Saturday, February 28, 2015

RODGERS AWAKINGIA KIFUA WACHEZAJI WAKE.

MENEJA wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers amedai kuwa kikosi chake sio cha kulaumiwa kufuatia kutolewa katika michuano ya Europa League. Liverpool inakabiliwa na mchezo mgumu Jumapili hii dhidi ya Manchester City na Rodgers anataka wachezaji wake kusahau kutolewa huko na kuzingatia mchezo huo. Rodgers amesema anajivunia kikosi chake na jinsi wanavyokabiliana na hali hiyo kwani itawasaidia katika siku zijazo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa jambo muhimu hivi sasa ni kuhakikisha wanakamata nafasi nne za juu ili waweze kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

PARMA YAAHIRISHA MECHI YAO YA SERIE A BAADA YA WACHEZAJI KUTISHIA KUGOMA KWA KUTOLIPWA MISHAHARA YAO.

KLABU ya Parma imelazimika kusogeza mbele mchezo wao wa Seria A dhidi ya Genoa uliokuwa uchezwe Jumapili hii baada ya ya wachezaji kutishia kugoma kutokana na kutolipwa mishahara. Wachezaji wa klabu hiyo ambayo inakabiliwa na matatizo ya kifedha, hawajalipwa toka msimu umeanza huku pia kukiwa na deni la paundi milioni 145. Mwishoni mwa wiki iliyopita mchezo wao dhidi ya Udinese ulilazimika kusitishwa kwasababu maofisa wa klabu kushindwa kulipa fedha walizokuwa wakidaiwa. Shirikisho la Soka la Italia-FIGC limeionya Parma dhidi ya kuahirisha mechi zake katika siku za usoni.

HENRY AKITAMANI KIBARUA CHA WENGER.

MCHEZAJI nyota wa zamani wa klabu ya Arsenal, Thierry Henry amedai kuwa ndoto yake ni kumrithi kocha wa sasa Arsene Wenger. Mapema mwezi huu Henry ambaye ndio anaongoza kwa kufunga mabao mengi katika klabu hiyo alipewa ofa ya kuanza kufundisha soka katika shule ya soka ya timu hiyo. Akihojiwa Henry raia wa Ufaransa amekiri kuwa anatamani siku moja aweze kurithi mikoba ya Wenger kama kocha wa Arsenal. Wakati akiichezea Arsenal Henry amefanikiwa kufunga mabao 228 idadi ambayo hakuna mshambuliaji yeyote wa timu amewahi kuifikia mpaka sasa.

VAN GAAL ADAI UNITED INAHITAJI MSHAMBULIAJI MWENYE UWEZO KUFUNGA MABAO 20 KWA MSIMU.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, Louis van Gaal amesema kikosi chake kinakosa mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao 20 kwa msimu. United kwasasa wanashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa nyuma ya vinara Chelsea kwa alama nne huku wakikabiliwa na upinzani mkali wa kupata nafasi ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Robin van Persie ndiye anaongoza kwa kufunga mabao United akiwa amefunga mabao 10 msimu huu lakini sasa anakabiliwa na kipindi kirefu cha kukaa nje kutokana na majeruhi yanayomsumbua. Radamel Falcao amekuwa akipambana kujaribu kuzoea soka la Uingereza huku Wayne Rooney mara nyingi akiwa anapangwa katika nafasi ya kiungo. Akihojiwa Van Gaal alikiri kuwa anakosa aina ya mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao zaidi ya 20 kwa msimu jambo limekuwa tatizo kwa kikosi chake msimu huu. Van Gaal amesema wachezaji karibu wote katika kikosi chake wamekuwa wakijaribu kuzoea mazingira mapya na mbinu mpya hivyo anadhani wanaweza kufikia malengo yao mpaka mwishoni mwa msimu.

UEFA YAILIMA FAINI HULL KWA KUKIUKA SHERIA YA MATUMIZI YA FEDHA, LIVERPOOL YASEVU.

KLABU ya Hull City imetozwa faini ya paundi 145,000 na Shirikisho la Soka La Ulaya-UEFA kwa kukiuka masharti ya matumizi ya fedha huku Liverpool wao wakitoka safi baada ya ukaguzi. Meneja wa Hull Steve Bruce anadhani kuwa adhabu hiyo wamepata kutokana na gharama walizotumia wakati wakijaribu kupatanda daraja msimu uliopita. Hull watalazimika kulipa faini nyingine ya paundi 290,000 kama wakikiuka masharti hayo msimu ujao. Bruce amesema taarifa hizo ni mbaya kwao kwani sababu kubwa ya wao kuingia katika uchunguzi huo ni kwasababu ya mikakati yao ya kupanda Ligi Kuu.

ANCELOTTI AWAPUUZA BARCELONA NA KUDAI KILA MECHI NI MUHIMU KWAKE.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema mechi tatu za La Liga zinazowakabili ni muhimu kama ulivyo mchezo dhidi ya Barcelona maarufu kama Clasico utakaochezwa Machi 22 mwaka huu. Kwasasa Madrid ndio wanaongoza msimamo wa La Liga wakitofautiana na Barcelona walioko nafasi ya pili kwa alama nne ambao watachuana nao katika Uwanja wa Camp Nou katika mchezo utakaotoa muelekeo wa bingwa wa msimu huu. Hata hivyo kabla ya mchezo huo, Ancelotti amesema wana michezo mingine mitatu dhidi ya Villarreal, Athletic Bilbao ba Levante ambayo inabidi waizingatie kabla ya kuanza kuwafikiria Barcelona. Ancelotti amesema michezo hiyo ni muhimu kwani kama wakipoteza alama wanaweza kuhatarisha matumaini yao ya kunyakuwa taji msimu huu.

HERRERA ATAMBA KUJA KUWA MCHEZAJI MUHIMU WA UNITED SIKU ZA USONI.

KIUNGO wa klabu ya Manchester United, Ander Herrera amekataa kulazimisha kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo chini ya meneja Louis van Gaal. Baada ya kununuliwa kwa fedha nyingi kutoka Athletic Bilbao katika kipindi cha majira ya kiangazi msimu uliopita, nyota huyo wa kimataifa wa Hispania amekuwa akianza kama mchezaji wa akiba mara nyingi zaidi kuliko katika kikosi cha kwanza. Pamoja na hayo Herrera amekubaliana hali hiyo kwani anajua itachukua muda mpaka aweze kushawishi na kupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza mara kwa mara. Akihojiwa Herrera amesema anapenda kucheza mara nyingi kadri iwezekanavyo akiwa United lakini hawezi kulazimisha kwakuwa anajua itachukua muda kumshawishi kocha. Herrera amesema anataka kushinda mataji na United na pia anataka kuwa mchezaji muhimu wa timu hiyo hivyo anadhani katika kipindi sio kirefu anaweza kufikia malengo hayo.

