Monday, March 28, 2016

NYARAKA ZAFUJA, BARCELONA BADO WANAILIPA LIVERPOOL KWA SUAREZ.

KLABU ya Barcelona inadaiwa bado inaendelea kuilipa Liverpool kutokana na mauzo ya Luis Suarez ambapo malipo ya mwisho yanatarajiwa kufanywa Julai mwaka huu. Mtandao wa Football Leakes umekuwa ukitoa nyaraka muhimu zilizohusisha usajili wa wachezaji nyota akiwemo Gareth Bale, Mesut Ozil na Anthony Martial kwa kipindi cha miezi kadhaa na sasa wamehamia katika usajili wa Suarez kwenda Barcelona. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay alihamia Camp Nou mwaka 2014 kipindi kifupi baada ya kusababisha utata mkubwa kwa kumng’ata beki wa Italia Giorgio Chiellini katika Kombe la Dunia. Nyaraka zilizovuja zinaonyesha Liverpool walikuwa na nia ya kuachana na mshambuliaji huyo haraka kutokana na tukio alilofanya tofauti ya dili zingine nyingi zinazohusiana na masuala hayo ya usajili. 
Taarifa kwenye nyaraka hizo zimeonyesha kuwa hakukuwa na masharti yeyote yaliyoweka kama ada ya kununulia au malipo mengine ya ziada kama Barcelona wakishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Badala yake ilikuwepo ada ya moja kwa moja ya paundi milioni 64.98 kwa ajili ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 ambaye katika kipindi hicho alikuwa amefungiwa miezi minne, na ilitakiwa kulipwa kwa kidogo kidogo kwa kipindi kwa awamu tano. Kila awamu Barcelona walitakiwa kulipa kiasi cha paundi milioni 13, wakianza majira ya kiangazi alipouzwa na sasa klabu hiyo inatarajia kumaliza awamu yake ya mwisho Julai 31 mwaka huu. Kiwango hicho cha ada kilichovuja kinathibitisha kuwa Suarez ni mchezaji wan ne ghali katika historia ya soka akiachwa kwa karibu na nyota mwenzake wa Barcelona Neymar na nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo na Gareth Bale.

No comments:

Post a Comment