Wednesday, September 30, 2015

WENGER AJIPA MATUMAINI.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesisitiza kikosi chake bado kinaweza kufuzu hatua ya timu 16 bora za michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kuburuza mkia katika kundi F wakiwa hawajaambulia alama yeyote. Arsenal jana walikubali kipigo cha pili mfululizo katika michuano hiyo baada ya kufungwa na Olympiakos kwa mabao 3-2 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Emirates huku wakikabiliwa na mechi zingine mbili ngumu dhidi ya Bayern Munich. Akihojiwa Wenger amesema matokeo hayo yamewaacha katika nafasi mbaya lakini bado anaamini wanaweza kufuzu hatua inayofuata. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa wanachotakiwa kufanya hivi sasa ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mechi zao zinazofuata dhidi ya bayern.

LEWANDOWSKI NA UCHU WA KUFUNGA MABAO.

MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich Robert Lewandowski amesisitiza kuwa hajaridhishwa na idadi ya mabao aliyofunga katika wiki za karibuni na anataka kuendelea wimbi hilo la ufungaji zaidi katika wiki zijazo. Nyota huyo wa kimataifa wa Poland alifunga hat-trick katika ushindi wa mabao 5-0 waliopata Bayern dhidi ya Dinamo Zagreb jana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufanya kufikisha idadi ya mabao 14 katika mechi 10 alizocheza za mashindano yote msimu huu. Akihojiwa Lewandowski amesema haijalishi amefunga mabao mangapi lakini uchu wake yeye ni kufunga mabao mengi zaidi. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa kuna nafasi kadhaa alipata ambazo zilikuwa za kufunga lakini hakufunga na hiyo inaonyesha ni jinsi anavyotakiwa kuendelea kujituma ili aweze kutumia kila nafasi anayopata.

MOURINHO AWALAUMU WACHEZAJI WAKE KWA KUKUBALI KUFUNGWA MABAO YA KIJINGA.

MENEJA wa Chelsea Jose Mourinho amelaumu nyakati mbili za kijinga baada ya kikosi chake kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Porto. Chelsea walipokea kipondo cha tano msimu huu katika mashindano yote baada ya kukubali kufungwa mabao 2-1 na Porto. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Mourinho amesema wametizama mara kadhaa jinsi Porto wanavyopiga kona zao na walikuwa wako tayari kwa hilo. Chelsea sasa wanakuwa wamepoteza michezo mingi zaidi msimu huu kuliko msimu wote wa 2014-2015ambao walipoteza michezo minne pekee. Mourinho aliendelea kudai kuwa anaamini walifanikiwa kumudu mchezo huo lakini walikubali kufungwa mabao ya kijinga jambo lililowagharimu kupoteza mchezo huo. Chelsea wanashika nafasi ya tatu katika kundi G wakiwa nyuma ya Porto na Dynamo Kiev kwa alama moja.

KLOPP ACHOMOA KUINOA MEXICO.

KATIBU mkuu wa Shirikisho la Soka la Mexico, Guillermo Cantu amethibitisha kuwa shirikisho lilimfuata meneja wa Borussia Dortmund Jurgen Klopp kuchukua mikoba ya kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo. Klopp aliondoka Dortmund kufuatia msimu usioridhisha wa 2014-2015 ambapo klabu hiyo ilikosa nafasi ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda kuinoa Liverpool pindi Brendan Rodgers muda wake utakapokwisha Anfield. Cantu amesema walizungumza na wawakilishi wake lakini waliwajibu kuwa kwasasa yuko mapumzikoni hivyo haitawezekana kukubali kuchukua mikoba ya kuinoa nchi hiyo. Hata hivyo, Cantu aliendelea kudai kuwa Klopp alikuwa katika mipango yao ya muda mfupi kwasababu hana ujuzi na soka la Mexico na hazungumzi Kihispania.

KHEDIRA FITI KUIVAA SEVILLA.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Ujerumani, Sami Khedira anatarajiwa kuanza kuitumikia kwa mara ya kwanza Juventus katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Sevilla baadae leo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 alipata majeruhi ya misuli katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Marseille Agosti lakini sasa amerejea kuwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha kwanza. Akihojiwa meneja wa Juventus, Massimiliano Allegri amesema hakuna shaka kuwa Khedira atakuwepo katika mchezo huo kwani amekuwa akifanya mazoezi vyema na wenzake. Pamoja na kusuasua katika Serie A Juventus walianza vyema katika michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Manchester City.

PLATINI ASISITIZA KUENDELEA KUGOMBEA URAIS FIFA PAMOJA NA KUCHUNGUZWA.

WAENDESHA mashitaka nchini Uswisi wamedai kuwa rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Michel Platini anatumiwa kama shahidi na mtuhumiwa katika uchunguzi wa masuala ya rushwa katika Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Waendesha mashitaka hao wanamtuhumu rais wa FIFA Sepp Blatter kulipa malipo yasiyo halali ya dola milioni 2 kwa Platini. Platini amewasilisha maelezo katika uchunguzi huo lakini amesema amefanya hivyo kama shahidi huku wote wawili wakikabusha kufanya jambo lolote baya. Platini amesema bado anataka kuendelea na harakati zake za kugombani urais wa FIFA pindi Blatter atakapoachia ngazi. Hata hivyo mwanasheria mkuu wa Uswisi Michael Lauber amesema hakumuhoji Platini kama shahidi kwani naye pia ni mtuhumiwa naayefanyiwa uchunguzi katika sakata hilo.

CASILLAS ADAI BIFU LAKE NA MOURINHO LILISHAPITA.