Thursday, February 26, 2015

STERLING KARIBUNI KUSAINI MKATABA MPYA LIVERPOOL.

MSHAMBULIAJI mahiri wa Liverpool, Raheem Sterling ana matumaini ya kusaini mkataba mpya na timu hiyo hivi karibuni na kudai kuwa Anfield ni mahali pazuri kwa wachezaji chipukizi ili waweze kukua katika Ligi Kuu. Mkataba wa sasa wa Sterling unamalizika mwaka 2017 na mazungumzo na mkataba mpya bado hayajafikia muafaka. Hivi karibuni meneja wa Liverpool, Brendan Rogders alidai kuwa klabu hiyo imepanga kumpa Sterling mwenye umri wa miaka dili nono. Sterling amesema anazungumza na wawakilishi wake kila siku na wamemuhakikishia kuwa yeye atilie mkazo soka na kuwaachia wao mambo mengine kwani watayamaliza hivi karibuni. Nyota huyo amesema kwasasa anatilia mkazo kuisaidia Liverpool kushinda mechi zake na ni matumaini yake mazungumzo ya mkataba wake mpya yatamalizika haraka.

LIPPI AACHANA NA GUANGZHOU EVERGRANDE.

KLABU ya Guangzhou Evergrande ya China imethibitisha kuwa kocha mkongwe Marcello Lippi ameachana na klabu hiyo. Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia na klabu ya Juventus alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo inayoshirikis Ligi Kuu ya China Mei mwaka 2012 kwa mkataba wa miaka miwili na nusu wenye thamani ya euro milioni 30. Lippi ameingoza klabu hiyo kushinda mataji manne ya ligi na taji moja la Kombe la FA la nchi hiyo lakini mafanikio yake makubwa yalikuja wakati alipoiwezesha timu hiyo kushinda taji la Ligi ya Mabingwa barani Asia maka jana. Kocha huyo sasa ndiye pekee aliyewahi kunyakuwa mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Asia. Lippi raia wa Italia alikuwa amesaini mkataba ambao ungemalizika mwaka 2017 Februari mwaka jana lakini alitangaza kustaafu ukocha Novemba na kupewa nafasi kama mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo.


TETESI ZA USAJILI ULAYA: MAN UNITED YATENGA PAUNDI MILIONI 30 KWA AJILI YA WINGA WA WOLFSBURG, LIVERPOOL, UNITED WAKABANA KOO KWA DANILO.

KATIKA habari za tetesi za usajili ambazo zimepamba vichwa vya habari vya magazeti na mitandao mbalimbali Ulaya ni pamoja na winga wa klabu ya Wolfsburg Kevin De Bruyne mwenye umri wa miaka 23 kukubali kurejea katika Ligi Kuu nchini Uingereza. Taarifa hizo zinaweza kuwa njema kwa manchester United ambao wako tayari kutoa kitita cha paundi milioni 30 kwa ajili ya kumsajili nyota huyo wa zamani wa Chelsea. Klabu za Liverpool na Manchester United zimeonyesha nia baada ya kugundua kuwa beki Danilo mwenye umri wa miaka 23 amekataa kusaini mkataba mpya na FC Porto. Klabu ya Tottenham Hotspurs inataka kumsajili beki wa Monaco Aymen Abdennour mwenye umri wa miaka 25 huku mchezaji huyo wa kimataifa wa Tunisia alionyesha nia ya kukubali uhamisho huo. Kiungo wa Manchester United Andreas Pereira mwenye umri wa miaka 19, anaweza kuhamia Juventus baada ya nyota huyo wa kimataifa wa Brazil kukataa kusaini mkataba mpya. Winga wa klabu ya Tottenham hotspurs Aaron Lennon mwenye umri wa miaka 27 amepania kusaini mkataba wao wa kudumu na Everton anapochezea kwa mkopo huku klabu hiyo ikiwa tayari kutoa kitita cha paundi milioni saba.

SIMEONE ATAMBA KUWA ATLETICO INAWEZA KUBADILI MATOKEO NA KUSONGA MBELE.

MENEJA wa klabu ya Atletico Madrid, Diego Simeone amesisitiza kikosi chake kinaweza kubadili matokeo katika mchezo wao wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuchapwa bao 1-0 jana na Bayer Leverkusen. Leverkusen wamepiga hatua moja kutinga katika hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza toka walipofika fainali ya michuano hiyo mwaka 2002. Akihojiwa Simeone amesema Leverkusen wangekuwa wajiweka vizuri zaidi kama wangewafunga bao zaidi ya moja lakini kutokana na mchezo ulivyokuwa jana ana uhakika wanaweza kubadili matokeo hayo na kusonga mbele. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kikosi chake hakikuwa kikicheza kwa uelewano wa kutosha jambo ambalo ana uhakika litakuwa limejirekebisha mpaka utakapofikia mchezo wao marudiano nchini Hispania wiki mbili zijazo.

KOCHA WA COLOGNE AKIRI ITAKUWA MIUJIZA KUIFUNGA BAYERN.

MENEJA wa klabu ya Cologne, Peter Stoeger amekiri kuwa watahitaji miujiza watakapocheza na mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich kesho kutokana na ubora waliokuwa nao hivi sasa. Bayern hawajafungwa bao lolote katika michezo yao mitatu iliyopita ambapo waliigaragaza Hamburg kwa mabao 8-0 huku Jumamosi iliyopita Paderborn nao wakichabangwa mabao 6-0 na kuifanya timu hiyo kukaa klileleni kwa tofautia ya alama sita. Wakati Wolfsburg wanashika nafasi ya pili wao wakicheza na Werder Bremen Jumapili hii, timu zote hizo zimecheza hazijafungwa katika mechi zao tano za mwanzo kwa mwaka huu. Bayern atakuwa na nafasi ya kutanua pengo la alama, labda Cologne wafanye miujiza ya kuisimamisha timu hiyo. Kocha huyo amesema Bayern wao hutumia kila nafasi wanayopata na kama wakifanikiwa kufanya hivyo katika mchezo wao anadhani itakuwa ngumu kusalimika.

NOBLE APEWA MKATABA MPYA WEST HAM.

KIUNGO wa klabu ya West Ham United, Mark Noble amesaini mkataba mpya utakaomuweka katika timu hiyo mpaka mwaka 2020 huku kukiwa na uwezekano wa kuongezwa mwaka mmoja zaidi. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27, ameshawahi kushinda tuzo ya mchezo bora wa mwaka wa timu hiyo mara mbili. Noble alijiunga na West Ham akiwa na umri wa miaka 13 mwaka 2000 na aliibuka katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo mwaka mmoja baadae. Toka wakati huo ameshacheza mecho zaidi ya 300 mpaka sasa.

MICUANO YA MATAIFA YA AFRIKA KUSOGEZWA MBELE KUPISHA KOMBE LA DUNIA NCHINI QATAR.

