Thursday, June 30, 2016

NEYMAR KUJITIA KITANZI BARCELONA.

RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amesema Neymar anatarajiwa kusaini mkataba mpya katika kipindi cha siku chache zijazo. Mkataba wa sasa wa neymar unamalizika Juni mwaka 2018 na mazungumzo ya mkataba mpya yamekuwa yakindelea kwa muda sasa hivyo kuzusha tetesi kuwa klabu za Real Madrid, Paris Saint-Germain au Manchester United zinaweza kulipa kitenzi cha euro milioni 200 kilichowekwa katika mkataba wake. Hata hivyo, akiongeza na wanahabari mapema leo, Bartomeu amesema Neymar hatakwenda popote na katika siku chache zijazo atasaini mkataba mpya wa miaka mitano zaidi. Wakala wa zamani wa Neymar, Wagner Ribeiro hivi karibuni alidai kuwa kuna klabu tatu kubwa zinazomfukuzia nyota huyo wa kimataifa wa Brazil lakini mwenyewe anafurahia kuendelea kubakia Camp Nou. Neymar alijiunga na Barcelona akitokea Santos mwaka 2013 a kufanikiwa kushinda taji la La Liga na Kombe la Mfalme mara mbili pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka jana.

WENGER ADAIWA KUWA TAYARI KUINOA UINGEREZA.

VYOMBO vya habari nchini Uingereza vimeripoti kuwa meneja wa Arsenal, Arsene Wenger yuko tayari kujadili kibarua cha kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo wakati mkataba wake utakapomalizika mwaka ujao. Wenger mwenye umri wa miaka 66, amekuwa akitajwa kama mmoja wa makocha wanaoweza kuchukua ya kuinoa Uingereza iliyoachwa wazi na Roy Hodgson, lakini kocha huyo amekuwa akisisitiza anataka kumaliza mkataba wake na Arsenal kabla ya kufanya maamuzi yeyote. Uingereza kwasasa haina kocha baada ya Hodgson kuondoka kufuatia kutolewa katika michuano ya Ulaya na Iceland lakini ofisa mkuu wa FA Martin Glenn amesema yuko tayari kusubiri mpaka watakapopata mtu wanayemuhitaji, huku magazeti ya The Times na Telegraph yakidai kuwa Wenger atakuwa tayari kwa kibarua hicho. Kama Mfaransa huyo atakuwa tayari, hata hivyo dili lolote kwa ajili ya kuchukua kibaua hicho itabidi lifanyike kiangazi mwakani hivyo FA italazimika kutafuta kocha wa muda katika kampeni zao za kufuzu Kombe la Dunia. Gareth Southgate ambaye anakinoa kikosi cha vijana wa chini ya umri wa miaka 21 wa nchi hiyo, amekuwa akitajwa kupewa kibarua cha muda kufundisha kikosi cha wakubwa wakati wakitafuta mbadala wa Hodgson.

CHILE KUCHEZA NA MABINGWA WA EURO 2016.

MABINGWA wa michuano ya Copa America, Chile wanatarajiwa kupambana na bingwa wa michuano ya Ulaya anakayepatikana baadae mwezi ujao. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na rais wa Shirikisho la Soka la America Kusini-CONMEBOL, Alejandro Dominguez, mchezo huo utakaokutanisha bingwa wa Copa America na Euro 2016 utachezwa katika miezi michache ijayo. Wakati Chile wakijihakikishia nafasi yao ya kushiriki Kombe la Shirikisho mwaka 2017, Dominguez amebainisha kuwa tayari wameshatuma barua ya maombi ya mchezo huo kwa Shirikisho la Soka la Ulaya. Dominguez amesema mara baada ya kutuma barua hiyo wamepata majibu ya matumaini kwamba mchezo huo unaweza kuwepo hivyo wanachotakiwa kufanya ni kutafuta tarehe itakayofaa.

HULK AKAMILISHA USAJILI WAKE CHINA.

KLABU ya Shanghai SIPG imekamilisha rasmi usajili wa nyota wa kimataifa wa Brazil, Hulk kutoka klabu ya Zenit St Petersburg ya Urusi. Klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya China-CLS imelipa kitita cha euro milioni 56 kwa mchezaji huyo ambachi kimeweka rekodi mpya ya usajili katika ligi hiyo. Zenit pia wanatarajiwa kupata bakshishi ya euro milioni mbili zaidi kama mshambuliaji huyo atafunga mabao zaidi ya 15. Inadaiwa kuwa Hulk amekubalia mshahara wa euro milioni 12.5 kabla ya bakshishi, kiasi ambacho kitamfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi CLS. Klabu hiyo ilithibitisha taarifa hizo kupitia mtandao wake na kudai kuwa Hulk alisaini mkataba wake pindi alipomaliza vipimo vyake vya afya.

SCOLARI ATAMANI KUINOA UINGEREZA.

KOCHA wa zamani wa Brazil, Luiz Felipe Scolari ametangaza nia yake ya kuja kuwa meneja ajaye wa timu ya taifa ya Uingereza. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 67 ambaye aliiongoza Brazil kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2002, alipata nafasi ya kuchukua mikoba ya Sven-Goran Eriksson kama meneja wa Uingereza mwaka 2006 kabla ya kujitoa kutokana na kushambuliwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo. Scolari ambaye alishindwa kupata mafanikio katika klabu ya Chelsea kwa kutimuliwa baada ya miezi sita, amesisitiza kuwa yuko tayari kwa chochote ambacho Chama cha Soka Uingereza kitahitaji kutoka kwake kama akiteuliwa kuwa kocha. Akihojiwa Scolari amesema kwasasa yeye bado ni meneja wa Guanghou na anakipenda kibarua chake lakini anafahamu umuhimu wa kibarua cha kuinoa Uingereza katika ulimwengu wa soka hivi sasa. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa anahusudu soka la Uingereza na anafahamu mahitaji ya timu ya taifa kuwa inahitaji mafanikio.

NOLITO ANUKIA CITY.

WINGA mahiri wa kimataifa wa Hispania, Nolito anadaiwa kuwa tayari ameshatua jijini Manchester kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wake kwenda Manchester City. Nyota huyo anatarajiwa kuwa mchezaji wa pili kusajili na meneja mpya wa klabu hiyo Pep Guardiola baada ya kufikia makubaliano mabo binafsi na timu hiyo ya Ligi Kuu. Nolito anatarajiwa kumalizia baadhi vitu vichache vilivyobaki katika uhamisho wake kutoka Celta Vigo ambao umegharimu kiasi cha paundi milioni 14, pindi atakapotembelea kituo cha michezo cha City. Mara baada ya kukamilisha vipimo vyake vya afya, Nolito anatarajiwa kutembezwa katika kituo hicho kabla ya kupigwa picha na kutambulishwa rasmi kwa vyombo vya habari. Nyota huyo atakuwa mchzaji pili kusajiliwa na City baada ya Ilkay Gundogan aliyesajiliwa kutokea Borussia Dortmund Juni 2 mwaka huu.

SIMEONE ASISITIZA KUENDELEA KUBAKIA ATLETICO.

MENEJA wa Atletico Madrid, Diego Simeone amefafanua kauli yake aliyoitoa kufuatia timu yake kupoteza mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi uliopita. Atletico ilishindwa kutamba kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu baada ya kutandikwa tena mahasimu wao wa jiji Real Madrid. Baada ya mchezo huo ambao walipoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penati jijini Milan, Simeone amesema anatarajiwa kuchukua muda kufikiria kuhusu mustakabali wake katika klabu hiyo. Lakini meneja huyo mwenye umri wa miaka 46 amesema kauli hiyo aliitoa wakati akiwa katika kipindi kibaya, kwani hana mpango wowote wa kuondoka Atletico kwasasa. Simeone aliendelea kudai kuwa Atletico itaendelea kuwa moja ya vikosi bora kabisa katika ulimwengu wa soka katika miaka mingi ijayo. Meneja huyo amesema timu pekee zinazowazidi kwa ubora ni Barcelona, Real Madrid na Bayern Munich, hakuna nyingine.

