Friday, November 28, 2014

RODRIGUEZ, DI MARIA, SCHWEINSTEIGER WAONGOZA ORODHA YA VIUNGO WATEULE KATIKA KIKOSI CHA FIFPro WORLD XI 2014.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetoa orodha ya wachezaji nafasi ya kati 15 ambao watapigiwa kura kwa ajili ya uchaguzi wa kikosi cha dunia ambapo majina matatu pekee ndio yatashinda nafasi hiyo. Kikosi hicho kinachojulikana kama World XI 2014, ambacho huteuliwa kwa kura za wachezaji duniani kote kinatarajiwa kutangazwa rasmi katika sherehe za utoaji tuzo ya Ballon d’Or Januari 12 mwakani. Wote waliojumuishwa katika orodha hiyo ni nyota waliokuwemo katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil akiwemo mfungaji bora James Rodriquez wa Colombia pamoja na Angel Di Maria ambaye timu yake ya Argentina ilishika nafasi ya pili pamoja na Bastian Schweinsteiger anaewawakilisha mabingwa wa dunia Ujerumani. Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wao wanatarajiwa kuwemo katika orodha ya washambuliaji ambayo itatolewa Desemba mosi mwaka huu, wakati wateule wa nafasi ya golikipa na mabeki wao wakiwa tayari wameshatangazwa. Orodha kamili ya wachezaji hao na timu zao ni pamoja na Xabi Alonso (Bayern Munich), Angel Di Maria (Manchester United), Cesc Fabregas (Chelsea), Eden Hazard (Chelsea), Xavi (Barcelona), Andres Iniesta (Barcelona), Toni Kroos (Real Madrid), Luka Modric (Real Madrid), Mesut Ozil (Arsenal), Andrea Pirlo (IJuventus), Paul Pogba (Juventus), James Rodriguez (Real Madrid), Bastian Schweinsteiger (Bayern Munich), Yaya Toure (Manchester City), Arturo Vidal (Juventus)

GALATASARAY YAMCHUKUA HAMZAOGLU KUZIBA NAFASI YA PRANDELLI.

KLABU kongwe jijini Instabul ya Galatasaray wanatarajia kumteua kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uturuki Hamza Hamzaoglu kuwa meneja mpya wa klabu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Muitaliano Cesare Prandelli. Klabu hiyo ilimtimua Prandelli baada ya kuitumikia chini ya nusu ya msimu kutokana na matokeo mabovu ambayo wamekuwa wakipata. Hamzaoglu amekuwa akiitumikia Uturuki chini ya kocha mkuu Fatih Terim toka mwaka 2013, na uamuzi wake huo umekuja baada ya kufanya mazungumzo na kocha huyo. Bodi ya klabu hiyo ilifikia uamuzi wa kumtimua Prandelli baada ya kutandikwa na Anderlecht kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano usiku na kufuta matumaini yao ya kufuzu hatua ya mtoano. Prandelli alitua katika klabu hiyo Julai mwaka huu akichukua nafasi ya Muitaliano mwenzake Roberto Mancini na kupewa mkataba wa miaka miwili uliokuwa na thamani ya euro milioni 2.3.

CONFEDERATION CUP FAINAL 2014: SEWE SPORT KUONYESHANA KAZI NA AL-AHLY.

KLABU ya Al-Ahly inatarajia kujitupa uwanjani mwishoni mwa wiki hii katika mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya klabu ya Sewe Sport ya Ivory Coast. Al-Alhy itaingia katika mchezo huo kutafuta ushindi kwa udi na uvumba ili kurejesha heshima ya soka la Misri ambalo katika siku za karibuni linaonekana kuporomoka. Sewe Sport itaikaribisha Al-Ahly katika mchezo wa mkondo wa kwanza utakaofanyika jijini Abdijan kesho huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kuchezwa Desemba 6 jijini Cairo. Baada ya miongo kadhaa ya mafanikio katika soka kwa timu ya taifa na ngazi ya vilabu, mwaka huu umekuwa sio mzuri kwa nchi hiyo baada ya kushuhudia timu ya taifa ikishindwa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika na vilabu kushindwa kutamba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

ROY KEANE AACHIA NGAZI ASTON VILLA.

KLABU ya Aston Villa imetangaza kuwa Roy Keane amejiuzulu wadhifa wake wa kocha wa msaidizi wa timu hiyo. Mapema Keane alikaririwa akidai kuwa anapata tabu kuhudumia vibarua viwili alivyokuwa navyo. Keane ambaye pia ni kocha msaidizi wa Ireland amesema sio haki kwa pande zote mbili, hivyo anatakiwa kufanya uamuzi wa kuchagua kibarua kimoja. Kocha wa Villa Paul Lambert alithibitisha asubuhi ya leo kuwa taarifa hizo na kudai kuwa ana heshimu uamuzi uliochukuliwa.

MOYES AMTEUA MCKINLAY KUWA MSAIDIZI WAKE REAL SOCIEDAD.

MENEJA wa klabu ya Real Sociedad, David Moyes amemteua Billy McKinlay kuwa msaidizi wake. Mckinlay ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Scotland amekuwa hana kibarua toka atimuliwe na klabu ya Watford baada ya kusimamia mechi mbili pekee. Moyes sasa ameamua kumchukua Mckinlay amsaidie katika benchi lake la ufundi baada ya kuiongoza Sociedad kupata sare ya bila kufungana katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Deportivo La Coruna. Ijumaa hii Moyes anakabiliwa na kibarua kingine pale Sociedad itakapoikaribisha Elche katika mchezo wake wa kwanza akiwa katika uwanja wa nyumbani.

SIDHANI KAMA ARSENAL WANANIHITAJI TENA - KLOPP.

MENEJA wa klabu ya Brussia Dortmund, Jurgen Klopp ametania kuwa mashabiki wa Arsenal hawatamuhitaji tena baada ya kuona timu yake ikitandikwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi. Klopp amekuwa akihusishwa na tetesi za kuchukua mikoba ya kionoa Arsenal katika wiki kadhaa zilizopita baada ya kuzuka msukumo kwa Arsene Wenger kufuatia kuanza vibaya msimu wa Ligi Kuu. Kocha huyo amekiri hivi karibuni kuwa anadhani anaweza kumudu kuhamia katika Ligi Kuu kama akiamua kuondoka Dortmund lakini sasa anadhani nafasi yake ya kutua Arsenal imetoweka. Akihojiwa Klopp amesema hafikirii baada ya kiwango cha Dortmund walichokionyesha katika Uwanja wa Emirates kama mashabiki wa Arsenal watamuhitaji. Klopp aliteuliwa kuwa kocha wa Dortmund kuanzia mwaka 2008 na kuisaidia timu hiyo kushinda mataji mawili ya Bundesliga, Kombe la Ujerumani, Supercup na kutinga fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Thursday, November 27, 2014

VERMAELEN KUKAA NJE YA UWANJA MIEZI MITANO.