KATIBU mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amesema michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2023 itasogezwa mbele kutoka Januari mpaka Juni ili kusaidia kusogezwa kwa michuano ya Kombe la Dunia 2022. Kikosi kazi cha FIFA kimependekeza Kombe la Dunia kuchezwa Novemba na Desemba ili kuepuka joto kali katika majira ya kiangazi nchini Qatar. Valcke amesema Shirikisho la Soka la Afrika-CAF limekubali kuwa halitafanya michuano hiyo ya Afcon Januari na badala yake watasogeza mbele mpaka Juni. Michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 imepangwa kumalizika Desemba na michuano ya Mataifa ya Afrika yenyewe kwa kawaida ilitakiwa kuanza kuchezwa katikati ya mwezi Januari mwaka 2023.

LIGI YA MISRI KUANZA TENA BILA MASHABIKI.

MECHI za soka nchini Misri zinatarajiwa kuanza tena lakini watalazimika kucheza bila mashabiki kuwepo viwanjani. Chama cha Soka cha Misri-EFA kimetangaza kuwa mechi za ligi zinatarajiwa kuanza tena mwezi ujao baada ya kusimamishwa wiki zilizopita kutokana na vurugu zilizotokea katika Uwanja wa Kijeshi uliopo jijini Cairo. EFA katika taarifa yake imedai kuwa baada ya jopo kati yao, wizara ya mambo ya ndani na wizara ya michezo kukutana wamefikia maamuzi kuwa ligi hiyo iendelee baada ya kupita siku 40 za maombolezo. Ligi Kuu ya Misri pamoja na mashindano mengine ya soka yalisimamishwa toka Februari 8 mwaka huu wakati mashabiki 20 wa Zamalek walipouawa baada ya polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya mashabiki waliotaka kuingia uwanjani kwa nguvu. Mechi nyingi za ligi zimekuwa zikichezwa bila mashabiki toka mashabiki zaidi ya 70 wauawe Februari mwaka 2012 baada ya kushambuliwa na mashabiki wa Al Masry katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Port Said.

WENGER ALIA NA SAFU YAKE YA ULINZI BAADA YA KIPIGO.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger ameiponda safu yake ya ulinzi baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-1 nyumbani na Monaco jana. Mabao yaliyofungwa na Geoffrey Kondogbia, Dimitar Barbatov na Yannick Ferreira-Carrasco yalitosha kuipa ushindi Monaco hivyo kuwaweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mara baada ya mchezo huo Wenger amekiri kikosi chake hakikujilinda vyema huku akiwapongeza wapinzani wao kwa kujipanga vyema. Wenger amesema ulikuwa usiku mbaya kwao lakini anawapongeza Monaco kwa kupambana, kujilinda vizuri na kutumia vyema mipira ya kushtukiza waliyopata.

Wednesday, February 25, 2015

CELTIC WALIMWA ADHABU NA UEFA WAKIWA NJIANI KUIFUATA INTER.

KLABU ya Celtic imetozwa faini ya paundi 7,300 na Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA kufuatia vurugu za mashabiki wake katika mchezo wa makundi ya Europa League dhidi ya Dinamo Zagreb. Hiyo inakuwa mara ya tano katika kipindi cha miaka mitatu Celtic kutozwa faini na UEFA kutokana na vurugu za mashabiki wao. Mashabiki hao walikwaana na polisi baada ya kurusha mafataki katika mchezo ambao Celtic walichapwa mabao 4-3 Desemba mwaka jana ingawa pamoja na kipigo hicho walifanikiwa kufuzu hatua ya timu 32 bora. Adhabu hiyo ya faini iliyotolewa na kamati ya maadili na nidhamu ya UEFA imekuja wakati Celtic na mashabiki wake wakisafiri kuelekea nchini Italia kwa ajili ya mchezo wao wa mkondo wa pili wa michuano hiyo dhidi ya Inter Milan. Katika mchezo wa mkondo wa kwanza Celtic walitoka sare ya kufungana mabao 3-3 na Inter katika mchezo uliofanyika jijinio Glasgow.


CHAMPIONS LEAGUE: BIG MATCH ARSENAL VS MONACO.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya timu 16 bora mechi za mkondo wa kwanza inaendelea tena leo ambapo katika michezo ya leo Arsenal watakuwa nyumbani kuwakaribisha Monaco huku Atletico Madrid wao wakiwa wenyeji wa Bayer Leverkusen. Arsenal watakuwa wakikwaana na Monaco kwa mara ya kwanza katika hatua hiyo lakini kwa meneja Arsene Wenger, Monaco hawatakuwa wageni kwake. Wenger amewahi kuinoa Monaco kwa miaka saba kuanzia mwaka 1987 mpaka 1994 kabla ya kuondoka na kwenda kuifundisha klabu ya Nagoya Grampus ya Japan. Huu utakuwa mchezo wa kwanza rasmi kwa Wenger dhidi ya timu yake hiyo ya zamani ambao wametinga hatua hiyo ya mtoano kwa mara ya kwanza baada ya kupita muongo mmoja. Monaco walitinga hatua hiyo wakiwa washindi wa kundi C, ingawa alama zao 11 walizopata hazikufikia zile za Arsenal ambao walimaliza katika nafasi ya pili katika kundi D nyuma ya Borrusia Dortmund. Pamoja na kutokutana katika mechi za mashindano lakini Monaco imewahi kucheza na Arsenal katika mchezo wa kirafiki Agosti 3 mwaka jana wakati wa maandalizi ya msimu mpya ambapo Monaco walishinda kwa bao 1-0 lilifungwa na Radamel Falcao kabla hajatimkia Manchester United.

FIFA YADAI HAKUNA KLABU ITAKAYOLIPWA KWA KOMBE LA DUNIA KUHAMISHWA.

SHIRIKISHO la Soka la Dunia-FIFA limetunisha misuli yake tena leo wakati walipotangaza kuwa hawatarajii kufidia klabu yeyote kwa kuwakosa wachezaji wao na kuleta mkanganyiko katika ligi kutokana na michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar kuandaliwa majira ya baridi. Siku moja baada ya kikosi kazi cha FIFA kutoa mapendekezo ya michuano hiyo kufanyika Novemba na Desemba, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Jerome Valcke amewaambia wana habari kuwa hakuta kuwa na malipo yeyote ya kifedha kwa usumbufu utakaojitokeza katika ligi. Valcke amesema hawatalipa fidia kwasababu ligi zote zina miaka saba mpaka kufikia muda wa mashindano kupanga mikakati yao kuhakikisha michuanpo hiyo haileti mvurugano katika ligi zao. Tarehe halisi ya kuchezwa michuano hiyo inatarajiwa kupangwa na FIFA katika kikao chake cha kamati ya utendaji mwezi ujao huku kukiwa na uwezekano wa timu kupungua kutoka 32 hadi 28 kutokana na muda watakaokuwa nao.