GOLIKIPA Iker Casillas amedai ushindi wamabao 2-1 iliyopata FC Porto dhidi ya Chelsea haukumpa furaha ya ziada kwasababu alishasahau na kusamehe mgogoro na kocha wake wa zamani Jose Mourinho. Casillas na Mourinho walifanya kazi pamoja kwa miaka mitatu katika klabu ya Real Madrid kati ya mwaka 2010 na 2013 ambapo katika kipindi hicho walikuwa hawana maelewano mazuri mpaka kufikia hatua ya Casillas aliyekuwa nahodha kuwekwa benchi. Mourinho alikuwa akiamini kuwa Casillas alikuwa akimhujumu kwa kuvujisha mipango yake katika vyombo vya habari hatua ambayo ilipelekea kuchagua kumtumia golikipa namba mbili Diego Lopez badala yake. Wawili hao jana walikutana tena kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya toka walipoachana Madrid ambapo Porto waliibuka kidedea kwa mabao taliyofungwa na Andre Andre na Maicon huku lile la kufutia machozi la Chelsea likifungwa na Willian. Akihojiwa kuhusiana na hilo Casillas amesema ni kitambo kirefu kimeshapita hivyo alishasahau mgogoro wake na Mourinho lakini jambo muhimu alilofurahia ni timu yake kupata matokeo muhimu katika mchezo huo. Porto sasa wanashika nafasi ya pili katika kundi G wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa na Dynamo Kyiv na Chelsea wanashika nafasi ya tatu wakiwa na alama moja.

ROSSI AKUBALI KULIMWA MSHAHARA FIORENTINA.

WAKALA wa mshambuliaji Giuseppe Rossi amedai kuwa mteja wake ameonyesha mapenzi na uaminifu kwa klabu ya Fiorentina baada ya kukubali kupunguziwa mshahara wake. Nyota huyo aliyekuwa akisumbuliwa na majeruhi ambaye amerejea hivi karibuni baada ya miezi 15 ya kujiuguza, amekubali kupunguziwa mshahara wake katika kipindi hiki ambacho anapambana kurejea katika ubora wake. Mkataba wa nyota huyo wa kimataifa wa Italia ambao aliusaini wakati akijiunga na klabu hiyo mwaka 2013 bado unatarajiwa kumalizika katika msimu wa 2016-2017. Wakala huyo Andrea Pastorello amesema kitendo cha Rossi kukubali kupunguza mshahara wake bila kushurutishwa ni kuonyesha makubwa aliyonayo kwa klabu na mashabiki wake kwa ujumla. Rossi ameshaitumikia Fiorentina katika michezo miwili msimu huu mpaka hivi sasa.

BARCELONA YAZIDI KUANDAMWA NA MAJERUHI.

MATATIZO ya majeruhi yameendelea kuiandama Barcelona kufuatia nahodha wake Andres Iniesta kutolewa nje katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayer Leverkusen jana kutokana na kusumbuliwa na msuli wa paja. Nafasi ya Iniesta ilichukuliwa na Jordi Alba wakati Barcelona wakiwa nyuma kwa bao 1-0 lakini mabao mawili yaliyofungwa katika dakika 10 za mwisho na Sergio Roberto na Luis Suarez yalitosha kuwapa ushindi wa mabao 2-1. Mabingwa hao wa Ulaya tayari wanamkosa nyota wao mshindi wa tuzo nne za Ballon d’Or Lionel Messi ambaye amajeruhi yatamuweka nje kwa muda wa miezi miwili. Barcelona walikataa kutaja muda halisi ambao Iniesta anaweza kukaa nje lakini tetesi zinadai kuwa wanaweza kumkosa kwa muda wa mwezi mmoja.

Tuesday, September 29, 2015

BARCELONA WAPATA TAARIFA NJEMA KWA ALBA.

KLABU ya Barcelona imepata ahueni baada ya Jordi Alba kuruhusiwa kucheza katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani kesho. Klabu hiyo tayari itawakosa Adriano ambaye anasumbuliwa na majeruhi msuli huku nyota wao Lionel Messi akitarajiwa kukaa nje kwa kipindi cha wiki nane baada ya kupata majeruhi ya goti Jumamosi iliyopita. Rafinha, Thomas Vermaelan na Claudio Bravo ni wachezaji wengine ambao watakosekana katika mchezo huo wa pili wa hatua za makundi ya michuano hiyo. Katika mchezo wa kwanza Barcelona waliambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya AS Roma ya Italia, mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Olimpico.

MOURINHO ADAI COSTA ANAONEWA.

MENEJA wa Chelsea Jose Mourinho amedai mshambuliaji wake Diego Costa amekuwa akionewa na maafisa wasimamizi wa soka. Akiongea na wanahabari kuhusu mechi ya leo dhidi ya klabu yake ya zamani ya FC Porto ya Ureno katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mourinho amesema waamuzi wamekuwa na hamu kubwa na kumsimamisha mshambuliaji huyo. Costa amefungiwa kutocheza mechi tatu na Shirikisho la Soka la Uingereza-FA baada ya kupatikana na hatia ya utovu wa nidhamu wakati wa mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Arsenal. Lakini yuko huru kucheza dhidi ya Porto leo kwani adhabu hiyo hiyo haigusi mechi za Ulaya.

ROONEY AMZODOA FERGUSON.

NAHODHA wa Manchester United, Wayne Rooney amekanusha kupeleka ombi la kutaka kuondoka mwaka 2013 katika kipindi chake kipya cha kusherekea mafanikio yake nchini Uingereza. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29, ambaye hivi karibuni amekuwa mfungaji bora wa wakati wote, amekuwa akivumilia mahusiano ya misukosuko na meneja wa zamani wa United Sir Alex Ferguson, na kuomba kuondoka mwaka 2010 kabla ya kupewa mkataba mpya. Wawili hao walikwaruzana tena miaka mitatu baadae wakati wa msimu wa mwisho wa Ferguson wakati Rooney alipojikuta akitengwa katika kikosi cha meneja huyo. Katika mchezo wake wa mwisho Old Trafford Ferguson alidai kuwa, mshambuliaji huyo aliomba kuondoka tena lakini Rooney mwenye anakanusha vikali kwa kueleza hali halisi ilivyokuwa. Rooney amesema alimfuata Ferguson na kumwambia kuwa kama hatakuwa akimchezesha ni bora akaondoka zake lakini anashangaa haraka jambo hilo lilidakwa na vyombo vya habari na kupotoshwa jambo ambalo halikuwa kweli.

