Friday, October 30, 2015

SIRI ZAZIDI KUFICHUKA FIFA.

MSHAURI wa rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amesema kulifanyika makubaliano ya kuipa Urusi uenyeji wa michuano ya Kombe la dunia mwaka 2018 kabla ya kura hazijafanyika zilizowahusisha wakubwa wa shirikisho hilo. Mshauri huyo Klaus Stohlker amesema kulikuwa na mazungumzo ya nyuma ya pazia yaliyowahusisha wajumbe wa kamati ya utendaji ya FIFA. Blatter ambaye amesimamishwa kwa siku 90 alibainisha kuwa kulikuwa ba maelewano ya kutoa uenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 kwa Urusi na Marekani. Michuano ya mwaka 2022 baadae walipewa Qatar baada ya kura kubadilika. Suala ya uenyeji wa michuano ya mwaka 2018 na 2022 ni jambo ambalo linafanyiwa uchunguzi na mamlaka nchini Uswisi wakishirikiana na Marekani.

SAMATTA, ULIMWENGU KIBARUANI KESHO ALGERIA.

KLABU ya USM Alger ya Algeria kesho itakuwa ikifukuzia taji lake la kwanza la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati watakapokuwa wenyeji wa TP Mazembe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mchezo wa fainali ya mkondo wa kwanza. Katika mchezo huo USM itakuwa na kiu na kufikia mafanikio ya wenzao Entente Setif ambao ndio walikuwa mabingwa wa michuano hiyo kwa mwaka jana. Soka la Algeria linaonekana kupata kwa kasi katika miaka ya karibuni kwani kwasasa wao ndio wanaongoza kwa ubora katika orodha za Afrika huku pia wakifanikiwa kutinga hatua ya pili ya michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika mwaka jana. Hata hivyo, USM haitakuwa na kazi rahisi katika mchezo huo kwani Mazembe imejijenga na kuwa timu ya kuogopewa barani Afrika wakiwa wameshinda taji hilo mara nne kati ya sita zilizopita. Mchezo wa mkondo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa kesho katika Uwanja wa Omar Hamadi uliopo Algiers na ule wa maruadiano utachezwa jijini Lubumbashi Jumapili ya Novemba 8 mwaka huu. Mshindi wa michuano hiyo ataliwakilisha bara la Afrika katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia itakayofanyika nchini Japan Desemba mwaka huu.

WENGER ATAMBA PAMOJA NA MSURURU MREFU WA MAJERUHI ALIONAO.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amepuuza tatizo la majeruhi na kusisitiza kuwa atatafuta suluhisho huku wachezaji nane wakikosekana katika kikosi chake. Theo Walcott na Alex Oxlade-Chamberlain nao wameingia katika orodha za majeruhi kufuatia kuumia katika mchezo dhidi ya Sheffield Wednesday, huku Wenger akithibitisha wote watakosekana mpaka baada ya mapumziko kupisha mechi za kimataifa Novemba mwaka huu. Sasa nyota hao wanaungana na Aaron Ramsey, Jack Wilshere, Danny Welbeck, Mikel Arteta, David Ospina na Tomas Rosicky ambao nao wote ni majeruhi. Lakini Wenger amesema ana imani na timu yake ya madaktari na ana uhakika wanaweza kukabiliana na hali hiyo katika mchezo wao dhidi ya Swansea City kesho. Akizungumza na wanahabari Wenger amesema watatafuta suluhisho na anatakiwa kupata suluhisho lenye uhakika.

VAN GAAL AMPUUZA SCHOLES.

MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal amepuuza ukosolewaji uliotolewa na kiungo wa zamani Paul Scholes kuhusu jinsi timu inavyocheza, akidai kuwa fimbo na mawe vinaweza kumvunja mfupa lakini majina hayamuumizi. Kiungo huyo wa zamani ambaye ameichezea United mechi 718, amesema asingefurahia kucheza akiwa chini ya Van Gaal kwani kikosi hicho kimekuwa na mapungufu katika masuala ya ubunifu. Kauli ya Scholes imekuja kufuatia United kung’olewa katika michuano ya Kombe la Ligi jana. Van Gaal aliwaambiwa wanahabari kuwa Scholes alikuwa hana wajibu wa kutoa kauli kwani hafahamu ilikuwa na manufaa kwa nani.

REMY AMPIGIA DEBE MOURINHO ABAKIE CHELSEA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Chelsea, Loic Remy amesisitiza kuwa bado anaona meneja wao Jose Mourinho ndio mtu sahihi wa kuendelea kuinoa klabu hiyo. Miezi mitano baada ya kuiongoza Chelsea kunyakuwa taji la Ligi Kuu, Mourinho amekuwa akipambana kutetea kibarua chake na ratiba ya mechi zinafuatia ikiongeza zaidi shinikizo kwa Mreno huyo. Wakiwa wamefungwa mechi tano kati ya 10 za ligi walizocheza, Chelsea wamejikuta wakiwa katika nafasi ya 15 katika msimamo wakikosa alam tisa kufikia nne bora. Lakini pamoja na taarifa tofauti zilizozagaa zikidai wachezaji kadhaa wamekuwa wakimtaka Mourinho kuondoka, Remy amesema meneja wao huyo bado anaungwa mkono na kikosi chake. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa, amesema ni muhimu kwa Mourinho kubakia kwani hawataki kukata tamaa sasa.

MAKOCHA WAJIUZULU ARGENTINA.

MAKOCHA wawili Edgardo Bauza wa klabu ya San Lorenzo na Diego Cocca wa Racing ambao waliziongoza timu zao kushinda mataji makubwa mwaka jana, wametangaza kujiuzulu nyadhfa zao hizo wakati msimu wa Ligi Kuu nchini humo utakapomalizika mwezi ujao.  Bauza aliiongoza Lorenzo kunyakuwa taji lao la kwanza la Kombe la Libertadores la Amerika Kusini mwaka jana kabla ya Cocca kuingoza Racing ksushinda taji la ligi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 13. Akihojiwa Bauza amesema yeye pamoja na wasaidizi wake wameamua kuachia ngazi na kuondoka kwani wameona ni jambo zuri kwa klabu na timu. Naye Cocca akizungumza na wanahabari alitangaza taarifa kama hizo za kuondoka mwishoni mwa msimu lakini alikanusha kama kuondoka kwake kunahusiana na masuala ya maslahi.

