Thursday, March 31, 2016

SUNDERLAND YAJIPANGA KUMTIMUA EBOUE.

KLABU ya Sunderland inajipanga kusitisha mkataba wa beki wao Emmanuel Eboue baada ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kumfungia mwaka mmoja kutojishughulisha na masuala ya soka. Beki huyo mwenye umri wa miaka 32 ambaye alijiunga na Sunderland Machi 9 mpaka mwishoni mwa msimu huu, alilimwa adhabu hiyo baada ya kushindwa kulipa fedha alizokuwa akidaiwa na wakala wake wa zamani. Sunderland wamesema katika taarifa yao Eboue hakuifahamisha klabu kuhusiana na suala hilo ambalo lilianza toka Julai mwaka 2013. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast amepewa wiki mbili kukat rufani kupinga adhabu hiyo.

POGBA KUBAKIA JUVENTUS AKIKOSA DAU KUBWA.

WAKALA wa Paul Pogba, Mino Raiola amebainisha kuwa mteja wake huyo yuko tayari kusaini mkataba mpya na Juventus kama hakutakuwa na ofa kubwa mwishoni mwa msimu huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa, mkataba wake wa sasa unamalizika Juni 2019 lakini klabu kama Paris Saint-Germain, Barcelona, Manchester City na Chelsea zinadaiwa kumfuatilia kwa karibu. Pogba mwenye umri wa miaka 23, hana haraka ya kuondoka kwa mabingwa hao wa Serie A na anaweza kusaini mkataba mpya kama hatakubaliana na masharti ya mahali pengine. Akihojiwa Raiola amesema hakuna lililobadilika kwa Pogba kulinganisha na mwaka mmoja uliopita kwani kila kitu kikosi. Wakala huyo aliendelea kudai kuwa kama hakuna ofa nzuri itakayopatikana Pogba atafurahia kuendelea kubakia Juventus na wako tayari kufanya mazungumzo na mkataba mpya.

FERGUSON ADAI LEICESTER WANASTAHILI KUWA MABINGWA LIGI KUU.

MENEJA wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson anaamini Leicester City wanastahili kutawadhwa mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu. Leicester wamekuwa na msimu mzuri 2015-2016 wakiwa wanaongoza ligi kwa tofauti ya alama tano huku wakiwa wamebaki na mechi saba. Msimu uliopita wote ulikuwa wa wasiwasi kwa Leicester kwani walikuwa wakipigania kutoshuka daraja lakini hali imekuwa tofauti kwa mwaka huu. Hata hivyo, kutokana na ari na moyo wa kujituma walioonyesha chini ya Claudio Ranieri msimu huu, Ferguson anadhani hakuna timu inayostahili kushinda taji la ligi zaidi ya Leicester. Akihojiwa Ferguson ambaye alinyakuwa mataji 13 ya ligi akiwa na United amesema kwa uwezo mkubwa walioonyesha Leicester hana shaka kuwa wanastahili kushinda taji hilo.

BILBAO YATHIBITISHA KUWA LAPORTE HATAWEZA KUMALIZA MSIMU.

KLABU ya Athletic Bilbao imethibitisha kuwa beki wake Aymeric Laporte ataukosa msimu wote uliobakia kwasababu ya kufanyiwa upasuaji kufuatia mguu wake uliovunjika wakati akiwa katika majukumu ya kimataifa. Beki huyo mwenye umri wa miaka 21 aliumia mguu wake wa kulia kufuatia kukwatuliwa wakati akikitumikia kikosi cha Ufaransa cha vijana chini ya umri wa miaka 21 dhidi ya Scotland Machi 24 mwaka huu. Bilbao imebainisha kuwa Laporte alifanyiwa upasuaji Jumanne na anatarajiwa kukaa nje kwa miezi minne hivyo kumfanya kukosa mechi zilizosalia msimu huu. Laporte amekuwa akihusishwa na tetesi na kuwania na Manchester City majira ya kiangazi huku taarifa zikidai kuwa meneja ajaye Pep Guardiola ameuweka katika orodha ya wachezaji anaowahitaji.

PIGO BARCELONA, KUMKOSA MATHIEU CLASICO.

BEKI wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Barcelona, Jeremy Mathieu anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa goti kutokana na majeruhi aliyopata wakati akiitumikia nchi yake Jumanne iliyopita. Taarifa ya klabu yake imedai kuwa kufuatia vipimo alivyofanyiwa imebainika kuwa Mathieu anatakiwa kufanyiwa upasuaji huo ili kurekebisha tatizo linalomkabili. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa beki huyo anatarajiwa kufanyiwa upasuaji leo na madaktari wa klabu hiyo Ramon Cugat na Ricard Pruna. Mathieu mwenye umri wa miaka 32 alitolewa wakati wa mapumziko katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki ambao Ufaransa ilishinda mabao 4-2 dhidi ya Urusi huko Stade de France. Sasa beki huyo anatarajiwa kuukosa mchezo wa Clasico dhidi ya Madrid mwishoni mwa wiki hii huku kukiwa na wasiwasi pia wa kutokucheza kabisa msimu huu.

RAMOS ATAMBA WATALIPA KISASI KWA BARCELONA.

BEKI wa Real Madrid, Sergio Ramos ana uhakika kikosi chao kinaweza kulipa kisasi dhidi ya mahasimu wao Barcelona wakati watakapokutana Jumamosi hii. Madrid walitandikwa mabao 4-0 katika mchezo wao wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Bernabeu ambapo Luis Suarez alifunga mabao mawili na Neymar na Andres Uniesta wakifunga moja kila mmoja. Madrid walio chini ya Zinedine Zidane wamekuwa na msimu mgumu katika kampeni zao za La Liga ambapo kwasasa wako nyuma ya Barcelona kwa alama 10. Ramos pamoja na kikosi kizima cha Barcelona hawajashinda mchezo wa ligi nyumbani kwa Barcelona Camp Nou kw karibu miaka minne lakini nyota huyo wa kimataifa wa Hispania ana uhakika wanaweza kujirudi na kushinda mchezo huo.