WENGER AMTAKA CHAMBERLAIN KUJIFUNZA KUTOKA KWA SANCHEZ.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema Alex Oxlade-Chamberlain anaweza kujifunza kutoka kwa mchezaji mwenzake Alex Sanchez jinsi ya kujiweka katika nafasi nzuri ili aweze kupata kufunga mabao. Nyota huyo wa kimataifa wa Chile ambaye amejiunga na Arsenal akitokea Barcelona msimu uliopita alifunga hat0trick katika ushindi wa mabao 5-2 waliopata dhidi ya Leicester City Jumamosi iliyopita. Sanchez alianza msimu wake wa kwanza vyema akiwa na Arsenal kwa kufunga mabao 25 katika mechi 52 alizocheza na kuisaidia timu hiyo kutetea taji lake la Kombe la FA. Oxlade-Chamberlin huu ni msimu wake wa tano akiwa na klabu hiyo ambapo ameambulia kufunga mabao 13 katika mechi 126 alizocheza. Hata hivyo Wenger ana imani kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza anaweza kuongeza kasi ya ufungaji pindi atakapojifunga kupokea mipira katika eneo la hatari.

UKATA WANUKIA WOLFSBURG BAADA YA WADHAMINI WAO VOLKSWAGEN KUBAMBWA KWA UDANGANYIFU.

KLABU ya Wolfsburg ya Ujerumani inaweza kukabiliwa na matatizo ya kifedha siku za usoni kwasababu ya ya kashfa ya inayowakabili wadhamini wao kampuni ya Volkswagen. Kampuni ya kutengeneza magari ya Kijerumani inaweza kukabiliwa na faini ya zaidi ya paundi bilioni 11.8 baada ya kukwepa majaribio ya kupima ubora wake nchini Marekani. Taarifa hizo zinakuja wakati Wolfsburg wakikabiliwa na mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester United kesho. Wataalamu wa masuala ya uchumi wametabiri kuwa klabu hiyo lazima itakumbwa na msukosuko wa kiuchumi kama kampuni hiyo ikilimwa faini hiyo kwani itabidi wapunguze matumizi ili kukabiliana na hali halisi na masuala ya udhamini ndio jambo la kwanza kuangaliwa.

RONALDO KUFUNGUA SHULE 30 ZA SOKA CHINA.

NGULI wa Brazil, Ronaldo anatarajiwa kufungua shule 30 za soka nchini China wakati nchi hiyo ikiendelea na mageuzi kabambe yenye lengo la kuwafanya kuwa vinara wa mchezo huo duniani. Uwekezaji huo unatarajiwa kufanyika katika miji ya Beijing, Shanghai na Shenzhen, Xinhua, huku nguli huyo wa zamani wa klabu za Barcelona, Real Madrid na Inter Milan akitarajiwa kuwepo katika ufunguzi wa kwanza utakaofanyika katika mji mkuu wa Beijing Novemba mwaka huu. Hatua inakuja wakati rais wa China Xi Jinping shabiki mkubwa wa soka ambaye anajaribu kulisukuma taifa hilo ili siku moja wawe wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia, kwa kuisafisha taswira ya mchezo huo baada ya kugubikwa na masuala ya rushwa kwa miaka kadhaa nyuma. Ronaldo mwenye umri wa miaka 39 ambaye amewahi kushinda Kombe la Dunia mara mbili akiwa na Brazil amesema kasi ya maendeleo na malengo ya rais Xi Jinping ndio vitu vilivyomsukuma kufanya hivyo.

MASCHERANO ASHITAKIWA KWA KUKWEPA KODI.

MAHAKAMA moja nchini Hispania, imemfungulia mashitaka mawili ya ukwepaji kodi kwa kiungo mahiri wa Barcelona Javier Mascherano. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina anatuhumiwa kushindwa kuweka hadharani kiasi cha euro milioni 1.5 mwaka 2011 na 2012 alizopata kupitia haki za matangazo ya picha yake na kutoa haki hiyo kwa kampuni anazomiliki nchini Ureno na Marekani na kuzitoza kodi za upendeleo. Jalada hilo pia limethibitisha Mascherano alitoa pungufu ya euro milioni 1.75 kwa mamlaka za kodi Septemba 9 mwaka huu ili kulipa kiasi anachodaiwa pamoja na riba. Mascherano anakuwa mchezaji wa pili kutuhumiwa na masuala ya ukwepaji kodi nchini Hispania baada ya Lionel Messi na baba yake kusimama kuzimani mwaka 2013 kujibu mashitaka kama hayo.

BLATTER ACHOMOA KUJIUZULU.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amesema hawezi kuachia wadhifa huo kwasababu ya mashitaka ya uhalifu yaliyofunguliwa dhidi yake na wachunguzi nchini Uswisi. Blatter mwenye umri wa miaka 79, anatuhumiwa kwa kusaini mkataba usiokuwa na manufaa kwa FIFA na kufanya malipo yasiokubalika kwa rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Michel Platini. Blatter ambaye anatarajiwa kuachia ngazi nafasi hiyo ifikapo Februari mwakani amesema kuwa hajafanya kosa lolote kinyume na sheria. Platini mwenye umri wa miaka 60, ameandika barua kwa wanachama wa UEFA akikana kufanya kosa lolote. Katika taarifa iliotolewa na mawakili wake, Blatter amesema kuwa pauni milioni 1.5 zilizotolewa kama malipo kwa Platini, ambaye ndio kiongozi wa UEFA mwaka 2011 ni halali na hakuna zaidi.

Monday, September 28, 2015

TIMU ZA MISRI MDEBWEDO MICHUANO YA KOMBE LA SHIRIKISHO.

KLABU ya Etoile du Sahel ya Tunisia jana imefanikiwa kupiga hatua moja kuelekea fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuwatandika mabingwa mara mbili Zamalek. Mahasimu wa Zamalek nchini Misri, Al Ahly nao pia waliambulia kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika mchezo uliofanyika huko Soweto. Al Ahly wana faida ya kucheza nyumbani katika mchezo wao wa marudiano utakaofanyika Jumapili ijayo huko Suez wakati Zamalek nao wataikaribisha Etoile Jumamosi jijini Cairo. Mechi za mikondo miwili za fainali ya michuano hiyo zimepangwa kuchezwa Novemba 20 au 22 huku marudiano ikiwa wiki moja baadae.