Tuesday, October 27, 2015

LUIS ENQRIQUE KUWAPUMZISHA SUAREZ NA NEYMAR KESHO.

MENEJA wa Barcelona, Luis Enrique amewaacha Luis Suarez na Neymar katika kikosi chake cha wachezaji 16 watakaocheza mchezo wa Kombe la Mfalme dhidi ya Villanovense. Barcelona itasafiri kwenda Extremadura kukwaana na timu hiyo ya daraja la pili kesho bila nyota wake hao pamoja na Lionel Messi aliyekuwa majeruhi. Hata hivyo, kocha huyo amekiri ana matumaini kuwa ataweza kuondoka na wachezaji wengi zaidi wa kikosi cha kwanza. Nyota wengine walioachwa ni pamoja na Sergio Busquets, Javier Marcherano, Gerard Pique na Claudio Bravo wakati Andres Iniesta yeye akiwa bado hajapona sawaswa majeruhi ya msuli wa paja yanayomsumbua.

ALLEGRI ATETEA UAMUZI WAKE WA KUMUWEKA BENCHI DYBALA.

MENEJA wa Juventus, Massimiliano Allegri ametetea uamuzi wake wa kutomtumia Paulo Dybala alisajiliwa kwa fedha nyingi wiki iliyopita baada ya kukosolewa na rais wa Palermo Maurizio Zamparini. Zamparini alimtuhuma Allegri kwa kumharibia Dybala kiwango chake baada ya kumchezesha kwa dakika tisa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Manchengladbach wiki iliyopita. Akizungumza na wanahabari kuelekea mchezo wao wa kesho dhidi ya Sassoulo, Allegri amesisitiza uchaguzi wa kikosi chake hutegemea kiwango cha wachezaji. Kocha huyo amesema yeye huwa hachagui wachezaji kutokana na fedha walizogharimu, huwa anachagua wachezaji wanaocheza vyema.

FA YAMSHITAKI RICHARDS KWA VURUGU.

BEKI wa Aston Villa, Micah Richards amefunguliwa mashitaka ya kinidhamu na Chama cha Soka cha Uingereza-FA. Hatua hiyo imefikiwa baada ya Richards kuzozana na beki wa Swansea City, Federico Fernandez katika mchezo baina yao uliochezwa Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Villa Park. FA ilithibitisha taarifa hizo kupitia mtandao wake huku Richards mwenyewe akipewa mpaka siku ya Alhamisi ya Octoba 29 mwaka huu kujitetea. Katika mchezo huo Villa walifungwa mabao 2-1 na Swansea hata ambayo ilipelekea kocha wake Tim Sherwood kutimuliwa.

ROONEY AMMWAGIA SIFA SMALLING.

NAHODHA wa Manchester United, Wayne Rooney amedai kuwa beki Chris Smalling ni miongoni mwa mabeki watatu bora duniani hivi sasa. Smalling ambaye ametoka kuwa mchezaji wa muda na kuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha kwanza chini meneja Louis van Gaal katika kpindi cha miezi 18 iliyopita, amekuwa katika kiwango bora akicheza mechi zote za United msimu huu. Akihojiwa Rooney alimsifu beki huyo na kudai kuwa ni miongoni mwa mabeki wa kati bora kabisa duniani kwasasa kutokana na kiwango chake. Kauli hiyo ya Rooney imekuja kufuatia Van Gaal kudai Smalling mwenye umri wa miaka 25 anaweza kuwa nahodha wa United katika siku za usoni.

SHEIKH SALMAN AKANUSHA TUHUMA ZA KUWATESA WACHEZAJI.

MGOMBEA urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa amekanusha vikali kuwa alishiriki kuwatesa wachezaji na kudai ni za uongo. Sheikh Salman anatuhumiwa na kundi la haki za binadamu nchini Bahrain kwa kusaidia kuwatambua wachezaji na wanamichezo wengine waliojihusisha na mandamano ya kutaka demokrasia mwaka 2011. Alikuwa kiongoza wa Chama cha Soka cha Bahrain na mwana familia ya kifalme wakati watu wa usalama walipowakamata watu wengi walioshiriki maandamano hayo. Watu kadhaa walifariki wakati wengine waliokamatwa walifungwa na kuteswa. Akihojiwa Sheikh Salman mwenye umri wa miaka 49 amesema hawezi kukanusha jambo ambalo hajawahi kulifanya na tuhuma kama hizo sio tu zinamharibia hadhi yake lakini pia zinaumiza.

TOKYO SEXWALE AJINADI KUIJENGA UPYA FIFA.

MGOMBEA urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Tokyo Sexwale anataka kulijenga upya shirikisho kwa kurekebisha yale yote mabaya ikiwemo kashfa ya ufisadi inayolikabili hivi sasa. Jumatatu mgombea huyo kutoka Afrika Kusini aliwasilisha maombi yake rasmi ya kugombea nafasi hiyo ya Sepp Blatter ambaye bado anachunguzwa na FIFA kuhusiana na tuhuma za kumlipa fedha Michel Platini bila kufuata utaratibu. Sexwale ambaye ni mfanyabiashara na mfungwa wa zamani wa kisiasa anaungwa mkono na Chama cha Soka cha Afrika Kusini-SAFA na amethibitisha kuwa atasafiri kuelekea jijini Cairo kuomba kuungwa mkono na Shirikisho la Soka la Afrika-CAF. Sexwale ameahidi kuirejesha heshima ya shirikisho hilo kama akishinda uchaguzi huo utakaofanyika Februari mwakani.

BARTOMEU AWASHUKIA WANAODAI MESSI ANATAKA KUONDOKA.

RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amejibu kwa hasira taarifa zinazodai kuwa Lionel Messi ataondoka katika klabu hiyo, akisisitiza kuwa taarifa hiyo ni ya kutia aibu. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina ambaye kwasasa yuko benchi akisumbuliwa na majeruhi ya goti, amekuwa akihusishwa na taarifa za kuondoka huku magazeti yakidai kuwa anaweza kutimkia Ligi Kuu. Akiulizwa suala hilo Bartomeu amesema watu wanaosambaza habari hizo za uongo wanapaswa kuona aibu kwa Messi hana mpango wa kwenda popote. Bartomeu aliendelea kudai kuwa kwasasa Messi anafanya bidii ili aweze kwa fiti kabla ya mchezo wa El Clasico ambao watakwaana na mahasimu wao Real Madrid.