MADRID YAMTENGEA ALABA EURO MILIONI 65.

KLABU ya Real Madrid inadaiwa kutoa ofa ya euro milioni 65 kwa ajili ya kumuwania nyota wa Bayern Munich David Alaba. Wakongwe hao wa soka wa Hispania wameamua kumuwinda kwa udi na uvumba nyota huyo wa kimataifa wa Austria kiangazi hiki na sasa wameboresha ofa yao kutoka euro milioni 50 walizotoa mara ya kwanza. Ingawa Bayern hawajatamka lolote kuhusu ofa hiyo, inafahamika kuwa wanataka euro milioni 80 kwa timu itakayomuhitaji Alaba. Mbali na Alaba, Madrid pia wameonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo wa mabingw awa Ligi Kuu Leicester City N’golo Kante.

MANC CITY YAKAMILISHA USAJILI WA MOOY.

KLABU ya Manchester City imekamilisha usajili wa nyota wa kimataifa wa Australia Aaron Mooy kutoka Meolbourne City klabu ambayo pia wanaimiliki. Uhamisho huo ulithibitishwa jana ambapo nyota huyo sasa anahamia City kwa mkataba wa miaka mitatu. Mooy mwenye umri wa miaka 25 amekuwa akitwaa tuzo ya mchezaji wa mwaka katika klabu hiyo toka alipojiunga nao akitokea kwa mahasimu wao Western Sidney Wanderers mwaka 2014. Hata hivyo, Mooy anatarajiwa kupelekwa kwa mkopo kwanza pindi atakapotua Manchester.

Tuesday, June 28, 2016

LIVERPOOL YAKAMILISHA USAJILI WA PAUNDI MILIONI 34 WA SADIO MANE.

KLABU ya Liverpool imekamilisha rasmi usajili wa Sadio Mane aliyetua Anfield kwa kitita cha paundi milioni 34 kutoka Southampton. Nyota huyo anajiunga kwa mkataba wa muda mrefu na usajili wa tatu kwa Liverpool kiangazi hiki baada ya kuwa tayari wamewanasa kipa wa kimataifa wa Ujerumani Loris Karius na beki wa Cameroon Joel Matip. Ada ya uhamisho wa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Senegal mwenye umri wa miaka 24, inadaiwa inaweza kupanda na kufikia paundi milioni 36 hivyo kupita ile ya paundi milioni 35 aliyosajiliwa Andy Carroll mwaka 2011 na kuwa mchezaji ghali zaidi wa klabu hiyo. Mane amefunga mabao 21 katika mechi 67 za Ligi Kuu alizoichezea Southampton baada ya kujiunga nao kwa kitita cha paundi milioni 10 akitokea Salzburg mwaka 2014.

BAADA YA KUTUA RASMI JUVENTUS, ALVES APANIA TAJI LA CHAMPIONS LEAGUE.

BEKI wa kimataifa wa Brazil, Dani Alves amepania kushinda kupelekea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya Juventus baada ya kukamilisha uhamisho wake kutoka Barcelona. Nyota huyo alioyeondoka Camp Nou kwenda Turin kama mchezaji huru, amesaini mkataba wa miaka miwili jana huku kukiwa na chaguo na kuongezewa mwingine mmoja. Beki huyo wa kulia alikuwa sehemu ya kikosi cha Barcelona kilichowanyima Juventus mataji matatu kwa kuwafunga katika hatua ya fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2015 iliyofanyika jijini Berlin. Lakini sasa Alves ana matumaini ya kuisaidia klabu hiyo kutwaa taji lake la kwanza la Ulaya toka walipofanya hivyo msimu wa 1995-1996. Akihojiwa Alves amesema ni heshima kubwa kuwa sehemu ya kikosi hicho kwani Juventus wana ndoto kubwa na angependa kuwasaidia kuzitimiza.


MARADONA, RAIS WA ARGENTINA WAMUANGUKIA MESSI ABADILI UAMUZI WA KUSTAAFU.

NGULI wa soka wa Argentina, Diego Maradona amemtaka Lionel Messi kutoendelea na uamuzi wake wa kustaafu soka la kimataifa baada ya kipigo walichopata katika fainali ya michuano ya Copa America. Maradona alikakariwa na gazeti moja nchini wake akimtaka Messi abakie katika timu ya taifa kwasababu bado muda wake rasmi wa kufanya hivyo haujafika. Nguli aliongeza kuwa ana imani Messi atakwenda nchini Urusi akiwa katika kiwango cha juu ili kuwa bingwa wa dunia katika Kombe la Dunia mwaka 2018. Messi mwenye umri wa miaka 29, aliwaambia wanahabari nchini Marekani uamuzi wake wa kuamua kustaafu soka la kimataifa baada ya Argentina kuchapwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati na Chile Jumatatu Alfajiri. Maradona ambaye amewahi kunyakuwa Kombe la Dunia mwaka 1986 akiwa na Argentina, alilaumu ukame wa mataji kwa nchi hiyo unatokana na Chama chao cha soka-AFA. Mbali na Mardona lakini pia wa rais wa Argentina, Mauricio Macri naye amemuangukia Messi akimtaka kuteungua uamuzi wake huo.

INIESTA APONDA KIWANGO KIBOVU CHA TIMU YAO.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Hispania, Andres Iniesta amekiri uchezaji wa hovyo wa kipindi cha kwanza ndio uliowagharimu na kuepelekea kutolewa katika michuano ya Ulaya na Italia jana. Akihojiwa Iniesta amesema ni vigumu kukubali kufungwa lakini wamekubali kwasababu tatizo lilikuwa katika masuala ya kiufundi zaidi. Italia walishinda mchezo huo kwa mabao 2-0 huko Stade de France huku Giorgio Chiellini akifunga bao la kuongoza katika kipindi cha kwanza kabla ya Graziano Pelle hajafunga la ushindi katika dakika za majeruhi. Iniesta amesema anadhani walikuwa wanasubiri sana kuona kitu gani wapinzani wao watafanya na mambo kama hayo muda mwingine lazima yakugharimu. Nyota huyo aliongeza kuwa hilo ndio kosa walilofanya kipindi kwanza lakini kipindi walikuwa tofauti na walicheza zaidi kama wlaivyozoea.

COPA AMERICA YAMUACHA SANCHEZ NA MAJERUHI.

MSHAMBULIAJI mahiri wa kimataifa wa Chile na klabu ya Arsenal Alexis Sanchez anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kw amuda kufuatia kuumia kifundo chake cha mguu katika mchezo wa fainali ya michuano ya Copa America dhidi ya Argentina jana. Nyota huyo alipiga picha na kuituma katika mitandao wa kijamii ikionyesha jinsi kifundo cha mkuu wake wa kushoto kilivyovimba huku picha nyingine ikionyesha bandeji gumu alilofunga. Sanchez alitwaa tuzo ya Mpira wa Dhahabu ya mchezo bora wa mashindano baada ya Chile kuichapa Argentina kwa changamoto ya mikwaju ya penati ikiw ani mara ya pili mfululizo kutwaa taji hilo. Nyota huyo alimaliza akiwa amefunga mabao matatu na kusaidia mengine mawili lakini alitolewa katika muda wa nyongeza wakati wa mchezo huo hali ambayo haikuwa ya kawaida kwa mchezaji kama yeye aliyezoea kucheza dakika zote. Akiwa hajatoa maelezo yeyote ni kwa kiasi gani alivyoumia, Sanchez aliandika katika mtandao wake kuwa anafuraha pamoja na kuumia kwake kwa ilistahili.