MAJERUHI YA VIUNGO WA KUKABA YAMTIA MAWAZO WENGER.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger anaweza kufanya mabadiliko katika safu yake ya kiungo ya kukaba wakati kikosi chake kitakapokabiliana na Olimpiakos katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho. Katika mchezo huo Arsenal itawakosa nyota wake Mathieu Flamini na Mikel Arteta lakini wakati Francis Coquelin akiwa ameanza mazoezi baada ya kupona majeruhi ya goti, Wenger amekiri kuwa hajaamua kama nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 atakuwa fiti kwa ajili ya kucheza. Akihojiwa kuelekea katika mchezo huo leo, Wenger anafahamu kuwa Coquelin ameanza mazoezi lakini bado anamfuatilia kwa karibu kama atafaa kucheza kesho. Arsenal inatafuta ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo baada ya kutandikwa mabao 2-1 na Dinamo Zagreb mapema mwezi huu.

SILVA, KOMPANY, HART FITI KUIVAA BORUSSIA MONCHS.

KLABU ya Manchester City ina uhakika wa wachezaji majeruhi kurejea kuelekea katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Monchengladbach kesho kutwa. Nyota hao ambao wanatumainiwa kurejea tena uwanjani ni pamoja na David Silva, Vicent Kompany na golikipa Joe Hart. City walipoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Juventus wiki mbili zilizopita na sasa wanahitaji alama tatu katika mchezo wao ujao ili waweze kuweka hai matumaini yao ya kusonga mbele katika kundi D ambalo linaongozwa na Sevilla na Juventus. Silva alikosa mechi tatu za mwisho za City kutokana na majeruhi ya nyonga lakini sasa anatarajiwa kuwepo katika mchezo wa Jumatano baada ya kuanza mazoezi vyema. Pia kuna habari nzuri kwa Hart na Kompany ambao wote walikuwa benchi katika mchezo wa juzi ambao walipokea kipigo kizito kutoka kwa Tottenham Hotspurs.

NYOTA WA ASTON VILLA ACHAGUA KUITUMIKIA UINGEREZA.

KIUNGO wa klabu ya Aston Villa Jack Grealish amechagua kulitumikia taifa la Uingereza katika mechi za kimataifa badala ya Jamhuri ya Ireland. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 ameshaichezea timu ya taifa ya vijana ya umri wa miaka chini ya 21 ya Jamhuri ya Ireland lakini alikataa mwito wa kuitwa katika kikosi cha wakubwa ambacho kilikuwa na mchezo wa kirafiki dhidi Uingereza Juni mwaka huu. Grealish alianza kucheza soka la kulipwa rasmi akiwa kwa mkopo katika klabu ya Nottingham County wakati walipocheza na MK Dons Septemba mwaka 2013. Mara ya kwanza kuitumikia Villa ilikuwa ni Mei mwaka 2014 akitokea benchi katika mchezo dhidi ya Manchester City.

SPURS YAMTIMUA MKURUGENZI WAKE WA UFUNDI.

KLABU ya Tottenham Hotspurs imetangaza kuachana na mkurugenzi wake wa ufundi Franco Baldini kwa maelewano. Baldini mwenye umri wa miaka 54 aliondoka AS Roma ya Italia kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na Spurs Juni mwaka 2013 akiwa kama msimamizi mkuu wa masuala ya usajili. Katika taarifa yake Spurs wamedai kuwa Baldini anaondoka kwenda kufanya shughuli nyingine nje ya soka na wanamtakia kila kheri. Baldini waliwahi kuwa meneja msaidizi wa Muitaliano mwenzake Fabio Capello wakati alipokuwa akiinoa timu ya taifa ya Uingereza.

USM ALGER YAICHAPA AL HILAL.

KLABU ya USM Alger ya Algeria jana wamefanikiwa kupata ushindi muhimu katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan. Katika mchezo huo USM Alger ambao walikuwa wageni walitoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ambao unawaweka katika nafasi nzuri ya kutinga fainali. Timu hizo zinatarajiwa kukutana tena Jumamosi ijayo katika mchezo wa marudiano ambapo kama USM wakifanikiwa kupata walau sare inaweza kuwavusha moja kwa moja katika hatua hiyo. Timu nyingine ya Sudan katika michuano hiyo Al Merreikh wao walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo juzi ambapo nao wanatarajiwa kurudiana Jumapili ijayo huko Lubumbashi. Bingwa wa michuano hiyo anatarajiwa kupata kitita cha dola milioni 1.5 na nafasi ya kucheza michuano ya Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia huko Japan.

GARI LA RAIS WA PSG LASHAMBULIWA.

TAARIFA kutoka nchini Ufaransa zimedai kuwa gari la rais wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG, Nasser Al-Khelaifi limeshambuliwa kwa mawe wakati akiondoka katika Uwanja wa Beaujoire unaomilikiwa na Nantes, Jumamosi iliyopita. Mabingwa hao wa Ligue 1 waliendelea kujiimarisha kileleni kufuatia ushindi mnono wa mabao 4-1 katika mchezo huo lakini baadhi ya mashabiki wapatao 20 hawakufurahishwa na matokeo ya timu yao kufungwa hatua iliyopelekea kulishambulia gari la rais huyo. Klabu ya Nantes imeomba radhi kwa rais huyo wa PSG na kulaani vikali tukio hilo lililofanywa na watu wasiojulikana. Polisi wa mji huo walithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini hakuna taarifa zozote rasmi zilizopelekwa polisi na PSG walikataa kutoa kauli yeyote kuhusiana na hilo.

GERRARD AIBEBA GALAXY.

NAHODHA wa zamani wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Liverpool, Steven Gerrard jana amefunga bao katika ushindi wa mabao 3-2 iliyopata klabu yake ya Los Angeles Galaxy dhidi ya FC Dallas ambao umewafanya kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Soka ya Marekani kanda ya Magharibi. Gerrard alifunga bao la tatu na kuifanya timu yake kuongoza kwa mabao 3-1 baada ya Giovani dos Santos na Robbie Keane kufunga mengine. Hilo linakuwa bao la pili kwa Gerrard katika mechi 10 ambazo ameichezea Galaxy mpaka sasa baada ya kufunga lingine katika mchezo wake wa kwanza Julai mwaka huu. Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 35 amesema hakuwa na tatizo lolote katika kujiamini kwake na anadhani goli alilofunga lilikuwa na umuhimu wake katika timu.

