Tuesday, May 31, 2016

MPEMBA WA UNITED APEWA NAFASI YA KUONYESHA UWEZO WAKE EURO 2016.

CHIPUKIZI wa Manchester United, Marcus Rashford ameitwa katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wa timu ya taifa ya Uingereza ambao watakwenda kushiriki michuano ya Euro 2016 huko Ufaransa. Rashford mwenye umri wa miaka 18, alifunga bao katika mechi yake ya kwanza ya kimataifa wakati Uingereza waliposhinda mabao 2-1 dhidi ya Australia katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Ijumaa iliyopita. Mshambuliaji wa Liverpool Daniel Sturridge naye pia amejumuishwa lakini Andros Townsend wa Newcastle United na Danny Drinkwater wa Leicester City wote wameachwa katika kikosi hicho. Uingereza inatarajiwa kuchuana na Ureno katika mchezo wa kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ambapo wanatarajiw akupambana na Urusi Juni 11 mwaka huu.

Kikosi kamili ni
Kipa: Joe Hart (Manchester City), Fraser Forster (Southampton), Tom Heaton (Burnley).

Mabeki: Gary Cahill (Chelsea), Chris Smalling (Manchester United), John Stones (Everton), Kyle Walker (Tottenham Hotspur), Ryan Bertrand (Southampton), Danny Rose (Tottenham Hotspur), Nathaniel Clyne (Liverpool).

Viungo: Dele Alli (Tottenham Hotspur), Ross Barkley (Everton), Eric Dier (Tottenham Hotspur), Jordan Henderson (Liverpool), Adam Lallana (Liverpool), James Milner (Liverpool), Raheem Sterling (Manchester City), Jack Wilshere (Arsenal).

Washambuliaji: Wayne Rooney (Manchester United), Harry Kane (Tottenham Hotspur), Jamie Vardy (Leicester City), Daniel Sturridge (Liverpool), Marcus Rashford (Manchester United).


MARCO REUS ATEMWA KIKOSI CHA UJERUMANI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Low amemuacha mshambuliaji wa Borussia Dortmund Marco Reus katika kikosi chake cha mwisho cha wachezaji 23 kwa ajili ya michuano ya Euro 2016. Low alitangaza kikosi chake huku mbali na kumuacha Reus lakini pia amewaacha Karim Bellarabi na Julian Brandt wa Bayer Leverkusen na Sebastian Rudy wa Hoffenheim. Nyota hao wanne sasa wanatarajiwa kuondoka katika kambi ya timu hiyo huo Uswisi. Ujerumani itacheza mechi yake ya mwisho ya kujipima nguvu dhidi ya Hungary kabla ya kucheza mechi yao ya ufunguzi wa michuano ya Euro 2016 dhidi ya Ukraine.

Kikosi kamili ni
Makipa: Manuel Neuer (Bayern Munich), Bernd Leno (Bayer Leverkusen), Marc-Andre ter Stegen (Barcelona)

Mabeki: Jerome Boateng (Bayern Munich), Emre Can (Liverpool), Jonas Hector (Cologne), Benedikt Howedes (Schalke), Mats Hummels (Borussia Dortmund), Shkodran Mustafi (Valencia), Antonio Rudiger (Roma)

Viungo: Julian Draxler (Wolfsburg), Mario Gotze (Bayern Munich), Sami Khedira (Juventus), Joshua Kimmich (Bayern Munich), Toni Kroos (Real Madrid), Mesut Ozil (Arsenal), Leroy Sane (Schalke), Bastian Schweinsteiger (Manchester United), Julian Weigl (Borussia Dortmund)

Washambuliaji: Mario Gomez (Besiktas), Thomas Muller (Bayern Munich), Lukas Podolski (Galatasaray), Andre Schurrle (Wolfsburg)

SENDEROS AACHWA TIMU YA TAIFA.

BEKI wa zamani wa Arsenal, Philippe Senderos ambaye amekuwa akihangaika kurejea katika kiwango chake katika misimu ya karibuni, ameachwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uswisi kwa ajili ya michuano ya Euro 2016. Senderos ambaye ametumia muda mwingi msimu uliopita akiwa na timu yake ya nyumbani ya Grasshopper Zurich, alishindw akuonyesha uwezo wake wakati Uswisi walipotandikwa mabao 2-1 na Ubelgiji katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu. Kocha wan chi hiyo Vladimir Petkovic ameamua kumuacha beki huyo mwenye umri wa miaka 31 pamoja an wasiwasi uliopo katika safu ya ulinzi kutokana na Timm Klose na Johan Djourou kuwa nje kutokana na majeruhi. Beki wa Udenese Silvan Widmer na kiungo wa basel Luca Zuffi ambye ameonyesha uwezo mkubwa msimu huu pia wamekatwa katika kikosi hicho. Uswisi inatarajiw akucheza na Moldova katika mechi yake ya mwisho ya kujipima nguvu Ijumaa hii kabla ya kuvaana na Albania, Romania na wenyeji Ufaransa katika kundi A.

Kikosi Kamili ni
Makipa: Yann Sommer (Borussia Monchengladbach), Roman Burki (Borussia Dortmund), Marwin Hitz (Augsburg)

Mabeki: Stephan Lichtsteiner (Juventus), Nico Elvedi (Borussia Monchengladbach), Michael Lang (Basel), Johan Djourou (Hamburg), Steve von Bergen (Young Boys), Fabian Schar (Hoffenheim), Francois Moubandje (Toulouse), Ricardo Rodriguez (Wolfsburg)

Viungo: Valon Behrami (Watford), Blerim Dzemaili (Genoa), Gelson Fernandes (Rennes), Fabian Frei (Mainz), Granit Xhaka (Arsenal), Xherdan Shaqiri (Stoke City), Renato Steffen (Basel), Denis Zakaria (Young Boys)

Washambuliaji: Breel Embolo (Basel), Haris Seferovic (Eintracht Frankfurt), Admir Mehmedi (Bayer Leverkusen), Eren Derdiyok (Kasimpasa), Shani Tarashaj (Everton)

CURRY AIPELEKA WARRIORS FAINALI YA NBA.