BEKI wa Barcelona, Thomas Vermaelen anatarajiwa kufanyiwa upasuaji ili kurekebisha tatizo la paja linalomsumbua wiki ijayo na anategemewa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi minne mpaka mitano. Beki huyo wa kati wa kimataifa wa Ubelgiji ambaye alipata majeruhi hayo wakati akiitumikia nchi yake katika mchezo dhidi ya Urusi katika Kombe la Dunia Juni mwaka huu mpaka hajacheza mechi yeyote ya mashindani toka ajiunge na timu hiyo akitokea Arsenal Agosti. Usajili huo umekuwa jambo lililoifedhehesha bodi ya klabu hiyo. Vermaelen mwenye umri wa miaka 29 amekuwa akisummbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara toka alipokuwa Arsenal ambapo amecheza mechi 21 pekee msimu uliopita akiwa na washika bunduki hao wa London.

HALI YA PELE YAENDELEA KUIMARIKA.

AFYA ya nguli wa soka wa Brazil, Pele inaendelea kuimarika lakini bado ameendelea kuwa chini ya uangalizi maalumu katika hospitali jijini Sao Paulo ambako alilazwa siku tatu zilizopita kutokana na kupata maambukizi katika njia ya mkojo. Katika taarifa iliyotolewa na hospitali hiyo ya Albert Einstein imedai kuwa hali ya nguli huyo inaendelea kuimarika pamoja na kuwa bado amewekwa katika wodi ya wagonjwa mahututi. Mapema baada ya kuthibitika kuwa Pele alipelekwa hospitali Jumatatu iliyopita, hospitali hiyo ilidai kuwa vipimo alivyofanyiwa vimeonyesha kuwa alipata maambukizi katika njia ya mkojo. Wakala wake Jose Fornos alidai kuwa mteja wake alichoka baada ya kupokea wageni wengi na kuongeza kuwa Pele anaweza kupokea matibabu yanayoweza kuchukua zaidi ya miezi mitatu. Pele alifanyiwa upasuaji kuondoa mawe katika figo Novemba 13 mwaka huu na alionekana kuwa katika hali nzuri aliporuhusiwa siku mbili baadae kwa kufungua dirisha lake na kuwapungia mkono mashabiki ambao walikusanyika hospitali.

EVERTON, SPURS ZUFUZU EUROPA LEAGUE.

KLABU za Ligi Kuu nchini Uingereza Everton na Tottenham Hotspurs zimefanikiwa kufuzu hatua ya mtoano ya michuano ya Europa League jana huku Celtic nao wakifuata nyayo hizo pamoja na kufungwa na Salzburg nyumbani. Everton wao walisonga mbele katika hatua ya timu 32 bora wakiwa kama vinara wa kundi H baada ya kuitandika mabao 2-0 VfL Wolfsburg katika mchezo uliochezwa nchini Ujerumani. Tottenham wao walisonga mbele katika kundi C kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 nyumbani kwa vinara wa Ligi Kuu ya Israel Partizan Belgrade huku Celtic wao pamoja na kufungwa mabao 3-1 na Salzburg jijini Glascow lakini wanasonga mbele huku wakiwa wamebakiwa na mchezo mmoja mkononi. Timu zingine zilizofuzu jana ni Dinamo Moscow ambao waliwatandika Panathinaikos kwa mabao 2-1 na kujihakikishia nafasi yao katika kundi E huku Inter Milan nao wakisonga mbele katika kundi F kwa kuifunga Dnipro kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa san Siro. Wengine ni Napoli ambao sare ya bila ya kufungana dhidi ya Sparta Prague katika kundi I ilitosha kuwavusha huku Fayenoord, Dynamo Kiev na Trabzonspor nazo zikifuzu baada ya kushinda michezo yao.

MMILIKI WA WIGAN MATATANI KWA KUKASHIFU.

MMILIKI wa klabu ya Wigan Athletic, Dave Whelan ameshitakiwa na Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwa kuwatukana watu wenye asili ya Kiyahudi na Kichina wakati akifanya mahojiano na gazeti. Katika taarifa yake FA inatuhumu Whelan kwa kufunja sheria za chama hizo kwa kutoa kauli hiyo kuudhi. FA iliendelea kudai kuwa inampa Whelan mpaka Desemba 5 kuwa amejibu tuhuma hizo kabla ya hatua zaidi hazijaendelea kuchukuliwa. Katika mahojiano yake na gazeti la Guardian baada ya kumtangaza kocha mpya Malky Mackay Whelan alikaririwa akidai kuwa watu kutoka China wana upeo mdogo huku akiwaambia Wayahudi kuwa wanapenda hela. Kiongozi wa jamii wa Wachina Jenny Wong alilaani vikali kauli hiyo ya Whelan huku kiongozi wa jamii ya Kiyahudi naye akidai kuwa kuomba radhi pekee kutokana na kauli yake hiyo haitoshi.

NYOTA WA ZAMANI WA KIMATAIFA WA NIGERIA AAGA DUNIA.

SHIRIKISHO la Soka la Nigeria-NFF limejiunga na waombolezaji wengine kufuatia kifo cha mchezaji wa zamani wa kimataifa wa nchi hiyo, Yomi Peters. Peters alifariki dunia hospitalini jijini Lagos juzi akiwa na umri wa miaka 74 baada ya kuugua saratani kwa kipindi kirefu. Katibu Mkuu wa NFF, Musa Ahmadu katika salamu zake za rambirambi amemuelezea Peters kama mmoja wa wanasoka aliyejituma zaidi enzi zake. Ahmadu amesema mashabiki wa soka ambao walimuona Peters enzi zake wakati aisakata kabumbu watakubaliana naye kuwa aliitumikia nchi yake kwa moyo wakati wote ambao alikuwa kivaa jezi za timu ya taifa.

EVERTON KUMUACHA ATSU.

KLABU ya Everton inafikiria uwezekano wa kumrejesha winga wa kimataifa wa Ghana Christian Atsu katika klabu yake ya Chelsea katika kipindi cha dirisha dogo la usajili Januari mwakani. Klabu hiyo ilipambana vikali kuhakikisha inampata winga huyo kwa mkopo katika majira ya kiangazi lakini ameshindwa kung’aa Goodison Park hivyo kuifanya timu hiyo kufikiria kumuachia. Atsu mwenye umri wa miaka 22 amefanikiwa kuanza katika mechi moja pekee katika Ligi Kuu toka ajiunge na Everton. Kuna taarifa kwamba Everton imeshaanza kutafuta mbadala wa Atsu kwa kutaka kumsajili Shaun Maloney kutoka klabu ya Wigan Athletic.