BREXIT KUCHELESHA USAJILI LIGI KUU.

WAKILI wa masuala ya michezo, Carol Couse amedai kuwa kura za kihistoria za Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya-EU Alhamisi iliyopita, kunaweza kupelekea kuchelewa kufanyika kwa usajili kwa kipindi hiki cha kiangazi. Uamuzi wa kura hizo tayari umeshaanza kuleta athari nchini Uingereza kwa kusababisha sarafu yao kuporomoka na kuzidiwa na ile ya euro. Timu zote 20 za Ligi Kuu zilikuwa zikiunga mkono kampeni ya kubakia ndani ya EU, kutokana na wasiwasi wa kupanda gharama kwa vibali vya kazi kwa wachezaji kutoka nje na kunyima uwezo wa kusajili wachezaji wapya. Dirisha la usajili limefunguliw arasmi Ijumma iliyopita kama ilivyo ada na Couse ambaye anafanya kazi katika klabu kadhaa kubwa ikiwemo Manchester United anafikiri timu za Ligi Kuu zitasubiri mpaka Agosti ili kununua wachezaji. Couse aliendelea kudai kuwa hatua hiyo itakuja ili wasubiri sarafu ya paundi itulie kwanza, hivyo kufanya klabu kufanya usajili wa haraka haraka mwishoni kukimbizana na muda.

HODGSON AWAJIBIKA KABLA YA KUWAJIBISHWA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, amejiuzulu punde kufuatia kipigo cha fedheha cha mabao 2-1 walichopata kutoka kwa timu ndogo ya Iceland katika michuano ya Ulaya inayoendelea nchini Ufaransa. Mkataba wa Hodgson ulikuwa umelizike baada ya michuano hii na kufuatia mchezo huo uliofanyika jijini Nice, aliwaambia wanahabari katika taarifa aliyoiandaa kuwa hataweza kuendelea tena kuinoa timu hiyo. Hodgson mwenye umri wa miaka 68 ambaye alichukua mikoba kutoka kwa Fabio Capello maka 2012 amesema angependa kuendelea kubakia lakini kutokana na hali ilivyo anadhani ni vyema kumpisha mtu mwingine. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kikosi cha Uingereza kimesheheni vijana wenye vipaji ambao wana uchu na nja ya mafanikio hivyo anadhani atakayechukua nafasi yake ataendeleza alipoachia. Mara baada ya kumaliza kusoma taarifa yake Hodgson aliondoka haraka na msemaji wa Chama cha Soka cha Uingereza-FA Ray Lewington akidai kuwa kocha huyo hatafanya mazungumzo mengine na wana habari.

Monday, June 27, 2016

MAN UNITED YAMSHIKIA BANGO POGBA, IBRAHIMOVIC NAYE ANUKIA.

KLABU ya Manchester United inadaiwa kutaka kuendelea na mpango wake wa kumrudisha tena kiungo mahiri wa kimataifa wa Ufaransa Paul Pogba. United ilimuuza Pogba akiwa mdogo kwenda Juventus mwaka 2012 kabla ya kiungo huyo hajapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Sir Alex Ferguson. Lakini Pogba amekwenda jijini Turin na kuimarika na kwa mmoja katia ya wachezaji duniani, akiisaidia Juventus kutwaa mataji manne mfululizo ya Serie A huku pia akiisaidia nchi yake katika kipindi cha miaka minne iliyopita. United wamepania kumrejesha Pogba Old Trafford lakini wameshaambiwa na Juventus kuwa anaweza kuwagharimu ada ya paundi milioni 100 ambayo itavunja rekodi ya usajili duniani. Mazungumzo pia yanaendelea kati ya Zlatan Ibrahimovic ambaye ni mchezaji huru kufuatia nchi yake kutolewa katika michuano ya Ulaya inayoendelea nchini Ufaransa na kuamua kustaafu soka la kimataifa.

RASMI BLANC AONDOKA PSG.

KLABU ya Paris Saint-Germain-PSG imetangaza rasmi kuwa Laurent Blanc ameondoka katika timu hiyo kwa maelewano. Mapema mwezi huu kuna taarifa zilizagaa kuwa Blanc alitarajiwa kutimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Unai Emery, meneja wa zamani wa Sevilla ambaye ameshinda mataji matatu mfululizo ya Europa League. PSG sasa wamethibitisha taarifa hizo za kuachana na Blanc ambaye ameiwezesha timu hiyo kutwaa mataji matatu ya nyumbani katika msimu miwili iliyopita lakini amekuwa akikwama katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa ulaya katika misimu mitatu aliyoinoa klabu hiyo. Katika taarifa ya klabu hiyo iliyotumwa katika mtandao wake imedai kuwa wameachana na Blanc baada ya kufikia makubaliano kwa faida ya pande zote mbili. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa kocha msaidizi Jean-Louis Gasset na mwalimu wa mazoezi Philippe Lambert nao pia wataondoka wakati klabu hiyo ikijaribu kuajiri benchi jipya kabisa la ufundi.

BRAVO ANA MATUMAINI MESSI ATABADILI UAMUZI WAKE.

KIPA wa mabingwa wa Copa America Chile, Claudio Bravo ana matumaini mchezaji mwenzake wa Barcelona Lionel Messi atafikiria tena uamuzi wa kustaafu soka la kimataifa na kuendelea kuitumikia Argentina. Messi akiwa katika huzuni aliushtusha ulimwengu baada ya Argentina kushindwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati kwa Chile katika fainali ya Copa America mapema leo, kutangaza kustaafu kuitumikia nchi yake. Nyota huyo ambaye ndio mfungaji bora wa wakati wote wan chi hiyo, alikuwa akibubujikwa na machozi kufuatia kukosa penati ambapo ilipelekea Argentina kupata kipigo cha tatu katika fainali za michuano mikubwa. Akihojiwa Bravo amesema kwake Messi ni mchezaji bora duniani na wote wanafahamu ubora wake hivyo ni matumaini atabadili uamuzi wake na kuendelea kuitumikia Argentina.

COPA AMERICA 2016: SANCHEZ ATWAA GOLDEN BALL WAKATI CHILE WAKIKWANGUA TUZO ZOTE.

MSHAMBULIAJI nyota wa Arsenal, Alexis Sanchez ametajwa kuwa mchezaji bora wa mashindano wakati mabingwa wa Copa America Chile wakichukua tuzo zote za mchezaji mmoja mmoja. Chile waliichapa Argentina kwa changamoto ya mikwaju ya penati kwa mwaka wa pili mfululizo katika fainali iliyofanyika mapema leo na Sachez akitwaa tuzo ya Mpira wa Dhahabu kama mchezaji bora baada ya kufunga mabao matatu na kusaidia mengine mawili katika mechi sita. 
Mchezaji mwenzake wa Chile Eduardo Vargas alitwaa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu baada ya kumaliza kinara wa mabao akiwa na mabao sita huku kipa Claudio Bravo yeye akishinda Golden Cloves kwa kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja pekee katika michuano hiyo. Chile ndio waliotawala katika kikosi bora cha michuano hiyo baada ya wachezaji nane kuteuliwa, pamoja na wengine watatu wa Argentina akiwemo Lionel Messi ambaye alikosa penati katika mchezo huo.

MAN CITY YAKARIBIA KULINASA CHIPUKIZI LA COLOMBIA.

