Thursday, February 26, 2015

LIGI YA MISRI KUANZA TENA BILA MASHABIKI.

MECHI za soka nchini Misri zinatarajiwa kuanza tena lakini watalazimika kucheza bila mashabiki kuwepo viwanjani. Chama cha Soka cha Misri-EFA kimetangaza kuwa mechi za ligi zinatarajiwa kuanza tena mwezi ujao baada ya kusimamishwa wiki zilizopita kutokana na vurugu zilizotokea katika Uwanja wa Kijeshi uliopo jijini Cairo. EFA katika taarifa yake imedai kuwa baada ya jopo kati yao, wizara ya mambo ya ndani na wizara ya michezo kukutana wamefikia maamuzi kuwa ligi hiyo iendelee baada ya kupita siku 40 za maombolezo. Ligi Kuu ya Misri pamoja na mashindano mengine ya soka yalisimamishwa toka Februari 8 mwaka huu wakati mashabiki 20 wa Zamalek walipouawa baada ya polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya mashabiki waliotaka kuingia uwanjani kwa nguvu. Mechi nyingi za ligi zimekuwa zikichezwa bila mashabiki toka mashabiki zaidi ya 70 wauawe Februari mwaka 2012 baada ya kushambuliwa na mashabiki wa Al Masry katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Port Said.

No comments:

Post a Comment