ALAMA 36 zilizofungwa na nyota Stephen Curry ziliiwezesha Golden State Warriors kuibuka na ushindi wa vikapu 96-88 dhidi ya Oklahoma City Thunder na kuwawezesha kutinga fainali ya Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani maarufu kama NBA. Warriors walikuwa nyuma kwa alama 13 wakati wa kipindi cha kwanza lakini walipambana katika na kurejea mchezoni katika robo ya mwisho katika mchezo huo. Ushindi wa jumla wa michezo 4-3 unaifanya Warriors kuwa timu ya 10 ambayo imepambana kutoka kufungwa kwa 3-1 na kuibuka washindi katika hatua hiyo ya mtoano. Mabingwa hao watetezi wa NBA sasa watakabiliaa kwa mara nyingine na Cleveland Cavaliers wakiwa na nyota wao LeBron James katika hatua ya fainali ambayo itakuwa na michezo saba. Warriors wataivaa Cavaliers katika mchezo wa kwanza utakaofanyika Alhamisi hii huku wakiwa na matumaini ya kuibuka mabingwa kama walivyofanya mwaka jana waliposhinda kwa michezo 4-2.

NAVAS KUIKOSA COPA AMERICA.

GOLIKIPA wa kimataifa wa Costa Rica na klabu ya Real Madrid, Keylor Navas anatarajiwa kuikosa michuano maalumu ya Copa Amerika kwasababu ya majeruhi ya kisigino. Majeruhi hayo aliyopata katika mguu wake wa kushoto yalimfanya kuukosa michezo muhimu ya Madrid mwishoni mwa msimu. Jana Shirikisho la Soka la Costa Rica-FEDEFUTBOL, lilithibitisha taarifa za kumuondoa nyota huyo na nafasi yake kuchukuliwa na kipa Deportivo Saprissa Danny Carvajal. Navas anatarajiwa kutafuta mtaalamu atakayetibu tatizo lake hilo ambalo pia lilimkosesha michuano ya michuano ya Kombe la CONCACAF Gold mwaka jana. Kukosekana kwa Navas na mshambuliaji nyota Ariel Rodriquez ni pigo kubwa kwa Costa Rica ambao wamepangwa katika kundi A sambamba na Marekani, Paraguay na Colombia.

ARGENTINA YATISHIA KUJITOA COPA AMERICA.

CHAMA cha Soka cha Argentina-AFA kimetishia kujitoa katika michuano maalumu ya Copa America baada ya kuituhumu serikali ya nchi yao kwa kuwaingilia. Argentina ni moja ya timu zinazopewa naafsi ya kufanya vizuri katika michuano hiyo itakayofanyika nchini Marekani huku wakitarajiwa kucheza mechi yao ya kwanza dhidi ya mabingwa watetezi Chile huko Santa Clara, California Juni 7 mwaka huu. Hata hivyo, AFA wamezusha wasiwasi wa kutokuwepo kwa mchezo huo baada ya serikali ya Argentina kusimamisha uchaguzi wa chama hicho ambao ulikuwa ufanyike Juni 30 na kuteua tume maalumu ya kuchunguza tuhuma za ubadhilifu wa mapato ya luninga. Katibu Mkuu wa AFA, Damian Dupiellet amesema mkutano wa dharura wa bodi ndio utakaoamua kama timu yao ya taifa itashiriki michuano hiyo au itarudishwa nyumbani kutoka katika kambi yao huko Marekani.

KESI YA MESSI YAANZA KUSIKILIZWA.

KESI ya ukwepaji kodi dhidi ya mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi imeanza kusikilizwa jijini Barcelona leo. Messi na baba yake wameshitakiwa kwa makosa matatu ya ukwepaji kodi yenye thamani ya euro milioni 4.1 kuanzia mwaka 2007 mpaka 2009. Nyota huyo wa Barcelona anatarajiwa kupanda kizimbani mwenyewe kutoa ushahidi wake Alhamisi hii, ikiwa ni siku nne kabla ya mechi ya ufunguzi ya michuano ya Copa America dhidi ya mabingwa watetezi Chile. Wakili wa Messi, Enrique Bacigalupo ndio aliyemwakilisha nyota huyo leo katika Mahakama hiyo ya Eighth.

Monday, May 30, 2016

RASHFORD APIGWA MIAKA MINNE MINGINE OLD TRAFFORD.

MSHAMBULIAJI nyota wa Manchester United, Marcus Rashford mwenye umri wa miaka 18 amesaini mkataba mpya ambao utamuweka Old Trafford mpaka Juni mwaka 2020. Chipukizi huyo alifunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wakubwa dhidi ya Midtjlland Februari mwaka huu na kumaliza akiwa amefunga mabao nane katika mechi 18 alizocheza. Kiwango hicho kizuri alichokionyesha kilimfanya kuteuliw akatika kikosi cha Uingereza na kufunga bao lake la kwanza katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Australia Ijumaa iliyopita. Akihojiwa Rashford amesema anajisikia furaha kwa kupewa nafasi ya kuonyesha uwezo wake na kuahidi wa mashabiki wa United kuwa wategemee mambo mazuri kutoka kwake.

Friday, May 27, 2016

WAKALA WA ALVES AKANUSHA TAARIFA ZA KWENDA JUVENTUS.

WAKALA wa Dani Alves amekanusha taarifa kuwa mteja wake amesaini mkataba wa awali na Juventus lakini amekiri mabingwa wa Italia na klabu zingine zinamuwania mchezaji huyo. Vyombo vya habari nchini Hispania viliripoti jana kuwa beki huyo wa Barcelona anatarajiwa kuondoka baada ya kutimukia timu hiyo kwa miaka nane na kwenda Turin kwa mkataba wa miaka mitatu. Hata hivyo, wakala wake ambaye pia amewahi kuwa mke wake, Dinorah Santa Ana da Silva alikanusha taarifa hizo akidai hazina ukweli wowote. Dinorah aliongeza kuwa hakuna klabu yeyote Alves aliyosaini hivi sasa kwani amehamishia nguvu zake zote katika timu ya taifa ya Brazil ambayo inakabiliwa na michuno ya Copa America mapema mwezi ujao. Wakala huyo aliendelea kudai kuwa ni kweli amekutana na Juventus lakini sio wao peke yao kwani amekutana pia na klabu zingine lakini hakuna dili lolote lililoafikiwa mpaka sasa.

KAKA AITWA BRAZIL.

MSHAMBULIAJI wa Orlando City, Kaka ameitwa katika katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kwa ajili ya michuano ya Copa America akichukua nafasi ya Douglas Costa. Costa mwenye umri wa miaka 25, amepata majeruhi misuli ambayo yatamfanya kukosa michuano hiyo maalumu ya kuadhimisha miaka 100 toka kuanzishwa kwake. Kaka mwenye umri wa miaka 34 ameichezea Brazil mechi 91 na kufunga mabao 29 katika kikosi cha Brazil. Costa alikuwa sehemu ya kikosi cha Bayern Munich ambacho kimeshinda taji la Bundesliga na Kombe la Ujerumani katika msimu wa mwisho wa Pep Guardiola na timu hiyo. Brazil itafungua pazia la Copa America kwa kucheza na Ecuador katika Uwanja wa Rose Bowl huko Pasadena, California Juni 4 mwaka huu huku mechi zao nyingine mbili za kundi B zitakuwa dhidi ya Haiti na Peru.