AUBAMEYANG AWEKA HISTORIA BUNDESLIGA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika mechi zote saba za Bundesliga wakati Borussia Dortmund walipotoa sare dhidi ya Darmstadt. Katika mchezo huo Aubameyang alifunga mabao mawili katika dakika ya 63 na 71 katika sare ya mabao 2-2 waliyopata katika mchezo huo. Wiki iliyopita Aubameyang alikuwa ameweka rekodi ya kushinda katika mechi za mwanzo za Bundesliga na jana aliongeza rekodi hiyo kufikia mechi saba. Sare hiyo imeifanya Dortmund kuwa nyuma ya vinara wa Bundesliga Bayern Munich kwa alama nne, ambapo wanatarajiwa kucheza nao Jumapili ijayo.

Sunday, September 27, 2015

MAJERUHI KUMUWEKA MESSI NJE WIKI NANE.

MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Lionel Messi anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki saba mpaka nane baada ya kuumia goti lake la kushoto katika mchezo wa La Liga walioshinda mabao 2-1 dhidi ya Las Palmas jana. Messi mwenye umri wa miaka 28 aliumia dakika ya tatu ya mchezo na kukimbizwa moja kwa moja hospitali baada ya kubalidishwa. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina anatarajiwa kukosa mechi nane zijazo za Barcelona lakini anaweza kurejea kwa wakati kwa ajili ya mchezo El Classico dhidi ya mahasimu wao Real Madrid Novemba 22 mwaka huu. Akihojiwa meneja wa Barcelona, Luis Enrique amesema siku zote amekuwa na majonzi pindi wachezaji wake wanapoumia na anahuzunikaga zaidi mchezaji huyo anapokuwa Messi.

EVRA ADAI WANAPASWA KUJILAUMU WENYEWE KWA MATOKEO MABOVU.

BEKI wa Juventus, Patrice Evra amesema hawana la kujitetea kwa timu yao kuanza kwa kusuasua msimu huu baada ya kukubali kipigo kingine jana. Kikosi cha Juventus kilichochini ya Massimiliano Allegri kilifanyiwa mabadiliko kiangazi kufuatia kuondoka kwa Andrea Pirlo, Arturo Vidal na Carlos Tevez, wakati majeruhi pia yamekuwa yakiwasumbua mapema msimu huu ambapo Claudio Marchisio na kiungo mpya Sami Khedira wakitarajiwa kukaa nje ka kipindi kirefu. Mabingwa hao watetezi walijikuta wakitandikwa mabao 2-1 na Napoli jana na kuwaacha wakiwa wamepata ushindi mmoja katika mechi zao sita za mwanzo na kuwafanya kuwa nyuma ya vinara Inter Milan kwa tofauti ya alama 10. Akihojiwa Evra amesema wachezaji chipukizi wengi waliopo katika kikosi chao hawapaswi kuchukuliwa kama sababu ya wao kufanya vibaya kwani wao wazoefu ndio wenye wajibu wa kuwasaidia. Beki huyo aliendelea kudai kuwa ni wakatu mgumu kwao hivi sasa na inaumiza lakini hawatakiwa kuchanganyikiwa kwasasa kwani mambo yanaweza kwenda mrama zaidi.

MOURINHO AKIPONDA KIKOSI CHAKE.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho amekipa kikosi chake hasi moja katika maksi kumi kutokana na kiwango kibovu walichoonyesha katika kipindi cha kwanza na kupelekea kuambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Newcastle United jana. Mourinho alishuhudia kikosi chake kikiimarika kwa kutoka nyuma na kufanikiwa kupata walau alama moja lakini walionekana kucheza hovyo katika kipindi cha kwanza. Akihojiwa kocha huyo amesema walicheza vibaya sana katika kipindi cha kwanza hatua ambayo ilimfanya kutaka kufanya walau mabadiliko sita badala ya matatu kama sheria zinavyotaka. Hata hivyo, Mourinho anashukuru kipindi cha pili waliimarika na kucheza vyema huku akiwapongeza viungo wake Willian na Ramirez kwa kuonyesha kiwango cha juu. Mourinho amesema wachezaji hao waliongeza nguvu kwa kikosi chake kutokana na kasi yao jambo ambalo Newcastle walishindwa kulimudu.

WENGER AMSIFU SANCHEZ BAADA YA HAT-TRICK.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema Alexis Sanchez amerejea katika ubora wake baada ya kufunga hat-trick katika mchezo wa Ligi Kuu walioibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Leicester City jana. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Chile amekua akisuasua msimu huu baada ya kufunga mabao 25 katika msimu wake kwanza akiwa na Arsenal baada ya kuondoka Barcelona. Wenger amesema alikuwa anafahamu kuwa itachukua muda kidogo kwa Sanchez kurejea katika ubora haswa kutokana na kupata mafanikio makubwa na timu yake ya taifa katika michuano ya Copa Amerika iliyomalizika mapema kiangazi. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa katika siku zijazo Sanchez ataweza kuwa hatari zaidi kwani amekuwa akijituma kwa bidii bila kuchoka.

NYOTA YA LEWANDOWSKI YAZIDI KUNG'AA BAYERN.

WIKI ya kukumbukwa kwa Robert Lewandowski imeendelea tena wakati mshambuliaji alipofikisha rekodi ya mabao 100 katika Bundesliga ambayo ni haraka zaidi kuliko mchezaji yeyote wa kigeni. Nyota huyo wa kimataifa wa Poland mwenye umri wa miaka 27, alifunga mabao matano ndani ya muda wa dakika tisa katika mchezo wa katikati ya wiki dhidi ya Wolfsburg na kufunga mabao mengine mawili zaidi dhidi ya Mainz na kuifanya Bayern kushinda mechi zao zote saba za ligi mpaka sasa. Lewandowski amefikia rekodi hiyo ya mabao 100 katika mechi 168 alizocheza rekodi ambayo haijafanywa na mchezaji yeyote wa kigeni katika Bundesliga. Sasa nyota hhuyo ambaye alisajiliwa Bayern kama mchezaji huru, amefikisha mabao 10 msimu huu na kumfanya kuwa mchezaji wa pili katika historia ya Bundesliga baada ya nguli wa zamani Gerd Muller kufikisha idadi hiyo katika mechi saba za mwanzo wa msimu.

THOMAS ULIMWENGU AIFUNGIA MZEMBE BAO MUHIMU KATIKA MICHUANO YA LIGI YA MABINGWA AFRIKA.