PELLEGRINI ADAI ALITUMIA MBINU SAHIHI KATIKA MCHEZO DHIDI YA BARCELONA.

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Manuel Pellegrini amesisitiza hajutii mbinu alizotumia katika mchezo wao dhidi ya Barcelona ambao wamechapwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Etihad jana. Katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, City walitumia mfumo wa 4-4-2 lakini walijikuta wakishindwa kuhimili vishindo vya Barcelona baada ya Luis Suarez kufunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza. Mabingwa hao wa Ligi Kuu sasa wanakabiliwa kibarua kizito katika mchezo wao wa marudiano ambao utachezwa baada ya wiki mbili katika Uwanja wa Camp Nou. Akihojiwa Pellegrini amesema amefurahi kwani ndio jinsi walivyotakiwa kucheza dhidi ya timu kama Barcelona. Kocha huyo aliongeza kuwa walicheza kwa mifumo miwili tofauti katika kipindi cha kwanza na cha pili kwani kwani kabla ya kufungwa bao la kwanza ulikuwa ni mchezo wa kawaida lakini baada ya kufungwa hali ikabadilika na wakaanza kuchezwa hovyo. Hata hivyo, Pellegrini anashukuru kwani katika kipindi cha pili wachezaji wake walibadilika na kuja kupata bao moja ambalo litakuwa muhimu kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano.

CHELSEA WALALAMA PAMOJA NA MATIC KUPUNGUZIWA ADHABU.

KIUNGO wa klabu ya Chelsea Nemanja Matic amepunguziwa adhabu yake kutoka mechi tatu mpaka mbili lakini bado anatarajiwa kukosa mchezo fainali ya Kombe la Ligi Jumapili hii. Chama cha Soka cha Uingereza-FA kiliamua kupunguza adhabu hiyo baada ya kuridhishwa na utetezi uliotolewa na Chelsea. Matic mwenye umri wa miaka 26 alitolewa nje Jumamosi iliyopita wakati Chelsea walipotoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Burnley baada ya kumchezea vibaya Ashley Barnes. Katika taarifa yake, klabu hiyo imedai kushtushwa na kusikitishwa kuwa Matic bado atatakiwa kutumikia adhabu. Matic sasa atakosa mchezo wa fainali wa Kombe la Ligi dhidi ya Tottenham Hotspurs ambao utafanyika katika Uwanja wa Wembley na mchezo mwingine dhidi ya West Ham United Machi 4 mwaka huu.

WAKILI WA PISTORIUS NAYE AFUNGUA MASHITAKA KUIWAPINGA WAENDESHA MASHITAKA.

WAKILI wa mwanariadha mlemavu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius anayetumikia kifungo, wamefungua mashitaka kupinga waendesha mashitaka kukata rufani dhidi ya huku iliyotolewa kutokana na kosa lake la mauaji. Jaji Thokozile Masipa Desemba mwaka jana aliruhusu waendesha mashitaka kukata rufani kutokana na hukumu aliyotoa kama watahitaji kufanya hivyo. Masipa alimhukumu Pistorius kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kuua bila kukusudia baada ya kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp Februari mwaka 2013. Pistorius alijitetea kuwa alimuua mpenzi wake huyo kimakosa akidhani kuwa ni jambazi, wakati waendesha mashitaka walikuwa wakidai kuwa alimuua kwa makusudi baada ya kutofautiana nyumbani kwake jijini Pretoria.

Tuesday, February 24, 2015

NEVILLE ADAI KOMBE LA DUNIA LA NOVEMBA NA DESEMBA LITAKUWA NA FAIDA KWA UINGEREZA.

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Uingereza, Phil Neville amesema kuandaliwa kwa michuano ya Kombe la Dunia kati ya Novemba na Desemba mwaka 2022 nchini Qatar ni jambo zuri kuwahi kutokea kwa nchi yake. Kikosi kazi cha Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA kilipendekeza michuano hiyo kuhamishwa wakati wa majira ya baridi kwasababu ya joto kali nchini Qatar. Wakati wadau wengi wakikosoa uamuzi huo, Neville yeye anafikiri michuano hiyo itakuwa na faida kubwa kwa matumaini ya Uingereza kunyakuwa taji hilo. Neville anaamini katika kipindi hicho wachezaji wanakuwa bado wako vyema na tayari kwa ajili ya kupambana na timu bora duniani. Mapendekezo hayo ambayo yanatarajiwa kufikishwa mbee ya kamati ya utendaji ya FIFA itakayokutana jijini Zurich, Machi mwaka huu, tayari inaungwa mkono na rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, Michel Platini, Shirikisho la Soka la Afrika-CAF, Concacaf na Shirikisho la Soka la Asia.

ENRIQUE AMKINGIA KIFUA MESSI PAMOJA NA KUKOSA PENATI.

MENEJA wa klabu ya Barcelona, Luis Enrique amesisitiza kuwa Lionel Messi ataendelea kuwa mpiga penati wa timu hiyo pamoja na kukosa penati yake ya tatu msimu huu katika mchezo dhidi ya Manchester City jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina alikuwa na nafasi ya kuipa ushindi Barcelona wa mabao 3-1 katika dakika za majeruhi lakini Joe Hart alifanikiwa kuokoa mchomo wake. Messi pia amekosa penati katika mchezo dhidi ya Levante Septemba mwaka jana na Brazil wakati akiitumikia timu yake ya taifa Octoba lakini Enrique anaamini kuwa nyota huyo bado ni mpigaji mzuri na anamuamini. Kocha huyo amesema wale wote wanaokosa penati ni wale wenye uthubutu wa kufanya hivyo na Messi bado ataendelea kuwa mpigani wao. Katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Etihad, Barcelona ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1.

Monday, February 23, 2015

KOMPANY ATAMBA KUWA HAWAIOGOPI CITY.

NAHODHA wa klabu ya Manchester City, Vincent Kompany amesema kikosi chao hakiwaogopi Barcelona ambao wanakutana nao katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya mtoano. Barcelona iliwang’oa City kwa kuwachapa kwa jumla ya mabao 4-1 katika hatua kama hiyo msimu uliopita. Mchezo wa mkondo wa kwanza baina ya timu hizo utafanyika katika Uwanja wa Etihad kesho kabla ya kurudiana tena Machi 18 katika Uwanja wa Camp Nou. Akihojiwa Kompany amesema hawana hofu yeyote na Barcelona na wana uhakika wanaweza kuwang’oa kutokana na kiwango bora walichonacho.

AOMBA RADHI KUFUATIA SAKATA LA TUHUMA ZA UBAGUZI LA MASHABIKI WA CHELSEA.