KIZUNGUMKUTI CHA MICHUANO YA CHELENJI CHAMUUMIZA KICHWA KOCHA WA RWANDA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Rwanda, Stephen Contantine ameonyesha wasiwasi kuwa kukosekana kwa michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Michezo Afrika Mashariki na Kati-Cecafa, inaweza kuathiri maandalizi yao ya michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani-Chan. Rwanda inatarajiwa kuandaa michuano ya CHAN mwaka 2016 na kocha huyo Mwingereza alikuwa amepanga kuitumia michuano hiyo kama kipimo kwa wachezaji wake. Wiki tatu zilizopita Ethiopia ilijitoa kuwa wenyeji wa michuano yeyote ya ndani na kimataifa ikiwemo ushiriki wa timu yao ya taifa katika michuano ya Mataifa ya Afrika na ligi inayoendelea nchini mwao. Katibu Mkuu wa Cecafa Nicholas Musonye ana matumaini kuwa makubaliano yatafikiwa na Sudan kuwa wenyeji wapya wa michuano hiyo. Nchi 14 zilizopo katika ukanda wa Cecafa zikiwemo Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, mabingwa watetezi Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda, Zanzibar na nchi mbili waalikwa zinategemewa kushiriki michuano ya mwaka huu.

WENGER AWAKATA VILIMILIMI WANAOMKOSOA.

KLABU ya Arsenal jana imefanikiwa kuitandika Borussia Dortmund na kufuzu hatua ya mtoano ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mabao yaliyofungwa na Yaya Sanogo katika ya pili ya mchezo na Alexis Senchez katika dakika ya 57 yalitosha kuihakikishia Arsenal ushindi katika uwanja wake wa Emirates. Arsenal sasa wamejiunga Dortmund ambayo walikuwa tayari wamefuzu kutoka kundi D jana usiku ambapo pia tulishuhudia Atletico Madrid na Bayer Leverkusen nao wakifuzu hatua hiyo. Kwa upande wa Liverpool wao wana kibarua kigumu cha kujihakikishia nafasi yao katika mchezo wa mwisho dhidi ya FC Basel Uswis baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Ludogorets ya Bulgaria. Real Madrid ndio timu pekee katika michuano hiyo ambayo haijapoteza mchezo kwa kujikusanyia jumla ya alama 15 baada ya kuifunga Basle kwa bao 1-0 jana lililofungwa na Cristiano Ronaldo. Barcelona, Bayern Munich, Paris saint-Germain, Chelsea, Porto na Shakhtar Donetsk ndio timu zingine zilizofuzu kutoka katika kundi E na H hivyo kuacha nafasi tano wazi kabla ya mechi za mwisho za makundi zitakazofanyika Desemba 9 na 10 mwaka huu.

Wednesday, November 26, 2014

CAF NA ADIDAS ZAZINDUA MPYA MAHSUSI WA MARHABA KWA AJILI YA MICHUANO YA AFCON MWAKANI.

SHIRIKISHO la Soka la Afrika-CAF na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas wametoa mpira wa Marhaba kuwa maalumu kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon itakayofanyika huko Guinea ya Ikweta mwakani. Mpira huo unatarajiwa kutambulishwa rasmi Desemba 3 mwaka huu katika shughuli za upangaji ratiba za michuano hiyo ambazo zitakazofanyika jijini Malabo. Mpira huo umebuniwa kwa rangi za aina mbalimbali ambazo zinawakilisha uwanda mpana wa bara la Afrika kuanzia jangwa la sahara, rangi ya ang’avu ya samawati katika anga la bahari ya Hindi na Atlantic. Mpira huo wa Marhaba umefanyiwa vipimo vyote stahiki na kuthibitishwa kuwa unaweza kutumika katika hali yeyote katika michuano hiyo.

BAYERN KUMUACHA SHAQIRI.

RAIS wa heshima wa klabu ya Bayern Munich, Franz Beckenbauer amedokeza kuwa timu hiyo inaweza kumuacha Xherdan Shaqiri katika dirisha dogo la usajili Januari mwakani. Shaqiri mwenye umri wa miaka 23 ameanza katika mechi tatu pekee za Bundesliga msimu huu huku akitokea benchi katika mechi nne za Ligi ya Mabingwa Ulaya alizocheza. Nyota huyo wa kimataifa wa Switzerland ameendelea kukosa muda wa kucheza hatua ambayo imezusha tetesi juu ya mustakabali wake na Beckernbauer anategemea Shaqiri kutafuta klabu mpya pindi dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa. Beckenbauer mwenye umri wa miaka 69 amesema Bayern tayari wameshaonyesha dalili za kutohitaji huduma ya mchezaji huyo hivyo anadhani anaweza kuondoka katika mapumziko ya majira ya baridi.

BARCELONA, MADRID, BAYERN WATAWALA ORODHA YA MABEKI WA FIFPro WORLD XI 2014.

KLABU za Barcelona, Real Madrid na Bayern Munich zimetawala orodha ya mabeki wateule katika kikosi cha dunia cha FIFPro World XI 2014, baada majina 12 ya wachezaji wao kuingia katika orodha kati ya majina 20 yaliyoteuliwa. Wachezaji wote wanne walioshinda nafasi ya kuwemo katika kikosi hicho mwaka jana wamejumuishwa wakiwemo Dani Alves, Philipp Lahm, Sergio Ramos na Thiago Silva. Leighton Baines, Ashley Cole, Dante na Nemanja Vidic ndio ambayo hayamo katika orodha hiyo ukilinganisha na ya mwaka jana. Kwa upande wa Madrid wamo Dani Carvajal, Pepe, Ramos, Raphael Varane na Marcelo wakati Barcelona wamo Jordi Alba, Alves, Javier Marscherano na Gerard Pique huku Bayern wakiwa na David Alaba, Lahm na Jerome Boateng. Mabeki wengine wnakamilisha orodha hiyo ni pamoja na David Luiz na Thiago Silva wa Paris Saint-Germain, Pablo Zabaleta na Vincent Kompany wa Manchester City, Branislav Ivanovic na Filipe Luis wa Chelsea, Diego Godin wa Atletico Madrid na Mats Hummels wa Borussia Dortmund. Majina manne ya washindi wa beki bora wa dunia yataamuliwa kwa kupiga kura miongoni mwa wachezaji ambapo zaidi ya wachezaji wa kulipwa 20,000 wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo.

MADRID VS BARCELONA NDIO MECHI GHALI ZAIDI DUNIANI.

GAZETI moja la michezo limetoa orodha ya mechi ambazo timu zilichezesha wachezaji ghali zaidi kutokana na ada walizosajiliwa. Gazeti hilo la CIES limekuwa likiangazia ligi tano kubwa duniani katika kutoa orodha hiyo toka mwaka 2009. Mechi ya Real Madrid na Barcelona ndio ambayo imeongoza kwa kuchezesha wachezaji wengi ghali ambapo kwa ujumla wake wachezaji waliocheza walikuwa na thamani ya euro milioni 690. Katika mechi zingine zilizokutanisha wachezaji ghali ni Manchester City na Chelsea ambao kwa pamoja walikuwa na wachezaji wenye thamani ya euro milioni 578, wakifuatiwa na Paris Saint-Germain na Marseille euro milioni 503. Mechi zingine ni Bayern Munich na Borussia Dortmund euro milioni 272 na Inter Milan na Napoli euro milioni 263.