KLABU ya Al Merreikh ya Sudan jana ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali ya mkondo wa kwanza wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Wenyeji Al Merreikh ndio walioanza kuona lango la wapinzani wao kupitia kwa nyota wa kimataifa wa Ghana Francis Coffie, muda mfupi kabla ya mapumziko. Bao hilo liliwagutusha Mazembe na kuanza kushambulia kwa kasi kabla ya mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Tamzania Thomas Ulimwengu hajasawazisha bao hilo katika dakika ya 77. Bao la ushindi la Al Merreikh liliwekwa kimiani na Barkry Babiker aliyefunga bao hilo dakika za majeruhi, mbele ya mashabiki 45,000 waliojitokeza katika Uwanja wa Omdurman. Katika mchezo wao wa marudiano utakaofanyika katika huko Lubumbashi Jumapili ijayo, Mazembe watahitaji ushindi wa bao 1-0 ili waweze kujikatia tiketi ya kucheza fainali ya michuano hiyo.

RONALDO ASHINDWA KUIBEBA MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo jana alishindwa kuifungia timu yake bao na kujikuta wakitoa sare ya bila kufungana dhidi ya Malaga na kupoteza nafasi yao ya kuongoza La Liga. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno anahitaji mabao matatu pekee kuipita rekodi ya Raul ya mabao 323 na kuweka rekodi mpya ya ufunguzi. Lakini pamoja na Madrid kumiliki sehemu kubwa ya mchezo wa jana, Ronaldo alishindwa kabisa kutikisa nyavu huku akikosa bao la wazi katika dakika za majeruhi. Malaga ilibidi wafanye kazi ya ziada kujilinda katika dakika 13 za mwisho baada ya Nordin Amrabat kulimwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko beki wa Madrid Marcelo. Ronaldo mwenye umri wa miaka 30 ametumia mechi 306 alizocheza kufunga mabao 321 wakati Raul yeye alitumia mechi 741 alizocheza kuweka rekodi yake.

Friday, September 25, 2015

NEYMAR AKIRI KUFANYA MAZUNGUMZO NA UNITED.

MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Neymar amethibitisha kufanya mazungumzo na Manchester United lakini hakuna ofa yeyote iliyotolewa. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil, ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Barcelona akifunga mabao 22 msimu uliopita na kupelekea kunyakuwa mataji matatu alikuwa akihuishwa na tetesi za kwenda United waliokuwa wakihitaji mshambuliaji kabla ya kumsajili Anthony Martial. Akihojiwa kuhusiana na hilo na ESPN Neymar amesema ni kweli kulikuwa na mazungumzo lakini hakuna ofa yeyote iliyowekwa mezani na United. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 aliongeza kuwa lengo lake kubwa ni kubakia Barcelona na kushirikiana na wenzake kunyakuwa mataji mengi kadri wawezavyo. Barcelona ambao wataikaribisha La Palmas kesho katika mchezo wa La Liga wanashika nafasi ya tano katika msimamo kufuatia kipigo cha mabao 4-1 walichopata kutoka kwa Celta Vigo.

GUARDIOLA AVUNJA MKUTANO BAADA YA KUTWANGWA SWALI KUHUSU UINGEREZA.

MENEJA wa Bayern Munich, Pep Guardiola ameukacha mkutano wake na wanahabari leo baada ya mwandishi kumuuliza kama atakuja kuwa kocha ajae wa timu ya taifa ya Uingereza. Gazeti la The Sun limedai kuwa Chama cha Soka cha Uingereza-FA kinamuwinda kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 kuja kuchukua nafasi ya Roy Hodgson ambaye ataachia nafasi hiyo baada ya michuano ya Euro mwakani kama nchi hiyo itashindwa katika kampeni zake. Pia mustakabali wa Guardiola katika klabu hiyo umekuwa shakani kutokana na ukweli kuwa mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu huku mazungumzo na mkataba yakiwa bado kuanza. Lakini alipohojiwa kuhusiana na taarifa hizo z kutakiwa na FA Guardiola alikataa kujibu huku akiomba swali lingine na lilipokosekana alinyanyuka na kuondoka zake akiwaacha wanahabari wakimkodolea macho. Mapema wiki hii Ofisa Mkuu wa bayern Karl-Heinz Rummenigge alidai kuwa wamemtengea fungu nene Guardiola ili aweze kubakia katika klabu hiyo.

PELE AMFUNDA DIEGO COSTA.

NGULI wa soka wa Brazil, Pele amesema tabia aliyoonyesha mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa katika mchezo dhidi ya Arsenal wiki iliyopita inatoa taswira mbaya kwa soka na kupeleka ujumbe mbaya kwa watoto. Pele alitoa kauli hiyo katika shughuli ya maonyesho ya sanaa jijini London kuelekea kusherekea miaka 75 ya kuzaliwa kwake. Nguli huyo alikaririwa na gazeti la Daily Telegraph akidai kuwa tukio la Costa halitoi ujumbe mzuri kwa watoto na sio nzuri kwa mchezo wa soka lakini ni kosa moja. Pele pia aliongeza kuwa angeweza kucheza soka Ulaya badala ya kubakia Santos karibu miaka yake yote ya soka kwasababu siku hizi sio mchezaji anayeamua ni wakala wake. Pele anatarajiwa kutimiza umri wa miaka 75, Octoba mwaka huu.

RODGERS KIKAANGONI LIVERPOOL.

BEKI wa zamani wa Liverpool, Mark Lawrenson amedai kuwa siku kumi zijazo zitakuwa ngumu kwa meneja Brendan Rodgers. Liverpool ilipata ushindi wa matuta 3-2 dhidi ya klabu ya daraja la pili ya Carslisle, baada ya timu hizo kwenda sare katika muda wa kawaida kwenye mchezo wa Kombe la Ligi. Klabu hiyo katika siku 10 zijazo inakabiliwa na michezo miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Aston Villa na Everton na Lawrenson amesema Rodgers yuko katika hatari kubwa huku kikosi chake kikikosa hamasa. Lawrenson aliendelea kudai kuwa hapendi kuona mameneja wakitimuliwa lakini kwa mwenendo wa Liverpool sio siri kibarua cha kinaweza kuwa shakani kama asipofanya vyema katika mechi zake zijazo. Naye Rodgers akihojiwa amedai kuwa hatishwi na minong’ono kwamba kibarua chake kiko shakani yeye anachotizama ni kufanya kazi yake kwa ufasaha ili kikosi chake kipate matokeo mazuri.

