GOLIKIPA Iker Casillas amedai ushindi wamabao 2-1 iliyopata FC Porto dhidi ya Chelsea haukumpa furaha ya ziada kwasababu alishasahau na kusamehe mgogoro na kocha wake wa zamani Jose Mourinho. Casillas na Mourinho walifanya kazi pamoja kwa miaka mitatu katika klabu ya Real Madrid kati ya mwaka 2010 na 2013 ambapo katika kipindi hicho walikuwa hawana maelewano mazuri mpaka kufikia hatua ya Casillas aliyekuwa nahodha kuwekwa benchi. Mourinho alikuwa akiamini kuwa Casillas alikuwa akimhujumu kwa kuvujisha mipango yake katika vyombo vya habari hatua ambayo ilipelekea kuchagua kumtumia golikipa namba mbili Diego Lopez badala yake. Wawili hao jana walikutana tena kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya toka walipoachana Madrid ambapo Porto waliibuka kidedea kwa mabao taliyofungwa na Andre Andre na Maicon huku lile la kufutia machozi la Chelsea likifungwa na Willian. Akihojiwa kuhusiana na hilo Casillas amesema ni kitambo kirefu kimeshapita hivyo alishasahau mgogoro wake na Mourinho lakini jambo muhimu alilofurahia ni timu yake kupata matokeo muhimu katika mchezo huo. Porto sasa wanashika nafasi ya pili katika kundi G wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa na Dynamo Kyiv na Chelsea wanashika nafasi ya tatu wakiwa na alama moja.
No comments:
Post a Comment