RONALDO AWANANGA BARCELONA NA MATAJI YAO MAWILI.


MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amesema kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kutakuwa na tahmani zaidi ya mataji mawili ambayo Barcelona wameshinda. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 alikuwa akisumbuliwa na majeruhi katika wiki za karibuni na kumfanya kukosa nusu fainali ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City. Hata hivyo juzi aliwaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo akidai kuwa atakuwa fiti kwa asilimia 100 kwa ajili ya fainali hiyo dhidi ya mahasimu wao Atletico Madrid. Akihojiwa Ronaldo amesema kama wakishinda taji la Ligi ya Mabingwa itakuwa na thamani zaidi kuliko mataji mawili ya Barcelona waliyoshinda kwani taji la michuano hiyo liko katika ndoto za kila mchezaji. Madrid na Atletico wanakutana katika fainali tatu ambazo zimekutanisha timu za Hispania na fainali mbili baina yao.

MOURINHO RASMI UNITED.

KLABU ya Manchester United imemthibitisha rasmi Jose Mourinho kuwa meneja wao mpya baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu. Mourinho anachukua nafasi ya Mholanzi Louis van Gaal ambaye alitimuliwa Jumatatu, siku mbili baada ya kutwaa taji la Kombe la FA. Makamu mwenyekiti wa United, Ed Woodward amesema Mourinho ndio meneja bora katika mchezo wa soka kwasasa. Naye Mourinho mwenye umri wa miaka 53, akihojiwa amesema kuwa meneja wa klabu hiyo ni heshima kubwa kwake kwani United inajulikana na kupendwa duniani kote. Mourinho amekuwa bila kibarua toka alipotimuliwa kuinoa Chelsea Desemba mwaka jana.

Wednesday, May 25, 2016

ARSENAL YAANZA USAJILI KWA KUMNASA XHAKA.

KLABU ya Arsenal imekamilisha rasmi usajili wa Grant Xhaka kutoka Borussia Monchengladbach kwa dili lenye thamani ya paundi milioni 33.1. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 aliwasili katika viwanja vya mazoezi vya klabu hiyo Ijumaa iliyopita kwa ajili ya vipimo vya afya na kumalizia hatua za mwisho za usajili wake wa miaka minne. Ujio wa Xhaka kabla ya kuanza kwa usajili kunaonyesha jinsi Arsene Wenger alivyopania kuimarisha kikosi chake ambacho kilishika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu msimu uliopita. Akihojiwa Xhaka amesema anajivunia kujiunga na Arsenal kwa ni moja ya klabu kubwa ambazo amekuwa akitamani siku nyingi kuzichezea. Naye Wenger akihojiwa amesema Xhaka ni mchezaji mzuri mwenye uzoefu wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Bundesliga na wamekuwa wakimfuatilia kwa kipindi kirefu.

POLISI ZAIDI 60,000 KUMWAGWA KUIMARISHA ULINZI EURO 2016.

UFARANSA imesema kuwa inatarajia kuweka polisi zaidi ya 60,000 ili kulinda usalama katika michuano ya Euro 2016 na kuapa kuwa watafanya kila wawezalo kuhakikisha wanazuia shalio lolote la kigaidi katika kipindi chote cha mashindano. Kauli hiyo ya waziri wa mambo ya ndani ya nchi hiyo Bernard Cazeneuve imekuja baada ya Uwanja wa Ufaransa uliopo jijini Paris ambao ndio utatumika kwa ajili ya mechi ya ufunguzi na fainali, kuleta rabsha Jumamosi iliyopita kabla ya fainali ya Kombe la Taifa. Moshi mkubwa uliohisiwa kuwa bomu ulilipuka ndani ya uwanja na kusababisha mashabiki kuchanganyikiwa na kukimbia hovyo kuelekea milango ya kutoka nje ya uwanja. Akihojiwa waziri huyo amesema tukio la Jumamosi iliyopita halihusiani na maandalizi yao kwani waandaaji walikuwa tofauti. Waziri huyo aliongeza kuwa katika michuano ya Euro 2016 inayotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao usalama utakuwa ni kipaumbele chao cha kwanza ili kuhakikisha hakuna tukio lolote hatarishi ya kigaidi litakaloweza kutokea.

JUVENTUS YATAKA KUMNG'OA MASCHERANO CAMP NOU.

KIUNGO mahiri wa Barcelona, Javier Mascherano anadaiwa kukubali dili la kujiunga na mabingwa wa Serie A Juventus. Taarifa zinadai kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Argentina amefanya mazungumzo na Juventus na anajiandaa kuhamia jijini Turin kiangazi hiki. Mpaka sasa inadaiwa kuwa hakuna makubaliano yeyote kati ya Barcelona na Juventus na mabingwa hao wa Hispania wanahisiwa kutokuwa na mpango wowote wa kumuachia kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31. Mascherano alijiunga na Barcelona mwaka 2010 akitokea Liverpool, na kufanikiwa kushinda mataji manne ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa Camp Nou.

PSG KUIPIGA BAO ARSENAL KWA KANTE.

KLABU ya Paris Saint-Germain inadaiwa kuipiga bao Arsenal katika mbio za kumuwania kiungo N’Golo Kante. Mabingwa hao wa Ufaransa walikutana na wawakilishi wa kiungo huyo mahiri wa Leicester City Aprili mwaka huu na toka wakati huo wamekuwa wakiendeleza na majadiliano huku wakiahidi kumuongeza mshahara wake. Kante ambaye mkataba wake unaweza kutenguliwa kwa kitita cha paundi milioni 20, alikata ofa ya mkataba mpya na kuna uwezekano mkubwa wa kuondoka Leicester kiangazi hiki. Arsenal bado inaonekana kuwa na nia ya kumnasa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 lakini tatizo dau lao linaweza kua dogo kulinganisha na PSG.

RANIERI ADAI MSIMU UJAO WATAPIGANIA KUBAKI LIGI KUU TU.

MENEJA wa Leicester City, Claudio Ranieri amedai kuwa lengo kubwa la kikosi chake msimu ujao litakuwa ni kubaki katika Ligi Kuu na sio kutetea taji lao. Leicester msimu uliopita walifanikiwa kuwashangaza wengi kwa kutwaa taji la ligi kwa mara ya kwanza katika historia yao huku wakimaliza kileleni kwa tofauti ya alama 10 dhidi ya Arsenal walioshika nafasi ya pili. Hatua hiyo inamaanisha kuwa Leicester msimu ujao watashiriki pia michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hivyo kuwaongezea majukumu kulinganisha nay ale waliyokuwa nayo msimu uliopita. Akihojiwa Ranieri amesema msimu ujao utakuwa msimu mwingine mzuri kwasababu ya ujio wa Pep Guardiola, Antonio Conte nap engine Jose Mourinho. Ranieri aliendelea kudai kuwa utakuwa msimu mzuri na mgumu lakini lengo lao kubwa halitakuwa kutetea taji lao bali kuhakikisha wanabaki katika Ligi Kuu.