HODGSON AHAHA KUTAFUTA BEKI WA KATI, ATETA NA TERRY.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amezungumza na John Terry wakati akiendelea kutafuta beki wa kati anayetumia mguu kushoto katik kikosi chake kuelekea michuano ya Euro 2016. Kikosi cha Uingereza kimefunga mabao manne katika mechi mbili za kimataifa za kirafiki zilizopita ambapo walishinda mabao 3-2 ugenini dhidi ya Ujerumani kabla ya kuchapwa mabao 2-1 nyumbani na Uholanzi. Gary Cahill na Chris Smalling ndio walioanza katika safu ya ulinzi katika mchezo wa Berlin kabla ya baadae kuungana na John Stones katika mchezo wa Wembley. Lakini beki wa kati imekuwa nafasi ambayo bado inalegalega katika kikosi cha Hodgson kuelekea michuano hiyo ya Ulaya mabapo Uingereza imepangwa sambamba na Urusi Wales na Slovakia katika kundi B.

Wednesday, March 30, 2016

MADRID WAJIPANGA KUFANYA KUFURU KWA AUBAMEYANG.

KLABU ya Real Madrid inadaiwa kujipanga kutoa ofa ya euro milioni 70 pamoja na Alvaro Morata ili waweze kumnasa mshambuliaji wa Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang. Jarida la AS limedai kuwa Madrid bado wana nafasi ya kumsajili tena Morata kutoka Juventus kwa euro milioni 30, lakini wanatarajia kumtumia nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 ili waweze kumpata Aubameyang. Nyota huyo wa kimataifa wa Gabon amekuwa katika kiwango cha juu msimu huu akifunga mabao 35 katika mechi 40 za mashindano alizoichezea Dortmund msimu huu. Mapema wiki hii, Aubameyang ambaye pia amehusishwa na tetesi za kuwindwa na Arsenal, alikiri kuwa anaweza kukubali kujiunga na Madrid kama wakimuhitaji lakini alidai kwasasa bado ana mkataba na Dortmund unaomalizika 2020.

TEVEZ AKIRI KUKARIBIA KUJIUNGA NA ATLETICO KABLA YA KWENDA BOCA.

MSHAMBULIAJI wa Boca Juniors, Carlos Tevez amekiri alikaribia kujiunga na Atletico Madrid wakati alipoondoka Juventus mwishoni mwa msimu uliopita, lakini aliamua kurejea nyumbani. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina, alicheza misimu miwili Juventus na kushinda mataji mawili ya Serie A na kuisaidia kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Tevez alikuwa ameshaweka nia ya kurejea Argentina lakini amesema alipitiwa na wazo la kutaka kucheza Atletico chini Muargentina mwenzake Diego Simeone. Akihojiwa Tevez amesema Simeone alimpigia simu na alifurahia mawazo yake lakini hakuweza kuikatalia Boca Juniors.

HODGSON ADAI WACHEZAJI WAKE WALIKOSA UBUNIFU.

MENEJA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amesema amesikitishwa kutokana na kikosi chake kukosa ubunifu kufuatia kichapo cha mabao 2-1 walichopata kutoka kwa Uholanzi katika Wembley jana. Kipigo hicho kimekuja siku baada ya Uingereza kuionyesha kiwango bora wakitoka nyuma na kuwafuunga mabingwa wa dunia Ujerumani mabao 3-2. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Hodgson amesema pamoja na kumiliki vyema mpira lakini wachezaji wake hawakuwa wabunifu jambo lilichangia kutotengeneza nafasi za kutosha. Meneja huyo aliongeza kuwa hawakucheza vyema sana kama ilivyokuwa katika mchezo dhidi ya Ujerumani kule Berlin. Hicho kinakuwa kipigo cha kwanza kwa Uingereza katika Uwanja wa Wembley toka Novemba mwaka 2013.

MESSI AIBEBA ARGENTINA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi amefunga bao lake la 50 la kimataifa wakati akiisaidia Argentina kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Bolivia katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2018. Ushindi unaifanya Argentina kukwea mpaka nafasi ya tatu katika kundi lao wakiwa na alama 11 kutokana na mechi sita, alama mbili nyuma ya vinara Ecuador na Uruguay. Ecuador wao walipoteza mchezo wao wa kwanza katika kundi hilo wakifungw amabao 3-1 na Colombia wakati Uruguay walishinda bao 1-0 nyumbani dhidi ya Peru. Beki wa Argentina, Gabriel Mercado ambaye alifunga bao la ushindi katika mchezo wa Alhamisi iliyopita dhidi ya Chile ndio aliyefunga bao kuongoza dakika ya 21 katika mchezo huo kabla ya Messi hajafunga lingine kwa penati. Paraguay na Brazil wote wana alama tisa baada ya kutoka sare ya kufunga mabao 2-2 huko Asuncion jana. Timu nne za juu kati ya 10 zilizopo katika kundi hilo la nchi za Amerika Kusini ndio zitafuzu moja kwa moja fainali hizo za Kombe la Dunia wakati ile ya tano itakwenda katika hatua ya mtoano.

MOROCCO WAMEKUWA WA KWANZA KUFUZU AFCON.

MOROCCO imekuwa nchi ya kwanza kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika mwakani nchini Gabon baada ya kuichapa Cape Verde mabao 2-0 huko Marrakech jana. Mshambuliaji nyota wan chi hiyo Youssef Al Arabi alifunga mabao hayo mawili mapema katika kipindi cha pili, bao moja likitokana na penati ambayo ilipelekea mchezaji wa Cape Verde kupewa kadi nyekundu. Morocco wamefikisha alama sita katika kundi F wakiongoza huku kukiwa kumebaki na mechi mbili hatua hiyo kukamilika. Mfaransa Herve Renard ambaye aliiongoza Zambia na Ivory Coast kunyakuwa taji la michuano hiyo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ndio aliyechukua mikoba ya kuinoa Morocco kutoka kwa Badou Zaki. Misri na Senegal nazo zinakaribia kufuzu michuano hiyo inayoshirikisha nchi 16 wakati Nigeria hali yao imekuwa mbaya pamoja na Afrika Kusini. Ushindi wa bao 1-0 waliopata Misri huko Alexandria umewafanya kujiimarisha kileleni mwa kundi G wakati Senegal nao walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Niger katika mchezo wa kundi K.

PELE AWASHITAKI SAMSUNG.