Friday, October 23, 2015

MESSI APIGWA CHINI ORODHA MPYA YA WANAMICHEZO WENYE THAMANI ZAIDI.

MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Lionel Messi ameondoshwa katika 10 bora ya orodha ya wanamichezo wenye thamani zaidi duniani. Orodha hizo ambazo hutolewa na gazeti maaruu la Forbes, mwaka 2014 Messi alishika nafasi ya tisa akikadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 12 lakini mwaka huu baada ya kushika kwa thamani ya dola milioni moja, nyota huyo ameondoshwa katika kumi bora. Badala yake mchezaji nyota wa gofu Roy Mcllroy na bondia Floyd Mayweather wameingia katika kumi bora ya orodha hiyo. Nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo ambaye alikuwa nafasi ya saba mwaka jana naye pia ameshuka kwa nafasi moja mpaka ya nane mwaka huu. 

Orodha kamili ya wanamichezo na thamani zao zilivyoadiriwa ni kama ifiatavyo.

1. Tiger Woods - Worth $30m
2. Phil Mickelson - $28m
3. LeBron James - $27m
- Roger Federer - $27m
5. MS Dhoni - $21m
6. Usain Bolt - $18m
- Kevin Durant - $18m
8. Cristiano Ronaldo - $16m
9. Rory McIlroy - $12m
10. Floyd Mayweather Jr - $11.5m

Orodha ya timu 10 bora za michezo zenye thamani zaidi.
1. New York Yankees - $661m
2. Los Angeles Lakers - $521m
3. Dallas Cowboys - $497m
4. New England Patriots - $465m
5. Real Madrid - $464m
6. Manchester United - $446m
7. Barcelona - $437m
8. Bayern Munich - $375m
9. Los Angeles Dodgers - $373m
10. New York Knicks - $361m

UINGEREZA KUJIPIMA NA UHOLANZI MWAKANI.

CHAMA cha Soka cha Uingereza-FA kimetanagza kuwa timu yao taifa itajipima nguvu kwa ajili ya michuano ya Euro 2016 kwa kucheza mchezo wa kirafiki na Uholanzi katika Uwanja wa Wembley mwakani. Uingereza inayonolewa na Roy Hodgson, ambao walifuzu michuano hiyo bila kufungwa mchezo wowote, watakwaana na Uholanzi ambao wao wameshindwa kufuzu fainali hizo, Machi 29 mwakani. Hiyo itakuwa mara ya 20 kwa timu hizo kukutana huku mara ya mwisho ikiwa Februari mwaka 2012 ambapo Uholanzi ilishinda kwa mabao 3-2.  Pamoja na kumaliza katika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana, Uholanzi walishindwa kutamba katika mechi za kufuzu wakimaliza katika nafasi ya nne katika kundi nyuma ya Jamhuri ya Czech, Iceland na Uturuki.

CHAMPAGNE KUJITOSA TENA URAIS FIFA.

MSHAURI wa zamani wa rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Sepp Blatter, Jerome Champagne amesema anafikiria kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi ujao. Champagne alijaribu kushindana na Blatter katika uchaguzi uliofanyika Mei mwaka huu lakini alishindwa kupata watu kumuunga mkono ili ateuliwe. Kusimamishwa kwa Blatter na rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Michel Platini kupisha uchunguzi wa malipo ya euro milioni 1.35, kunamsukuma Champagne kutaka kujaribu tena kugombea nafasi hiyo. Champagne ametangaza kuwa kama akichaguliwa wakati atakapogombea ataweka wazi mishahara na marupurupu ya maofisa wa shirikisho hilo. Champagne sasa anaungana na Prince Ali bin al-Hussein wa Jordan, mchezaji wa zamani wa Trinidad na Tobago David Nakhid na rais wa Shirikisho la Soka la Asia, Sheikh Salman bin Ebrahim Al Khalifa ambao tayari wametangaza nia ya kugombea.

MOROCCO, TUNISIA ZAFUZU CHAN.

TIMU ya taifa ya Morocco imefanikiwa kuichapa Libya kwa mabao 4-0 jana katika mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani-CHAN Ukanda wa Kaskazini. Ushindi huo umewafanya kufuzu kwa pamoja na Tunisia michuano hiyo itakayofanyika nchini Rwanda mwakani. Libya walikuwa wakihitaji ushindi katika mchezo huo ili waweze kuwa na nafasi ya kusonga mbele kufuatia kuifunga Tunisia kwa bao 1-0 Jumatatu iliyopita. Morocco ndio wamesonga mbele wakiwa vinara wa kundi lao kwa alama saba wakifuatiwa na Tunisia walioshika nafasi ya pili kwa kuwa na alama nne.

BAYERN YAFUKUZIA USHINDI WA 1,000 BUNDESLIGA.

KLABU ya Bayern Munich inaweza kupata ushindi wake wa 1,000 katika Bundesliga kama wakifanikiwa kuifunga Cologne katika mchezo wa kesho utakaofanyika katika huko Allianz Arena. Mabingwa hao wa Ujerumani katika mchezo huo watakuwa wakijaribu kusahau machungu ya kutandikwa na Arsenal mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa juzi. Kipigo dhidi ya Arsenal kinakuwa cha kwanza kwa Bayern msimu huu katika mechi 13 walizocheza. Pamoja na kufungwa huko Bayern bado wameendelea kuongoza kundi F na sasa wanaelekea kupambana na Cologne wakiwa na rekodi nzuri ya kushinda mechi zao zote tisa za Bundesliga walizocheza mpaka sasa. Ushindi wao bao 1-0 waliopata Jumamosi iliyopita dhidi ya Werder Bremen ulikuwa wa 999 kwa Bayern toka kuanzishwa kwa Bundesliga mwaka 1963.

CRUYFF AWASHUKURU MASHABIKI WAKE KWA POLE ZAO.

NGULI wan soka wa zamani wa Uholanzi, Johan Cruyff amewashukuru mashabiki wake kwa maombi yao baada ya kuthibitishwa kuwa amegundulika na maradhi ya saratani ya mapafu. Cruyff mwenye umri wa miaka 68 ambaye ni mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or mara tatu alitaarifiwa kuhusu maradhi hayo Jumanne baada ya kufanyiwa vipimo. Nguli huyo wa zamani wa klabu ya Ajax Amsterdam aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akiwashukuru wote ambao wamemtakia pole huku wakimuombea katika kipindi hiki kigumu. Mtoto wa kiume wa Cruyff ambaye alikuwa kiungo wa zamani wa Manchester United Jordi naye pia aliwashukuru watu wote ambao wamekuwa wakituma ujumbe wao wa pole. Cruyff amewahi kutinga fainali akiwa na kikosi cha Uholanzi katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1974 ambapo walifungwa na Ujerumani Magharibi.