NUSU FAINALI YA LIGI YA MABINGWA AFRIKA KUANZA KUTIMUA VUMBI KESHO.


MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika inatarajiwa kuendelea mwishoni mwa wiki hii kwa mechi za mkondo wa kwanza za nusu fainali kuanza kutimua vumbi. Kesho vigogo wa soka wa Sudan Al Merreikh wataikaribisha TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC. Mazembe ambao ni mabingwa mara nne wa michuano hiyo, walipata nafasi hiyo kwa kumaliza wakiwa vinara wa kundi A wakati wenzake Al Merreikh wao walimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya ASM Alger katika kundi B. Mchezo huo utakuwa ni nafasi kwa kocha wa Al Merreikh Diego Garzitto kukutana tena na klabu yake ya zamani ambayo aliiongoza kunyakuwa taji la michuano hiyo mwaka 2009. Mara baada ya mchezo huo wa kesho timu hizo zitarudiana tena jijini Lubumbashi Octoba 2 mwaka huu.

VALCKE AWEKWA KITANZINI.

WAENDESHA mashitaka wa Uswisi wamethibitisha kwamba Shirikisho la Soka Duniani-FIFA limekubali kuweka wazi akaunti ya barua pepe mali ya katibu mkuu wa shirikisho Jerome Valcke. Valcke alisimamishwa kibarua chake hicho wiki iliyopita kufuatia madai kwamba alihusika katika mpango wa kuuza tiketi za Kombe la Dunia kwa thamani ya juu. Wanasheria wa Valcke wamekanusha madai ya mteja wao kuhusika katika tukio hilo. Maafisa wa Uswisi wameanzisha uchunguzi wa rushwa sambamba na idara moja ya Haki ya Marekani, ambayo ina washitaki maafisa kumi wa soka kwa tuhuma za rushwa.

WENGER AKIRI KUMTUMIA MAPEMA SANCHEZ.


MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri Alexis Sanchez ameanza taratibu msimu huu lakini amesisitiza kiwango cha nyota huyo wa kimataifa wa Chile kitaimarika. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Barcelona aliisaidia kwa kiasi kikubwa Arsenal msimu uliopita akifunga mabao 25 lilikiwemo moja katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA ambao walishinda mabao 4-0 dhidi ya Aston Villa. Baada ya kuisaidia Chile kupata mafanikio katika michuano ya Copa America iliyofanyika kwao majira ya kiangazi, Sanchez amekuwa akisuasua kurejea katika kiwango chake toka kuanza kwa msimu huu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 mpaka sasa hajafunga bao lolote pamoja na kuwa mchezaji aliyepiga mashuti mengi kuliko mchezaji yeyote wa Ligi Kuu. Akihojiwa kuhusiana na hilo Wenger alikiri Sanchez kutokuwa katika kiwango chake lakini alimtetea akidai kuwa alimtumia mapema na anaamin taratibu atarejea katika ubora wake uliozoeleka.

Thursday, September 24, 2015

UONGOZI WA BEKI3 UNAWATAKIA WASOMAJI WAKE WOTE HERI YA SIKUKUU YA EID EL HADJ.


MZUNGUKO WA NNE CARLING CUP: ARSENAL KUIVAA SHEFFIELD, CITY VS PALACE, CHELSEA VS STOKE.

KLABU ya Arsenal intarajiwa kuwa mgeni wa timu ya daraja la pili ya Sheffield Wednesday katika mchezo wa mzunguko wa nne wa michuano ya Kombe la Ligi. Wednesday walipata bahati ya kusonga mbele kufuatia kuichapa Newcastle United bao 1-0 katika Uwanja wa St James Park huku Arsenal wao wakiwaondosha majirani zao Tottenham Hotspurs kwa kuwafunga mabao 2-1. Baada ya kupenya kwa matuta dhidi ya timu ya daraja la nne ya Carlisle, Liverpool wao sasa watakutana na Bournemouth ambao wamepanda Ligi Kuu msimu huu. Kwa upande mwingine vinara wa Ligi Kuu Manchester City wao wataivaa Crystal Palace, wakati mabingwa watetezi wa michuano hiyo Chelsea wao watakuwa wageni wa Stoke City. Manchester United wao watakuwa wenyeji wa Middlesbrough baada ya kuichapa Ipwich Town kwa mabao 3-0.

BAYERN YAMTENGEA FUNGU NENE GUARDIOLA.

OFISA mkuu wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge amebainisha klabu hiyo imemtengea ofa nono Pep Guardiola na wana uhakika kocha huyo atasaini mkataba mpya na mabingwa hao wa Bundesliga. Mkataba wa sasa wa Guardiola unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu na mpaka sasa hakuna mazungumzo yeyote yalioanza jambo ambalo linazua tetesi za uwezekano wa kocha huyo kuondoka. Pamoja na hayo, Rummenigge anaamini meneja huyo wa zamani wa Barcelona atapata wakati mgumu ofa nono waliyomtengea. Rummenigge amesema ana uhakika Guardiola ataongeza mkataba mwingine kwani fungu walilomtengea ni kubwa na hadhani kama anaweza kulikataa.

BARUA PEPE ZA VALCKE KUPEKULIWA.

WACHUNGUZI wa Switzerland wamelitaka Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuwapa kibali cha kupekua barua pepe za katibu mkuu wa shirikisho hilo aliyesimamishwa Jerome Valcke. Baadhi ya magazeti yamekuwa yakimtuhumu Valcke mwenye umri wa miaka 54, kuuza tiketi za Kombe la Dunia kwa bei ya juu tofauti iliyopangwa. Toka wakati huo Valcke amesimamishwa kibarua chake hicho akipisha uchunguzi. Katika taarifa ya kamati inayoongoza uchunguzi huo imedai kuwa wanataka kibali toka FIFA kwani kwasasa barua pepe hizo zitakuwa chini yao. Valcke raia wa Ufaransa ambaye ameshikilia wadhifa huo toka mwaka 2007 amekanusha madai hayo.

TOURE AWASIF KINA DE BRUYNE NA STERLING.