NGULI wa soka wa Brazil, Pele ameishitaki kampuni ya vifaa vya elektroniki ya Samsung akiidai fidia ya dola milioni 30 akiituhumu kampuni hiyo kutumia picha yake katika matangazo bila ruhusa yake. Kwa mujibu wa malalamiko yaliyopelekwa katika mahakama ya rufaa jijini Chicago, Samsung wanatuhumiwa kutumia picha inayofanana na nguli huyo katika tangazo lake huku kukiwa hakuna makubaliano yeyote baina yao. Pele mwenye umri wa miaka 75 ambaye jina lake kamili ni Edson Arantes do Nascimento, anahesabiwa kama mmoja wa wachezaji bora kabisa kuwahi kutokea duniani. Pamoja na kwamba tangazo hilo halimtaji Pele moja kwa moja lakini picha iliyotumika inadaiw kufanana kwa kila kitu na nguli huyo.

VILLA MAJANGA, GARDE AONDOKA.

MENEJA wa Aston Villa Remi Garde amejizulu wadhifa wake kwa maelewano baada ya kuinoa klabu hiyo kwa siku 147. Meneja huyo raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 49 alichukua mikoba ya Tim Sherwood akisaini mkataba wa miaka mitatu na nusu na klabu hiyo Novemba mwaka jana, lakini ameondoka baada ya kupokea vipigo sita mfululizo. Mechi ya mwisho kusimamia ilikuwa ile waliyochapwa bao 1-0 na Swansea Machi 19 mwaka huu, matokeo ambayo yameiacha Villa wakiburuza mkia huku wakidaiwa alama 12 ili waweze kujinasua kutoka nafasi hiyo. Villa wameshinda mechi mbili pekee kati ya 20 za ligi walizocheza chini ya Garde.

YAYA TOURE KUONDOKA MAN CITY.

WAKALA wa Yaya Toure, Dimitri Seluk amedai kuwa kiungo huyo anajiandaa kuondoka Manchester City na tayari wameshaanza mazungumzo na vilabu kadhaa Ulaya. Seluk aliwaonya City kuwa Toure ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu ujao, anaweza kuondoka labda wampe ofa ya mkataba mwingine kabla ya kumalizika kwa msimu. Lakini hakuna ofa yeyote aliyopewa nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast jambo ambalo limemfanya kuanza kutafuta mahali pengine huku klabu za Paris Saint-Germain, Bayern Munich na Juventus zikitajwa kumuwania. Seluk amesema tayari wameshaanza kuzungumza na vilabu vingine ili kujua wapi Toure ataelekea baada ya msimu kumalizika.

Monday, March 28, 2016

WALIOKATA TIKETI KURUDISHIWA FEDHA ZAO.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kuwarudishia fedha zao kesho Jumanne, wapenzi wa mpira wa miguu waliokuwa wameshakata tiketi za kushuhudia mchezo wa kundi G kati ya Tanzania v Chad jijini Dar es salaam. TFF inawaomba washabiki wa mpira wa miguu waliokua wamekata tiketi za mchezo huo, kufika kesho Jumanne saa 5 kamili asubuhi katika vituo walivyonunulia wakiwa na tiketi zao ili waweze kurudishiwa fedha zao. Zoezi la kuwarudishia fedha washabiki waliokuwa wameshakata tiketi za mchezo kati ya Tanzania v Chad litafanyika katika vituo vinne vilivyokua vikiuza tiketi siku ya Jumapili, hivyo wenye tiketi za mchezo huo wanaombwa kufika na tiketi zao ili waweza kurudishiwa fedha zao. Aidha TFF inawaomba radhi watanzania na wapenzi wa mpira wa miguu kwa usumbufu uliojitokeza na kuwataka kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki ambacho wanasubiria taarifa zaidi kutoka CAF. Chad imejiondoa jana katika kinyanganyiro cha kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) nchini Gabon mwaka 2017, ambapo iliku kundi G na timu za Misri, Nigeria pamoja na Tanzania.

WEST HAM KUMUWANIA IBRAHIMOVIC KIANGAZI.

KLABU ya West Ham United imethibitisha kutaka kumuwania Zlatan Ibrahomovic majira ya kiangazi lakini mmiliki mwenza wa timu hiyo David Sullivan hana uhakika kama Paris Saint-Germain watakuwa tayari kumuachia. Mshambuliaji huyo ambaye amefunga mabao 102 katika mechi 116 alizocheza Ligue 1, anatarajiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu na anategemewa kuondoka baada ya kushinda mataji manne katika kipindi miaka minne aliyokuwepo Ufaransa. Klabu za Ligi Kuu zimekuwa zikihusishwa kumuwania huku Ibrahimovic mwenyewe akielezea kuihusudu ligi hiyo na sasa West ham wamejitokeza hadharani kuonyesha kumuhitaji. Akihojiwa Sullivan amesema wana orodha ya karibu washambuliaji 10 kutoka sehemu mbalimbali Ulaya na fedha zao nyingi zaidi katika usajili zitakwenda kusajili mshambuliaji. Tajiri huyo aliendelea kudai kuwa anampenda Ibrahimovic na watajaribu kumsajili kama PSG wataamua kumuachia.

MOURINHO ADAIWA KUANZA MIKAKATI YA USAJILI MAN UNITED.

MENEJA wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho anadaiwa kuwa tayari ameshaanza mipango yake akiwa na Manchester United kama atachukua nafasi ya Louis van Gaal na anataka kusajili nyota watatu kwa mujibu wa jarida la Don Balon. Jarida la Hispania limedai kuwa Mourinho ameshaanza mipango ya usajili kwa kuweka wachezaji kadhaa nyota katika orodha yake akiwemo mshambuliaji wa Napoli Gonzalo Higuain, kiungo wa Real Madrid James Rodriguez na mshambuliaji wa Juventus Alvaro Morata. Mourinho ameshawahi kufanya kazi na Higuain wakati akiwa Madrid na United wameonyesha kuwa tayari ingawa watalazimika kulipa kitita cha paundi milioni 58 kwa ajili ya kumnasa nyota huyo wa kimataifa wa Argentina. United pia watakabiliwa na upinzani kwa Morata ingawa Madrid wako tayari kumnunua tena kama mkataba unavyotaka ili waje kumuuza kwa kiwango cha juu wakati Rodriguez yeye anatarajiwa kuondoka kiangazi kutokana na kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza.

NYARAKA ZAFUJA, BARCELONA BADO WANAILIPA LIVERPOOL KWA SUAREZ.