WENGER AMSHUSHUA VAN GAAL.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema atalia kama mechi za Ligi Kuu zitasimamishwa kupisha mapumziko ya sikukuu za Chrismass na mwaka mpya. Arsenal watacheza mechi saba kati ya Desemba 13 mpaka Januari 16, ikiwemo michezo mitatu ndani ya siku saba mwezi Desemba. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Wenger hiyo imekuwa sehemu y utamaduni wa soka la Uingereza hivyo anapenda kuendelea nao. Meneja wa Manchester United Louis van Gaal ameuita utaratibu huyo wakutotoa mapumziko katika kipindi hicho kama utamaduni wa kikatili. Kauli ambayo imepingwa vikali na Wenger akidai kuwa utamaduni huo umekuwa ukilitangaza soka la Uingereza kwani mashabiki wengi Ulaya wamekuwa wakienda kutizama wakati wa kipindi hicho. Ligi za Hispania, Italia, Ufaransa na Ujerumani zote husimamishwa kwa muda kupisha kipindi hicho cha mapumziko.

COSTA KUENDELEA KUCHEZA UNDAVA.

MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Diego Costa amedai kuwa anafahamu yeye sio malaika pindi awapo uwanjani na hatabadilika aina yake ya uchezaji wa kutumia nguvu. Costa amefungwa mara mbili kutocheza mechi tatu baada ya kumkanyaga mchezaji wa Liverpool Emre Can na baadae kumpiga kibao beki wa Arsenal Laurent Koscielny. Akihojiwa nyota huyo wa kimataifa wa Hispania aliyezaliwa Brazil mwenye umri wa miaka 27, amesema amefikia hapo alipo kutokana na jinsi anavyocheza hivyo hawezi kubadilika kwasababu watu wanataka hivyo. Costa alihamia Stamford Bridge Julai mwaka 2014 akitokea Atletico Madrid na kuisaidia Chelsea kushinda taji la Ligi Kuu na Kombe la Ligi msimu uliopita. Meneja wa Manchester City Manuel Pellegrini amemtaka Costa kupunguza mchezo wake wa kutumia nguvu sana, wakati meneja wa Arsenal Arsene Wenger akimtuhumu mshambuliaji huyo siku kujihusisha na vurugu.

Thursday, October 22, 2015

UCHOYO WA PASI WA MORATA WAMUUDHI POGBA.

KIUNGO wa Juventus, Paul Pogba amekiri kukasirishwa na mchezaji mwenzake Alvaro Morata kwa kushindwa kumpa pasi katka mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Monchengladbach uliomalizika kwa sare ya bila kufungana. Pogba alikaribia kuipatia bao Juventus katika mchezo huo ulofanyika jijini Turin kwa mpira wa adhabu ambayo iliokolewa vyema na golikipa Yann Sommer na alipata nafasi nyingine nzuri ya kufunga kama Morata angempatia pasi badala ya kujaribu kupiga mwenyewe. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Pogba amesema alikasirishwa na Morata na anatumaini katika mechi nyingine atampasia mpira katika eneo muhimu kama lile. Kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Barcelona na Chelsea, amefunga bao moja pekee msimu huu lakini amesisitiza kuwa atarejea katika kiwango chake cha juu hivi karibuni.

MAJANGA YA MAJERUHI YAZIDI KUMUANDAMA RIBERY.

WINGA mahiri wa Bayern Munich, Franck Ribery amepata majeruhi mengine tena baada ya kushindwa kuendelea na mazoezi leo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 hajacheza mechi yeyote toka Machi mwaka jana ikiwa ni matokeo ya majeruhi ya kifundo cha mguu aliyopata katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Shakhtar Donetsk msimu uliopita. Mwezi uliopita ofisa mkuu wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge alidai kuwa Ribery anaweza kurejea tena uwanjani kabla ya kumalizika kwa mwaka huu. Lakini kutokana na na leo kundolewa mazoezini zikiwa zimepita dakika 17 kuna uwezekano mkubwa wa winga huyo mkongwe wa kuendelea kukaa nje kwa kipindi kirefu zaidi.

CELTIC YALINASA JEMBE LA ZAMANI LA WEST HAM.

KLABU ya Celtic imefanikiwa kumsajili mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Uingereza Carlton Cole kwa mkataba utakaomalizika mwaka 2017. Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 32 alikuwa mchezaji huru na amekuwa akifanya mazoezi na klabu ya Parkhead kwa wiki kadhaa baada ya kuondoka West Ham United. Cole amefunga mabao 85 katika mechi zaidi ya 380 za klabu alizocheza zikiwemo Chelsea, Wolves, Charlton, Aston Villa na West Ham. Mkongwe huyo ametambulishwa rasmi katika mkutano na wanahabari uliofanyika mapema leo jijini Glasgow.

WALES KUCHEZA NA UHOLANZI KIRAFIKI.

TIMU ya taifa ya Wales inatarajiwa kuanza maandalizi yake ya michuano ya Euro 2016 kwa kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Uholanzi ambao wameshindwa kufuzu michuano hiyo. Mchezo huo unatarajiwa kufanyika Novemba 13 mwaka huu katika Uwanja wa Cardiff City uliopo jijini Cardiff. Wakati Wales wakisheherekea kufuzu michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kupita miongo kadhaa hali ni tofauti kwa Uholanzi ambao wameshindwa kufanya hivyo kwa kumaliza wakiwa nafasi ya nne katika kundi lao. Timu hizo zitakwaana kwa mara ya kwanza toka Juni mwaka 2014 wakati Uholanzi walipoichapa Wales mabao 2-0 katika maandalizi ya Kombe la Dunia nchini Brazil mchezo uliofanyika jijini Amsterdam.

DYNAMO KIEV YAINGIA TENA 18 ZA UEFA.