DANI ALVES AISHABIKIA ATLETICO.

BEKI wa Barcelona, Dani Alves amekiri kuwa angependelea zaidi Atletico Madrid washinde taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya badala ya mahasimu wao Real Madrid katika mchezo wa fainali unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi hii. Atletico walio chini Diego Simeone ndio waliowang’oa mabingwa watetezi Barcelona katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kabla ya kuitoa tena Bayern Munich kwenye hatua ya nusu fainali. Madrid ndio timu pekee iliyopo mbele ya Atletico kwasasa ikiwa ni kama marudiano baada ya ile fainali ya mwaka 2014 ambapo Madrid waliibuka kidedea kwa kushinda mabao 4-1 katika muda wa nyongeza. Hata hivyo, Alves ana mawazo tofauti katika fainali hiyo itakayofanyika katika Uwanja wa San Siro jijini Milan, kwani anadhani Atletico wanastahili zaidi taji hilo kuliko Madrid. Alves amesema Atletico ni timu ambayo imepambana sana mpaka kufikia hapo walipo hivyo anadhani wanastahili taji hilo.

LENS YAPIGA MARUFUKU MASHABIKI KULEWA MITAANI WAKATI EURO 2016.

MASHABIKI wa Uingereza na Wales hawataruhusiwa kunywa pombe katika mitaa ya jiji la Lens kabla na baada ya mchezo wao wa michuano ya Euro 2016 kwasababu amri ya saa 24 iliyotolewa. Mchezo huo utakaokuwa wa kundi B utafanyika katika mji huo siku ya Alhamisi ya Juni 16 mwaka huu. Siku ya mchezo huo polisi wa mji huo watakuwa wakikagua magari yanayoingia kuona kama yamebeba pombe. Mashabiki wasiokuwa na tiketi za mchezo huo au tiketi za eneo la mashabiki nje ya uwanja wameshauriwa kutosafiri kwenda Lens. Pombe zitaruhusiwa katika maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya mashabiki na hatua hiyo imekuja ili kuimarisha zaidi ulinzi na amri itakuwa ikitekelezwa katika kila mchezo utakaofanyika kwenye mji huo wakati wote wa mashindano.

Tuesday, May 24, 2016

PAMOJA NA KULIKOSA TAJI LAKINI ARSENAL NDIO KLABU ILITENGENEZA FEDHA NYINGI LIGI KUU MSIMU WA 2015-2016.


MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO: YANGA KUANZA UGENINI NA KUMALIZA UGENINI.

MABINGWA wa soka wa Tanzania, Yanga imepangwa kundi A katika ratiba ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika-CAF. Katika kundi hilo litakalokuwa na timu nne Yanga wamepangwa sambamba na Mo Bejaia ya Algeria, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-RDC na Medeama ya Ghana. Kundi B katika michuano hiyo litazikutanisha timu zote kutoka ukanda wa kaskazini mwa Afrika ambazo ni mabingwa watetezi Etoile du Sahel ya Tunisia, Ahly Tripoli ya Libya na Kawbab Athletic na FUS Rabat zote za Morocco. 
Kwa upande wa ratiba ya makundi michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kundi A limepangwa kuwa na timu za Zesco ya Zambia, Al Ahly ya Misri, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Wydad Athletic ya Morocco. Kundi B litakuwa na timu za Enyimba ya Nigeria, Zamalek ya Misri, ES Setif ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao wamechukua nafasi ya AS Vita ya DR Congo ambao walitolewa kwa kucheza mchezaji asiyeruhusiwa. Timu hizo zitacheza na kila mmoja wapo nyumbani na ugenini huku washindi wawili kutoka katika kila kundi wakisonga mbele katika hatua ya nusu fainali. Mechi za makundi zinatarajiwa kuanza kuchezwa Juni 17 mwaka huu.

RONALDO AWATOA HOFU MASHABIKI WA MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid amewasisitizia mashabiki wa klabu hiyo kuwa hawana sababu ya kuhofu baada ya kuondoka mazoezini mapema leo kufuatia kukwatuliwa na Kiko Casilla. Madrid walikuwa mazoezini kuelekea mchezo wao wa Jumamosi hii katika Uwanja wa San Siro dhidi ya mahasimu wao wa jiji Atletico Madrid, wakati Ronaldo alipogongana na golikipa huyo kabla ya kunyanyuka na kuondoka akiwa anachechemea kabla ya mazoezi kumalizika. Hata hivyo, mshambuliaji huyo amewaondoa hofu mashabiki wa klabu hiyo akiwaambia wana habari kuwa yuko fiti kwa asilimia 100. Akihojiwa Ronaldo amesema tatizo linalomkabili sio kubwa na katika muda mchache atakuwa fiti tena.

GOTZE HAENDI LIVERPOOL.

MENEJA mpya na baba wa mshambuliaji nyota wa Bayern Munich, Mario Gotze amesema kijana wake hatakwenda Liverpool kama taarifa zilivyokuwa zimezagaa kona mbalimbali. Kwasasa nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 amesema anataka kuanza upya akiwa katika klabu hiyo yenye maskani Allianz Arena. Jana Gotze alisitisha mkataba wake na kampuni ya uwakala ya Sports Total ambayo pia inawawakilisha nyota wengine wakiwemo Toni Kroos, Marco Reus na Benedikt Howedes na kuamua shughuli zake ziwe zikisimamiwa na familia yake. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo, meneja wake huyo Jurgen Gotze amesema hafamu kuhusu taarifa hizo za kwenda Liverpool kwani amekuwa akizungumza na mwanae mara kwa mara lakini hajawahi kumwambia suala hilo.

AS VITA WATOLEWA LIGI YA MABINGWA AFRIKA.

KLABU ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC imetolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kosa la kumchezesha mchezaji asiyeruhusiwa. Idrissa Traore alichezeshwa katika mzunguko wa awali pamoja na kuwa bdo kumaliza adhabu yake ya kutochza mechi nne wakati akiwa mchezaji wa Stade Malien. Nafasi ya Vita katika michuano hiyo sasa itachukuliwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Vita waliwaondoa Sundowns katika hatua ya timu 16 bora kwa bao la ugenini baada ya timu hizo kutoka sare ya jumla ya mabao 2-2 katika michezo miwili waliyokutana. Traore alitumikia mechi moja pekee katika adhabu yake hiyo wakati alipopangwa katika mchezo dhidi ya Mafunzo uliochezwa Februari mwaka huu.