KLABU ya Barcelona inadaiwa bado inaendelea kuilipa Liverpool kutokana na mauzo ya Luis Suarez ambapo malipo ya mwisho yanatarajiwa kufanywa Julai mwaka huu. Mtandao wa Football Leakes umekuwa ukitoa nyaraka muhimu zilizohusisha usajili wa wachezaji nyota akiwemo Gareth Bale, Mesut Ozil na Anthony Martial kwa kipindi cha miezi kadhaa na sasa wamehamia katika usajili wa Suarez kwenda Barcelona. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay alihamia Camp Nou mwaka 2014 kipindi kifupi baada ya kusababisha utata mkubwa kwa kumng’ata beki wa Italia Giorgio Chiellini katika Kombe la Dunia. Nyaraka zilizovuja zinaonyesha Liverpool walikuwa na nia ya kuachana na mshambuliaji huyo haraka kutokana na tukio alilofanya tofauti ya dili zingine nyingi zinazohusiana na masuala hayo ya usajili. 
Taarifa kwenye nyaraka hizo zimeonyesha kuwa hakukuwa na masharti yeyote yaliyoweka kama ada ya kununulia au malipo mengine ya ziada kama Barcelona wakishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Badala yake ilikuwepo ada ya moja kwa moja ya paundi milioni 64.98 kwa ajili ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 ambaye katika kipindi hicho alikuwa amefungiwa miezi minne, na ilitakiwa kulipwa kwa kidogo kidogo kwa kipindi kwa awamu tano. Kila awamu Barcelona walitakiwa kulipa kiasi cha paundi milioni 13, wakianza majira ya kiangazi alipouzwa na sasa klabu hiyo inatarajia kumaliza awamu yake ya mwisho Julai 31 mwaka huu. Kiwango hicho cha ada kilichovuja kinathibitisha kuwa Suarez ni mchezaji wan ne ghali katika historia ya soka akiachwa kwa karibu na nyota mwenzake wa Barcelona Neymar na nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo na Gareth Bale.

ARSENAL BADO INA NAFASI YA KUTWAA LIGI KUU - OZIL.

KIUNGO mahiri wa Arsenal, Mesut Ozil ana uhakika kikosi chao bado kiko katika mbio za kufukuzia taji la Ligi Kuu pamoja na kuwa nyuma ya vinara Leicester City kwa alama 11 huku wakiwa wamebaki na mechi nane za kucheza. Arsenal walikuwa wakiongoza ligi mwanzoni mwa mwaka huu lakini wameteleza mpaka nafasi ya tatu baada ya kushinda mechi tatu kati ya 10 za mwisho walizocheza. Pamoja na pengo kubwa lililopo, Ozil bado anaamini Arsenal wanaweza kuwafukuzia vinara hao ingawa amekiri kuwa hawapaswi kufanya makosa mengine zaidi kama wanataka kurejea kileleni. Akihojiwa akiwa katika majukumu ya kimataifa na Ujerumani, Ozil hadhani kama kuna kitu kinashindikana pamoja na kuwa michezo imebaki michache kwani Leicester bado ana kibarua cha kukutana na timu kubwa.

ISCO AWAZODOA JUVENTUS.

MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Isco amesisitiza anafuraha kuitumikia timu hiyo kufuatia tetesi zilizozagaa zikimhusisha na yeye kwenda Juventus. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alikuwa akiripotiwa kuwindwa na mabingwa hao wa Serie A sambamba na nyota wa Paris Saint-Germain Edinson Cavani. Hata hivyo, akiwa amebakia na misimu miwili katika mkataba wake, Isco amesema hana mpango wa kuondoka Santiago Bernabeu katika kipindi cha karibuni. Isco aliongeza kuwa anafurahia kuwepo Madrid na anataka kumaliza mkataba wake mpaka mwisho halafu ndio ataona kitu atafanya baada ya hapo.

PELLEGRINI KUENDELEA KUBAKIA UINGEREZA.

MENEJA wa Manchester City anayeondoka, Manuel Pellegrini amedokeza kuwa anaweza kubakia katika Ligi Kuu msimu ujao kama akipata klabu ambayo itakuwa na mipango mizuri. Meneja huyo raia wa Chile nafasi yake inatarajiwa kuchukuliwa na Pep Guardiola majira ya kiangazi na amekuwa akihusishwa na kwenda katika vilabu kadhaa ikiwemo Valencia, Zenit St, Petersburg na Arsenal. Pellegrini amesema anaweza kubakia Uingereza sababu kubwa ikiwa ni fungu kubwa wanalopata klabu ambalo linaruhusu hata zile ndogo kama Leicester City nazo kushindania taji. Meneja huyo aliongeza kuwa klabu zote Uingereza zina fedha na mipango mizuri ndio maana kila meneja anapenda kuja kufundisha humo.

HODGSON AMKINGIA KIFUA ROONEY BAADA YA VIJANA KUMFUNIKA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amesisitiza nahodha wake Wayne Rooney bado yuko katika mipango yake kuelekea katika michuano ya Euro 2016 hata kama kikosi chake kiliwafunga mabingwa wa dunia Ujerumani bila uwepo wake. Mshambuliaji huyo wa Manchester United aliachwa katika kikosi cha Hodgson kutokana na majeruhi ya goti wakati Uingereza ilipofanikiwa kutoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ujerumani katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jijini Berlin. Nyota Tottenham Hotspurs Dele Alli mwenye umri wa miaka 19 ndio alikuwa nyota wa mchezo na ushiriano wake na Harry Kane ndio uliochangia kwa kiasi kikubwa Uingereza kurejea mchezoni. Mbali na hao lakini moto alioonyesha mshambuliaji wa Leicester City Jamie Vardy nao umeongeza shinikizo katika nafasi ya Rooney kwenye kikosi cha kwanza cha nchi hiyo. Hata hivyo, Hodgson amempoza Rooney akisisitiza kuwa bado nahodha huyo yuko katika mipango yake kwani amekiongoza kikosi chake vyema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

SEAMAN AWAONYA ARSENAL KUHUSU WENGER.