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limefungua kesi ya kinidhamu dhidi ya klabu ya Dynamo Kiev kutokana na vurugu zilizofanywa na mashabiki wake na mambo ya kibaguzi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Chelsea jana. Katika mchezo huo uliofanyika katika mji mkuu wa Ukraine Chelsea waliambulia sare ya bila kufungana. Matokeo hayo ynaifanya Chelsea kubaki katika nafasi ya tatu katika kundi G wakiwa alama moja nyuma ya Dynamo. Katika taarifa yake UEFA imesema itaanza kusikiliza kesi hiyo Octoba 27 mwaka huu. Hiyo sio mara ya kwanza kwa mashabiki wa timu hiyo kuinia matatani kwani msimu uliopita Dynamo walitozwa faini ya kufungiwa upande mmoja wa uwanja kwa makosa mawili mojawapo likiwa vurugu na lingine ubaguzi katika mchezo wa Europa League.

CRUYFF AGUNDULIKA NA SARATANI YA MAPAFU.

TAARIFA kutoka nchini Hispania zimedai kuwa nguli wa soka wa Uholanzi, Johan Cruyff amegundulika kuwa na saratani ya mapafu. Vyombo vya habari vikiwemo vile vya radio na magazeti vimeripoti kuwa nguli huyo mwenye umri wa miaka 68 aligundilika na maradhi hayo Jumanne na kwasasa anaendelea kufanyiwa vipimo kujua ukubwa wa tatizo linalomkabili. Cruyff aliisaidia timu yake ya taifa ya Uholanzi kufika hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1974. Nguli huyo pia amewahi kushinda mataji matatu ya Kombe la Ulaya akiwa na klabu ya Ajax Amsterdam na baadae kwenda kucheza na kuifundisha Barcelona. Akiwa kocha wa Barcelona alifanikiwa kuisaidia kushinda taji lao la kwanza la Kombe la Ulaya mwaka 1992 na Kombe la Washindi la Ulaya mwaka 1989.

SARE DHIDI YA MADRID YAMPA KIBURI MENEJA WA PSG.

KUFUATIA Paris Saint-Germain-PSG kupata sare ya bila kufungana na Real Madrid katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya jana, meneja wake Laurent Blanc anaamini kikosi chake kina uwezo wa kupata mafanikio zaidi msimu huu. Blanc aliingoza PSG kushinda mataji matatu ya ndani msimu uliopita na Blanc bado ana uhakika kikosi chake kina ubora wa kupata mataji zaidi msimu huu. Kocha huyo amesema siri kubwa ya kuwa na kikosi imara kinacheza kwa umoja ni kutofanya mabadiliko makubwa kwa mwaka jambo ambalo walilifanya ndio maana anaamini wanaweza kufanya vizuri. Sare hiyo waliyopata jana imezifanya timu hizo kufungana alama katika kundi A kabla ya kuendelea katika mchezo wao marudiano wiki mbili zijazo.

Wednesday, October 21, 2015

RAMSEY PANCHA TENA.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kiungo wa kimataifa wa Wales Aaron Ramsey amekuwa na huzuni baada ya kupata majeruhi mengine ya msuli wa paja.Ramsey mwenye umri wa miaka 24, alitolewa katika kipindi cha pili katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao Arsenal iliifunga Bayern Munich mabao 2-0 jana.Wenger amesema Ramsey anatarajiwa kuukosa mchezo wa Ligi Kuu Jumamosi hii dhidi ya Everton na anaweza kuendelea kuwa nje ya uwanja kwa muda.Kocha huyo aliendelea kudai kuwa nyota huyo amemwambia kuwa amehuzunishwa na kuumia kwake lakini ameahidi kurejea akiwa imara zaidi.Majeruhi ya msuli wa paja yamekuwa yakimsumbua Ramsey mara kwa mara kwani msimu uliopita pekee aliwahi kukaa nje ya uwanja kwa vipindi vitatu tofauti.

NEYMAR AIONGOZA BARCELONA KUINYUKA BATE.

MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Neymar kwa mara nyingine ameonyesha uwezo wa kuongoza na kusiba nafasi ya Lionel Messi kufuatia ushindi waliopata dhidi ya BATE Borislov katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.Huku Messi akiwa nje kwa miezi miwili kutokana na majeruhi ya goti majukumu yameangukia kwa Neymar kuiongoza Barcelona katika safu ya ushambuliaji jambo ambalo amekuwa akilifanya vyema.Jumamosi iliyopita Neymar alifunga mabao manne katika ushindi mnono wa La Liga waliopata dhidi ya Rayo Vallecano na jana alifanikiwa kutoa pasi zote mbili za mwisho za mabao yaliyofungwa na Ivan Rakitic katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya BATE.Beki wa Barcelona, Marc Bartra alimsifia mshambuliaji huyo akidai amekuwa akifanya vyema katika kutengeneza mashambulizi kama anavyofanya Messi.

MASHABIKI WA BAYERN WAANDAMANA KUPINGA UGHALI WA TIKETI.

KUNDI la mashabiki wa Bayern Munich waliingia uwanjani wakiwa wamechelewa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliofanyika katika Uwanja wa Emirates, wakipinga bei kubwa ya tiketi katika mchezo huo.Kundi hilo ambalo lilibainisha maandamano yao wiki iliyopita, hawakuingia uwanjani kwa dakika tano za kwanza za mchezo huo ambao tiketi zake zilipatikana kwa paundi 64.Mashabiki wa Bayern pia walionyesha mabango yaliyokuwa yakisomeka kwa maandishi makubwa kupinga bei hiyo waliouziwa tiketi.Meneja wa Bayern, Pep Guardiola amesema atazungumza na meneja wa Arsenal, Arsene Wenger ili katika mchezo ujao waweze kufanya tiketi rahisi kwa mashabiki wao.Arsenal ilishinda mabao 2-0 katika mchezo wa jana na watarudiana tena Novemba 4 mwaka huu.

ROONEY ATAMBA KUENDELEA KUNG’AA PAMOJA NA UMRI KUMTUPA MKONO.

NYOTA wa Manchester United, Wayne Rooney ana uhakika bado ana miaka mingi mbele yake ya kucheza soka pamoja na kujiandaa kusheherekea miaka 30 ya siku yake ya kuzaliwa Jumamosi hii.Nahodha huyo wa United na timu ya taifa ya Uingereza tayari yuko katika msimu wake wa 14 katika Ligi Kuu toka alipoibuka kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Everton akiwa na miaka 16 mwaka 2002.Akihojiwa Rooney amesema kimwili bado anajisikia vyema na pamoja na umri aliokuwa nao sasa lakini bado anajiona mdogo katika soka hivyo anaweza kucheza kwa miaka mingi ijayo.Nyota huyo amesema anashukuru kwa kutokuwa na majeruhi makubwa makubwa hivyo kumpa nafasi ya kuwa na uwezo wa kuendelea kuchza kwa kipindi kirefu zaidi.