MENEJA WA ROMA AJIPA MOYO BAADA YA SARE DHIDI YA CSKA.

MENEJA wa klabu ya AS Roma, Rudi Garcia amesema kikosi chake kilifanya kazi ya kutosha kuhakikisha wanapata na ushindi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya CSKA Moscow jana. Bao la kusawazisha lililofungwa na Vasili Berezutski alilofunga dakika za majeruhi lilitosha kufanya timu hizo kugawana alama kwa kufungana bao 1-1 hivyo kuweka hai matumaini yao ya kusonga mbele katika mechi zao mwisho za makundi. Garcia amesema alikuwa amefikiria tayari wameshinda mchezo huo lakini wakajikuta wakiruhusu bao katika sekunde 15 za mwisho. Huku Bayern Munich wakiwa tayari wameshatinga hatua ya timu mtoano, Roma wako katika nafasi nzuri ya kuungana nao wakijua kuwa ushindi dhidi ya Manchester City nyumbani utatosha kuwawezesha kufuzu.

BERAHINO AKAMATWA AKIENDESHA AKIWA AMELEWA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya West Bromwich Albion Saido Berahino anatarajiwa kuhojiwa baada ya kukamatwa akiendesha gari huku amelewa. Mchezaji huyo mzaliwa wa Burundi mwenye umri wa miaka 21 alikamatwa kwa kuendesha mwendo kasi huko Lymm, Cheshire. Berahino alifunga bao katika sare ya mabao 2-2 iliyopata Southampton dhidi ya Manchester United. Nyota huyo anatarajiwa kurejea tena kituo cha polisi cha Cheshire kwa mahojiano zaidi Desemba baada ya kuachiwa kwa dhamana.

ZIAYA FITI KUCHEZA KLABU BINGWA YA DUNIA - SETIF.

MABINGWA wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ES Setif wametangaza kuwa mshambuliaji Abdelmalek Ziaya anatarajiwa kuwa fiti kwa ajili ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia. Ziaya alipata majeruhi wakati wa mchezo wa fainali ya michuano hiyo dhidi ya AS Vita ya DR Congo mapema mwezi huu. Katika taarifa yake Setif walithibitisha nyota wao huyo kuanza mazoezi jana na kwamba yuko fiti kwa ajili ya mechi za mashindano. Michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia inatarajiwa kuanza kutimua vumbi mapema mwakani nchini Morocco.

WEZI WAMKOMBA KILA KITU WANYAMA.

MAOFISA wa polisi nchini Uingereza wanachunguza tukio la wizi lililomtokea mchezaji wa klabu ya Southampton Victor Wanyama. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Kenya aliibiwa nyumbani vitu kadhaa vikiwemo fulana ya kiungo wa Barcelona Lionel Messi, nguo za wanamitindo mbalimbali na jozi 20 za viatu. Mbali na hivyo pia aliibiwa gari lake la kifahari aina ya Land Rover lenye thamani ya shilingi milioni 8.4 kwa fedha za Kenya, fanicha, luninga pamoja na vifaa vingine vya kielektroniki. Polisi wanashangazwa na hatua kwamba majirahi wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 hawakusikia kelele zozote za uvunjaji huo.

KOMPANY AMMWAGIA MISIFA AGUERO BAADA YA KUIOKOA CITY.

NAHODHA wa klabu ya Manchester City, Vincent Kompany amesema Sergio Agueri ni mchezaji wa kipekee ambaye anaweza kufanya jambo lisilowezekana likawezekana. Aguero mwenye umri wa miaka 26 alifunga mabao matatu yaliyoihakikishia ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Bayern Munich waliocheza pungufu ya mtu mmoja jana na kufufua matumaini yao ya kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kompany amesema Aguaero anafanya vitu visivyowezekana vifanikiwe na hilo ni jambo muhimu kwa mchezaji wa kiwango chake. Mbali na Kompany naye meneja wa timu Manuel Pellegrini amesema nyota huyo wa kimataifa wa Argentina ni mmoja kati ya wachezaji bora kabisa duniani. City wanaweza kufuzu hatua ya timu 16 bora ya michuano hiyo kama wakifanikiwa kuitandika AS Roma katika mchezo wa mwisho wa kundi E na CSKA Moscow ikishindwa kuifunga Bayern.

MESSI NDIO KIDUME ULAYA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi amekuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufunga mabao matatu au hat-trick dhidi ya APOEL Nicosia. Messi aliingia katika mchezo wa kundi F huko Cyprus akiwa amelingana kwa mabao 71 na mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid Raul. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo ambao pia ulishuhudia Luis Suarez akifunga bao lake la kwanza toka sajiliwe, Messi mwenye umri wa miaka 27 amesema anajisikia furaha kuweka rekodi hiyo nzuri katika michuano muhimu kama hiyo. Messi aliendelea kudai kuwa pamoja na hilo lakini jambo muhimu kwake ni alama tatu walizopata na kuwapongeza wachezaji wenzake kwa kuonyesha soka safi. Hiyo inakuwa rekodi ya pili kubwa kwa Messi aliyoweka ndani ya siku nne, baada ya kuwa mfungaji bora la Liga kwa kufikisha mabao 253 kwa kufunga hat-trick nyingine katika mchezo dhidi ya Sevilla Jumamosi iliyopita. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina sasa anakuwa amefunga mabao 74 katika mechi 91 za michuano ya Ligi ya Mabingwa alizocheza wakati Raul yeye ana mabao 71 katika mechi 104 za michuano hiyo alizocheza.

MABINTI WA MOHAMMAD ALI WADAI BABA YAO YUKO FITI.

MABINTI wa bondia nguli Muhammad Ali wamedai kuwa baba yao huwa anacheka akisikia tetesi za kuzushiwa kifo. Ali mwenye umri wa miaka 72 anaugua ugonjwa wa kutetemeka toka mwaka 1984 na kumekuwa na uvumi wa mara kwa mara kuwa afya yake imekuwa ikizorota. Lakini mabinti zake Maryum na Hana waliiambia BBC kuwa baba yao yuko katia hali njema na huwa anapenda kusikia watu wakimzungumzia kwani anaona kama vichekesho. Mabinti hao waliendelea kudai kuwa hata kama tetesi zinapotoka baba yao huwa na hamu kubwa kwani hufikiria kuwa atapamba kurasa za magazeti mbalimbali. Maryum amesema habari nyingi huwa zinatoka kwa watu ambao hawaufahamu vizuri ugonjwa hu ndio maana zinapotoshwa.

Monday, November 24, 2014

NEUER AONGOZA ORODHA YA MAKIPA WATEULE WA FIFA WORLD IX, CASILLAS NDANI.