DILI LA MOURINHO LANUKIA OLD TRAFFORD.

WAWAKILISHI wa Jose Mourinho wanatarajiwa kukutana na maofisa wa Manchester United leo ili kukamilisha taratibu za Mreno huyo kuwa meneja mpya wa klabu hiyo. Wakala wa Mourinho, Jorge Mendes amesafiri leo asubuhi kwenda jijini London na anatarajiwa kuongoza majadiliano hayo. Kuna hatihati ya taarifa kutotangazwa leo lakini uthibitisho kuwa Mourinho ndio atakuwa meneja ajaye wa klabu hiyo unategemewa kutangazwa baadae wiki hii. United ilimtimua meneja wake Louis van Gaal mwenye umri wa miaka 64 jana, ikiwa zimepita siku mbili baada ya kushinda taji la Kombe la FA.

UNITED YAJIPANGA KUMTENGENEA FUNGU NENE IBRAHIMOVIC.

KLABU ya Manchester United inadaiwa kuwa tayari kumtengea ofa nono Zlatan Ibrahimovic ili awe moja ya usajili muhimu wa Jose Mourinho katika kipindi hiki cha kiangazi. Nyota huyo wa kimataifa wa Sweden anatafuta klabu mpya baada ya kuondoka kwa mabingwa wa Ufaransa Paris Saint-Germain. Wakati mkongwe huyo akiwa tayari kukubali uhamisho wa kwenda kucheza Ligi Kuu ya Marekani-MLS ka dau kubwa, United inajipanga kumpa bonge la ofa ambalo linaweza kumshawishi kuahirisha kwenda Marekani. Inadaiwa kuwa Ibrahimovic anatafuta mkataba ambao utalingana sawa na mshahara wa euro 350,000 alizokuwa akipata PSG na United wako katika mchakato wa kuliwezesha hilo ili waweze kumshawishi kutua Old Trafford.

SANDRO KUONYESHWA MLANGO WA KUTOKEA BARCELONA.

KATIBU wa Ufundi wa Barcelona, Robert Fernandez amethibitisha Sandro hataitumikia klabu hiyo msimu ujao. Sandro amewatumikia mabingwa hao wa Hispania katika michezo 20 msimu huu lakini amefanikiwa kucheza mara mbili pekee mwaka huu baada ya kupata majeruhi. Fernandez alibainisha kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alikuwa na machaguo mengi ya kuondoka msimu uliopita lakini alichagua kubakia huku Barcelona ikiwa imefungiwa kufanya usajili. Fernandez amesema wanamshukuru Sandro kwa uamuzi wake wa kubakia msimu uliopita lakini wameshindwa kumuongeza mkataba mwingine kutokana na tabia alizoonyesha.

Monday, May 23, 2016

MESSI ADAI MSIMU HUU WALIPAMBANA SANA KUPATA MAFANIKIO.MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi amedai kuwa walilazimika kupambana ili kuhakikisha wanatetea mataji yao mawili ya nyumbani msimu huu. Barcelona walifanikiwa kutwaa taji la Kombe la Mfalme kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sevilla na kuijiongezea taji lingine baada ya lile la La Liga ambayo walilinyakuwa siku ya mwisho wa ligi. Katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Vicente Calderone Barcelona ilishuhudia kiungo wake Javier Mascherano akitolewa nje kwa kadi nyekundu kabla ya mapumziko lakini mabao ya Jordi Alba na neymar ambayo yalitengenezwa na Messi yalitosha kuwapa ushindi huo. Messi aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wao kijamii wa Facebook kuwa ubingwa wao wa safari haukuja kirahisi lakini juhudi zao za kucheza kwa umoja na kupambana kwa bidii kuliwasaidia kupata mataji hayo. Kombe la Mfalme linakuwa taji nne kwa Barcelona msimu huu baada ya kutwaa taji la Super Cup la UEFA na klabu bingwa ya dunia mwishoni mwa mwaka jana.

Friday, May 20, 2016

SUAREZ ADAI HAKUTEGEMEA KAMA ATAWEZA KUCHUKUA NAFASI YA MESSI.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Luis Suarez amesema hakutegemea kuchukua nafasi ya Lionel Messi ya mshambuliaji kiongozi kama alivyofanya msimu huu. Suarez amekuwa akiimarika toa ajiunge na Barcelona akitokea Liverpool na amefanikiwa kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la La Liga mara mbili huku mwenyewe akimaliza kama mfungaji kinara. Suarez amefunga mabao 40 katika mechi 35 za ligi alizocheza msimu huu na kumzidi mshambuliaji nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo katika tuzo ya Pichichi kwa kufunga hat-trick katika mchezo wao mwisho wa msimu. Kwasasa Messi ambaye ni mshindi wa tuzo tano za Ballon d’Or amerudi nyuma na kushambulia akitokea upande wa kushoto ili kumpisha Suarez nafasi ya katikati. Akihojiwa Suarez amesema hakutegemea kucheza nafasi hiyo kwani ndio ilikuwa ikitumiwa na Messi lakini wamekuwa wakielewana vyema ndani na nje ya uwanja.

CHELSEA WATAKA KUMSAJILI LUKAKU.

KLABU ya Chelsea inadaiwa kutaka kumsajili tena mshambuliaji wao wa zamani Romelu Lukaku kutoka klabu ya Everton. Chelsea walimuuza Lukaku kwa kitita cha paundi milioni 28 kwenda Everton mwaka 2014, baada ya kuitumikia timu hiyo kwa mkopo na toka wakati huo nyota huyo amefunga mabao 61 katika mechi 127 alizocheza. Chelsea sasa wanadaiwa kutaka kumrejesha tena mshambuliaji huyo ingawa inadaiwa Everton watataka kulipwa ada ya paundi milioni 61 kiasi ambacho kinadaiwa kitaweza kulipwa. Chelsea pia inawawinda nyota wa Napoli Gonzalo Higuain na mshambuliaji wa Juventus Alvaro Morata ili kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.

BENTEKE KUTETA NA KLOPP KUHUSU MUSTAKABALI WAKE.

MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Christian Benteke anataka kufanya mazungumzo na klabu hiyo kujadili mustakabali wake baada ya kumaliza msimu wake wa kwanza ambao haukua mzuri kama ulivyotegemewa. Benteke amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda klabu kadhaa katika kipindi cha kiangazi ikiwemo West Ham United baada ya kushindwa kung’aa akiwa Anfield akifunga mabao 10 katika mechi 42 za mashindano yote aliyocheza toka anunuliwe kwa kitita cha paudi milioni 32.5 kutoka Aston Villa. Kukiwa hakuna uwezekano wa kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao baada ya kufungw amabao 3-1 na Sevilla katika fainali ya Europa League juzi, Benteke amesema yeye sambamba na wachezaji wengine wana matumaini ya kuzungumza na Jurgen Klopp kuhusu mipango ya msimu ujao. Akihojiwa Benteke amesema anafahamu kuwa bado anatakiwa kuzoea mazingira na kwasababu msimu umemalizika anadhani sasa ni wakati wa kukaa chini ya Klopp na kujaribu kutafuta suluhisho kwa ajili ya msimu ujao.

KAKA NDIO MCHEZAJI ANAYELIPWA ZAIDI MAREKANI.

KIUNGO wa kimataifa wa Brazil, Kaka ndio mchezaji anayelipwa zaidi katika Ligi Kuu ya Marekani-MLS, akimzidi nyota wa kimataifa wa Italia Sebastian Giovinco na nahodha wa Marekani Michael Bradley kufuatia viwango vilivyotolewa jana. Kaka mshindi wa ballon d’Or ambaye anacheza katika klabu ya Orlando City ya Florida anakunja mshahara wa dola 7,167,500 akifuatiwa na Giovinco anayechukua dola milioni 7,115,556 huku Bradley yeye akichukua dola milioni 6.5.  Wachezaji wenye majina makubwa waliojiunga na MLS katika miaka ya karibuni ndio wanafuatia akiwemo Steven Gerrard anayecheza Los Angeles Galaxy anashika nafasi ya nne kwa kupokea kiasi cha dola 6,132,500. Wengine ni nyota wa New York City FC Frank Lampard anayekunja dola milioni sita, Andrea Pirlo dola milioni 5.9 na David Villa dola milioni 5.6.

OZIL NDIO MCHEZAJI BORA WA MWAKA WA ARSENAL.

KIUNGO wa mahiri wa kimataifa wa Ujerumani, Mesut Ozil amechaguliwa na mashabiki kuwa mchezaji bora wa mwaka wa Arsenal kutokana na kiwango cha juu alichoonyesha msimu huu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 ameshinda tuzo hiyo akiwazidi Alexis Sanchez aliyeshika nafasi ya pili na Hector Bellerin aliyeshika nafasi ya tatu. Ozil amekuwa katika kiwango kizuri akifunga mabao nane na kutengeneza nafasi zingine 181 msimu huu ambazo zimechagiza kwa kiasi kikubwa Arsenal kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Leicester City. Kiwango hicho pia kilimfanya Ozil kuteuliwa katika orodha ya tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa PFA ambayo ilinyakuliwa na Riyad Mahrez wa Leicester.

GOTZE ASHAURIWA KUONDOKA BAYERN.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Loew amemshauri Mario Gotze kuondoka Bayern Munich ili kupiga hatua zaidi katika soka lake. Gotze mwenye umri wa miaka 23 anakaribia kumaliza mkataba wake na Bayern na amekuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka Allianz Arena kiangazi hiki. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani ameshindw akupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Bayern katika kipindi cha miaka mitatu toka ajiunge nao akitokea Borussia Dortmund. Akihojiwa Loew amesema Gotze ni mchezaji mzuri na hana shaka na uwezo wake lakini anadhani uhamisho unaweza kumletea changamoto mpya na kumfanya kuimarika zaidi ya alivyo sasa.

Thursday, May 19, 2016

MAKUNDI KUWAPA YANGA ZAIDI MILIONI 300.

BAADA ya Yanga kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho sasa klabu hiyo ina uhakika wa kuingiza kiasi cha dola 150,000 sawa na shilingi 327,900,000 au zaidi kulingana na hatua watakayoishia. Yanga ambayo imekuwa timu pekee kwa nchi za Afrika Mashariki kutinga hatua hiyo sasa inasubiri upangaji wa makundi ambao unatarajiwa kufanyika Jumanne Mei 24 mwaka huu. Katika hatua hii kutakuwa na timu nane ambapo mbali na Yanga lakini pia watakuwepo Etoile du Sahel ya Tunisia, TP Mazembe ya Congo DRC, Mo Bejaia ya Algeria, Madeama ya Ghana, Kawkab Marrakech ya Morocco, Al Ahly Tripoli ya Libya na Fus Rabat ya Morocco. Makundi yatakuwa mawili yenye timu nne nne ambapo mshindi wa kwanza na wa pili kutoka katika kila kundi ndio atakuwa amesonga mbele katika hatua nusu fainali. Bingwa wa michuano hii atajivunia kitita cha dola 625,000 sawa na shilingi 1,366,250,000 huku mshindi wa pili katika fainali akikunja kitita cha dola 432,000 sawa na shilingi 944,352,000. Mshindi wa pili na wa tatu kutoka katika makundi kila mmoja atapata dola 239,000 sawa na shilingi 522,454,000 na wa nne atakunja dola 150,000 sawa na shilingi 327,900,000.

KLOPP AKUBALI LAWAMA.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amekubali kutupia lawama kufuatia kipigo cha mabao 3-1 walichopata kutoka kwa Sevilla katika mchezo wa fainali ya Europa League na kudai kuwa watarejea wakiwa imara zaidi. Liverpool walianza vyema mchezo huo kwa kuongoza lakini walijikuta wakipoteana katika kipindi cha pili na kuipa mwanya Sevilla kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kushinda taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo. Kipigo hicho pia kinamaanisha Liverpool hawatashiriki michuano yoyote ya Ulaya msimu ujao. Akihojiwa Klopp ambaye alichukua mikoba ya kuinoa Liverpool Octoba mwaka jana, amesema kikosi chake kilicho kwa asilimia 50 mpaka 60 ya kiwango chao cha kawaida na wanatakiwa kukubaliana na hilo. Klopp aliongeza kuwa anawajibika kwa kikosi chake kucheza kwa kiwango hicho na kuahidi kuwa watatumia kama mfano ili wakirejea wawe imara zaidi.

MABINGWA LEICESTER KUONGEZA WATATU KIANGAZI.