KLABU ya Manchester City inadaiwa kukaribia kukamilisha usajili wa winga machachari wa kimataifa wa Colombia Marlos Moreno. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19 ambaye anakipiga katika klabu yake ya nyumbani ya Atletico Nacional, anatarajiwa kuwagharimu City euro milioni 10. City wanaamini kuwa wamewashinda wapinzani wao Manchester United na Banfica katika mbio za kumuwania winga huyo mwenye mbio. Kuna uwezekano wa Moreno kutopata kibali cha kufanya kazi Uingereza na City wamepanga kumpeleka kwa mkopo nchini Hispania kwa ajili ya msimu wa 2016-2017.

DONE DEAL: SAIDO MANE TO LIVERPOOL.

MSHAMBULIAJI wa Southampton, Sadio Mane anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya leo Liverpool baada ya klabu hizo kukubaliano ada ya uhamisho wake ambayo inakadiriwa kufikia kiasi cha paundi milioni 30. Kama dili hilo likikamilika, itakuwa moja ya usajili ghali Liverpool ukishindana na ule wa paundi milioni 32.5 zilizolipwa kwa ajili ya Christian Benteke na paundi milioni 35 kwa ajili ya Andy Carroll. Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp anataka kuimarisha safu yake ya ushambuliaji na alimpa Mane kipaumbele katika usajili wa kipindi hiki cha kiangazi. Klopp alivutiwa na Mane wakati alipowafunga mara mbili wakati Southampton walipotoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuja kuifunga Liverpool mabao 3-2 katika Uwanja wa St Mary’s Machi 20 mwaka huu. Mane sasa anaungana na mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Uingereza Daniel Sturridge na chipukizi wa Ubelgiji Divock Origi ambaye alifunga mabao 11 katika mechi 37 msimu uliopita.

ALMOST DONE DEAL: DANI ALVES TO JUVENTUS.

BEKI wa Barcelona, Dani Alves anatarajiwa kukamilisha uhamisho wake kwenda kwa mabingwa wa Serie A Juventus baada ya kusafiri jana jioni kuelekea jijini Turin. Alves alithibitisha mwanzoni mwa mwezi huu kuwa atajiunga na Juventus baada ya kukaa Barcelona kwa misimu nane na sasa uhamisho huo unaonekana kukaribia kukamilika. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Barcelona lakini klabu hiyo imekubali kumruhusu kuhama akiwa kama mchezaji huru. Juventus walituma picha na video ya mchezaji huyo katika ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa twitter wakionyesha akitua jijini Turin. Juventus imefanikiwa kutwaa taji la tano la Serie A msimu uliopita pamoja na kuondoka kwa nyota wake kadhaa akiwemo Andra Pirlo, Arturo Vidal na carlos Tevez ambao wlaiisaidia timu hiyo kutinga fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2014 na kuja kupoteza kwa kufungwa na Barcelona mabao 3-1.

COPA AMERICA 2016: BAADA YA KUSHINDWA FAINALI NNE, MESSI AAMUA KUTUNDIKA DARUGA ZAKE.MSHABULIAJI nyota Lionel Messi ametangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya kukosa mkwaju wa penati wakati Argentina iliposhindwa katika fainali yake nne kubwa katika kipindi cha miaka tisa. Akihojiwa mara baada ya kipigo hicho kutoka kwa Chile katika michuano ya Copa America, Messi mwenye umri wa miaka 29 amesema amefanya kila analoweza na ameona sio bahati yake hivyo ameamua kustaafu kuitumikia nchi yake. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa wamefanikiwa kufika katika fainali nne za mashindano makubwa na alikuwa akihitaji hilo kwa hamu kubwa lakini ameshindwa hivyo anaona inatosha ili aweze kuwapisha wengine. Akiwa na Barcelona, Messi amefanikiwa kunyakua mataji nane ya La Liga na manne ya Ligi ya Mabingwa ulaya lakini akiwa na Argentina amefanikiwa kutwaa medali ya dhahabu mwaka 2008 pekee. Argentina walitandikwa bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014 kabla ya kupoteza fainali mbili za Copa America kwa Chile zote zikiamuliwa na changamoto ya mikwaju ya penati. Messi pia alikuwepo katika kikosi cha Argentina kilichopoteza mchezo wa fainali ya michuano ya Copa America dhidi ya Brazil mwaka 2007. Katika mchezo huo uliochezwa mapema leo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana katika muda wa kawaida na ule wa nyongeza kabla ta Chile hawajashinda kwa penati 4-2.

Sunday, June 26, 2016

KOCHA WA URUSI AJIUZULU.

KOCHA wa timu ya taifa ya Urusi, Leonid Slutsky amejiuzulu rasmi nafasi hiyo kufuatia kufanya vibaya kwa nchi hiyo katika michuano ya Ulaya inayoendelea nchini Ufaransa. Kocha huyo wa CSKA Moscow sasa atahamishia nguvu zake katika klabu yake, baada ya kuchuka kibarua cha timu ya taifa Agosti mwaka jana baada ya kutimuliwa kwa Fabio Capello. Baada ya kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Wales, Slutsky amesema kikosi hicho kinahitaji kocha mwingine na sasa Shirikisho la Soka la nchi hiyo-RFS limethibitisha kuondoka kwake. Rais wa RFS, Vitaly Mutko alimshukuru Slutsky kwa kazi aliyofanya kwa kipindi chote walichokuwa naye na kudai kuwa aliikuta timu hiyo katika kipindi kigumu wakati ambapo walikuwa hawana hata matumaini ya kufuzu micuano ya Ulaya. Mutko aliongeza kuwa kilichotokea Ufaransa kimesababishwa na mambo mengi ambayo hataki kuyazungumzia lakini kwa mwazo yake Slutsky alifanya kazi yake vyema.


SWANSEA LANASA BEKI LA AJAX.

BEKI Mike van der Hoorn amedai anatarajia kusafiri kuelekea Wales wiki hii kwa ajili ya makubaliano binafsi na Swansea City baada ya klabu hiyo kukubalia kulipa euro milioni 2.5 kwa uhamisho wake kutoka Ajax Amsterdam ya Uholanzi. Van der Hoorn amesema atafanya majadiliano yeye mwenyewe kuhusiana na mshahara wake na bakshishi baada ya makubaliao kati ya klabu hizo mbili kuafikiwa. Akihojiwa beki huyo amesema amefurahi kupata nafasi ya kucheza katika Ligi Kuu hususani katika klabu kubwa kama Swansea. Van der Hoorn mwenye umri wa miaka 23, ni mchezaji wa zamani wa kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi kwa vijana chini ya umri wa miaka 21, aliyeigharimu Ajax euro milioni nne kumuhamisha kutoka Utrecht miaka mitatu iliyopita.

HODGSON AGOMA AKUIPIGIA MAGOTI FA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amesema hataweza kukipigia magoti Chama cha Soka cha nchi hiyo-FA ili kimuongeze mkataba mpya baada ya michuano ya Ulaya inayoendelea nchini Ufaransa. Mkataba wa Hodgson unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa michuano hiyo na mwenyekiti wa FA Greg Dyke amesema kocha huyo mwenye umri wa miaka 68 atabakia endapo kama Uingereza itafanya vyema nchini Ufaransa. Akihojiwa kuelekea mchezo wao wa haua ya mtoano utakaofanyika kesho dhidi ya Iceland, Hodgson amesema atakuwa tayari kuendelea kuinoa timu hiyo kama FA watamtaka afanye hivyo lakini kamwe hatawapigia magoti. Uingereza ilianza michuano hiyo kwa sare ya 1-1 dhidi ya Urusi kabla ya kwenda kuifunga Wales mabao 2-1 na kuja kutoa sare ya bila kufungana na Slovakia katika mechi zao za kundi B, matokeo mbayo yaliwafanya kumaliza katika nafasi ya pili. Uamuzi wa Hodgson kufanya mabadiliko sita katika kikosi chake kwneye mchezo dhidi ya Slovakia ulikosolewa vikali na wadau mbalimbali huku kukiwa na taarifa kuwa uliwaudhi viongozi wa FA.