OFISA wa zamani wa polisi na mshabiki wa Chelsea ameomba radhi kwa kuhusika na tuhuma za tukio la ubaguzi katika kituo cha treni jijini Paris lakini amedai yeye sio mbaguzi. Richard Barklie mwenye umri wa miaka 50 alitambuliwa kama mmoja wa watu ambao wanafanyiwa uchunguzi na polisi. Katika taarifa yake, Barklie alikanusha kuimba nyimbo za kibaguzi na kudai kuwa alikuwa akitaka kufafanua kwa polisi jinsi tukio hilo lililovyokuwa. Chelsea imeshawasimamisha mashabiki watano baada ya picha za video kuonyesha mtu mwenye asili ya kiafrika akizuiwa kuingia katika treni.

RANALDO APAA MPAKA NAFASI YA TATU KATIKA ORODHA YA WAFUNGAJI BORA MADRID, ABAKISHA MABAO 33 AFIKIE REKODI YA RAUL.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo amepaa mpaka nafasi ya ya tatu katika orodha ya wafungaji bora wa klabu hiyo baada ya kufunga bao katika mchezo dhidi ya Elche uliochezwa jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno alifunga bao lake la 290 toka aanze kuitumikia Madrid na kupanda juu ya nguli wa zamani wa klabu hiyo Carlos Santillana na sasa amebakisha mabao 33 kumfikia nyota wa zamani Raul mwenye mabao 323. Katika mchezo huo Karim Benzema aliifungia Madrid bao la kuongoza kabla ya Ronaldo hajafunga bao la pili katika kipindi cha pili na kuifanya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0. Madrid bado wanaendelea kushikilia usukani wa La Liga kwa tofauti ya alama nne dhidi ya mahasimu wao Barcelona.

ANCELOTTI AKIRI KUSHANGAZWA NA KICHAPO CHA BARCELONA.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti amekiri kuwa alishtushwa na kipigo cha bao 1-0 walichopata Barcelona dhidi ya Malaga lakini bado anategemea mbio za ubingwa wa La Liga kuendelea mpaka siku ya mwisho. Barcelona walikuwa wakitawala kwa kushinda mechi 11 mfululizo katika mashindano yote kabla ya rekodi hiyo kutibuliwa na Malaga katika Uwanja wa Camp Nou Jumapili iliyopita. Akihojiwa mara baada ya Madrid kuichapa Elche mabao 2-0, Ancelotti amesema mchezo huo ulikuwa muhimu hususani baada ya mahasimu wao Barcelona kuteleza. Ancelotti aliendelea kudai kuwa ni wazi kipigo hicho kiliwashangaza watu wote kutokana na kiwango bora walichonacho sasa.

CHELSEA KUKATIA RUFANI KADI NYEKUNDU YA MATIC.

KLABU ya Chelsea inajipanga kukata rufani dhidi ya kadi nyekundu aliyopewa Nemanja Matic wakati wa mchezo wao dhidi ya Burnley ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 Jumamosi uliyopita. Kiungo huyo wa kimataifa wa Serbia mwenye umri wa miaka 26 alitolewa kwa kumsukuma Ashley Barnes mpaka kuanguka baada ya kugongana wakigombea mpira. Chelsea ambao ndio vinara wa Ligi Kuu wamepewa mpaka kesho wawe wamewasilisha ushahidi wao Chama cha Soka cha Uingereza-FA. Kama rufani yao ikikataliwa Matic anatarajiwa kukosa mchezo wa fainali ya Kombe la Ligi utakaofanyika Jumapili hii dhidi ya Tottenham Hotspurs.

Friday, February 20, 2015

TETESI ZA USAJILI UALAYA: VAN GAAL KUTUMIA EURO MILIONI 200 KATIKA USAJILI KIANGAZI, CHELSEA KUMPA MOURINHO MIAKA MINGINE MINNE.

KATIKA habari za tetesi za usajili zilizopamba vichwa habari katika mitandao mbalimbali barani Ulaya ni pamoja na meneja wa Manchester United Louis van Gaal ametaja majina ya wachezaji anaoweza kuwasajili katika majira kiangazi huku akiwa tayari kutumia kitita cha euro milioni 200. Van Gaal amewataja wachezaji anaowawinda ambao ni Nathaniel Clyne, Mats Hummels, Kevin Strootman, Memphis Depay na Paulo Dybala. Meneja wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho anatarajiwa kusaini mkataba mpya na timu hiyo katika majira ya kiangazi. Kocha huyo raia wa Ureno kwasasa anafurahia kuwepo Stamford Bridge na anataka kuendelea kubakia hapo huku klabu hiyo ikitegemea kumsainisha mkataba wa miaka minne. Klabu ya Arsenal imepata upinzani katika mbio zao za kutaka kumsajili Lars Benders baada ya Barcelona kuonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo huyo wa Bayer Leverkusen. Barcelona wameamua kumuweka Bender katika mipango yao ya usajili huku Arsenal wakihamishia nguvu zao kwa Morgan Schneiderlin. Manchester United wamejitoa katika mbio za kutaka kumsajili Paulo Pogba katika majira ya kiangazi. Meneja wa United Louis van Gaal anamhusudu kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa lakini klabu haiku tayari kumnunua tena mchezaji huyo ambaye walimruhusu kuondoka kama mchezaji huru kwenda Juventus. Chelsea wameipiga bao Arsenal katika kinyang’anyiro cha kutaka kumsajili nyota wa Palermo Paulo Dybala. Arsenal walifanya mazungumzo na klabu hiyo ya Italia lakini Jose Mourinho sasa ndio anaongoza mbio hizo kwa kuwa tayari kutoa kitita cha euro milioni 40 kwa ajili ya mshambuliaji huyo ili aweze kuziba nafasi ya Drogba.

BONY ATAMBA KUISAIDIA CITY KUTETEA TAJI LA LIGI KUU.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ivory Coast, Wilfried Bony anaamini anaweza kuwa silaha ya siri kwa Manchester City katika mbio zao za ubingwa wa Ligi Kuu wakati akijiandaa kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Newcastle United Jumamosi hii. Bony alijiunga na City inayonolewa na Manuel Pellegrini akitokea Swansea City kwa kitita cha paundi milioni 28 Januari mwaka huu lakini bado hajacheza mechi yeyote kutokana na majukumu ya kimataifa aliyokuwa nayo katika michuano ya Mataifa ya Afrika. Sasa nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 atapata nafasi kwa mara ya kwanza kuwaonyesha mashabiki wa City na kuwapa matumaini mapya ya kutetea taji lao. Bony ambaye alifunga mabao 34 katika mechi 70 alizoichezea Swansea ana uhakika kuwa anaweza kuisaidia timu hiyo kufikia malengo yake. City wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi wakiwa nyuma ya vinara ya Chelsea.

MARTINEZ AMMWAGIA SIFA LUKAKU BAADA YA KUPIGA HAT-TRICK.