MAKAMU mwenyekiti wa Leicester City, Aiyawatt Srivaddhanaprabha amedai klabu hiyo inatarajia kusajili wachezaji watatu au wanne katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi ili waweze kujiimarisha kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ubingwa Ligi Kuu uliwafanya Leicester kupata tiketi ya kushiriki michuano hiyo msimu uja ikiwa ni mara yao ya kwanza. Leicester pia watashiriki michuano ya Kombe la Kimataifa litakalofanyika kipindi hiki cha kiangazi na wanatajia kupambana na bingwa wa Kombe la FA katika mchezo wa Ngao Hisani. Akizungumza wakiwa nchini Bangkok walipokwenda kwa ziara makamu mwenyekiti huyo amesema wanafurahia kikosi walichonacho hivi sasa lakini msimu ujao wana mashindano mengi zaidi hivyo inabidi waongeze baadhi ya wachezaji ili kujiimarisha.

RONALDO, RODRIGUEZ KUIKOSA OLIMPIKI.

NYOTA wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo na James Rodriquez wanatarajiwa kuikosa michuano ya Olimpiki inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu nchini Brazil. Ronaldo nahodha wa Ureno na Rodriguez anayeiwakilisha Colombia wote hawatarajiwi kuteuliwa katika vikosi vitakavyotumika kwa ajili ya michuano hiyo kwasababu ya ushiriki wao katika michuano ya Euro 2016 na baadae Copa America. Kocha wa kikosi cha Olimpiki cha Ureno Rui Jorge amesema pamoja na kwamba hajafanya maamuzi ya wachezaji gani waliozidi umri wa miaka 23 atakaowatumia katika michuano hiyo lakini hadhani kama Ronaldo atakuwa mmoja wapo. Kwa upande wa Rodriquez, rais wa Chama cha Soka cha Colombia, Ramon Jesurun amesema tayari nyota huyo ameshafanya maamuzi kuwa atacheza Copa America badala ya Olimpiki.

MKATABA MPYA WA NIKE WAIPA JEURI BARCELONA YA KUWAONGEZA MKATABA NEYMAR NA BUSQUETS.

KLABU ya Barcelona inadaiwa kuwa tayari imeanza kuweka sawa mipango yao ya baadae baada ya kutwaa taji lao la sita la La Liga katika kipindi cha miaka nane Jumamosi iliyopita. Utawala wa soka wa Barcelona nchini Hispania unaonekana hautaweza kuisha katika siku za karibuni kwani tayari wanadaiwa kufikia makubaliano ya mikataba mipya kwa nyota wake Neymar na Sergio Busquets pamoja na wadhamini wao kampuni ya vifaa vya michezo ya Marekani, Nike. Neymar anadaiwa kufikia makubaliano ya awali ya nyongeza ya mkataba ambao utadumu mpaka mwaka 2021 na kufanya nyongeza ya kuvunja mkataba huo kuongezeka mpaka kufikia dola milioni 213. Barcelona wana matumaini mkataba huo mpya Neymar atausaini kabla ya mchezo wao wa fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya mabingwa wa Europa League Sevilla. Kiungo Busquets pia anatarajiwa kusaini mkataba mpya ambao utamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi katika orodha ya klabu hiyo. Yote hayo yanatarajiwa kuweza kufanikishwa kutokana na mkataba mpya watakaosaini na Nike ambao unakadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 112 kwa mwaka ukiwa unazidi ule wa Manchester United waliosaini na kampuni ya Adidas ya Ujerumani.

TORRES ADAI HANA SHIDA NA EURO.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Hispania, Fernando Torres amedai kuachwa kwake katika kikosi cha nchi hiyo kwa ajili ya michuano ya Euro 2016 hakujamzuia kujiandaa kwa kila kitu kwa ajili ya kuiongoza Atletico Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Torres ambaye hajaitumikia Hispania toka Kombe la Dunia mwaka 2014, amekuwa katika kiwango kizuri msimu huu huku mabao ake yakiisaidia klabu yake kumaliza katika nafasi ya tatu katika msimamo wa La Liga. Mbali na kuisaidia Atletico katika La Liga lakini pia ameisaidia kutinga hatua ya fainali ambapo sasa watakwaana na majirani zao Real Madrid Mei 28 mwaka huu katika Uwanja wa San Siro jijini Milan. Pamoja na kufunga mabao 12 msimu huu, Torres mwenye umri wa miaka 32 hakuchaguliwa katika kikosi cha awali cha kocha Vicente Del Bosque kwa ajili ya michuano ya Euro 2016 itakayofanyika huko Ufaransa mapema mwezi ujao. Akihojiwa Torres amesema hajali sana kuhusu Euro kwani ana mchezo mkubwa wa maisha yake atakaocheza hivi karibuni.

OFISA WA EL MERREIKH ACHUNGUZWA NA CAF KUFUATIA MADAI YA KUMPIGA MWAMUZI.

SHIRIKISHO la Soka la Afrika-CAF linamfanyia uchunguzi ofisa wa klabu ya Al Merreikh ya Sudan, Hatim Mohamed Ahmed baada ya kunaswa akimpiga mwamuzi Eric Otogo-Castane wa Gabon usoni. Tukio hilo lilitokea katika dakika ya 84 ya mchezo wa jana wa Kombe la Shirikisho kati ya Merreikh na Kawkab Marrakech ya Morocco. CAF inalifanyia uchunguzi kwa karibu tukio hilo huku wakisubiri ripoti ya waamuzi. Kawkab walishinda mchezo huo kwa mabao 2-0 ambayo yote yalifungwa kwa njia ya panati na kuwafanya kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1.


Tuesday, May 17, 2016

DEL BOSQUE ATAJA SILAHA ZAKE, AWAACHA KINA TORRES, CAZORLA, COSTA NA MATA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Chelsea, Diego Costa ameachwa katika kikosi cha awali cha wachezaji 25 cha timu ya taifa ya Hispania kwa ajili ya michuano ya Euro 2016. Kocha wa timu hiyo Vicente del Bosque pia amewatema kiungo wa Manchester United Juan Mata na mashambuliaji wa zamani wa Liverpool na Chelsea ambaye kwasasa yuko Atletico Madrid Fernando Torres. Hispania ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo wamepangwa kundi D sambamba na timu za Croatia, Jamhuri ya Czech na Uturuki. 
Costa mwenye umri wa miaka 27 ambaye alikosa michezo miwili ya mwisho ya Chelsea kutokana na kusumbuliwa na msuli wa paja, ameifungia Hispania bao moja pekee katika mechi alizocheza. Beki wa Bayern Munich Javi Martinez na kiungo wa Arsenal Santi Cazorla ni miongoni mwa wachezaji wengine walioachwa katika kikosi hicho cha Del Bosque.

LALLANA AKANUSHA TAARIFA ZA KUTAKA KWENDA SPURS.

