MWANARIADHA nyota wa mbio fupi ambaye ni bingwa mara sita wa michuano ya olimpiki, Usain Bolt kutoka Jamaica amefanikiwa kuweka rekodi ya muda bora msimu huu katika mbio za mita 100 za kuadhimisha mwaka mmoja toka kufanyika michuano olimpiki jijini London. Katika michuano ya olimpiki mwaka jana Bolt alifanikiwa kutetea medali zake za dhahabu katika mbuio za mita 100 na mita 200 huku pia akiweka rekodi katika mbio za mita 400 kupokezana vijiti. Mwanariadha nyota chipukizi wa Uingereza James Dasaolu ambaye alitegemewa kuleta upinzani kwa Bolt alijitoa kabla ya kuanza kwa mbio hizo kutokana na kuumia wakati akipasha misuli moto. Katika mbio za jana Bolt alianza taratibu kama ilivyo kawaida yake lakini aliongeza kasi na kuwapita wapinzani wake mwishoni mwa mbio hizo na kupelekea kushinda mbio hizo kwa kutumia muda wa sekunde 9.85. Nafasi ya pili katika mbio hizo ilishikiliwa na Michael Rodgers wa Marekani aliyetumia muda sekunde 9.98 akifuatiwa na Nesta Carter wa Jamaica aliyetumia sekunde 9.99 wakati Dwain Chambers Muingereza pekee aliyebakia katika mbio hizo baada ya Dasaolu kujitoa alishika nafasi ya tano kwa kutumia muda wa sekunde 10.10.
No comments:
Post a Comment