GOLIKIPA wa kimataifa wa Hispania na klabu ya Real Madrid, Iker Casillas ametajwa katika kikosi bora cha dunia cha Shirikisho la Soka Duniani-FIFA mwaka huu pamoja na kushindwa kucheza kwa kiwango cha juu katika Kombe la Dunia na ligi. Golikipa wa Chelsea Thibaut Courtois pia yumo katika orodha hiyo sambamba na golikipa wa Bayern Munich Manuel Neuer, Claudio Bravo wa Barcelona na Gianluigi Buffon wa Juventus. Katika orodha hiyo jina la Casillas ndio liloshangaza wengi kuwemo pamoja na kuwepo katika kikosi hicho kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2008 mpaka 2012. Casillas amecheza mechi mbili pekee za La Liga msimu wa 2013-2014 huku akicheza mechi zingine 10 msimu huu. Golikipa huyo mwenye umri wa miaka 33 ambaye alinyakuwa taji la Ligi ya Mabingwa akiwa na Madrid msimu uliopita, alionekana akifanya makosa ya wazi katika kila bao walilofungwa Hispania katika michezo ya Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi na Chile. Golikipa akayeibuka mshindi katika kura zinazopigwa na wachezaji zaidi ya 20,000 duniani kote atatangazwa Januari 12 katika sherehe za utoaji tuzo za Ballon d’Or. Orodha ya nafasi nyingine katika kikosi hicho bado hazijatangazwa.

REUS NJE MPAKA JANUARI.

KIUNGO wa klabu ya Borussia Dortmund, Marco Reus anatarajiwa kukaa nje ya uwanja mpaka Januari mwakani baada ya kuchanika msuli katika kifundo chake cha mguu wa kulia wakati wa mchezo dhidi ya Paderborn ambao ulimazika kwa sare ya mabao 2-2 Jumamosi iliyopita. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 alikoza michuano ya Kombe la Dunia ambapo nchi yake ya Ujerumani ilinyakuwa taji hilo kutokana na matatizo ya kifundo cha mguu na baadae mwanzoni mwa msimu alikosa michezo saba ya klabu yake kwa matatizo kama hayo. Nyota aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akiwashukuru mashabiki wake kwa kumtakia heri ya kupona mapema na kudai kuwa atarejea akiwa imara zaidi. Dortmund ambao msimu uliopita walimaliza katika nafasi ya pili katika msimamo wa Bundesliga kwasasa wanashika nafasi ya tatu kutoka mkiani wakiwa wameshinda mechi tatu pekee kati ya 12 walizocheza.

BLATTER ANAPSWA KUJIUZULU - RAUBALL.

RAIS wa Ligi ya Soka ya Ujerumani-DFL, Reinhard Rauball amedai kumwambia rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Sepp Blatter kujiuzulu nafasi hiyo. Rauball alikaririwa na gazeti la Kicker akidai kuwa anadhani wakati wa Blatter kuachia nafasi hiyo umefika kutokana na kashfa mbalimbali ambazo zimeendelea kuliandama shirikisho hilo. Kashfa ambayo inaiandama shirikisho hilo kwasasa ni kuhusu ripoti ya uchunguzi ya Michael Garcia yenye kurasa 430 ambayo FIFA imegoma kuichapisha kwa kuogopa kukiuka sheria. Rauball amesistiza kuwa kashfa hiyo inayohusu mchakato wa kutafuta weneywe wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 inapaswa kumpelekea Blatter kujiuzulu ili kulinda heshima ya michuano hiyo. Rauball alifafanua kuwa jambo hilo kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari alimpigia simu Blatter na kumueleza mawazo yake kuhusiana na hilo.

NATAKA KUWA BORA KAMA ZIDANE - POGBA.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Ufaransa, Paul Pogba amebainisha kuwa anataka kuwa bora kama Zinedine Zidane, huku akidai Juventus ni klabu kubwa kama ilivyo Real Madrid. Pogba amekuwa akifananishwa na Yaya Toure na Patrick Vieira kutokana na aina yake ya mchezo lakini mwenyewe amesema kuna mchezaji mwingine ambaye anapenda kufikia mafanikio yake ambaye ni Zidane. Akihojiwa kuhusiana na tetesi za kuhamia nchini Hispania, Pogba amesema anadhani Madrid ni klabu kubwa kama ilivyo kwa Juventus, kwani alikuwa Manchester United lakini bado aliamua kujiunga na timu hiyo ya Turin. Pogba amesema anajisikia vyema nchini Italia kwani kila mtu amekuwa kama sehemu ya familia katika klabu hiyo, jambo pekee analofikiria ni kuimarika kama mchezaji na ni matumaini yake atafikia mafanikio ya Zidane.

KOCHA STUTTGART AJIUZULU KUFUATIA VIPIGO MFULULIZO.

MENEJA wa klabu ya VfB Stuttgart, Armin Veh amejiuzulu wadhifa wake huo leo, siku moja baada ya mabingwa hao wa zamani wa Bundesliga kuchapwa bao 1-0 na Augsburg na kubakia mkiano mwa msimamo wa ligi. Veh, ambaye aliingoza timu hiyo kushinda taji la Bundesliga mwaka 2007, amerejea msimu huu lakini baada ya kufungwa mechi tatu mfululizo ameamua kuachia ngazi. Katika taarifa yake Veh amesema ilikuwa ni hatua ngumu kuchukua kwasababu amekuwa karibu na timu hiyo lakini ana uhakika uamuzi wake ni sahihi. Stuttgart imefanikiwa kushinda mechi mbili msimu huu na kukubalia kufungwa mabao 26, wakiwa na safu mbaya ya ulinzi katika ligi sambamba na Werder Bremen wanaosika nafasi ya 17. Veh anakuwa kocha wa nne katika Bundesliga kubwaga manyanga msimu huu kufuatia Mirko Slomka wa Hamburg SV, Jens Keller wa Schalke na Robin Dutt wa Bremen nao kuachia ngazi.

GYAN ABAINISHA YUKO FITI.

NAHODHA wa timu ya taifa ya Ghana, Asamoah Gyan amebainisha kuwa yuko fiti baada ya kupita michezo miwili ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon mwakani. Kabla ya michezo hiyo dhidi ya Uganda na Togo, mshambuliaji huyo alikuwa akisumbuliwa na majeruhi yaliyomfanya kushindwa kucheza. Akihojiwa Gyan amesema alikuwa akitamani sana kucheza mechi dhidi ya Togo lakini daktari alimwambia litakuwa jambo la hatari hivyo akashindwa kufanya hivyo. Hata hivyo nyota huyo amesema kwasasa anajisikia kuwa fiti tayari kuitumikia klabu yake ya Al Ain. Gyan aliifungia Ghana mabao matatu katika michezo ya kufuzu Afcon.

APPIAH NJIANI KUCHUKUA MIKOBA YA KUINOA AL KHARTOUM.

KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana, Kwesi Appiah anatarajiwa kufikia makubaliano ya kuinoa klabu ya soka ya Al Khartoum ya Sudan. Vyombo vya habari nchini Sudan vimedai kuwa klabu hiyo tayari imeshamaliza mazungumzo na kocha huyo ambaye aliingoza Ghana katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil. Appiah mwenye umri wa miaka 54 alitimuliwa na Shirikisho la Soka la nchi yake Septemba mwaka huu na sasa amesaini mkataba wa awali wa makubaliano hayo. Taarifa za ndani zinadai kuwa Appiah alitumia siku mbili jijini Khartoum kukamilisha dili hilo ambalo litamuwezesha kupokea kitita cha dola 39,000 kwa mwezi. Klabu ya Al Khartoum ambayo inamilikiwa na jeshi la Sudan ilimaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita na wanatarajiwa kushiriki michuano ijayo ya Kombe la Shirikisho.

SCHUMACHER BADO ANA SAFARI NDEFU NA NGUMU KUELEKEA KUPONA KUFUATIA AJALI MBAYA ALIYOPATA.

MENEJA wa Michael Schumacher amesema bado hakuna muda kamili kwa nyota huyo wa zamani wa mashindano ya langalanga kupona kufuatia ajali mbaya aliyopata wakati akiteleza katika barafu karibu mwaka mmoja uliopita. Sabine Kehm amesema haiwezekani kujua ni muda gani haswa utachukua kwa Schumacher kupona kabisa kwani bado anakabiliwa na safari ndefu na ngumu kuelekea huko. Schumacher alipata majeraha ya kichwa wakati akiwa na familia yake katika mapumziko katika milima ya Ufaransa Desemba 29, ajali ambayo ilimuacha na majeraha ya ubongo yaliyomfanya kutojitambua kwa muda wa miezi sita. Kwasasa nguli huyo anajiuguza nyumbani kwake huko Gland, Switzerland toka Juni mwaka huu. Kehm amesema Schumacher anaendelea vyema lakini bado ana kipindi kirefu na kigumu ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida.

CRUZEIRO YANYAKUWA TAJI LA PILI MFULULIZO LIGI KUU NCHINI BRAZIL.

KLABU ya Cruzeiro imefanikiwa kunyakuwa ubingwa wa Ligi Kuu nchini Brazil kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuitandika Goias kwa mabao 2-1 jana. Mabao yaliyofungwa na kiungo Ricardo Goulart na Everton Ribeiro yalitosha kuihakikishia timu hiyo ubingwa wake wa nne wa ligi huku kukiwa kumebaki michezo miwili kabla ya ligi kumalizika. Matokeo hayo mbele ya mashabiki karibu 60,000 waliohudhuria mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Mineirao huko Belo Horizonte yamewahakikishia ubingwa huo baada ya Sao Paulo waliokuwa nafasi ya pili kufungwa na Santos kwa bao 1-0 huko Cuiaba. Cruzeiro inakuwa timu ya kwanza kushinda mataji mfululizo toka Sao Paulo walipofanya hivyo kuanzia mwaka 2006 mpaka 2008.

LENGO NI KUCHEZA LIGI YA MABINGWA ULAYA - MANCINI.

MENEJA mpya wa klabu ya Inter Milan, Roberto Mancini amedai kuwa lengo lake kubwa ni kuirejesha timu hiyo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo wameshindwa kufuzu kwa kipindi cha miaka sita. Kauli hiyo ya Mancini imekuja kufuatia mpambano mkali na mahasimu wao AC Milan katika mchezo wa Serie A ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 jana. Mancini amesema wanahitaji muda lakini malengo yao ni kushinda mechi nyingi kadri iwezekanavyo ili waweze kumaliza katika nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi. Kocha huyo ambaye amewahi kuingoza Inter kushinda mataji saba yakiwemo matatu ya Serie kuanzia mwaka 2004 mpaka 2008, alipewa kwa mara nyingine mikoba ya kuinoa timu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Walter Mazzarri wiki chache zilizopita. Katika kipindi chote ambacho Mancini alipokuwa akiinoa Inter amefanikiwa kushinda mara nne, kupoteza mara tano na sare moja katika michezo iliyowakutanisha na maahsimu wao wa jiji AC Milan.

RATIBA YA COPA AMERICA MWAKANI KUJULIKANA.

RATIBA ya michuano ya Copa America inatarajiwa kupangwa baadae leo huku nyota wa Barcelona Lionel Messi na Neymar wakiwa miongoni mwa wachezaji wanatarajiwa kushiriki michuano hiyo itakayofanyika majira ya kiangazi mwakani nchini Chile. Wenyeji Chile ni mojawapo mwa nchi tatu zitakazoongoza upangaji wa ratiba hiyo wakiwa sambamba na Brazil pamoja na washindi wa pili katika Kombe la Dunia Argentina. Timu 12 zinatarajiwa kukwaana katika michuano hiyo ya Amerika Kusini zikiwemo nchi zilizolikwa ambazo ni Mexico, Jamaica na mabingwa watetezi Uruguay. Hata hivyo mabingwa hao watetezi watamkosa mshambuliaji wao nyota Luis Suarez katika michuano hiyo kutokana na kuendelea kutumikia adhabu yake ya kufungiwa mechi tisa za kimataifa kwa kosa la kumng’ata beki wa Italia Giorgio Chiellini katika Kombe la Dunia nchini Brazil. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi rasmi jijini Santiago Juni 11 mwakani.

CHEKI MAJANGA YA LIVERPOOL.

CHEKI MABAO MATATU YA MESSI YALIYOMUWEZESHA KUWEKA HISTORIA MPYA LA LIGA.

KAMA ULI-MISS JINSI MAN UNITED ILIVYOIADHIBU ARSENAL NYUMBANI.

Friday, November 21, 2014

FIFA KUPITIA UPYA RIPOTI YA GARCIA.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limethibitisha kamati yake ya ukaguzi itapitia upya taarifa yote ya mchakato wa uenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 baada ya kikao kati ya wakili Michael Garcia na jaji wa maadili Hans-Joachim Eckert. Taarifa ya mapitio ya ripoti ya uchunguzi wa Garcia kuhusiana na masuala ya rushwa ilitolewa na jaji Eckert wiki iliyopita huku Urusi na Qatar zikisafishwa kuwa wenyeji halali wa michuano hiyo ya mwaka 2018 na 2022. Jaji Eckert alikiri kuwepo matukio kadha katika ripoti hiyo lakini hayakuingilia mchakato wa kutafuta wenyeji katika michuano hiyo. Haraka taarifa hiyo iliyokuwa na kurasa 42 ilipingwa vikali na wakili Garcia alioongoza uchunguzi huo kwa miaka miwili akisisitiza kumekuwa na makosa kadhaa kadhaa kulinganisha na ripoti yake iliyokuwa na kurasa 430. Jaji Eckert na Garcia alikutana ili kusawazisha mambo na kufikia uamuzi huo wa kupeleka ripoti yote kwa kamati ya ukaguzi kwa ajili ya kufanyiwa kazi zaidi.

NADAL AMUOSHESHA VYOMBO RONALDO BAADA YA KUMFUNGA KATIKA KARATA.