BREXIT ITAATHIRI LIGI KUU - FABREGAS.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Hispania na klabu ya Chelsea, Cesc Fabregas ameelezea kujitoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya-EU kama kitendo cha makosa na kinaweza kuja kusababisha matatizo mengi. Fabregas mwenye umri wa miaka 29, ametumia mud wake wa kucheza soka katika Ligi Kuu akianzia Arsenal ambako alicheza kuanzia mwaka 2003 mpaka 2011 na sasa Chelsea ambao alijiunga nao akitokea Barcelona mwaka 2014. Nyota huyo anaamini kuwa uamuzi huo hautaathiri uchumi na maisha ya kila ya kila nchini huko lakini pia itakuwa na athari kubwa katika soka na uwezo wa kusajili wachezaji. Akihojiwa Fabregas amesema amesikitishwa na uamuzi huo kwani binafsi anaona ni makosa na kitu ambacho hakukitegemea Uingereza kujitenga. Nyota huyo aliongeza uamuzi huo utaathiri Ligi Kuu, itakuwa vigumu kusajili wachezaji na mishahara itabadilika kama paundi itakaribiana na euro.

ZIDANE ADOKEZA MADRID KUMUWANIA POGBA.

MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amedokeza kuwa klabu hiyo inaweza kumuwania Paul Pogba kufuatia michuano ya Ulaya inayoendelea nchini Ufaransa. Zidane mara kadhaa ameshakaririw akieleza jinsi anavyomhusudu Pogba, na wakala wa nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa, Mino Raiola amesema hivi karibuni kuwa mazungumzo ya awali yameshaanza na Juventus kwa ajili ya uhamisho wake. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo, Zidane alikataa kuingia kwa ungani akidai kuwa kwasasa bado lakini katika kipindi cha wiki mbili zijazo itajulikana. Kwa upande mwingine, kuna taarifa kuwa James Rodriquez anatarajia kukutana na Zidane ili kujadili mustakabali wake huku ikitarajiwa matokeo ya mazungumzo yao yanaweza kupelekea mchezaji huyo kuondoka. Rodriquez amekuwa katika rada za Manchester United, lakini anatarajiwa kuchelewa kurejea Madrid baada ya kushiriki michuano ya Copa America ambapo Colombia imemaliza katika nafasi ya tatu.

MARTINO AMMWAGIA SIFA MESSI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Argentina, Gerardo Martino amesema Lionel Messi amekuwa akicheza kwa kiwango chake cha juu wakati wote wa michuano ya Copa America kama anavyokuwa katika klabu yake ya Barcelona. Argentina wanatarajiwa kukutana na mabingwa watetezi Chile baadae leo katika mchezo wa fainali ikiwa ni kama marudio ya fainali ya mwaka jana ambapo wenyeji Chile walishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana huko Santiago. Messi alifanikiwa kufunga bao moja pekee katika michuano hiyo ya mwaka jana, lakini pamoja na majeruhi yaliyomfanya asicheze katika mechi ya kwanza ya michuano ya mwaka huu ambayo ni maalumu kusherekea miaka 100, tayari ameshafunga mabao matano na kusaidia mengine manne katika mechi tano alizocheza. Akihojiwa kuelekea katika mchezo huo mapema leo, Martino amesema Messi amekuwa katika kiwango bora kama anavyokuwa Barcelona na hilo limetokana na kucheza pamoja na wachezaji haohao kwa kipindi kirefu jambo ambalo linamfanya kujisikia vyema na furaha. Messi alifunga mabao manne katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014, yote akifunga katika hatua ya makundi na kuingoza nchi yake kutinga fainali ambapo walipoteza kwa Ujerumani katika dakika za nyongeza. Lakini aliondoka na tuzo ya mpira wa dhahabu akiwa mchezaji bora wa mashindano hayo yaliyofanyika nchini Brazil na pia alitajwa kama kikosi cha mashindano katika michuano ya Copa Amerika mwaka 2015.

COPA AMERICA 2016: COLOMBIA WATWAA NAFASI YA TATU.MSHAMBULIAJI nyota wa AC Milan, Carlos Bacca alifunga bao pekee wakati Colombia ilipowachapa wenyeji Marekani kwa bao 1-0 ba kutwaa nafasi ya tatu ya michuano ya Copa America mapema leo. Bacca mwenye umri wa miaka 29 alifungwa bao hilo la ushindi katika dakika 31 ya mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Phoenix huko Glendale, Arizona. Hii ni mara ya pili kwa Colombia kuwafunga Marekani katika michuano hiyo baada ya pia kufanya hivyo katika mchezo wao wa ufunguzi ambao walishinda mabao 2-0. Mchezo wa fainali ya michuano hiyo unatarajiwa kupigwa Alfajiri ya kuamkia kesho ambapo Argentina watakwaana na mabingwa watetezi Chile huko East Rutherford, New Jersey.

Saturday, June 25, 2016

BREXIT YAMUWEKA BALE NJIA PANDA.

WAKILI mmoja wa masuala ya michezo, amedai kuwa hadhi ya Gareth Bale inaweza kuwa katika tishio kwasababu ya uamuzi wa Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya-EU. Timu za Hispania ni miongoni mwa timu ambazo zina viwango maalumu kwa wachezaji wanaotoka nje ya EU, kitu ambacho nyota huyo wa kimataifa wa Wales anaweza kuwa Uingereza ikijenga rasmi na umoja huo. Kwasasa Madrid ni kama wamepita kiwango cha zaidi ya wachezaji watatu wanaotoka nje ya EU kwasababu ya kuwa na James Rodriquez, Danilo, Casemiro na Bale, lakini taarifa zinadai kuwa taratibu za kujitoa huko zinaweza kuchukua miaka miwili mpaka saba. Kama Bale akiendelea kuwepo Madrid mpaka Uingereza itakapojitenga rasmi ni wazi kuwa atahesabika kama mchezaji anayetoka nje ya EU hivyo klabu hiyo italazimika kupunguza mchezaji mmoja.

FIFA YAINGILIA KATI MGOGORO WA SOKA ARGENTINA.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limesema limetwaa madaraka ya Shirikisho la Soka la Argentina kutoka kwa uongozi wa sasa na watasaidia kuteua jopo la dharura litakaloweza kushughulikia mambo yake. FIFA ilitangaza uamuzi huo jana, siku mbili kabla ya Lionel Messi hajaiongoza Argentina kucheza fainali ya michuano ya Copa America dhidi ya Chile huko Rutherford, New Jersey. Alhamisi rais wa shirikisho hilo, Luis Segura ambaye pia ni mjumbe ya baraza la FIFA, alishitakiwa kwa kosa ufisadi kuhusiana na haki za matangazo ya luninga. Wakiongozwa na Julio Grondona toka miaka ya sabini, shirikisho hilo limekuwa katika migogoro toka alipofariki makamu huyo wa rais wa FIFA mwaka 2014. Taarifa ya FIFA imedai kuwa kamati maalumu ya kuweka mambo sawa itakayokuwa na wajumbe wasiozidi saba ndio itakayopewa jukumu la kuongoza shughuli za kila siku za shirikisho hilo. Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Julai 2017.

MAKUNDI YA KUFUZU KOMBE LA DUNIA AFRIKA HADHARANI.

