro FC kwa mabao 67-0. Mbali na adhabu hizo kwa wachezaji na viongozi vilabu navyo vimefungiwa miaka 10 huku kamati ya NFF iliyokuwa ikichunguza tukio hilo imependekeza waamuzi nao wafungiwe maisha kujishughulisha na mambo ya michezo. Plateau United Feeders na Police Machine zilikwenda kwenye mechi zikiwa na alama sawa huku kila timu ikitaka kupanda daraja ambapo mabao 72 ya Feeders yalifungwa katika kipindi cha pili wakati Police Machine nao walifunga mabao 61 baada ya kipindi cha mapumziko. Matokeo hayo yalizua gumzo kubwa na kupelekea NFF kuanza uchunguzi haraka huku Shirikisho la Soka Duniani-FIFA nalo likifuatilia tukio hilo kujua hatma yake.

Monday, July 22, 2013

KUONDOKA KWA VILANOVA PIGO KWA BARCA - PUYOL.

NAHODHA wa klabu ya Barcelona, Carles Puyol ameeleza uamuzi wa Tito Vilanova kuachia ngazi kuinoa klabu hiyo kuwa ni pigo kubwa. Vilanova mwenye umri wa miaka 44 alitangaza kuachia ngazi wiki iliyopita ili zweze kuendelea na matibabu yake ya saratani baada ya kuiongoza Barcelona kunyakuwa taji la La Liga katika msimu wa 2012-2013. Puyol amekiri kuwa habari ya kujizulu kwa Vilanova imekuja kwa mshituko lakini ameahidi kuonyesha kiwango cha hali ya juu msimu ujao ikiwa kama sehemu ya kumshukuru kocha huyo. Beki huyo ambaye msimu uliopita alikuwa akisumbuliwa na majeruhi amedai kuwa wakati Vilanova akiwaaga aliwaomba kujituma kwa bidii katika msimu mpya uliopo mbele yao na watafanya hivyo kwa heshima yake.


MOYES AMKOMALIA FABREGAS.

MENEJA wa klabu ya Manchester United David Moyes amethibitisha kuwa klabu hiyo imetuma ofa nyingine kwa ajili ya kujaribu kumsajili Cesc Fabregas na kuonya kuwa bado hajakata tamaa na kiungo huyo wa Barcelona. Akihojiwa na waandishi wa habari katika Uwanja wa Nissan jijini Yokohama, Japan, Moyes amesema ofisa mkuu wa klabu hiyo Ed Woodward bado anafanya mawasiliano na Barcelona kuhusiana na Fabregas baada ya kutuma ofa ya pili inayokadiriwa kufikia paundi milioni 30 ambayo itakuwa rekodi mpya ya klabu kwenye usajili. Moyes alidai kuwa ingawa wana wachezaji kadhaa ambao wako katika mipango yao kama usajili wa Fabregas ukishindikana lakini kwasasa bado hawajakata tamaa ya kupata saini ya nyota huyo. United kwasasa wako katika ziara yao ya tatu jijini Tokyo ambapo tayari nyota wake Shinji Kagawa, Ashley Young na Chris Smalling wameshaungana na wenzake baada ya kupona majeraha yao.

MOURINHO AMTAKA MOYES KUACHANA NA NDOTO ZA KUMREJESHA RONALDO OLD TRAFORD.

MENEJA mpya wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amempasha meneja wa Manchester United, David Moyes kusahau ndoto zake za kujaribu kumrejesha Cristiano Ronaldo Old Traford. Kuna tetesi kuwa United wako katika harakati za kujaribu kumrejesha nyota huyo wa kimataifa wa Ureno pamoja na meneja mpya wa Real Madrid Carlo Ancelotti kusisitiza kuwa hawatamuuza. Lakini Mourinho ambaye msimu uliopita alikuwa akiinoa klabu hiyo amedai kuwa hadhani kama Madrid wanaweza kumruhusu Ronaldo kuondoka kwasababu ya uwezo mkubwa wa kifedha walionao kwasasa. Mourinho amesema Madrid ni klabu tajiri duniani na hawana sababu ya kumuuza nyota huyo hivyo wanaweza kukataa ofa yoyote itakayotolewa kwa ajili ya kumchukua.

FROOME BINGWA WA MICHUANO YA TOURE DE FRANCE.

MSHINDANO ya baiskeli yajulikanayo kama Tour de France yamefikia tamati jana kwa Chris Froome wa Uingereza kutawadhwa bingwa mpya wa mashindano ambayo ni ya 100 toka kuanzishwa kwake. Akishinda taji hilo kwa zaidi ya dakika nne, Froome alishikana mikono na na wenzake wa timu ya Sky wakati akikatisha katika msitari wa ushindi jijini Paris, Ufaransa. Huo unakuwa ushindi wa pili kwa Uingereza kwenye michuano hiyo baada ya mwendesha baiskeli Sir Bradley Wiggins ambaye naye anatoka katika timu ya Sky kushinda michuano hiyo mwaka jana. Mashindano yalishirikisha waendesha baiskeli kutoka nchi mbalimbali ambapo waliendesha baiskeli kwa kilometa 3,200 katika miji mbalimbali ya ya Ufaransa katika kipindi cha wiki mbili cha mashindano hayo.