Wednesday, May 25, 2016

POLISI ZAIDI 60,000 KUMWAGWA KUIMARISHA ULINZI EURO 2016.

UFARANSA imesema kuwa inatarajia kuweka polisi zaidi ya 60,000 ili kulinda usalama katika michuano ya Euro 2016 na kuapa kuwa watafanya kila wawezalo kuhakikisha wanazuia shalio lolote la kigaidi katika kipindi chote cha mashindano. Kauli hiyo ya waziri wa mambo ya ndani ya nchi hiyo Bernard Cazeneuve imekuja baada ya Uwanja wa Ufaransa uliopo jijini Paris ambao ndio utatumika kwa ajili ya mechi ya ufunguzi na fainali, kuleta rabsha Jumamosi iliyopita kabla ya fainali ya Kombe la Taifa. Moshi mkubwa uliohisiwa kuwa bomu ulilipuka ndani ya uwanja na kusababisha mashabiki kuchanganyikiwa na kukimbia hovyo kuelekea milango ya kutoka nje ya uwanja. Akihojiwa waziri huyo amesema tukio la Jumamosi iliyopita halihusiani na maandalizi yao kwani waandaaji walikuwa tofauti. Waziri huyo aliongeza kuwa katika michuano ya Euro 2016 inayotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao usalama utakuwa ni kipaumbele chao cha kwanza ili kuhakikisha hakuna tukio lolote hatarishi ya kigaidi litakaloweza kutokea.

No comments:

Post a Comment