TIMU tatu kati ya tano za Afrika zilizoshiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 zimepangwa katika kundi moja katika mechi za kufuzu michuano hiyo mwaka 2018. Timu moja kati ya Algeria, Cameroon na Nigeria ndio zitaweza kushiriki michuano hiyo ya Urusi baada ya Shirikisho la Soka la Afrika-CAF kupanga ratiba ya makundi matano ta kufuzu jana. Timu hizo tatu zenye nguvu kisoka barani Afrika zimepangwa na Zambia. Ni mshindi mmoja pekee katika makundi hayo matano ndio atafuzu michuano hiyo itakayoshirikisha timu 32. Ivory Coast ambao watakuwa wakitafuta nafasi ya kufuzu michuano hiyo kw amara ya nne, wamepangwa kundi moja na Gabon, Mali na Morocco. Mechi hizo za makundi zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi Octoba mwaka huu na kuendelea mpaka Novemba mwaka 2017.

Makundi hayo ni
Kundi A: Tunisia, Libya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Guinea.
Kundi B: Zambia, Cameroon, Algeria, Nigeria
Kundi C: Gabon, Mali, Ivory Coast, Morocco
Kundi D: Senegal, Afrika Kusini, Burkina Faso, Cape Verde
Kundi E: Ghana, Misri, Congo, Uganda

MORATA BADO KIPUSA LIGI KUU.

WAKALA wa mshambuliaji Alvaro Morata, Juanna Lopez amedai kuwa bado mteja wake amepata ofa kutoka klabu kubwa Ligi Kuu. Ilithibitishwa Jumatano iliyopita kuwa Morata mwenye umri wa miaka 23, atarejea Real Madrid kutoka Juventus kama makubaliano yalivyokuwa. Lakini Lopez amedokeza kuwa mustakabali wa mteja wake unaweza usiwe Santiago Bernabeu chini Zinedine Zidane na kuongeza tetesi kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Hispania anaweza kuuzwa na Madrid kwa faida. Akihojiwa Lopez amesema Morata bado ana ofa kutoka klabu kubwa Ligi Kuu, hivyo wanasubiri kuona iakavyokuwa baada ya kuzungumza na Zidane.

PENATI YA RAMOS ILIPASWA KURUDIWA - UEFA.

MWAMUZI kiongozi wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, Pierluigi Collina amesema beki wa Hispania Sergio Ramso alipaswa kuruhusiwa kurudia penati yake dhidi ya Croatia Jumanne iliyopita baada ya kipa Danijel Subasic kutoka katika mstari wake mapema. Collina amekiri ilikuwa sio sawa kwa mwamuzi Bjorn Kuipers kumruhusu Subasic kutoka katika mstari wake mapema na kwenda kuokoa penati ya Ramos. Kukosa kwa penati hiyo kulifanya matokeo kubaki sare ya bao 1-1 kabla ya Croatia hawajakwenda na kuongeza lingine na kuwafanya waongoze kundi lao na kuifanya Hispania kwenda kukwaana na Italia katika hatua ya mtoano. Akihojiwa Collina amesema baada ya timu ya waamuzi kupitia mchezo huo waling’amua makosa ya wazi kwa kipa huyo aliyesogea mbele hivyo haukuwa uamuzi sahihi. Kuelekea hatua ya mtoano ambapo penati zinanafasi kubwa katika mechi hizo, Collina amesema watafanya jitihada kuhakikisha makosa hayo hayajirudii tena.

LIVERPOOL WAONGOZA MBIO ZA KUMNASA SADIO MANE.

TAARIFA zinadai kuwa Liverpool wanazidi kuwa na uhakika wa kumnasa mshambuliaji wa Southampton Sadio Mane. Liverpool imekuwa katika mzungumzo na Southmpton kwa muda mrefu sasa wakijaribu kushawishi kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Senegal na taarifa zilizotoka karibuni zinadai kuwa klabu hiyo inakaribia kufanikiwa suala hilo. Meneja wa Liverpool, Jurgen Klopp amemtaja Mane kama moja ya vipaumbele vyake wakati akijaribu kuimarisha kiksoi chake kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu. Mane alimkuna Klopp wakati timu hizo zilipokutana katika mechi za Ligi Kuu wakati alipofunga katika mchezo wa sare ya bao 1-1 uliofanyika Anfield na ule aliofunga mabao mawili na kuipa Southmpton ushindi wa mabao 3-2 katika Uwanja wa St, Mary’s. Manchester United na Manchester nazo pia zimekuwa zikimuwania mane lakini Liverpool wamepania kushinda mbio hizo.

MESSI AKIRI KUKOSEA KUIKOSOA AFA KIPINDI HIKI.

MSHAMBULIAJI nyota wa Argentina, Lionel Messi amekiri kufanya makosa kwa kauli yake ya kuponda Shirikisho la Soka la nchi yake-AFA, lakini amekataa kutumia hali hiyo kama sababu ya kushindwa mchezo wa fainali ya Copa America dhidi ya Chile kesho. Nyota huyo wa Barcelona aliweka wazi hisia zake kuhusu AFA Alhamisi iliyopita wakati alipotuma picha katika mitandao wa kijamii huku kukiwa na Ujumbe mkali wa kuiponda AFA. Nahodha huyo wa Argentina amekiri kufanya kosa kwa kutuma huo lakini ni kwasababu tu wanakabiliwa na mchezo wa fainali. Messi amesema anafahamu hakupaswa kutoa kauli hiyo kwasababu mchezo wao fainali uko karibu lakini ni wazi shirikisho lao linapswa kujipanga na kuweka mambo yake sawa. Argentina itakuwa ikifukizia taji lake la kwanza michuano hiyo toka mwaka 1993 baada ya mwaka jana pia kulikosa kwa kufungwa na Chile kwa changamoto ya mikwaju ya penati.

Thursday, June 23, 2016

COPA AMERICA 2016: FAINALI NI CHILE VS ARGENTINA.MABINGWA watetezi Chile wanatarajiwa kupambana na Argentina katika fainali ya michuano ya Copa America Jumapili hii baada ya kuiangamiza Colombia kwa mabao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa mapema leo ambao ulilazimika kuchelewa kwa saa mbili kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha. Chile walikuwa wakiongoza kwa mabao mawili baada ya mapumziko lakini kipindi cha pili cha mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Soldier Field jijini Chicago, kilikumbwa na mvua hiyo ikabidi wazsubiri mpaka ilipokatika. Mabao ya Chile katika mchezo huo yalifungwa na Charles Aranguiz na Jose Pedro Fuenzalida aliyefunga la pili na kuzamisha jahazi la Colombia. Fainali hiyo ni kama marudio ya ile ya mwaka jana ambayo Chile waliokuwa wenyeji walishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati. Colombia sasa watachuana na wenyeji Marekani katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu Jumamosi hii.

Wednesday, June 22, 2016

CHELSEA YAPANIA KUNASA SAINI YA BEKI YA NAPOLI.

KLABU ya Chelsea inadaiwa kuanza kumuwania beki wa Napoli Kalidou Koulibaly kwa kutoa ofa ya paundi milioni 19.2. Chelsea wamekuwa wakimhusudu kwa kiasi kikubwa beki huyo wa kimataifa wa Senegal, ambaye ameingia katika mzozo na klabu yake kuhusiana na uhamisho wake. Hata hivyo, ofa hiyo ya Chelsea tayari imeshakataliwa na Napoli wamedai wanataka kitita cha paundi milioni 30 ili waweze kumuachia nyota huyo mwenye umri wa miaka 24. Napoli walichukizwa na Koulibaly kufuatia madai aliyotoa kuwa yuko tayari kuzungumza na Chelsea. Beki huyo amesema hajazungumza na Antonio Conte lakini anadhani hilo litafanyika hivi karibuni.

NOLITO ANUKIA MAN CITY.