KIPA wa zamani wa Arsenal, David Seaman amesema klabu hiyo inapaswa kubaki na meneja Arsene Wenger kwasababu wanaweza kuhatarisha kupitia matatizo kama yaliyowakuta Manchester United kufuatia kuondoka meneja wao mzoefu Sir Alex Ferguson. Wenger amekuwa chini ya shinikizo baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA huku kukiwa na matumaini finyu ya kutwaa taji la Ligi Kuu kutokana na kuwa nyuma ya vinara Leicester City kwa alama 11. Hata hivyo, Seaman bado anaamini Wenger ndio kocha sahihi kwa klabu hiyo na kumuunga mkono kwa kila anachofanya. Seaman amesema kama Arsenal wakiamua kumtimua Wenger wanaweza kukumbwa na matatizo kama yaliyowakuta United wakati Ferguson alipoondoka.

Sunday, March 27, 2016

LUKAKU MGUU NJE MGUU NDANI EVERTON.

MSHAMBULIAJI nyota wa Everton, Romelu Lukaku amezidi kuongeza uwezekano wa kuondoka katika klabu hiyo baada ya kukiri kuwa angependelea zaidi kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Baba wa nyota huyo aliwahi kuzungumza katika moja mahojiano yake ambapo alidai kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji atajiunga na aidha Manchester United au Bayern Munich mwishoni mwa msimu huu. Lukaku amesema hashangai kuona baba yake akizitaja timu anazozipenda lakini amedokeza kuwa anaweza kuondoka Goodison Park ili atafute timu inayoshiriki michuano ya hiyo mikubwa Ulaya kwa vilabu msimu ujao. Lukaku aliendelea kudai kuwa msimu ujao atatimiza miaka 23 na anadhani itakuwa vyema kama akicheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

MAN CITY YAKUBALIANA NA DORTMUND KWA AJILI YA KUMSAJILI GUNDOGAN.

KLABU ya Manchester City inadaiwa kukubali kutoa kitita cha paundi milioni 25 kwa ajili ya kumnasa nyota wa Borussia Dortmund Ilkay Gundogan. Meneja ajaye Pep Guardiola anaripotiwa kutaka kukijenga upya kikosi cha City ambapo anataka kukamilisha usajili wake pindi michuano ya Euro 2016 itakapoanza. Gundogan ambaye mkataba wake na Dortmund unatarajiwa kumalizika mwaka 2017, anategemewa kusajiliwa wa kwanza wakati mzungumzo ya nyota wa Juventus Paul Pogba yakianza tena pamoja na dau kubwa la Mfaransa huyo. Isco ambaye meneja wa sasa wa City alitaka kumsajili kutoka Malaga kabla ya Real Madrid hawajaingilia na Aymeric Laporte nao pia wametajwa kuwepo katika orodha ya City.

BRENDAN RODGERS KURUDI SWANSEA.

MENEJA wa zamani wa Liverpool, Brendan Rodgers anatarajiwa kuchukua mikoba ya kuinoa Swansea City katika msimu ujao wa Ligi Kuu 2016-2017. Meneja huyo raia wa Ireland ya Kaskazini aliisaidia Swansea kupata daraja mwaka 2011 kabla ya kujiunga na Liverpool mwaka mmoja baadae na kuwaongoza kumalizika katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi msimu 2013-2014. Miaka mitatu ya Rodgers katika Liverpool ilimalizika Octoba mwaka jana kufuatia matokeo mabovu na toka wakati huo aliamua kuchukua mapumziko. Francesco Guidolin ndio meneja wa muda wa Swansea kwasasa baada ya Garry Monk kuachia ngazi Desemba mwaka jana lakini taarifa zinadai kuwa Rodgers ndiye atakayepewa mikoba ya moja kwa moja kuinoa klabu hiyo.

NILICHUKIA KUCHEZA WINGA NIKIWA UFARANSA - HENRY.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Thierry Henry amekiri alikuwa akichukizwa kupangwa kucheza winga katika kikosi cha nchi yake. Henry mwenye umri wa 38, ambaye alistaafu soka mwaka 2014, bado ameendelea kubakia mfungaji bora wa wakati wote katika klabu ya Arsenal na Ufaransa. Lakini pamoja na kuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 1998 na michuano ya Ulaya miaka miwili baadae, Henry amekiri hakuwa akifurahia kucheza nje ya eneo. Henry amesema pamoja na kutofurahia lakini alikuwa akijitahidi kuzoea hali hiyo ili aweze kuisaidia timu.

GOTZE KUMFUATA KLOPP KIANGAZI.

MCHEZAJI nyota wa Bayern Munich, Mario Gotze anadaiwa kuamua kuondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu na kwenda kujiunga na meneja wake wa zamani Jurgen Klopp katika klabu ya Liverpool. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani, ameshindwa kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha Bayern chini meneja anayeondoka Pep Guardiola baada ya kucheza mechi 12 pekee msimu huu. Inaripotiwa kuwa sasa Gotze ameamua kwenda kuungana na Klopp ambaye alicheza chini yake wakati akiinoa Borussia Dortmund na kufanikiwa kushinda mataji mawili ya Bundesliga. Gotze ambaye alibanisha mapema mwezi huu kuwa bado anawasiliana na Klopp kwa kutumia ujumbe mfupi, amebakisha miezi 12 katika mkataba wake na anadaiwa kuwa hataki kusaini mkataba mwingine.

KOCHA WA UINGEREZA AWAPONGEZA WACHEZAJI WAKE KWA KUICHAPA UJERUMANI.KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amesema kutoka nyuma kwa kikosi chake na kuja kushinda mchezo dhidi ya mabingwa wa dunia Ujerumani jana, ilikuwa moja kati ya siku nzuri akiwa kama meneja wa timu hiyo. Bao la dakika za majeruhi lililofungwa na Eric Dier liliwahakikishia ushindi wa mabao 3-2, baada ya Uingereza kutoka nyuma kufuatia kufungwa mabao mawili katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Olimpiki jijini Berlin. Akihojiwa Hodgson amesema pamoja na kwamba ulikuwa mchezo wa kirafiki lakini kikosi chake kilicheza vyema ingawa bado wana safari ndefu ili waweze kuwafikia mabingwa hao wa dunia. Toni Kroos na Mario Gomez ndio waliofunga mabao ya Ujerumani kabla ya Harry Kane na Jamie Vardy aliyeingia akitokea benchi hawajasawazisha. Hodgson alichukua mikoba ya kuinoa Uingereza kutoka kwa kocha aliyejizulu nafasi hiyo Fabio Capello kuelekea katika michuano ya Euro 2012 ambako walitolewa katika hatua ya robo fainali na Italia.