KIUNGO Yaya Toure anaamini Manchester City sasa wana kikosi kinachovutia zaidi Ulaya kufuatia usajili wa majira ya kiangazi wa Kevin De Bruyne na Raheem Sterling. City wanaongoza Ligi Kuu kwa tofauti ya alama mbili baada ya kucheza michezo sita huku wakitumia karibu paundi milioni 100 kununua wachezaji wapya. Wawili kati ya wachezaji walionunuliwa tayari wameshaanza kuonyesha makali yao na Toure amewamwagia sifa kwa kuipa timu hiyo chaguo zaidi katika safu ya ushambuliaji. Toure amesema De Bruyne ni mchezaji mwenye kipaji cha kipekee kwani ana uwezo wa kutengeneza nafasi za mabao huku na yeye mwenyewe akifunga kama alivyofanya katika mchezo wao dhidi ya Sunderland. Kiungo huyo aliendelea kudai kuwa pia yupo Sterling na Sergio Aguero kitendo ambacho kinafanya safu yao ya ushambuliaji kuwa hatari zaidi kwasasa.

MOURINHO AIKOSOA FA.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho amekikosoa Chama cha Soka cha Uingereza-FA kufuta kadi nyekundu aliyopewa beki wa Arsenal Gabriel. Beki huyo alilimwa kadi nyekundu kwa kosa la kumkwatua Diego Costa kwa nyuma katika ushindi wa mabao 2-0 iliyopata Chelsea dhidi ya Arsenal. Akihojiwa kuhusiana na hilo Mourinho amesema sasa wanafahamu kuwa kitendo cha kulipiza kisasi kinaruhusiwa kutokana na hatua zilizochukuliwa na FA. Kocha huyo pia aligoma kuzungumzia adhabu ya mechi tatu aliyopewa Costa akidai kuwa kama akifanya hivyo adhabu kubwa dhidi yake ingekuwa ikimsubiri. Kwa upande wake meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema FA wametatua tatizo hilo kwa asilimia tano.

MASHABIKI WA ARSENAL WASHITAKIWA KWA KUBOMOA BANGO LA SPURS.

SEHEMU ya upande wa jukwaa la mashabiki wa Arsenal inetarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa polisi na Chama cha Soka cha Uingereza-FA baada ya bango kung’olewa katika Uwanja wa White Hart Lane jana. Baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo baina ya timu hiyo dhidi ya wenyeji wao Tottenham Hotspurs, mashabiki walianza kung’oa mabango yaliyokuwa yamebandikwa upande wa jukwaa walilokuwa wamekaa na kulazimisha polisi na wasimamizi wa uwanja kuingilia kati kuwatawanya. Polisi wamethibitisha kuwa watu 10 wamekamatwa kuhusiana na tukio na wanatarajiwa kufunguliwa mashitaka kwa vurugu hizo. Msemaji wa Arsenal amesisitiza kuwa klabu itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika katika uchunguzi wowote utakaofanyika. Katika mchezo huo Arsenal walifanikiwa kuwafunga majirani zao hao mabao 2-1 ambayo yote yalifungwa na Mathieu Flamini.

BARCELONA WACHEZEA KICHAPO KIKALI KUTOKA CELTA VIGO.

KLABU ya Barcelona jana ilipokea kipigo kizito cha kwanza katika La Liga wakiwa chini ya meneja Luis Enrique kufuatia Celta Vigo kutibua rekodi yao ya kutofungwa msimu huu. Mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Iago Aspas alifunga mabao mawili baada ya Nolito kufunga bao la kuongoza wakati la mwisho likifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Manchester City na Stoke City John Guidetti. Bao la kufutia machozi la Barcelona lilifungwa na Neymar na kuifanya timu hiyo kupoteza mchezo wa kwanza kati ya michezo 25 ya La Liga waliyocheza. Akihojiwa baada ya mchezo huo Enrique amesema kikubwa kilichoamua mchezo huo ni jinsi Celta Vigo walivyocheza kwa umahiri mkubwa kuliko wao. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa walijaribu kutengeneza nafasi lakini walikuwa hawakujipanga vyema kwani wapinzani wao walikuwa bora zaidi yao.

Wednesday, September 23, 2015

RAFINHA AICHOMOLEA BRAZIL.

BEKI wa Bayern Munich, Rafinha amekataa wito wa kwenda katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil ambacho kinakabiliwa na mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2018, baadae mwezi ujao. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 alikuwa akitarajiwa kuiwakilisha nchi yake kwa mara ya kwanza toka Machi mwaka 2014, wakati kocha wa zamani Luiz Felipe Scolari alipomjumuisha katika kikosi ambacho kilipamban ana Afrika Kusini jijini Johanessburg. Sambamba na nyota wa Real Madrid Danilo na Dani Alves wa Barcelona, Rafinha alipata nafasi ya kuita kwa mara ya kwanza na kocha wa sasa Dunga wiki iliyopita huku akionekana kufurahia wito huo. Lakini beki huyo wa zamani wa klabu za Schalke na Genoa alilishangaza Shirikisho la Soka la Brazil-CBF kwa kugeuka ghafla na kukataa wito huo hivyo hatakuwepo katika mechi dhidi ya Chile na Venezuela. Rafinha alifafanua kuwa sio mchezaji tegemeo sana kwa nchi yake kwani kuna wachezaji wengine wanaoweza kucheza nafasi yake vyema ndio maana ameamua kukataa wito huo ili kuongeza nguvu zaidi kwa klabu yake.

IBRAHIMOVIC AANZA TAMBO BAADA YA KUFUNGA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Paris Saint-Germain-PSG, Zlatan Ibrahimovic amesema atahitaji muda zaidi wa kucheza mara kwa mara kama anataka kurejea katika kiwango chake bora. Nyota huyo wa kimataifa wa Sweden, mwenye umri wa miaka 33, amekuwa akikosolewa kufuatia kuanza msimu akiwa katika kiwango cha chini. Majeruhi tayari yamemfanya kukosa michezo minne ya ligi lakini baada ya kupona na kupata nafasi alifunga bao lake la kwanza jana katika ushindi wa mabao 3-0 waliopata PSg dhidi ya Guinamp. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Ibrahimovic amesema anashukuru kwasababu ameanza kurejea katika kiwango chake taratibu ingawa bado anahitaji mechi nyingi zaidi ili arejee katika ubora wake. PSG wanatarajiwa kusafiri kuifuata Nantes Jumamosi hii kabla ya kuifuata Shakhtar Donetsk katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki ijayo.