MCHEZAJI nyota wa zamani wa kimataifa wa Brazil, Ronaldo amelazimika kuosha vyombo baada ya kushindwa katika mchezo wa karata na mchezaji tenisi nyota kutoka Hispania Rafael Nadal. Katika mchezo huo Nadal alipokea kitita cha dola 50,000 katika mfuko wake wa misaada huku Ronaldo akiosha vyombo baada ya kushindwa. Mchezo huo ulikuwa maalumu kwa ajili ya hafla ya chakula kilichoandaliwa katika Casino ya Hippodrome jijini London, Uingereza. Kitendo cha Ronaldo kukubali kuosha vyombo alivyokuwa ametumia Nadal wakati wa kula kiliwafurahisha wageni waalikwa katika hafla hiyo mahsusi.

UEFA KUTOA MSIMAMO WAKE DESEMBA 4 KUHUSIANA NA TIMU ZA CRIMEA.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA, Michel Platini amesema shirikisho hilo litafanya uamuzi wa kama watatambua michezo ya vilabu kutoka Crimea chini uangalizi wa Shirikisho la Soka Urusi-RFU Desemba 4 mwaka huu. Klabu tatu za Crimea ambazo ni TSK Simferopol, SKChF Sevastopol na Zhemchuzhina Yalta zimekubaliwa kucheza katika ligi ya ubingwa ya Urusi kufuatia matatizo ya kisiasa katika eneo lao. Shirikisho la Soka la Ukraine-FFU lilikata rufani Shirikisho la Soka Duniani-FIFA na UEFA kutoa adhabu kwa RFS kwa kile walichokiita kufuruga sheria za soka. UEFA ilifanya kikao na RFS na FFU katika makao makuu yake jijini Nyon Septemba mwaka huu na pande zote zilikubaliana kuundwa kwa kikosi kazi kutafuta suluhu katika suala hilo. Platini alikaririwa katika mtandao wa UEFA akidai kuwa kikosi kazi kilichoundwa kinatafuta suluhu katika suala hilo na uamuzi wa mwisho utatolewa mapema mwezi ujao.

SAMMER AONGEZWA MIAKA MITATU BAYERN.

KLABU ya Bayern Munich imetangaza kumuongeza mkataba wa miaka mitatu zaidi mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo Matthias Sammer ambao utamalizika mwaka 2018. Sammer ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani na kocha, alijiunga na Bayern mwaka 2012 akitokea Shirikisho la Soka la Ujerumani ambako nako alikuwa mkurugenzi wa michezo. Akihojiwa na wanahabari Sammer amesema miaka miwili na nusu ambayo ameitumikia klabu hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwani walifikia malengo yao mengi waliyojiwekea. Toka atue Bayern, Sammer amefanikiwa kuisaidia timu hiyo kushinda taji la Bundesliga katika msimu wa 2013-2014, Kombe la Ligi sambamba na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2013.

ARSENAL VS MAN UNITED: GIROUD FITI, WELBECK HATIHATI.

MSHAMBULIAJI nyota wa Arsenal, Olivier Giroud yuko fiti kwa ajili ya mchezo dhidi ya Manchester United kesho katika Uwanja wa Emirates baada ya kupona kupona majeruhi ya mguu wake uliovunjika. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 28 alikadiriwa kuweza kurejea uwanjani baada ya mwaka mpya kutokana na majeri hayo aliyopata Agosti mwaka huu lakini sasa anaonekana kuwa fiti kwa ajili ya kurejea. Nahodha wa klabu hiyo Mikel Arteta pia yuko fiti baada ya kupona majeruhi ya msuli lakini meneja wa timu hiyo Arsenal Wenger amesema mabeki wake Laurent Koscielny na Mathieu Debuchy bado hawako fiti. Wenger amesema mbali na hao lakini pia bado ataendelea kumkosa Theo Walcott katika mchezo wa kesho huku Danny Welbeck naye akiwa katika hatihati kutokana na kupata matatizo ya msuli akiwa katika majukumu ya kimataifa.

CITY BADO INA NAFASI YA SKUHINDA TAJI LA LIGI KUU - PELLEGRINI.

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Manuel Pellegrini bado ana uhakika wa kutetea taji la Ligi Kuu pamoja na kupitwa kwa alama nane na vinara Chelsea. City ambao watakuwa wenyeji wa Swansea City kesho baada ya mapumziko kupisha mechi za kimataifa kumalizika, wamefanikiwa kushinda mechi moja kati ya sita za mashindano yote walizocheza hivi karibuni. Kiwango cha timu hiyo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pia imekuwa ya kusuasua huku wakiwa katika hatari ya kushindwa kuvuka hatua ya makundi. Hata hivyo Pellegrini bado amekuwa na imani na kikosi chake kufanya vyema katika ligi ya nyumbani na Ulaya msimu huu. Pellegrini amesema sasa sio wakati wa kuangalia yaliyotokea nyuma kwani bado kuna mechi nyingi za kucheza katika ligi na Ulaya. Kocha huyo aliongeza kuwa bado kuna mechi 27 hivyo kuna alama zaidi za kupigania hivyo wataona itakavyokuwa mpaka mwishoni mwa msimu.

UNITED KUMKOSA BLIND WIKI SITA.

KLABU ya Manchester United amedai kuwa majeraha ya goti ya kiungo Daley Blind yatamuweka nje ya uwanja kwa wiki kadhaa na sio miezi sita kama ilivyotangazwa. Meneja wa United, Louis van Gaal amesema kitakachofanyika kwanza ni nyota huyo kupumzika kwa muda wa siku 10 halafu ndiyo waangalie ukubwa wa tatizo lake. Klabu hiyo ilileta mkanganyiko baada ya kutuma ujumbe katika ukurasa wake mtandao wa kijamii wa twitter kuwa kiungo huyo atakuwa nje kwa miezi sita ujumbe ambao hata hivyo ulifutwa haraka baadae. Van Gaal amesema hawezi kutabiri ni muda gani haswa Blind anaweza kuwa nje ya uwanja kwani wanasubiria vipimo vya afya lakini hadhani kama inaweza kufikia miezi sita. Blind aliumia wakati akiitumikia timu yake ya taifa ya Uholanzi katika mchezo wa kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016 dhidi ya Latvia ambao walishinda kwa mabao 6-0.

MANCINI KUANZA NA AC MILAN KESHO.

MENEJA mpya wa klabu ya Inter Milan Roberto Mancini anakabiliwa na kibarua kigumu mwishoni mwa wiki hii wakati atakapoanza kibarua chake kwa kupambana na mahasimu wao AC Milan katika mchezo wa Serie A. Mancini alirejea tena kuinoa Inter wiki iliyopita baada ya kutimuliwa kwa Walter Mazzarri kutokana na matokeo mabovu ya timu hiyo katika mechi za hivi karibuni. Wakati akiinoa klabu hiyo kati ya mwaka 2004 na 2008, Mancini aliisaidia kushinda mataji matatu mfululizo ya Serie A, mawili ya Kombe la Italia na moja la Super Cup. Mbali na mchezo huo ambao utachezwa Jumapili, kesho kutakuwa na mchezo mwingine utakaozikutanisha Lazio na Juventus.