KLABU ya Manchester City, inadaiwa kukaribia kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Hispania, Nolito kutoka Celta Vigo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 amethaminishwa kwa kiasi cha euro milioni 18 katika mkataba wake, na rais wa Celta Vigo Carlos Mourino tayari ameshadokeza kuwa anategemea ataondoka kiangazi hiki. Taarifa zilizotolewa na gazeti la Gurdian la Uingereza zimedai kuwa City wana uhakika wa kukamilisha dili hilo na kuongeza kuwa Nolito tayari ameshakubali mambo binafsi katika mkataba wa miaka mitatu atakaopewa wenye thamani ya euro milioni nne kila msimu. Mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona, ambaye amecheza katika mechi zote tatu za Hispania katika michuano ya Ulaya inayoendelea nchini Ufaransa, amekuwa pia akihusishwa na tetesi za kurejea Camp Nou. Nolito ambaye atafikisha miaka 30 Octoba mwaka huu, aliondoka Barcelona na kwenda Benfica mwaka 2011 kabla ya kujiunga na Celta Vigo miaka miwili baadae.

MADRID YATHIBITISHA KUMREJESHA MORATA.

KLABU ya Real Madrid imethibitisha kuwa Alvaro Morata atarejea Santiago Bernabeu kipindi hiki cha kiangazi. Taarifa hizo zimekuwa mapema baada ya mkurugenzi mtendaji wa Juventus Beppe Marotta kubainisha kuwa Morata anategemewa kurejea Madrid. Madrid walikuwa na nafasi ya upendeleo ya kumnunua tena Morata mwenye umri wa miaka 23, ikiwa ni sehemu ya mkataba uliopelekea nyota huyo wa kimataifa wa Hispania kujiunga na Juventus miaka miwili iliyopita na sasa wamethibitisha kufanya hivyo. Katika taarifa yao iliyotumwa katika mtandao, Madrid walithibitisha taarifa hiyo na kudai kuwa Morata atajiunga na mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya wa La Liga chini ya meneja Zinedine Zidane. Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa Madrid wanaweza kumuuza Morata kwa klabu nyingine ili wapate faida.

CHELSEA YAPANIA KUNASA SAINI YA BEKI WA NAPOLI.

KLABU ya Chelsea inadaiwa kuanza kumuwania beki wa Napoli Kalidou Koulibaly kwa kutoa ofa ya paundi milioni 19.2. Chelsea wamekuwa wakimhusudu kwa kiasi kikubwa beki huyo wa kimataifa wa Senegal, ambaye ameingia katika mzozo na klabu yake kuhusiana na uhamisho wake. Hata hivyo, ofa hiyo ya Chelsea tayari imeshakataliwa na Napoli wamedai wanataka kitita cha paundi milioni 30 ili waweze kumuachia nyota huyo mwenye umri wa miaka 24. Napoli walichukizwa na Koulibaly kufuatia madai aliyotoa kuwa yuko tayari kuzungumza na Chelsea. Beki huyo amesema hajazungumza na Antonio Conte lakini anadhani hilo litafanyika hivi karibuni.

PAUL CLEMENT KUWA MSAIDIZI WA ANCELOTTI BAYERN.

KLABU ya Bayern Munich, imemteua Paul Clement kuwa meneja msaidizi wa timu hiyo. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 ataungana bosi wake wa zamani Muitaliano Carlo Ancelotti katika benchi la ufundi la klabu hiyo, wakiwa wameshawahi kufanya kazi pamoja katika klabu za Chelsea, Paris Saint-Germain na Real Madrid. Clement aliteuliwa kuwa kocha wa Derby Count Juni mwaka 2015 kufuatia Ancelotti kutimuliwa Madrid lakini alitimuliwa na timu hiyo Februari mwaka huu wakati wakishika nafasi ya tano katika Ligi ya Ubingwa. Kocha huyo Muingerza ataanza kufanya kazi pindi mabingwa hao wa Bundesliga na Kombe la Ujerumani watakaporejea katika mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya katika kipindi cha wiki tatu zijazo.

CHAMPIONSHIP 2016-2017: DI MATTEO KUANZA NA DERBY YA BIRMINGHAM, BENITEZ KUKWAANA NA FULHAM.

KLABU ya Newcastle United chini ya Rafa Benitez inatarajiwa kuanza maisha mapya katika Ligi ya Ubingwa kwa kusafiri kuifuata Fulham katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo msimu wa 2016-2017. Newcastle wanataka kurejea haraka katika Ligi Kuu kufuatia kushushwa kutoka huko msimu uliopita. Mchezaji wa kwanza wa Newcastle watakaochezwa nyumbani katika ligi hiyo utakuwa dhidi ya Huddersfield Town Agosti 13 mwaka huu. Nayo Aston Villa mchezo wa kwanza toka washushwe daraja utakuwa dhidi ya Sheffield Wadnesday huko Hillsborough. Villa ambao watakuwa chini ya meneja wao mpya Roberto Di Matteo watavaana na Birmingham ambao ni mahasimu wao kutoka mji mmoja Octoba 29 mwaka huu huko St.Andrews huku marudiano yakitarajiwa kuwa Aprili 22 mwakani. Norwich City, ambao walijiunga na Newcastle na Villa katika timu zilizoshuka daraja msimu uliopita, wao wataanza kampeni zao kwa kupambana na Blackburn Rovers.

COPA AMERICA 2016: ARGENTINA YATINGA FAINALI KWA KISHINDO, MESSI AVUNJA REKODI.MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi amekuwa mfungaji anayeongoza kwa nchi hiyo baada ya kuibamiza Marekani kwa mabao 4-0 na kutinga fainali ya michuano ya Copa America mapema leo. Nyota huyo wa Barcelona mwenye umri wa miaka 28, aliipita rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa Argentina Gabriel Batistuta ya mabao 54, kwa bao murua la mpira wa adhabu alilofunga katika mchezo huo. Mbali na kufunga bao hilo Messi pia alitoa pasi ya bao la kuongoza lililofungwa na Ezequiel Lavezzi huku mengine mengine mawili yakifungwa na Gonzalo Higuain. Akihojiwa Messi ambaye Ijumaa hii anatimiza miaka 29, amesema amefurahi kuifikia na kuipita rekodi ya Batistuta na kuwashukuru wachezaji wenzake kwakuwa wanastahili pia kutokana na mchango wao. Argentina sasa wanatarajiwa kucheza na aidha Colombia au mabingwa watetezi Chile ambao watapambana Afajiri ya kesho huko Chicago.

Monday, June 20, 2016

AWEKA REKODI YA KUWA MCHEZAJI MWENYE UMRI MKUBWA ZAIDI KUFUNGA BAO JAPAN.

MCHEZAJI soka wa Japan, Kazuyoshi Miura amevunja rekodi yake mwenyewe ya kuwa mchezaji mzee zaidi kufunga bao katika ligi ya nchi hiyo. Miura alifunga bao katika dakika ya 22 ya mchezo wa ligi daraja la pili lakini timu yake ya Fc Yokohama ilifungwa mabao 2-1 na Fc Gifu katika mchezo huo. Mchezaji huyo amefunga bao hilo akiwa amefikisha umri wa miaka 49, miezi mitatu na siku 24, akivunja rekodi yake mwenyewe aliyoweka mwaka jana. Mshambuliaji huyo kwasasa amecheza misimu 31 ya soka baada ya kusaini mkataba mpya wa nyongeza Novemba mwaka jana. Miura amefunga mabao 55 katika mechi 89 alizoichezea Japan baada ya kuitwa katika kikosi hicho kwa mara ya kwanza mwaka 1990 lakini hakuwahi kushiriki fainali zozote za Kombe la Dunia. Anayeshikilia rekodi ya mchezaji mzee zaidi kufunga bao katika Ligi Kuu ya Japan maarufu kama J-League ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo Zico ambaye alifunga bao akiwa na timu ya Kashima Antlers akiwa na umri wa miaka 41 mwaka 1994.

