Monday, November 24, 2014

NEUER AONGOZA ORODHA YA MAKIPA WATEULE WA FIFA WORLD IX, CASILLAS NDANI.

GOLIKIPA wa kimataifa wa Hispania na klabu ya Real Madrid, Iker Casillas ametajwa katika kikosi bora cha dunia cha Shirikisho la Soka Duniani-FIFA mwaka huu pamoja na kushindwa kucheza kwa kiwango cha juu katika Kombe la Dunia na ligi. Golikipa wa Chelsea Thibaut Courtois pia yumo katika orodha hiyo sambamba na golikipa wa Bayern Munich Manuel Neuer, Claudio Bravo wa Barcelona na Gianluigi Buffon wa Juventus. Katika orodha hiyo jina la Casillas ndio liloshangaza wengi kuwemo pamoja na kuwepo katika kikosi hicho kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2008 mpaka 2012. Casillas amecheza mechi mbili pekee za La Liga msimu wa 2013-2014 huku akicheza mechi zingine 10 msimu huu. Golikipa huyo mwenye umri wa miaka 33 ambaye alinyakuwa taji la Ligi ya Mabingwa akiwa na Madrid msimu uliopita, alionekana akifanya makosa ya wazi katika kila bao walilofungwa Hispania katika michezo ya Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi na Chile. Golikipa akayeibuka mshindi katika kura zinazopigwa na wachezaji zaidi ya 20,000 duniani kote atatangazwa Januari 12 katika sherehe za utoaji tuzo za Ballon d’Or. Orodha ya nafasi nyingine katika kikosi hicho bado hazijatangazwa.

No comments:

Post a Comment