MENEJA wa klabu ya Everton Roberto Martinez amesema mshambuliaji Romelu Lukaku ameonyesha kujitoa kutokana na kiwango chake katika mchezo wa jana ambao walishinda mabao 4-1 dhidi ya Young Boys. Katika mchezo huo Lukaku alifunga hat-trick yake ya kwanza akiwa na klabu hiyo na kuipa uahindi muhimu katka mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa michuano ya Europa League. Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21 aliwakera mashabiki wa timu hiyo mapema mwezi huu kwa kukaririwa na gezeti moja akiwa kuwa na matumaini ya kuondoka kwenda katika klabu kubwa. Hata hivyo, Martinez alimtetea Lukaku na kudai kuwa anapenda kuitumikia Everton na hilo ameonyesha jana kwa kiwango bora alichoonyesha.

IBRAHIMOVIC ALIMWA ADHABU MECHI MBILI.

LIGI Kuu nchini Ufaransa-LFP imetangaza jana kumfungia mechi mbili mshambuliaji nyota wa Paris Saint-Germain-PSG, Zlatan Ibrahimovic. Nyota huyo wa kimataifa wa Sweden alilimwa adhabu hiyo katika kikao cha kamati ya nidhamu ya ligi kilichokutana kufuatia tukio lake na Romain Hamouma katika ushindi wa bao 1-0 waliopata PSG dhidi ya Saint-Etienne mwezi uliopita. Ibrahimovic sasa atakosa mchezo dhidi ya Monaco utakaochezwa Jumapili hii na mchezo mwingine war obo fainali ya Kombe la Ligi utakaochezwa Jumatano ijayo na timu hiyohiyo. Nyota huyo ameshafunga mabao 17 katika mshindano yote msimu huu akiwa sambamba na Edinsoni Cavani.

MASHABIKI 23 WA FEYENOORD WAKAMATWA JIJINI ROME.

MASHABIKI 23 wa klabu ya Feyenoord wamekamatwa jijini Rome na 19 kati yao wakishitakiwa baada ya kufanyika vurugu kabla ya mchezo wa michuano ya Europa League dhidi ya AS Roma jana na kusababisha hasara katika mji huo. Mashabiki waliokuwa wamelewa waliharibu baadhi ya majengo na kuwarushia chupa polisi Jumatano usiku kabla ya mamia wengine kugombana na polisi jana kabla ya kuanza kwa mchezo huo. Polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi na kuwatawanya mashabiki hao ambao waliacha eneo hilo likiwa limejaa chupa tupu za bia. Kwa mujibu wa maofisa wa polisi wa Rome mashabiki wengi wameshitakiwa kwa kosa la kukataa kukamatwa na kuongeza kuwa wanaweza kukabiliwa kifungo cha miezi sita au faini ya euro 45,000. Mashabiki wapatao 6,500 walisafiri kwenda jiji Rome kwa ajili ya kushuhudia mchezo huo wa mkondo wa kwanza ambao Feyenoord walifanikiwa kupata sare ya bao 1-1.

FIGO ATAKA MDAHALO NA BLATTER.

MGOMBEA urais wa Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA, Luis Figo ana matumaini ya kumpa shinikizo rais wa sasa Sepp Blatter kwa kutaka kufanyika mdahalo wa wazi kabla ya uchaguzi miongoni mwa wagombea wote wanne. Prince Ali bin Al Hussein alitoa wazo hilo wakati akifungua kampeni zake kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo mapema mwezi huu na wakati Figo akiulizwa kama amejiandaa na hilo akadai hana shaka. Figo amesema anaamini katika mawazo yake kwani kama yakifanyiwa kazi hakuna shaka kwamba yatabadilisha mfumo mzima wa shirikisho hilo kwa ajili ya faida ya siku zijazo. Winga huyo wa zamani wa kimataifa wa Ureno na klabu za Barcelona na Real Madrid mwenye umri wa miaka 42 anatarajiwa kuchuana na Blatter, Prince Ali rais wa Shirikisho la Soka la Asia na Jordan na rais wa Shirikisho la Soka la Uholanzi Michael van Praag katika kinyang’anyiro hicho kitakachofanyika Mei 29 mwaka huu jijini Zurich.

MODRIC AANZA KUFANYA MAZOEZI.

KIUNGO wa Real Madrid Luka Modric ameanza kufanya mazoezi na wenzake kwa mara ya kwanza jana baada ya kupita kipindi cha miezi mitatu ikiwa ni ishara za kukaribia kurejea uwanjani baada ya kupona majeruhi yaliyokuwa yakimsumbua. Klabu hiyo ilithibitisha nyota huyo wa kimataifa wa Croatia kufanya mazoezi sambamba na wachezaji ambao hawakuanza katika mchezo wa Ligi ya mabingwa Ulaya ambao Madrid ilishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Schalke Jumatano. Modric alipata majeruhi wakati akiitumikia timu yake ya taifa katika mechi ya kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016 dhidi ya Italia Novemba mwaka jana. Nyota huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs amekosa mechi 21 zilizopita za Madrid ikiwamo michuano ya Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia iliyofanyika Desemba mwaka jana.

TUNISIA YAKATA RUFANI CAS.

TUNISIA nayo imekata rufani Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS jana kufuatia utata uliojitokeza katika michuano ya Mataifa ya Afrika yaliyomalizika mapema mwezi huu. Tunisia ambao walichapwa kwa mabao 2-1 na wenyeji Guinea ya Ikweta katika hatua ya robo fainali, wamekata rufani kupinga amri ya kuwataka kuomba radhi kwa kulituhumu Shirikisho la Soka la Afrika-CAF kwa upendeleo. Tunisia iliamriwa na CAF kuwa watatolewa katika mashindani ya kufuzu michuano hiyo katika michuano ijayo ya Afcon mwaka 2017 kama hawatatimiza amri hiyo mpaka mwishoni mwezi ujao. Tunisia walikuja juu baada ya wenyeji Guinea ya ikweta kuzawadiwa penati katika dakika za majeruhi ambayo iliwafanya kusawazisha bao kabla ya kushinda kwa mabao 2-1 katika muda wa nyongeza. Picha za video ziliwaonyesha wachezaji wa Tunisia wakimkimbiza mwmauzi na kujaribu kumpiga mwishoni mwa mchezo huo.

CHELSEA YASIMAMISHA WATATU KUHUSIANA UBAGUZI PARIS.

KLABU ya Chelsea imewasimamisha watu watatu kuhudhuria katika Uwanja wake wa Stamford Bridge baada ya kutolewa kwa picha za video zikiwaonyesha mashabiki wa timu hiyo wakimzuia mtu mwenye asili ya Afrika kuingia katika treni jijini Paris. Klabu hiyo imedai kuwa adhabu ya kufungiwa maisha inaweza kuwakabili mashabiki hao kama wakikutwa na hatia ya kujihusisha na kitendo. Picha za video zilionyesha mtu huyo akisukumwa kutoka katika treni wakati kundi la mashabiki likiimba nyimbo za kibaguzi. Polisi wanalifanyia uchunguzi tukio hilo lililotokea kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Chelsea na Paris saint-Germain ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 Jumanne iliyopita.

