Monday, May 16, 2016

MGANGA MKUU FIFA ATAKA SHERIA KALI KWA MATIBABU YA UWANJANI.

MGANGA mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Profesa Jiri Dvorak amelitaka shirikisho hilo kuweka sheria kali zaidi kwa matibabu ya uwanjani. Kauli hiyo imekuja kufuata kifo cha mchezaji wa kimataifa wa Cameroon Patrick Ekeng. Ekeng aliyekuwa na umri wa miaka 26 alifariki duniani kwa kinachodhaniwa shambulio la moyo Mei 6 mwaka huu wakati akiitumikia klabu yake ya Dinamo Bucharest ya Romania huku gari la wagonjwa lililomhudumia likidaiwa kutokuwa na mashine maalumu kwa ajili ya kuustua moyo uliosimama kufanya kazi kitaalamu ikijulikana kama defibrillator. 
Akihojiwa Dvorak amesema katika mechi za soka kunapaswa kuwepo kwa kifaa hicho maalumu pembeni na maofisa wa afya wanatakiwa kuwa wamefundishwa jinsi ya kukitumia. Dvorak aliongeza kuwa atalipeleka suala hilo katika baraza la FIFA ili kutoa maamuzi ya kimkakati yatakayowawezesha kuweka sheria kali zaidi kwa wanachama wake. Ekeng alizikwa jana nyumbani kwao Younde katika mazishi yaliyohudhuriwa na wachezaji mbalimbali wa timu hiyo pamoja na rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon-Fecafoot, Paul Biya.

No comments:

Post a Comment