Thursday, March 24, 2016

JABALI LA SOKA LA UHOLANZI NA BARCELONA LAFARIKI.

NGULI wa soka wa zamani wa Uholanzi na Barcelona, Johan Cruyff amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68 kufuatia kusumbuliwa na maradhi ya saratani. Mchezaji huyo wa zamani wa Ajax Amsterdam na Barcelona alitangaza kusumbuliwa na maradhi hayo Octoba mwaka jana akieleza kuwa alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wake, imedai kuwa Cruyff alifariki dunia leo akiwa amezungukwa na familia yake hospitalini. Cruyff alijitengenezea jina akiwa na Ajax akishinda mataji manane ya ligi na klabu hiyo ktika vipindi viwili tofauti na kuanzisha falsafa yake katika soka ambayo ilikuja kujulikana kama Total Football. Akiwa chini ya kocha Rinus Michels, Cruyff pia alifanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1974 akiwa na Uholanzi watu wengi wakimtaja kama mchezaji bora kabisa wa taifa hilo kuwahi kutokea. Mbali na kupata mafanikio akiwa mchezaji, Cruyff pia alifanikiwa akiwa kocha na kufanikiwa kuingoza Barcelona kushinda mataji manne ya La Liga, Kombe la Washindi Ulay na Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanzia mwaka 1988 mpaka 1996. Nguli huyo atakumbukwa kwa kuanzisha falsafa nyingine ya tiki-take ambayo imewapa umaarufu mkubwa Barcelona kwa kuitumia kwenye mfumo wao wa vijana ambao uliwaibua kina Xavi, Andres Iniesta pamoja na Lionel Messi.

WEST HAM KUONGEZA UWANJA WA OLIMPIKI.

KLABU ya West Ham United imethibitisha kuwa wanatarajia kuongeza vito 6,000 katika uwanja wao wa Olimpiki ili vifikie 60,000. Mahitaji ya tiketi kwa msimu yameongezeka katika klabu hiyo ambayo inashikilia nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu msimu huu. Kutokana na hilo, klabu hiyo imedai kufanya mazungumzo na wabia wenzao katika uwanja huo ili waweze kuongeza viti. Makamu mwenyekiti wa West Ham, Karren Brady amesema wamefurahi kwani hatua waliyopiga ni kubwa na ni matumaini yao wataweza kutimiza malengo yao.

STERLING HATARINI KUKOSA MSIMU ULIOBAKIA.

WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita mpaka nane kufuatia majeruhi ya nyonga yanayomsumbua, hivyo kumaanisha kuwa anaweza asicheze tena msimu huu. Kama akikaa nje kwa wiki nane inaanisha Sterling anaweza kurejea baada ya siku ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu Mei 15 lakini kabla ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo itapigwa Mei 28. Kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amedai watakuwa wakifuatia maendeleo ya mchezaji huyo kama ataweza kucheza katika michuano ya Euro 2016. Kikosi cha Uingereza kinatarajiwa kutangazwa Mei 12 na Hodgson atakuwa na mpaka mwisho wa mwezi kabla ya kutangaza kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 kwa ajili ya michuao hiyo.

DEL BOSQUE ADOKEZA KUENDELEA KUINOA HISPANIA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque amedokeza kuwa anaweza kuendelea kuinoa timu hiyo baada ya michuano ya Euro 2016. Del Bosque amekuwa kocha wan chi hiyo toka mwaka 2008 na kuwoangoza kushinda taji lao la kwanza la Kombe la Dunia mwaka 2010 na taji la pili mfululizo la michuano ya Euro 2012. Mkataba wa Del Bosque unatarajiwa kumalizika Julai 31, baada ya kumalizika michuano ya Euro itakayofanyika Ufaransa. Hata hivyo pamoja na siku za nyuma kudai michuano hiyo itakuwa ya mwisho, Del Bosque sasa ameonyesha kubadili mawazo na kudai anawez kuongeza siku.

UJERUMANI YATHIBITSIHA MECHI ZAKE KUENDELEA KAMA ZILIVYOPANGWA.

MKUU wa usalama wa Chama cha Soka cha Ujerumani-DFB amesema jana kuwa mechi za kirafiki za kimataifa zinazotarajiwa kuchezwa nyumbani kati ya Ujerumani dhidi ya Uingereza na Italia haziko katika hatari yeyote kufuatia mashabulio ya kigaidi jijini Brussels. Ofisa huyo, Hendrick Grosse-Lefert amesema hakuna ushahidi wowote unaonyesha kuwa kutakuwa na hatari katika mechi hizo zijazo. Hata hivyo, Lefert aliendelea kudai kuwa wanachukua tahadhari zote ili kuhakikisha michezo hiyo inachezwa katika hali ya usalama. Magaidi wa kujitoa mhanga walifanya mashabulio katika Uwanja wa Ndege jijini Brussels na stesheni ya treni na kusababisha vifo vya watu 31 na wengine 270 wakiachwa majeruhi. Ujerumani inatarajiwa kukwaana na Uingereza Jumamosi hii mbele ya mashabiki wapatao 72,000 wanaotarajiwa kutokea katika Uwanja wa Olimpiki uliopo jijini Berlin.

VARDY ATENGENEZEWA FILAMU.

MSHAMBULIAJI nyota wa Leicester City, Jamie Vardy amekiri alikuwa haamini kama kuna filamu inatengenezwa ikielezea mafanikio yake ya ghafla aliyopata toka aibuke Ligi Kuu. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 29 alithibitisha kuzungumza na mwandishi wa filamu hiyo Adrian Butchart. Vardy ameibuka ghafla na kuwa nyota wa kutegemewa katika klabu hiyo ambayo alijiunga nayo akitokea timu ya daraja la chini mwaka 2012. Vardy amekuwa mfano wa kuigwa wa wachezaji wa ligi za chini nchini Uingereza, kufuatia kuweka rekodi mpya ya kufunga mabao 11 katika mechi 11 mfululizo za ligi msimun huu. Mara ya kwanza Vardy amesema alisikia taarifa hizo katika magazeti na hakuziamini mpaka alipokutana na Butchart na kumthibitishia hilo.

FA YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA WAHANGA WA BRUSSELS.