NYOTA wa Liverpool, Adam Lallana amesema ataendelea kubakia katika klabu hiyo pamoja na kuvuma kwa tetesi kuwa anaweza kuwindwa na Tottenham hotspurs. Lallana mwenye umri wa miaka 28 alisajiliwa Liverpool akitokea Southampton kwa kitita cha paundi milioni 25 mwaka 2014 na toka wakati huo amefanikiwa kucheza mechi 57 za ligi na kufunga mabao tisa. Gazeti la The Sun la Uingereza liliripoti kuwa meneja wa zamani wa Southampton Mauricio Pochettino ambaye kwasasa ndio anayeinoa Spurs anaweza kutaka kumleta Lallana White Hart Lane. Lakini hata hivyo, Lallana alikanusha tetesi hizo na kudai kuwa bado amebakisha mkataba wa miaka mitatu Liverpool na anafurahia kufanya kazi chini Jurgen Klopp. Akihojiwa Lallana amesema amekuwa na mahusiano mazuri na Pochettino nje ya uwanja kwasababu ni marafiki lakini kwasasa yuko katika klabu kubwa na hana mpango wowote wa kuondoka.

WAKALA WA IBRAHIMOVIC ADAI MAN UNITED HAWAJATOA OFA YEYOTE.

WAKALA wa mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic, amedai kuwa hakuna ofa yeyote ya mkataba iliyotolewa na Manchester United kwa mteja wake. Siku chache kabla ya Ibrahimovic hajacheza mechi yake ya mwisho akiwa na Paris saint-Germain-PSG vyombo vya habari nchini Ufaransa vilidai kuwa United tayari wamemtumia ofa ya mkataba wa mwaka mmoja nyota huyo. Lakini wakala wake Mino Raiola alikanusha taarifa hizo akidai kuwa wanahabari siku hizi wamekuwa wakijitengenezea habari wenyewe zisizokuwa na ukweli wowote. Ibrahimovic alithibitisha Ijumaa iliyopita kuwa ataondoka Parc des Princes na kusheherekea taji la ligi baada ya kucheza mechi yake ya mwisho siku moja baadae. Nyota huyo anatarajiwa kukamilisha kibarua chake PSG Jumamosi hii katika mchezo wa fainali ya Kombe la Ufaransa dhidi ya Marseille.

FAINALI EUROPA LEAGUE: LIVERPOOL WATUA SALAMA BASEL TAYARI KUIVAA SEVILLA, ORIGI, HENDERSON NDANI.

MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Divock Origi amesafiri na kikosi cha timu hiyo kuelekea Basel ka ajili ya mchezo wao wa fainali ya Europa League dhidi ya Sevilla utakaofanyika kesho. Origi alikuwa amepata majeruhi ya kifundo cha mguu katika mchezo dhidi ya Everton uliofanyika Aprili 20 mwaka huu lakini alidai kuwa matumaini ya kurejea kabla ya msimu kumalizika. Katika mchezo huo Daniel Sturridge ndio anayetarajiwa kuanza huku Christian Benteke pia akipewa nafasi hiyo na sasa taarifa zinadai Origi yuko fiti baada ya kufanya mazoezi na wenzake jana. 
Origi anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba sambamba na kiungo Jordan Henderson ambaye naye pia amesafiri kwenda Basel baada ya kurejea uwanjani katika sare ya bao 1-1 waliyopata Liverpool dhidi ya West Bromwich Albion. Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp ametamba kuwa kikosi chake kiko tayari kukabiliana na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Sevilla ambao wanalitafuta kulichukua kwa mara ya tatu mfululizo.

CHELSEA, SPURS WALIMWA ADHABU NA FA.

CHAMA cha Soka cha Uingereza-FA kimezitoza faini klabu za Chelsea na Tottenham Hotspurs jumla ya paundi 600,000 jana kwa kushindwa kuwazuia wachezaji wake baada ya kuzuka ugomvi baina yao katika Uwanja wa Stamford Bridge wezi huu. Chelsea wao watalipa kiasi cha paundi 375,000 na Spurs paundi 225,000 baada ya klabu zote kukiri kuvunja sheria katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 Mei 2 mwaka huu. Katika mchezo huo Chelsea walitoka nyuma na kuzima ndoto za Spurs kufukuzia taji la Ligi Kuu kwa kurudisha mabao mawili waliyokuwa wamefungwa na kupelekea mchezo huo kumalizika kwa sare. Mapema Spurs wao walinyukwa fainali ya moja kwa moja ya paundi 25,000 kwa wachezaji wake tisa kupokea kadi za njano kutoka kwa mwamuzi Mike Clattenburg kwenye mchezo huo.

LEICESTER WAZUNGUKA NA KOMBE LAO MTAANI.

WATU wanaokadiriwa kuwa robo milioni wameandamana mitaani kwa lengo la kuipongeza klabu ya Leicester City iliyoibuka bingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza katika historia yake ya miaka 132. Mistari miwili mikubwa pamoja na gari kubwa lililo wazi vilizunguka mji huo ulio katikati ya Uingereza. Meneja wa Leicester Muitaliano Claudio Ranieri ameiambia BBC kuwa mji mzima ulifurika watu waliokuwa wakiishangilia timu yao ambayo ilicheza kwa kujitolea sana. Leicester walipewa nafasi moja tu kati ya 5000 ya kushinda taji hilo la ligi mwanzoni mwa msimu.

Monday, May 16, 2016

MGANGA MKUU FIFA ATAKA SHERIA KALI KWA MATIBABU YA UWANJANI.

MGANGA mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Profesa Jiri Dvorak amelitaka shirikisho hilo kuweka sheria kali zaidi kwa matibabu ya uwanjani. Kauli hiyo imekuja kufuata kifo cha mchezaji wa kimataifa wa Cameroon Patrick Ekeng. Ekeng aliyekuwa na umri wa miaka 26 alifariki duniani kwa kinachodhaniwa shambulio la moyo Mei 6 mwaka huu wakati akiitumikia klabu yake ya Dinamo Bucharest ya Romania huku gari la wagonjwa lililomhudumia likidaiwa kutokuwa na mashine maalumu kwa ajili ya kuustua moyo uliosimama kufanya kazi kitaalamu ikijulikana kama defibrillator. 
Akihojiwa Dvorak amesema katika mechi za soka kunapaswa kuwepo kwa kifaa hicho maalumu pembeni na maofisa wa afya wanatakiwa kuwa wamefundishwa jinsi ya kukitumia. Dvorak aliongeza kuwa atalipeleka suala hilo katika baraza la FIFA ili kutoa maamuzi ya kimkakati yatakayowawezesha kuweka sheria kali zaidi kwa wanachama wake. Ekeng alizikwa jana nyumbani kwao Younde katika mazishi yaliyohudhuriwa na wachezaji mbalimbali wa timu hiyo pamoja na rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon-Fecafoot, Paul Biya.