MOURINHO KAMA KAWAIDA YAKE ALIA NA MWAMUZI BAADA YA SARE.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho amemfananisha mwamuzi aliyechezesha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao walitoka sare ya bila ya kufungana na Dynamo Kiev, na mwamuzi waliyechezesha mchezo wa Kombe la Dunia la Raga kati ya Scotland na Australia.Mwamuzi Craig Joubert wa Afrika Kusini alikosolewa vikali baada ya kuizawadia penati Australia katika dakika za laa salama katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Scotland jana.Mourinho alimshambulia mwamuzi Damir Skomina kwa kuwanyima penati wakati Cesc Frabregas alipofanyiwa faulo katika eneo la hatari.Kocha huyo amesema kama mwamuzi huyo angewapa penati hiyo hali ya mchezo ingebadilika lakini hakufanya hivyo.Chelsea inashika nafasi ya tatu katika kundi G wakiwa na alama nne katika michezo mitatu waliyocheza, alama tatu nyuma ya vinara FC Porto.

TOURE AWAPASHA WACHEZAJI WENZAKE.

KIUNGO mahiri wa Manchester City, Yaya Toure amesema hawatakuwa na chakujitetea kama wakishindwa kunyakuwa taji lolote msimu huu baada ya kuimarisha kikosi chao kwa kusajili wachezaji kadhaa wakubwa majira ya kiangazi.City walifanikiwa kuwasajili Raheem Sterling, Kevin De Bruyne na Nicolas Otamendi wakijaribu kuimarisha kikosi chao kufuatia kutoka kapa bila taji msimu wa 2014-2015.Na Toure sasa amesema hawatakuwa na sababu msimu huu, kwani mafanikio ndio jukumu lao kuu baada ya kikosi kuimarishwa vyema.Toure amesema kwa kipindi kirefu wamekuwa katika kivuli cha Manchester United lakini sasa ni wakati wao wa kutoka huko na kuonyesha dunia kuwa wanaweza.City ambao wanaongoza Ligi Kuu kwa tofauti ya alama mbili dhidi ya Arsenal wanaoshka nafasi ya pili, watakuwa wenyeji wa Sevilla katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baadae leo.

LAMAR ODOM ARUHUSIWA KUJIUGUZA NYUMBANI.

MCHEZAJI nyota wa zamani wa Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani-NBA, Lamar Odom amerejeshwa jijini Los Angeles baada ya kupatiwa matibabu katika hospitali huko Las Vegas, wiki moja baada ya kukutwa hajitambui katika danguro huko Nevada.Katika taarifa iliyotolewa na familia yake Odom ataendelea kujiuguza Los Angeles na amedaiwa kupona kwa haraka kwani ameshaanza kutembea kidogo kidogo.Mke wake ambaye walikuwa mbioni kuachana Khloe Kardashian, baba yake na watoto wake wawili wote wako pamoja na mkongwe aliyekuwa akicheza katika timu ya Los Angeles Lakers.Odom ambaye alimuoa Kardashian nyota wa vipindi vya luninga mwaka 2009, amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya kwa kipindi kirefu.Polisi bado wanaendelea kufanyia uchunguzi vipimo ili kubaini haswa kilichotokea kabla ya kukumbwa na tukio hilo.

WENGER AANZA KUCHONGA BAADA YA KUICHAPA BAYERN.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema ushindi dhidi ya Bayern Munich utaongeza imani katika Uwanja wa Emirates.Arsenal ilipoteza mechi zake mbili za mwanzo za Ligi ya Mabingwa lakini mabao ya Olivier Giroud na Mesut Ozil yameifanya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Bayern jana.Klabu hiyo ambayo bado inashikilia mkia katika kundi F inatarajiwa kupambana tena na Bayern Novemba 4 mwaka huu.Wenger amesema ilikuwa muhimu kushinda mchezo huo na wamefanya hivyo wakiwa chini ya shinikizo kubwa jambo ambalo litaimarisha imani yao na imani ya mashabiki wao.

Sunday, October 18, 2015

PSG IKO TAYARI KUPAMBANA NA MADRID - IBRAHIMOVIC.

MSHAMBULIAJI nyota wa Paris Saint-Germain-PSG, Zlatan Ibrahimovic amewaonya Real Madrid kuwa wako tayari kwa ajili yao baada ya kufunga mara mbili katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Bastia. Mabao yote yalipatikana katika dakika 20 za mwisho katika mchezo huo uliofanyika jana ambao umeifanya PSG kuendelea kukaa kilele mwa msimamo wa Ligue 1 kwa tofauti ya alama tano. PSG inayonolewa na Laurent Blanc sasa wanakuwa hawajafungwa katika mechi 10 za ligi huku pia wakishinda mechi zao mbili za kwanza za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Ibrahimovic amesema matokeo waliyopata ni mazuri kwani wameifunga timu ngumu kwani mara ya mwisho waliondoka wakiwa wamefungwa mabao 4-2. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa sasa wanahamishia nguvu zao katika mchezo dhidi ya Madrid ambao watakuwa nyumbani na ni matumaini yao watapata matokeo wanayohitaji.


USHINDI DHIDI YA EVERTON WAMPA JEURI VAN GAAL KUELEKEA MCHEZO WAO DHIDI YA CITY.

MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal amesema kikosi chake kinaweza kujumuishwa katika kinyang’anyiro cha ubingwa wa Ligi Kuu kama wakifanikiwa kuwafunga mahasimu wao Manchester City Jumapili ijayo. United jana ilifanikiwa kuifunga Everton kwa mabao 3-0 wakati vinara wa ligi City wakiicharaza Bournemouth kwa mabao 5-1 katika Uwanja wa Etihad. Akihojiwa Van Gaal amesema siku zote lengo lao limekuwa ni ubingwa na wataweza kuingia katika kinyang’anyiro hicho kama wakifanikiwa kuifunga City katika mchezo wao ujao. Kocha huyo alikuwa akitaka kikosi chake kurejea katika kiwango chao baada ya kufungwa na Arsenal mabao 3-0 kabla ya mapumziko kupisha mechi za kimataifa na mabao mawili ya mapema waliyopata jana yalifanya ushindi wao kuwa rahisi. Van Gaal aliwapongeza wachezaji wake kwa kiwango kizuri walichoonyesha katika mchezo huo na anadhani kuwa huo ni mwanzo wa ushindi katika mechi zingine zitakazofuata.