GERRARD AMPASHA BALOTELLI KWA KUKOSA HESHIMA.

KIUNGO wa Liverpool, Steven Gerrard amemtuhumu Mario Balotelli kwa kukosa heshima kutokana na kuchukua jukumu la kupiga penati badala ya Jordan Henderson katika mchezo dhidi ya Besiktas. Balotelli alifunga penati hiyo kwenye mchezo wa michuano ya Europa League hatua ya 32 bora na kuifanya Liverpool kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0. Hatua ya Balotelli imekuja kufuatia nahodha wa mchezo huo Henderson na Daniel Sturridge kutokubaliana juu ya nani haswa anayestahili kupiga mkwaju huo wa penati. Akihojiwa Gerrard amesema Henderson ndiye aliyekuwa nahodha na Balotelli alionyesha utovu wa nidhamu kidogo. Katika mchezo huo Gerrard alikuwa nje kutokana na na kusumbuliwa na majeruhi.

Thursday, February 19, 2015

ALIYEBAGULIWA NA MASHABIKI WA CHELSEA JIJINI PARIS ATAKA KUCHUKULIWA HATUA.

MTU aliyekuwa akizuiwa kuingia katika treni jijini Paris na mashabiki wa soka wa Chelsea waliokuwa wakiimba nyimbo za kibaguzi, ametaka wote waliohusika kuchukuliwa hatua. Mtu huyo aliyejulikana kwa jina la Souleymane S, mwenye umri wa miaka 33 alikaririwa na gazeti moja nchini Ufaransa akidai watu hao ambao ni mashabiki wa Uingereza wanapaswa kuwekwa lupango. Katika picha za video ziliomuonyesha Souleymane akiingia katika treni lakini alisukumwa na mashabiki hao waliokuwa wakiimba nyimbo kuwa wao ni wabaguzi. Kitendo hicho kimekemewa vikali na watu mbalimbali ikiwemo klabu ya Chelsea ambayo msemaji wake ametaka hatua stahiki kuchukuliwa kwa wale wote waliohusika.

TERRY ADAI BADO KUFANYA MAZUNGUMZO YA MKATABA NA CHELSEA.

NAHODHA wa Chelsea, John Terry amekiri kuwa bado hajafanya mazungumzo yeyote na klabu hiyo kuhusu mkataba mpya lakini ana uhakika kuwa anaweza kuendelea kuitumikia katika msimu ujao wa Ligi Kuu. Terry mwenye umri wa miaka 34 amekuwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya kikosi cha Jose Mourinho msimu huu akiwa amecheza pia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain waliotoka sare ya bao 1-1 Juzi. Mkataba wa sasa wa Terry unamalizika mwishoni mwa mwezi Juni na kutokana na kuachiwa kuondoka kwa wakongwe wengine akiwemo Frank Lampard na Ashley Cole msimu uliopita kuna uwezekano pia Terry nao akaondoka. Akihojiwa Terry amesema klabu hiyo inajua nafasi yake pamoja na kutozungumza chochote kwani anajua kuna wachezaji wengine muhimu ambao wanatakiwa kubaki kuliko yeye.

SENEGAL YATAFUTA KOCHA MPYA.

SHIRIKISHO la Soka la Senegal, kimetoa orodha ya majina ya makocha 11 ambao wanawania nafasi ya kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo inayojulikana kama Simba wa Teranga. Aliyekuwa kocha wa timu hiyo Alain Giresse raia wa Ufaransa alijiuzulu nafasi hiyo Januari 29 mwaka huu baada ya kutolewa katika hatua ya makundi ya michuano ya Mataifa ya Afrika yaliyofanyika huko Guinea ya Ikweta. Makocha wa zamani wa Burkina Faso Paulo Duarte na Paul Put pamoja na Michel Dussuyer ambaye aliingoza Guinea katika michuano ya mwaka huu na Patric Neveu wote wametuma maombi yao. Wengine ni Jose Anigo, Frederic Antonetti, Luis Fernandez na Jean-Pierre Parin wote kutoka Ufaransa pamoja na Michel Pont kutoka Switzerland. Makocha wazawa waliotuma maombi yao ni pamoja na Amara Traore ambaye aliwahi kuiongoza Senegal kati ya mwaka 2009 na 2012, Aliou Cisse, Lamine Dieng na Oumar Diop. Shirikisho hilo limesema linategemea maombi zaidi kabla ya muda wa mwisho huku wakitarajia kutangaza jina la kocha mpya Machi mosi mwaka huu.

KOMBE LA DUNIA MWAKA NCHINI QATAR KUFANYIKA NOVEMBA NA DESEMBA MWAKA 2022.

MTANDAO mmoja barani Ulaya umetoa taarifa kuwa tayari muafaka umeshafikiwa kwa michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Qatar mwaka 2022 kufanyika katika kipindi cha Novemba na Desemba ili kuwepa joto kali katika kipindi cha kiangazi. Wakiorodhesha vyanzo mbalimbali mtandao huo umedai kuwa uamuzi umeshafanyika kwani kikosi kazi kilichoteuliwa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kinatarajia kuwasilisha miezi hiyo katika kikao chao kitakachofanyika wiki ijayo jijini Doha kabla ya kamati ya utendaji haijakamilisha mpango huo wakati wa kikao cha mwezi ujao jijini Zurich. Wiki tatu zilizopita, katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke katika mahoajiano yake na radio moja nchini Ufaransa alisema Kombe la Dunia nchini Qatar linatakiwa kuandaliwa wakati wa majira ya baridi lakini kugongana na michuano ya olimpiki ya kwenye baridi Februari mwaka 2022 pia ni hatihati. Hata hivyo mpango huo haujafafanua kwa undani zaidi kuwa michuano ya Kombe la Shirikisho ambayo huchezwa mwaka mmoja kabla ya Kombe la Dunia kama nayo itasogezwa mbele kuepuka majira ya kiangazi. Desemba mwaka jana Chama cha Vilabu barani Ulaya na Muungano wa Ligi za Soka barani humo vilipendekeza michuano hiyo ya Qatar kuchezwa kati ya May na Juni ili kutovuruga ratiba zingine za kawaida za msimu.

HATIMAYE WEST HAM WAMNASA NENE.