CHAMA cha Soka nchini Uingereza-FA kimetuma salamu zake za rambirambi kufuatia mashabulio ya mabomu huko Brussels kwa kuweka taa kuzunguka mnara wa Uwanja wa Wembley ambazo zina rangi ya bendera ya taifa ya Ubelgiji. Jumanne mashabulio kadhaa mabomu katika Uwanja wa Ndege na Stesheni ya Treni katika mji huo mkuu yalisababisha vifo vya watu 31 na wengine zaidi ya 270 kujeruhiwa. Nchi hiyo iko katika siku tatu za maombolezo kufuatia mashabulio hayo ya kigaidi. Mbali na uwanja wa Wembley lakini pia majengo mengine kadhaa yanayojulikana nchini Uingereza usiku yalikuwa yakiwaka taa za bendera la taifa hilo.

Tuesday, March 22, 2016

TETESI MBALIMBALI ZILIZOJIRI HUKO MAJUU.

MENEJA ajaye wa Manchester City, Pep Guardiola anataka kumuwania winga wa Arsenal Alex Oxlade-Chamberlain kufuatia kumtaja katika orodha ya wachezaji wanne anaowahitaji.
Chanzo: Times

KLABU ya Real Madrid inadaiwa kuwepo katika mzungumzo na wakala Mino Raiola juu ya uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Everton Romelu Lukaku kwa kitita cha paundi milioni 60.
Chanzo: The Sun

MENEJA wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho anadaiwa kumtaka mkurugenzi wa michezo wa Atletico Madrid Andrea Berta kujiunga naye Old Trafford kama akiteuliwa kuchukua nafasi ya Louis van Gaal Manchester United.
Chanzo: Telegraph

KLABU ya Southampton inadaiwa kumfuatilia kwa karibu beki wa kushoto wa Walsall Rico henry ambaye anafananishwa na beki wa zamani wa kimataifa wa Uingereza Ashley Cole. Henry pia anadaiwa kuwaniwa na Liverpool, Arsenal, Leicester City na Swansea City.
Chanzo: Daily Mail

KLABU ya Tottenham Hotspurs inadaiwa kujipanga kumpa ofa ya mkataba mwingine Harry Kane ili kuzifukuza klabu ambazo zinataka kumuwania.
Chanzo: Football Insider

MSHAMBULIAJI WA NORWICH ANUSURIKA KATIKA MILIPUKO HUKO BRUSSELS.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Norwich City Dieumerci Mbokani ameponea chupuchupu katika milipuko iliyotokea katika Uwanja wa wa Ndege wa jijini Brussels leo. Mbokani mwenye umri wa miaka 30 alikuwa uwanjani hapo wakati milipuko miwili ilipotokea lakini klabu yake imesema mchezaji huyo sasa amesharejea nyumbani. Watu kadhaa wameuawa katika milipuko hiyo ambapo vyombo vya habari vimedai idadi yao imefikia 13. Waziri Mkuu wa nchi hiyo amesema matukio hayo yaliyotokea katika Uwanja wa Ndege na stesheni ya treni ni kigaidi.

QATAR KUTOA MALAZI KWENYE MAHEMA YA ASILI KOMBE LA DUNIA 2022.

MASHABIKI watakaokwenda kushuhudia michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 litakalofanyika nchini Qatar wanaweza kupewa malazi katika mahema ya asili ya jangwani. Baadhi ya mashabiki kati ya 500,000 wanaotegemewa kwenda nchini humo wanaweza kupewa malazi katika mahema hayo ambayo yatakuwa karibu na viwanja. Msemaji wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo amesema watafanya hivyo ili kuonyesha ukarimu na urafiki wa watu wa Mashariki ya Kati.M Mahema hayo ya asili yanayojulikana kama Bedouin yatawawezesha mashabiki kulala huku wakiona nyota kwa juu. Michuano hiyo tayari imeshahamishwa kutoka muda wake uliozoeleka kwa Juni na Julai na kupelekwa Desemba kutokana na wasiwasi wa joto kali majira ya kiangazi.

PELLEGRINI ANATAKA KWENDA KUMNG'OA GARY NEVILLE.

MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini anadaiwa kutaka kuchukua mikoba ya kuinoa Valencia kutoka kwa Gary Neville katika kipindi cha majira ya kiangazi. Meneja huyo raia wa Chile anatarajiwa kuondoka City mwishoni mwa msimu huu huku meneja wa Bayern Munich Pep Guardiola akitarajiwa kuchukua nafasi yake. Vyombo vya habari nchini Chile vimekuwa vikidai kuwa Pellegrini mwenye umri wa miaka 62 anaweza kwenda Arsenal au Zenit St. Petersburg. Hata hivyo inadaiwa kuwa mwenyewe angependa zaidi kwenda Valencia kutokana na uzoefu alionao na La Liga kufuatia kuinoa Villarreal kwa miaka mitano kabla ya kwenda City.

DESCHAMPS AWATAKA WACHEZAJI WAKE KUSAHAU TUKIO LA PARIS.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps amesema kikosi chake kinapaswa kuendelea mbele wakati wakijiandaa kurejea tena Stade de France. Uwanja huo ulikuwa moja kati ya sehemu zilizolengwa katika mashambulio kadhaa yaliyotokea jijini Paris Novemba mwaka jana na kuua watu 130. Ufaransa ambao walikuwa wakicheza na Ujerumani wakati wa mashambulio hayo yakitokea, watarudi tena kwenye uwanja huo kuchuana na Urusi Machi 29 mwaka katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa. Akihojiwa Deschamps ambaye alikuwa kiungo wa zamani wa Chelsea, amesema hakuna anaweza kusahau yaliyotokea lakini hakuna haja ya kuzungumzia suala hilo kwani wanapaswa kuendelea mbele. Vikosi vya Ufaransa na Ujerumani wote walilazimika kulala uwanjani hapo baada ya tukio hilo la Novemba 13 huku milio ya milipuko ikisikika nje ya uwanja wakati wa mchezo.

CECH KIPA BORA CZECH.

KIPA wa kimataifa ya Jamuhuri ya Czech, Petr Cech ametangazwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa nchi hiyo. Cech Mwenye umri wa miaka 33, alichaguliwa na makocha, wachezaji na viongozi wa timu kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya nane. Cech aliwazidi wachezaji wengine wa nchi hiyo waliokuwepo katika kinyang’anyiro hicho akiwemo mshambuliaji wa Sparta Praque David Lafata na kiungo wa Hertha Berlin Vladimir Darida. Cech anayekipiga Arsenal ameichezea nchi yake mechi 118 toka alipoitwa kwa mara ya kwanza mwaka 2002.