SPURS YAKUBALI KUTOA PAUNDI MILIONI 11 KWA AJILI YA WANYAMA.

KLABU ya Tottenham Hotspurs inadaiwa kukubali kutoa ada ya paundi milioni 11 ka ajili ya kumnasa kiungo wa Southampton Victor Wanyama. Inadaiwa kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Kenya mwenye umri wa miaka 24, ambaye alijiunga na Southampton kwa kitita cha paundi milioni 12.5 kutokea Celtic Julaia mwaka 2013, anafanyiwa vipimo vya afya katika klabu hiyo White Hart Lane. Uhamisho huo utamfanya Wanyama kuungana na kocha wake wa zamani ambaye ndio aliyemtoa Celtic Mauricio Pochettino. Wanyama aliomba kuondoka kiangazi mwaka jana baada ya Tottenham Hotspurs kuonyesha nia ya kumtaka lakini alibakia St. Mary’s na kuisaidia Southampton kumaliza katika nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu.

WENGER KUSAJILI WATATU TU KIANGAZI.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema hataweza kununua wachezaji zaidi ya watatu katika kipindi cha usajili wa kiangazi kwani inaweza kukiyumbisha kikosi chake. Klabu hiyo mpaka sasa tayari wamemsajili kiungo Granit Xhaka kutoka Borussia Monchengladbach na Wenger alikuwa na matumaini ya kumfanya Jamie Vardy kuwa usajili wake wa pili katika kipindi hiki. Lakini akihojiwa hivi karibuni Wenger alidai kuwa anategemea mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uingereza kukataa ofa yao na kuamuai kubakia Leicester City. Katika mahojiano hayohayo, Wenger alieleza mikakati yake kuwa hana kufanya mabadiliko makubwa sana katika kikosi chake lakini bado anaangalia baadhi ya wachezaji ambao ataweza kuwanunua. Wenger amesema baada ya kupata kiungo Xhaka bado wataendelea kutafuta wachezaji wengine mmoja au wawili lakini haitakuwa kazi rahisi.

SHABIKI WA RONALDO AIPONZA URENO.

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limetangaza kuwa shabiki wa Ureno aliyeingia uwanjani na kwenda kupiga picha na Cristiano Ronaldo anaweza kulipnza Shirikisho la Soka la nchi hiyo kutozwa faini. UEFA imedai kuwa imefungua kesi ya kinidhamu dhidi ya shirikisho hilo kwa kosa la uvamizi wa uwanja. UEFA huwa inazichukulia hatua timu za taifa ambazo zinashindwa kuwadhibiti mashabiki wake uwanjani. Katika tkio hlo shabiki mmoja alikimbia uwanjani katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana kati ya Ureno na Austria Jumamosi iliyopita, kabla ya Ronaldo kuwapa ishara ya kuamuacha kwa watu wa usalama waliojaribu kumzuia.

INTER YAPANIA KUMNASA YAYA TOURE.

KLABU ya Inter Milan imepania kumsajili kiungo mkongwe wa kimataifa wa Ivory Coast na klabu ya Manchester City Yaya Toure. Toure mwenye umri wa miaka 33, kwasasa amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake kwenye klabu hiyo yenye maskani yake katika Uwanja wa Etihad. Kiungo huyo aliuzwa kwa City wakati huyo ikiongozwa na meneja wa sasa wa Inter Milan Roberto Mancini, kwa kitita cha paundi milioni 24 na Pep Guardiola mwaka 2010 wakati wawili hao walipokuwa wote Barcelona. Hakuna makubaliano yeyote yaliyoafikiwa lakini tetesi zinadai kuwa kuna nafasi ya asilimia 50 kama usajili utafanyika.

CAVALIERS WAWEKA HISTORIA NBA.TIMU ya Cleveland Cavaliers imekuwa ya kwanza kubadili matokeo wakitokea nyuma kwa kufungwa 3-1 na kushinda taji la Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani NBA kwa kuichapa Golden State Warriors. Nyota wa Cavaliers, LeBron James ndio aliyekuwa nyota katika mchezo huo wa saba wa fainali akifunga alama 27, kusaidia zingine 11 na kuokoa mara 11. Akihojiwa James ambaye aliahidi kuwakata kiu mashabiki wa Cavaliers ambao kwa kipindi kirefu walikuwa hawajatwaa taji hilo, amesema alijitoa kwa kila kitu na anashukuru ahadi yake aliyotoa miaka miwili iliyopita imetimia.  Naye kocha wa Cavaliers, Tyronn Lue ambaye alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo Januari baada ya kutimuliwa kwa David Blatt amesema wameweka historia ya kipekee kwa kupeleka taji hilo katika ardhi ya mji wa Cleveland baada ya kupita kipindi kirefu cha miaka 52. Katika mchezo huo ulioshuhudiwa na mamilioni ya watu duniani kote akiwemo rais wa Marekani Barack Obama, James aliteuliwa kuwa mchezaji bora wa fainali hizo ikiwa ni mara ya tatu kutwaa tuzo hiyo baada ya kuitwaa mara mbili akiwa na timu ya Miami Heat. Obama aliutizama mchezo huo akiwa katika ndege yake ya Air Force One na ilimbidi asubiri mchezo umalizike ndio ashuke na kuendelea na shughuli nyingine pindi walipowasili jijini Calfornia akiwa na familia yake.

Sunday, June 19, 2016

WENGER AKATA TAMAA NA VARDY.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri Jamie Vardy anajipanga kukaa uhamisho wa kwenda katika klabu hiyo ili aweze kubakia Leicester City. Mshambuliaji huyo ambaye alitwaa taji la Ligi Kuu akiwa na Leicester msimu uliopita, mustakabali wake umekuwa ukijadiliwa sana baada ya Arsenal kutenga paundi milioni 20 ambazo zingeweza kutengua mkataba wake. Vardy mwenyewe alikataa kufanya uamuzi wowote wa uhamisho kwenda Emirates mpaka baada ya kumalizika kwa michuano ya Ulaya ili aweze kujipa muda wa kuweka mkazo katika michuano hiyo akiwa na Uingereza. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo, Wenger amesema Vardy bado ni mchezaji wa Leicester na anadhani ataamua kubakia katika klabu yake kwa msimu ujao.

RONALDO AWATAKA WACHEZAJI WENZAKE KUTOKATA TAMAA.

MSHAMBULIAJI nyota na nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo amesisitiza kuwa hawapaswi kukata tamaa ya kutinga hatua ya 16 bora pamoja na sare mbili walizopata katika mechi zao zilizopita. Kauli ya Ronaldo imekuja kufuatia sare ya bila kufungana walipata dhidi ya Austria huku nyota huyo akikosa penati. Pamoja na kuanza kwao taratibu Ronaldo amewataka wachezaji wenzake kutokukata tamaa kwani bado wana uwezo wa kutinga hatua ya mtoano. Ronaldo ambaye amefikia rekodi ya Luis Figo ya kucheza mechi nyingi za kimataifa, amesema matokeo dhidi ya Austria walikuwa hawayahitaji lakini huo ndio mchezo wa soka sio siku zote utaweza kushinda. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa walitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini bahati haikuwa kwao hivyo jambo muhimu ni kuendelea kuamini kuwa wanaweza kufanya vizuri na kusonga mbele. Hungary ndio wanaoongoza kundi F wakiwa na alama nne, Iceland wanashikilia nafasi ya pili wakiwa na alama mbili, Ureno wa tatu wakiwa pia na alama mbili lakini wakitofautiana mabao na Austria ndio wanashikilia mkia kwenye hilo wakiwa na alama moja. Ureno wanatarajiwa kucheza na Hungary Jumanne ijayo jijini Lyon wakati Iceland wakipepetana na Austria siku hiyohiyo huko Stade de France.