KLABU ya West Ham United imefanikiwa kumnasa winga wa kimataifa wa Brazil Nene kwa mkataba wa muda mfupi. West Ham ililazimika kuchukua hatua hiyo haraka ili kuziba nafasi ya Andy Carroll ambaye hatacheza kw amsimu wote uliobakia kutokana na majeruhi ya goti. Nene mwenye umri wa miaka 33 alikuwa akizichezea klabu za Ligi Kuu Ufaransa Monaco na Paris Saint-Germain kabla ya kujiunga na klabu ya Al-Gharafa ya Qatar mwaka 2013. Akihojiwa Nene amesema anajivunia kwenda katika klabu kubwa kama West Ham kwani alikuwa akifikiria kwa miezi kadhaa kurejea katika soka la Ulaya kutokana na ushindani uliopo.

KOCHA WA PORTO ALALAMIKIA MATOKEO WALIYOPATA.

MENEJA wa klabu ya FC Porto Julen Lopetegui amesisitiza kuwa kikosi chake kilikuwa imara zaidi katika mchezo dhidi ya FC Basel kuliko zilivyokuwa Real Madrid na Liverpool mwanzoni mwa msimu, hivyo hadhani kama walistahili sare ya bao 1-1 waliyopata. Wenyeji Basel ndio waliotangulia kufunga bao kupitia kwa Derlis Gonzalez katika dakika ya 11 na kuwafanya Porto kuwa nyuma kwa kipindi kirefu cha mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora kabla ya Danilo kuisawazishia bao kwa penati dakika 79. Akihojiwa na wanahabari mara baada ya mchezo huo kocha huyo amesema hatua ya mtoano katika michuano hiyo huwa inachanganya hivyo walikuwa wako tayari kupambana na magumu yeyote. Lopetegui amesema wapinzani wao Basel walifunga bao kwa shuti moja lililolenga lango lakini wao walipiga mengi lakini wakaambulia goli moja lakini anadhani walistahili matokeo zaidi ya hayo.

VAN GAAL AONYWA KWA KAULI YAKE.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, Louis van Gaal ameonywa kwa siku zijazo kuhusiana na kauli yake aliyotoa baada ya mchezo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana na Cambridge United katika mchezo wa Kombe la FA mwezi uliopita. Mara baada ya mchezo huo Van Gaal aliiambia BBC kuwa kila kitu kilikuwa tofauti na kikosi chake aikiwemo na mwmauzi wa mchezo. Chama cha Soka cha Uingereza-FA kiliamua kuw akauli hiyo ilikuwa sheria lakini kocha huyo aliepuka faini na kupewa onyo. United sasa itachuana na Arsenal katika Uwanja wa Old Trafford kwenye mchezo wa robo fainali ya michuano hiyo ambapo Van Gaal atakuwa akitafuta ushindi ili aweze kunyakuwa taji lake la kwanza katika msimu wa kwanza akiwa kocha.

ANCELOTTI ADAI RONALDO AMEREJESHA MAKALI YAKE.

MENEJA wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema Cristiano Ronaldo amerejea katika makali yake baada ya nyota huyo kumaliza ukame wa mabao katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Schalke jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno amekuwa katika kipindi kigumu kidogo katika wiki za karibuni akiwa amekosa mechi mbili za La Liga akitumikia adhabu huku akiwa hajafunga bao toka Januari 18 mwaka huu. Hata hivyo bao la kichwa alilofunga katika kipindi ca kwanza katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya mtoano uliwaziba mdomo wale wote waliokuwa wakihoji uwezo wake. Sasa Ronaldo anakuwa amekuwa Lionel Messi na Raul kwa kufikisha mabao 76 katika michuano hiyo. Akihojiwa Ancelotti amesema anafurahi kwani Ronaldo amerejea katika kiwango chake kutokana na alivyocheza vyema katika mchezo huo.

UEFA CHAMPIONS LEAGUE: PORTO YANG'ANG'ANIWA NA BASEL, MADRID WAPETA.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliendelea jana kwa mechi mbili zingine kuchezwa ambapo mabingwa watetezi Real Madrid walikuwa wageni wa Schalke ya Ujerumani huku FC Basel ya Uswisi wenyewe wakiikaribisha FC Porto ya Ureno. Katika mchezo kati ya Basel na Porto ambao ulishuhudia mwamuzi Clattenburg akitoa kadi tisa za njano timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1. Kwa upande wa Madrid wao kazi yao haikuwa ngumu sana kwani walifanikiwa kuibuka na ushindi mzuri wa mabao 2-0 dhidi ya Schalke huku mshambuliaji wake nyota Cristiano Ronaldo akimaliza ukame wa mabao kwa kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 26 huku lingine likifungwa na Marcelo katika dakika ya 79. Kabla ya kwenda katika mechi za marudiano za michuano hiyo kutakuwa na mechi zingine za mkondo zitakazochezwa wiki ijayo ya Februari 24 na 25 ambapo mabingwa wa Italia Juventus watakuwa wenyeji wa Borussia Dortmund ya Italia na mabingwa wa Ligi Kuu Manchester City wakiwakaribisha Barcelona ya Hispania. Katika michezo itakayochezwa Februari 25 Arsenal ya uingereza watakuwa wenyeji wa Monaco ya Ufaransa huku Bayer Leverkusen ya Ujerumani wao wakipepetana na Atletico Madrid ya Hispania.

Wednesday, February 18, 2015

MOURINHO AKIRI ILIKUWA BAHATI KUPATA SARE KWA PSG.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amekiri kikosi cha kilikuwa na bahati kupata sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya timu 16 bora dhidi ya Paris Saint-Germain. Katika mchezo huo Branislav Ivanovic ndiye aliyeifungiwa Chelsea bao la kuongoza kabla ya Edinson Cavani hajasawazisha. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Mourinho amesema ukiona jinsi golikipa wake Thibaut Courtois alivyokuwa akiokoa michomo mingi ya wapinzani hakuna shaka kuwa ilikuwa bahati kwao kuibuka na ushindi. Mourinho amesema sasa karata iko upande wao kwani mchezo huo utaamuliwa katika Uwanja wa Stamford Bridge baada ya wiki mbili zijazo.

NYOTA WA LIVERPOOL ALIMWA ADHABU YA MECHI NNE UEFA.

MCHEZAJI wa Liverpool Lazar Markovic amefungiwa mechi nne za Ulaya na Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA kwa kadi nyekundu aliyopewa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya FC Basel Desemba mwaka jana. Markovic mwenye umri wa miaka 20 alitolewa nje kwa kumpiga kofi usoni Behrang Safari katika dakika za mwisho za mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 na Liverpool kuenguliwa katika michuano hiyo. UEFA imeongeza mechi zaidi baada ya Markovic pia kutolewa nje akiitumikia Benfica msimu uliopita katika nusu fainali ya Europa League. Liverpool haitakata rufani kutokana na adhabu hiyo hivyo kumfanya kuukosa mchezo wa Europa League dhidi ya Besiktas kesho na kama wakifanikiwa kusonga mbele ataweza tena kuwepo katika kikosi cha timu hiyo katika hatua ya robo fainali.