WALCOTT ADAI ARSENAL IKO TAYARI KWA AJILI YA BAYERN.

MSHAMBULIAJI wa Arsenal, Theo Walcott anaamini wanaweza kuifunga Bayern Munich kama wakifanikiwa kucheza kwa kiwango cha juu katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Manchester United. Arsenal waliishangaza United kwa kuonyesha soka maridadi la kushambulia na kufuatiwa na ushindi mwingine wa mabao 3-0 dhidi ya Watford katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa jana. Timu hiyo sasa inakabiliwa na mchezo mwingine wa hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern ambapo watakuwa wakihitaji alama tatu muhimu baada ya kushindwa kupata alama yeyote katika mechi zao mbili za kwanza. Akihojiwa Walcott amesema kucheza dhidi ya bayern kwa kiwango walichonacho hivi sasa itakuwa changamoto kwao lakini wakiwa nyumbani na mashabiki wao watahitaji kucheza kwa kiwango cha juu kama walivyofanya dhidi ya United. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa wanafahamu kuwa wanaweza kumfunga yeyote na watakwenda katika mchezo huo wakiwa tayari.

KLOPP AMKINGIA KIFUA ORIGI.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp anaamini Divock Origi anaweza kupunguza tatizo la majeruhi katika safu ya ushambuliaji wa klabu hiyo baada ya kuanza katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu jana walipotoa sare ya bila kufungana na Tottenham Hotspurs. Nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 20 ndiye aliyekuwa mshambuliaji kiongozi katika kikosi kilichoitwa na Klopp katika mechi yake ya kwanza akiwa Liverpool baada ya kuchukua na Brendan Rodgers aliyetimuliwa. Mapema katika kipindi cha kwanza Origi alipiga kichwa safi kilichogonga mwamba kabla ya kupotea mchezoni lakini Klopp amesema chipukizi huyo atacheza vyema akipata uzoefu na kubainisha alitaka kumsajili kutoka Lille wakati akiinoa Borussia Dortmund. Klopp amesema alitaka kumchukua Origi wakati akiwa Dortmund lakini aliwahiwa na Liverpool ambao baadae walimrudisha kwa mkopo hukohuko Lille. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa Origi ni mchezaji mzuri mwenye kasi na ufundi mzuri, kwasasa anapungukiwa na suala la uzoefu kwasababu hajapata nafasi ya kucheza mara kwa mara ila ana uhakika ataimarika vyema.

PELLEGRINI AWAMWAGIA SIFA STERLING NA BONY.

MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amepongeza muunganiko wa Raheem Sterling na Wilfried Bony kwani wawili wameonyesha wanaweza kuziba nafasi ya Sergio Aguero na David Silva waliokuwa majeruhi. Sterling alicheza kama mshambuliaji wa kati na kufunga hat-trick, wakati Bony naye akifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-1 walioupata dhidi ya Bournemouth jana. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Pellegrini amesema walilazimika kufanya kitu tofauti wakiwa bila Aguero na Silva. Aguero na Silva pia wanatarajiwa kuuukosa mchezo wa Jumapili ijayo dhidi ya Manchester United kutokana na majeruhi yanayowasumbua. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa anashukuru kwasababu alimbadilisha Sterling nafasi kwa kumchezxesha katikati huku Bony akiwa mbele yake na mbinu yake hiyo kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

RONALDO RASMI AIPITA REKODI YA RAUL.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo amefanikiwa rasmi kuwa mfungaji bora wa wakati wote wa Real Madrid kufuatia kufunga bao katika ushindi waliopata dhidi ya Levante jana. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 alifunga bao lake la 324 katika La Liga kwenye mechi 310 alizocheza na kuipita rekodi iliyowekwa na nguli wa zamani wa klabu hiyo Raul. Madrid tayari walikuwa wakitambua rekodi hiyo ya Ronaldo, wakimpa bao ambalo lilimgonga Pepe mwaka 2010. Mwaka huo Ronaldo alipiga mpira wa adhabu ambao ulimgonga Pepe na kutinga wavuni na La Liga kuhesabu bao hilo kuwa la Pepe lakini Madrid wao waking’ang’ania kuwa ni la mshambuliaji huyo. Hata hivyo kwa bao alilofunga jana inamfanya Ronaldo rasmi kuivunja rekodi hiyo hata kama ukiliondoa bao hilo moja.

NEYMAR APIGA NNE BARCELONA IKICHARAZA VALLECANO.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Neymar jana alifanikiwa kufunga mabao manne yakiwemo mawili ya penati wakati walipoitandika Rayo Vallecano na kuwafanya kulinga alama katika msimamo wa La Liga na vinara Real Madrid. Barcelona walifanikiwa kutoka nyuma kufuatia kufungwa bao la mapema na Javi Guerra na kupata ushindi huo wa pili katika michezo yao minne iliyopita. Faulo alizofanyiwa Neymar katika eneo la hatari zilimfanya kufunga mabao mawili kwa penati katika kipindi cha kwanza kabla ya kuongeza mengine mawili kipindi cha pili na Luis Suarez kufunga lingine katika dakika za majeruhi katika ushindi wa mabao 5-1. Neymar mwenye umri wa miaka 23 sasa anakuwa amefikisha mabao nane msimu huu na kumfanya kuwa mfungaji anayeongoza La Liga.  Hata hivyo, pongezi nyingi zinapaswa kumuendea mlinda mlango wa barcelona Claudio Bravo ambaye aliokoa michomo mingi ya hatari kutoka kwa Vallecano.

BONY AKIRI KUUMWA MALARIA.

MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Wilfried Bony amebainisha kupata maradhi ya malaria mapema mwaka huu. Bony alishindwa kusafiri katika ziara ya City yakujianda na msimu walizokwenda Australia na Vietnam kwasababu ya maradhi hayo. City hawakutoa taarifa kamili ya sababu za kukosekana kwa Bony kipindi hicho zaidi ya kusema kuwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Swansea City alikuwa akiumwa. Lakini baada ya meneja wa City Manuel Pellegrini kutaja katika mkutano na wanahabari wiki hii kuwa alizungumza na Bony kuhusu majeruhi yaliyokuwa yakimsumbua na maradhi, nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amekiri kuugua ugonjwa huo. Akizungumza mara baada ya mchezo dhidi ya Bournemouth walioshinda mabao 5-1 huku yeye akifunga mawili, Bony amesema alipata malaria kutoka Afrika wakati akirejea lakini sasa hivi yuko sawa.