KIKOSI CHA UBELGIJI CHASITISHA MAZOEZI KUTOKANA NA MILIPUKO.

KIKOSI cha timu ya taifa ya Ubelgiji leo kimesitisha mazoezi yake kwa ajili ya heshima kwa wahanga wa shambulio lililofanyika jijini Brussels. Kikosi cha nchi hiyo kinatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Ureno katika Uwanja wa King Baudouin uliopo Brussels Machi 29 mwaka huu lakini sasa ratiba hiyo iko katika hatihati. Milipuko kadhaa ilitokea katika Uwanja wa Ndege wa mji huo pamoja na stesheni ya treni na kupelekea vifo vya watu 13. Ubelgiji imefuzu michuano ya Euro 2016 itakayofanyika Ufaransa na wamepangwa kundi E sambamba na timu za Italia, Jamhuri ya Ireland na Sweden.

Monday, March 21, 2016

OZIL KUONDOKA ARSENAL.

KIUNGO mahiri wa Arsenal, Mesut Ozil anadaiwa kuwa anaweza kuondoka majira ya kiangazi kama Arsene Wenger ataendelea kuinoa klabu hiyo msimu ujao. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani amekuwa katika kiwango bora msimu huu lakini amechoshwa na ukame wa mataji na hataki kuendelea kuichezea timu hiyo chini ya Wenger. Taarifa hizo zinaendelea kudai kuwa Ozil na wakala wake tayari wameanza kuangalia uwezekano wa kurejea La Liga ingawa rais wa Real Madrid Florentino Perez hana shauku sana ya kumrejesha kiungo huyo Santiago Bernabeu. Hatua hiyo inaweza kuwaruhusu Atletico Madrid kupata nafasi kama wakiweza kulipa mshahara wa kiungo huo wakati Valencia na Sevilla nazo zikidaiwa kumuwania.

PIQUE AJITETEA.

BEKI wa Barcelona, Gerard Pique amepuuza taarifa zinazodai kuwa alistahili kutolewa nje katika mchezo waliotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Villarreal jana. Barcelona walishindwa kulinda mabao yao mawili waliyopata awali kupitia kwa Ivan Rakitic na Neymar aliyefunga kwa penati baada ya Villarreal kurudisha mabao yote hayo na kulazimisha kugawana alama. Pique alilimwa kadi ya njano katika dakika ya 16 kwa kushika mpira na alirudia tukio hilo tena wakati akichuana na kiungo wa Villarreal Denis Suarez lakini hakupewa adhabu nyingine na mwamuzi. Akihojiwa Pique amesema kadi ya kwanza hakustahili kwani mpira ulimgonga kifuani na sio mkononi kama mwamuzi alivyoona hivyo hadhani kama alistahili.

MARTINEZ AWAONYA WACHEZAJI WAKE.

MENEJA wa Everton, Roberto Martinez amewaonya wachezaji wake kuwa wanatakiwa kuimarika haraka kwani wanaweza kujikuta wakitolewa katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA itakayofanyika katika Uwanja wa Wembley. Everton walipata nafasi hiyo kufuatia ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Chelsea, mabao ambayo yote yalifungwa na Romelu Lukaku Machi 12. Everton inatarajiwa kukabiliana na aidha Manchester United au West Ham United katika mchezo wao wa nusu fainali. Hata hivyo kufuatia kufungwa na Arsenal mabao 2-0 jana, Martinez ameonyesha wasiwasi na kuwataka wachezaji wake kusahau kipigo hicho haraka na kujiimarisha ili wasipoteze mchezo wao utakaofuata.

TUCHEL AIPONGEZA DORTMUND.

MENEJA wa Borussia Dortmund, Thomas Tuchel amekipongeza kikosi chake kwa uwezo mkubwa wlaiouonyesha katika ushindi waliopata dhidi ya Augsburg jana. Dortmund walitoka nyuma na kufanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa WWK Arena na kuongeza shinikizo kwa vinara wa Bundesliga Bayern Munich. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Tuchel amesema pamoja na kikosi chake kunza vibaya mchezo huo lakini walifanikiwa kujirudi na kucheza vyema baadae hatua ambalo ilisaidia kupata ushindi huo. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa sio mara zote timu inaweza kuanza kucheza vyema lakini jambo muhimu ni kuwa wlaipambana na kuhakikisha wanasawazisha bao na kutafuta mengine ya ushindi.

ZIDANE ATAMBA KUWA YUKO TAYARI KWA CLASICO.

MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amedai kuwa kikosi chake kimeonyesha kuwa kiko tayari kwa ajili ya mchezo wa Clasico kufuatia ushindi mnono wa mabao 4-0 waliopata dhidi ya Sevilla. Mabao ya Karim Benzema, Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na James Rodriguez yalitosha kuifanya Madrid kubakisha alama moja kuifikia Atletico Madrid iliyoko nafasi ya pili katika msimamo wa La Liga baada ya nijana hao wa Diego Simeone kutandikwa na Sporting Gijon. Mchezo wa kwanza wa Madrid baada ya mapumziko kupisha mechi za kimataifa ni dhidi ya vinara wa ligi Barcelona ambapo watacheza katika Uwanja wa Camp Nou Aprili 2 na Zidane ana uhakika kikosi chake kiko tayari kwa ajili kutokana na kiwango bora walichoonyesha jana. Akihojiwa Zidane amesema amefurahishwa sana na mchezo huo kwani ni moja kati ya mechi walizocheza mechi walizocheza kwa kiwango kikubwa toka akabidhiwe mikoba ya kuinoa timu hiyo.

USHINDI WAMPA JEURI VAN GAAL.

MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal amesema matumaini yao ya kumaliza katika nne za juu yangekuwa yamefutika kama wangefungwa na Manchester city lakini anaamini sasa wana nafasi kubwa ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bao pekee lililofungwa na chipukizi Marcus Rashford lilitosha kuipa United ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mahasimu wao City jana. United kwasasa wako nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu lakini wako nyuma ya City wanaoshika nafasi ya nne kwa alama moja. Akihojiwa Van Gaal amesema pengo hilo linegkuwa kubwa kama wangetoa sare au kufungwa lakini kwa ushindi waliopa anadhani sasa wana nafasi kubwa ya kufuzu michuano hiyo.