SHEFFIELD YAMCHOMOLEA MBAKAJI EVANS KUFANYA NAO MAZOEZI.

KLABU ya Sheffield United imesitisha ofa yake ya kumruhusu Ched Evans aliyehukumiwa kwa kosa la ubakaji kutumia vifaa vyao vya mazoezi. Klabu hiyo imekuwa ikishutumiwa vikali kwa kumruhusu Evans kufanya mazoezi katika klabu hiyo baada ya kuachiwa kutoka jela. Mwanariadha bingwa wa olimpiki Jessica Ennis-Hill alieleza kuwa anataka jina lake kuondolewa katika upande mmoja wa jukwaa la klabu hiyo kama mchezaji huyo angeruhusiwa kuitumikia klabu hiyop tena. Katika taarifa yake klabu hiyo imedai kuwa kutokana na malalamiko kutoka kwa mashabiki na wadau mbalimbali imeazimia kusitisha ofa yake ya kumruhusu mchezaji huyo kufanya mazoezi tena na timu hiyo. Evans aliachiwa huru mwezi uliopita baada ya kutumikia nusu ya kifungo chake cha miaka mitano jela alichohukumiwa kwa kumbakla msichana mwenye umri wa miaka 19 katika chumba cha hoteli mwaka 2011.

VAN GAAL AMFAGILIA WELBECK.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Louis van Gaal amesisitiza anafurahi kumuona Danny Welbeck akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika klabu ya Arsenal kwasababu asingeweza kupata nafasi hiyo katika kikosi chake. Welbeck ameanza vyema maisha mapya Arsenal baada ya usajili wa dakika za mwisho kutoka Old Trafford majira ya kiangazi ambapo mpaka sasa ameshafunga mabao matano katika mechi 12 za mashindano yote aliyocheza huku akifunga mengine matano katika mechi za Uingereza. Van Gaal amesisitiza kuwa ameshangazwa na kiwango cha nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 na anaamini maendeleo yake yametokana na kupata nafasi ya kucheza kila wiki jambo ambalo asingeweza kumuhakikishia katika kikosi chake kutokana na uwepo wa Robin van Persie, Wayne Rooney na Radamel Falcao. Kocha huyo amesema angeweza kuendelea kuitumikia United lakini waliamua kuwa anaweza kuondoka na amenufaika kwa uamuzi huo. Van Gaal amesema mchezaji yeyote anayepata nafasi ya kucheza katika timu siku huwa anaimarika na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Welbeck.

Thursday, November 20, 2014

MICHUANO YA AFCON YAIVA BAADA YA TIMU 15 ZITAKAZOSHIRIKI KUJULIKANA.

MICHEZO ya makundi ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani ilimalizika jana usiku huku timu tano zaidi zikifuzu huku tukishuhudia mabingwa watetezi wa michuano hiyo Nigeria wakiaga mapema. Katika michezo ya jana, Guinea moja ya nchi iliyoathirika sana na ugonjwa wa Ebola, Ivory Coast, Mali, Ghana na DR Congo zilifanikiwa kufuzu moja kwa moja na kuungana na nchi za Algeria, Burkina faso, Cameroon, Cape Verde, Congo Brazzaville, Gabon, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia na Zambia. Mabingwa watetezi Nigeria wao walishindwa kufuzu baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Afrika Kusini ambao walikuwa tayari wamefuzu hivyo kuwafanya kumaliza katika nafasi ya tatu katika kundi A. Nafasi ya mwisho ya kufuzu ilinyakuliwa na DR Congo wakiwa kama washindi watatu bora huku Equatorial Guinea wao wakipata nafasi ya moja kwa moja kufuzu kutokana na kuwa wenyeji wa michuano hiyo. 
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Januari 17 hadi Februari na ratiba inatarajiwa kupangwa Desemba 3 mwaka huu.

MERTESACKER ABAINISHA KUMSHAWISHI OZIL KUJIUNGA NA ARSENAL.

BEKI Per Martesacker amebainisha kuwa yeye na Mesut Ozil wamezungumza na kiungo wa Real Madrid Sami Khedira kuhusu kujiunga na klabu ya Arsenal. Khedira amefanikiwa kucheza mara tano pekee tena akitokea benchi msimu huu baada ya kocha wa Madrid Carlo Ancelotti kuamua kuwatumia Toni Kroos na Luka Modric katika nafasi ya kiungo. Khedira amesisitiza hana mpango wa kuondoka Madrid pamoja na mkataba wake kukaribia kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Hata hivyo Mertesacker amesema ana hamu kubwa kwa Mjerumani mwenzake huyo kujiunga na Arsenal na hata kufikia hatua ya kumshawishi yeye pamoja na ozil. Octoba ilibainika kuwa Manchester United wamemtengea euro milioni 13 Khedira katik dirisha dogo la usajili Januari mwakani baada ya kuambiwa na AS Roma kuwa Kevin Strootman hatauzwa.

BUFFON SASA KUZEEKEA JUVENTUS.

GOLIKIPA mkongwe wa Juventus, Gianluigi Buffon amesaini mkataba mpya wa miaka mitatu ambao utamuweka katika klabu hiyo mpaka katika umri wa miaka 39. Buffon mwenye umri wa miaka 36 alibuka katika Serie A akiwa na klabu ya Parma mwaka 1995 na amecheza mechi 400 akiwa na Juventus toka mwaka 2001. Mkataba huo mpya wa Buffon unatarajiwa kumalizika mwaka 2017. Akihojiwa Buffon amesema anataka kuendelea kucheza katika kiwango cha juu kuisifu klabu hiyo kwani imemfanya ajivunie uamuzi wake aliofanya miaka 14 iliyopita. Mbali na Buffon Juventus pia imempa mkataba mpya beki wake wa kati Giorgio Chiellini mwenye umri wa miaka 30 ambao utamalizika mwaka 2018.

KOCHA WA MISRI AOMBA RADHI KWA KUSHINDWA KUFUZU.

KOCHA wa timu ya taifa ya Misri, Shawky Gharib ameomba radhi kwa kushindwa kuiwezesha nchi hiyo kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani. Misri walishindwa kushinda mchezo wao mwisho wa makundi dhidi ya Tunisia kwa kukubalia kkichapo cha mabao 2-1. Akihojiwa mara baada ya mchezo Gharib aliwaomba radhi mashabiki wa soka wa Misri kwa kushindwa kutimiza ndoto zao. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa hajali uamuzi wowote utakaochukuliwa na Chama cha Soka cha nchi hiyo kama abaki au aondoke kwani takakubaliana nao yeye pamoja na benchi lake la ufundi. Gharib amesema alijaribu kutengeneza kikosi kipya lakini majeruhi wengi waliwakwamisha kuonyesha ubora wao. Gharib alichukua mikoba ya kuinoa nchi hiyo mwaka jana baada ya Bob Bradley kushindwa kuiwezesha timu hiyo kufuzu Kombe la Dunia.