Friday, October 16, 2015

YAYA TOURE, NASRI WAREJEA KIKOSI CHA CITY.

MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amesema Yaya Toure na Samir Nasri wote wako fiti kwa ajili ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Bournemouth. Viungo hao walikuwa wakisumbuliwa na majeruhi ya msuli wa paja hatua iliyowakosesha mchezo wa ligi dhidi ya Newcastle United ambao walishinda kwa mabao 6-1 lakini sasa wanaonekana kuwa fiti tayari kwa kesho. Pellegrini alithibitisha taarifa hizo lakini kwa Fabian Delph amesema atahitaji wiki moja zaidi ya kujiuguza kabla ya kurejea uwanjani. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa majeruhi aliyopata Sergio Aguero katika mechi za kimataifa hadhani kama ataweza kurejea uwanjani kabla ya mwezi mmoja.

ROONEY FITI KUIVAA EVERTON.

MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Wayne Rooney amefaulu vipimo vya afya kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Everton kesho. Nahodha huyo wa United alizikosa mechi za kufuzu michuano ya Euro 2016 dhidi ya Estonia na Lithuania kutokana na majeruhi ya kifundo cha mguu aliyopata katika mchezo waliotandikwa mabao 3-0 na Arsenal kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa. Hata hivyo, sasa United imethibitisha nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 yuko fiti na atakuwepo katika mchezo huo dhidi ya Everton. Beki Michael Carrick naye pia ameruhusiwa kucheza baada ya kukosa mechi zote za kimataifa za Uingereza kutokana na majeruhi ya nyonga. Marco Rojo aliyekuwa akisumbuliwa na msuli wa paja na Ander Herrera wote wamepimwa na kuonekana kuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo ingawa wanaweza wasicheza dakika zote 90.

MOURINHO KUPINGA ADHABU YA FA.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho anatarajia kukata rufani kupinga adhabu aliyopewa na Chama cha Soka cha Uingereza-FA ya kufungiwa mechi moja na faini ya paundi 50,000 kwa kauli yake dhidi ya mwamuzi aliyechezesha mchezo kati ya timu yake na Southampton. Mourinho anayefahamika kwa kauli zake zenye utata, alilimwa adhabu hiyo kufuatia kumtuhumu mwamuzi kwa kuwanyima penati kutoka uoga katika mchezo ho ambao walitandikwa mabao 3-1 katika Uwanja wa Stamford Bridge. Lakini akizungumza na wanahabari leo kuelekea katika mchezo wao wa keshi dhidi ya Aston Villa, Mourinho aliwahakikishia kuwa atapambana kupinga adhabu hiyo. Mourinho amesema anataka kuwa mkweli mwake mwenyewe hilo ndio jambo la muhimu hivyo atakata rufani kupinga adhabu hiyo. Kocha huyo pia alikiri kuwa tabia yake inaweza kumpa wakati mgumu siku moja kuja kuinoa timu ya taifa ya Uingereza chini ya chama hicho.

BABA YAKE NEYMAR ATHIBITISHA MAN UNITED KUMTAKA MWANAE.

BABA wa mshambuliaji nyota wa Barcelona Neymar amethibitisha kuwa Manchester United walijaribu kutaka kumshawishi aende Ligi Kuu lakini walikataliwa ofa yao. Nahodha huyo wa kimataifa wa Brazil kwasasa yuko katika mzungumzo na kusaini mkataba mpya wa muda mrefu huku makubaliano ya mwisho yakitarajiwa kuwa mwanzoni mwa mwakani. Lakini jana jioni, baba wa nyota huyo ambaye pia ndio wakala wake alibainisha kuwa tetesi ambazo zinavuma kuwa United iliwahi kutaka kumsajili mwanae ni kweli. Mzee huyo aitwaye Neymar Sr amesema ni kweli ofa ya United ilifika Barcelona na klabu iliwasiliana nao wakiwaambia kuwa hawana mpango wa kumuuza. Neymar Sr aliendelea kudai kuwa klabu iliwauliza kama wanaitaka lakini hilo halikuwa tatizo kwani Barcelona wasingemwachia kwasababu alikuwa bado ana mkataba wa miaka mitatu.

ALABA AMTABIRIA MAKUBWA LEWANDOWSKI.

BEKI wa Bayern Munich, David Alaba amedai kuwa Robert Lewandowski anaweza kufikia rekodi ya Bundesliga iliyowekwa na Thomas Mueller mwaka 1972 kwa kufunga mabao 40 kwa msimu. Nyota huyo wa kimataifa wa Poland amekuwa katika kiwango bora msimu huu akiwa ameshafunga mabao 12 katika mechi nane za ligi walizocheza yakiwemo na mabao matano aliyofunga ndani ya dakika tisa katika mchezo dhidi ya Wolfsburg mwezi uliopita. Bayern ambao wameshinda mechi zao zote nane za walizocheza na kuongoza Bundesliga kwa tofauti ya alama saba dhidi ya Borussia Dortmund, watasafiri mwishoni mwa wiki hii kuifuata Werder Bremen. Akizungumza na wanahabari Alaba amesema mabao 40 yanaweza kuonekana mengi lakini kila kitu kinawezekana kwa Lewandowski.

UEFA KUMUUNGA MKONO PLATINI.

RAIS wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, Michel Platini ameungwa mkono na shirikisho hilo katika kinyang’anyiro cha urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Naye rais wa Shirikisho la Soka la Asia, Sheikh Salman bin Ebrahim Al Khalifa anatarajia kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo. Platini anatuhumiwa kulipwa kiasi cha paundi milioni 1.35 na rais wa FIFA anayeondoka Sepp Blatter malipo ambayo yanadaiwa kufanyika mwaka 2011. Pamoja na kuungwa mkono huko kwa Platini, wachambuzi wa masuala ya soka wamedai kuwa nafasi yake hivi sasa inaweza kuwa mashakani kutokana na Sheikh Salman kuonyesha nia ya kugombania. Wadau hao wamesema Sheikh Salman anaungwa mkono na mataifa mengi Ulaya na duniani kwa ujumla hivyo kashfa aliyopata Platini inaweza kumuharibia kwa wajumbe kuona wamepata mbadala wake.